Maisha na Huduma ya Yesu
Unyenyekevu Kwenye Sikukuu-Kupitwa ya Mwisho
PETRO na Yohana, kwa maagizo kutoka kwa Yesu, tayari wamewasili katika Yerusalemu kufanya matayarisho kwa ajili ya Sikukuu-Kupitwa. Yesu awasili baadaye alasiri, yaonekana akiwa na mitume wengine kumi. Jua linazama chini kwenye upeo wa macho huku Yesu na kikundi chake wakiteremka chini ya Mlima wa Mizeituni na kuvuka Bonde la Kidroni. Hii ndiyo mara ya mwisho ya Yesu kuliona jiji wakati wa mchana mpaka baada ya ufufuo wake.
Muda si muda Yesu na kikundi chake wawasili katika jiji na kushika njia kwenda kwenye nyumba ambako wataadhimisha Sikukuu-Kupitwa. Wazipanda ngazi kwenda kwenye chumba kikubwa cha juu, ambako wapata matayarisho yote yamefanywa kwa ajili ya mwadhimisho wao wa faragha wa Sikukuu-Kupitwa. Yesu ameitazamia pindi hii, kwa vile asema: “Mimi nimetamani sana kuila sikukuu-kupitwa hii pamoja na nyinyi kabla sijateseka.”
Kimapokeo, vikombe vinne vya divai hunywewa na washiriki wa Sikukuu-Kupitwa. Baada ya kupokea kile ambacho yaonekana ndicho kikombe cha tatu, Yesu ashukuru na kusema: “Chukueni hiki na mkipitishe kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine miongoni mwenu wenyewe; kwa maana mimi nawaambia nyinyi, Kuanzia sasa na kuendelea sitakunywa tena kutoka zao la mzabibu mpaka ufalme wa Mungu uwasili.”
Wakati fulani katika mlo huo, Yesu ainuka, aweka kando mavazi yake ya nje, achukua taulo, na kujaza karai maji. Kwa kawaida, mwenye kupokea wageni ndiye angehakikisha kwamba nyayo za mgeni zimeoshwa. Lakini kwa kuwa katika pindi hii hakuna mwenye kupokea wageni, Yesu afanya utumishi huu wa kibinafsi. Yeyote wa mitume angaliweza kuwa amebamba fursa hiyo ili kufanya hivyo; na bado, yaonekana kwa sababu ushindani fulani ungali miongoni mwao, hakuna afanyaye hivyo. Sasa wao waaibika Yesu aanzapo kuosha nyayo zao.
Yesu amjiapo, Petro ateta akisema: “Kwa uhakika wewe hutaosha kamwe nyayo zangu.”
“Mimi nisipokuosha wewe, wewe huna sehemu na mimi,” Yesu asema.
“Bwana,” Petro aitikia, “si nyayo zangu tu, bali pia mikono yangu na kichwa changu.”
“Yeye ambaye ameoga,” Yesu ajibu, “hahitaji kuoshwa zaidi ya nyayo zake, bali ni safi kabisa. Na nyinyi watu ni safi, lakini si nyote.” Asema hivyo kwa sababu ajua kwamba Yuda Iskariote anapanga kumsaliti.
Yesu akiisha kuosha nyayo za wote 12, kutia na nyayo za msaliti wake, Yuda, avaa mavazi yake ya nje na kuegemea mezani tena. Halafu auliza: “Je! nyinyi mwajua lile ambalo mimi nimewafanyia nyinyi? Nyinyi huniita, ‘Mwalimu,’ na, ‘Bwana,’ na mwasema ifaavyo, kwa maana ndivyo nilivyo. Kwa hiyo, ikiwa mimi, ingawa Bwana na Mwalimu, nimeosha nyayo zenu, nyinyi pia mwapaswa kuosha nyayo za mmoja na mwenzake. Kwa maana mimi niliwawekea nyinyi kigezo, kwamba, kama vile mimi nilivyowafanyia nyinyi, nyinyi mwapaswa kufanya hivyo pia. Kwa kweli kabisa mimi nasema kwa nyinyi, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana-mkubwa wake, wala mwenye kutumwa si mkubwa kuliko mwenye kumtuma. Ikiwa mwajua mambo haya, wenye furaha ni nyinyi ikiwa mwayafanya.”
Lo, somo zuri kama nini la utumishi wa unyenyekevu! Mitume hawapaswi kuwa wakitafuta mahali pa kwanza, wakifikiri kwamba wao ni wa maana sana hivi kwamba wengine wapaswa kuwatumikia wao sikuzote. Wao wahitaji kufuata kigezo kilichowekwa na Yesu. Hicho si kigezo cha uoshaji nyayo kidesturi tu. Sivyo, bali ni cha nia ya kutumikia bila upendeleo, hata kama kazi ile ni ya umaana mdogo au isiyopendeza kwa kadiri gani. Mathayo 26:20, 21; Marko 14:17, 18; Luka 22:14-18; 7:44; Yohana 13:1-17, NW.
◆ Ni jambo la pekee juu ya Yesu kuona Yerusalemu aingiapo ili kuadhimisha Sikukuu-Kupitwa?
◆ Wakati wa Sikukuu-Kupitwa, yaonekana ni kikombe gani ambacho Yesu aagiza kipitishwe kwa wale mitume 12 baada ya kusema baraka?
◆ Ni utumishi gani wa kibinafsi ulioandaliwa kidesturi Yesu alipokuwa duniani, na kwa nini haukuandaliwa wakati wa Sikukuu-Kupitwa iliyoadhimishwa na Yesu na mitume?
◆ Kusudi la Yesu lilikuwa nini katika kufanya utumishi huo wenye umaana mdogo wa kuosha nyayo za mitume wake?