Pontio Pilato Alikuwa Nani?
“PILATO alikuwa mtu mwenye dhihaka, mwenye kutilia shaka mambo, na anayewashangaza watu. Watu fulani humwona kuwa mtakatifu, wengine humwona kuwa mtu dhaifu, mwanasiasa aliyekuwa tayari kumdhabihu mtu mmoja ili kuepuka mizozo.”—Pontius Pilate, kitabu kilichoandikwa na Ann Wroe.
Uwe unakubaliana na maoni hayo au la, Pontio Pilato alijulikana sana kwa sababu ya jinsi alivyomtendea Yesu Kristo. Pilato alikuwa nani? Tunajua nini kumhusu? Kufahamu vizuri cheo chake kutatusaidia kuelewa matukio muhimu zaidi kuwahi kutukia duniani.
Cheo, Kazi, na Mamlaka
Maliki Mroma Tiberio alimtawaza Pilato kuwa gavana wa mkoa wa Yudea mwaka wa 26 W.K. Maliwali kama hao walikuwa wanajeshi wa kupanda farasi, yaani, walikuwa na cheo cha chini, wakilinganishwa na watu waliokuwa na vyeo vya juu serikalini. Yaelekea Pilato alijiunga na jeshi akiwa kamanda wa cheo cha chini; kisha akapandishwa cheo hatua kwa hatua; na hatimaye akawekwa rasmi kuwa gavana akiwa na umri usiozidi miaka 30.
Pindi fulani, Pilato alivalia mavazi ya kijeshi, yaani, koti la ngozi na bamba la kifuani la chuma. Hadharani alivalia kanzu nyeupe yenye pindo za zambarau. Huenda alikuwa na nywele fupi na alinyoa ndevu zote. Ingawa watu fulani huamini kwamba alitoka Hispania, jina lake linaonyesha alikuwa wa kabila la Pontii, yaani, wakuu wa Wasamnite kutoka kusini mwa Italia.
Kwa kawaida maliwali wa cheo cha Pilato walitumwa katika maeneo yasiyostaarabika. Waroma waliona Yudea kuwa mojawapo ya maeneo hayo. Mbali na kudumisha amani, Pilato alisimamia kodi zisizo za moja kwa moja na kodi ya kichwa. Kila siku mahakama za Wayahudi zilishughulikia udumishaji wa haki, lakini kesi zilizohitaji hukumu ya kifo zilipelekwa kwa gavana, ambaye alikuwa na mamlaka kuu zaidi ya kuhukumu.
Pilato na mke wake pamoja na waandishi wachache, marafiki na wajumbe kadhaa, waliishi katika jiji la bandarini la Kaisaria. Pilato alisimamia vikosi vitano vya wanajeshi wa kwenda kwa miguu, kila kimoja kikiwa na watu 500 hadi 1,000 na pia wanajeshi 500 wanaopanda farasi. Kwa ukawaida askari wake waliwatundika watu waliovunja sheria. Kulipokuwa na amani, wakosaji waliuawa baada ya kesi kusikilizwa kwa muda mfupi, lakini kulipokuwa na ghasia, waasi waliuawa papo hapo wakiwa wengi. Kwa mfano, Waroma waliwatundika watumwa 6,000 ili kukomesha uasi ulioongozwa na Spartacus. Kulipokuwa na matatizo huko Yudea, kwa kawaida gavana aliwasiliana na mwakilishi wa maliki huko Siria ambaye alisimamia vikosi vya wanajeshi 3,000 hadi 6,000. Hata hivyo, kwa muda mwingi ambao Pilato alikuwa gavana, hakukuwa na mwakilishi huko Siria na hivyo Pilato alilazimika kukomesha ghasia upesi.
Kwa kawaida, magavana waliwasiliana na maliki. Mambo yaliyohusu cheo chake au tisho lolote kuelekea utawala wa Roma lilipaswa kuripotiwa kwa maliki, kisha sheria za kifalme zingetungwa. Yaelekea gavana alijitahidi kumweleza maliki mambo yanayohusu mkoa wake kabla ya watu kulalamika. Matatizo yalipoanza huko Yudea, Pilato alikuwa na wasiwasi sana.
