Masomo Yenye Kutumika Kutokana na Bara Lililoahidiwa
BARA Lililoahidiwa jinsi linavyoelezwa katika Biblia lilikuwa la kipekee sana. Katika eneo hili dogo kwa kulinganishwa, twapata maumbo mbalimbali ya kijiografia. Kaskazini, kuna milima yenye vilele vyenye theluji; kusini ni eneo lenye hali-hewa ya joto. Yapo mabonde yenye kuzaa sana, maeneo ya nyika yenye ukiwa, na mashamba yenye vilima yanayofaa kwa matunda na kwa kulisha mifugo.
Utofauti katika kimo, tabia ya nchi na udongo huruhusu miti ya aina nyingi tofauti, vichaka, na mimea mingine—kutia na inayositawi katika maeneo ya baridi ya milima, mingine inayokua katika jangwa lenye joto, na bado mingine ambayo husitawi kwenye uwanda wenye rutuba au uwanda wa juu wenye mawe-mawe. Mtaalamu mmoja wa miti na mimea akadiria kwamba aina tofauti-tofauti 2,600 za mimea zaweza kupatikana katika eneo hilo. Waisraeli wa kwanza ambao walifanya safari ya uvumbuzi katika bara hilo waliona ushahidi wenye kupatikana mara moja wa uwezekano walo. Kutoka moja ya mabonde yenye maji walichukua kishada cha zabibu kikubwa sana hivi kwamba kilipaswa kibebwe kwenye ufito katikati ya wanaume wawili! Kwa kufaa bonde hilo liliitwa Eshkoli, ikimaanisha “kishada [cha Zabibu].”a—Hesabu 13:21-24.
Lakini acheni sasa tuchunguze kwa ukaribu baadhi ya maumbo ya kijiografia ya Bara Lililoahidiwa, hasa sehemu ya kusini.
Shefela
Pwani ya magharibi ya Bara Lililoahidiwa ni mwambao wake na Bahari ya Mediterania. Shefela iko karibu kilometa 40 kuelekea ndani ya bara. Neno “Shefela” lamaanisha “Bonde,” lakini kihalisi hili ni eneo la vilima na linaweza tu kuitwa bonde lilinganishwapo na milima ya Yuda iliyo mashariki.
Angalia ramani na uangalie uhusiano kati ya Shefela na maeneo yalo yanayozunguka. Mashariki kuna milima ya Yuda; magharibi, uwanda wa mwambao wa Ufilisti. Hivyo, Shefela lilitumika likiwa eneo lenye kutenganisha pande zenye kuhitilafiana, kizuizi ambacho katika nyakati za Biblia kilitenganisha watu wa Mungu na maadui wao wa zamani. Jeshi lolote, linalovamia kutoka magharibi lingelazimika kupenya Shefela kabla ya kusonga dhidi ya Yerusalemu, jiji kuu la Israeli.
Tukio kama hilo lilitukia karne ya tisa K.W.K. Mfalme Hazaeli wa Shamu, Biblia yaripoti, ‘akakwea akapigana na Gathi, [yaelekea kwenye mpaka wa Shefela] akautwaa; Hazaeli akaelekeza uso ili akwee kwenda Yerusalemu.’ Mfalme Yoashi alifanikiwa kumzuia Hazaeli, kwa kumpa rushwa ya vitu vya thamani kutoka hekaluni na jumba la kifalme. Hata hivyo, habari hii yaonyesha kwamba Shefela lilikuwa lenye umaana mkubwa kwa usalama wa Yerusalemu.—2 Wafalme 12:17, 18.
Twaweza kujifunza somo lenye kutumika kutokana na hilo. Hazaeli alitaka kulishinda Yerusalemu, lakini kwanza alilazimika kupenya Shefela. Kadhalika, Shetani Ibilisi ‘anatafuta kumeza’ watumishi wa Mungu, lakini mara nyingi ni lazima kwanza ajipenyeze eneo imara lenye kutenganisha pande zenye kuhitilafiana—uaminifu wao kwa kanuni za Biblia, kama zile zinazohusu mashirika mbaya na kupenda mali. (1 Petro 5:8; 1 Wakorintho 15:33; 1 Timotheo 6:10) Ridhiano la kanuni za Biblia mara nyingi ndiyo hatua ya kwanza kuelekea kufanya dhambi nzito. Hivyo basi tunza salama eneo lile la kutenganisha pande mbili zenye kuhitilafiana. Fuata kanuni za Biblia leo, na kesho hutavunja amri za Mungu.
