Sura ya 12
Msiogope Ashuru
1, 2. (a) Kwa maoni ya binadamu, kwa nini yaonekana kwamba Yona alikuwa na sababu nzuri ya kusita kuukubali utume wake wa kuwahubiria Waashuri? (b) Waninawi waliitikiaje ujumbe wa Yona?
KATIKATI ya karne ya tisa K.W.K., Yona nabii Mwebrania, mwana wa Amitai, alienda kwa ujasiri huko Ninewi, jiji kuu la Milki ya Ashuru. Alikuwa na ujumbe muhimu sana. Yehova alikuwa amemwambia: “Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.”—Yona 1:2, 3.
2 Mwanzoni alipopokea utume wake, Yona alikimbilia upande mwingine, huko Tarshishi. Kwa maoni ya binadamu, Yona alikuwa na sababu nzuri ya kusita. Waashuri walikuwa watu wakatili. Ona mtawala mmoja Mwashuri alivyowatenda adui zake: “Nilikata miguu na mikono ya maofisa . . . Nikachoma kwa moto mateka wengi miongoni mwao, nami nikachukua mateka wengi walio hai. Nilikata mikono na vidole vya baadhi yao, na kukata pua za wengine wao.” Licha ya hayo, hatimaye Yona alipokabidhi ujumbe wa Yehova, Waninawi walitubu dhambi zao na Yehova akahurumia jiji hilo wakati huo.—Yona 3:3-10; Mathayo 12:41.
Yehova Atwaa “Fimbo”
3. Itikio la Waisraeli kwa maonyo yaliyotolewa na manabii wa Yehova latofautianaje na lile la Waninawi?
3 Je, Waisraeli, ambao Yona aliwahubiria pia, waitikia? (2 Wafalme 14:25) La. Wao waipa kisogo ibada safi. Naam, wao hata ‘waliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali.’ Isitoshe, “wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha.” (2 Wafalme 17:16, 17) Tofauti na Waninawi, Israeli hawaitikii Yehova atumapo manabii kuwaonya. Basi Yehova aazimia kuchukua hatua kali zaidi.
4, 5. (a) Usemi “Ashuru” wamaanisha nini, na Yehova atamtumiaje kama “fimbo”? (b) Samaria laanguka lini?
4 Uchokozi wa Ashuru wapungua kwa muda fulani baada ya ziara ya Yona huko Ninawi.a Hata hivyo, mwanzoni mwa karne ya nane K.W.K., Ashuru yadhihirisha tena uwezo wake mkubwa wa kijeshi, na Yehova aitumia kwa njia yenye kutisha. Nabii Isaya atoa onyo la Yehova kwa ufalme wa kaskazini wa Israeli: “Ole wake Ashuru! fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani.”—Isaya 10:5, 6.
5 Waisraeli waaibishwa kama nini! Mungu atumia taifa la kipagani—“Ashuru”—kama “fimbo” ya kuwaadhibu. Mwaka wa 742 K.W.K., Mfalme Shalmanesa wa Tano wa Ashuru azingira Samaria, jiji kuu la taifa la Israeli lenye kuasi. Samaria, lililo mahali muhimu kwenye kilima cha urefu wa meta 90, lafaulu kujikinga dhidi ya adui kwa karibu miaka mitatu. Lakini hakuna mpango wowote wa kibinadamu uwezao kuzuia kusudi la Mungu. Samaria laanguka mwaka wa 740 K.W.K., na kukanyagwa-kanyagwa chini ya miguu ya Ashuru.—2 Wafalme 18:10.
6. Ashuru apitaje kusudi la Yehova kumhusu?
6 Ijapokuwa Yehova aliwatumia kuwaadhibu watu wake, Waashuri wenyewe hawamtambui Yehova. Hiyo ndiyo sababu aendelea kusema: “Lakini hivyo sivyo [Ashuru] akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache.” (Isaya 10:7) Yehova ataka Ashuru awe chombo mkononi mwake. Lakini Ashuru ataka kuwa tofauti. Moyo wake wamhimiza afanye mpango wa kupata kitu kikubwa zaidi—ushindi dhidi ya ulimwengu uliojulikana wakati huo!
