Sura ya 18
Mafundisho Kuhusu Kukosa Uaminifu
1. Huenda hali ilikuwaje ndani ya jiji la kale lenye kuzingiwa?
WAZIA jinsi hali ilivyokuwa ndani ya jiji la kale lenye kuzingiwa. Nje ya kuta za jiji kuna adui—mwenye nguvu na mkatili. Unafahamu kwamba tayari amekwisha angusha majiji mengine. Na sasa ameazimia kushinda na kupora jiji lenu na kuteka na kuua wakazi wake. Majeshi ya adui yana uwezo mkubwa sana hivi kwamba haiwezekani kupambana nayo moja kwa moja; unatumaini tu kwamba kuta za jiji zitawazuia wasiingie. Utazamapo nje ukiwa juu ya kuta, waweza kuiona minara ya mazingiwa ambayo adui ameleta. Wao pia wana mitambo ya mazingiwa iwezayo kurusha mawe makubwa ya kuvunja kinga zenu. Unaona mitambo yao ya kubomoa kuta na ngazi za kushambulia, wapiga mishale na magari yao, vikosi vya wanajeshi wao. Hayo yatisha kama nini!
2. Mazingiwa yanayoelezwa katika Isaya sura ya 22 yatukia lini?
2 Katika Isaya sura ya 22, twasoma kuhusu mazingiwa kama hayo—kuzingiwa kwa Yerusalemu. Hayo yatukia lini? Ni vigumu kutaja mazingiwa yoyote hususa ambapo mambo yote yaliyofafanuliwa yatimizwa. Yaonekana unabii huo waeleweka kwa njia bora zaidi kama ufafanuzi wa jumla wa mazingiwa mbalimbali yatakayoikumba Yerusalemu, onyo la jumla kuhusu mambo yaliyo mbele.
3. Wakazi wa Yerusalemu waitikiaje mazingiwa ambayo Isaya afafanua?
3 Wakazi wa Yerusalemu wanafanya nini wakabilipo mazingiwa ambayo Isaya afafanua? Wakiwa watu wa agano wa Mungu, je, wanamlilia Yehova awaokoe? La, wanaonyesha mtazamo usio wa hekima hata kidogo, mtazamo ambao watu wengi leo wanaodai kumwabudu Mungu wanao.
Jiji Limezingiwa
4. (a) “Bonde la maono” ni nini, na kwa nini laitwa hivyo? (b) Wakazi wa Yerusalemu wana hali gani ya kiroho?
4 Katika sura ya 21 ya Isaya, kila mmoja wa ule ujumbe wa aina tatu wa hukumu ulianza kwa neno “Ufunuo.” (Isaya 21:1, 11, 13) Sura ya 22 yaanza vivyo hivyo: “Ufunuo juu ya bonde la maono. Sasa una nini, wewe, hata umepanda pia juu ya dari za nyumba?” (Isaya 22:1) Usemi “bonde la maono” warejezea Yerusalemu. Jiji hilo laitwa bonde kwa sababu hata ingawa liko juu, linazungukwa na milima mirefu zaidi. Lahusianishwa na “maono” kwa sababu maono na ufunuo mwingi wa kimungu ulitolewa humo. Kwa sababu hiyo, wakazi wa jiji hilo wapaswa kuzingatia maneno ya Yehova. Badala yake, wamempuuza nao wamepotoka na kuingia katika ibada isiyo ya kweli. Mungu amtumia adui anayezingira jiji hilo kuhukumu watu wake waliopotoka.—Kumbukumbu la Torati 28:45, 49, 50, 52.
5. Labda ni kwa nini watu wapanda juu ya dari zao?
5 Ona kwamba wakazi wa Yerusalemu ‘wamepanda juu ya dari’ za nyumba zao. Nyakati za kale, dari za nyumba za Waisraeli zilikuwa sawasawa na mara nyingi familia zilikusanyika huko. Isaya hataji sababu ya kukusanyika kwao kwenye pindi hii, ingawa maneno yake yadokeza lawama. Labda, basi, wamepanda juu ya dari ili kuomba miungu yao isiyo ya kweli. Hiyo ndiyo desturi yao katika miaka inayoongoza kwenye kuharibiwa kwa Yerusalemu mwaka wa 607 K.W.K.—Yeremia 19:13; Sefania 1:5.