Nchi ya Vilima ya Yuda
Ndani zaidi ya bara kutoka Shefela kuna nchi ya vilima ya Yuda. Hilo ni eneo la milima-milima ambalo hutokeza nafaka nzuri, mafuta mazuri ya mzeituni, na divai nzuri. Kwa sababu ya mwinuko wake wa juu, Yuda pia lilikuwa makimbilio bora. Hivyo, Mfalme Yothamu alijenga “ngome na minara” huko. Nyakati za taabu, watu wangeweza kukimbilia huko wapate usalama.—2 Mambo ya Nyakati 27:4.
Yerusalemu, liitwalo pia Sayuni, lilikuwa sehemu maarufu ya nchi ya vilima ya Yuda. Yerusalemu lilionekana salama kwa kuwa lilizungukwa kwa sehemu tatu na mabonde yaliyochongoka upande wa kaskazini, kulingana na mwana-historia wa karne ya kwanza Yosefo, lililindwa na kuta tatu zilizofuatana. Lakini makimbilio huhitaji mengi zaidi ya kuta na silaha ili kudumisha usalama wayo. Ni lazima yawe na maji. Hilo ni muhimu wakati wa mazingiwa, kwani bila maji, wakaaji walionaswa wangelazimika kujisalimisha haraka.
Yerusalemu lilichota ugavi wa maji kutoka Kidimbwi cha Siloami. Hata hivyo, katika karne ya nane K.W.K., akitazamia kimbele mazingiwa ya Waashuru, Mfalme Hezekia alijenga ukuta wa nje ili kulinda Kidimbwi cha Siloami akikizingira kabisa ndani ya jiji. Pia aliziba chemchemi za nje ya jiji ili kwamba Waashuru wenye kuwazingira wangetatizika kupata maji ya kutumia. (2 Mambo ya Nyakati 32:2-5; Isaya 22:11) Si hayo tu aliyofanya. Hezekia alipata njia ya kupitisha ugavi wa ziada wa maji na kuyaingiza ndani ya Yerusalemu.
Katika ule ambao umekuwa ukiitwa mojawapo wa ujenzi wa uhandisi wa ajabu wa kale, Hezekia alichimba mtaro kutoka chemchemi ya Gihoni hadi kwenye Kidimbwi cha Siloami.b Ukiwa wastani wa kimo cha meta 1.8, mtaro huo ulikuwa na urefu wa meta 533. Ebu wazia—mtaro wenye urefu wa karibu nusu kilometa, uliokatwa mwambani! Leo, miaka zaidi ya 2,700 baadaye, wageni wanaozuru Yerusalemu waweza kutembea kwa miguu katika ujenzi huu wa uhandisi ulio kazi bora sana; kwa kawaida huitwa mtaro wa Hezekia.—2 Wafalme 20:20; 2 Mambo ya Nyakati 32:30.
Jitihada za Hezekia za kulinda na kuongezea ugavi wa maji wa Yerusalemu zaweza kutufundisha somo lenye kutumika. Yehova ni “chemchemi ya maji ya uzima.” (Yeremia 2:13) Mawazo yake, yaliyo katika Biblia huendeleza uhai. Hiyo ndiyo sababu funzo la Biblia la kibinafsi ni la lazima. Lakini nafasi ya funzo, na ujuzi unaofuata, havitamiminika tu kwako. Huenda ukalazimika ‘kuchimba mitaro,’ kama vile kupitia shughuli zako nyingi za kila siku, ili kupata nafasi. (Mithali 2:1-5; Waefeso 5:15, 16) Mara uanzapo, shikamana na ratiba yako, ukilipa nafasi ya kwanza funzo lako la kibinafsi. Uwe mwangalifu usiruhusu yeyote au chochote kukunyang’anya ugavi huu wa maji wenye thamani.—Wafilipi 1:9, 10.