Mbali na masimulizi ya Injili, wanahistoria Flavio Yosefo na Philo ndio walioandika mambo mengi kumhusu Pilato. Pia, mwanahistoria Mroma, Tasito alieleza kwamba Pilato alimuua Christus, ambaye Wakristo wanaitwa kwa jina lake.
Hasira ya Wayahudi Yachochewa
Yosefo anasema kwamba kwa sababu ya sheria ya Wayahudi iliyopinga kutengeneza sanamu, magavana Waroma hawakupeleka huko Yerusalemu bendera za kijeshi zilizokuwa na sanamu za maliki. Kwa kuwa Pilato hakuheshimu sheria hiyo, Wayahudi wenye hasira walipeleka malalamiko yao Kaisaria. Kwa siku tano, Pilato hakuchukua hatua yoyote. Siku ya sita, akawaamuru askari wake wawazingire walalamikaji na kutisha kuwaua iwapo hawatatawanyika. Wayahudi waliposema kwamba afadhali wafe kuliko kuona Sheria yao ikivunjwa, Pilato alitulia na kuamuru sanamu hizo ziondolewe.
Pilato hakujizuia kutumia nguvu. Katika kisa kimoja kilichoandikwa na Yosefo, Pilato alianzisha mradi wa kutengeneza mfereji wa kuleta maji Yerusalemu na kuendeleza mradi huo kwa kutumia pesa za hazina ya hekalu. Pilato hakuchukua pesa hizo waziwazi, kwa kuwa alijua kwamba ni kukufuru kupora hekalu, na hilo lingewafanya Wayahudi wenye hasira wamwombe Tiberio amfute kazi. Hivyo, yaelekea Pilato alishirikiana na wasimamizi wa hekalu. Pesa zilizowekwa wakfu, zilizoitwa “korbani” zingeweza kutumiwa kihalali kufanya kazi ambazo zingewanufaisha wakaaji wa jiji. Lakini maelfu ya Wayahudi walikusanyika kuonyesha ghadhabu yao.
Pilato aliwaagiza askari wachangamane na umati, naye akawaamuru wasitumie upanga bali wawapige walalamikaji kwa rungu. Yaelekea alitaka kuudhibiti umati bila kuchochea mauaji. Inaonekana alifaulu, ingawa watu kadhaa walikufa. Huenda watu waliomwambia Yesu kwamba Pilato alichanganya damu ya Wagalilaya na dhabihu zao walikuwa wakirejelea tukio hilo.—Luka 13:1.
“Kweli Ni Nini?”
Pilato alijulikana kwa sababu ya uchunguzi aliofanya kuhusu mashtaka ya makuhani wakuu Wayahudi na wanaume wazee yaliyosema kwamba Yesu alijifanya kuwa Mfalme. Aliposikia kwamba Yesu alikuja kutoa ushahidi kwa ajili ya ile kweli, Pilato aliona kwamba mfungwa huyo hakuwa tisho kwa Roma. “Kweli ni nini?” akauliza, akifikiri kwamba kweli ni wazo lisiloweza kueleweka na halihitaji kufikiriwa sana. Alikata kauli gani? “Mimi sioni uhalifu wa mtu huyu.”—Yohana 18:37, 38; Luka 23:4.
Huo ungekuwa mwisho wa kesi ya Yesu, lakini Wayahudi walisisitiza kwamba alikuwa analipindua taifa. Wivu ndio uliowafanya makuhani wakuu wamshtaki Yesu, na Pilato alijua hivyo. Pia, alijua kwamba kumwachilia Yesu kungeleta shida, na alitaka kuepuka jambo hilo. Tayari kulikuwa na matatizo mengi, kwa kuwa Baraba na wengine walikuwa kifungoni kwa shtaka la uchochezi na mauaji. (Marko 15:7, 10; Luka 23:2) Isitoshe, mizozo iliyokuwa imetokea kati ya Pilato na Wayahudi ilikuwa imemharibia sifa mbele ya Tiberio aliyejulikana kwa kuwachukulia hatua kali magavana wabaya. Hata hivyo, kukubaliana na Wayahudi kungeonyesha udhaifu. Hivyo, Pilato hakujua la kufanya.
Baada ya kujua Yesu alitoka eneo gani, Pilato alijaribu kutuma kesi hiyo kwa Herode Antipa, mtawala wa wilaya ya Galilaya. Hilo lilipokosa kufaulu, Pilato alijaribu kuwashawishi watu waliokusanyika nje ya nyumba yake waombe Yesu aachiliwe kulingana na desturi yake ya kumfungulia mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Umati ulipaaza sauti ukimtaka Baraba.—Luka 23:5-19.
