Sura ya 15
Shauri la Yehova Dhidi ya Mataifa
1. Isaya arekodi tangazo gani la hukumu dhidi ya Ashuru?
YEHOVA aweza kutumia mataifa kuwatia nidhamu watu wake kwa sababu ya uovu wao. Ijapokuwa hivyo, hayapi msamaha mataifa hayo kwa ajili ya ukatili wao usiostahili, kiburi, na kuchukia kwao ibada ya kweli. Basi, muda mrefu mapema, yeye ampulizia Isaya kurekodi “ufunuo juu ya Babiloni.” (Isaya 13:1) Hata hivyo, Babiloni ni tisho la wakati ujao. Katika siku ya Isaya, Ashuru yawakandamiza watu wa agano wa Mungu. Ashuru yaharibu ufalme wa kaskazini wa Israeli na kuangamiza sehemu nyingi za Yuda. Lakini ushindi wa Ashuru ni wa muda tu. Isaya aandika: “BWANA wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa . . . kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo nira yake iliyo juu yao itakapoondoka, na mzigo wake utatoka mabegani mwao.” (Isaya 14:24, 25) Muda mfupi baada ya Isaya kutangaza unabii huo, tisho la Ashuru laondolewa nchini Yuda.
2, 3. (a) Katika nyakati za kale, Yehova anyosha mkono wake juu ya nani? (b) Usemi wa kwamba Yehova anyosha mkono wake juu ya “mataifa yote” wamaanisha nini?
2 Hata hivyo, namna gani kuhusu mataifa mengine ambayo ni adui za watu wa agano wa Mungu? Hayo pia sharti yahukumiwe. Isaya atangaza: “Hilo ndilo kusudi [“shauri,” “NW”] lililokusudiwa duniani mwote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote. Maana BWANA wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?” (Isaya 14:26, 27) ‘Shauri’ la Yehova lamaanisha mengi zaidi kuliko pendekezo tu. Lamaanisha azimio lake thabiti, agizo lake. (Yeremia 49:20, 30) “Mkono” wa Mungu ni nguvu yake yenye kutenda. Kwenye mistari ya mwisho ya Isaya sura ya 14 na katika sura ya 15 hadi 19, shauri la Yehova liko dhidi ya Ufilisti, Moabu, Dameski, Ethiopia, na Misri.
3 Hata hivyo, Isaya asema kuwa mkono wa Yehova umenyoshwa juu ya “mataifa yote.” Basi, ingawa unabii huo mbalimbali wa Isaya watimizwa kwa mara ya kwanza katika nyakati za kale, kanuni ya unabii huo yahusu pia “wakati wa mwisho” Yehova anyoshapo mkono wake juu ya falme zote za dunia. (Danieli 2:44; 12:9; Waroma 15:4; Ufunuo 19:11, 19-21) Muda mrefu mapema, Mungu Mweza Yote, Yehova, afunua kusudi lake akiwa na uhakika. Hakuna awezaye kuuzuia mkono wake ulionyoshwa.—Zaburi 33:11; Isaya 46:10.
“Joka la Moto Arukaye” Dhidi ya Ufilisti
4. Ni yapi baadhi ya mambo makuu ya tangazo la Yehova dhidi ya Ufilisti?
4 Wafilisti wazingatiwa kwanza. “Ufunuo huu ulikuja mwaka ule alipokufa mfalme Ahazi. Usifurahi, Ee Ufilisti, pia wote, kwa sababu fimbo ile iliyokupiga imevunjika; maana katika shina la nyoka atatoka fira, na uzao wake ni joka la moto arukaye.”—Isaya 14:28, 29.
5, 6. (a) Uzia alikuwaje kama nyoka kwa Wafilisti? (b) Hezekia athibitika kuwa nini dhidi ya Ufilisti?
5 Mfalme Uzia alikuwa na nguvu za kutosha kuzuia tisho la Ufilisti. (2 Mambo ya Nyakati 26:6-8) Machoni pao, Uzia alikuwa kama nyoka, na fimbo yake ilimpiga-piga jirani huyo mwenye uadui. Baada ya kifo cha Uzia—‘fimbo yake ilivunjika’—Yothamu mwaminifu akatawala, ingawa “watu waliendelea kufanya maovu.” Kisha Ahazi akawa mfalme. Hali ikabadilika, na Wafilisti wakafanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yuda kwa mafanikio. (2 Mambo ya Nyakati 27:2, BHN; 28:17, 18) Hata hivyo, sasa hali yabadilika tena. Mfalme Ahazi afa mwaka wa 746 K.W.K., na Hezekia mchanga achukua kiti cha ufalme. Iwapo Wafilisti wafikiri kuwa hali yao itaendelea kuwa shwari, basi wamekosea kabisa. Hezekia athibitika kuwa adui motomoto. Hezekia, aliye mzao wa Uzia (“uzao” kutoka katika “shina” lake), ni kama “joka la moto arukaye”—huku akipiga mbio kwenda kushambulia kwa haraka, na kutokeza madhara makali, kana kwamba anawadunga majeruhi wake sindano ya sumu.
6 Huo ni ufafanuzi ufaao kuhusu mfalme huyo mpya. Hezekia ndiye ‘aliyewapiga Wafilisti mpaka Gaza na mipaka yake.’ (2 Wafalme 18:8) Kwa mujibu wa kumbukumbu za kihistoria za Mfalme Senakeribu wa Ashuru, Wafilisti waja kutiishwa chini ya Hezekia. “Walio maskini”—ufalme wa Yuda uliofifia—wapata kufurahia usalama na wingi wa mali, huku Ufilisti ikidhikika kwa njaa.—Soma Isaya 14:30, 31.