Maeneo ya Nyika
Kuelekea mashariki ya vilima vya Yuda kuna Nyika la Yuda, pia huitwa Yeshimoni, ikimaanisha “jangwa.” (1 Samweli 23:19, NW, kielezi chini) Katika Bahari ya Chumvi, eneo hilo kame huonyesha mabonde yenye mawe na magenge yaliyochongoka-chongoka. Ikishuka meta 1,200 katika kilometa 24 tu, Nyika ya Yuda inakingwa dhidi ya pepo zenye mvua zinazotoka magharibi, na hivyo hupata kiasi kidogo cha mvua. Bila shaka hii ndiyo nyika ambayo mbuzi wa Azazeli alipelekwa wakati wa Siku ya Kufunika ya kila mwaka. Pia ndipo Daudi alipokimbilia alipokuwa akimtoroka Sauli. Hapo Yesu alifunga kwa siku 40 na baadaye akajaribiwa na Ibilisi.—Mambo ya Walawi 16:21, 22; Zaburi 63, linganisha maelezo ya utangulizi ya NW; Mathayo 4:1-11.
Karibu kilometa 160 kusini-magharibi ya Nyika ya Yuda ipo Nyika ya Parani. Kambi nyingi za Waisraeli wakati wa safari yao ya miaka 40 kutoka Misri kwenda Bara Lililoahidiwa zilikuwa hapa. (Hesabu 33:1-49) Musa aliandika juu ya “jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji.” (Kumbukumbu la Torati 8:15) Ni ajabu kwamba mamilioni ya Waisraeli yaliokoka! Hata hivyo, Yehova aliwahifadhi.
Hili na litumike likiwa kikumbusha kwamba Yehova aweza kutuhifadhi sisi pia, hata katika ulimwengu huu ulio jangwa kiroho. Ndiyo, sisi pia twatembea miongoni mwa nyoka na nge ingawa si halisi. Huenda tukalazimika kuwa na mahusiano ya kila siku na watu ambao hawasumbuliwi dhamiri wanaporopoka usemi wenye sumu ambao waweza kwa urahisi kudhuru kufikiri kwetu. (Waefeso 5:3, 4; 1 Timotheo 6:20) Wajitahidio kumtumikia Mungu licha ya vizuizi hivyo wastahili pongezi. Uaminifu wao ni uthibitisho wenye nguvu kwamba kwelikweli Yehova anawahifadhi.
Vilima vya Karmeli
Jina Karmeli humaanisha “Shamba la Matunda.” Eneo hili lenye rutuba, kuelekea magharibi, urefu wa karibu kilometa 50 hivi, limerembwa kwa mashamba ya mizabibu, miti ya mizeituni, na miti ya matunda. Safu hiyo yenye vilima-vilima hukumbukwa kwa sababu ya uzuri na urembo wayo. Isaya 35:2 husema juu ya “uzuri wa Karmeli” ikiwa ishara ya utukufu wenye kuzaa wa bara lililorudishwa la Israeli.
Matukio kadhaa yenye kujulikana yalitukia Karmeli. Ilikuwa hapa ambapo Eliya aliwatolea manabii wa Baali mwito wa ushindani na ambapo ‘moto wa BWANA ulishuka’ katika kuthibitisha ukuu Wake. Pia, ilikuwa kutoka kilele cha Karmeli kwamba Eliya alielekeza fikira kwenye wingu dogo lililokuja kuwa mvua kubwa, hivyo kumaliza kimuujiza ukame juu ya Israeli. (1 Wafalme 18:17-46) Mwandamizi wa Eliya, Elisha, alikuwa kwenye Mlima Karmeli mwanamke wa Shunemu alipokuja kuomba msaada wake kwa ajili ya mtoto wake aliyekufa, ambaye baadaye Elisha alimfufua.—2 Wafalme 4:8, 20, 25-37.
Mitelemko ya Karmeli bado ina mashamba ya matunda, miti ya mizeituni, na mizabibu. Wakati wa vuli, mitelemko hii hufunikwa na wonyesho mzuri sana wa maua. “Kichwa chako juu yako ni kama Karmeli,” Sulemani akamwambia mwanamwali Mshulami, alipokuwa anarejezea uzuri wa nywele zake au kichwa chake kizuri kilichotokeza kwa fahari kutoka kwenye shingo yake.—Wimbo Ulio Bora 7:5.