6. (a) Ni hali gani zaenea ndani ya Yerusalemu? (b) Kwa nini wengine wafurahi, lakini kuna nini mbele?
6 Isaya aendelea: “Ewe uliyejaa makelele, mji wa ghasia, mji wenye furaha; watu wako waliouawa hawakuuawa kwa upanga, wala hawakufa vitani.” (Isaya 22:2) Umati wa watu umeingia jijini, nalo limejaa makelele. Watu mitaani wanapiga makelele nao wanahofu. Hata hivyo, baadhi yao wanafurahi, labda kwa sababu wanahisi wako salama au wanaamini kuwa hatari inapitilia mbali.a Lakini ni upumbavu kufurahi wakati huu. Wengi jijini humo watakufa kifo chenye ukatili zaidi kuliko kile cha upanga. Jiji lililozingiwa halina njia yoyote ya kupata chakula kutoka nje. Akiba zilizo ndani ya jiji zapungua. Watu wanaokufa njaa na hali zenye kusongamana zasababisha magonjwa ya mlipuko. Kwa hiyo wengi jijini Yerusalemu watakufa kutokana na njaa na magonjwa ya kuambukiza. Mambo hayo yatukia mwaka wa 607 K.W.K. na vilevile mwaka wa 70 W.K.—2 Wafalme 25:3; Maombolezo 4:9, 10.b
7. Watawala wa Yerusalemu wafanya nini wakati wa mazingiwa, na ni nini kinachowapata?
7 Katika mgogoro huo, watawala wa Yerusalemu watoa mwongozo gani? Isaya ajibu: “Wakuu wako wote wamekimbia pamoja, wamefungwa wasiutumie upinde. Wote walioonekana wamefungwa pamoja, wamekimbia mbali sana.” (Isaya 22:3) Watawala na watu wenye uwezo wakimbia kisha washikwa! Pasipo hata upinde kutumiwa dhidi yao, wakamatwa na kupelekwa kifungoni. Hayo yatukia mwaka wa 607 K.W.K. Baada ya kubomolewa tundu katika ukuta wa Yerusalemu, Mfalme Zedekia akimbia usiku pamoja na watu wake wenye uwezo. Adui afahamu hilo, awaandama, na kuwafikia kwenye nyanda za Yeriko. Watu wenye uwezo watawanyika. Zedekia akamatwa, apofushwa, afungwa kwa pingu za shaba, na kukokotwa hadi Babiloni. (2 Wafalme 25:2-7) Hayo ni matokeo yenye msiba kama nini kwa ukosefu wake wa uaminifu!
Kufadhaika kwa Sababu ya Maafa
8. (a) Isaya aitikiaje unabii unaotabiri msiba kwa Yerusalemu? (b) Hali itakuwaje ndani ya Yerusalemu?
8 Unabii huo wamhuzunisha sana Isaya. Asema hivi: “Geuza uso wako usinitazame, nipate kulia kwa uchungu; usijishughulishe kunifariji, kwa ajili ya kuharibika kwake binti ya watu wangu.” (Isaya 22:4) Isaya alihuzunika kwa sababu ya mambo yaliyotabiriwa kwamba yangekumba Moabu na Babiloni. (Isaya 16:11; 21:3) Sasa afadhaika na kuomboleza hata zaidi anapofikiria msiba unaokuja juu ya watu wake mwenyewe. Hafarijiki. Kwa nini? “Kwa maana siku ya kutaabika, siku ya kukanyagwa, siku ya fujo inakuja, itokayo kwa Bwana, BWANA wa majeshi, katika bonde la Maono; inabomoa kuta; na kuililia milima.” (Isaya 22:5) Yerusalemu itajaa fujo tele. Watu watazurura huku na huku kwa hofu kubwa, bila kusudi. Adui aanzapo kupenya kuta za jiji, kutakuwepo hali ya “kuililia milima.” Je, yamaanisha kwamba wakazi wa jiji watamlilia Mungu katika hekalu lake takatifu kwenye Mlima Moria? Labda. Hata hivyo, kwa kuzingatia ukosefu wao wa uaminifu, labda yamaanisha tu kwamba vilio vyao vya hofu vitasikika katika milima inayowazunguka.