7. Hezekia apaswa kutoa tangazo gani lenye imani kwa mabalozi waliomo Yerusalemu?
7 Yaonekana kwamba kuna mabalozi nchini Yuda—labda wanatafuta msaada dhidi ya Ashuru. Wapaswa kuambiwa nini? “Wajumbe wa taifa hilo waletewe jibu gani?” Je, Hezekia atafute usalama kwa kushirikiana na wageni? Hata! Yampasa awaambie wajumbe hao: “BWANA ameiweka misingi ya Sayuni, na ndani yake wale walioonewa katika watu wake wataona kimbilio.” (Isaya 14:32) Ni lazima mfalme huyo amtumaini Yehova kabisa-kabisa. Msingi wa Sayuni ni thabiti. Jiji hilo litadumu likiwa mahali salama kutokana na tisho la Ashuru.—Zaburi 46:1-7.
8. (a) Mataifa fulani leo yamekuwaje kama Ufilisti? (b) Yehova amefanya nini ili kuwasaidia watu wake leo, kama alivyofanya nyakati za kale?
8 Sawa na Ufilisti, mataifa fulani leo huwapinga vikali waabudu wa Mungu. Mashahidi Wakristo wa Yehova wametupwa magerezani na katika kambi za mateso. Wamepigwa marufuku. Baadhi yao wameuawa. Wapinzani wazidi ‘kuishambulia nafsi yake mwenye haki.’ (Zaburi 94:21) Machoni pa adui zao, kikundi hicho cha Wakristo huenda kikaonekana kuwa “maskini” na “wahitaji.” Hata hivyo, kwa msaada wa Yehova, wao hufurahia chakula kingi cha kiroho, huku adui zao wakidhikika kwa njaa. (Isaya 65:13, 14; Amosi 8:11) Yehova atakaponyosha mkono wake dhidi ya Wafilisti wa siku za kisasa, “maskini” hao watakuwa salama. Wapi? Kwa kushirikiana na ‘nyumba ya Mungu,’ ambamo Yesu ndiye jiwe la pembeni la msingi lililo thabiti. (Waefeso 2:19, 20) Nao watakuwa chini ya ulinzi wa “Yerusalemu la kimbingu,” Ufalme wa Yehova wa mbinguni, ambapo Yesu Kristo ndiye Mfalme wake.—Waebrania 12:22; Ufunuo 14:1.
Moabu Yanyamazishwa
9. Ufunuo unaofuata unatolewa dhidi ya nani, na watu hao wamethibitikaje kuwa adui za watu wa Mungu?
9 Mashariki mwa Bahari ya Chumvi, kuna jirani mwingine wa Israeli—Moabu. Tofauti na Wafilisti, Wamoabi wanahusiana kiukoo na Israeli, kwa kuwa wao ni wazao wa Loti, mpwa wa Abrahamu. (Mwanzo 19:37) Licha ya uhusiano huo, Moabu ni adui wa muda mrefu wa Israeli. Kwa kielelezo, huko nyuma katika siku za Musa, mfalme wa Moabu alimkodi nabii Balaamu, akitumaini kwamba nabii huyo angewalaani Waisraeli. Mbinu hiyo iliposhindwa, Moabu ilitumia ukosefu wa adili na ibada ya Baali ili kunasa Israeli. (Hesabu 22:4-6; 25:1-5) Basi haishangazi kwamba Yehova sasa ampulizia Isaya kurekodi “ufunuo juu ya Moabu”!—Isaya 15:1a.
10, 11. Ni nini kitakachotukia kwa Moabu?
10 Unabii wa Isaya wahusu majiji na sehemu mbalimbali katika nchi ya Moabu, kutia ndani Ari, Kiri (au Kir-haresethi), na Diboni. (Isaya 15:1b, 2a) Wamoabi watalia kwa sababu ya mikate ya zabibu ya Kir-haresethi, ambayo labda ni zao kuu la jiji hilo. (Isaya 16:6, 7) Sibma na Yazeri, miji maarufu kwa ukuzaji wa zabibu, itapigwa. (Isaya 16:8-10) Eglath-shelishiya, ambao labda jina lake lamaanisha “Ndama wa Miaka Mitatu,” utakuwa kama ng’ombe jike mchanga anayepaza sauti zenye huzuni kwa kukata tamaa. (Isaya 15:5, “BHN”) Majani ya nchi yatakauka huku “maji ya Dimoni” yakijaa damu kwa sababu ya machinjo ya Wamoabi. “Maji ya Nimrimu” yatakuwa “mahali palipoharibika,” kitamathali au kihalisi—yaelekea kwa sababu majeshi ya adui yazuia vijito vyao.—Isaya 15:6-9.
11 Wamoabi watavaa nguo za gunia, mavazi ya maombolezo. Watanyoa vichwa vyao upaa ili kuonyesha aibu na maombolezo. Ndevu zao ‘zitanyolewa,’ kuonyesha huzuni kali na kutwezwa. (Isaya 15:2b-4) Isaya mwenyewe, akiwa na uhakika kuhusu kutimizwa kwa hukumu hizo, apata hisia kali. Sawa na kamba za kinubi zenye kutikisika, sehemu zake za ndani zakumbwa na sikitiko kwa sababu ya ujumbe wa ole dhidi ya Moabu.—Isaya 16:11, 12.
