Je! Kanisa la Mapema Lilifundisha Kwamba Mungu Ni Utatu?
Sehemu ya 3-Je! Wateteaji-Ukristo Walifundisha Fundisho la Utatu?
Katika matoleo yalo ya Novemba 1, 1991, na Februari 1, 1992, gazeti Mnara wa Mlinzi lilionyesha kwamba fundisho la Utatu halikufundishwa na Yesu wala wanafunzi wake wala Mababa wa Kimitume wa mwishoni-mwishoni mwa karne ya kwanza na wa mapema mwa karne ya pili W.K. Je! wanaume wa kanisa wa mwishoni mwa karne ya pili walilifundisha?
TOKEA karibu katikati ya karne ya pili ya Wakati wa Kawaida wetu hadi mwisho wayo, walitokea wanaume wa kanisa ambao leo huitwa Wateteaji-Ukristo. Waliandika ili kutetea Ukristo walioujua dhidi ya falsafa zenye uadui zilizoenea katika ulimwengu wa Roma wa wakati ule. Waliandika vitabu vyao kuelekea mwishoni mwa, na baada ya, maandishi ya Mababa wa Kimitume.
Miongoni mwa Wateteaji-Ukristo walioandika katika Kigiriki walikuwa Justin Martyr, Tatian, Athenagoras, Theofilo, na Klementi wa Aleksandria. Tertuliano alikuwa Mteteaji-Ukristo aliyeandika katika Kilatini. Je! wao walifundisha fundisho la Utatu la Jumuiya ya Wakristo ya ki-siku-hizi—watu watatu walio sawa (Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu) katika Uungu, kila mmoja akiwa Mungu wa kweli, na hata hivyo kusiwe na Miungu watatu bali Mungu mmoja?
“Mwana Ni Mdogo Kwa Cheo”
Dakt. H. R. Boer, katika kitabu chake A Short History of the Early Church, aeleza wazo kuu la fundisho la Wateteaji-Ukristo:
“Justin [Martyr] alifundisha kwamba kabla ya ulimwengu kuumbwa Mungu alikuwa peke yake na kwamba hakukuwako Mwana. . . . Mungu alipotaka kuumba ulimwengu, . . . yeye alizaa mtu mwingine wa kimungu ili amwumbie ulimwengu. Mtu huyo wa kimungu aliitwa . . . Mwana kwa sababu yeye alikuwa amezaliwa; aliitwa Logosi kwa sababu alitolewa katika Fikira au Akili ya Mungu. . . .
“Kwa hiyo, Justin pamoja na wale Wateteaji-Ukristo wengine walifundisha kwamba Mwana ni kiumbe. Yeye ni kiumbe wa hali ya juu, kiumbe mwenye uwezo wa kutosha kuumba ulimwengu lakini, hata hivyo, ni kiumbe. Katika theolojia uhusiano huo wa Mwana na Baba huitwa subordinationism. Mwana ni mdogo, yaani, ni wa pili, ategemea, na ametokezwa na Baba. Wateteaji-Ukristo waliamini katika cheo kidogo [cha Mwana].”
Katika kitabu The formation of Christian Dogma, Dakt. Martin Werner husema hivi juu ya uelewevu wa mapema zaidi wa uhusiano wa Mwana kwa Mungu:
“Uhusiano huo ulieleweka pasipo shaka yoyote kuwa wa ‘cheo kidogo [cha Mwana]’ yaani, katika maana ya Kristo kuwa mdogo kwa Mungu. Popote katika Agano Jipya uhusiano wa Yesu kwa Mungu, Baba, ufikiriwapo, . . . huonwa na kuwakilishwa kabisa kuwa [Mwana ana cheo kidogo]. Na mwamini mwenye kukata maneno kabisa wa Fundisho la Cheo Kidogo [cha Mwana] la Agano Jipya, kulingana na maandishi ya Gospeli tatu za kwanza, ni Yesu mwenyewe . . . Msimamo huu wa kwanza, imara na dhahiri kama ulivyokuwa, uliweza kujidumisha wenyewe kwa muda mrefu. ‘Wanatheolojia wote wakuu wa kabla ya baraza la Nisea waliamini katika cheo kidogo [cha Logosi] kwa Mungu.’”
