Rahabu—Atangazwa Kuwa Mwadilifu kwa Matendo ya Imani
EBU wazia! Kahaba atangazwa kuwa mwadilifu kwa maoni ya Mungu. “Haiwezekani kamwe!” wengi wangepaaza sauti kwa mshangao. Lakini, hilo ndilo lilimpata yule malaya Rahabu wa Yeriko, jiji la Kanaani la kale.
Mwandishi wa Biblia Yakobo arekodi hivi: “Mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake. Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! hakuhesabiwa kuwa ana haki [hakutangazwa kuwa mwadilifu, NW] kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.” (Yakobo 2:24-26) Kwa nini Rahabu alitangazwa kuwa mwadilifu? Alifanya nini ili kupokea msimamo pamoja na Mungu wenye pendeleo jinsi hiyo?
Waisraeli Wanakuja!
Ebu tufikirie mwaka wa 1473 K.W.K. Jionee akilini mandhari hii. Yeriko limeimarishwa sana. Nyumba ya Rahabu yule kahaba iko juu ya kuta za jiji hilo. Kutoka mahali hapo pafaapo, yaelekea kwamba aweza kutazama mashariki kuelekea maji yaliyofurika ya mto Yordani. (Yoshua 3:15) Kwenye ukingo wao wa mashariki, huenda akawa aliweza kuona kambi ya Waisraeli, yenye wanajeshi zaidi ya 600,000. Wako kilometa chache tu kutoka hapo!
Rahabu amejifunza juu ya ushindi mbalimbali wa kivita wa Israeli. Pia amesikia juu ya maonyesho ya nguvu za Yehova, hasa katika kuwafungulia Waisraeli njia ya kuponyokea kupitia Bahari Nyekundu. Basi, kwa hakika, yale maji yaliyofurika ya Yordani hayatakuwa kizuizi. Huu ni wakati wa hatari! Rahabu ataitikia kwa tendo gani?
Rahabu Achukua Msimamo Wake
Upesi, Rahabu apokea wageni wawili wasiotazamiwa—wapelelezi kutoka kambi ya Waisraeli. Wao watafuta mahali pa kukaa, naye awaruhusu waingie nyumbani mwake. Lakini mfalme wa Yeriko apata habari kuhusu kuwapo kwao. Upesi awatuma maofisa wake wa kutekeleza sheria waende kuwakamata.—Yoshua 2:1, 2.
Kufikia wakati ambapo maofisa wa mfalme wawasili, Rahabu amekwisha kuchukua msimamo wake kwa ajili ya Yehova Mungu. “Watoe watu wale waliokuja kwako,” wale maofisa wa mfalme waamuru. Rahabu amewaficha wapelelezi hao miongoni mwa mabua ya kitani yaliyotandikwa juu ya dari ili kukauka. Yeye asema: “Naam, wale watu walikuja kwangu, lakini sijui walikotoka; ikawa kama wakati wa kufungwa lango la mji, kulipokuwa giza, watu wale wakatoka, wala sijui walikokwenda; wafuatieni upesi, maana mtawapata.” (Yoshua 2:3-5) Watu wa mfalme wafanya hivyo—bila matokeo.
Rahabu wamewaongoza maadui hao vibaya. Mara hiyo achukua hatua nyingine zinazoonyesha imani yake katika Yehova kwa matendo. Aenda kwenye dari na kuwaambia wapelelezi hao hivi: “Mimi najua ya kuwa BWANA [Yehova, NW] amewapa ninyi nchi hii.” Rahabu akiri kwamba wakazi wote wa bara hilo wanaogopa sababu wamesikia jinsi Mungu “alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu” mbele ya Waisraeli miaka 40 kabla ya hapo. Watu wajua pia kwamba Waisraeli waliangamiza wafalme wawili Waamori. “Mara tuliposikia hayo,” asema Rahabu, “mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa BWANA [Yehova, NW] Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini.”—Yoshua 2:8-11.
Rahabu asihi hivi: “Basi sasa, nawasihi, niapieni kwa BWANA [Yehova, NW], kwa kuwa nimewatendea ihisani, ya kwamba ninyi nanyi mtaitendea ihisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu; ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na wanawake, na vitu vyote walivyo navyo.”—Yoshua 2:12, 13.