12. Maneno ya Isaya dhidi ya Moabu yalitimizwaje?
12 Unabii huo utatimizwa lini? Hivi karibuni. “Hilo ndilo neno lile alilolisema BWANA juu ya Moabu zamani. Lakini sasa BWANA asema hivi, Katika muda wa miaka mitatu, kama miaka ya mtu wa mshahara, utukufu wa Moabu utadharauliwa, pamoja na wingi wake wote; mabaki yake yatakuwa machache sana, kama si kitu kabisa.” (Isaya 16:13, 14) Kwa kupatana na hayo, kuna uthibitisho wa kiakiolojia kwamba, mnamo karne ya nane K.W.K., Moabu iliteseka sana na sehemu nyingi nchini mwake zikaachwa ukiwa. Tiglath-pilesa wa Tatu alimtaja Salamanu wa Moabu miongoni mwa watawala waliomlipa ushuru. Senakeribu alipokea ushuru kutoka kwa Kamusunadbi, mfalme wa Moabu. Watawala wa Ashuru, Esar-hadoni na Ashurbanipali walisema kuwa waliwatawala Wafalme Musuri na Kamashaltu wa Moabu. Karne kadhaa zilizopita, Wamoabi walikoma kuwa kikundi cha watu. Magofu ya majiji yanayodhaniwa kuwa ya Wamoabi yamevumbuliwa, ingawa hadi sasa kuna uthibitisho mchache ambao umefukuliwa unaohusu adui huyo wa Israeli ambaye hapo awali alikuwa mwenye nguvu sana.
“Moabu” ya Siku ya Kisasa Yaangamia
13. Ni tengenezo gani leo liwezalo kulinganishwa na Moabu?
13 Leo, kuna tengenezo la ulimwenguni kote linalofanana na Moabu ya kale. Tengenezo hilo ni Jumuiya ya Wakristo, sehemu kuu ya “Babiloni Mkubwa.” (Ufunuo 17:5) Moabu na Israeli zilitokana na baba ya Abrahamu, Tera. Vivyo hivyo, Jumuiya ya Wakristo, kama vile kutaniko la Wakristo watiwa-mafuta, hudai kwamba mwanzo wake uko katika kutaniko la Kikristo la karne ya kwanza. (Wagalatia 6:16) Hata hivyo, Jumuiya ya Wakristo—sawa na Moabu—ni fisadi, nayo yaendeleza ibada ya miungu tofauti na Mungu mmoja wa kweli, Yehova. (Yakobo 4:4; 1 Yohana 5:21) Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, wakiwa kikundi, hupinga wale wanaohubiri habari njema ya Ufalme.—Mathayo 24:9, 14.
14. Licha ya shauri la Yehova dhidi ya “Moabu” ya leo, kuna tumaini gani kwa washiriki mmoja-mmoja wa tengenezo hilo?
14 Hatimaye Moabu ilinyamazishwa. Jambo hilohilo litakumba Jumuiya ya Wakristo. Yehova, huku akitumia mfano wa kisasa wa Ashuru, atamfanya ukiwa. (Ufunuo 17:16, 17) Hata hivyo, kuna tumaini kwa watu katika “Moabu” ya siku ya kisasa. Katikati ya unabii wake dhidi ya Moabu, Isaya asema: “Kiti cha enzi kitafanywa imara kwa rehema; na mmoja ataketi juu yake katika kweli, katika hema ya Daudi; akifanya hukumu, akitaka sana yaliyo haki, mwepesi wa kutenda haki.” (Isaya 16:5) Mwaka wa 1914, Yehova alikisimamisha imara kiti cha ufalme cha Yesu, Mtawala katika ukoo wa Mfalme Daudi. Umaliki wa Yesu ni wonyesho wa rehema ya Yehova, nao utadumu milele, kwa kutimiza agano la Mungu pamoja na Mfalme Daudi. (Zaburi 72:2; 85:10, 11; 89:3, 4; Luka 1:32) Wasikivu wengi wameacha “Moabu” ya siku ya kisasa nao wamejitiisha chini ya Yesu ili wapate uhai. (Ufunuo 18:4) Inawafariji kama nini kujua kwamba Yesu ‘atafanya lililo haki kuwa wazi kwa mataifa’!—Mathayo 12:18; Yeremia 33:15.
Dameski Yawa Magofu Yenye Kuoza
15, 16. (a) Dameski na Israeli zachukua hatua gani kali dhidi ya Yuda, na kuna tokeo gani kwa Dameski? (b) Ni nani anayetiwa ndani katika ufunuo dhidi ya Dameski? (c) Wakristo leo waweza kujifunza nini kutokana na kielelezo cha Israeli?
15 Kisha, Isaya arekodi “ufunuo juu ya Dameski.” (Soma Isaya 17:1-6.) Dameski, jiji lililo sehemu ya kaskazini ya Israeli, ni “kichwa cha Siria.” (Isaya 7:8, NW) Wakati wa utawala wa Mfalme Ahazi wa Yuda, Resini wa Dameski akishirikiana na Peka wa Israeli, avamia Yuda. Hata hivyo, kwa kujibu ombi la Ahazi, Tiglath-pilesa wa Tatu apiga vita dhidi ya Dameski, alishinda na kuwahamisha wengi wa wakazi wake. Baada ya hapo, Dameski lakoma kuwa tisho kwa Yuda.—2 Wafalme 16:5-9; 2 Mambo ya Nyakati 28:5, 16.