Kupatana na hilo, R. P. C. Hanson, katika The Search for the Christian Doctrine of God, hutaarifu hivi:
“Hapana mwanatheolojia katika Kanisa la Mashariki au Magharibi kabla ya kutokea kwa Mabishano ya Aria [katika karne ya nne], ambaye hamwoni Mwana kwa njia fulani kuwa mdogo kwa Baba.”
Dakt. Alvan Lamson, katika The Church of the First Three Centuries, huongeza ushuhuda huu kuhusu fundisho la wenye mamlaka wa kanisa kabla ya Baraza la Nisea (325 W.K.):
“[Fundisho la] cheo cha chini cha Mwana kwa ujumla, ikiwa si kwa upatani kabisa, lilifundishwa bila kutiliwa shaka na Mababa wa kabla ya [Baraza la] Nisea . . . Kwamba walimwona Mwana kuwa tofauti na Baba ni dhahiri kutokana na hali ambazo katika hizo wao hufundisha waziwazi bila kutilia shaka cheo chake cha chini. . . . Wao walimwona kuwa tofauti na [kuwa ni] mdogo.”
Hali kadhalika, katika kitabu Gods and the One God, Robert M. Grant husema yafuatayo juu ya wateteaji-ukristo:
“Fundisho la Kikristo la wateteaji-ukristo, kama lile la Agano Jipya, kwa msingi ni la kuamini cheo kidogo [cha Mwana]. Sikuzote Mwana ni mdogo kuliko Baba, ambaye ndiye Mungu mmoja wa Agano la Kale. . . . Tupatacho katika watungaji vitabu hao wa mapema, si fundisho la Utatu . . . Kabla ya Nisea, theolojia ya Ukristo ilikuwa karibu inakubaliwa na wote kuwa ya cheo kidogo [cha Mwana].”
Utatu wa Jumuiya ya Wakristo hufundisha kwamba Mwana yu sawa na Mungu Baba katika umilele, uweza, cheo, na hekima. Lakini Wateteaji-Ukristo walisema kwamba Mwana si sawa na Mungu Baba. Wao walimwona Mwana kuwa mdogo. Hilo si fundisho la Utatu.
Kuonyesha Fundisho la Karne ya Kwanza
Wateteaji-Ukristo na Mababa wengine wa Kanisa la mapema walionyesha kwa kadiri kubwa yale waliyofundisha Wakristo wa karne ya kwanza juu ya uhusiano wa Baba na Mwana. Angalia jinsi hilo limesemwa katika kitabu The Formation of Christian Dogma:
“Katika enzi ya Ukristo wa Mapema hakukuwa na ishara yoyote ya aina ya tatizo au bishano kuhusu Utatu, kama lile lililotokeza baadaye mahitilafiano katika Kanisa. Pasipo shaka sababu ya hilo ilikuwa uhakika wa kwamba, kwa Ukristo wa Mapema, Kristo alikuwa . . . mtu wa ulimwengu wa malaika wa kimbingu wa hali ya juu, ambaye aliumbwa na kuchaguliwa na Mungu kwa ajili ya kazi ya kuleta, . . . Ufalme wa Mungu mwishoni mwa enzi.”
Kuhusu zaidi fundisho la Mababa wa Kanisa wa mapema, The International Standard Bible Encyclopedia hukubali hivi:
“Katika kufikiri kwa mapema kwa Kanisa mwelekeo wakati wa kusema juu ya Mungu Baba ulikuwa kumwona Yeye kuwa kwanza, si kuwa Baba wa Yesu Kristo, bali kuwa chanzo cha watu wote. Kwa sababu hiyo Mungu Baba, ni kana kwamba, ndiye Mungu apitaye wote. Yeye ndiye huelezwa kuwa bila mwanzo, asiyeweza kufa, asiyeweza kubadilika, asiyeelezeka, asiyeonekana, na asiyeumbwa. Ni Yeye ameumba vitu vyote, kutia na kitu chenyewe kilichotumiwa katika uumbaji, pasipo kitu. . . .
