Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Je, Mashahidi wa Yehova hukubali tiba zozote ambazo zimetokana na damu?
Kwa ujumla Mashahidi wa Yehova hawakubali damu. Tunaamini kabisa kwamba sheria ya Mungu kuhusu damu haiwezi kubadilishwa ili ipatane na maoni yanayobadilika-badilika. Hata hivyo, bado masuala mapya huzuka kwa sababu sasa damu inaweza kutenganishwa katika sehemu kuu nne na sehemu hizo kuu zinaweza kutenganishwa katika visehemu vingi. Ili Mkristo aamue kama atakubali sehemu hizo, anapaswa kuchunguza mambo mengi kuliko tu manufaa na hatari za kitiba ambazo huenda zikatokea. Mkristo anapaswa kuzingatia maoni ya Biblia na jinsi uhusiano wake na Mungu Mweza-Yote uwezavyo kuathiriwa.
Masuala muhimu yanayohusika si magumu. Na ili uone ni kwa nini tunasema hivyo, ebu uyafikirie mambo hayo Kibiblia, kihistoria, na kitiba.
Yehova Mungu alimwambia babu yetu Noa kwamba lazima damu ionwe kuwa kitu cha pekee. (Mwanzo 9:3, 4) Baadaye, sheria ambazo Mungu aliwapa Waisraeli zilionyesha utakatifu wa damu: “Mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni . . . atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu.” Mwisraeli anayekataa kufuata sheria ya Mungu angeweza kuwaathiri wengine; basi Mungu akaendelea kusema: “Nitamkatilia mbali na watu wake.” (Mambo ya Walawi 17:10) Baadaye, kwenye mkutano mmoja uliofanyiwa Yerusalemu, mitume na wazee waliagiza kwamba ni lazima ‘tujiepushe na damu.’ Kujiepusha na damu ni muhimu kama tu kujiepusha na ukosefu wa adili kingono na ibada ya sanamu.—Matendo 15:28, 29.
“Kujiepusha” kulimaanisha nini wakati huo? Wakristo hawakuwa wakila damu, iwe mbichi au iwe imegandishwa; wala hawakuwa wakila nyama ya mnyama ambaye damu yake haikumwagwa. Pia hawangekula vyakula ambavyo vilitiwa damu, kama vile soseji zenye damu. Kula damu katika njia yoyote kati ya hizo kungevunja sheria ya Mungu.—1 Samweli 14:32, 33.
Watu wengi katika nyakati za kale walikula damu bila wasiwasi, kama tuwezavyo kuona katika maandishi ya Tertullian (karne ya pili na ya tatu W.K.). Tertullian alitaja makabila ambayo yalifanya mkataba kwa kuonja damu alipokuwa akikanusha mashtaka ya uwongo yaliyodai eti Wakristo walikuwa wakila damu. Pia alisema kwamba “kunapokuwa na tamasha kwenye uwanja wa mchezo, [wengine] wamekunywa kwa pupa damu inayomtoka mtu mwenye hatia . . . ili wapone ugonjwa wa kifafa.”
Matendo hayo (hata kama Waroma fulani waliyafanya ili wawe na afya nzuri) hayakukubaliwa kwa Wakristo: “Hata hatuweki damu ya wanyama katika vyakula vyetu,” akaandika Tertullian. Waroma walikuwa wakitumia vyakula vyenye damu ili kujaribu uaminifu-maadili wa Wakristo halisi. Tertullian aliendelea kusema: “Sasa, ebu niwaulize, mnajua kwa hakika ya [kwamba Wakristo] huchukizwa kabisa na damu ya wanyama, basi kwa nini mseme eti wao wana tamaa ya kunywa damu ya wanadamu?”
Leo, si watu wengi wanafikiria kwamba sheria za Mungu Mweza Yote zinahusika daktari anapowadokezea kwamba watumie damu. Ingawa kwa kweli Mashahidi wa Yehova wanataka kuendelea kuishi, tumeazimia kutii sheria ya Yehova kuhusu damu. Hilo lamaanisha nini kuhusu tiba ya wakati huu?
Utiaji-damu mishipani ulipoongezeka sana baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, Mashahidi wa Yehova waling’amua kwamba jambo hilo linapinga sheria ya Mungu—na bado tunaamini hivyo. Lakini tiba imebadilika katika muda ambao umepita. Leo, mara nyingi watu hawatiwi mishipani damu nzima ambayo haijatenganishwa, bali wao hutiwa mojawapo ya zile sehemu zake kuu: (1) chembe nyekundu; (2) chembe nyeupe; (3) vigandisha-damu; (4) plazima (umajimaji wa damu). Ikitegemea hali ya mgonjwa, matabibu wanaweza kuagiza wagonjwa wapewe chembe nyekundu, chembe nyeupe, vigandisha-damu, au plazima. Kutia mishipani sehemu hizo kuu za damu hufanya iwezekane kugawa painti ya damu na kuitumia kwa wagonjwa wengi. Mashahidi wa Yehova wanaamini kwamba kukubali damu nzima ambayo haijatenganishwa au kutiwa yoyote kati ya zile sehemu zake kuu nne kunapinga sheria ya Mungu. Jambo la kutokeza ni kwamba kushikilia msimamo huo unaoungwa mkono na Biblia kumewaepusha na hatari nyingi, kama maradhi ya mchochota wa ini na UKIMWI ambayo yanaweza kuambukiza mtu kupitia damu.