16 Labda kwa sababu ya mwungano wa Israeli na Dameski, ufunuo wa Yehova dhidi ya Dameski watia ndani pia udhihirisho mbalimbali wa hukumu dhidi ya ufalme wa kaskazini usio mwaminifu. (Isaya 17:3-6) Israeli itakuwa kama shamba lenye nafaka chache sana wakati wa mavuno au kama mzeituni ambapo zeituni zilizo nyingi zimetikiswa kutoka kwenye matawi. (Isaya 17:4-6) Hicho ni kielelezo chenye kuamsha fikira kama nini kwa wale ambao wamejiweka wakfu kwa Yehova! Yeye atarajia ujitoaji usiohusisha wengine naye hukubali tu utumishi mtakatifu unaotolewa kwa moyo wote. Naye huchukia wale wanaochukia ndugu zao.—Kutoka 20:5; Isaya 17:10, 11; Mathayo 24:48-50.
Uhakika Kamili Katika Yehova
17, 18. (a) Baadhi ya watu katika Israeli waitikiaje ufunuo mbalimbali wa Yehova, lakini itikio la jumla ni nini? (b) Matukio ya leo yafananaje na yale ya siku ya Hezekia?
17 Isaya sasa asema: “Katika siku hiyo mwanadamu atamwangalia Muumba wake, na macho yake yatamtazama Mtakatifu wa Israeli. Wala hataziangalia madhabahu, kazi ya mikono yake; wala hatavitazama vilivyofanyika kwa vidole vyake, maashera na sanamu za jua.” (Isaya 17:7, 8) Naam, baadhi ya watu katika Israeli watii ufunuo wa Yehova wenye onyo. Kwa kielelezo, Hezekia aalikapo wakazi wa Israeli waungane na Yuda kusherehekea Sikukuu ya Kupitwa, Waisraeli fulani wakubali na kusafiri kwenda kusini kuungana na ndugu zao katika ibada safi. (2 Mambo ya Nyakati 30:1-12) Ijapokuwa hivyo, walio wengi wa wakazi wa Israeli wawadhihaki wajumbe waliotumwa kuwaalika. Nchi imeasi kabisa. Kwa hiyo, shauri la Yehova dhidi yake latimizwa. Ashuru yaharibu majiji ya Israeli, nchi yatiwa ukiwa, na malisho yakoma kutoa mazao.—Soma Isaya 17:9-11.
18 Namna gani leo? Israeli lilikuwa taifa lenye kuasi. Basi, jinsi Hezekia alivyojaribu kusaidia watu mmoja-mmoja katika taifa hilo wairudie ibada ya kweli hutukumbusha kuhusu jinsi Wakristo wa kweli leo wanavyojaribu kusaidia watu mmoja-mmoja katika tengenezo lenye kuasi la Jumuiya ya Wakristo. Tangu mwaka wa 1919, wajumbe kutoka katika “Israeli wa Mungu” wameenda kote katika Jumuiya ya Wakristo, wakiwaalika watu washiriki katika ibada safi. (Wagalatia 6:16) Walio wengi wamekataa. Wengi wamewadhihaki wajumbe hao. Ingawa hivyo, baadhi yao wameitikia. Idadi yao sasa imefikia mamilioni, nao hufurahia ‘kumtazama Mtakatifu wa Israeli,’ anayewafundisha. (Isaya 54:13) Wao huachilia mbali ibada kwenye madhabahu zisizo takatifu—ujitoaji na kutumaini miungu iliyotengenezwa na wanadamu—nao kwa hamu humgeukia Yehova. (Zaburi 146:3, 4) Sawa na Mika aliyeishi wakati mmoja na Isaya, kila mmoja wao husema: “Lakini mimi, nitamtazamia BWANA; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia.”—Mika 7:7.
19. Yehova atakemea nani, na jambo hilo litamaanisha nini kwao?
19 Kuna tofauti iliyoje kati yao na wale wanaomtumaini binadamu awezaye kufa! Mawimbi yenye michafuko ya jeuri na misukosuko hupiga binadamu katika siku hizi za mwisho. “Bahari” ya binadamu wasiotulia, wenye kuasi, hutokeza kutoridhika na mapinduzi. (Isaya 57:20; Ufunuo 8:8, 9; 13:1) Yehova ‘ataukemea’ umati huo wenye kelele. Ufalme wake wa mbinguni utaharibu kila tengenezo na watu mmoja-mmoja wenye kusababisha matata, nao “watakimbia mbali sana . . . kama mavumbi vuruvuru mbele ya tufani.”—Isaya 17:12, 13; Ufunuo 16:14, 16.
20. Licha ya mataifa ‘kuwanyang’anya mali zao,’ Wakristo wa kweli wana uhakika gani?
20 Tokeo ni nini? Isaya asema: “Wakati wa jioni, tazama, kuna hofu; na kabla ya mapambazuko hawako; hilo ndilo fungu lao watutekao, na ajali yao wanaotunyang’anya mali zetu.” (Isaya 17:14) Wengi wanawanyang’anya watu wa Yehova mali zao, wakiwatenda kwa ukali na kwa dharau. Kwa sababu Wakristo wa kweli si sehemu ya—nao hawataki kuwa sehemu ya—dini kubwa-kubwa za ulimwengu, wachambuzi wenye kuonea na wapinzani washupavu huwaona kuwa windo rahisi. Lakini watu wa Mungu wana uhakika kwamba wakati wa “mapambazuko” ambapo dhiki zao zitakwisha wakaribia upesi.—2 Wathesalonike 1:6-9; 1 Petro 5:6-11.
