“Mkiwiwa Kodi, Lipeni Kodi”
“HAKUNA jambo lolote lililo hakika katika ulimwengu huu ila kifo na kodi.” Ndivyo alivyosema mkuu wa serikali Mmarekani aliyekuwa pia mvumbuzi wa karne ya 18 Benjamin Franklin. Maneno yake, ambayo hunakiliwa mara nyingi sana, hayaonyeshi tu kutoepukika kwa kodi bali pia yaonyesha ile hofu zinazotokeza. Kwa watu wengi, kulipa kodi ni kama kufa.
Ingawa kulipa kodi huenda kusipendeze, huko ni wajibu ambao ni lazima Wakristo wa kweli wachukue kwa uzito. Mtume Paulo aliandikia kutaniko la Kikristo katika Roma: “Mpeni kila mtu mnachowiwa: Mkiwiwa kodi, lipeni kodi; kama ni ushuru, basi ushuru; kama ni staha, basi staha; kama ni heshima, basi heshima.” (Warumi 13:7, New International Version) Na Yesu Kristo hasa alikuwa akirejezea kodi aliposema hivi: “Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu.”—Marko 12:14, 17.
Yehova ameruhusu “mamlaka iliyo kuu” ya serikali kuwapo naye anataka watumishi wake waipe ujitiisho wa kadiri. Basi, ni kwa nini Mungu anasisitiza kwamba waabudu wake walipe kodi? Paulo ataja sababu tatu za msingi: (1) “ghadhabu” ya “mamlaka iliyo kuu” katika kuadhibu wahalifu; (2) dhamiri ya Mkristo, ambayo haitakuwa safi akidanganya juu ya kodi zake; (3) uhitaji wa kuwalipa hao “wahudumu” kwa kutuhudumia na kudumisha kiwango fulani cha utaratibu. (Warumi 13:1-7) Huenda wengi wasipende kulipa kodi. Lakini, bila shaka wao wasingependelea hata kidogo kuishi katika nchi isiyo na polisi au ulinzi kwa moto, ambayo barabara hazirekebishwi, isiyo na shule za umma, na isiyo na njia ya kupeleka barua. Mwanasheria mmoja Mmarekani Oliver Wendell Holmes pindi fulani alisema hivi: “Kodi ni kile tunacholipa kwa jumuiya yenye ustaarabu.”
Kulipa kodi si jambo jipya kwa watumishi wa Mungu. Wakazi wa Israeli ya kale walilipa aina fulani ya kodi ili kutegemeza wafalme wao, na baadhi ya watawala hao walitwika watu sana kwa kuwatoza kodi kupita kiasi. Wayahudi vilevile walilipa ushuru na kodi kwa mamlaka za kigeni zilizowatawala, kama vile Misri, Uajemi, na Roma. Kwa hiyo Wakristo katika siku ya Paulo walijua vizuri kile alichokuwa akisema alipotaja kulipwa kwa kodi. Walijua kwamba iwe kodi zilikuwa za kiasi au la, na bila kujali jinsi serikali zingetumia pesa hizo, ilikuwa lazima walipe kodi yoyote waliyowiwa. Ndivyo ilivyo na Wakristo leo. Lakini, ni kanuni zipi ziwezazo kutupa mwongozo tunapolipa kodi zetu katika nyakati hizi zilizo ngumu?
Kanuni Tano Zenye Kutoa Mwongozo
Uwe mwenye utaratibu. Twamtumikia na kumwiga Yehova, ambaye si “Mungu wa machafuko, bali wa amani.” (1 Wakorintho 14:33; Waefeso 5:1) Kuwa mwenye utaratibu ni muhimu sana wakati wa kulipa kodi. Je, rekodi zako zimekamilika, ni sahihi, na kupangwa kwa utaratibu? Mara nyingi, si lazima kuwe na njia ghali sana ya kuweka faili. Waweza kuwa na folda moja yenye majina ya kila aina ya rekodi (kama vile risiti zinazoonyesha matumizi yako mbalimbali). Laweza kuwa jambo la kufaa kuziweka pamoja katika folda kubwa zaidi ya kila mwaka. Katika nchi nyingi inahitajika kuweka faili kama hizo kwa miaka kadhaa iwapo serikali itaamua kuchunguza rekodi za zamani. Kwa hiyo usitupe kitu chochote mpaka uwe na hakika kwamba hakihitajiki tena.
Fuatia haki. Paulo aliandika: “Tuombeeni; maana tunaamini kwamba tuna dhamiri njema, tukitaka kuwa na mwenendo mwema [“kujiendesha kwa unyoofu,” NW] katika mambo yote.” (Waebrania 13:18) Tamaa ya moyoni ya kutaka kuwa mwenye kufuatia haki yapasa iongoze kila uamuzi tunaofanya tunapolipa kodi zetu. Kwanza, fikiria kodi zipaswazo kulipwa kwa mapato yanayoripotiwa. Katika nchi nyingi, mapato ya ziada—kutoka bakshishi, kazi za hapa na pale, mauzo—hutozwa kodi mara tu yapitapo kiwango fulani kilichowekwa. Mkristo mwenye “dhamiri njema” atatafuta kujua ni mapato gani hutozwa kodi kule anakoishi naye atalipa kodi itakikanayo.