Kwa kuwa damu inaweza kutenganishwa hata zaidi ya sehemu hizo kuu, maswali huzuka kuhusu visehemu vya zile sehemu kuu za damu. Visehemu hivyo hutumiwaje, na Mkristo anapaswa kuzingatia nini anapofanya uamuzi kuvihusu?
Damu ina sehemu nyingi sana. Hata plazima—ambayo asilimia 90 yake ni maji—ina homoni nyingi, chumvi, vimeng’enya, na lishe, kutia ndani madini na sukari. Plazima pia ina protini kama vile albumin, vigandishaji, na fingo za kupigana na maradhi. Wataalamu hutoa protini kutoka kwenye plazima na kuzitumia. Kwa mfano, kigandishaji aina ya factor VIII kimetumiwa kuwatibu watu ambao damu zao hazigandi, ambao huvuja damu kwa urahisi. Au kama mtu yuko katika hatari ya kuambukizwa maradhi ya aina fulani, madaktari wanaweza kuagiza mtu huyo adungwe sindano za gamma globulin, ambazo zimetolewa kwenye plazima ya damu ya watu ambao tayari wana kinga dhidi ya maradhi hayo. Protini nyingine za plazima hutumiwa kwa tiba, lakini zile ambazo zimetajwa zinaonyesha jinsi sehemu kuu ya damu (plazima) inavyoweza kutenganishwa ili kupata visehemu vyake.a
Kama vile tu plazima ya damu inavyoweza kutokeza visehemu kadhaa, zile sehemu kuu nyinginezo (chembe nyekundu, chembe nyeupe, vigandisha-damu) zinaweza kutenganishwa ili kupata sehemu nyinginezo ndogo zaidi. Kwa mfano, chembe nyeupe za damu zinaweza kutokeza protini zinazoitwa interferon na interleukin, ambazo hutumiwa kutibu maambukizo fulani ya virusi na kansa. Vigandisha-damu vinaweza kutenganishwa ili kupata ile sehemu yake ambayo huponesha vidonda. Na dawa nyinginezo bado zinaendelea kutengenezwa (angalau dawa zilizotengenezwa kwanza-kwanza) kutokana na sehemu za damu. Tiba hizo hazihusishi kutiwa mishipani zile sehemu kuu za damu; mara nyingi huhusisha visehemu vyake tu. Je, Wakristo wakubali kutibiwa kwa kutumia visehemu hivyo? Hatuwezi kusema. Biblia haitaji mambo hayo madogo-madogo, kwa hiyo ni lazima Mkristo afanye uamuzi wake mwenyewe unaotegemea dhamiri yake mbele za Mungu.
Watu wengine watakataa kitu chochote ambacho kimetokana na damu (hata vile visehemu ambavyo vimekusudiwa kuandaa kinga ya muda). Hivyo ndivyo wao wanavyoelewa amri ya Mungu ya ‘kujiepusha na damu.’ Wanaona kwamba sheria aliyowapa Waisraeli ilisema kwamba damu iliyotolewa kwa mnyama ilipaswa ‘kumwagwa juu ya nchi.’ (Kumbukumbu la Torati 12:22-24) Kwa nini jambo hilo linatuhusu? Ili kutayarisha gamma globulin, vigandishaji ambavyo vimetolewa kwenye damu, na kadhalika, kwahitaji damu ikusanywe na kutenganishwa. Kwa hiyo, Wakristo wengine hukataa visehemu hivyo vya damu, kama wanavyokataa kutiwa mishipani damu nzima ambayo haijatenganishwa au sehemu zake kuu nne. Msimamo wao wa moyo mweupe na unaotegemea dhamiri zao wapasa kustahiwa.
Wakristo wengine hufanya uamuzi tofauti. Wao pia hukataa kutiwa mishipani damu nzima ambayo haijatenganishwa, chembe nyekundu, chembe nyeupe, au vigandisha-damu, au plazima. Lakini wanaweza kumruhusu daktari awatibu akitumia visehemu vilivyotolewa kwenye zile sehemu kuu za damu. Na kunaweza kuwa na tofauti katika mambo haya vilevile. Mkristo mmoja anaweza kukubali adungwe sindano za gamma globulin, lakini huenda akubali au akatae kudungwa sindano ambayo ina kitu kilichotolewa kwenye chembe nyekundu au chembe nyeupe. Lakini, kwa ujumla ni nini ambacho huenda kikawafanya Wakristo wengine wafikie uamuzi wa kwamba wanaweza kukubali visehemu vya damu?
