Barabara—Njia Kuu za Ustaarabu
TANGU zamani za kale, watu wamewasiliana kupitia kwa mfumo mkubwa wa vijia, barabara, na barabara kuu. Hizi huthibitisha tamaa ya mwanadamu ya kusafiri na ya kufanya biashara—na pia kupigana vita na kujenga milki. Vilevile barabara hufunua upande mbaya wa utu wa mwanadamu.
Historia ya barabara, tangu wakati wanadamu na wanyama walipoanza kutumia vijia vya awali, hadi njia zetu za kisasa za kasi zenye migawanyo mingi, si safari ya kuwaziwa tu ya wakati uliopita. Ni uchunguzi wa asili ya kibinadamu pia.
Barabara za Awali
“Wajenzi wa kwanza wenye dhati wa barabara,” yasema The New Encyclopædia Britannica, “yawezekana walikuwa Wamesopotamia.” Watu hawa waliishi katika eneo la mito Tigri na Frati. Barabara zao za kufanyia maandamano, chanzo hiki chaongeza kusema, “zilikuwa barabara zilizolainishwa ambapo matofali na mawe yaliyochomwa yalitandazwa kwa chokaa ya lami.” Ufafanuzi huo hutukumbusha isemavyo Biblia kuhusu vifaa vya mapema vya ujenzi: “Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa.”—Mwanzo 11:3.
Barabara zilikuwa muhimu kwa Waisraeli wa kale katika kuwawezesha kutimiza wajibu wao wa kidini. Yapata miaka 1,500 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Waisraeli waliamriwa hivi: “Mara tatu kwa mwaka na watokee [wanaume] wako wote mbele za BWANA, Mungu wako, [kuadhimisha sherehe ya kiroho] mahali atakapochagua.” (Kumbukumbu la Torati 16:16) Mahali hapo pakawa Yerusalemu, na nyakati nyingi, familia nzima-nzima zingehudhuria pindi hizi zenye shangwe. Barabara nzuri zilikuwa za lazima!
Kwa wazi, njia kuu zilijengwa vizuri. Mwanahistoria Myahudi Flavius Josephus alisema hivi juu ya Solomoni, aliyetawala miaka elfu moja kabla ya kuzaliwa kwa Kristo: “Hakuachilia kutunza barabara, bali kandokando mwa barabara alijenga njia zilizoinuka zilizoelekea Yerusalemu kwa mawe meusi.”
Israeli lilikuwa na majiji sita ya makimbilio yaliyowapa waua-binadamu hifadhi. Barabara za kuingia majiji haya zilitunzwa vizuri pia. Na mapokeo ya Kiyahudi huonyesha kwamba vigingi vya kuonyesha ishara vilivyotunzwa vizuri vilivyoelekeza kwenye jiji la makimbilio la karibu, viliwekwa kwenye kila mkingamo wa barabara.—Hesabu 35:6, 11-34.
Barabara zikaja kuwa muhimu katika kueneza biashara, na moja ya bidhaa za nyakati za kale zilizotamaniwa zaidi ilikuwa hariri. Yasemekana kwamba muda mrefu kabla ya Waisraeli kuwa taifa, Wachina waligundua namna ya kutengeneza hariri kutoka kwenye uzi uliotengenezwa na nondo wa hariri lakini wakaiweka ikiwa siri hadi baada ya kuzaliwa kwa Kristo. Hata kabla ya wakati huo, hariri ilipendwa sana katika ulimwengu wa Magharibi hivi kwamba kulingana na kitabu A History of Roads, cha Geoffrey Hindley, amri zilitolewa “ili kuzuia wanaume kutozitumia,” kwani kuzitumia “kulionwa kuwa hali ya kike.”
