Je, Mali Zaweza Kukufanya Uwe Mwenye Furaha?
Mfalme Solomoni alijua thamani ya fedha. Yeye aliandika hivi: “Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, na divai huyafurahisha maisha; na fedha huleta jawabu la mambo yote.” (Mhubiri 10:19) Kula mlo pamoja na marafiki kwaweza kufurahisha zaidi, lakini kupata mkate au divai, wahitaji fedha. Kwa kuwa fedha ni njia ya kupata vitu vya kimwili, hizo “huleta jawabu la mambo yote.”
INGAWA Solomoni alikuwa mwenye mali nyingi mno, alijua kwamba utajiri una mipaka yake. Alitambua kwamba njia ya kufuatia vitu vya kimwili haiongozi kwenye furaha. Aliandika hivi: “Apendaye fedha hatashiba fedha, wala apendaye wingi hatashiba nyongeza.”—Mhubiri 5:10.
Tuseme kwamba, mtu mwenye mali anapata hata mali nyingi zaidi. Solomoni asema: “Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka.” (Mhubiri 5:11) “Mali” ya mtu, inapoongezeka, watu wengi wanahitajiwa kuitunza. Warekebishaji, watunzaji, watumishi, walinzi, na wengine—wote lazima walipwe kwa huduma zao. Kisha, kufanya hivyo kwahitaji fedha zaidi.
Hali kama hiyo huathiri moja kwa moja furaha ya mtu. Mwanahistoria Mgiriki Xenophon, aliyeishi katika karne ya nne K.W.K, aliandika maelezo ya mtu mmoja maskini aliyepata kuwa tajiri:
“Kumbe, kwa kweli wadhani . . . kwamba kadiri ninavyokuwa na vitu vingi zaidi, ndivyo ninavyoishi kwa furaha zaidi? Wewe hujui,” akaendelea, “hainiletei hata chembe moja ya raha zaidi, kula na kunywa na kulala sasa kuliko ilivyokuwa nilipokuwa maskini. Faida yangu tu ya kuwa na vitu vingi ni kwamba inanibidi kushughulikia mengi, kugawia wengine vingi, na kutaabika kutunza vingi zaidi ya vile nilivyokuwa navyo. Kwa sasa, watumishi wa nyumbani walio wengi wananitegemea kupata chakula, wengi kwa ajili ya kinywaji, na wengi kwa ajili ya mavazi, huku wengine wakihitaji madaktari; na mwingine hunijia na kisa cha kondoo kushambuliwa na mbwa-mwitu, au ng’ombe-dume kuangukia poromoko, au akisema kwamba maradhi fulani yameenea miongoni mwa ng’ombe. Na hivyo yaonekana kwangu . . . kana kwamba nimepata taabu nyingi zaidi sasa kwa sababu ya kuwa na vitu vingi kuliko vile nilivyopata nilipokuwa na vitu vichache.”
Sababu nyingine ambayo hufanya watu wafuatie mali nyingi hata zaidi ni kwamba, wanadanganywa kwa werevu na kile ambacho Yesu Kristo alikiita “nguvu za udanganyifu wa mali.” (Mathayo 13:22) Wanadanganywa kwa sababu katika utajiri huu wanaotafuta kwa umotomoto, hawapati kamwe uradhi au furaha waliyotazamia kupata. Wao husababu kwamba kile ambacho mali ndogo yashindwa kufanya, mali nyingi itafanya. Kwa hiyo wao hufanya jitihada ya daima ili wapate mali nyingi zaidi.
Kupenda Fedha Hakuongozi Kwenye Furaha
Kuhangaikia mali kwaweza kumzuia tajiri kufurahia usingizi wenye amani. Solomoni aandika: “Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi.”—Mhubiri 5:12.
Wasiwasi juu ya uwezekano wa mtu kupoteza mali yake unapofikiriwa kupita kiasi, mengi yahusika zaidi ya kukosa usingizi tu. Akimfafanua bahili (mwenye uchoyo), Solomoni aliandika hivi: “Siku zake zote hula gizani, mwenye fadhaa nyingi, mwenye ugonjwa na uchungu.” (Mhubiri 5:17) Badala ya kupata furaha katika mali yake, yeye hula ‘kwa fadhaa,’ kana kwamba aonea wivu hata fedha anazotumia kununua chakula. Mtazamo huo wa kiakili uliovurugika waweza kuchangia kuwa na afya mbaya. Kisha, afya mbaya huongeza wasiwasi wa huyo bahili, kwa kuwa humzuia kurundika mali nyingi zaidi.