Uzuri ambao ulionyeshwa na vilima vya Karmeli hutukumbusha juu ya uzuri wa kiroho ambao Yehova amelitolea tengenezo la waabudu wake wa kisasa. (Isaya 35:1, 2) Kwa kweli Mashahidi wa Yehova huishi katika paradiso ya kiroho, wao hukubaliana na maneno ya hisia ya Mfalme Daudi, ambaye aliandika: “Kamba zangu zimeniangukia mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri.”—Zaburi 16:6.
Ni kweli kwamba, kuna magumu mengi ambayo taifa la kiroho la Mungu la leo hulazimika kukabili, jinsi Waisraeli wa kale walivyokabiliana na upinzani wenye kuendelea kutoka kwa maadui wa Mungu. Lakini, Wakristo wa kweli sikuzote wanatambua baraka ambazo Yehova ameandaa—kutia ndani nuru yenye kuongezeka ya kweli ya Biblia, udugu wa ulimwenguni pote, na fursa ya kupata uhai wa milele katika dunia iliyo paradiso.—Mithali 4:18; Yohana 3:16; 13:35.
‘Kama Bustani ya Yehova’
Bara Lililoahidiwa la zamani lilikuwa linapendeza. Lilifafanuliwa vizuri kuwa ‘lijaalo maziwa na asali.’ (Mwanzo 13:10; Kutoka 3:8) Musa aliiita “nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na vilima; nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali; nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba.”—Kumbukumbu la Torati 8:7-9.
Ikiwa Yehova aliweza kuwaandalia watu wake wa kale nchi yenye kuzaa, nzuri namna hiyo, kwa hakika aweza kuwapa watumishi wake waaminifu wa kisasa paradiso nzuri sana yenye kuenea dunia nzima—ikiwa na milima, mabonde, mito na maziwa. Ndiyo, Bara Lililoahidiwa la zamani likiwa na utofauti-tofauti wake wote lilikuwa tu mwonjo wa Paradiso ya kiroho ambayo Mashahidi wake hufurahia leo na ni mwonjo wa paradiso ijayo ya ulimwengu mpya. Ahadi iliyorekodiwa katika Zaburi 37:29 itatimizwa humo: “Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele.” Yehova atoapo makao ya Paradiso kwa wanadamu watiifu watakuwa wenye furaha kama nini kuchunguza “vyumba” vyake vyote na kwa umilele kuweza kufanya hivyo!
[Maelezo ya Chini]
a Kishada kimoja cha zabibu kutoka eneo hilo kilirekodiwa kuwa na uzito wa kilogramu 12, na kingine, zaidi ya kilogramu 20.
b Chemchemi ya Gihoni ilikuwa nje kidogo ya mpaka wa mashariki wa Yerusalemu. Ilifichwa pangoni; hivyo yaelekea Waashuru hawakujua kuwapo kwayo.
[Ramani katika ukurasa wa 4]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
GALILAYA
Ml. Karmeli
Bahari ya Galilaya
SAMARIA
SHEFELA
Milima ya Yuda
Bahari ya Chumvi
[Hisani]
Picha ya NASA
[Ramani katika ukurasa wa 4]
Shefela lilikuwa kizuizi kati ya watu wa Mungu na maadui wao
MI 0 5 10
KM 0 8 16
Uwanda wa Ufilisti
Shefela
Nchi ya Vilima ya Yuda
Nyika ya Yuda
Bonde la Ufa
Bahari ya Chumvi
Bara la Amoni na Moabu
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 5]
Mtaro wa Hezekia: meta 533 kwa urefu, uliokatwa katika mwamba mgumu
Bonde la Tiropoe
Siloami
JIJI LA DAUDI
Bonde la Kidroni
Gihoni
[Picha katika ukurasa wa 6]
Katika Nyika ya Yuda, Daudi alitafuta makimbilio alipokuwa akimtoroka Sauli. Baadaye Yesu alijaribiwa na Ibilisi hapo
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mlima Karmeli, ambapo Eliya aliwafedhehesha makuhani wa Baali
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Picha katika ukurasa wa 8]
“BWANA, Mungu wako yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima.”—Kumbukumbu la Torati 8:7