“Meli za Kitimu” Zatawala Baharini
MAPIGANO mengi ya baharini yamepiganwa katika eneo la Mediterania mashariki. Jaribu kuwazia pambano lililotukia karne tano kabla ya Kristo. Meli ya kivita yenye safu tatu za makasia na inayoweza kuelekezwa kwa urahisi, inasafiri kwa mwendo wa kasi zaidi. Wanaume 170 hivi katika safu tatu za makasia wanakaza kabisa misuli yao yenye nguvu wanapopiga makasia, huku wakisogea mbele na nyuma kwenye matandiko ya ngozi yaliyofungiliwa kwenye makalio yao.
Meli hiyo inayosafiri kwa mwendo wa kilomita 13 hadi 17 kwa saa inapita kasi kwenye mawimbi kuelekea meli ya adui. Meli ya adui inajaribu kuepa. Wakati huo hatari, meli hiyo inayumbayumba, nao ubavu wake unaelekeana na meli inayoshambulia. Mdomo wa shaba nyeusi wa meli hiyo ya vita unatoboa ubavu mwembamba wa meli ya adui. Wapiga-makasia wa meli hiyo ya adui wanaogopeshwa na kishindo cha kuvunjika kwa mbao za meli yao na maji ya bahari yanayoingia melini kupitia shimo kubwa lililotobolewa. Kikosi kidogo cha mashujaa wenye silaha nyingi katika meli hiyo ya vita kinapita haraka kwenye ubao wa katikati wa kuingilia melini ili kuwashambulia adui. Ndiyo, meli fulani za kale zilikuwa zenye kutisha kwelikweli!
Wanafunzi wa Biblia wamevutiwa na mitajo kuhusu “Kitimu” na “meli za Kitimu.” Baadhi ya mitajo hiyo ni ya kinabii. (Hesabu 24:24; Danieli 11:30; Isaya 23:1) Kitimu ilikuwa wapi? Tunajua nini kuhusu meli za Kitimu? Na kwa nini upendezwe na majibu ya maswali hayo?
Josephus, mwanahistoria Myahudi, aliita nchi ya Kitimu “Chethimos,” akiihusianisha na kisiwa cha Saiprasi. Jiji la Kition (au, Citium) lililoko kusini-mashariki mwa kisiwa hicho linahusianisha zaidi Kitimu na Saiprasi. Kisiwa cha Saiprasi ambacho kilikuwa katika makutano ya njia za zamani za biashara, kilikuwa mahali panapofaa sana na hivyo kingenufaika kwa sababu ya kuwa karibu na bandari za mashariki ya Mediterania. Kwa sababu ya mahali kilipokuwa na pia kwa sababu za kisiasa, kisiwa hicho kililazimika kuunga mkono mojawapo ya mataifa yaliyokuwa yakipigana na hivyo kikawa ama mshirika mwenye nguvu au kizuizi chenye kusumbua.
Wakaaji wa Saiprasi na Bahari
Ushuhuda wa vitu vya kale vilivyochimbuliwa baharini na makaburini, na pia maandishi ya kale na michoro kwenye vyombo vya udongo unatusaidia kuwazia jinsi meli za Saiprasi zilivyokuwa. Wakaaji wa kale wa Saiprasi walikuwa watengenezaji stadi wa meli. Kisiwa chao kilikuwa na misitu mikubwa, na ghuba zake zenye kingo zilikuwa bandari za kiasili. Miti haikukatwa tu ili kutengeneza meli bali pia kuyeyusha shaba nyekundu, ambayo ilikuwa mali ya asili iliyofanya Saiprasi iwe mashuhuri katika ulimwengu huo wa kale.
Biashara kubwa ya Saiprasi iliwavutia Wafoinike, ambao walianzisha koloni katika maeneo mbalimbali waliyopitia walipokuwa wakifanya biashara. Jiji la Kition huko Saiprasi lilikuwa moja ya makoloni hayo.—Isaya 23:10-12.
Baada ya Tiro kuanguka, ni wazi kwamba baadhi ya wakaaji wake walikimbilia Kitimu. Inaelekea kwamba wakoloni Wafoinike waliokuwa na uzoefu wa kusafiri baharini walichangia sana teknolojia ya jeshi la baharini la Wasaiprasi. Kition lilikuwa mahali pazuri sana na hivyo liliandaa ulinzi kwa meli za Wafoinike.
