Sura ya 22
Isaya Atabiri ‘Tendo la Ajabu’ la Yehova
1, 2. Kwa nini Israeli na Yuda zahisi ziko salama?
ISRAELI na Yuda zahisi kwa kitambo kidogo kwamba ziko salama. Viongozi wao wameanzisha miungano ya kisiasa na mataifa makubwa zaidi na yenye nguvu, katika jitihada ya kupata usalama katika ulimwengu hatari. Samaria, jiji kuu la Israeli, limegeukia Siria iliyo karibu, ilhali Yerusalemu, jiji kuu la Yuda, limetumainia Ashuru yenye ukatili.
2 Mbali na kuwatumainia washirika wao wapya wa kisiasa, baadhi ya watu katika ufalme wa kaskazini huenda wakamtazamia Yehova awalinde—licha ya kwamba wanaendelea kuabudu ndama za dhahabu. Vivyo hivyo, Yuda inasadiki kwamba Yehova atailinda. Kwani, hekalu la Yehova haliko Yerusalemu, jiji lao kuu? Ijapokuwa hivyo, kuna matukio yasiyotarajiwa yatakayoyapata mataifa hayo mawili. Yehova ampulizia Isaya kutabiri matukio yatakayoonekana kuwa ya ajabu kwelikweli kwa watu wake waliopotoka. Maneno yake pia yana mafundisho muhimu kwa kila mtu leo.
“Walevi wa Efraimu”
3, 4. Ufalme wa kaskazini wa Israeli wajivunia nini?
3 Isaya aanza unabii wake kwa maneno yenye kushangaza: “Ole wa taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu, na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, la hao walioshindwa na divai! Tazama, BWANA ana mmoja aliye hodari, mwenye nguvu; kama dhoruba ya mvua ya mawe, . . . ndivyo atakavyotupa chini kwa mkono. Taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu itakanyagwa kwa miguu.”—Isaya 28:1-3.
4 Kabila la Efraimu, ambalo ndilo mashuhuri zaidi kati ya makabila kumi ya kaskazini, lawakilisha ufalme wote wa Israeli. Samaria, jiji lake kuu, liko “kichwani mwa bonde linalositawi,” mahali pazuri penye umashuhuri. Viongozi wa Efraimu wanajivunia ‘taji yao ya kiburi’ ya kuwa huru kutokana na wafalme wa nasaba ya Daudi huko Yerusalemu. Lakini wao ni “walevi,” ulevi wa kiroho kwa sababu ya ushirikiano wao na Siria dhidi ya Yuda. Kila kitu wakipendacho chakaribia kukanyagwa chini ya miguu ya wavamizi.—Linganisha Isaya 29:9.
5. Israeli imo katika hatari gani, lakini Isaya atoa tumaini gani?
5 Efraimu haitambui kuwa imo hatarini. Isaya aendelea: “Ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, litakuwa kama tini iliyotangulia kuiva kabla ya wakati wa hari, ambayo, aionapo yeye aiangaliaye, huila mara anapoishika mkononi mwake.” (Isaya 28:4) Efraimu itaanguka mkononi mwa Ashuru, kama tonge tamu linaloliwa mara moja. Basi, je, hilo lamaanisha kwamba hakuna tumaini lolote? Kama ilivyo mara nyingi, unabii mbalimbali wa hukumu wa Isaya hutia ndani tumaini. Taifa hilo lijapoanguka, watu mmoja-mmoja walio waaminifu wataokoka kwa msaada wa Yehova. “BWANA [“Yehova,” “NW”] wa majeshi atakuwa ni taji ya fahari, na kilemba cha uzuri, kwa mabaki ya watu wake. Naye atakuwa roho ya hukumu kwake yeye aketiye ili ahukumu; naye atakuwa nguvu kwao wageuzao nyuma vita langoni.”—Isaya 28:5, 6.
“Wamekosa”
6. Israeli yaangamizwa lini, lakini kwa nini haipasi Yuda ifurahi?
6 Siku ya kulipiza kisasi juu ya Samaria yafika mwaka wa 740 K.W.K., Waashuri waiharibupo nchi na ufalme wa kaskazini ukomeshwapo ukiwa taifa huru. Na Yuda je? Nchi yake itavamiwa na Ashuru, na baadaye Babiloni itaharibu jiji lake kuu. Lakini katika wakati wa maisha ya Isaya, hekalu na ukuhani wa Yuda zitaendelea kutenda na manabii wake wataendelea kutoa unabii. Je, Yuda ifurahie maangamizi yanayokuja juu ya jirani yake wa kaskazini? La hasha! Yuda na viongozi wake watawajibika mbele za Yehova kwa sababu ya kutotii kwao na kukosa imani.
