Kuzikumbuka Siku za Mwisho za Yesu Duniani
NI SIKU ya saba ya mwezi wa Kiyahudi wa Nisani mwaka wa 33 W.K. Wazia kwamba unaangalia matukio katika jimbo la Roma la Yudea. Wakiondoka Yeriko na majani yake yenye kusitawi sana, Yesu Kristo na wanafunzi wake wanapanda kwa uchovu barabara yenye vumbi, yenye kujipinda. Wasafiri wengine wengi pia wako njiani kupanda kwenda Yerusalemu kwa ajili ya sherehe ya kila mwaka ya Sikukuu ya Kupitwa. Hata hivyo, mengi zaidi ya kupanda huko kwenye kuchosha yamo akilini mwa wanafunzi wa Kristo.
Wayahudi wamekuwa wakitamani sana Mesiya awezaye kuleta kitulizo kutoka katika nira ya Roma. Wengi waamini kwamba Yesu wa Nazareti ndiye Mwokozi huyo ambaye amengojewa kwa muda mrefu. Kwa miaka mitatu na nusu, amekuwa akisema juu ya Ufalme wa Mungu. Amewaponya wagonjwa na kulisha wenye njaa. Ndiyo, amewaletea watu faraja. Lakini viongozi wa kidini wanaudhika kwa sababu ya shutumu kali la hadharani la Yesu dhidi yao na wameazimia kufanya auawe. Lakini, yule pale, akitembea kimakusudi kupanda ile barabara ambayo imekauka akiwa mbele ya wanafunzi wake.—Marko 10:32.
Jua lishukapo nyuma ya Mlima wa Mizeituni huko mbele, Yesu na waandamani wake wafika kwenye kijiji cha Bethania, ambako watakaa masiku sita yanayofuata. Rafiki zao wapendwa Lazaro, Maria, na Martha wako huko ili kuwakaribisha. Jioni yaandaa kitulizo chenye kupoza kutoka katika safari yenye joto na yatia alama mwanzo wa Sabato ya Nisani 8.—Yohana 12:1, 2.
Nisani 9
Baada ya Sabato, Yerusalemu inavuma kwa utendaji. Maelfu ya wageni tayari wamekusanyika kwenye jiji kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa. Lakini rabsha yenye kelele tusikiayo ni zaidi ya ilivyo kawaida wakati huu wa mwaka. Umati wenye udadisi unateremka kasi katika barabara nyembamba kwenda kwenye njia za malango ya jiji. Wasukumanapo kutoka nje ya malango yaliyojaa watu, walakiwa na mwono ulioje! Watu wengi wenye kushangilia sana wanateremka Mlima wa Mizeituni kwenye barabara ya kutoka Bethfage. (Luka 19:37) Hayo yote yamaanisha nini?
Tazama! Yesu wa Nazareti aja akiwa amepanda mwana-punda. Watu watandaza mavazi barabarani mbele yake. Wengine wapeperusha matawi ya mitende yaliyotoka kukatwa na kwa shangwe wapaaza sauti hivi: “Mbarikiwa ni yeye ajaye katika jina la Yehova, naam, mfalme wa Israeli!”—Yohana 12:12-15.
Umati ukaribiapo Yerusalemu, Yesu atazama jiji na aguswa hisia sana. Aanza kutoa machozi, nasi twamsikia akitabiri kwamba jiji hilo litaharibiwa. Yesu awasilipo hekaluni muda mfupi baadaye, yeye afundisha umati na kuponya vipofu na walemavu wamjiao.—Mathayo 21:14; Luka 19:41-44, 47.
Jambo hilo laonwa na makuhani wakuu na waandishi. Waudhika kama nini kuona mambo yenye kustaajabisha afanyayo Yesu na kuona shangwe ya umati! Wakiwa hawawezi kuficha ghadhabu yao, Mafarisayo wadai hivi: “Mwalimu, kemea wanafunzi wako.” “Mimi nawaambia nyinyi,” Yesu ajibu, “Kama hawa wangekaa kimya, mawe yangepaaza kilio.” Kabla ya kuondoka, Yesu aona utendaji wa kibiashara katika hekalu.—Luka 19:39, 40; Mathayo 21:15, 16; Marko 11:11.