Makala ya “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika Mnara wa Mlinzi la Juni 1, 1990, ilisema kwamba protini za plazima (visehemu) hutoka kwenye damu ya mwanamke mja-mzito na kuingia kwenye mfumo tofauti wa damu wa kijusi. Kwa njia hiyo, mama humpitishia mtoto wake protini za kinga, akimpa kinga muhimu. Zikiwa peke yao, chembe nyekundu za kijusi zimalizapo duru yao ya kawaida ya maisha, sehemu zao zenye kubeba oksijeni hutenganishwa. Sehemu zake nyingine huwa bilirubin, ambayo huvuka kondo la nyuma na kuingia kwenye mama na kuondolewa pamoja na takataka za mwili. Wakristo wengine wanaweza kuamua kwamba kwa kuwa visehemu vya damu vinaweza kupita na kuingia katika mtu mwingine kiasili, wao wanaweza kukubali kisehemu cha damu ambacho kimetolewa kwenye plazima au chembe za damu.
Je, jambo la kwamba maoni na maamuzi yanayotegemea dhamiri yaweza kutofautiana laonyesha kwamba hilo ni jambo dogo tu? La. Jambo hilo ni zito. Lakini, jambo moja ni wazi. Habari ambazo zimetajwa zaonyesha kwamba Mashahidi wa Yehova hukataa kutiwa mishipani damu nzima ambayo haijatenganishwa na pia zile sehemu kuu za damu. Biblia inawaagiza Wakristo ‘wajiepushe na vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu na damu na kutokana na vitu vilivyonyongwa na uasherati.’ (Matendo 15:29) Mbali na hayo, tiba inapohusu visehemu vya sehemu yoyote kuu ya damu, ni lazima kila Mkristo ajiamulie kulingana na dhamiri yake baada ya kutafakari jambo hilo kwa sala.
Watu wengi wangekubali tiba yoyote ambayo inaonekana kuwapa nafuu mara moja, hata tiba inayojulikana kuwa hatari kwa afya, kama tiba inayotokana na damu. Mkristo mwenye moyo mweupe hujaribu kuwa na maoni pana na yenye usawaziko, yanayofikiria mambo mengi kuliko kuzingatia tu faida za sasa. Mashahidi wa Yehova huthamini jitihada zinazofanywa ili kuandaa tiba bora, nao hupima hatari na manufaa za tiba yoyote ile. Lakini, kuhusu tiba inayotokana na damu, wao hufikiria kwa makini maoni ya Mungu na uhusiano wao binafsi na Mpaji wetu wa Uhai.—Zaburi 36:9.
Ni baraka kama nini kwa Mkristo kuwa na uhakika kama wa mtunga-zaburi aliyeandika: “BWANA, Mungu, ni jua na ngao, BWANA atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema hao waendao kwa ukamilifu. Ee BWANA . . . , heri mwanadamu anayekutumaini wewe”!—Zaburi 84:11, 12.
[Maelezo ya Chini]
a Ona “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika Mnara wa Mlinzi la Novemba 15, 1978, na Oktoba 1, 1994. Kampuni za dawa zimetengeneza dawa fulani ambazo hazitokani na damu na ambazo unaweza kuagizwa utumie badala ya visehemu vya damu vilivyotumiwa wakati uliopita.
[Sanduku katika ukurasa wa 30]
MASWALI YANAYOPENDEKEZWA KUMWULIZA DAKTARI
Ikiwa utafanyiwa upasuaji au kutibiwa kwa dawa ambayo huenda inatokana na damu, uliza:
Je, wote wanaohusika kunitibu wanajua ya kwamba, mimi nikiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, naagiza ya kwamba nisitiwe damu mishipani kamwe (damu nzima ambayo haijatenganishwa, chembe nyekundu, chembe nyeupe, vigandisha-damu, au plazima ya damu) katika hali yoyote ile?
Ikiwa unaagizwa kutumia dawa yoyote ambayo huenda imetokana na plazima ya damu, chembe nyekundu au chembe nyeupe, au vigandisha-damu, uliza:
Je, dawa hiyo imetokana na mojawapo ya zile sehemu kuu nne za damu? Ikiwa ndivyo, nieleze imefanyizwa kwa vitu gani?
Huenda nikatumia kiasi gani cha dawa hii ambayo imetokana na damu, na nitaitumia kwa njia gani?
Dhamiri yangu ikiniruhusu kukubali dawa hii yenye kisehemu cha damu, kuna hatari gani za kiafya?
Dhamiri yangu ikinifanya nikatae dawa hii yenye kisehemu cha damu, kuna tiba gani nyingine ambayo inaweza kutumiwa?
Baada ya kufikiria zaidi jambo hili, naweza kukujulisha lini uamuzi wangu?