Ethiopia Yamletea Yehova Zawadi
21, 22. Ni taifa gani ambalo sasa lapata ufunuo wa hukumu, na maneno ya Isaya yaliyopuliziwa yatimizwaje?
21 Ethiopia, iliyoko kusini mwa Misri, imepambana kijeshi dhidi ya Yuda angalau mara mbili. (2 Mambo ya Nyakati 12:2, 3; 14:1, 9-15; 16:8) Sasa Isaya atabiri hukumu juu ya taifa hilo: “Ole wa nchi ya uvumi wa mabawa, iliyoko mbali kupita mito ya Kushi [“Ethiopia,” “NW”].” (Soma Isaya 18:1-6.)a Yehova aamuru kuwa Ethiopia ‘itakatwa na kuondolewa.’
22 Historia ya kilimwengu hutueleza kwamba mwishoni mwa karne ya nane K.W.K., Ethiopia ilishinda Misri na kuitawala kwa miaka ipatayo 60. Kisha Maliki wa Ashuru Esar-hadoni na Ashurbanipali wakavamia. Baada ya Ashurbanipali kuharibu Thebesi, Ashuru iliitiisha Misri, kwa hiyo ikakomesha utawala wa Ethiopia juu ya Bonde la Nile. (Ona pia Isaya 20:3-6.) Vipi sasa?
23. “Ethiopia” ya siku ya kisasa hutimiza fungu gani, na kwa nini yaangamizwa?
23 Katika unabii wa Danieli juu ya “wakati wa mwisho,” yaelezwa kuwa Libya na Ethiopia ‘zafuata nyayo zake,’ yaani, zafuata mwongozo wa “mfalme wa kaskazini” aliye mchokozi. (Danieli 11:40-43, linganisha NW.) Ethiopia pia yatajwa kuwa sehemu ya majeshi ya “Gogu, wa nchi ya Magogu.” (Ezekieli 38:2-5, 8) Majeshi ya Gogu, kutia ndani mfalme wa kaskazini, yaangamizwa yashambuliapo taifa takatifu la Yehova. Kwa hiyo, mkono wa Yehova pia utanyoshwa dhidi ya “Ethiopia” ya siku ya kisasa kwa sababu ya upinzani wake kwa enzi kuu ya Yehova.—Ezekieli 38:21-23; Danieli 11:45.
24. Yehova amepokeaje “zawadi” kutoka kwa mataifa?
24 Ingawa hivyo, unabii huo pia wasema: “Wakati huo BWANA wa majeshi ataletewa hedaya [“zawadi,” “NW”] na watu warefu, laini; watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa . . . mpaka mahali pa jina la BWANA wa majeshi, mlima Sayuni.” (Isaya 18:7) Ijapokuwa mataifa hayatambui enzi kuu ya Yehova, nyakati fulani hayo yametenda kwa njia ambazo zawanufaisha watu wa Yehova. Katika nchi fulani, wenye mamlaka wametunga sheria na kutoa hukumu za mahakamani zinazowapa waabudu waaminifu wa Yehova haki za kisheria. (Matendo 5:29; Ufunuo 12:15, 16) Na pia kuna zawadi nyingine. “Wafalme watakuletea hedaya [“zawadi,” NW] . . . Masheki watakuja kutoka Misri, Kushi [Ethiopia] itamnyoshea Mungu mikono yake mara.” (Zaburi 68:29-31) Leo, mamilioni ya “Waethiopia” wanaomhofu Yehova wanaleta “zawadi” kwa namna ya ibada. (Malaki 1:11) Wao wanaishiriki kazi kubwa ya kuhubiri habari njema ya Ufalme duniani kote. (Mathayo 24:14; Ufunuo 14:6, 7) Hiyo ni zawadi bora kama nini ya kumtolea Yehova!—Waebrania 13:15.
Moyo wa Misri Wayeyuka
25. Ni nini linalotukia juu ya Misri ya kale kwa utimizo wa Isaya 19:1-11?
25 Jirani wa karibu zaidi wa Yuda upande wa kusini ni Misri, adui wa muda mrefu wa watu wa agano wa Mungu. Isaya sura ya 19 yasimulia hali zenye vurugu nchini Misri wakati wa maisha ya Isaya. Kuna vita ya wenyewe kwa wenyewe Misri, kukiwa vita ya “mji juu ya mji, na ufalme juu ya ufalme.” (Isaya 19:2, 13, 14) Wanahistoria watoa uthibitisho unaohusu nasaba za wafalme zenye kupambana zikitawala sehemu mbalimbali za nchi hiyo kwa wakati mmoja. Hekima wanayojivunia Wamisri, pamoja na ‘sanamu zao, na waganga wao,’ haiwaokoi kutoka katika “mikono ya bwana mgumu.” (Isaya 19:3, 4) Ashuru, Babiloni, Uajemi, Ugiriki, na Roma, zaishinda Misri kabisa. Matukio hayo yote yatimiza unabii mbalimbali wa Isaya 19:1-11.