Njia ya kufanyia biashara iliyotumiwa kusafirisha hariri kutoka China ilijulikana kama Barabara ya hariri. Kufikia wakati Marco Polo alipotumia barabara hiyo kwenda China mwishoni mwa karne ya 13 W.K., tayari ilikuwapo kwa miaka 1,400. Kwa zaidi ya miaka 2,000, Barabara ya Hariri ndiyo iliyokuwa ndefu zaidi ulimwenguni. Barabara hiyo ilikuwa na urefu wa kilometa zipatazo 12,800 tokea Shanghai, China, ambako hariri ilianzia, hadi Gades (Cádiz ya kisasa), Hispania.
Umuhimu wa Kijeshi
Hatua kubwa zaidi katika ujenzi wa barabara zilitokana na ile tamaa ya kuwa na milki. Kwa kielelezo, mfumo wa barabara ya Milki ya Roma chini ya Kaisari, ulienea kotekote katika Ulaya, Afrika Kaskazini, na Mashariki ya Kati kufikia jumla iliyokadiriwa kuwa kilometa 80,000. Wakati majeshi ya Roma hayakuwa vitani, mara nyingine yalipewa kazi ya kujenga na kurekebisha barabara.
Umuhimu wa barabara katika ushindi ulitolewa kielezi katika nyakati za karibuni pia. Utafutaji wa Adolf Hitler wa kutawala watu wengine uliharakishwa na mpango wake wa kujengwa kwa barabara pana za Ujerumani ulioanza katika 1934. Kulingana na mwanahistoria Hindley, programu hii iliwawezesha Wajerumani kuwa na “mfumo wa kwanza wa barabara kuu za magari ya mwendo wa kasi ulimwenguni.”
Ujenzi wa Barabara—Ni Ufundi
Wapima-barabara wa Roma, wakitumia chombo kilichoitwa groma, walijenga barabara zilizonyooka kama mkuki. Waashi walichonga kistadi mawe, ya kuonyesha umbali, na wahandisi wakaweka kiwango cha uzito wa mashehena. Barabara zilikuwa zenye msingi na nyuso imara. Jambo hasa lililofanya barabara zidumu ni mfumo bora wa kupitisha maji machafu ulioboreshwa na mpindo wa kadiri kutia na mwinuko wa barabara juu ya maeneo yaliyokuwa karibu. Hivyo, neno “barabara kuu” likatungwa. Hata maduka yaliuza ramani za barabara.
“Akikabiliwa na mafanikio ya Waroma wakiwa wajenzi wa barabara,” asema mwanahistoria fulani, “mwandikaji hujipata akijizuia kutoa pongezi zinazopita kiasi, na inatilika shaka kama kuna nguzo ya ukumbusho nyingineyo ya Mwanadamu iliyotoa utumishi wa muda mrefu kuliko barabara za Italia.”
Barabara ya Apio, ianziayo kusini kutoka Roma, kulingana na A History of Roads, “ndiyo barabara ya kwanza iliyolainishwa yenye urefu wowote ule katika historia ya wafanyakazi wa nchi za Magharibi.” Hii barabara kuu mashuhuri ilikuwa na upana wa meta sita na ililainishwa kwa vipande vikubwa vya lava. Akiwa njiani kwenda Roma akiwa mfungwa, mtume Paulo alisafiri kupitia njia hii, ambayo sehemu zake fulani zingali zatumika leo.—Matendo 28:15, 16.
Watu wengi waweza kuona ustadi wa ujenzi wa barabara wa Wahindi wa Amerika Kusini wa mapema, kuwa wenye kushangaza vilevile. Kuanzia miaka ya 1200 kufikia miaka ya 1500, Wainka walijenga mfumo wa barabara wa kilometa 16,000, uliounganisha taifa la watu wapatao 10,000,000. Barabara hizi zilipitia sehemu mbovu zaidi zilizochongoka ziwazikazo, zikipitia jangwani na misitu ya mvua na hata zikipita ng’ambo ya milima yenye fahari ya Andes ya Peru!