“Hiyo yaelekea kudokeza kwamba Baba pekee kwa kufaa ndiye Mungu na Mwana na Roho wako hivyo wakiwa na cheo cha pili. Taarifa nyingi za mapema huonekana zikitegemeza hilo.”
Ingawa encyclopedia hiyo huendelea na kupunguza mkazo juu ya kweli hizo na kudai kwamba fundisho la Utatu lilikubaliwa katika pindi hiyo ya mapema, mambo ya hakika huonyesha uongo wa dai hilo. Fikiria maneno ya John Henry Cardinal Newman mwanatheolojia Mkatoliki mwenye sifa sana:
“Na tukubali kwamba jumla ya mafundisho yote, ambayo huzungumza juu ya Bwana wetu, yalikubaliwa kwa upatani na kwa umoja na Kanisa la Mapema . . . Lakini sivyo ilivyo kwa fundisho la Utatu la Kikatoliki. Mimi sioni ni katika maana gani yaweza kusemwa kwamba kuna upatani wa ujumla wa wenye [mamlaka wa kanisa la] mapema katika kuliunga mkono . . .
“Imani za siku hizo za mapema hazitaji . . . [Utatu] hata kidogo. Kwa kweli wao hutaja Watatu; bali kwamba kuna fumbo lolote katika fundisho, kwamba Watatu hao ni Mmoja, kwamba Wao ni wenye usawa, wenye umilele sawa, wote hawakuumbwa, wote wenye nguvu zote, wote ni wasiofahamika, haisemwi [nao], wala haingeweza kamwe kupatikana kutoka kwao.”
Yale Aliyofundisha Justin Martyr
Mmojawapo Wateteaji-Ukristo wa mapema zaidi alikuwa Justin Martyr, ambaye aliishi kutoka yapata 110 hadi 165 W.K. Hakuna yoyote ya maandishi yake yaliyopo hutaja watu watatu wenye usawa katika Mungu mmoja.
Kwa mfano, kulingana na Jerusalem Bible ya Katoliki, Mithali 8:22-30 husema hivi kuhusu Yesu kabla hajawa binadamu: “Yahweh aliniumba wakati kusudi lake lilipofunguka kwanza, kabla ya kazi zake za zamani zaidi. . . . Kilindi hakikuwako, nilipozaliwa . . . Kabla ya vilima, nikapata kuzaliwa . . . Nilikuwa kando yake [Mungu], nikiwa fundi stadi.” Akizungumza juu ya mistari hii, Justin husema hivi katika kitabu chake Dialogue With Trypho:
“Andiko limetangaza wazi kwamba Uzao huu ulizaliwa na Baba kabla ya vitu vyote kuumbwa; na yeyote atakubali kwamba, kihesabu huyo aliyezaliwa ni tofauti na yule azaaye.”
Kwa kuwa Mwana alizaliwa kutoka kwa Mungu, Justin hutumia usemi “Mungu” kuhusiana na Mwana. Yeye husema hivi katika kitabu chake First Apology: “Baba wa ulimwengu wote mzima ana Mwana; ambaye pia, akiwa Neno mzaliwa wa kwanza wa Mungu, ni Mungu hata yeye.” Biblia pia humwita Mwana wa Mungu kwa jina la cheo “Mungu.” Kwenye Isaya 9:6 yeye huitwa “Mungu Mweza.” Lakini katika Biblia, malaika, wanadamu, miungu bandia, na Shetani pia wanaitwa “miungu.” (Malaika: Zaburi 8:5; linganisha Waebrania 2:6, 7. Wanadamu: Zaburi 82:6. Miungu bandia: Kutoka 12:12; 1 Wakorintho 8:5. Shetani 2 Wakorintho 4:4) Katika Maandiko ya Kiebrania, neno litafsiriwalo “Mungu,” ʼEl, humaanisha tu “Mwenye Uweza” au “Mwenye Nguvu.” Neno linalolingana katika Maandiko ya Kigiriki ni the.os’.
Zaidi ya hilo, neno la Kiebrania lililotumiwa kwenye Isaya 9:6 huonyesha tofauti kati ya Mwana na Mungu. Humo Mwana huitwa “Mungu Mweza”, ʼEl Gib.bohr’, si “Mungu Mweza Yote.” Neno hilo katika Kiebrania ni ʼEl Shad.dai’ na hutumiwa kipekee kwa Yehova Mungu.