7. (a) Eleza usemi “Je! wakuu wangu si wote wafalme?” (b) Wale wanaomwacha Yehova leo wapasa kuzingatia nini?
7 Hapo awali, majiji mengi ya wasio Waisraeli yaliyoshindwa na Ashuru, yalitawaliwa na wafalme. Sasa wafalme hao wa awali wapaswa kuwa chini ya mfalme wa Ashuru wakiwa wakuu vibaraka, hivyo ikimfanya ajisifu kwa kusema: “Je! wakuu wangu si wote wafalme?” (Isaya 10:8) Miungu isiyo ya kweli ya majiji muhimu ya mataifa haingeweza kuokoa waabudu wao wasiharibiwe. Miungu wanayoabudu wakazi wa Samaria, kama vile Baali, Moleki, na ndama wa dhahabu, haitalinda jiji hilo. Kwa kuwa Samaria limemwacha Yehova, halina haki ya kumtarajia aingilie kati. Wote wanaomwacha Yehova leo na wazingatie mwisho mbaya wa Samaria! Ashuru aweza kujisifu ipasavyo kuhusiana na Samaria na majiji mengine ambayo ameshinda: “Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski?” (Isaya 10:9) Kwa Ashuru, yote hayo ni sawasawa tu—nyara kwake.
8, 9. Kwa nini Ashuru apita kiasi apangapo kushambulia Yerusalemu?
8 Hata hivyo, Ashuru ajisifu kupita kiasi. Asema hivi: “Kama vile mkono wangu ulivyofikilia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria; je! sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?” (Isaya 10:10, 11) Falme ambazo tayari zimeshindwa na Ashuru zilikuwa na sanamu nyingi kuliko Yerusalemu au hata Samaria. ‘Ni nini,’ yeye asababu, ‘kiwezacho kunizuia kulitenda Yerusalemu kama nilivyolitenda Samaria?’
9 Mjisifu! Yehova hatamruhusu atwae Yerusalemu. Ni kweli kwamba, Yuda pia haikutegemeza kikamili ibada ya kweli. (2 Wafalme 16:7-9; 2 Mambo ya Nyakati 28:24) Yehova ameonya kuwa Yuda itateseka sana wakati wa uvamizi wa Ashuru kwa sababu ya ukosefu wake wa uaminifu. Lakini Yerusalemu litaokoka. (Isaya 1:7, 8) Hezekia ni mfalme katika Yerusalemu Ashuru ifanyapo uvamizi. Hezekia si kama babake, Ahazi. Kwani, katika mwezi wa kwanza kabisa wa utawala wake, Hezekia afungua tena milango ya hekalu na kurudisha ibada safi!—2 Mambo ya Nyakati 29:3-5.
10. Yehova aahidi nini kuhusu Ashuru?
10 Kwa hiyo Yehova hakubali shambulio ambalo Ashuru yakusudia dhidi ya Yerusalemu. Yehova aahidi kuitoza hesabu serikali hiyo ya ulimwengu yenye kujisifu: “Itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitayaadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake.”—Isaya 10:12.
Kuelekea Yuda na Yerusalemu!
11. Kwa nini Ashuru afikiri kwamba Yerusalemu litatekwa kwa urahisi?
11 Miaka minane baada ya kuanguka kwa ufalme wa kaskazini mwaka wa 740 K.W.K., mtawala mpya wa Ashuru, Senakeribu, apanda dhidi ya Yerusalemu. Isaya afafanua kishairi mpango wenye kiburi wa Senakeribu: “Nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia.” (Isaya 10:13, 14) Senakeribu awazia kuwa majiji mengine yameanguka na Samaria halipo tena, kwa hiyo Yerusalemu litatekwa kwa urahisi! Huenda jiji hilo likapigana shingo upande, lakini wakazi wake watashindwa upesi, bila kulia, na mali zao kutwaliwa kama mayai kutoka katika kiota kilichoachwa.
