Uumbaji Husema, ‘Hawana Udhuru’
“Sifa zake zisizoonekana zinaonekana wazi tangu kuumbwa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zinafahamika kwa vitu vile vilivyofanywa, hata uweza wake wa milele na Uungu, hata wasiwe na udhuru.”—WARUMI 1:20, NW.
1, 2. (a) Ayubu alimlalamikia Yehova kwa uchungu juu ya nini? (b) Baadaye Ayubu alionyeshaje maoni tofauti kabisa?
AYUBU, mtu wa nyakati za kale aliyekuwa na uaminifu-maadili usiovunjika kwa Yehova Mungu, alikuwa ametahiniwa vibaya sana na Shetani. Ibilisi alimsababisha Ayubu apoteze mali zake zote za kimwili, alikuwa ameleta kifo cha wana na binti zake, na alikuwa amemtesa kwa ugonjwa wenye kuchukiza sana. Ayubu alifikiri ni Mungu aliyekuwa akileta misiba hiyo juu yake, naye akamlalamikia Yehova kwa uchungu hivi: “Je! ni vema kwako wewe kuonea, . . . hata ukauliza-uliza habari za uovu wangu, na kuitafuta dhambi yangu, ujapojua ya kuwa mimi si mwovu?”—Ayubu 1:12-19; 2:5-8; 10:3, 6, 7.
2 Muda fulani baada ya hayo, maneno ya Ayubu kwa Mungu yalionyesha hali tofauti kabisa: “Nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua. Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu.” (Ayubu 42:3, 5, 6) Ni nini kilichokuwa kimetokea ili kubadili mtazamo wa Ayubu?
3. Ayubu alipata maoni gani mapya juu ya uumbaji?
3 Katika muda wa kati, Yehova alikuwa amemkabili Ayubu katika upepo wa kisulisuli. (Ayubu 38:1) Alikuwa amemwuliza Ayubu maswali mengi. ‘Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya dunia? Ni nani aliyeifunga bahari kwa milango na kuyawekea mipaka mawimbi yayo? Je! waweza kuyasababisha mawingu yamwage mvua yayo duniani? Waweza kukuza nyasi? Waweza kukusanya pamoja sayari na kuziongoza katika miendo yazo?’ Kotekote katika sura 38 hadi 41 za kitabu cha Ayubu, Yehova alimwuliza Ayubu maswali mengi ya jinsi hiyo na mengi zaidi juu ya uumbaji Wake. Alimfanya Ayubu aone lile pengo kubwa mno kati ya Mungu na mwanadamu, akimkumbusha Ayubu kwa nguvu juu ya hekima na nguvu zinazoonyeshwa katika uumbaji wa Mungu, mambo yanayozidi kwa mbali nguvu za Ayubu kuyafanya au hata kuyaelewa. Ayubu, akiwa ameshindwa na nguvu zenye kutisha na hekima ya ajabu sana ya Mungu mweza yote kama ilivyofunuliwa kupitia uumbaji wake, alichukizwa kufikiri kwamba alikuwa amedhubutu kubishana na Yehova. Kwa hiyo alisema hivi: “Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; bali sasa jicho langu linakuona.”—Ayubu 42:5.
4. Twapaswa kufahamu nini kutokana na uumbaji mbalimbali wa Yehova, na wale wanaoshindwa kuliona jambo hilo wana hali gani?
4 Karne nyingi baadaye mwandishi mmoja wa Biblia aliyepuliziwa alithibitisha kwamba sifa za Yehova zingeweza kuonwa kupitia uumbaji wake. Mtume Paulo aliandika hivi kwenye Warumi 1:19, 20, NW: “Sifa zake zisizoonekana zinaonekana wazi tangu kuumbwa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zinafahamika kwa vitu vile vilivyofanywa, hata uweza wake wa milele na Uungu, hata wasiwe na udhuru.”
5. (a) Wanadamu wana uhitaji gani wa asili, na wengine huitimizaje uhitaji huo isivyofaa? (b) Pendekezo la Paulo kwa Wagiriki katika Athene lilikuwa nini?