Chahusika Katika Biashara Kubwa ya Kimataifa
Shughuli za kale za kibiashara za mashariki ya Mediterania katika kipindi hicho zilikuwa nyingi. Bidhaa za thamani kutoka Saiprasi zilisafirishwa kwa meli hadi Krete, Sardinia, na Sisili na pia katika visiwa vya Aegea. Magudulia na vyombo vya maua kutoka Saiprasi vimepatikana katika maeneo hayo, na vyombo bora vya udongo kutoka Ugiriki vimepatikana kwa wingi huko Saiprasi. Wasomi fulani ambao wamechunguza vipande vya shaba nyekundu vilivyopatikana huko Sardinia, wanaamini kwamba vilitoka Saiprasi.
Mnamo 1982 meli iliyovunjika mwishoni mwa karne ya 14 K.W.K. ilipatikana karibu na pwani ya kusini ya Uturuki. Vitu vingi vyenye thamani vilipatikana chini ya maji. Vitu hivyo vinatia ndani vipande vya shaba nyekundu vinavyoaminika kuwa vilitoka Saiprasi, kaharabu, magudulia ya Wakanaani, mbao za mpingo, pembe za tembo, vito vingi vya Wakanaani vya dhahabu na fedha, na mapambo fulani mfano wa mbawakavu ambaye Wamisri walimwona kuwa mtakatifu, na pia vitu vingine kutoka Misri. Baada ya kuchunguza udongo uliopatikana katika meli hiyo, wachunguzi fulani wamesema kwamba inaelekea meli hiyo ilitoka Saiprasi.
Inapendeza kwamba meli hiyo inakadiriwa kuwa ilivunjika katika kipindi ambacho Balaamu alizungumzia meli za Kitimu kwenye “neno lake la kimethali.” (Hesabu 24:15, 24) Kwa wazi, meli za Saiprasi zilikuwa maarufu sana katika Mashariki ya Kati. Meli hizo zilitengenezwa namna gani?
Meli za Biashara
Maumbo mengi ya udongo ya meli na mashua yamepatikana katika maeneo ya makaburi ya jiji la kale la Amathus huko Saiprasi. Maumbo hayo yanasaidia sana kufahamu aina mbalimbali za meli za Wasaiprasi. Baadhi ya maumbo hayo ya meli yamewekwa katika majumba ya ukumbusho.
Maumbo hayo ya udongo yanaonyesha kwamba kwa wazi meli za mapema zilitumiwa kwa shughuli zenye amani za biashara. Meli ndogo ziliendeshwa na wanaume 20 ambao walipiga makasia. Meli kubwa zilitengenezwa ili kusafirisha bidhaa na abiria ambao walitaka kwenda kwenye maeneo ya karibu kandokando ya pwani ya Saiprasi. Plini Mkubwa anasema kwamba Wasaiprasi waliunda meli nyepesi ambayo iliendeshwa kwa makasia ambayo ingeweza kubeba uzito wa tani 90.
Halafu kulikuwa na meli kubwa za biashara kama ile iliyopatikana karibu na pwani ya Uturuki. Baadhi ya meli hizo zingeweza kubeba mizigo yenye uzito wa tani 450. Idadi ya waliopiga makasia katika meli kubwa ingefikia wanaume 50, wanaume 25 wakiwa kila upande, na meli hiyo ingekuwa na urefu wa mita 30 na mlingoti wenye urefu wa mita 10.
Meli za Kivita za “Kitimu” Katika Unabii wa Biblia
Roho ya Yehova ndiyo iliyoongoza maneno haya: “Kutakuwako meli kutoka pwani ya Kitimu, nazo hakika zitatesa Ashuru.” (Hesabu 24:2, 24) Je, utabiri huo ulitimia? Meli kutoka Saiprasi zilihusika kwa njia gani katika utimizo huo? ‘Meli hizo kutoka pwani ya Kitimu’ hazikuwa za kufanya biashara ya amani katika Bahari ya Mediterania. Zilikuwa meli za vita zilizowaletea watu taabu.
Kadiri mahitaji ya kivita yalivyobadilika, ndivyo miundo ya msingi ya meli ilivyobadilishwa ili kutokeza meli ambazo zingeendeshwa haraka zaidi na zenye nguvu zaidi. Huenda meli za kivita za mapema zaidi za Saiprasi zilikuwa katika mchoro uliopatikana huko Amathus. Meli hiyo ni nyembamba na ndefu nayo ina tezi iliyoinuka na kujipinda kuelekea ndani ya meli, kama meli ya vita ya Foinike. Ina mdomo wa kutoboa meli ya adui na ngao za mviringo pande zote mbili za tezi na kuelekea omo ya meli hiyo.