Nisani 10
Yesu afika kwenye hekalu mapema. Jana, aliwaka hasira kwa sababu ya kule kutumia kwa kadiri kubwa ibada ya Babake, Yehova Mungu, kwa faida za kibiashara. Kwa hiyo, kwa bidii kubwa, aanza kuwatupa nje wale wenye kununua na kuuza hekaluni. Kisha apindua meza za wabadili-fedha wenye pupa na mabenchi ya hao waliokuwa wakiuza njiwa. “Imeandikwa,” Yesu asema kwa mkazo, “‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini nyinyi mnaifanya pango la wapokonyaji.”—Mathayo 21:12, 13.
Makuhani wakuu, waandishi, na watu walio wakubwa wachukizwa sana na matendo na ufundishaji wa Yesu wa hadharani. Jinsi watamanivyo sana kumwua! Lakini wazuiwa na umati kwa sababu watu washangazwa na kufundisha kwa Yesu na wafuliza “kushikamana sana naye ili wamsikie.” (Luka 19:47, 48) Jioni ikaribiapo, Yesu na waandamani wake waonea shangwe matembezi yenye kupendeza ya kurudi Bethania ili kupata pumziko zuri la usiku.
Nisani 11
Ni mapema asubuhi, na Yesu na wanafunzi wake tayari wanavuka Mlima wa Mizeituni kwenda Yerusalemu. Wawasilipo hekaluni, makuhani wakuu na wanaume wazee wafanya haraka kumkabili Yesu. Wao wakumbuka waziwazi tendo lake dhidi ya wabadili-fedha na wafanya-biashara hekaluni. Maadui wake wadai hivi kwa chuki: “Ni kwa mamlaka gani wewe wafanya mambo haya? Na ni nani aliyekupa wewe mamlaka hii?” “Mimi pia, nitawauliza nyinyi jambo moja,” Yesu ajibu. “Mkiniambia hilo, hakika mimi pia nitawaambia nyinyi ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya: Ubatizo wa Yohana, ulikuwa wa kutoka chanzo gani? Kutoka mbinguni au kutoka kwa wanadamu?” Wakishauriana pamoja, hao wapinzani wasababu hivi: “Tukisema, ‘Kutoka mbinguni,’ atatuambia, ‘Basi, kwa nini hamkumwamini?’ Ingawa hivyo, tukisema, ‘Kutoka kwa wanadamu,’ tunao umati kuuhofu, kwa maana wao wote wamchukua Yohana kuwa nabii.” Wakiwa wametatanishwa, wao wajibu hivi kwa udhaifu: “Hatujui.” Kwa utulivu Yesu aitikia hivi: “Wala mimi siwaambii nyinyi ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”—Mathayo 21:23-27.
Maadui wa Yesu sasa wajaribu kumtega aseme jambo fulani ambalo kwalo wao waweza kufanya akamatwe. “Je, yaruhusika kisheria,” wauliza, “kumlipa Kaisari kodi ya kichwa au la?” “Nionyesheni sarafu ya kodi ya kichwa,” Yesu ajibu vikali. Kisha auliza hivi: “Sanamu na mwandiko huu ni wa nani?” “Wa Kaisari,” wao wasema. Akiwatatanisha, Yesu ataarifu waziwazi ili wote wasikie: “Basi, mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, lakini mlipeni Mungu vitu vya Mungu.”—Mathayo 22:15-22.
Akiwa amewanyamazisha maadui wake kwa hoja zisizokanushika, Yesu sasa awashambulia mbele ya umati na wanafunzi wake. Sikiliza awashutumupo waandishi na Mafarisayo bila hofu. “Msifanye kulingana na vitendo vyao,” asema, “kwa maana wao husema lakini hawafanyi.” Kwa ujasiri, yeye atamka mfululizo wa ole juu yao, akiwatambulisha kuwa viongozi vipofu na wanafiki. “Nyoka, uzao wa nyoka-vipiri,” Yesu asema “nyinyi mtaikimbiaje hukumu ya Gehena?”—Mathayo 23:1-33.
Mashutumu hayo makali hayamaanishi kwamba Yesu haoni sifa nzuri za wengine. Baadaye, yeye aona watu wakitumbukiza fedha ndani ya masanduku ya hazina ya hekalu. Inagusa moyo kama nini kumwona mjane mwenye uhitaji akitumbukiza riziki yake yote—sarafu ndogo mbili za thamani ndogo sana! Kwa uthamini wenye uchangamshi, Yesu aonyesha kwamba, kwa kweli, ametumbukiza nyingi zaidi kuliko wote ambao walitoa michango yao kwa wingi “kutokana na ziada yao.” Kwa huruma yake nyororo, Yesu huthamini sana chochote kile mtu awezacho kufanya.—Luka 21:1-4.