9. Fafanua jeshi linalotisha Yerusalemu.
9 Ni adui wa aina gani anayetisha Yerusalemu? Isaya atuambia: “Elamu wameshika podo, pamoja na magari ya vita, na watu wenye kupanda farasi; na Kiri wameifunua ngao.” (Isaya 22:6) Adui wana silaha za kutosha. Wana wapiga-mishale ambao podo zao zimejaa mishale. Wapiganaji wanatayarisha ngao zao kwa ajili ya vita. Kuna magari ya vita na farasi waliozoezwa vita. Jeshi latia ndani wanajeshi kutoka Elamu, iliyo sehemu ya kaskazini ya Ghuba ya Uajemi ya sasa, na kutoka Kiri, labda iliyo karibu na Elamu. Kutajwa kwa nchi hizo kwaonyesha kwamba wavamizi hao watoka mbali sana. Pia wadokeza kuwa huenda wapiga-mishale Waelami walikuwa miongoni mwa jeshi linalotisha Yerusalemu katika siku ya Hezekia.
Majaribio ya Kujilinda
10. Ni matukio gani yanayotoa ishara ya mambo mabaya kwa jiji?
10 Isaya afafanua hali inayobadilika: “Ikawa mabonde yako mateule yamejaa magari ya vita, nao wapandao farasi wamejipanga wakielekea malango. Kisha alikiondoa kifuniko cha Yuda.” (Isaya 22:7, 8a) Magari na farasi zajaa kwenye nyanda nje ya jiji la Yerusalemu nazo zajiandaa kushambulia malango ya jiji. “Kifuniko cha Yuda” kinachoondolewa ni nini? Huenda ni lango fulani la jiji hilo, ambalo kutekwa kwake ni ishara ya mabaya kwa walinzi.c Kifuniko hicho chenye ulinzi kiondolewapo, jiji labaki wazi ili washambuliaji waingie.
11, 12. Wakazi wa Yerusalemu wachukua hatua zipi za kujilinda?
11 Isaya sasa akaza fikira kwenye majaribio ya watu ya kujilinda. Wanachofikiria kwanza ni silaha! “Nawe siku hiyo ulivitazama vyombo vya vita katika nyumba ya mwituni. Nanyi mlipaona mahali palipobomoka katika mji wa Daudi ya kuwa ni pengi, nanyi mliyakusanya maji ya birika la chini.” (Isaya 22:8b, 9) Silaha zimewekwa katika ghala ya silaha kwenye nyumba ya mwituni. Solomoni ndiye aliyeijenga ghala hiyo ya silaha. Kwa kuwa ilijengwa kwa mierezi kutoka Lebanoni, ilikuja kuitwa “nyumba ya mwitu wa Lebanoni.” (1 Wafalme 7:2-5) Mahali palipobomoka ukutani pachunguzwa. Maji yakusanywa—hatua muhimu ya kujilinda. Watu hao wanahitaji maji ili kuishi. Pasipo maji, jiji haliwezi kudumu. Hata hivyo, ona kwamba haitajwi popote kuwa wanamtegemea Yehova ili kupata ukombozi. Badala yake, wanazitegemea njia zao wenyewe. Na tusifanye kamwe kosa kama hilo!—Zaburi 127:1.
12 Je, mahali hapo palipobomoka kwenye ukuta wa jiji pashughulikiweje? “Nanyi mlizihesabu nyumba za Yerusalemu, mkazibomoa nyumba ili kuutia nguvu ukuta.” (Isaya 22:10) Nyumba zachunguzwa ili kuona zile ziwezazo kubomolewa kwa minajili ya kuandaa vifaa vya kurekebisha mahali palipobomoka. Hatua hiyo yanuiwa kuzuia adui asipate kuteka ukuta kikamili.