Hata hivyo, angalia kwamba, ingawa Justin humwita Mwana “Mungu,” yeye hasemi hata kidogo kwamba Mwana ni mmoja wa watu watatu walio sawa, kila mmoja wao akiwa Mungu lakini wakifanyiza Mungu mmoja tu. Badala ya hivyo, yeye husema katika kitabu chake Dialogue With Trypho:
“Kuna . . . Mungu na Bwana mwingine [Yesu kabla ya kuwa binadamu] ambaye hutii Mfanyi wa vitu vyote [Mungu Mweza Yote]; ambaye [Mwana] pia huitwa Malaika, kwa sababu Yeye [Mwana] hutangazia watu lolote ambalo Mfanyi wa vitu vyote—ambaye juu yake hapana Mungu mwingine—atakalo kuwatangazia wao. . . .
“[Mwana] ni tofauti na Yeye ambaye alifanya vitu vyote,—namaanisha kihesabu, si [tofauti] katika mapenzi.”
Fungu la maneno lenye kupendeza huonekana katika First Apology cha Justin, sura ya 6, ambapo yeye hutetea dhidi ya shtaka la kipagani kwamba Wakristo hawaamini kuwako kwa Mungu. Aandika hivi:
“Wote wawili Yeye [Mungu], na Mwana (ambaye alitoka Kwake akatufundisha mambo hayo, na umati wa malaika wengine wema ambao hufuata na [ambao] wamefanyizwa kwa mfano Wake), na Roho ya kiunabii, twaabudu na kuheshimu sana.”
Mtafsiri wa fungu hili la maneno, Bernhard Lohse, hutoa maelezo haya: “Kana kwamba haitoshi kwamba katika kutaja mmoja mmoja malaika wametajwa kuwa watu ambao huheshimiwa na kuabudiwa na Wakristo, Justin hasiti kutaja malaika kabla ya kutaja Roho Mtakatifu.”—Ona pia An Esaay on the Development of Christian Doctrine.
Hivyo, ingawa Justin Martyr huonekana kuwa alikuwa ameondoka kwenye fundisho safi la Biblia kwa habari ya kwamba ni nani ambaye apasa kuwa kitu cha kuabudiwa na Mkristo, kwa wazi yeye hakumwona Mwana kuwa sawa na Baba, kama vile malaika hawakuonwa kuwa sawa na Yeye. Kuhusu Justin, twanukuu tena kutoka kitabu cha Lamson Church of the First Three Centuries:
“Justin alimwona Mwana kuwa tofauti na Mungu, na aliye chini yake: tofauti, si katika maana ya ki-siku-hizi, kuwa akifanyiza mmoja wa watu watatu, . . . bali tofauti katika nafsi na asili; akiwa na uhai wake binafsi, ulio halisi, hakika, ulio mbali na Mungu, ambaye kutoka kwake alipata nguvu na vyeo vyake vyote; akiwa amefanyizwa chini yake, na ametiishwa kwa mapenzi yake katika mambo yote. Baba ni mkuu kupita wote; Mwana ni mdogo: Baba ndiye chanzo cha nguvu; Mwana ni mpokeaji: Baba huanzisha; Mwana, akiwa mhudumu au chombo cha kutumiwa, hutekeleza. Kwa hesabu ni wawili, lakini hukubaliana, au wako mmoja, katika mapenzi; sikuzote mapenzi ya Baba yakimwongoza Mwana.”
Kwa kuongeza, hapana mahali popote ambapo Justin husema kwamba roho takatifu ni mtu aliye sawa na Baba na Mwana. Kwa hiyo haiwezi kusemwa kwa unyofu katika maana yoyote kwamba Justin alifundisha Utatu wa ki-siku-hizi wa Jumuiya ya Wakristo.