Yesu sasa anaondoka hekaluni kwa mara ya mwisho. Baadhi ya wanafunzi wake wasema juu ya fahari ya hekalu, kwamba “limerembwa kwa mawe bora na vitu vilivyowekwa wakfu.” Kwa mshangao wao, Yesu ajibu hivi: “Siku zitakuja ambazo katika hizo hakuna jiwe juu ya jiwe ambalo litaachwa hapa lisiangushwe.” (Luka 21:5, 6) Mitume wamfuatapo Yesu kutoka katika jiji lililojaa watu, wao wajiuliza kile ambacho angeweza kuwa amaanisha.
Muda mfupi baadaye Yesu na mitume wake waketi na kuonea shangwe amani na utulivu wa Mlima wa Mizeituni. Waangaliapo mandhari maridadi ya Yerusalemu na hekalu, Petro, Yakobo, Yohana, na Andrea watafuta kuelezwa wazi juu ya utabiri wa Yesu wenye kushtusha. “Tuambie,” wao wasema, “Ni wakati gani mambo haya yatakuwa, nayo itakuwa ni nini ishara ya kuwapo kwako na ya umalizio wa mfumo wa mambo?”—Mathayo 24:3; Marko 13:3, 4.
Kwa kujibu huyo Mwalimu Stadi atoa unabii wenye kutokeza kikweli. Yeye atabiri kuwepo kwa vita vikali, matetemeko ya dunia, upungufu wa chakula, na magonjwa ya kuambukiza. Yesu pia atabiri kwamba habari njema ya Ufalme itahubiriwa duniani kote. “Kisha,” yeye aonya, “kutakuwa na dhiki kubwa ya namna ambayo haijapata kutukia tangu mwanzo wa ulimwengu hadi sasa, la, wala haitatukia tena.”—Mathayo 24:7, 14, 21; Luka 21:10, 11.
Hao mitume wanne wasikiliza kwa makini Yesu azungumziapo pande nyingine za ‘ishara ya kuwapo kwake.’ Yeye akazia uhitaji wa ‘kufuliza kulinda.’ Kwa nini? “Kwa sababu,” yeye asema, “hamjui ni siku gani Bwana yenu anakuja.”—Mathayo 24:42; Marko 13:33, 35, 37.
Hiyo imekuwa siku isiyoweza kusahaulika kwa Yesu na mitume wake. Kwa hakika, ni siku ya mwisho ya huduma ya Yesu ya hadharani kabla ya kukamatwa kwake, kufanyiwa kesi, na kufishwa. Kwa kuwa wakati wazidi kusonga, wao waanza kutembea ule umbali mfupi juu ya kilima kwenda Bethania.
Nisani 12 na 13
Yesu apisha Nisani 12 kwa utulivu pamoja na wanafunzi wake. Ang’amua kwamba viongozi wa kidini wataka sana kumwua, na hataki wamzuie kusherehekea Sikukuu ya Kupitwa jioni inayofuata. (Marko 14:1, 2) Siku inayofuata, Nisani 13, watu wana shughuli nyingi wakifanya matayarisho ya mwisho kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa. Mapema alasiri, Yesu amtuma Petro na Yohana ili kutayarisha Sikukuu ya Kupitwa kwa ajili yao katika chumba cha juu huko Yerusalemu. (Marko 14:12-16; Luka 22:8) Muda mfupi kabla ya mshuko-jua, Yesu na wale mitume wengine kumi wakutana nao huko kwa ajili ya sherehe yao ya mwisho ya Sikukuu ya Kupitwa.
Nisani 14, Baada ya Mshuko-Jua
Yerusalemu limefunikwa kwa nuru yenye kupendeza ya jioni-jioni huku mwezi mpevu ukichomoza juu ya Mlima wa Mizeituni. Katika chumba kikubwa chenye vifaa, Yesu na wale 12 wanaegama kwenye meza iliyotayarishwa. “Nimetamani sana kula hii sikukuu ya kupitwa pamoja nanyi kabla sijateseka,” yeye asema. (Luka 22:14, 15) Baada ya muda fulani mitume wanashangaa kumwona Yesu akiinuka na kuyaweka mavazi yake ya nje upande mmoja. Akichukua taulo na beseni la maji, aanza kuosha miguu yao. Ni somo lililoje la utumishi mnyenyekevu ambalo haliwezi kusahaulika!—Yohana 13:2-15.