Katika karne ya nane K.W.K., meli za kwanza zenye safu mbili za makasia zilianza kutengenezwa huko Ugiriki. Meli hizo zilikuwa na urefu wa mita 24 hivi na upana wa mita 3. Mwanzoni, meli hizo zilitumiwa tu kusafirisha askari-jeshi, lakini vita vilipiganwa kwenye nchi kavu. Muda si muda, faida ya kuongeza safu ya tatu ya makasia ilionekana, nao mdomo uliofunikwa na shaba nyeusi ukaunganishwa na omo ya meli. Meli hiyo mpya ndiyo meli yenye safu tatu za makasia kama ile inayotajwa mwanzoni mwa habari hii. Meli za aina hiyo zilipata umaarufu wakati wa vita vya Salamisi (480 K.W.K.) Wagiriki waliposhinda jeshi la maji la Uajemi.
Baadaye, katika harakati za kupanua milki yake, Aleksanda Mkuu alielekeza meli zake upande wa mashariki. Meli kama hizo zenye safu tatu za makasia zilibuniwa kwa ajili ya vita, wala si kwa ajili ya safari ndefu za baharini, kwa kuwa zilikuwa na nafasi ndogo ya kubebea chakula. Kwa sababu hiyo, ilikuwa lazima kutua katika visiwa vya Aegea ili kupata chakula na vifaa vya kurekebisha meli. Kusudi la Aleksanda lilikuwa kuharibu meli za Waajemi. Hata hivyo, ili afanikiwe, alipaswa kwanza kushinda ngome imara ya kisiwa cha Tiro. Saiprasi kilikuwa kituo tu njiani kuelekea Tiro.
Wasaiprasi walimuunga mkono Aleksanda Mkuu alipozingira Tiro (332 K.W.K.), kwa kumpa meli 120. Wafalme watatu wa Saiprasi waliziongoza meli hizo kwenda kujiunga na Aleksanda. Walishiriki kulizingira Tiro kwa muda wa miezi saba. Tiro lilianguka, na unabii wa Biblia ukatimia. (Ezekieli 26:3, 4; Zekaria 9:3, 4) Aleksanda aliwashukuru wafalme wa Saiprasi kwa kuwapa mamlaka ya pekee.
Utimizo Wenye Kustaajabisha
Strabo, mwanahistoria wa karne ya kwanza, anasema kwamba Aleksanda aliomba meli kutoka Saiprasi na Foinike ili azitumie katika harakati zake za kuingia Arabia. Meli hizo zilikuwa nyepesi na zingeweza kubomolewa kwa urahisi, hivyo ilichukua siku saba tu kuzifikisha Thapsacus (Tiphsah), kaskazini mwa Siria. (1 Wafalme 4:24) Kutoka hapo ilikuwa rahisi kushuka kwenda Babiloni zikifuata mto.
Hivyo, taarifa isiyo wazi sana ya Biblia ilipata utimizo wenye kustaajabisha karne kumi hivi baadaye! Kupatana na maneno ya Hesabu 24:24, jeshi la Aleksanda Mkuu lilizidi kusonga mbele kutoka Makedonia kuelekea mashariki na kuishinda nchi ya Ashuru, na mwishowe likaishinda Milki yenye nguvu ya Umedi na Uajemi.
Bila shaka, hata habari chache tulizo nazo kuhusu “meli za Kitimu” zinaonyesha utimizo wenye kustaajabisha wa unabii wa Biblia. Ushuhuda kama huo wa kihistoria unaimarisha usadikisho wetu kwamba utabiri ulio katika Biblia unategemeka. Unabii mwingi kama huo unahusu wakati wetu ujao, na hivyo tunapaswa kuuchukua kwa uzito.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
ITALIA
Sardinia
Sisili
Bahari ya Aegea
UGIRIKI
Krete
LIBYA
UTURUKI
SAIPRASI
Kition
Tiro
MISRI
[Picha katika ukurasa wa 16]
Umbo la meli ya kivita ya Ugiriki iliyo na safu tatu za makasia
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Umbo la meli ya kale ya kivita ya Foinike iliyo na safu mbili za makasia
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Meli ya Saiprasi kwenye chombo cha maua
[Hisani]
Published by permission of the Director of Antiquities and the Cyprus Museum
[Picha katika ukurasa wa 18]
Meli za kale za mizigo, kama zile zinazotajwa katika Isaya 60:9