Yale Ambayo Klementi Alifundisha
Klementi wa Aleksandria (yapata 150 hadi 215 W.K.) pia humwita Mwana “Mungu.” Hata humwita “Muumba,” neno ambalo halitumiwi kamwe katika Biblia kumwita Yesu. Je! yeye alimaanisha kwamba Mwana alikuwa sawa na Muumba mweza yote katika njia zote? Hapana. Kwa wazi Klementi alikuwa akirejezea Yohana 1:3, ambalo husema juu ya Mwana: “Vyote vilifanyika kwa huyo.” Mungu alitumia Mwana akiwa wakala katika kazi Zake za kuumba.—Wakolosai 1:15-17.
Klementi humwita yule Mungu Mkuu Kupita Wote “Mungu na Baba ya Bwana yetu Yesu” na kusema kwamba “Bwana ni Mwana wa Muumba.” Pia yeye husema: “Mungu wa wote ni Muumba mmoja tu aliye mwema na mwenye haki, na Mwana [yu] katika Baba.” Hivyo yeye aliandika kwamba Mwana ana Mungu aliye juu yake.
Klementi hunena juu ya Mungu kuwa “mtoaji wa kwanza na wa pekee wa uhai wa milele, ambao Mwana, aliyeupokea Kwake [Mungu], hutupa sisi.” Mpaji wa kwanza wa uhai wa milele kwa wazi ni mkuu kuliko yeye ambaye, ni kana kwamba, huupitisha. Hivyo, Klementi husema kwamba Mungu “ni wa kwanza, na apita wote.” Zaidi ya hilo, yeye husema kwamba Mwana “ndiye akaribiaye zaidi Yeye ambaye ni Mweza Yote pekee” na kwamba Mwana “huratibu vitu vyote kupatana na mapenzi ya Baba.” Mara nyingi sana Klementi huonyesha ukuu upitao wote wa Mungu Mweza Yote juu ya Mwana.
Kuhusu Klementi wa Aleksandria, twasoma hivi katika The Church of the First Three Centuries:
“Twaweza kunukuu vifungu vingi vya maneno kutoka kwa Klementi ambavyo katika hivyo cheo cha chini cha Mwana hufundishwa waziwazi bila kutiliwa shaka yoyote. . . .
“Tunashangaa kwamba yeyote anaweza kusoma kwa umakini wa kawaida kitabu cha Klementi, na kuwazia kwa kitambo kidogo kwamba yeye alimwona Mwana kuwa sawa kihesabu—mmoja—na Baba. Hali yake ya kutegemea na iliyo ya chini, kama ionekanavyo kwetu, yatambuliwa kila mahali. Klementi aliamini Mungu na Mwana walikuwa tofauti kihesabu; yaani, watu wawili—yule mmoja mkuu kupita wote, na yule mwingine mdogo.”
Zaidi ya hilo, yaweza kusemwa tena: Hata kama Klementi huonekana akipita yale ambayo Biblia husema juu ya Yesu, hapana mahali popote ambapo yeye hunena juu ya Utatu unaofanyizwa na watu watatu walio sawa katika Mungu mmoja. Wateteaji-Ukristo kama vile Tatian, Theofilo, na Athenagoras, walioishi kati ya wakati wa Justin na Klementi, walikuwa na maoni ayo hayo. Lamson husema kwamba “hawakuwa Wanautatu bora zaidi ya Justin mwenyewe; yaani, wao hawakuamini katika [watu] Watatu walio sawa, wasiogawanyika, bali walifundisha fundisho lisiloweza kupatanishwa kabisa na imani hiyo.”
Theolojia ya Tertuliano
Tertuliano (yapata 160 hadi 230 W.K.) alikuwa wa kwanza kutumia neno la Kilatini trinitas. Kama ilivyotajwa na Henry Chadwick, Tertuliano alitokeza wazo la kwamba Mungu ni ‘kitu kimoja chenye watu watatu.’ Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba akilini yeye alikuwa na wazo la watu watatu walio sawa na wenye umilele sawa. Walakini, mawazo yake yaliongezewa na waandikaji wa baadaye ambao walikuwa wakisonga mbele kuelekea fundisho la Utatu.