Hata hivyo, Yesu ajua kwamba mmojawapo wa wanaume hao—Yudasi Iskariote—tayari amepanga kumsaliti kwa viongozi wa kidini. Kwa kueleweka, Yesu asononeka sana. “Mmoja wenu atanisaliti mimi,” yeye afunua. Mitume wahuzunishwa sana na hilo. (Mathayo 26:21, 22) Baada ya kusherehekea Sikukuu ya Kupitwa, Yesu amwambia Yudasi hivi: “Lile unalofanya lifanye upesi zaidi.”—Yohana 13:27.
Mara Yudasi aondokapo, Yesu aanzisha mlo wa kukumbuka kifo chake kinachokaribia. Yeye achukua mkate usiotiwa chachu, ashukuru katika sala, aumega, na kuwaagiza wale 11 waushiriki. “Huu wamaanisha mwili wangu,” yeye asema, “ambao wapasa kutolewa kwa ajili yenu. Fulizeni kufanya hili katika ukumbuko wangu.” Kisha achukua kikombe cha divai isiyokolezwa. Baada ya kusema baraka, awapa kikombe, akiwaambia wanywe kutoka hicho. Yesu aongeza kusema hivi: “Hii yamaanisha ‘damu yangu ya agano,’ inayopaswa kumwagwa kwa niaba ya wengi kwa msamaha wa dhambi.”—Luka 22:19, 20; Mathayo 26:26-28.
Wakati wa jioni hiyo yenye maana, Yesu awafundisha mitume wake waaminifu masomo mengi yenye thamani, miongoni mwayo umaana wa upendo wa kidugu. (Yohana 13:34, 35) Awahakikishia kwamba watapokea “msaidizi,” roho takatifu. Itawakumbusha mambo yote ambayo amewaambia. (Yohana 14:26) Baadaye jioni, lazima wawe wametiwa moyo sana kumsikia Yesu akitoa sala yenye bidii kwa niaba yao. (Yohana, sura ya 17) Baada ya kuimba nyimbo za sifa, wao waondoka katika chumba cha juu na kumfuata Yesu nje katika hewa yenye baridi kidogo ya usiku uliokuwa umekwenda sana.
Akivuka Bonde la Kidroni, Yesu na mitume wake waenda hadi bustani la Gethsemane, mojawapo ya mahali pao wapapendapo sana. (Yohana 18:1, 2) Huku mitume wake wakingoja, Yesu aenda umbali mfupi ili kusali. Mkazo wake wa kihisia-moyo ni mwingi kuliko vile maneno yawezavyo kufafanua aombapo Mungu kwa bidii ili apate msaada. (Luka 22:44) Kule kufikiria hasa aibu ambayo ingerundikwa juu ya Baba yake mpendwa wa kimbingu ikiwa angeshindwa kunaumiza kupita kiasi.
Yesu amemaliza tu kusali Yudasi Iskariote awasilipo pamoja na umati ukiwa na panga, marungu, na mienge. “Siku njema, Rabi!” Yudasi asema, akimbusu Yesu kwa wororo. Hiyo ndiyo ishara kwa hao watu ili wamkamate Yesu. Kwa ghafula, Petro akata kwa upanga wake na alikata sikio la mtumwa wa kuhani mkuu. “Rudisha upanga wako mahali pao,” Yesu asema huku akiliponya sikio la huyo mwanamume. “Wale wote wauchukuao upanga wataangamia kwa upanga.”—Mathayo 26:47-52.