Watu Wasio na Imani
13. Watu wafanya jitihada gani ili kuhakikisha wanapata maji, lakini wanamsahau nani?
13 “Nanyi mlifanya birika la maji katikati ya kuta mbili, la kuwekea maji ya birika la kale; lakini hamkumwangalia yeye aliyeyafanya hayo, wala kumjali yeye aliyeyatengeneza zamani.” (Isaya 22:11) Jitihada za kukusanya maji, zinazofafanuliwa hapa na pia katika mstari wa 9, zatukumbusha juu ya hatua ambayo Mfalme Hezekia alichukua kulinda jiji dhidi ya Waashuri wenye kuvamia. (2 Mambo ya Nyakati 32:2-5) Hata hivyo, watu walio kwenye jiji katika unabii huu wa Isaya hawana imani hata kidogo. Wasongapo mbele kuimarisha ulinzi wa jiji, hawamfikirii Muumba hata kidogo, ijapokuwa Hezekia alimfikiria.
14. Licha ya ujumbe wa Yehova wenye onyo, watu wana mtazamo gani usio wa hekima?
14 Isaya aendelea: “Siku hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, akawaita watu walie na kuomboleza, na kung’oa nywele zao, na kuvaa nguo za magunia; na kumbe! furaha, na kuchekelea, na kuchinja ng’ombe, na kuchinja kondoo, na kula nyama, na kunywa mvinyo; tule, tunywe, kwa maana kesho tutakufa.” (Isaya 22:12, 13) Wakazi wa Yerusalemu hawajuti kamwe kwa sababu ya uasi wao dhidi ya Yehova. Hawalii, hawanyoi nywele zao, wala kuvaa nguo za magunia kama ishara ya toba. Iwapo wangekuwa wakifanya hivyo, yaelekea Yehova angewaokoa wasipatwe na matisho yanayokuja. Badala yake, wajiachilia wenyewe na kuingilia furaha yenye anasa. Mtazamo kama huo leo umo miongoni mwa watu wengi wasiomwamini Mungu. Kwa kuwa hawana tumaini lolote—ama la ufufuo wa wafu au la Paradiso ya wakati ujao—wao hufuatilia maisha ya kutimiza tamaa za kibinafsi, wakisema: “Acheni tule na tunywe, kwa maana kesho tutapaswa kufa.” (1 Wakorintho 15:32) Lo, hawafikirii mambo yajayo! Iwapo tu wangemtumaini Yehova, basi wangekuwa na tumaini lidumulo!—Zaburi 4:6-8; Mithali 1:33.
15. (a) Ujumbe wa hukumu ya Yehova dhidi ya Yerusalemu ni nini, na ni nani wanaoitekeleza hukumu yake? (b) Kwa nini Jumuiya ya Wakristo itakumbwa na msiba unaofanana na ule wa Yerusalemu?
15 Wakazi waliozingiwa wa Yerusalemu hawatapata usalama. Isaya asema: “Yeye BWANA [“Yehova,” “NW”] wa majeshi akafunua haya masikioni mwangu, Ni kweli, uovu huu hautatakaswa wala kuwatokeni hata mfe; asema Bwana, BWANA wa majeshi.” (Isaya 22:14) Kwa sababu ya ugumu wa moyo wa watu hao, hawatasamehewa. Kifo kitakuja pasipo shaka. Hayo ni hakika. Bwana Mwenye Enzi Kuu, Yehova wa majeshi, ameyasema hayo. Kwa utimizo wa maneno ya unabii ya Isaya, maafa yaja mara mbili juu ya Yerusalemu lenye kukosa uaminifu. Jiji laharibiwa na majeshi ya Babiloni na baadaye na yale ya Roma. Vivyo hivyo, maafa yataipata Jumuiya ya Wakristo isiyo na uaminifu, ambayo washiriki wake hudai kumwabudu Mungu lakini ambao hasa humkana kwa kazi zao. (Tito 1:16) Dhambi za Jumuiya ya Wakristo, pamoja na zile za dini nyingine za ulimwengu zinazokiuka njia zenye uadilifu za Mungu, “zimetungamana pamoja hadi mbinguni.” Kama yalivyokuwa makosa ya Yerusalemu lenye kuasi, makosa yao ni mengi mno yasiweze kufunikwa.—Ufunuo 18:5, 8, 21.