5 Mwanadamu aliumbwa akiwa na uhitaji wa asili wa kuabudu nguvu iliyo juu zaidi. Dakt. C. G. Jung, katika kitabu chake The Undiscovered Self, alirejezea uhitaji huo kuwa “mtazamo wa kisilika ulio wa mwanadamu pekee, na umedhihirishwa kwa njia mbalimbali muda wote wa historia ya kibinadamu.” Mtume Paulo alisema juu ya uhitaji wa asili wa mwanadamu kuabudu, jambo lililoeleza ni kwa nini Wagiriki katika Athene walifanya mifano na madhabahu kwa miungu mingi, iliyojulikana na isiyojulikana. Paulo pia alimtambulisha Mungu wa kweli kwao na akaonyesha kwamba walipaswa waridhishe uhitaji huo wa asili ifaavyo kwa kumtafuta Yehova Mungu wa kweli, “ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.” (Matendo 17:22-30) Kadiri tulivyo karibu na uumbaji wake, ndivyo tulivyo karibu kuweza kufahamu sifa na njia zake.
Kawaida ya Maji Iliyo ya Ajabu
6. Ni sifa zipi za Yehova tunazoona katika kawaida ya maji?
6 Kwa kielelezo, ni sifa zipi za Yehova tunazofahamu katika ule uwezo wa mawingu laini, wa kushikilia tani kadhaa za maji? Twaona upendo na hekima yake, kwani hivyo yeye huandaa manyunyu ya mvua kwa baraka ya dunia. Yeye hufanya hivyo kwa njia ya ule utaratibu mzuri ajabu unaohusika katika ile kawaida ya maji, inayotajwa kwenye Mhubiri 1:7: “Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena.” Kitabu cha Biblia cha Ayubu hueleza hasa jinsi ambavyo hilo hutukia.
7. Maji hutokaje kwa bahari hadi kwenye mawingu, na mawingu laini yanaweza kushikaje tani kadhaa za maji?
7 Mito inapoingia baharini, haibaki humo. Yehova “huvuta juu matone ya maji, yamwagikayo katika mvua kutoka kungeni mwake.” Kwa sababu maji hayo yamo katika namna ya mvuke na mwishoni yanakuwa kungugu (matone ya maji) laini, “mawingu huning’inia kwa utulivu yakiwa juu, kazi nzuri ajabu ya ustadi wake mkamilifu.” (Ayubu 36:27; 37:16; The New English Bible) Mawingu huelea maadamu ni kungugu: “Yeye huyashikamanisha maji katika mawingu yake—na kungugu hazivunjiki chini ya uzito wazo.” Au kama vile tafsiri nyingine husema: “Yeye huyafunga maji katika vifungu vizito, na mawingu hayafunguki kwa kishindo chini ya uzito wayo.”—Ayubu 26:8, The Jerusalem Bible; NE.
8. “Chupa za mbinguni” humiminwa kwa hatua zipi tofauti ili kawaida ya maji ikamilike?
8 “Ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni” ili kusababisha mvua ianguke duniani? (Ayubu 38:37) Yule ambaye kwa “ustadi wake mkamilifu” aliziweka hapo mwanzoni, ambaye “huvuta juu matone ya maji, yamwagikayo katika mvua kutoka kungeni mwake.” Na ni nini kinachohitajiwa ili kuvuta juu matone ya maji kutoka kungeni? Lazima kuwa kitu kidogo mno chenye uzani, kama vile mavumbi au chembe za chumvi—kutoka maelfu hadi mamia ya maelfu yavyo katika kila sentimeta ya mraba ya hewa—viwe kama viini ili matone yafanyizwe kando-kando yavyo. Imekadiriwa kwamba milioni moja ya yale matone madogo mno ya mawingu yanahitajiwa ili kufanyiza tone moja la mvua. Ni baada tu ya mambo hayo yote kutukia ndipo mawingu yawezayo kumwaga mvua yayo duniani ili kufanyiza vijito vinavyorudisha maji hayo baharini. Hivyo kawaida ya maji hujikamilisha. Je! hayo yote yalitukia tu bila mwongozo? Kwa kweli maoni kama hayo hayana “udhuru”!
Chanzo Kimoja cha Hekima ya Sulemani
9. Sulemani aliona jambo gani kuwa la ajabu kuhusu aina moja ya chungu?
9 Katika ulimwengu wa kale, hekima ya Sulemani haikuwa na kifani. Sehemu kubwa ya hekima hiyo ilihusu uumbaji wa Yehova: “[Sulemani] akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.” (1 Wafalme 4:33) Ndiye Mfalme Sulemani uyo huyo aliyeandika hivi: “Ewe mvivu, mwendee chungu, zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa kuwa yeye hana akida, wala msimamizi, wala mkuu, lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.”—Mithali 6:6-8.