26. Kwenye utimizo ulio mkubwa zaidi, wakazi wa “Misri” ya siku ya kisasa wataitikiaje hukumu za Yehova?
26 Hata hivyo, katika Biblia, mara nyingi Misri hufananisha ulimwengu wa Shetani. (Ezekieli 29:3; Yoeli 3:19; Ufunuo 11:8) Basi, je, “ufunuo [wa Isaya] juu ya Misri” una utimizo mkubwa zaidi? Kwa kweli ndiyo! Maneno ya mwanzo-mwanzo ya unabii huo yapasa kumfanya kila mtu kukaza uangalifu: “Tazama, BWANA amepanda juu ya wingu jepesi, anafika Misri; na sanamu za Misri zinatikisika mbele zake, na moyo wa Misri unayeyuka ndani yake.” (Isaya 19:1) Yehova atachukua hatua dhidi ya tengenezo la Shetani hivi karibuni. Wakati huo ufikapo, miungu ya mfumo huu wa mambo itathibitishwa kuwa isiyofaa kitu. (Zaburi 96:5; 97:7) ‘Moyo wa Misri utayeyuka’ kwa hofu. Yesu aliutabiri wakati huo: “Kutakuwa . . . maumivu makali ya mataifa, bila kujua njia ya kutokea kwa sababu ya kunguruma kwa bahari na msukosuko wayo, huku watu wakizimia moyo kutokana na hofu na tarajio la mambo yanayokuja juu ya dunia inayokaliwa.”—Luka 21:25, 26.
27. Ni migawanyiko ipi ya kindani iliyotabiriwa kuhusu “Misri,” na mambo hayo yanatimizwaje leo?
27 Yehova asema hivi kwa maneno ya unabii kuhusiana na wakati utakaoongoza kwenye kutekelezwa kwa hukumu: “Nitawaamsha Wamisri juu ya Wamisri; nao watapigana, kila mtu na ndugu yake, na kila mtu na jirani yake, mji juu ya mji, na ufalme juu ya ufalme.” (Isaya 19:2) Tangu kusimamishwa kwa Ufalme wa Mungu mwaka wa 1914, “ishara ya kuwapo [kwa Yesu]” imeonekana taifa liinukapo dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Mamilioni ya watu katika siku hizi za mwisho wamekufa kwa sababu ya mauaji ya kikabila, maangamizi ya kijamii yenye umwagikaji wa damu, na maangamizi ya watu wa jamii fulani hususa. “Maumivu [hayo] makali ya ghafula ya taabu” hayana budi kuwa mabaya zaidi mwisho ukaribiapo.—Mathayo 24:3, 7, 8.
28. Katika siku ya hukumu, dini isiyo ya kweli itaweza kufanya nini ili kuuokoa mfumo huu wa mambo?
28 “Roho ya Misri itamwagika kabisa katikati yake, nami nitayabatilisha mashauri yake, nao watakwenda kwa sanamu zao, na kwa waganga, na kwa wapiga ramli, na kwa wachawi.” (Isaya 19:3) Musa alipoenda mbele ya Farao, makuhani wa Misri waliaibishwa, kwa kuwa hawakuweza kulingana na Yehova katika nguvu. (Kutoka 8:18, 19; Matendo 13:8; 2 Timotheo 3:8) Vivyo hivyo, katika siku ya hukumu, dini isiyo ya kweli haitaweza kuuokoa mfumo huu wenye ufisadi. (Linganisha Isaya 47:1, 11-13.) Hatimaye, Misri ikaja chini ya “bwana mgumu,” Ashuru. (Isaya 19:4) Hilo laonyesha kimbele wakati wenye huzuni unaokabili mfumo huu wa mambo.
29. Siku ya Yehova ifikapo, wanasiasa watatoa msaada gani?
29 Hata hivyo, vipi kuhusu viongozi wa kisiasa? Je, waweza kutoa msaada? “Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu kabisa; washauri wenye hekima wa Farao, shauri lao limepumbazika.” (Soma Isaya 19:5-11.) Ni upumbavu kama nini kutumaini kwamba washauri wa kibinadamu watatoa msaada wowote katika siku ya hukumu! Licha ya kuwa na ujuzi wote unaopatikana ulimwenguni, wao hawana hekima ya Mungu. (1 Wakorintho 3:19) Wamemkataa Yehova nao wamegeukia mambo yaitwayo eti sayansi, falsafa, fedha, raha, na miungu mingine ya badala. Kwa hiyo hawana ujuzi wowote wa makusudi ya Mungu. Wamedanganyika na kuvurugika. Kazi zao ni bure tu. (Soma Isaya 19:12-15.) “Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la BWANA, wana akili gani ndani yao?”—Yeremia 8:9.
Ishara na Ushuhuda kwa Yehova
30. ‘Nchi ya Yuda itakuwaje sababu ya utisho kwa Misri’?
30 Ijapokuwa viongozi wa “Misri” ni dhaifu, “kama wanawake,” kungalipo watu fulani wanaotafuta hekima ya Mungu. Watiwa-mafuta wa Yehova na waandamani wao ‘wanatangaza kotekote sifa bora kabisa za Mungu.’ (Isaya 19:16; 1 Petro 2:9) Wanafanya yote wawezayo ili kuwaonya watu kuhusu angamizo linalokuja la tengenezo la Shetani. Akitazama mbele kwenye hali hiyo, Isaya asema: “Nchi ya Yuda itakuwa sababu ya utisho kwa Misri; kila mtu atakayeambiwa habari zake ataingiwa na woga, kwa sababu ya kusudi [“shauri,” “NW”] la BWANA wa majeshi, analolikusudia juu yake.” (Isaya 19:17) Wajumbe waaminifu wa Yehova huendelea kuwaambia watu kweli—kutia ndani tangazo la tauni ambazo Yehova alizitabiri. (Ufunuo 8:7-12; 16:2-12) Hilo lawakera viongozi wa kidini wa ulimwengu.