Huenda Pilato alitaka kufanya lililo sawa, lakini alitaka pia kutetea cheo chake na kuupendeza umati. Mwishowe, badala ya kusikiliza dhamiri yake na kufuatia haki, alitanguliza kazi yake. Aliomba maji, akanawa mikono na kudai kwamba hakuwa na hatia kwa kifo ambacho aliamuru.a Ingawa alijua kwamba Yesu hakuwa na hatia, Pilato aliagiza apigwe mijeledi na kuwaruhusu askari-jeshi wamdhihaki, wampige, na kumtemea mate.—Mathayo 27:24-31.
Pilato alijaribu kwa mara ya mwisho kumwachilia Yesu, lakini watu wakapaaza sauti kwamba akimfungua, yeye si rafiki ya Kaisari. (Yohana 19:12) Pilato aliposikia hivyo, alifanya walivyotaka. Msomi mmoja alisema hivi kuhusu uamuzi wa Pilato: “Suluhisho ni rahisi: muue mtu huyo. Kinachopotea tu ni uhai wa Myahudi mmoja ambaye anaonekana kuwa hana maana yoyote; ungekuwa upumbavu kusababisha ghasia kwa sababu yake.”
Ni Nini Kilichompata Pilato?
Tukio la mwisho lililorekodiwa kuhusu maisha ya Pilato lilihusu mapambano. Yosefo anasema kwamba Wasamaria wengi wenye silaha walikusanyika kwenye Mlima Gerizimu wakitaka kufukua hazina ambazo walidhani zilizikwa huko na Musa. Pilato aliingilia kati, na majeshi yake yakawaua watu kadhaa. Wasamaria walipeleka malalamiko yao kwa Lusio Vitelio, gavana wa Siria aliyekuwa na cheo cha juu kuliko Pilato. Hatujui iwapo Vitelio aliona kwamba Pilato alikuwa amepita mipaka. Hata hivyo, alimwamuru Pilato aende Roma kujibu mashtaka hayo mbele ya maliki. Lakini kabla ya kufika huko, Tiberio akafa.
“Baada ya hapo, Pilato hatajwi tena katika historia ila katika hekaya mbalimbali,” lasema gazeti moja. Lakini watu kadhaa wamejaribu kueleza zaidi. Imedaiwa kwamba Pilato alibadilika akawa Mkristo. “Wakristo” wa Ethiopia wanamwona kuwa “mtakatifu.” Eusebio, aliyeandika mwishoni mwa karne ya tatu na mwanzoni mwa karne ya nne, alikuwa wa kwanza kati ya wengi kusema kwamba Pilato alijiua kama Yuda Iskariote. Hata hivyo, hakuna anayejua kwa hakika kilichompata Pilato.
Yaelekea Pilato alikuwa mkaidi, asiyejali, na mkandamizaji. Hata hivyo, tofauti na maliwali wengi wa Yudea ambao walikuwa na cheo hicho kwa muda mfupi, Pilato alikuwa gavana kwa miaka kumi. Kwa maoni ya Waroma, Pilato alikuwa gavana hodari. Ametajwa kuwa mtu mwoga ambaye alikuwa na hatia ya kuruhusu Yesu ateswe na kuuawa ili ajifaidi. Wengine wanasema kwamba kazi ya Pilato haikuwa kutetea haki bali ilikuwa kudumisha amani na hali njema ya Waroma.
Siku za Pilato zilikuwa tofauti sana na zetu. Hata hivyo, hakuna hakimu anayefuata haki anayeweza kumhukumu mtu ikiwa anamwona kuwa hana hatia. Kama Pontio Pilato hangekutana na Yesu, jina lake halingekuwa maarufu sana.
[Maelezo ya Chini]
a Kunawa mikono kulikuwa desturi ya Kiyahudi wala si ya Kiroma, njia ambayo ilionyesha kwamba mtu hakuwa na hatia ya damu.—Kumbukumbu la Torati 21:6, 7.
[Picha katika ukurasa wa 11]
Maandishi haya yanayomtambulisha Pontio Pilato kuwa liwali wa Yudea yalipatikana Kaisaria