Kuhusu barabara moja, The New Encyclopædia Britannica huripoti hivi: “Njia ya mlima Andes ilikuwa ya kipekee. Njia ya barabara hiyo ilikuwa yenye upana wa meta 7.5 na ilipitia kwenye safu za milima mirefu zaidi zenye kujipindapinda na miteremko rahisi. Ilihusisha miingilio myembamba iliyotengenezwa kwa jiwe gumu na iliyoshikilia kuta ndefu zilizojengwa ili kutegemeza njia ya barabara. Mabonde na nyufa kubwa yalizibwa kwa mawe mazito nayo madaraja ya kuning’inizwa ya kamba nene za kitani au sufu yalipita juu ya vijito vinene vya mlima. Sehemu yake ya juu ilikuwa ya mawe, nayo lami ilitumiwa kwa kiasi kikubwa.”
Farasi hakujulikana kwa Wainka, lakini mfumo wa barabara zao uliwaandaa na kilichoitwa “uwanja halisi wa wajumbe wa kifalme wa kukimbilia.” Mwanahistoria mmoja aliandika hivi: “Kandokando ya kijia chote mlikuwa na vigingi vya vituo vya kupumzikia, vyenye umbali wa kilometa mbili kutoka kingine, kila kimoja kikiwa na kijumba kidogo cha kijeshi na wapokezanaji wa wakimbiaji wa kulipwa. Kila kituo kilikuwa na umbali mfupi kwa ajili ya mpokezano wa upesi na, kikifanya kazi mchana na usiku, utumishi huo ungepeleka ujumbe kutoka mji mkuu wa Cuzco hadi jiji la Quito, umbali wa kilometa 2,000 kwa siku tano tu. Hii ilimaanisha kutumia kwa wastani kilometa 15 kwa saa moja katika barabara isiyopungua meta 4,000 juu ya usawa wa bahari—mwendo usiopata kufikiwa kamwe na mfumo wa kawaida wa posta ya serikali ya Roma!”
Chanzo cha Misiba
Mishipa ya damu ya mwili wa kibinadamu yaweza kuzibika, na hili laweza kuwa na matokeo mabaya sana. Vivyohivyo, barabara zilizowahi kutumika katika kuendeleza ubora wa maisha, zaweza kuzibika na kuchangia kupunguza ubora wake. Barabara zinazopitia kwenye misitu ya mvua, nyikani, kichakani, na mbuga za kitaifa huwadhuru wanyama. Na nyakati nyingi wazaliwa na nyumba zao za msituni hudhurika pia. Kitabu How We Build Roads chasema hivi: “Barabara Kuu ya Amazon, ijapokuwa ilitengenezwa kwa sababu ya maendeleo, iliharibu sehemu kubwa ya msitu wa mvua na ilikuwa msiba kwa wakazi wengi wa msituni, kwa kuwa iliharibu namna yao yote ya maisha.”
Majiji pia yanapata matokeo mabaya kwa kuwa kila mwaka magari zaidi na zaidi yanaziba njia kuu za mijini. Hatimaye, fedha zipatikanapo, barabara kuu hujengwa. Lakini hatimaye, barabara hizi kuu huendeleza misongamano zaidi ya magari, inayoongeza uchafuzi wa hewa yenye kudhuru mamilioni ya watu. Isitoshe, watu wapatao 500,000 ulimwenguni pote hufa barabarani kila mwaka, na wengine milioni 15 hujeruhiwa, wengine vibaya sana. Kwa kulinganisha, katika Vita ya Ulimwengu ya Kwanza wapiganaji wapatao milioni tisa walikufa. Lakini vita hivyo vilikoma. Kwa upande mwingine, vifo vya barabarani ni vya kila siku—zaidi ya vifo 1,000 kila siku, siku baada ya siku!
Naam, kwa njia nyingi barabara zetu ni taarifa kutuhusu sisi—shahidi anayedokeza uwezo na udhaifu wetu. Hizo pia husema tuyawazayo juu ya sayari hii yetu yenye fahari tuliyopewa tuitunze.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Njia ya Apio, aliyopitia mtume Paulo, ingali yatumika
[Picha katika ukurasa wa 22]
Karibu watu 500,000 ulimwenguni pote hufa kila mwaka katika aksidenti za barabarani