Nyakati Nzuri Zaidi Mbele Yetu
“SISI huwa na moja-sufuri-moja,” asema mwanamke mmoja.
“Mambo kwangu ni mabaya hata zaidi,” ajibu rafiki yake. “Mimi nina sufuri-sufuri-moja.”
Katika sehemu fulani za Afrika Magharibi, mazungumzo kama hayo hayahitaji maelezo. Badala ya kula milo mitatu kwa siku (moja-moja-moja), mtu aliye na moja-sufuri-moja anaweza kugharimia milo miwili tu kwa siku—mara moja asubuhi na mara moja jioni. Kijana mwanamume aliye wa sufuri-sufuri-moja aeleza hali yake hivi: “Mimi hula mara moja kwa siku. Mimi hujaza maji friji yangu. Mimi hula gari [mhogo] usiku kabla ya kwenda kulala. Hivyo ndivyo nimekuwa nikikabiliana na hali hiyo.”
Hiyo ndiyo hali ya idadi kubwa inayoongezeka ya watu leo. Bei huongezeka, na thamani ya pesa hupungua.
Upungufu wa Chakula Ulitabiriwa
Katika mfululizo wa maono aliyoonyeshwa mtume Yohana, Mungu alitabiri hali ngumu ambazo watu wengi wanakabili leo. Miongoni mwazo mngekuwa upungufu wa chakula. Yohana asimulia hivi: “Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake.” (Ufunuo 6:5) Farasi huyo mwenye kuogofya na mpandaji wake wafananisha njaa kuu—chakula kingekuwa kidogo sana hivi kwamba kingepimwa kwa mizani.
Kisha mtume Yohana asema hivi: “Nami nikasikia sauti . . . ikisema: ‘Kisaga cha ngano kwa nusu dinari moja, na visaga vitatu vya shayiri kwa dinari moja.’” Katika siku ya Yohana, kisaga cha ngano kilikuwa kipimo cha kila siku cha mwanajeshi, na dinari ilikuwa mshahara wa siku moja. Hivyo, tafsiri ya Richard Weymouth yatafsiri mstari huo hivi: “Mshahara wa siku nzima kwa mkate mmoja, mshahara wa siku nzima kwa keki tatu za shayiri.”—Ufunuo 6:6, New World Translation.
Ni nini mshahara wa siku nzima leo? Ripoti ya State of World Population, 1994 yasema: “Watu kama bilioni 1.1, karibu asilimia 30 ya idadi ya watu katika ulimwengu wenye kusitawi, wanaishi kwa dola 1 hivi kwa siku.” Hivyo, kwa maskini wa ulimwengu, mshahara wa siku moja kwa njia halisi unanunua kitu kama mkate mmoja.
Bila shaka, hilo si jambo la ajabu kwa wale walio maskini sana. “Mkate!” mtu mmoja akasema. “Nani hula mkate? Siku hizi mkate ni chakula cha wakati wa sherehe!”
Ajabu ni kwamba hakuna upungufu wa chakula. Kulingana na habari za UM, wakati wa miaka kumi iliyopita, ukuzi wa chakula ulimwenguni uliongezeka kwa asilimia 24, huo ukizidi ongezeko la idadi ya watu ulimwenguni. Hata hivyo, kuongezeka huku kwa chakula hakukufurahiwa na wote. Kwa kielelezo, katika Afrika, ukuzi wa chakula ulishuka kwa asilimia 5, huku idadi ya watu ikiongezeka kwa asilimia 34. Kwa hiyo chakula kijapokuwa kingi ulimwenguni pote, upungufu wa chakula unaendelea katika nchi nyingi.
Upungufu wa chakula humaanisha kupanda kwa gharama. Ukosefu wa kazi, mishahara midogo, na kuongezeka kwa infleshoni kunafanya iwe vigumu hata zaidi kupata pesa za kununua kile kinachopatikana. Yasema Human Development Report 1994: “Watu hupatwa na njaa si kwa sababu hakuna chakula—bali kwa sababu hawawezi kukinunua.”