Wanaume hao wakubali na wamwambia Rahabu jambo la kufanya. Ni lazima afunge dirishani pake ile kamba nyekundu iliyotumiwa kuwashusha chini wale wapelelezi nje ya kuta za Yeriko. Ni lazima akusanye pamoja familia yake ndani ya nyumba yake, ambamo ni lazima wabaki ili kupata ulinzi. Rahabu awapa wale wapelelezi wanaoondoka habari yenye kusaidia juu ya umbo la bara na awaambia jinsi ya kuwaepa wale wanaowafuatia. Wapelelezi wafanya hivyo. Baada ya kufunga ile kamba nyekundu na kuwakusanya pamoja washiriki wa familia yake, Rahabu angoja matukio mengine.—Yoshua 2:14-24.
Rahabu amefanya nini? Amethibitisha kwamba imani yake yategemea Mungu Mweza Yote, Yehova! Yeye ataishi kulingana na viwango vyake. Ndiyo yeye atatangazwa kuwa mwadilifu kwa matendo hayo ya imani.
Kuta Zaporomoka!
Majuma machache yapita. Wakiandamana na makuhani—wengine wakiwa na pembe za kondoo-dume na wengine wakibeba lile sanduku takatifu la agano—wanavita Waisraeli wanalizunguka Yeriko. Wamekuwa wakifanya hivyo mara moja kila siku kwa muda wa siku sita sasa. Hata hivyo, kwenye siku hii ya saba, tayari wamezunguka jiji hilo mara sita. Wanazunguka mara nyingine tena!
Mzunguko wa saba ukiwa umemalizika, milio mirefu kutoka kwenye pembe zaenea hewani. Sasa Waisraeli wapaaza sauti kwa nguvu. Ndipo, Yehova asababisha kuta za Yeriko zenye ulinzi ziporomoke zikinguruma kwa nguvu. Ni ile sehemu tu inayotegemeza nyumba ya Rahabu ibakiyo ikiwa imesimama. Sehemu inayobaki ya jiji hilo na wakazi walo wanaangamizwa. Imani yake ikiwa imethibitishwa kwa matendo, malaya huyo mwenye kutubu anahifadhiwa pamoja na nyumba yake, naye aanza kuishi miongoni mwa watu wa Yehova.—Yoshua 6:1-25.
Kuchunguza Vitabia vya Rahabu
Rahabu hakuwa mwanamke mvivu mwenye kujibembeleza, kwani kulikuwa na mabua ya kitani kwenye dari lake yakikaushwa juani. Nyuzi za kitani zingetumiwa kutengeneza nguo ya kitani. Pia kulikuwa akiba ya uzi mwekundu nyumbani mwa Rahabu. (Yoshua 2:6, 18) Basi huenda ikawa alifanya kazi ya kutengeneza nguo ya kitani na labda alijua ufundi wa kutia rangi. Ndiyo, Rahabu alikuwa mwanamke mwenye bidii ya kazi. Juu ya yote, alikuja kupata hofu ya Yehova yenye staha.—Linganisha Mithali 31:13, 19, 21, 22, 30.
Namna gani ile kazi nyingine ya Rahabu? Yeye hakuwa mkaribishaji tu wa mkahawa mdogo. La, Maandiko humtambulisha kwa kutumia maneno ya Kiebrania na ya Kigiriki yanayomaanisha malaya. Kwa kielelezo, sikuzote neno la Kiebrania zoh·nahʹ laonyesha uhusiano usio halali. Kwa kweli, miongoni mwa Wakanaani ukahaba haukuwa biashara yenye sifa mbaya.
Kutumia kwa Yehova kahaba kwaonyesha rehema yake kuu. Sura za nje zaweza kutudanganya, lakini Mungu “huutazama moyo.” (1 Samweli 16:7) Kwa hiyo, malaya wenye mioyo ifaayo watubuo ukahaba wao waweza kupokea msamaha wa Yehova Mungu. (Linganisha Mathayo 21:23, 31, 32.) Rahabu mwenyewe aliacha dhambi akawa mwenye mwendo mwadilifu wenye kibali cha kimungu.