Kila kitu chatukia upesi sana! Yesu akamatwa na kufungwa. Katika hali ya hofu na vurugu, mitume wamwacha Bwana-Mkubwa wao na kukimbia. Yesu apelekwa kwa Anasi, kuhani wa cheo cha juu wa hapo zamani. Kisha apelekwa kwa Kayafa, kuhani wa cheo cha juu wa wakati huo, ili afanyiwe kesi. Mapema asubuhi, Sanhedrini yamshtaki Yesu isivyo kweli juu ya kukufuru. Halafu, Kayafa aamuru apelekwe kwa gavana Mroma Pontio Pilato. Yeye ampeleka Yesu kwa Herode Antipasi, mtawala wa Galilaya. Herode na walinzi wake wamdhihaki Yesu. Kisha arudishwa kwa Pilato. Kutokuwa na hatia kwa Yesu kwathibitishwa na Pilato. Lakini viongozi wa kidini wa Kiyahudi wamsonga amhukumie Yesu adhabu ya kifo. Baada ya kutukanwa sana na kutendwa vibaya kimwili, Yesu apelekwa Golgotha ambako apigiliwa misumari bila huruma kwenye mti wa mateso na apatwa na kifo chenye maumivu makali.—Marko 14:50–15:39; Luka 23:4-25.
Ungalikuwa msiba ulio mkubwa zaidi katika historia ikiwa kifo cha Yesu kingalileta mwisho wa kudumu kwa uhai wake. Kwa kufurahisha, haikuwa hivyo. Nisani 16, 33 W.K., wanafunzi wake walishangaa kuona kwamba alikuwa amefufuliwa kutoka kwa wafu. Halafu, watu zaidi ya 500 waliweza kuthibitisha kwamba Yesu alikuwa hai tena. Na siku 40 baada ya kufufuliwa kwake, kikundi cha wafuasi wake waaminifu kilimwona akipaa kuingia mbinguni.—Matendo 1:9-11; 1 Wakorintho 15:3-8.
Maisha ya Yesu na Wewe
Hilo lakuathirije—kwa kweli, laathirije sisi sote? Bila shaka, huduma, kifo, na ufufuo wa Yesu zamtukuza Yehova Mungu na ni za maana katika kukamilisha kusudi Lake tukufu. (Wakolosai 1:18-20) Ni zenye umuhimu mkubwa kwetu kwa kuwa twaweza kusamehewa dhambi zetu kwa msingi wa dhabihu ya Yesu na hivyo kuweza kuwa na uhusiano wa kibinafsi na Yehova Mungu.—Yohana 14:6; 1 Yohana 2:1, 2.
Hata wafu waathiriwa. Ufufuo wa Yesu hufungua njia ya kuwarudisha kwenye uhai katika dunia iliyo Paradiso ambayo imeahidiwa na Mungu. (Luka 23:39-43; 1 Wakorintho 15:20-22) Ikiwa wataka kujua zaidi juu ya mambo hayo, twakualika uhudhurie Ukumbusho wa kifo cha Kristo Aprili 11, 1998, kwenye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova katika eneo lako.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
“Pango la Wapokonyaji”
YESU alikuwa na sababu ya kutosha kusema kwamba wafanya-biashara wenye pupa walikuwa wameligeuza hekalu la Mungu kuwa “pango la wapokonyaji.” (Mathayo 21:12, 13) Ili kulipa kodi ya hekalu, Wayahudi na wageuzwa-imani kutoka nchi nyingine walipaswa kubadilisha fedha zao za kigeni ili kupata fedha zilizokubalika. Katika kitabu chake The Life and Times of Jesus the Messiah, Alfred Edersheim aeleza kwamba wabadili-fedha walikuwa wakianzisha biashara kwenye majimbo katika Adari 15, mwezi mmoja kabla ya Sikukuu ya Kupitwa. Kuanzia Adari 25, waliingia katika eneo la hekalu huko Yerusalemu ili kujinufaisha na ule mmiminiko mkubwa wa Wayahudi na wageuzwa-imani. Wachuuzi waliendesha biashara yenye kusitawi, wakitoza ada fulani kwa kila kipande cha fedha walichobadilisha. Rejezo la Yesu kwao kuwa wapokonyaji ladokeza kwamba ada zao zilikuwa zenye kupita kiasi sana hivi kwamba walikuwa, kwa kweli, wakiwanyang’anya maskini fedha.
Baadhi yao hawangeweza kuleta wanyama wao wenyewe wa dhabihu. Yeyote aliyefanya hivyo ilimbidi mnyama wake achunguzwe na mkaguzi kwenye hekalu—kwa ada fulani. Wakiwa hawataki kujitia katika hatari ya kukataliwa kwa mnyama baada ya kumleta kutoka umbali mrefu, wengi walinunua mnyama “aliyekubaliwa” Kilawi kutoka kwa wachuuzi hao wafisadi kwenye hekalu. “Huko, wengi wa wakulima maskini walitozwa fedha kupita kiasi,” asema msomi mmoja.