12. Yehova aonyeshaje maoni yanayofaa juu ya mambo kuhusiana na kujisifu kwa Ashuru?
12 Hata hivyo, Senakeribu asahau jambo fulani. Samaria lenye kuasi lilistahili kupata adhabu liliyopokea. Ingawa hivyo, chini ya Mfalme Hezekia, Yerusalemu limekuwa ngome ya ibada safi tena. Yehova atakabiliana na yeyote atakaye kuligusa Yerusalemu! Isaya auliza kwa hasira: “Je! shoka lijisifu juu yake alitumiaye? je! msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti.” (Isaya 10:15) Milki ya Ashuru ni chombo tu mkononi mwa Yehova, kama vile seremala, mpasua-mbao, au mchungaji wawezavyo kutumia shoka, msumeno, bakora, au fimbo. Basi fimbo yawezaje sasa kuthubutu kujitukuza kuliko yeye aitumiaye!
13. Tambulisha na utaje kinachotukia kwa (a) “walionona.” (b) ‘mbigili na miiba.’ (c) “utukufu wa msitu wake.”
13 Ni nini kitakachompata Ashuru? “Bwana, BWANA wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto. Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa mwali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake katika siku moja. Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa. Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu.” (Isaya 10:16-19) Naam, Yehova atachonga-chonga “fimbo” hiyo ya Ashuru! “Walionona” katika jeshi la Ashuru, wanajeshi wake hodari, wataambukizwa ugonjwa wa “kukonda.” Hawataonekana kuwa na nguvu hivyo! Kama vile mbigili na miiba mingi, vikosi vyake vya nchi kavu vitachomwa kwa Mwanga wa Israeli, Yehova Mungu. Na “utukufu wa msitu wake,” maofisa wake wa kijeshi, utaangamia. Baada ya Yehova kushughulikia Ashuru, ni maofisa wachache sana watakaobaki hivi kwamba mtoto mdogo atawahesabu kwa vidole vyake!—Ona pia Isaya 10:33, 34.
14. Fafanua jinsi Ashuru anavyosonga nchini Yuda kufikia mwaka wa 732 K.W.K.
14 Hata hivyo, lazima iwe Wayahudi wanaoishi Yerusalemu mwaka wa 732 K.W.K. waona vigumu kuamini kwamba Ashuru atashindwa. Jeshi kubwa mno la Ashuru lasonga mbele bila huruma. Sikiliza orodha ya majiji ya Yuda yaliyoanguka: “Amefika Ayathi . . . Migroni . . . Mikmashi . . . Geba . . . Rama . . . Gibea wa Sauli . . . Galimu . . . Laisha . . . Anathothi . . . Madmena . . . Gebimu . . . Nobu.” (Isaya 10:28-32a)b Hatimaye, wavamizi wafika Lakishi, kilometa 50 tu kutoka Yerusalemu. Punde si punde, jeshi kubwa la Ashuru latisha jiji hilo. “Anatikisa mkono wake juu ya mlima wa binti Sayuni, mlima wa Yerusalemu.” (Isaya 10:32b) Ni nini kiwezacho kumzuia Ashuru?
15, 16. (a) Kwa nini Mfalme Hezekia ahitaji imani thabiti? (b) Kuna msingi gani kwa Hezekia kuamini kwamba Yehova atamsaidia?
15 Mfalme Hezekia aanza kuhangaika katika jumba lake la kifalme jijini. Ararua nguo zake na kujivika nguo za gunia. (Isaya 37:1) Awatuma wanaume kwa nabii Isaya amwombe Yehova kwa niaba ya Yuda. Punde wao warudi na jibu la Yehova: ‘Usiogope . . . nitaulinda mji huu.’ (Isaya 37:6, 35) Hata hivyo, Waashuri wanatisha sana nao wana ushujaa mwingi.
16 Imani—ndiyo itakayomtegemeza Mfalme Hezekia katika mgogoro huo mkubwa. Imani ni “wonyesho dhahiri wa mambo halisi ingawa hayaonwi.” (Waebrania 11:1) Yahusisha kutazamia mambo zaidi ya yale yaonekanayo waziwazi. Ingawa imani yategemea ujuzi. Labda Hezekia akumbuka kuwa hapo mapema Yehova alinena mambo haya yenye kufariji: “Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru . . . Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza. Na BWANA wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kwa namna ya Kimisri.” (Isaya 10:24-26)c Naam, watu wa Mungu wamewahi kukabili hali ngumu awali. Mababu wa Hezekia walionekana duni sana mbele ya jeshi la Misri kwenye Bahari Nyekundu. Karne kadhaa awali, Gideoni alikabiliwa na jeshi kubwa mno Wamidiani na Waamaleki walipovamia Israeli. Ingawa hivyo Yehova aliwakomboa watu wake kwenye pindi hizo mbili.—Kutoka 14:7-9, 13, 28; Waamuzi 6:33; 7:21, 22.