Pili, kuna jambo la mapunguzo ya kodi. Kwa kawaida serikali huruhusu walipa kodi kupunguza matumizi fulani kutoka kwa mapato yao yanayotozwa kodi. Katika ulimwengu huu usiofuatia haki, wengi hawaoni ubaya wa kuwa “watungaji” wanapodai mapunguzo kama hayo ya kodi. Inaripotiwa kwamba mtu mmoja katika Marekani alimnunulia mke wake koti la bei ghali sana la ngozi, kisha akaliangika mahali pake pa biashara kwa siku moja hivi ili aweze kupunguziwa kodi, hilo likiwa namna fulani ya “umaridadi” wa mahali pake pa kazi! Mtu mwingine alidai gharama za harusi ya binti yake kuwa mapunguzo ya kodi katika biashara. Na mwingine naye alijaribu kudai gharama alizotumia kwa kodi ya mapato yake kwa kusafiri na mke wake kwa miezi kadhaa katika Mashariki ya Mbali, ingawa mke huyo kwa kweli alikuwa huko kwa matembezi na starehe tu. Inaonekana kuwa hakuna mwisho wa visa kama hivyo. Ikisemwa waziwazi, kusema kitu ni mapunguzo ya kodi katika biashara hali kwa kweli si hivyo ni namna ya kudanganya—jambo ambalo Mungu wetu, Yehova, analichukia kabisa.—Mithali 6:16-19.
Uwe mwenye hadhari. Yesu aliwahimiza wafuasi wake wawe “na busara [“wenye hadhari,” NW] kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.” (Mathayo 10:16) Shauri hilo lapasa kutumiwa katika mazoea yetu ya kulipa kodi. Hasa katika nchi zilizositawi, watu wanaozidi kuongezeka siku hizi hulipa kampuni ya hesabu au mstadi mwingine kuwatayarishia kodi zao. Kisha wao hutia tu sahihi fomu na kupeleka hundi. Hiyo yaweza kuwa pindi nzuri ya kutii tahadhari iliyoandikwa kwenye Mithali 14:15: “Mjinga huamini kila neno; bali mwenyewe busara huangalia sana aendavyo.”
Walipa kodi wengi wamepata matatizo na serikali kwa sababu wao “huamini kila neno” la mfanya-hesabu asiye na maadili mazuri au mtayarishaji kodi asiye na ujuzi. Ni afadhali kama nini kuwa mwerevu! Ujihadhari kwa kusoma kwa uangalifu hati yoyote kabla uitie sahihi. Ikiwa jambo fulani lililowekwa, au kurukwa, laonekana kwako kuwa si la kawaida, pata maelezo—hata kama ni kwa kurudia-rudia—mpaka utosheke kwamba jambo hilo ni la kufuatia haki na ni halali. Ni kweli kwamba katika nchi nyingi sheria za kodi zimekuwa ngumu sana kuelewa, lakini kwa kadiri iwezekanavyo, ni jambo la hekima kuelewa kitu chochote unachotia sahihi. Katika visa fulani, unaweza kupata kwamba Mkristo mwenzako anayefahamu sheria ya kodi aweza kukupa ufahamu wa ndani kwa jambo hilo. Mzee mmoja wa Kikristo ambaye hushughulikia mambo ya kodi akiwa wakili wa kisheria alisema hivi kwa udhahiri: “Mfanya-hesabu wako akipendekeza jambo lionekanalo kuwa zuri sana, basi labda si jambo la haki!”