Msimamizi-Nyumba Mwenye Ubinafsi
16, 17. (a) Ni nani sasa anayepokea ujumbe wenye onyo kutoka kwa Yehova, na kwa nini? (b) Kwa sababu ya tamaa yake ya makuu, ni nini kitakachompata Shebna?
16 Nabii sasa aacha kuzungumzia watu wasio waaminifu na kuanza kuzungumzia mtu mmoja asiye mwaminifu. Isaya aandika: “Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Haya! enenda kwa huyu mtunza hazina [“msimamizi-nyumba,” “NW”], yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie, Unafanyaje hapa? nawe una nani hapa? hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali!”—Isaya 22:15, 16.
17 Shebna ni ‘msimamizi-nyumba aliye juu ya nyumba,’ labda nyumba ya Mfalme Hezekia. Kwa hiyo, ana wadhifa mkubwa, wa pili kutoka kwa mfalme. Atarajiwa kufanya mengi. (1 Wakorintho 4:2) Ingawa hivyo, badala ya kukazia uangalifu mambo ya taifa, Shebna afuatilia utukufu wake mwenyewe. Apanga kaburi lake la anasa—kama la mfalme—lichongwe juu katika jabali. Yehova, huku akiangalia hilo, ampulizia Isaya amwonye msimamizi-nyumba huyo asiye mwaminifu: “Tazama, BWANA atakutupa kwa nguvu, kama mtu mwenye nguvu; naam, atakuzonga-zonga. Hakika atakukunja na kukutupa kama mpira, mpaka nchi iliyo mbali; huko utakufa, na magari ya utukufu wako yatakuwa kuko huko, ewe uliye aibu ya nyumba ya bwana wako. Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo.” (Isaya 22:17-19) Kwa sababu ya ubinafsi wake, Shebna hatakuwa na kaburi katika Yerusalemu, hata lile la kawaida. Badala yake, atatupwa kama mpira, afe katika nchi ya mbali. Hapo pana onyo kwa wote waliokabidhiwa mamlaka miongoni mwa watu wa Mungu. Kutumia mamlaka vibaya kutasababisha kupoteza mamlaka hiyo na labda kufukuziwa mbali.
18. Ni nani atakayechukua mahali pa Shebna, na yamaanisha nini kwamba huyo atapokea mavazi rasmi ya Shebna na ufunguo wa nyumba ya Daudi?
18 Hata hivyo, Shebna ataondolewaje kwenye wadhifa wake? Yehova aeleza kupitia Isaya: “Itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia; nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda. Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua.” (Isaya 22:20-22) Eliakimu, atakayechukua mahali pa Shebna, atapewa mavazi rasmi ya msimamizi-nyumba huyo pamoja na ufunguo wa nyumba ya Daudi. Biblia hufananisha “ufunguo” na mamlaka, serikali, au uwezo. (Linganisha Mathayo 16:19.) Nyakati za kale, mshauri wa mfalme, aliyekabidhiwa funguo, angeweza kusimamia kwa jumla nyumba za mfalme, hata kutoa uamuzi juu ya wale wanaoteuliwa katika utumishi wa mfalme. (Linganisha Ufunuo 3:7, 8.) Basi, ofisi ya msimamizi-nyumba ni muhimu, na yeyote anayetumikia humo hutarajiwa kufanya mengi. (Luka 12:48) Huenda Shebna anastahili, lakini kwa kuwa yeye si mwaminifu, Yehova ataweka mwingine badala yake.