17. Nira ya Ashuru ‘yaharibiwaje,’ na kwa nini?
17 Je, Yehova atafanya tena yale aliyofanya kwenye pindi mbili hizo? Ndiyo. Yehova aahidi: “Itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” (Isaya 10:27) Nira ya Ashuru itaondolewa begani na shingoni mwa watu wa agano wa Mungu. Naam, nira “itaharibiwa”—na kwa kweli yaharibiwa! Katika usiku mmoja, malaika wa Yehova aua Waashuri 185,000. Tisho hilo laondolewa, na Waashuri waondoka nchini Yuda milele. (2 Wafalme 19:35, 36) Kwa nini? “Kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Huenda hilo larejezea mafuta yaliyotumiwa kumtia mafuta Hezekia ili awe mfalme katika nasaba ya Daudi. Hivyo, Yehova atimiza ahadi yake: “Nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.”—2 Wafalme 19:34.
18. (a) Je, unabii wa Isaya una utimizo zaidi ya mmoja? Eleza. (b) Ni tengenezo gani leo linalofanana na Samaria la kale?
18 Masimulizi ya Isaya ambayo yamechunguzwa katika sura hii yahusu matukio katika Yuda miaka zaidi ya 2,700 iliyopita. Lakini matukio hayo yafaa sana leo. (Waroma 15:4) Je, yamaanisha kwamba wahusika wakuu katika masimulizi hayo yenye kusisimua—wakazi wa Samaria na Yerusalemu pamoja na Waashuri—wana watu wanaolingana nao siku hizi? Ndiyo. Sawa na Samaria lenye kuabudu sanamu, Jumuiya ya Wakristo yadai kumwabudu Yehova, lakini imeasi kupindukia. Katika kichapo An Essay on the Development of Christian Doctrine, Mkatoliki John Henry Cardinal Newman akiri kwamba vifaa ambavyo Jumuiya ya Wakristo imetumia kwa karne nyingi, kama vile uvumba, mishumaa, maji matakatifu, mavazi ya kikasisi, na mifano, “vyote vilikuwa na chanzo cha kipagani.” Ibada ya kipagani ya Jumuiya ya Wakristo yamchukiza Yehova kabisa kama vile ibada ya sanamu ya Samaria.
19. Jumuiya ya Wakristo imeonywa juu ya nini, na onyo hilo limetolewa na nani?
19 Mashahidi wa Yehova wameionya Jumuiya ya Wakristo kwa miaka mingi kuhusu kuudhika kwa Yehova. Kwa kielelezo, mwaka wa 1955, hotuba ya watu wote yenye kichwa “Jumuiya ya Wakristo au Ukristo—‘Nuru ya Ulimwengu’ Ni Gani?” ilitolewa ulimwenguni kote. Hotuba hiyo ilieleza kinaganaga jinsi ambavyo Jumuiya ya Wakristo imepotoka kutoka katika fundisho na mazoea ya kweli ya Ukristo. Kisha makasisi katika nchi nyingi wakatumiwa nakala za hotuba hiyo kali. Ikiwa tengenezo, Jumuiya ya Wakristo imeshindwa kutii onyo hilo. Yehova hana jingine ila kuitia nidhamu kwa “fimbo.”
20. (a) Ni nini kitakachokuwa Ashuru wa kisasa, nacho kitatumiwaje kama fimbo? (b) Jumuiya ya Wakristo itaadhibiwa kwa kadiri gani?