10. Kielezi cha Sulemani kuhusu chungu wenye kuvuna kilitetewaje?
10 Ni nani aliyewafundisha chungu waweke akiba ya chakula katika kiangazi ya kuwalisha wakati wa kipupwe chenye ubaridi? Kwa karne kadhaa usahihi wa usimulizi wa Sulemani wa chungu hao ulitiliwa shaka. Hakuna aliyekuwa amepata uthibitisho wowote wa kuwako kwao. Hata hivyo, katika 1871, mtaalamu mmoja wa asili kutoka Uingereza, aligundua ghala zao za chini ya ardhi, na usahihi wa Biblia katika kuripoti juu yao ukatetewa. Lakini chungu hao walipata wapi mwono wa kimbele kujua katika kiangazi kwamba ubaridi wa kipupwe ulikuwa ukija na hekima ya kujua jambo la kufanya juu ya habari hiyo? Biblia yenyewe hueleza kwamba viumbe vingi vya Yehova vina hekima iliyopangwa ndani yavyo ili viweze kuokoka. Chungu mwenye kuvuna ni wapokeaji wa baraka hiyo kutoka kwa Muumba wao. Mithali 30:24, NW, yasema juu ya hilo: “Wao ni wenye hekima kisilika.” Kusema kwamba hekima hiyo ingeweza kutukia tu bila mwongozo si kusababu ifaavyo; kushindwa kumfahamu Muumba mwenye hekima aliye chanzo chalo hakuna udhuru.
11. (a) Kwa nini ule mti sekoia mkubwa mno ni wenye kutisha sana? (b) Ni nini kinachostaajabisha sana juu ya utaratibu wa kwanza katika usanidimwanga (fotosinthesisi)?
11 Kwa kueleweka, mtu aliye chini ya mti sekoia ulio kubwa mno, anayestaajabia utukufu wao mwingi sana, hujihisi kama chungu mdogo. Ukubwa wa mti huo ni wenye kutisha: urefu wa meta 90, wenye kipenyo cha meta 11, na gamba lenye unene wa meta 0.6, mizizi ikienea kufikia hektari 7 hadi 10. Hata hivyo, jambo lenye kutisha hata zaidi ni kemia (muundo) na fizikia (hali) inayohusika na ukuzi wao. Majani yao hutwaa maji kutoka kwa mizizi, kaboni dayoksaidi kutoka kwa hewa, na nishati kutoka kwa jua ili kutengeneza sukari na kutoa oksijeni—utaratibu uitwao usanidimwanga (fotosinthesisi) unaohusisha taratibu za kemia karibu 70, ambazo si zote zinazoeleweka. Kwa kustaajabisha, utaratibu wa kwanza hutegemea mwangaza wa jua wenye rangi hususa, na wenye urefu hususa wa wimbi; ama sivyo isingetwaliwa na zile chembe ndogo za klorofili (kemikali ya rangi ya kijani) ili kuanzisha ule utaratibu wa usanidimwanga.
12. (a) Ni nini lililo la ajabu kuhusu matumizi ya maji ya mti sekoia? (b) Kwa nini nitrojeni huhitajiwa katika ukuzi wa mmea, na kawaida yayo hukamilishwaje?
12 Jambo linaostaajabisha pia ni kwamba mti huo unaweza kuvuta juu safu za maji kutoka kwa mizizi hadi kilele cha mti huo mkubwa mno wa meta 90. Maji mengi zaidi huvutwa kuliko yale yanayohitajiwa kwa ajili ya usanidimwanga. Majani huyaondoa maji ya ziada hewani kupitia transpiresheni (upoteaji wa maji hewani kupitia majani). Hiyo inafanya mti upozwe na maji, kama vile tunavyopozwa na jasho. Ili kufanyiza protini kwa ajili ya ukuzi, nitrojeni inahitaji kuongezwa kwenye sukari, au kabohidrati (chakula chenye asili ya sukari). Jani haliwezi kutumia nitrojeni ya namna ya gesi kutoka hewani, lakini viumbe hai vilivyomo udongoni vyaweza kugeuza nitrojeni ya namna ya gesi iliyomo ardhini iwe nitrati na nitriti (chumvi kutoka kwa gesi nitrojeni) zinazoweza kumumunyika katika maji, ambayo sasa husafiri kutoka mizizi hadi kwenye majani. Mimea na wanyama ambao wametumia hiyo nitrojeni katika protini zao wanapokufa na kuoza, nitrojeni hiyo inatoka, ikikamilisha kawaida ya nitrojeni. Katika hayo yote, yale mambo magumu yanayohusika ni ya ajabu sana, yasiweze kutimizwa bila mwongozo fulani.
