Maisha na Huduma ya Yesu
Ni Mambo Gani Yanayochafua Mtu?
UPINZANI kwa Yesu ukawa wenye nguvu zaidi. Si kwamba tu wengi wa wanafunzi wake wanaondoka bali Wayahudi katika Yudea wanatafuta kuua yeye, hata kama vile wao walivyojaribu kufanya wakati yeye alipokuwa katika Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Kupitwa ya 31 W.K.
Sasa ni wakati wa Sikukuu ya Kupitwa ya 32 W.K. Inaelekea, kupatana na takwa la Mungu la kuhudhuria, Yesu anakwea kwenda kwenye Sikukuu ya Kupitwa katika Yerusalemu. Hata hivyo, yeye anafanya hivyo kwa tahadhari kwa sababu maisha yake yamo katika hatari. Baadaye yeye anarudi Galilaya.
Yesu pengine yuko Kapernaumu wakati Mafarisayo na waandishi kutoka Yerusalemu wanapomjia. Wao wanatafuta msingi ambao juu ya huo wanaweza kumshtaki kuvunja sheria ya kidini. “Sababu gani wanafunzi wako wanapita lile pokeo la watu wa nyakati zilizopita?” wao wanauliza. “Kwa mfano, wao hawanawi mikono yao wakati wanapokaribia kula mlo.” Hili si jambo fulani linalotakwa na Mungu, hata hivyo Mafarisayo wanalifikiria kuwa kosa zito kutofanya sherehe hii ya kimapokeo, iliyotia ndani kuosha mikono kufika viwiko.
Badala ya kujibu shtaka lao, Yesu anaelekeza kwenye uovu wao na kuvunja makusudi kwao sheria ya Mungu. “Sababu gani ninyi pia mnapita ile amri ya Mungu kwa sababu ya pokeo lenu?” yeye anataka kujua. “Kwa mfano, Mungu alisema, ‘Heshimu baba yako na mama yako’ na, ‘acha yeye ambaye hutukana kwa maneno ya dharau baba au mama aishie katika kifo.’ Lakini ninyi husema, ‘Ye yote anayesema kwa baba au mama yake: “Cho chote mimi nilicho nacho ambacho kwacho wewe ungepata manufaa kutoka kwangu mimi ni zawadi iliyowekwa wakfu kwa Mungu,” yeye si lazima aheshimu baba yake hata kidogo.
Kweli kweli, hao Mafarisayo hufundisha kwamba pesa, mali, au kitu cho chote ambacho kimewekwa wakfu kuwa zawadi kwa Mungu ni mali ya hekalu, na hakiwezi kutumiwa kwa kusudi jingenelo. Hata hivyo, kwa kweli, ile zawadi iliyowekwa wakfu inabaki na yule mtu ambaye aliiweka wakfu. Katika njia hii mwana, kwa kusema tu kwamba pesa au mali yake ni “korbani”—zawadi iliyowekwa wakfu kwa Mungu au kwa hekalu—anaepa daraka lake la kusaidia wazazi wake waliozeeka, ambao huenda wakawa katika shida kubwa sana.
Akighadhibikia kwa kufaa Mafarisayo kwa kupotosha vibaya sheria ya Mungu, Yesu anasema: “Ninyi mnafanya neno la Mungu kuwa bure kwa sababu ya pokeo lenu. Ninyi wanafiki, Isaya alitoa unabii kwa kufaa juu yenu ninyi, wakati yeye alisema, ‘Watu hawa huheshimu mimi kwa midomo yao, hata hivyo mioyo yao imeondolewa mbali kutoka kwangu mimi. Ni kwa bure kwamba wao wanaendelea kuabudu mimi, kwa sababu wao hufundisha amri za wanadamu kuwa mafundisho ya dini.’”
Pengine umati wa watu ulikuwa umerudi nyuma kuruhusu Mafarisayo wamswali Yesu. Sasa, wakati hao Mafarisayo wanapokosa jibu kwa kemeo lenye nguvu la Yesu kuwahusu yeye anaita umati wa watu karibu. “Sikilizeni mimi,” yeye asema, “na mpate maana. Hakuna kitu kutoka nje ya mtu ambacho hupita ndani yake yeye ambacho kinaweza kuchafua yeye; lakini vile vitu ambavyo hutoka nje kutoka ndani ya mtu ndivyo vitu ambavyo huchafua mtu.”
Baadaye, wakati wanapoingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wanauliza: “Je! wewe unajua kwamba wale Mafarisayo walikwazika kwa kusikia yale wewe ulisema?”
“Kila mpando ambao Baba yangu wa kimbingu hakupanda utang’olewa,” Yesu anajibu. “Acheni wao. Viongozi vipofu ndivyo wao walivyo. Ikiwa, basi, mtu kipofu amwongoza kipofu, wote wawili wataanguka ndani ya shimo.”
Yesu anaonekana kushangaa wakati, kwa niaba ya wanafunzi, Petro anaomba maelezo kuhusu mambo yanayochafua mtu. “Je! ninyi pia mngali bila ufahamu?” Yesu aitikia. “Je! ninyi hamjui kwamba kila kitu kinachoingia kinywani hupitia ndani ya matumbo nacho hutoka na kuingia ndani ya shimo la takataka? Lakini, vile vitu vinavyotoka katika kinywa hutoka ndani ya moyo, na vitu hivyo vinachafua mtu. Kwa mfano, ndani ya moyo hutoka mawazo maovu, mauaji ya kukusudia, uzinzi, uasherati, wivi, mashuhuda yasiyo ya kweli, makufuru. Haya ndiyo mambo ambayo huchafua mtu; bali kula mlo kwa mikono isiyooshwa hakumchafui mtu.”
Hapa Yesu hakuwa akikataza kuwa na usafi wa afya wa kawaida. Yeye hatoi hoja kwamba mtu hahitaji kuosha mikono yake kabla ya kutayarisha chakula au kula mlo. Badala ya hiyo, Yesu analaumu vikali unafiki wa viongozi wa kidini ambao kwa hila hujaribu kuzunguka sheria za uadilifu za Mungu kwa kusisitiza juu ya mapokeo yasiyo ya kimaandiko. Ndiyo, ni vitendo vibaya ambavyo huchafua mtu, na Yesu anaonyesha kwamba hivyo huanzia katika moyo wa mtu. Yohana 7:1, NW; Mathayo 15:1-20, NW; Marko 7:1-23; Kutoka 20:12, NW; 21:17, NW; Isaya 29:13; Kumbukumbu 16:16, NW.
◆ Ni upinzani gani ambao sasa Yesu anaelekeana nao?
◆ Ni shtaka gani ambalo Mafarisayo wanafanya, lakini kulingana na Yesu, ni kwa jinsi gani hao Mafarisayo wanavunja sheria ya Mungu kwa makusudi?
◆ Yesu anafunua kwamba ni mambo gani ambayo huchafua mtu?