20 Yehova atatumia nani kuitia nidhamu Jumuiya ya Wakristo yenye kuasi? Twajibiwa katika sura ya 17 ya Ufunuo. Humo twajulishwa kuhusu kahaba, “Babiloni Mkubwa,” anayewakilisha dini zisizo za kweli ulimwenguni kote, kutia ndani Jumuiya ya Wakristo. Kahaba huyo amempanda hayawani-mwitu mwenye rangi-nyekundu-nyangavu aliye na vichwa saba na pembe kumi. (Ufunuo 17:3, 5, 7-12) Hayawani-mwitu huyo awakilisha shirika la Umoja wa Mataifa.d Kama vile Ashuru wa kale alivyoharibu Samaria, ndivyo hayawani-mwitu mwenye rangi-nyekundu-nyangavu ‘atakavyomchukia kahaba na kumfanya ukiwa na kuwa uchi, na kula kabisa sehemu zake zenye nyama na kumchoma kabisa kwa moto.’ (Ufunuo 17:16) Hivyo Ashuru wa kisasa (mataifa yanayoshirikiana na UM) atapiga dafrao na kutwanga kabisa Jumuiya ya Wakristo hata isiwepo tena kamwe.
21, 22. Ni nani atakayemchochea hayawani-mwitu awashambulie watu wa Mungu?
21 Je, Mashahidi waaminifu wa Yehova wataangamia pamoja na Babiloni Mkubwa? La. Mungu hachukizwi nao. Ibada safi itaokoka. Hata hivyo, hayawani-mwitu anayeangamiza Babiloni Mkubwa pia awatazama watu wa Yehova kwa pupa. Kwa kufanya hivyo, hayawani huyo atatekeleza, si fikira ya Mungu, bali fikira ya mtu mwingine. Fikira ya nani? Shetani Ibilisi.
22 Yehova afichua njama ya Shetani yenye kiburi: “Itakuwa katika siku hiyo, mawazo yataingia moyoni mwako [mwa Shetani], nawe utakusudia kusudi baya; nawe utasema, Nitapanda . . . [niwaendee] watu wanaostarehe, wanaokaa salama, wote wakikaa pasipo kuta [za kuwalinda] . . . ili kuteka mateka, na kuwinda mawindo.” (Ezekieli 38:10-12) Shetani atawazia hivi, ‘Ehee, mbona nisichochee mataifa yawashambulie Mashahidi wa Yehova? Hawana ulinzi wala uvutano wa kisiasa. Hawatapigana. Itakuwa rahisi kama nini kuwanyakua kama mayai kutoka katika kiota kisicholindwa!’
23. Kwa nini Ashuru wa kisasa hataweza kuwatenda watu wa Mungu yale anayoitenda Jumuiya ya Wakristo?
23 Lakini jihadharini, enyi mataifa! Jueni kuwa mkiwagusa watu wa Yehova, Mungu mwenyewe atakabiliana nanyi! Yehova awapenda watu wake, naye atawapigania kama vile alivyopigania Yerusalemu katika siku za Hezekia. Ashuru wa kisasa atakapojaribu kuwaangamiza watumishi wa Yehova, kwa kweli atakuwa akipigana na Yehova Mungu na Mwana-Kondoo, Yesu Kristo. Ashuru hawezi kuibuka mshindi katika pigano hilo. “Mwana-Kondoo atawashinda,” Biblia yasema, “kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme.” (Ufunuo 17:14; linganisha Mathayo 25:40.) Kama vile Ashuru wa zamani, hayawani-mwitu mwenye rangi-nyekundu-nyangavu ‘ataondoka kwenda zake katika uharibifu.’ Hatahofiwa tena kamwe.—Ufunuo 17:11.
24. (a) Wakristo wa kweli wameazimia kufanya nini ili kujitayarishia wakati ujao? (b) Isaya atazamaje mbele zaidi? (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 155.)
24 Wakristo wa kweli waweza kutazamia wakati ujao bila hofu iwapo wadumisha uhusiano thabiti na Yehova na iwapo kufanya mapenzi yake ndiko jambo kuu maishani mwao. (Mathayo 6:33) Ndipo hawatahitaji ‘kuogopa mabaya.’ (Zaburi 23:4) Kwa macho yao ya imani, wataona mkono wa Mungu wenye uweza ukiwa umenyoshwa juu, si kwa kuwaadhibu, bali kuwalinda dhidi ya adui zake. Na masikio yao yatasikia maneno haya yanayotia moyo: “Msiogope.”—Isaya 10:24.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Insight on the Scriptures, Buku la 1, ukurasa wa 203.
b Ili ieleweke kwa urahisi, Isaya 10:28-32 imezungumzwa kabla ya Isaya 10:20-27.