Kuna ukosefu wa tumaini, kutojua la kufanya, na kukata tamaa kunakoongezeka. “Watu wanahisi kwamba siku ya leo ni mbaya, lakini kesho itakuwa mbaya hata zaidi,” akasema Glory, aishiye Afrika Magharibi. Mwanamke mwingine alisema hivi: “Watu huhisi kwamba wanakaribia msiba mkubwa. Wanahisi kwamba siku itakuja ambapo hakutakuwa na chochote sokoni.”
Yehova Aliwatunza Watumishi Wake Nyakati Zilizopita
Watumishi wa Mungu wanajua kwamba Yehova huthawabisha waaminifu wake kwa kuwapa mahitaji yao na kwa kuwapa uwezo wa kukabiliana na hali ngumu. Kwa kweli, uhakika kama huo katika uwezo wa Mungu wa kutoa uandalizi ni sehemu muhimu ya imani yao. Mtume Paulo aliandika hivi: “Mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”—Waebrania 11:6.
Sikuzote Yehova amewajali watumishi wake walio waaminifu. Wakati wa ukame wa miaka mitatu na nusu, Yehova alimwandalia chakula nabii Eliya. Mwanzoni, Mungu aliwaamuru kunguru wampelekee Eliya mkate na nyama. (1 Wafalme 17:2-6) Baadaye, kwa muujiza Yehova alihifadhi unga na mafuta ya mjane aliyemwandalia Eliya chakula. (1 Wafalme 17:8-16) Manabii wajapopatwa na mnyanyaso mkali wa kidini kutoka kwa Malkia Yezebeli mwovu, Yehova alihakikisha kwamba manabii wake waliandaliwa mkate na maji wakati wa njaa hiyo kuu.—1 Wafalme 18:13.
Baadaye, wakati mfalme wa Babiloni alipozingira Yerusalemu iliyoasi imani, iliwabidi watu ‘kula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana.’ (Ezekieli 4:16) Hali hiyo ikawa yenye kukatisha tamaa hivi kwamba wanawake wengine wakala nyama ya watoto wao wenyewe. (Maombolezo 2:20) Hata hivyo, ingawa nabii Yeremia alikuwa mfungwa kwa sababu ya kuhubiri, Yehova alihakikisha kwamba ‘walimpa Yeremia kila siku mkate mmoja uliotoka katika njia ya waokaji, hata mkate wote wa mji ulipokwisha.’—Yeremia 37:21.
Je, Yehova alimsahau Yeremia mkate ulipokwisha? Inaonekana hakumsahau, kwa kuwa mji huo ulipoanguka mikononi mwa Wababiloni, Yeremia ‘alipewa vyakula na zawadi, wakamwacha aende zake.’—Yeremia 40:5, 6; ona pia Zaburi 37:25.
Mungu Huwategemeza Watumishi Wake Leo
Kama Yehova alivyowategemeza watumishi wake katika vizazi vya kale, ndivyo anavyofanya leo, akiwatunza kimwili na kiroho. Kwa kielelezo, fikiria ono hili la Lamitunde, aishiye Afrika Magharibi. Yeye aeleza hivi: “Nilikuwa na shamba kubwa la kuku. Siku moja, majambazi wenye silaha wakaja kwenye shamba hilo na kuiba wengi wa kuku, genereta ya wakati wa dharura, na pesa tulizokuwa nazo. Muda mfupi baada ya kisa hicho, kuku wachache waliobaki wakafa kwa maradhi. Hilo likaharibu biashara yangu ya kuku. Kwa miaka miwili nilijaribu kutafuta kazi bila kufaulu. Mambo yalikuwa magumu sana, lakini Yehova alitutegemeza.
