JE, NI KAZI YA UBUNI?
Umbo la V la Kipepeo Anayeitwa Cabbage White
Kipepeo anategemea joto la jua kupasha misuli yake kabla ya kuanza kuruka. Lakini katika siku zenye mawingu kipepeo wa cabbage white anaruka mapema kabla ya vipepeo wengine. Kwa nini anafaulu kufanya hivyo?
Jambo la kufikiria: Kabla ya kuruka, vipepeo wengi huota jua mabawa yao yakiwa yamefungwa au yakiwa yamelazwa chali. Hata hivyo, kipepeo wa cabbage white hufanya hivyo mabawa yake yakiwa wima katika umbo la herufi V. Utafiti umeonyesha kwamba ili kupata joto jingi iwezekanavyo, kipepeo anahitaji kuwa na kila bawa likiwa limefunguka katika pembe ya digrii 17 hivi. Mkao huo huelekeza joto la jua moja kwa moja kwenye misuli inayomsaidia kuruka na kuipasha joto ili kipepeo aweze kuruka.
Watafiti katika Chuo Kikuu cha Exeter, Uingereza, walichunguza ikiwa wanaweza kuboresha vifaa vinavyotokeza umeme kwa kutumia miale ya jua kwa kuviweka katika umbo la herufi V la kipepeo huyo. Walipofanya hivyo, waligundua kwamba nishati iliyotokezwa iliongezeka kwa asilimia 50 hivi.
Pia, watafiti waligundua kwamba sehemu ya juu ya bawa la kipepeo inaakisi mwanga sana. Kwa kuiga umbo la kipepeo huyo na muundo wa bawa lake unaoakisi mwanga, watafiti walitokeza vifaa vyepesi na vinavyotokeza umeme mwingi zaidi kutokana na jua. Matokeo hayo yalifanya Profesa Richard ffrench-Constant, ambaye ni mshiriki wa kikundi hicho cha watafiti, aseme kwamba kipepeo huyo ni “mtaalamu wa kuvuna nishati ya jua.”
Una maoni gani? Je, umbo la V la kipepeo anayeitwa cabbage white lilijitokeza lenyewe? Au lilibuniwa?