Wapelelezi Waisraeli waliishi kulingana na Sheria ya Mungu, kwa hiyo hawakukaa nyumbani kwa Rahabu kwa sababu zisizo za kiadili. Huenda sababu yao ikawa kwamba isingeelekea sana kwamba wangetiliwa shaka kwa kuwamo nyumbani mwa kahaba. Mahali payo ukutani mwa jiji pangewawezesha watoroke. Kwa wazi Yehova aliwaongoza kwa mtenda dhambi ambaye moyo wake ulikuwa umeathiriwa ifaavyo sana na zile ripoti juu ya jinsi Mungu alivyoshughulika na Waisraeli hivi kwamba alitubu na kubadili njia zake. Taarifa ya Mungu kwamba Israeli lilipaswa kuangamiza Wakanaani kwa sababu ya mazoea yao yasiyo ya kiadili, na baraka yake juu ya Rahabu na juu ya kushindwa kwa Yeriko, ilionyesha wazi kwamba wapelelezi hao hawakutenda kosa la adili.—Mambo ya Walawi 18:24-30.
Namna gani maneno ya Rahabu yenye kuongoza vibaya wale waliowafuatia wapelelezi? Mungu alikubali mwendo wake. (Linganisha Warumi 14:4.) Alijihatarisha mwenyewe ili kuwalinda watumishi wa Mungu, akitoa ithibati ya imani yake. Ingawa uwongo wenye nia ya kudhuru ni mbaya machoni pa Yehova, mtu hana wajibu wa kutoa habari ya kweli kwa watu ambao hawana haki ya kuipokea. Hata Yesu Kristo hakutoa habari kamili au majibu ya moja kwa moja wakati ambapo kufanya hivyo kungaliweza kuleta madhara yasiyo ya lazima. (Mathayo 7:6; 15:1-6; 21:23-27; Yohana 7:3-10) Kwa wazi, mwendo wa Rahabu wa kuwaelekeza vibaya wale maofisa adui wapaswa kuonwa kwa njia hiyo.
Thawabu ya Rahabu
Rahabu alithawabishwaje kwa ajili ya kuzoea imani? Kwa hakika kuhifadhiwa kwake wakati wa uharibifu wa Yeriko kulikuwa baraka kutoka kwa Yehova. Baadaye, aliolewa na Salmoni (Salma), mwana wa Nashoni mkuu mmoja jangwani wa kabila la Yuda. Wakiwa wazazi wa yule Boazi mwenye kumwogopa Mungu, Salmoni na Rahabu walifanyiza kiungo katika nasaba iliyoongoza kwenye Mfalme Daudi wa Israeli. (1 Mambo ya Nyakati 2:3-15; Ruthu 4:20-22) La maana zaidi, Rahabu aliyekuwa malaya hapo kwanza ni mmoja wa wanawake wanne pekee wanaotajwa katika orodha ya Mathayo ya ukoo wa Yesu Kristo. (Mathayo 1:5, 6) Ni baraka iliyoje kutoka kwa Yehova!
Ingawa hakuwa Mwisraeli na alikuwa malaya wakati mmoja, Rahabu ni kielelezo chenye kutokeza cha mwanamke aliyethibitisha kwa matendo yake kwamba alikuwa na imani kamili katika Yehova. (Waebrania 11:30, 31) Kama vile wengine, ambao baadhi yao wameacha maisha ya umalaya, yeye atapokea thawabu nyingine bado—ufufuo kutoka kwa wafu kwenye uhai juu ya dunia-paradiso. (Luka 23:43) Kwa sababu ya imani yake yenye kuungwa mkono na matendo, Rahabu alipata kibali cha Baba yetu wa kimbingu mwenye upendo na mwenye kusamehe. (Zaburi 130:3, 4) Na kwa hakika kielelezo chake chema chaandaa kitia-moyo kwa wote wapendao uadilifu wamtumainie Yehova Mungu kwa ajili ya uhai wa milele.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Rahabu alitangazwa kuwa mwadilifu kwa sababu matendo yake yalithibitisha kwamba alikuwa na imani
[Picha katika ukurasa wa 24]
Waakiolojia wamefukua mabaki ya Yeriko la kale, kutia ndani sehemu ndogo ya ukuta wa mapema
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.