Misumari Miwili ya Mfano
19, 20. (a) Eliakimu atathibitikaje kuwa baraka kwa watu wake? (b) Ni nini kitakachowapata wale wanaoendelea kumtegemea Shebna?
19 Hatimaye, Yehova atumia mfano kueleza kuhamishwa kwa mamlaka kutoka kwa Shebna hadi kwa Eliakimu. Ataarifu hivi: “Nitamkaza [Eliakimu] kama msumari mahali palipo imara; naye atakuwa kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake. Nao wataangika juu yake utukufu wote wa nyumba ya baba yake; wazao wake na watoto wao, kila chombo kidogo tangu vyombo vya vikombe hata vyombo vya makopo vyote pia. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, ule msumari [Shebna] uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana BWANA amesema haya.”—Isaya 22:23-25.
20 Katika mistari hiyo msumari wa kwanza ni Eliakimu. Atakuwa “kiti cha utukufu” kwa nyumba ya baba yake, Hilkia. Tofauti na Shebna, hataiaibisha nyumba ya baba yake wala sifa yake. Eliakimu atakuwa tegemeo lenye kudumu kwa vyombo vya nyumbani, yaani, kwa wengine walio katika utumishi wa mfalme. (2 Timotheo 2:20, 21) Kinyume chake, msumari wa pili wamrejezea Shebna. Ingawa huenda akaonekana kuwa imara, ataondolewa. Yeyote anayeendelea kumtegemea ataanguka.
21. Nyakati za kisasa, ni nani, kama Shebna, ambaye mahali pake palichukuliwa, kwa nini palichukuliwa, na ni nani aliyepachukua?
21 Mambo yaliyompata Shebna yatukumbusha kwamba miongoni mwa wale wanaodai kumwabudu Mungu, wale wanaokubali mapendeleo ya utumishi wapaswa kuyatumia kwa minajili ya kutumikia wengine na kumletea Yehova sifa. Hawapaswi kutumia vibaya cheo chao ili kujitajirisha au kupata umashuhuri wa kibinafsi. Kwa kielelezo, kwa muda mrefu Jumuiya ya Wakristo imejikweza yenyewe kuwa msimamizi-nyumba aliyeteuliwa, mwakilishi wa Yesu Kristo duniani. Hata hivyo, kama vile tu Shebna alivyomwaibisha baba yake kwa kutafuta utukufu wake mwenyewe, ndivyo viongozi wa Jumuiya ya Wakristo wamemletea Muumba aibu kwa kujikusanyia mali na mamlaka. Basi, wakati wa hukumu “kuanza na nyumba ya Mungu” ulipofika mwaka wa 1918, Yehova aliiondoa Jumuiya ya Wakristo. Msimamizi-nyumba mwingine aliteuliwa—“msimamizi-nyumba mwaminifu, mwenye busara”—na kuwekwa rasmi juu ya nyumba ya Yesu duniani. (1 Petro 4:17; Luka 12:42-44) Jamii hiyo yenye washiriki wengi imejithibitisha yenyewe kuwa yastahili kubeba “ufunguo” wa kifalme wa nyumba ya Daudi. Sawa na “msumari” unaotumainika, imethibitika kuwa muungaji mkono anayetegemeka kwa ajili ya “vyombo” vyote mbalimbali, Wakristo watiwa-mafuta walio na wajibu mbalimbali wanaoitegemea iwaruzuku kiroho. “Kondoo wengine” pia, kama ‘mgeni aliye katika malango’ ya Yerusalemu la kale, huutegemea “msumari” huo, Eliakimu wa leo.—Yohana 10:16; Kumbukumbu la Torati 5:14.
22. (a) Kwa nini kuchukuliwa kwa mahali pa Shebna akiwa msimamizi-nyumba kulikuwa kwa wakati unaofaa? (b) Katika nyakati za kisasa, kwa nini kuwekwa rasmi kwa “msimamizi-nyumba mwaminifu, mwenye busara,” kulikuwa kwa wakati unaofaa?
