Maisha na Huduma ya Yesu
Yesu Aondolea Mbali Huzuni ya Mjane
MUDA mfupi baada ya kumponya mtumishi wa Akida, Yesu aondoka kwenda Naini, mji ulio kilometa 32 kusini-magharibi mwa Kapernaumu. Wanafunzi wake pamoja na makutano mengi wanaambatana naye. Wanakaribia mpakani mwa Naini ikielekea jioni, ambapo wanakutana na mwandamano wa mazishi. Mwili wa kijana mmoja umebebwa kutoka katika mji ukazikwe.
Hali ya mama ni yenye huzuni sana, kwa kuwa yeye ni mjane na huyo ni mwana wake wa pekee. Mumeye alipokufa, alipata faraja kwa sababu yeye alikuwa na mwana. Matumaini yake, tamaa, na fahari yalitiwa katika wakati ujao wa mwanaye. Lakini sasa hakuna mtu wa kumpa faraja. Huzuni yake ni kubwa sana wakati watu wa mjini wanapoambatana naye mahali pa kuzika.
Yesu anapomwona mwanamke huyo, moyo wake unaguswa kwa sababu ya huzuni yake kuu. Basi kwa huruma, lakini kwa uthabiti unaotoa tumaini, anamwambia mwanamke: “Usilie.” Namna yake na kutenda kwake kwavuta fikira za umati. Basi anapokaribia na kuligusa jeneza ambalo limebeba maiti, wale wanaolibeba wanasimama. Ni lazima wote wawe wanataka kujua ni jambo gani atakalofanya.
Ni kweli kwamba wanaoambatana na Yesu wamemwona akiponya magonjwa ya watu wengi kwa mwujiza. Lakini labda hawajamwona akimfufua ye yote kutoka kwa wafu. Je! anaweza kufanya jambo hilo? Akimwambia maiti, Yesu anaamuru: “Kijana, nakuambia, Inuka!” Yule mwanamume aketi! Aanza kusema, naye Yesu anamoa kwa mamaye.
Watu wanapoona ya kwamba kweli kijana yu hai, wanaanza kusema: “Nabii mkuu ametokea kwetu.” Wengine wanasema: “Mungu amewaangalia watu wake.” Upesi habari zinazohusu tendo hili la kushangaza zinaenea kote kote katika Yudea na nchi zote za kando kando.
Yohana Mbatizaji angali gerezani. Lakini wanafunzi wake wanamwambia mambo yote hayo wanayomwona Yesu akifanya. Yohana anaitikiaje? Na watu wengine wengi katika sehemu ambazo Yesu anafanya miujiza wanaitikiaje? Makala yetu inayofuata itatoa jibu. Luka 7:11-18.
◆ Ni jambo gani linalotukia Yesu anapokaribia Naini?
◆ Anayoona Yehova yanakuwa na matokeo gani kwake, naye anafanya nini?
◆ Watu wanaitikiaje mwujiza wa Yesu?