Ufahamu wa Tertuliano juu ya Baba, Mwana, na roho takatifu ulikuwa tofauti sana na Utatu wa Jumuiya ya Wakristo, kwa kuwa yeye aliamini katika cheo kidogo cha Mwana. Alimwona Mwana kuwa mdogo kwa Baba. Katika kichapo Against Hermogenes yeye aliandika hivi:
“Haitupasi kudhani kwamba kuna mtu mwingine isipokuwa Mungu pekee ambaye hakuzaliwa na hakuumbwa. . . . Yawezaje kuwa chochote, isipokuwa Baba, chapasa kuwa chenye umri mkubwa zaidi, na kwa habari hiyo kwa kweli chenye cheo bora zaidi, ya Mwana wa Mungu, Neno mzaliwa-pekee na mzaliwa-wa-kwanza? . . . Kwamba [Mungu] ambaye hakuhitaji Mfanyi ili kumfanya aweko, atakwezwa zaidi sana katika cheo kuliko huyo [Mwana] ambaye alikuwa na mwanzilishi wa kumwezesha aweko.”
Pia, katika kichapo Against Praxeas, yeye huonyesha kwamba Mwana ni tofauti na ni mdogo kuliko Mungu Mweza Yote kwa kusema:
“Baba ndiye kitu chote kizima, bali Mwana hutolewa kwa na ni sehemu ya hicho chote kizima, kama vile Yeye Mwenyewe hukiri: ‘Baba yangu ni mkuu kuliko mimi.’ . . . Hivyo Baba ni tofauti na Mwana, akiwa mkuu kuliko Mwana, kwa kuwa Yeye azaaye ni mmoja, na Yeye azaliwaye ni mwingine; Yeye, pia, atumaye ni mmoja, na Yeye atumwaye ni mwingine; na Yeye, tena, afanyizaye ni mmoja, na Yeye ambaye kupitia kwake kitu hufanyizwa ni mwingine.”
Tertuliano, katika Against Hermogenes, hutaarifu zaidi kwamba kulikuwako wakati ambao Mwana hakuwako akiwa mtu, kuonyesha kwamba yeye hakumwona Mwana kuwa mtu wa milele katika maana ile ile alivyokuwa Baba. Cardinal Newman alisema: “Lazima Tertuliano aonwe kuwa heterodoksi [mwamini wa mafundisho yasiyo ya kiorthodoksi] kuhusu fundisho la uzaliwa wa umilele wa Bwana yetu.” Kuhusu Tertuliano, Lamson hutangaza hivi:
“Huyo fikira, Logosi, kama alivyoitwa na Wagiriki, baadaye, kama alivyoamini Tertuliano, aligeuzwa kuwa Neno, au Mwana, yaani, mtu halisi, akiwa amekuwako tangu umilele akiwa tu sifa ya Baba. Hata hivyo, Tertuliano alimhesabia cheo kidogo kuliko cha Baba . . .
“Akihukumiwa kulingana na maelezo yoyote yaliyokubaliwa kwa ujumla juu ya Utatu wa siku za sasa, jaribio lolote la kumwokoa Tertuliano kutoka hukumu mbaya [akiwa mzushi] lingekuwa bure. Yeye hangeweza kustahimili jaribu hilo kwa kitambo kidogo.”
Hakuna Utatu
Kama ungesoma maneno yote ya Wateteaji-Ukristo, ungepata kwamba ingawa waliondoka katika mafundisho ya Biblia kwa njia fulani, hapana yeyote wao alifundisha kwamba Baba, Mwana, na roho takatifu walikuwa sawa katika umilele, nguvu, cheo, na hekima.
Ndivyo ilivyo pia kwa waandikaji wengine wa karne ya pili na ya tatu, kama vile Irenayo, Hippolytus, Origen, Cyprian, na Novatian. Ingawa wengine wafikia kuwaweka Baba na Mwana katika hali sawa katika njia fulani, katika njia nyinginezo walimwona Mwana kuwa mdogo kwa Mungu Baba. Na hapana yeyote wao hata alikisia kwamba roho takatifu ilikuwa sawa na Baba na Mwana. Kwa mfano, Origen (yapata 185 hadi 254 W.K.) hutaarifu kwamba Mwana wa Mungu ndiye “mzaliwa-wa-kwanza wa viumbe vyote” na kwamba Maandiko “hujua Yeye kuwa ndiye wa kale zaidi katika kazi zote za uumbaji.”