Hizo Husema, Bila Usemi Wala Maneno Wala Sauti!
13. Mbingu zenye nyote zilimtangazia Daudi nini, nazo huendelea kutuambia nini?
13 Anga la usiku lenye nyota ni wonyesho wa Muumba wenye kutisha kama nini unaowajaza watazamaji na kicho! Kwenye Zaburi 8:3, 4, Daudi alionyesha jinsi alivyohisi kutishwa: “Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizoziratibisha; mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie?” Kwa wale walio na macho ya kuona, masikio ya kusikiliza, na moyo wa kuhisi, mbingu hizo zenye nyota husema nao, kama vile zilivyosema na Daudi: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu.”—Zaburi 19:1-4.
14. Kwa nini nishati yenye kutendesha ya mojawapo nyota ni muhimu sana kwetu?
14 Kadiri tujuavyo zaidi kuhusu nyota, ndivyo zinavyosema na sisi kwa sauti kubwa zaidi. Kwenye Isaya 40:26, tunaalikwa kutazama nishati yazo kubwa mno: “Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake [wingi wa nishati yenye kutendesha, NW], na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.” Kani ya uvutano na nishati yenye kutendesha ya moja yazo, yaani jua letu, huishika dunia katika mzunguko wayo, huikuza mimea, hutuweka tukiwa na ujoto, na kuuwezesha uhai wote ulio hapa duniani. Mtume Paulo alisema hivi chini ya upulizio: “Iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.” (1 Wakorintho 15:41) Sayansi yajua juu ya nyota za kimanjano kama jua letu, pia nyota za buluu, nyota nyekundu zilizo kubwa sana, nyota nyeupe zilizo ndogo sana, nyota za nutroni (zilizofanyizwa kwa chembe zisizo na chaji) na nyota kubwa mno zinazolipuka na kutokeza nguvu isiyoeleweka.
15. Wavumbuzi wengi wamejifunza nini na wamejaribu kuiga nini kutokana na uumbaji?
15 Wavumbuzi wengi wamejifunza kutokana na uumbaji na wamejaribu kuiga uwezo wa viumbe hai. (Ayubu 12:7-10) Ebu ona sehemu chache zenye kutokeza za uumbaji. Ndege wa bahari wenye tezi zinazoondoa chumvi kutoka kwa maji ya bahari; samaki na mikunga (samaki walio kama nyoka) wanaofanyiza stima; samaki, mabuu, na wadudu wanaotoa mng’aro; popo na dolifina wanaotumia mawimbi ya sauti kujua mahali vitu vilipo; duduvule wanaotengeneza karatasi; chungu wanaojenga madaraja; viangushamiti (beva) wanaojenga mabwawa; nyoka wenye vipimamoto vya kiasili; wadudu wa madimbwi wanaotumia mirija ya kupumulia hewa na vyombo vya kupigia mbizi vyenye hewa iliyobanwa; pweza (oktopasi) wanaotumia usukumaji wenye mshindo; buibui wanaotengeneza aina saba za tando na wanaotengeneza milango ya kunasia, nyavu, na kamba zenye tanzi na walio na watoto ambao huruka katika mifuko iliyojaa hewa, wakisafiri mwendo wa kilometa nyingi wakiwa juu sana; samaki na wanyama wenye magamba wanaotumia tangi za kuelea kama vile manowari sabmarini; na ndege, wadudu, kasa wa bahari, samaki, na mamalia wanaofanya harakati za kuhama za ajabu—uwezo mbalimbali usioweza kuelezwa na sayansi.