Labda hilo lakukumbusha yale aliyoandika mtume Paulo: “Wale waazimiao kuwa matajiri huanguka ndani ya kishawishi na mtego na tamaa nyingi zisizo za akili na zenye kuumiza, ambazo hutumbukiza watu ndani ya uharibifu na uangamizo. Kwa maana kupenda fedha ni mzizi wa mambo mabaya ya namna zote, na kwa kujitahidi kufikilia kupenda huku wengine . . . wamejichoma wenyewe kotekote kwa maumivu mengi.” (1 Timotheo 6:9, 10) Katika kufuatia fedha, watu hupunja, husema uwongo, huiba, hujifanya kuwa malaya, na hata huua kimakusudi. Matokeo huwa ni mtu aliyechomwa kihisia-moyo, kimwili, na maumivu ya kiroho kwa sababu ya kujaribu kukamata na kushikilia utajiri. Je, hiyo yaonekana kuwa njia ya kupata furaha? Hata kidogo!
Kuridhika na Kile Tulicho Nacho
Solomoni alikuwa na mengi ya kusema juu ya maoni yaliyosawazika kuhusu mali. Aliandika hivi: “Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tupu-tupu kama alivyokuja; asichume kitu cho chote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake. Tazama, mimi niliyoyaona kuwa ndiyo mema na ya kufaa, ni mtu kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote anayoifanya chini ya jua, siku zote za maisha yake alizopewa na Mungu; maana hilo ndilo fungu lake.”—Mhubiri 5:15, 18.
Maneno hayo yanaonyesha kwamba furaha haitegemei kujitahidi kurundika mali kwa ajili ya wakati tusiojua kama tutaishi. Ni afadhali zaidi kutosheka na kufurahia matokeo ya kazi yetu ngumu. Mtume Paulo alieleza wazo kama hilo katika barua yake yenye kupuliziwa ambayo alimwandikia Timotheo, akisema: “Hatukuleta kitu katika ulimwengu, wala hatuwezi kupeleka kitu chochote nje. Kwa hiyo, tukiwa na riziki na cha kujifunika, tutakuwa wenye kuridhika na vitu hivi.”—1 Timotheo 6:7, 8; linganisha Luka 12:16-21.
Ufunguo wa Kupata Furaha
Solomoni alikuwa na wingi wa mali na hekima ya kimungu. Lakini alihusianisha furaha yake na hekima, si na fedha. Yeye alisema: “Heri mtu yule aonaye hekima, na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, wala vyote uvitamanivyo havilingani naye. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. Njia zake ni njia za kupendeza sana, na mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; ana heri kila mtu ashikamanaye naye.”—Mithali 3:13-18.
Kwa nini hekima ni kuu kupita mali za kimwili? Solomoni aliandika hivi: “Hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.” (Mhubiri 7:12) Ingawa fedha zaweza kuandaa ulinzi wa kadiri fulani, zikimwezesha mwenye kuzimiliki kununua anachohitaji, hekima yaweza kumkinga mtu kutoka katika mambo yawezayo kuhatarisha uhai wake. Hekima ya kweli humwokoa mtu kutoka katika kifo kisichotazamiwa, na kwa kuwa inategemea hofu ifaayo kwa Mungu, pia itaongoza kwenye uhai udumuo milele.
Kwa nini hekima ya kimungu huongoza kwenye furaha? Kwa sababu furaha ya kweli yaweza kutokana na Yehova Mungu pekee. Mambo yaliyoonwa yaonyesha kwamba furaha ya kweli yaweza kupatikana tu kupitia kumtii Aliye Juu Zaidi. Furaha yenye kudumu yategemea msimamo uliokubaliwa na Mungu. (Mathayo 5:3-10) Kwa kutumia yale tujifunzayo kutokana na funzo la Biblia, tutasitawisha “hekima ya kutoka juu.” (Yakobo 3:17) Itatupatia furaha ambayo mali haiwezi kuleta kamwe.
[Picha katika ukurasa wa 4, 5]
Mfalme Solomoni alijua kimfanyacho mtu awe mwenye furaha. Je, wewe wakijua?