31. “Lugha ya Kanaani” yasemwaje kwenye majiji ya Misri (a) katika nyakati za kale? (b) katika nyakati za kisasa?
31 Kazi hiyo ya kutangaza imekuwa na matokeo gani yenye kushangaza? “Katika siku hiyo itakuwako miji mitano katika nchi ya Misri itumiayo lugha ya Kanaani, na kumwapia BWANA wa majeshi; mji mmoja utaitwa Mji wa uharibifu.” (Isaya 19:18) Katika nyakati za kale yaelekea unabii huo ulitimizwa Wayahudi waliokuwa wamekimbilia Misri waliposema lugha ya Kiebrania kwenye majiji ya Misri. (Yeremia 24:1, 8-10; 41:1-3; 42:9–43:7; 44:1) Leo, kuna watu kwenye eneo la “Misri” ya siku ya kisasa ambao wamejifunza kusema “lugha iliyo safi” ya kweli ya Biblia. (Sefania 3:9) Mojawapo ya majiji matano ya kitamathali laitwa ‘Mji wa Uharibifu,’ ikimaanisha kwamba sehemu ya “lugha iliyo safi” yahusisha kufichua na ‘kuharibu’ tengenezo la Shetani.
32. (a) Ni “madhabahu” gani iliyoko katikati ya nchi ya Misri? (b) Watiwa-mafuta wakoje kama “nguzo” mpakani mwa Misri?
32 Kwa msaada wa kazi ya kutangaza ya watu wa Yehova, hapana shaka jina lake kuu litajulikana katika mfumo huu wa mambo. “Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa BWANA [“Yehova,” “NW”], na nguzo mpakani mwake kwa BWANA.” (Isaya 19:19) Maneno hayo yarejezea cheo cha Wakristo watiwa-mafuta, ambao wako katika uhusiano wa agano pamoja na Mungu. (Zaburi 50:5) Wakiwa kama “madhabahu” wao wanatoa dhabihu zao; wakiwa kama “nguzo na tegemezo la ile kweli,” wanatoa ushahidi kuhusu Yehova. (1 Timotheo 3:15; Waroma 12:1; Waebrania 13:15, 16) Wako “katika nchi,” nao wapatikana—pamoja na waandamani wao wa “kondoo wengine”—katika nchi na visiwa vya bahari zaidi ya 230. Lakini wao “si sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 10:16; 17:15, 16) Ni kana kwamba wanasimama kwenye mpaka kati ya ulimwengu huu na Ufalme wa Mungu, wakiwa wamejiandaa kuvuka mpaka huo na kupokea thawabu yao ya mbinguni.
33. Watiwa-mafuta ni “ishara” na “ushuhuda” nchini “Misri” kwa njia zipi?
33 Isaya aendelea: “Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa BWANA [“Yehova,” “NW”] wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia BWANA kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa.” (Isaya 19:20) Wakiwa kama “ishara” na “ushuhuda,” watiwa-mafuta huongoza katika kazi ya kuhubiri nao hulikweza jina la Yehova katika mfumo huu wa mambo. (Isaya 8:18; Waebrania 2:13) Vilio vya watu wanaoonewa vyasikika ulimwenguni kote, lakini kwa jumla, serikali za kibinadamu zimeshindwa kuwasaidia. Hata hivyo, Yehova atamtuma Mwokozi Mtukufu, Mfalme Yesu Kristo, ili awaokoe wanyenyekevu wote. Siku hizi za mwisho zifikiapo upeo kwenye vita vya Har–Magedoni, atawaletea wanadamu wanaomhofu Mungu kitulizo na baraka zidumuzo milele.—Zaburi 72:2, 4, 7, 12-14.
34. (a) Yehova atajulikanaje kwa “Wamisri,” nao watamtolea dhabihu na zawadi gani? (b) Yehova ataipiga “Misri” lini, na ni uponyaji gani utakaofuata?
34 Kwa sasa, ni mapenzi ya Mungu kwamba watu wa namna zote wapate ujuzi sahihi nao waokolewe. (1 Timotheo 2:4) Basi, Isaya aandika: “BWANA [“Yehova,” “NW”] atajulikana na Misri, na Wamisri watamjua BWANA katika siku hiyo; naam watamtumikia kwa dhabihu na matoleo, nao watamwekea BWANA nadhiri, na kuzitekeleza. Naye BWANA atapiga Misri, akipiga na kuponya; nao wakirudi kwa BWANA, atakubali maombi yao na kuwaponya.” (Isaya 19:21, 22) Watu kutoka katika mataifa yote ya ulimwengu wa Shetani, “Wamisri” mmoja-mmoja, wapata kumjua Yehova na kumtolea dhabihu, “tunda la midomo ambayo hulifanyia jina lake tangazo la hadharani.” (Waebrania 13:15) Wao huweka nadhiri kwa Yehova kwa kujiweka wakfu kwake, nao huitekeleza nadhiri yao kwa kuishi maisha ya utumishi wenye uaminifu-mshikamanifu. Baada ya ‘pigo’ ambalo Yehova atapiga mfumo huu wa mambo kwenye Har–Magedoni, atautumia Ufalme wake ili kuponya jamii ya kibinadamu. Wakati wa Utawala wa Yesu wa Mileani, jamii ya kibinadamu itainuliwa kufikia ukamilifu wa kiroho, kiakili, kiadili, na kimwili—uponyaji ulioje!—Ufunuo 22:1, 2.
