Maisha na Huduma ya Yesu
Kusalitiwa na Kukamatwa
UMEPITA sana usiku wa kati wakati Yuda aongozapo umati mkubwa wa askari, wakuu wa makuhani, Mafarisayo, na wengine kuingia bustani ya Gethsemane. Makuhani wameafiki kumlipa Yuda vipande 30 vya fedha ili amsaliti Yesu.
Mapema kidogo, Yuda alipoagizwa aondoke kwenye mlo wa Kupitwa, kwa wazi aliwaendea moja kwa moja wakuu wa makuhani. Nao wakawakusanya maofisa wao wenyewe mara hiyo, na pia kikosi cha askari. Labda kwanza Yuda aliwaongoza mahali Yesu na mitume walikuwa wameadhimisha Kupitwa. Kwa kugundua kwamba walikuwa wameondoka, ule umati mkubwa wenye kubeba silaha na kuchukua taa na mienge ulimfuata Yuda kutoka Yerusalemu na kwenda ng’ambo ya Bonde la Kidroni.
Yuda aongozapo msafara huo kuupanda Mlima wa Mizeituni, ahisi akiwa na uhakika kwamba ajua mahali pa kumpata Yesu. Wakati wa juma lililopita, Yesu na mitume walipokuwa wakisafiri huku na huku kati ya Bethania na Yerusalemu, walisimama mara nyingi katika bustani ya Gethsemane kupumzika na kuongea. Lakini, sasa, kukiwa na uwezekano wa kwamba Yesu amefichika gizani chinichini ya ile mizeituni, askari watamtambuaje? Huenda ikawa walikuwa hawajapata kumwona kamwe. Yuda aandaa ishara, akisema: “Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama.”
Yuda aongoza ule umati mkubwa kuingia bustanini, amwona Yesu pamoja na mitume wake, na kumwendea moja kwa moja. “[Siku njema, NW] Rabi,” asema na kumbusu kwa wororo sana.
“Rafiki, fanya ulilolijia [Jamaa, wewe upo kwa kusudi gani?, NW] Yesu ang’aka. Ndipo, akijibu swali lake mwenyewe, asema hivi: “Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu [wa binadamu, NW] kwa kumbusu?” Lakini hataki mengi zaidi na msaliti wake! Yesu apiga hatua mbele kuingia katika ile nuru ya mienge na taa zinazowaka na kuuliza hivi: “Ni nani mnayemtafuta?”
“Ni Yesu Mnazareti,” jibu laja.
“Ni mimi,” Yesu ajibu, huku akisimama kwa moyo mkuu mbele yao. Kwa kugutushwa na ujasiri wake na bila kujua watarajie nini, wanaume hao warudi nyuma na kuanguka chini.
“Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi,” Yesu aendelea kwa utulivu. “Basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” Kitambo kifupi kabla ya hapo akiwa katika kile chumba cha juu, Yesu alikuwa amemwambia Baba yake katika sala kwamba alikuwa amewatunza mitume wake waaminifu na hakuna hata mmoja wao aliyekuwa amepotezwa “ila yule mwana wa upotevu.” Hivyo basi, ili neno lake liweze kutimizwa, yeye aomba kwamba wafuasi wake waachwe waende.
Askari wanaporudiwa na umakini wao, kusimama, na kuanza kumfunga Yesu, mitume watambua likaribialo kutendeka. “Bwana, tuwapige kwa upanga?” wao wauliza. Kabla Yesu hajajibu, Petro, akitumia mmoja wa panga mbili ambazo mitume wameleta, amshambulia Malko, mtumwa wa kuhani wa juu. Dharuba ya Petro yakikosa kichwa cha mtumwa huyo lakini akata sikio lake la kulia.
“Mwe radhi kwa hili,” Yesu asema akiingilia. Kwa kugusa sikio hilo, aponya lile jeraha. Halafu afundisha somo la maana, akimwamuru Petro hivi: “Rudisha upanga wako mahali pake; maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi ku-msihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?”
Yesu ana nia ya kukamatwa. Kwa maana aeleza hivi: “Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?” Na aongeza hivi: “Je! kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?” Yeye aafikiana kabisa na mapenzi ya Mungu kwake!
Halafu Yesu aelekeza maneno yake kwenye ule umati. “Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika?” auliza. “Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe.”
Hapo kile kikosi cha askari na yule amiri wa kijeshi na wale maofisa wa Wayahudi wambamba Yesu na kumfunga. Kuona hilo, mitume wamwacha Yesu na kukimbia. Hata hivyo, mwanamume kijana—yaelekea ni mwanafunzi Marko—abaki miongoni mwa umati. Huenda akawa alikuwa kwenye makao ambapo Yesu aliadhimisha Kupitwa na baadaye akaufuata umati kutoka huko. Hata hivyo, sasa yeye atambuliwa, na jaribio la kumbamba lafanywa. Lakini yeye aacha nyuma vazi lake la kitani na kutoroka bila nguo za kutosha. Mathayo 26:47-56; Marko 14:43-52; Luka 22:47-53; Yohana 17:12; 18:3-12.
◆ Kwa nini Yuda alihisi akiwa na uhakika kwamba angempata Yesu katika bustani ya Gethsemane?
◆ Yesu adhihirishaje hangaiko kwa mitume wake?
◆ Petro achukua kitendo gani kumkinga Yesu, lakini Yesu asema nini kwake?
◆ Yesu afunuaje kwamba yeye aafikiana kabisa na mapenzi ya Mungu kwake?
◆ Mitume wamwachapo Yesu, nani abakia, naye apatwa na nini?