16. Biblia ilirekodi kweli zipi za kisayansi maelfu ya miaka kabla ya sayansi kuzigundua?
16 Biblia ilirekodi kweli za kisayansi maelfu ya miaka kabla ya sayansi kuzijua. Sheria ya Kimusa (karne ya 16 K.W.K.) ilionyesha ufahamu wa vijidudu vinavyosababisha magonjwa maelfu ya miaka kabla ya Pasteur. (Mambo ya Walawi, sura 13, 14) Katika karne ya 17 K.W.K., Ayubu alisema hivi: “Akiining’iniza dunia pasipo na kitu.” (Ayubu 26:7, NW) Miaka elfu moja kabla ya Kristo, Sulemani aliandika juu ya mzunguko wa damu; sayansi ya kitiba ilihitaji kungojea mpaka karne ya 17 W.K. ili kujifunza juu ya jambo hilo. (Mhubiri 12:6) Kabla ya wakati huo, Zaburi 139:16 ilionyesha juu ya ujuzi wa msimbo jeni (utaratibu wa urithi): “Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; chuoni mwako ziliandikwa zote pia, siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.” Katika karne ya 7 K.W.K, kabla ya wataalamu wa asili kuelewa juu ya harakati za kuhama, Yeremia aliandika, kama ilivyorekodiwa kwenye Yeremia 8:7: “Koikoi angani hujua wakati wa kuhama, hua na mbayuwayu na korongo hujua majira ya kurudi.”—NE.
“Muumbaji” Ambaye Wanamageuzi Wanachagua
17. (a) Warumi 1:21-23 husema nini juu ya wengine wanaokataa kuona kwamba ni Muumba mwenye akili aliye chanzo cha vitu vya ajabu vilivyoumbwa? (b) Katika maana fulani, wanamageuzi wanachagua nini kuwa “muumba” wao?
17 Andiko moja husema hivi kuhusu wale wanaokataa kufahamu kwamba Muumba mwenye akili ndiye chanzo cha vitu vya ajabu vilivyoumbwa: “Walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.” “Walibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba.” (Warumi 1:21-23, 25) Ndivyo ilivyo na wanasayansi wa mageuzi, ambao, kwa kweli, huutukuza kama “muumba” wao, ule mfululizo uliowaziwa tu wenye kuongezeka ubora hatua kwa hatua wa protozoa (viumbe vyenye seli moja)-mabuu-samaki-amfibia-reptilia-mamalia-“watu-nyani.” Hata hivyo, wanajua kwamba kwa kweli hakuna kiumbe hai sahili chenye chembe moja cha kuanza mfululizo huo. Kiumbe hai sahili zaidi kijulikanacho kina atomu bilioni mia moja, kukiwa na maelfu ya taratibu za kikemia yakitukia ndani yacho wakati uleule.
18, 19. (a) Ni nani Yule afaaye kuhesabiwa kuwa chanzo cha uhai? (b) Twaweza kuona kadiri gani ya uumbaji wa Yehova?
18 Yehova Mungu ndiye Muumba wa uhai. (Zaburi 36:9) Yeye ndiye Kisababishi kikuu cha Kwanza. Jina lake, Yehova, humaanisha “Yeye husababisha iwe.” Hatuwezi kuhesabu viumbe vyake. Kwa hakika hivyo ni mamilioni mengi kuliko vile ambavyo mwanadamu anafahamu. Zaburi 104:24, 25 yatoa kidokezo cha jambo hilo: “Ee BWANA [Yehova, NW], jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia.” Ayubu 26:14 linaeleza hilo kwa wazi: “Tazama, hivi ni viunga tu vya njia zake; na jinsi yalivyo madogo manong’ono tusikiayo katika habari zake! Lakini ngurumo za uweza wake ni nani awezaye kuelewa nazo?” Sisi twaona viunga vichache, twasikia manong’ono machache, lakini hatuwezi kuelewa kikamili ngurumo yake ya uweza.
19 Hata hivyo, tuna chanzo kizuri zaidi cha kumwona kuliko kupitia uumbaji wake halisi. Chanzo hicho kizuri zaidi ni Neno lake, Biblia. Tunageukia chanzo hicho sasa katika makala ifuatayo.
Je! Wakumbuka?
◻ Ayubu alipata kujifunza nini wakati Yehova aliposema naye katika upepo wa kisulisuli?
◻ Kwa nini Paulo alisema kwamba watu wengine hawakuwa na udhuru?
◻ Kawaida ya maji hufanyaje kazi?
◻ Mwangaza wa jua hutufanyia mambo gani ya muhimu?
◻ Biblia ilifunua kweli zipi za kisayansi kabla ya sayansi kuzigundua?