“Wabarikiwe Watu Wangu”
35, 36. Kwa utimizo wa Isaya 19:23-25, ni uhusiano gani uliokuja kuwapo kati ya Misri, Ashuru, na Israeli katika nyakati za kale?
35 Kisha nabii huyo aona kimbele tukio la ajabu: “Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hata Ashuru; Mwashuri atafika Misri, na Mmisri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri. Katika siku hiyo Israeli atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka kati ya dunia; kwa kuwa BWANA wa majeshi amewabariki, akisema, Wabarikiwe watu wangu Misri; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israeli, urithi wangu.” (Isaya 19:23-25) Naam, siku moja, kutakuwepo uhusiano wa kirafiki kati ya Misri na Ashuru. Jinsi gani?
36 Yehova alipowaokoa watu wake kutoka katika mataifa nyakati zilizopita, ni kana kwamba aliwafanyia njia kuu zinazoelekea kwenye uhuru. (Isaya 11:16; 35:8-10; 49:11-13; Yeremia 31:21) Utimizo mdogo wa unabii huo ulitukia baada ya kushindwa kwa Babiloni wakati wahamishwa kutoka Ashuru na Misri, na vilevile kutoka Babiloni, walipoletwa tena kwenye Bara Lililoahidiwa. (Isaya 11:11) Lakini namna gani nyakati za kisasa?
37. Mamilioni leo waishije kana kwamba kuna njia kuu kati ya “Ashuru” na “Misri”?
37 Leo, mabaki ya Waisraeli watiwa-mafuta ni “baraka kati ya dunia.” Wao huendeleza ibada ya kweli nao wanawatangazia watu katika mataifa yote ujumbe wa Ufalme. Baadhi ya mataifa hayo ni kama Ashuru, yana uwezo mkubwa wa kijeshi. Mataifa mengine ni yenye uhuru zaidi, labda kama Misri—ambayo wakati mmoja ilikuwa “mfalme wa kusini” katika unabii wa Danieli. (Danieli 11:5, 8) Mamilioni ya watu mmoja-mmoja kutoka katika mataifa yenye uwezo mkubwa wa kijeshi na yale yenye uhuru zaidi wameikubali njia ya ibada ya kweli. Kwa hiyo, watu kutoka katika mataifa yote wameungana katika ‘ibada.’ Hakuna migawanyiko yoyote ya kitaifa miongoni mwao. Wao hupendana, na yaweza kusemwa kikweli kwamba ‘Mwashuri afika Misri, na Mmisri afika Ashuru.’ Ni kana kwamba kuna njia kuu kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine.—1 Petro 2:17.
38. (a) Israeli ‘atakuwaje wa tatu pamoja na Misri na Ashuru’? (b) Kwa nini Yehova asema “Wabarikiwe watu wangu”?
38 Hata hivyo, Israeli ‘apataje kuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru’? Mapema katika “wakati wa mwisho,” walio wengi wa wale wanaomtumikia Yehova duniani walikuwa washiriki wa “Israeli wa Mungu.” (Danieli 12:9; Wagalatia 6:16) Tangu miaka ya 1930, umati mkubwa wa “kondoo wengine,” walio na tumaini la kuishi duniani, umetokea. (Yohana 10:16a; Ufunuo 7:9) Huku wakitoka katika mataifa—yaliyowakilishwa na Misri na Ashuru—wamiminika kwenye nyumba ya ibada ya Yehova na kuwaalika wengine wajiunge nao. (Isaya 2:2-4) Wanafanya kazi ileile ya kuhubiri kama ndugu zao watiwa-mafuta, huvumilia majaribu yaleyale, hudhihirisha uaminifu na uaminifu-maadili uleule, nao hujilisha kwenye meza ileile ya kiroho. Kwa kweli, watiwa-mafuta na “kondoo wengine” ni “kundi moja, mchungaji mmoja.” (Yohana 10:16b) Je, yeyote aweza kutilia shaka kuwa Yehova, aonapo bidii na uvumilivu wao, apendezwa na utendaji wao? Basi haishangazi kwamba yeye atangaza baraka kwao, akisema: “Wabarikiwe watu wangu”!
[Maelezo ya Chini]
a Wasomi fulani hudokeza kwamba usemi “nchi ya uvumi wa mabawa” warejezea nzige ambao husongamana huko Ethiopia mara kwa mara. Wengine husema kuwa sauti ya neno la Kiebrania linalotafsiriwa “uvumi,” tsela·tsalʹ, yafanana na sauti ya jina ambalo Wagala, wanaoishi katika Ethiopia ya sasa, walimwita mbung’o, yaani, tsaltsalya.
[Picha katika ukurasa wa 191]
Wapiganaji Wafilisti wakishambulia adui zao (mchongo wa Kimisri wa karne ya 12 K.W.K.)
[Picha katika ukurasa wa 192]
Mchongo wa mpiganaji au mungu wa Moabu kwenye jiwe (kati ya karne ya 11 na ya 8 K.W.K.)
[Picha katika ukurasa wa 196]
Mpiganaji wa Siria amepanda ngamia (karne ya tisa K.W.K.)
[Picha katika ukurasa wa 198]
“Bahari” ya binadamu wenye kuasi hutokeza kutoridhika na pia mapinduzi
[Picha katika ukurasa wa 203]
Makuhani wa Misri hawakuweza kulingana na Yehova katika nguvu