c Kwa mazungumzo juu ya Isaya 10:20-23, ona “Isaya Atazama Mbele Zaidi,” katika ukurasa wa 155.
d Habari zaidi kuhusu kahaba na hayawani-mwitu mwenye rangi-nyekundu-nyangavu zapatikana katika sura ya 34 na 35 ya kitabu cha Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 155, 156]
ISAYA ATAZAMA MBELE ZAIDI
Sura ya 10 ya Isaya yakazia hasa jinsi ambavyo Yehova atatumia uvamizi wa Ashuru ili kutekeleza hukumu juu ya Israeli na pia kuhusu ahadi yake ya kukinga Yerusalemu. Kwa kuwa mistari ya 20 hadi 23 yapatikana katikati ya unabii huo, yaweza kuonwa kuwa ina utimizo wa jumla katika kipindi kilekile. (Linganisha Isaya 1:7-9.) Hata hivyo, maneno yake yadokeza kuwa mistari hiyo yahusu hasa nyakati za baadaye ambapo Yerusalemu pia litatozwa hesabu kwa sababu ya dhambi za wakazi wake.
Mfalme Ahazi ajaribu kupata usalama kwa kutafuta msaada kwa Ashuru. Nabii Isaya atabiri kuwa wakati fulani baadaye, waliosalia katika nyumba ya Israeli hawatafuatia tena kamwe mwendo huo wa kipumbavu. Isaya 10:20 yasema kwamba “watamtegemea BWANA [“Yehova,” NW], Mtakatifu wa Israeli, kwa kweli.” Hata hivyo, mstari wa 21 waonyesha kuwa ni wachache tu watakaofanya hivyo: “Mabaki . . . watamrudia Mungu.” Hilo latukumbusha Shear-yashubu, mwana wa Isaya, aliye ishara katika Israeli na ambaye jina lamaanisha “Mabaki Wachache Tu Ndio Watakaorudi.” (Isaya 7:3) Mstari wa 22 katika sura ya 10 waonya juu ya kuja kwa “kuangamiza” ambako kumekusudiwa. Kuangamiza huko kutakuwa kwa haki kwa sababu ni adhabu inayofaa kwa watu waasi. Tokeo ni kwamba, kutoka kwa taifa lenye wakazi wengi “kama mchanga wa pwani,” ni mabaki wachache tu watakaorudi. Mstari wa 23 waonya kuwa angamizo hilo linalokuja litaathiri nchi nzima. Yerusalemu halitaachwa salama mara hii.
Mistari hiyo yafafanua ipasavyo mambo yaliyotukia mwaka wa 607 K.W.K. Yehova alipotumia Milki ya Babiloni kama “fimbo” yake. Nchi yote, kutia ndani Yerusalemu, ilianguka mkononi mwa mvamizi. Wayahudi walipelekwa mateka huko Babiloni kwa miaka 70. Hata hivyo, baada ya hapo baadhi yao—hata kama ni “mabaki” tu—walirudi kuanzisha upya ibada ya kweli Yerusalemu.
Unabii katika Isaya 10:20-23 ulikuwa na utimizo mwingine zaidi katika karne ya kwanza, kama ionyeshwavyo katika Waroma 9:27, 28. (Linganisha Isaya 1:9; Waroma 9:29.) Paulo aeleza kwamba kwa njia ya kiroho, “mabaki” ya Wayahudi ‘walimrudia’ Yehova katika karne ya kwanza W.K., kwa vile ni Wayahudi waaminifu wachache waliokuja kuwa wafuasi wa Yesu Kristo na kuanza kumwabudu Yehova “kwa roho na kweli.” (Yohana 4:24) Baadaye wasio Wayahudi wenye kuamini wakajiunga nao, wakifanyiza taifa la kiroho, “Israeli wa Mungu.” (Wagalatia 6:16) Katika pindi hiyo, maneno ya Isaya 10:20 yalitimizwa: Taifa lililojiweka wakfu kwa Yehova halikumwacha “tena” kamwe ili kutegemezwa na binadamu.
[Picha katika ukurasa wa 147]
Senakeribu asababu kwamba kukusanya mataifa ni rahisi kama vile kukusanya mayai kutoka katika kiota