Kuna uthibitisho kwamba Anasi, kuhani wa cheo cha juu wa zamani na familia yake walitarajia kunufaika kutokana na wafanya-biashara katika hekalu. Maandishi ya kirabi yasema juu ya “ile Minada ya [hekaluni] ya wana wa Anasi.” Ushuru kutoka kwa wabadili-fedha na kutokana na kuuza wanyama katika ardhi ya hekalu ulikuwa mojawapo ya vyanzo vyao vikuu vya mapato. Msomi mmoja asema kwamba tendo la Yesu la kuwafukuza wafanya-biashara “halikukusudiwa kuathiri tu hadhi ya makuhani bali pia chanzo chao cha mapato.” Hata sababu iwe nini, hapana shaka maadui wake walitaka kumwua!—Luka 19:45-48.
[Chati katika ukurasa wa 4]
Siku za Mwisho za Uhai wa Yesu wa Kibinadamu
Nisani 33 W.K. Matukio Mtu Mkuu Zaidi*
7 Ijumaa Yesu na mitume wake wasafiri kutoka 101, fu. 1
Yeriko kwenda Yerusalemu
(Nisani 7 yalingana na Jumapili,
Aprili 5, 1998, ingawa siku za
Kiebrania zilianza toka jioni moja
hadi ile nyingine)
8 Ijumaa jioni Yesu na wanafunzi wake wawasili 101, fu. 2-4
Bethania; Sabato yaanza
Jumamosi Sabato (Jumatatu, Aprili 6, 1998) 101, fu. 4
9 Jumamosi Mlo pamoja na Simoni mwenye ukoma; 101, fu. 5-9
jioni Maria amtia Yesu mafuta ya nardo;
wengi waja kutoka Yerusalemu kumwona
na kumsikiliza Yesu
Jumapili Kuingia kwa shangwe ya ushindi 102
Yerusalemu; afundisha hekaluni
10 Jumatatu Safari ya mapema kuingia Yerusalemu; 103, 104
asafisha hekalu; Yehova asema kutoka
mbinguni
11 Jumanne Katika Yerusalemu, afundisha hekaluni 105 hadi 112,
akitumia vielezi; awalaumu Mafarisayo; fu. 1
aona mchango wa mjane; atoa ishara ya
kuwapo kwake wakati ujao
12 Jumatano Siku yenye utulivu pamoja na wanafunzi 112, fu. 2-4
katika Bethania; Yudasi apanga usaliti
13 Alhamisi Petro na Yohana watayarisha kwa ajili ya 112, fu. 5 hadi Sikukuu ya Kupitwa katika 113, fu. 1
Yerusalemu; Yesu na wale mitume wengine
kumi wafuata baadaye alasiri
(Jumamosi, Aprili 11, 1998)
14 Alhamisi Sherehe ya Sikukuu ya Kupitwa; jioni 113, fu. 2
Yesu aosha miguu ya mitume; Yudasi hadi 117
aondoka kumsaliti Yesu; Kristo aanzisha
Ukumbusho wa kifo chake (Baada ya
mshuko-jua, Jumamosi, Aprili 11, 1998)
Baada ya Kusalitiwa na kukamatwa katika bustani 118 hadi 120
usiku wa ya Gethsemane; mitume wakimbia;
manane kufanyiwa kesi mbele ya makuhani wakuu
na Sanhedrini; Petro amkana Yesu
Ijumaa Mbele ya Sanhedrini tena; kwa Pilato, 121 hadi 127,
macheo hadi kisha kwa Herode, kisha kurudi kwa fu. 7
mshuko-jua Pilato; ahukumiwa kifo; atundikwa mtini;
azikwa
15 Jumamosi Sabato; Pilato aruhusu walinzi kwa ajili 127, fu. 8-10
ya kaburi la Yesu
16 Jumapili Yesu afufuliwa 128
* Nambari zenye kuorodheshwa hapa zinatambulisha sura kwenye kitabu Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi. Ili upate chati yenye marejezo ya Kimaandiko yenye mambo mengi kuhusu huduma ya Yesu ya mwisho, ona “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa,” ukurasa wa 290. Vitabu hivyo vimechapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.