Uwe mwenye kuchukua daraka. “Kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe,” akaandika mtume Paulo. (Wagalatia 6:5) Wakati wa kulipa kodi ufikapo, ni lazima kila Mkristo abebe daraka la kuwa mwenye kufuatia haki na mwenye kutii sheria. Hili si jambo ambalo wazee wa kutaniko watasimamia kundi lililo chini ya utunzi wao. (Linganisha 2 Wakorintho 1:24.) Wao hawajiingizi katika mambo ya kodi ila tu wanapojua juu ya kosa zito, labda linalohusu kashfa katika jumuiya. Kwa ujumla, hiyo ni hali ambayo Mkristo mmoja-mmoja ana daraka la kutumia dhamiri yake iliyozoezwa vizuri katika kutumia kanuni za Kimaandiko. (Waebrania 5:14) Hilo latia ndani kujua kwamba kutia sahihi hati ya kodi—hata iwe imetayarishwa na nani—kwa kweli kwamaanisha hiyo ni taarifa ya kisheria na kwamba umeisoma na kuamini kwamba yaliyomo ni kweli.a
Kuwa mtu asiyelaumika. Waangalizi wa Kikristo ni lazima wawe ‘wasiolaumika’ ili wastahili cheo chao. Vivyo hivyo, kutaniko lote lapaswa liwe lisilolaumika machoni pa Mungu. (1 Timotheo 3:2; linganisha Waefeso 5:27.) Kwa hiyo wao hujaribu kudumisha sifa nzuri katika jumuiya, hata kama ni habari ya kulipa kodi. Yesu Kristo mwenyewe aliweka kielelezo kizuri katika habari hii. Mwanafunzi wake Petro aliulizwa kama Yesu alilipa kodi ya hekalu, jambo dogo la drakma mbili tu. Kwa kweli, Yesu hakupaswa kulipa kodi hiyo, kwa kuwa hekalu lilikuwa nyumba ya Baba yake na hakuna mfalme atozaye mwana wake kodi. Yesu alisema hivyo; lakini alilipa kodi hiyo. Kwa kweli, yeye hata alitumia mwujiza kutoa pesa iliyohitajika! Kwa nini alipe kodi ambayo yeye kwa kufaa hakupaswa kulipa? Kama Yesu mwenyewe alivyosema, ilikuwa kwamba “tusije tukawakwaza.”—Mathayo 17:24-27.b
Kudumisha Sifa ya Kumheshimu Mungu
Mashahidi wa Yehova leo vilevile wanahangaika kwamba wasiwakwaze wengine. Basi, si ajabu kwamba kwa ujumla, wao huwa na sifa nzuri ulimwenguni pote kuwa watu wanyoofu, wananchi wenye kulipa kodi. Mathalani, gazeti la habari la Kihispania El Diario Vasco lilieleza juu ya uepukaji wa kulipa kodi ulioenea sana katika Hispania, lakini likataja hivi: “Ila tu Mashahidi wa Yehova. Wanunuapo au kuuza, thamani ya [mali] hiyo ni ukweli kabisa.” Vivyo hivyo, gazeti la Marekani San Francisco Examiner lilisema hivi miaka kadhaa iliyopita: “Unaweza kuwachukua [Mashahidi wa Yehova] kuwa wananchi wapaswao kuigwa. Wao hulipa kodi zao kwa bidii, huwatunza wagonjwa, hujitahidi kuondoa kutojua kusoma na kuandika.”
Hakuna Mkristo wa kweli anayetaka kufanya kitu chochote kinachoweza kutia doa sifa hii iliyopatikana kwa jasho. Tukikabiliwa na machaguo, je, ungejihatarisha kuja kujulikana kama mwepa kodi kwa sababu ya kuokoa pesa fulani? La. Kwa kweli ni afadhali kupoteza pesa kuliko kuharibu sifa nzuri na kuharibu maadili yako na hata ibada yako kwa Yehova.
Ni kweli kwamba kudumisha sifa ya kuwa mtu mwenye haki, afuataye haki kwaweza kukugharimu pesa nyakati fulani. Kama mwanafalsafa wa kale Mgiriki Plato alivyosema karne 24 zilizopita: “Kunapokuwa na kodi ya mapato, mtu mwenye haki atalipa zaidi na asiye haki kidogo kwa kiwango kilekile cha mapato.” Huenda aliongezea kwamba mtu mwenye haki haghairi kulipa pesa kwa kuwa mwenye haki. Hata kuwa na sifa kama hiyo inastahili gharama hiyo. Hakika ndivyo ilivyo kwa Wakristo wa kweli. Sifa yao nzuri ni yenye thamani sana kwao kwa sababu inamheshimu Baba yao wa kimbingu nayo yaweza kuvutia wengine kwa njia yao ya maisha na kwa Mungu wao, Yehova.—Mithali 11:30; 1 Petro 3:1.
Ingawa hivyo, zaidi ya yote, Wakristo wa kweli huthamini uhusiano wao wenyewe pamoja na Yehova. Mungu huona kila kitu wanachofanya, nao hutamani kumpendeza. (Waebrania 4:13) Kwa hiyo, wao hukataa kishawishi cha kujaribu kudanganya serikali. Wao hutambua kwamba Mungu hufurahia tabia inayofuatia haki, yenye unyoofu. (Zaburi 15:1-3) Na kwa kuwa wao wanataka kuufurahisha moyo wa Yehova, wao hulipa kodi zote wanazowiwa.—Mithali 27:11; Warumi 13:7.
[Maelezo ya Chini]
a Hilo laweza kutokeza ugumu kwa Wakristo ambao wanajaza fomu ya malipo ya kodi wakiwa pamoja na mwenzi asiyeamini. Mke Mkristo anaweza kufanya jitihada za kudhamiria za kusawazisha kanuni ya ukichwa na uhitaji wa kutii sheria za kodi za Kaisari. Lakini ni lazima ajue juu ya matokeo ya baadaye ya kisheria ya kutia sahihi hati bandia akiwa anajua.—Linganisha Warumi 13:1; 1 Wakorintho 11:3.
b Kwa kupendeza, ni Gospeli ya Mathayo pekee iliyorekodi tukio hili katika maisha ya duniani ya Yesu. Kwa kuwa mbeleni Mathayo mwenyewe alikuwa mtoza kodi, bila shaka alivutiwa sana na mtazamo wa Yesu juu ya jambo hilo.