“Lazima Tumtii Mungu Kuwa Mtawala Kuliko Wanadamu”
“Vita Ni vya Yehova”
MAJESHI ya pande mbili zinazozozana yakabiliana uso kwa uso katika bonde. Kwa siku 40 wanaume wa Israeli wajikunyata kwa woga huku wakitukanwa na Goliathi, shujaa wa Wafilisti.—1 Samweli 17:1-4, 16.
Kwa sauti, Goliathi anawadhihaki Waisraeli hivi: “Jichagulieni mwanamume, naye ashuke, anijie. Akiweza kupigana nami na kunipiga, ndipo sisi tutakapokuwa watumishi wenu. Lakini nikimweza na kumpiga, ndipo ninyi pia mtakapokuwa watumishi wetu, nanyi mtatutumikia. . . . Mimi ninavitukana vikosi vya Israeli leo. Nipeni mwanamume, tupigane naye!”—1 Samweli 17:8-10.
Nyakati za kale, ilikuwa kawaida kwa mashujaa wa pande mbili kuwakilisha majeshi yao kwa kupigana wao kwa wao. Aliyeshinda, alilipatia jeshi lake ushindi. Lakini mpinzani huyu wa Israeli si askari-jeshi wa kawaida. Ni jitu refu, adui mwenye kuogofya na kutisha. Hata hivyo, Goliathi ataona cha mtema kuni kwa kulidhihaki jeshi la watu wa Yehova.
Hivi si vita vya kijeshi tu. Ni vita kati ya Yehova na miungu ya Wafilisti. Badala ya kuliongoza jeshi lake dhidi ya adui za Mungu, Sauli, Mfalme wa Israeli ameingiwa na hofu.—1 Samweli 17:11.
Kijana Amtumaini Yehova
Kabla ya vita kuanza, kijana ambaye tayari ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli atakayefuata, anawatembelea ndugu zake walio katika jeshi la Sauli. Kijana huyo ni Daudi. Anaposikia maneno ya Goliathi, anauliza hivi: “Kwani huyu Mfilisti asiyetahiriwa ni nani hata avitukane vikosi vya Mungu aliye hai?” (1 Samweli 17:26) Kwa maoni ya Daudi, Goliathi anawawakilisha Wafilisti pamoja na miungu yao. Akiwa na haki ya kukasirika, Daudi atamani kumwakilisha Yehova na Waisraeli na kupigana na jitu hilo la kipagani. Hata hivyo, Mfalme Sauli asema hivi: “Wewe huwezi kwenda juu ya huyu Mfilisti kupigana naye, kwa maana wewe ni mvulana tu.”—1 Samweli 17:33.
Jinsi maoni ya Sauli na Daudi yanavyotofautiana! Sauli amwona kuwa mvulana mchungaji anayetaka kupigana na jitu sugu. Lakini Daudi amwona Goliathi kuwa mtu tu anayemkaidi Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova. Ujasiri wa Daudi watokana na usadikisho wake kwamba Mungu hatatazama tu huku jina Lake na watu Wake wakiendelea kudhihakiwa. Huku Goliathi akijivunia nguvu zake, Daudi anamtegemea Yehova na kupima mambo kupatana na maoni ya Yehova.
“Naja Kwako Nikiwa na Jina la Yehova”
Imani ya Daudi ina msingi imara. Anakumbuka kwamba Mungu alimsaidia kuokoa kondoo zake kutokana na dubu na simba. Kijana huyo mchungaji ana hakika kwamba Yehova atamsaidia kupigana na adui huyo Mfilisti mwenye kutisha. (1 Samweli 17:34-37) Akiwa na kombeo na mawe matano yaliyo laini, Daudi anaenda kupigana na Goliathi.
Kijana huyo Daudi akubali mgawo huo unaoonekana kuwa mgumu sana akitegemea kupata nguvu kutoka kwa Yehova. Kwa ujasiri Daudi amwambia yule Mfilisti: “Unakuja kwangu ukiwa na upanga na mkuki na fumo, lakini mimi naja kwako nikiwa na jina la Yehova wa majeshi, Mungu wa vikosi vya Israeli, ambaye umemtukana. Leo Yehova atakutia mkononi mwangu . . . Watu wa dunia yote watajua kwamba kuna Mungu aliye wa Israeli. Na kutaniko hili lote watajua kwamba Yehova haokoi kwa upanga wala kwa mkuki, kwa sababu vita ni vya Yehova.”—1 Samweli 17:45-47.
Matokeo? Masimulizi yaliyoongozwa kwa roho yanasema: “Daudi, akiwa na kombeo na jiwe, akawa mwenye nguvu zaidi kuliko yule Mfilisti, akampiga Mfilisti na kumuua; na hakuna upanga uliokuwa mkononi mwa Daudi.” (1 Samweli 17:50) Daudi hakuwa na upanga wowote mkononi, lakini alipata utegemezo wenye nguvu wa Yehova Mungu.a
Pigano hilo lilidhihirisha wazi kwamba Daudi hakuwa amekosea hata kidogo kuwa na imani katika Yehova! Tunapohitaji kuamua iwapo tutawaogopa wanadamu au tutamtegemea Yehova atuokoe kwa nguvu zake, ni wazi kwamba “lazima tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.” (Matendo 5:29) Isitoshe, tunapoziona hali ngumu tukiwa na maoni ya Yehova Mungu, tunaweza kuwa na usawaziko kuhusu matatizo yanayoonekana kuwa yenye kulemea.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Kalenda ya Mashahidi wa Yehova ya 2006, Mei/Juni.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
GOLIATHI ALIKUWA MKUBWA KADIRI GANI?
Masimulizi ya 1 Samweli 17:4-7 yanasema kwamba urefu wa Goliathi ulizidi mikono sita, yaani zaidi ya meta tatu. Kinachoweza kutusaidia kuelewa ukubwa na nguvu za Mfilisti huyo ni lile vazi lake la shaba. Lilikuwa na uzito wa kilo 57! Mpini wa mkuki wake ulikuwa kama boriti la mbao, nacho kichwa cha mkuki wake kilikuwa na uzito wa kilo 7. Haikosi kwamba silaha za Goliathi zilikuwa nzito kuliko Daudi mwenyewe!