“Kilichonisaidia kukabili nyakati ngumu ilikuwa kutambua kwamba Yehova huruhusu mambo yatokee kwetu ili kutulainisha. Mke wangu na mimi tuliendelea na kawaida yetu ya funzo la Biblia la familia, na hilo lilitusaidia sana. Pia sala ilikuwa chanzo kikubwa cha nguvu. Nyakati nyingine sikutaka kusali, lakini niliposali, nilihisi vema.
“Wakati wa kipindi hicho kigumu, nilijifunza ubora wa kutafakari juu ya Maandiko. Nilikuwa nafikiria sana Zaburi 23, izungumzayo juu ya Yehova kuwa Mchungaji wetu. Andiko lingine lililonitia moyo lilikuwa Wafilipi 4:6, 7, lirejezealo ‘amani ya Mungu, ipitayo akili zote.’ Fungu lingine lililonitegemeza lilikuwa 1 Petro 5:6, 7, lisemalo hivi: ‘Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.’ Mistari hii yote ilinisaidia wakati wa nyakati hizo ngumu. Ukitafakari, unaweza kubadili mambo yaliyo akilini mwako yanayoleta mshuko-moyo.
“Sasa nimeajiriwa tena, lakini kusema kweli, hiyo haimaanishi kwamba mambo ni rahisi. Kama tu vile Biblia ilivyotabiri kwenye 2 Timotheo 3:1-5, (NW) tunaishi katika ‘siku za mwisho,’ zinazoonyeshwa na ‘nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.’ Hatuwezi kubadili yale andiko husema. Hivyo sitazamii hali ya maisha iwe rahisi. Hata hivyo, nahisi kwamba roho ya Yehova inanisaidia kukabili hali.”
Tujapoishi katika nyakati ngumu, wale wamtumainio Yehova na Mwanaye Mfalme, Kristo Yesu, hawavunjwi moyo. (Warumi 10:11) Yesu mwenyewe atuhakikishia hivi: “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia?”—Mathayo 6:25-28.
Hayo ni maswali ya kujichunguza moyoni katika nyakati hizi zilizo ngumu. Lakini Yesu aliendelea na maneno haya yenye kufariji: “Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? au Tunywe nini? au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”—Mathayo 6:28-33.
Nyakati Bora Mbele Yetu
Kuna kila ishara kwamba katika sehemu nyingi za ulimwengu, hali ya kiuchumi na kijamii inayozidi kuharibika itaendelea kuwa mbaya hata zaidi. Hata hivyo watu wa Mungu hutambua kwamba hali hizi ni za muda tu. Utawala wenye utukufu wa Mfalme Sulemani ulitangulia kuonyesha utawala mwadilifu wa Mfalme mkubwa zaidi kuliko Sulemani atakayetawala juu ya dunia yote. (Mathayo 12:42) Mfalme huyo ni Kristo Yesu, aliye “Mfalme wa Wafalme, na Bwana wa Mabwana.”—Ufunuo 19:16.
Zaburi 72, lililopata utimizo wa kwanza kuhusu Mfalme Sulemani, linafafanua utawala mtukufu wa Yesu Kristo. Fikiria mambo kadhaa mazuri ajabu linayotabiri kuhusu wakati ujao wa dunia chini ya Kristo akiwa Mfalme.
Hali za Amani Ulimwenguni Pote: “Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma. Na awe na enzi toka bahari hata bahari, toka Mto hata miisho ya dunia.”—Zaburi 72:7, 8.
Kuwajali Walio Dhaifu: “Atamwokoa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa. Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu, na damu yao ina thamani machoni pake.”—Zaburi 72:12-14.
Wingi wa Chakula: “Na uwepo wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima.”—Zaburi 72:16.
Utukufu wa Yehova Utajaa Dunia: “Na ahimidiwe BWANA, Mungu, Mungu wa Israeli, atendaye miujiza Yeye peke yake; jina lake tukufu na lihimidiwe milele; dunia yote na ijae utukufu wake.”—Zaburi 72:18, 19.
Hivyo, kwa kweli kuna nyakati bora mbele yetu.