Hawakujifanyia Jina Maarufu
BIBLIA haitoi majina ya wajenzi wa ule mnara wa Babeli wenye sifa mbaya. Simulizi lataarifu hivi: “Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina [“jina maarufu,” NW); ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.”—Mwanzo 11:4, italiki ni zetu.
‘Waliosema’ walikuwa nani? Tukio hilo lilitokea yapata miaka 200 baada ya Furiko. Kufikia wakati huo Noa, aliyekuwa na umri wa karibu miaka 800, aliishi miongoni mwa maelfu ya wazao wake. Wote walisema lugha ileile na waliishi pamoja katika eneo la ujumla ambako yeye na wana wake walifanya makazi baada ya Furiko. (Mwanzo 11:1) Kufikia wakati fulani, sehemu fulani ya hiyo idadi ya watu iliyokuwa imeongezeka ilihama kuelekea mashariki na ‘kuona bonde tambarare katika nchi ya Shinari.’—Mwanzo 11:2.
Kushindwa Kabisa
Ilikuwa katika bonde hilo ambako hicho kikundi kiliamua kuasi dhidi ya Mungu. Jinsi gani? Yehova Mungu alikuwa ameonyesha kusudi lake alipowaamuru wenzi wa kwanza wa kibinadamu ‘wazae, waongezeke, waijaze nchi, na kuitiisha.’ (Mwanzo 1:28) Amri hiyo ilirudiwa kwa Noa na wana wake baada ya Furiko. Mungu aliwaagiza hivi: “Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni sana katika nchi, mkaongezeke ndani yake.” (Mwanzo 9:7) Wakipinga mwelekezo wa Yehova, hao watu walijenga jiji ili ‘wasitawanyike usoni pa nchi yote.’
Watu hao pia walianza kujenga mnara kwa kusudi la ‘kujifanyia jina maarufu.’ Lakini kinyume cha matarajio yao, hawakumaliza ujenzi wa huo mnara. Rekodi ya Biblia yaonyesha kwamba Yehova alitatanisha lugha yao ili wasiweze kuelewana. “Basi,” lasema simulizi lililopuliziwa, “BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji.”—Mwanzo 11:7, 8.
Kushindwa kabisa kwa jaribio hilo kwatiliwa mkazo na uhakika wa kwamba majina ya hao wajenzi hayakupata kamwe kuwa “maarufu,” au kujulikana sana. Kwa kweli, majina yao hayajulikani na yamefutwa kutoka katika historia ya kibinadamu. Lakini vipi Nimrodi, kitukuu wa Noa? Je, hakuwa kiongozi wa uasi huo dhidi ya Mungu? Je, jina lake halijulikani sana?
Nimrodi—Mwasi Mfidhuli
Bila shaka, Nimrodi alikuwa ndiye kiongozi wa uasi huo. Mwanzo sura ya 10 humtambulisha kuwa “hodari kuwinda wanyama mbele ya BWANA [“kwa kumpinga Yehova,” NW].” (Mwanzo 10:9) Maandiko pia yasema kwamba ‘alianza kuwa mtu hodari katika nchi.’ (Mwanzo 10:8) Nimrodi alikuwa mwanavita, mtu wa ujeuri. Alipata kuwa mtawala wa kwanza wa kibinadamu baada ya Furiko, akijiweka rasmi kuwa mfalme. Nimrodi pia alikuwa mjenzi. Biblia humtambulisha kuwa mwanzilishi wa majiji manane, kutia na Babeli.—Mwanzo 10:10-12.
Kwa sababu hiyo, bila shaka Nimrodi—mpingaji wa Mungu, mfalme wa Babeli, mjenzi wa majiji—alishiriki katika kujenga mnara wa Babeli. Je, hakujifanyia jina maarufu? Kuhusu jina Nimrodi, Mtaalamu wa Mambo ya Nchi za Mashariki, E. F. C. Rosenmüller, aliandika hivi: “Nimrodi alipewa hilo jina kutokana na neno [ma·radhʹ], ambalo kulingana na Kiebrania lamaanisha ‘aliasi,’ ‘alisaliti.’” Kisha Rosenmüller aeleza kwamba “watu wa Mashariki mara nyingi wana desturi ya kuwaita watu mashuhuri kwa majina wapewayo baada ya kifo, ambayo kutoka kwayo upatano wenye kushangaza kati ya majina na mambo yaliyofanywa hutokea mara kwa mara.”
Wasomi kadhaa wana maoni yaliyo sawa kwamba jina Nimrodi halikuwa jina alilopewa wakati wa kuzaliwa. Badala ya hivyo, wao huliona kuwa jina ambalo alipewa baadaye ili lifaane na sifa yake ya kuasi baada ya hiyo sifa kuwa dhahiri. Kwa kielelezo, C. F. Keil ataarifu hivi: “Jina lenyewe, Nimrodi, ambalo latokana na neno [ma·radhʹ], ‘tutaasi,’ laonyesha ukinzani fulani wenye jeuri dhidi ya Mungu. Ni lenye kubainisha sana hivi kwamba laweza kuwa tu alipewa na watu walioishi wakati mmoja naye, na hivyo limekuwa jina la kibinafsi.” Katika kielezi-chini, Keil amnukuu mwanahistoria Jacob Perizonius, kuwa aliandika hivi: “Ningeamini kwamba mtu huyo [Nimrodi], akiwa mwindaji mkali na akiwa amezingirwa na kikosi cha washiriki wa karibu, ili kuchochea wale wengine kuasi, sikuzote alisema na kurudia neno hilo, ‘nimrodi, nimrodi,’ yaani, ‘Na tuasi! Na tuasi!’ Kwa sababu hiyo, nyakati za baadaye, aliitwa na wengine, hata Musa mwenyewe, kwa neno hilo likiwa jina la kibinafsi.”
Kwa wazi, Nimrodi hakujifanyia jina maarufu. Yaonekana jina alilopewa wakati wa kuzaliwa halijulikani. Limefutwa kutoka katika historia, sawa na majina ya wale waliofuata uongozi wake. Hata hakuacha uzao wowote kuendeleza jina lake. Badala ya kupokea utukufu na umaarufu, amevikwa fedheha. Jina Nimrodi limemtambulisha kwa umilele kuwa mwasi mwenye ufidhuli aliyempinga Yehova Mungu kwa upumbavu.