Usomaji wowote wa bila mafasirio ya kibinafsi wa maandishi ya wenye mamlaka hao wa mapema wa kanisa utaonyesha kwamba fundisho la Utatu la Jumuiya ya Wakristo halikuwako katika wakati wao. Kama The Church of the First Three Centuries husema:
“Fundisho la ki-siku-hizi la Utatu lenye kupendwa na wengi . . . haliungwi mkono na maandishi ya Justin: na maoni hayo yaweza kutumiwa kuhusu Mababa wote waliokuwa kabla ya [baraza la] Nisea; yaani, waandikaji wote Wakristo wa karne tatu baada ya kuzaliwa kwa Kristo. Ni kweli, wao husema juu ya Baba, Mwana, na yule wa kiunabii, au Roho takatifu, lakini si wakiwa sawa, si wakiwa kitu kimoja kihesabu, si wakiwa Watatu katika Mmoja, katika maana yoyote inayokubaliwa sasa na Wanautatu. Kinyume kabisa ndio uhakika. Fundisho la Utatu, kama lielezwavyo na Mababa hao, kwa msingi lilikuwa tofauti na fundisho la ki-siku-hizi. Twataarifu hivyo ukiwa uhakika ambao utastahimili jaribu kama uhakika wowote katika historia ya maoni ya kibinadamu.”
Kwa kweli, kabla ya Tertuliano Utatu hata haukuwa umetajwa. Na Utatu wa Tertuliano wa “heterodoksi” ulikuwa tofauti sana na ule unaoaminiwa leo. Basi, fundisho la Utatu, kama linavyoeleweka leo, lilisitawije? Je! ilikuwa ni wakati wa Baraza la Nisea katika 325 W.K.? Tutachunguza maswali hayo katika Sehemu ya 4 ya mfululizo huu katika toleo la wakati ujao la Mnara wa Minzi.
Marejezeo:
1. A Short History of the Early Church, by Harry R. Boer, 1976, page 110.
2. The Formation of Christian Dogma, by Martin Werner, 1957, page 125.
3. The Search for the Christian Doctrine of God, by R. P. C. Hanson, 1988, page 64.
4. The Church of the First Three Centuries, by Alvan Lamson, 1869, pages 70-1.
5. Gods and the One God, by Robert M. Grant, 1986, pages 109, 156, 160.
6. The Formation of Christian Dogma, pages 122, 125.
7. The International Standard Bible Encyclopedia, 1982, Volume 2, page 513.
8. An Essay on the Development of Christian Doctrine, by John Henry Cardinal Newman, Sixth Edition, 1989, pages 14-18.
9. The Ante-Nicene Fathers, edited by Alexander Roberts and James Donaldson, American Reprint of the Edinburgh Edition, 1885, Volume I, page 264.
10. Ibid., page 184.
11. The Ante-Nicene Fathers, Volume 1, page 223.
12. Ibid., page 164.
13. A Short History of Christian Doctrine, by Bernhard Lohse, translated from the German by F. Ernest Stoefller, 1963, second paperback printing, 1980, page 43.
14. An Essay on the Development of Christian Doctrine, page 20.
15. The Church of the First Three Centuries, pages 73-4, 76.
16. The Ante-Nicene Fathers, Volume II, page 234.
17. Ibid., page 227.
18. Ibid., page 228.
19. Ibid.
20. Ibid., page 593.
21. Ibid.
22. Ibid., page 524.
23. The Church of the First Three Centuries, pages 124-5.
24. Ibid., page 95.
25. The Early Church, by Henry Chadwick, 1980 printing, page 89.
26. The Ante-Nicene Fathers, Volume III, page 487.
27. Ibid., pages 603-4.
28. Ibid., page 478.
29. An Essay on the Development of Christian Doctrine, pages 19, 20.
30. The Church of the First Three Centuries, pages 108-9.
31. The Ante-Nicene Fathers, Volume IV, page 560.
32. The Church of the First Three Centuries, pages 75-6.
[Picha katika ukurasa wa 27]
Klementi
[Hisani]
Historical Pictures Service
[Picha katika ukurasa wa 28]
Tertuliano
[Hisani]
Historical Pictures Service