22 Eliakimu alichukua mahali pa Shebna wakati ambapo Senakeribu na majeshi yake walikuwa wakitisha Yerusalemu. Vivyo hivyo, “msimamizi-nyumba mwaminifu, mwenye busara,” amewekwa rasmi kutumikia wakati wa mwisho, ambao utafikia kikomo Shetani na majeshi yake wajapo kushambulia mara ya mwisho “Israeli wa Mungu” na waandamani wao wa kondoo wengine. (Wagalatia 6:16) Kama ilivyokuwa katika siku ya Hezekia, shambulio hilo litaishia kwenye kuharibiwa kwa adui za uadilifu. Wale wanaoegemea kwenye “msumari mahali palipo imara,” msimamizi-nyumba mwaminifu, wataokoka, kama vile tu wakazi waaminifu wa Yerusalemu walivyookoka uvamizi wa Ashuru dhidi ya Yuda. Ni busara kama nini, basi, kuepuka kushikilia “msumari” uliokataliwa wa Jumuiya ya Wakristo!
23. Ni nini kinachompata Shebna hatimaye, nasi twaweza kujifunza nini kutokana na hilo?
23 Ni nini kinachompata Shebna? Hatuna rekodi yoyote juu ya jinsi unabii unaomhusu, uliorekodiwa kwenye Isaya 22:18, ulivyotimizwa. Anapojiinua mwenyewe kisha kuaibishwa, afanana na Jumuiya ya Wakristo, lakini huenda alijifunza kutokana na nidhamu hiyo. Kwa habari hiyo, yeye ni tofauti sana na Jumuiya ya Wakristo. Rabshake wa Ashuru anapotaka wakazi wa Yerusalemu wasalimu amri, msimamizi-nyumba mpya wa Hezekia, Eliakimu, aongoza wajumbe wanaoenda kumlaki. Hata hivyo, Shebna yupo pamoja naye akiwa mwandishi wa mfalme. Yaonekana kwamba Shebna angali katika utumishi wa mfalme. (Isaya 36:2, 22, kielezi-chini) Hilo ni fundisho jema kama nini kwa wale wanaopoteza nyadhifa zao za utumishi katika tengenezo la Mungu! Badala ya kusikia uchungu na kuudhika, ni jambo la hekima waendelee kumtumikia Yehova katika fursa yoyote ile anayoruhusu. (Waebrania 12:6) Kwa kufanya hivyo, wataepuka msiba utakaoikumba Jumuiya ya Wakristo. Watafurahia milele upendeleo na baraka za Mungu.
[Maelezo ya Chini]
a Mwaka wa 66 W.K., Wayahudi wengi walifurahi majeshi ya Roma yaliyokuwa yakizingira Yerusalemu yalipoondoka.
b Kwa mujibu wa mwanahistoria wa karne ya kwanza, Josephus, kulikuwepo njaa kali sana huko Yerusalemu mwaka wa 70 W.K. hivi kwamba watu wakala ngozi, nyasi, na nyasi kavu. Katika kisa kimoja kilichoripotiwa, mama mmoja alimchoma na kumla mwana wake.
c Au, huenda usemi “kifuniko cha Yuda” warejezea kitu kingine tofauti kinacholinda jiji, kama vile ngome ambazo ni hifadhi za silaha na makao ya wanajeshi.
[Picha katika ukurasa wa 231]
Zedekia anapotoroka, akamatwa na kupofushwa
[Picha katika ukurasa wa 232, 233]
Wayahudi waliokwama jijini Yerusalemu wana matazamio yenye kuhofisha
[Picha katika ukurasa wa 239]
Hezekia amfanya Eliakimu kuwa “msumari mahali palipo imara”
[Picha katika ukurasa wa 241]
Kama Shebna, viongozi wengi wa Jumuiya ya Wakristo wamemletea Muumba aibu kwa kukusanya mali
[Picha katika ukurasa wa 242]
Leo jamii ya msimamizi-nyumba mwaminifu imewekwa rasmi juu ya nyumba ya Yesu