Fumbo la Kodeksi ya Vatikani
CODEX Vaticanus 1209 imo katika orodha ya kwanza ya Maktaba ya Vatikani, iliyotayarishwa mwaka 1475. Hakuna ajuaye ilivyoingia humo. Ni moja ya kodeksi tatu kubwa za Kigiriki ambazo zimeweza kubakia mpaka leo, ikiwa katika kiwango kimoja na ile nyingine ya rika moja nayo, Sinaiticus ya karne ya nne, na Alexandrinus ya mapema katika karne ya tano.
Ingawa wanachuo walijua sana umaana wa hatimkono hii ya Vatikani mapema katika karne ya 16, ni wachache waliopata kuruhusiwa waichunguze. Maktaba ya Vatikani ilitayarisha ulinganisho wa misomeko mbalimbali ya hati-mkono hiyo katika 1669, lakini ikapotea na haikugunduliwa tena mpaka 1819.
Mmaliki Napoleon wa Ufaransa aliteka Roma katika 1809 na kuipeleka Paris hatimkono hiyo yenye kuthaminiwa sana, ikachunguzwa huko na Leonhard Hug, mwanachuo mwenye sifa, lakini Napoleon alipoanguka kodeksi hiyo ikarudishwa Vatikani katika 1815. Kwa miaka 75 iliyofuata ikawa tena fumbo, kwa kufichwa na Vatikani.
Konstantin von Tischendorf, mmoja wa wanachuo wa hatim-kono walio wakubwa zaidi ulimwenguni, aliruhusiwa kuchunguza hati-mkono hiyo katika 1843 kwa muda wa saa sita tu, baada ya kuendelea kungojeshwa kwa miezi kadhaa. Miaka miwili baadaye, mwanachuo Mwingereza Dakt. S. P. Tregelles aliruhusiwa kuiona kodeksi hiyo lakini asiichunguze. Yeye alitaarifu hivi: “Ni kweli kwamba mimi niliiona mara nyingi hati-mkono hiyo, lakini hawakutaka kuniruhusu niitumie; na hawakutaka kuniacha niifungue bila kunipekua mifukoni, na kuninyima kalamu, wino, na karatasi; na wakati uo huo prelati [mapadri] wawili walizidi tu kuongea nami katika Kilatini, na ikiwa nilitazama kifungu fulani kwa muda mrefu mno, walikuwa wakinipokonya kitabu kile.”
Kwa nini Kanisa Katoliki la Kiroma lilikataa sana kuonyesha ulimwengu hati-mkono yalo yenye thamani kubwa sana?
Kwa Nini Ilifichwa?
Kwa Kanisa Katoliki la Kiroma, fasiri Latin Vulgate ya Maandiko Matakatifu imebaki ikiwa “mamlaka [yalo] iliyo kubwa zaidi.” Kulingana na barua ya kipapa Divino Afflante Spiritu ya Pius wa 12, iliyotangazwa kwa chapa katika mwaka 1943, tafsiri hiyo ya Kilatini iliyofanywa na Jerome karne ya nne inaonwa pia kuwa “isiyoweza kabisa kuwa na kosa katika mambo ya imani na maadili.” Namna gani maandiko ya Kiebrania na Kigiriki ambayo Vulgate ilitafsiriwa kutokana nayo? Barua hiyo ya kipapa inasema maandiko hayo ni yenye thamani ili ‘kuthibitisha’ mamlaka ya Vulgate. Kwa hiyo hati-mkono yoyote ya Kigiriki, hata Kodeksi ya Vatikani, haijapata kamwe kufikiriwa kuwa yenye mamlaka kama Vulgate ya Kilatini. Ni wazi kwamba msimamo huo uliochukuliwa na Kanisa Katoliki la Kiroma umesababisha matatizo.
Kwa kielelezo, wakati Erasmus mwanachuo wa karne ya 16 alipotafsiri “Agano Jipya,” lake la Kigiriki alisihi wenye mamlaka juu ya Kodeksi ya Vatikani ili kuondoa maneno yale bandia katika 1 Yohana sura 5, mistari 7 na 8. Erasmus alikuwa sawa, na bado hata baadaye sana kufikia 1897 Papa John Leo 13 aliunga mkono maandishi ya Kilatini yaliyofisidiwa ya hiyo Vulgate. Wakati tu tafsiri za ki-siku-hizi za Katoliki ya Kiroma zilipochapishwa ndipo kosa hilo la kimaandishi lilipokuja kukubaliwa.
Wakati Codex Sinaiticus ilipofunuliwa kwa ulimwengu katika sehemu ya mwisho ya karne ya 19, wenye mamlaka wa Katoliki ya Kiroma waliona wazi kwamba Codex Vaticanus yao ilikuwa katika hatari ya kupitwa na hati nyinginezo. Karne hiyo ilipokuwa ikimalizika, mwishowe zilipatikana nakala nzuri za kupigwa foto.
Hati-mkono hiyo ina karatasi 759 za kurasa. Imekosa sehemu kubwa ya Mwanzo, zaburi fulani-fulani, na sehemu za kumalizia za Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Imeandikwa juu ya pachimenti laini sana na nyembamba, inayofikiriwa kuwa imetolewa katika ngozi za paa, kwa mtindo rahisi, wa kuvutia. Mtajo wayo rasmi ni Codex B, na inaweza kuonwa leo katika Maktaba ya Vatikani. Haifichwi tena, na hatimaye thamani yayo inaeleweka na kuthaminiwa sehemu zote za ulimwengu.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Codex Vaticanus 1209 yenye umaana ilifichiva na Vatikani kioa karne kadhaa
[Hisani]
Nakala ya sawasawa kabisa kutokana na Codices E Vaticanis Selecti