7. Viongozi wa Yuda wamelewaje, na matokeo ni nini?
7 Akielekeza ujumbe wake kwa Yuda, Isaya aendelea: “Lakini hawa nao wamekosa kwa divai, wamepotea kwa kileo; kuhani na nabii wamekosa kwa kileo, wamemezwa kwa divai, wamepotea kwa kileo; hukosa katika maono, hujikwaa katika hukumu. Maana meza zote zimejaa matapiko na uchafu, hapana mahali palipo safi.” (Isaya 28:7, 8) Yachukiza kama nini! Ulevi halisi nyumbani mwa Mungu ni mbaya sana. Lakini makuhani na manabii hao wamelewa kiroho—akili zao zimepumbazwa kwa kuitumaini mno miungano ya kibinadamu. Wamejidanganya kwa kufikiri kwamba mwendo wao ndio mwendo pekee unaofaa, labda wakiamini kwamba sasa wana mpango mwingine iwapo ulinzi wa Yehova wakosa kutosha. Katika hali yao ya ulevi wa kiroho, viongozi hao wa kidini waropoka usemi wenye kuchukiza na mchafu, unaoonyesha ukosefu mbaya wa imani ya kweli katika ahadi za Mungu.
8. Ujumbe wa Isaya wapokewaje?
8 Viongozi wa Yuda waitikiaje onyo la Yehova? Wamdhihaki Isaya, wakimshutumu kwamba anasema nao kama watoto: “Atamfundisha nani maarifa? atamfahamisha nani habari hii? Je! ni wale walioachishwa maziwa, walioondolewa matitini? Kwa maana ni amri juu ya amri, amri juu ya amri; kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; huku kidogo na huku kidogo.” (Isaya 28:9, 10) Kwa maoni yao, Isaya arudia-rudia mambo kiajabu! Ayarudia-rudia maneno yake mwenyewe, akisema: ‘Yehova ameamuru hivi! Yehova ameamuru hivi! Hii ndiyo kanuni ya Yehova! Hii ndiyo kanuni ya Yehova!’a Lakini karibuni Yehova “atasema” na wakazi wa Yuda kupitia tendo fulani. Atatuma majeshi ya Babiloni dhidi yao—wageni ambao kwa kweli wanasema lugha nyingine. Pasipo shaka, majeshi hayo yatatekeleza “amri juu ya amri,” za Yehova, na Yuda itaanguka.—Soma Isaya 28:11-13.
Walevi wa Kiroho Leo
9, 10. Maneno ya Isaya yamepata kuwa na maana kwa vizazi vya baadaye lini, na jinsi gani?
9 Je, unabii mbalimbali wa Isaya ulitimizwa juu ya Israeli na Yuda za kale pekee? Hata kidogo! Yesu na Paulo waliyanukuu maneno yake na kuyahusianisha na taifa la wakati wao. (Isaya 29:10, 13; Mathayo 15:8, 9; Waroma 11:8) Hali kadhalika, leo hali fulani inayofanana na ile ya siku ya Isaya imezuka.
10 Wakati huu, viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo ndio wanaotumaini siasa. Wao huyumba-yumba huku na huku, kama walevi wa Israeli na Yuda, wakijiingiza katika masuala ya kisiasa, wakifurahia kuombwa mashauri na wale waitwao eti wakuu katika ulimwengu huu. Badala ya kusema kweli safi ya Biblia, wao husema uchafu. Mwono wao wa kiroho umefifia, nao sio viongozi salama wa wanadamu.—Mathayo 15:14.
11. Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo huitikiaje habari njema ya Ufalme wa Mungu?
11 Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo hutendaje Mashahidi wa Yehova wanapowaonyesha tumaini pekee la kweli, yaani, Ufalme wa Mungu? Hawaelewi. Wanaona kwamba Mashahidi wanaropoka kwa kurudia-rudia, kama watoto. Viongozi wa kidini huwadharau wajumbe hao na kuwadhihaki. Sawa na Wayahudi wa siku ya Yesu, hawautaki Ufalme wa Mungu wala hawataki wafuasi wao waelezwe kuuhusu. (Mathayo 23:13) Kwa hiyo, wanaonywa kuwa Yehova hatasema nao daima kupitia wajumbe wake wapole. Wakati utafika ambapo wale wasiotaka kujitiisha kwa Ufalme wa Mungu ‘watavunjwa, na kunaswa, na kuchukuliwa,’ naam, waangamizwe kabisa.
“Agano na Mauti”
12. Ni nini kinachodaiwa kuwa “agano na mauti” la Yuda?
12 Isaya aendelea na tangazo lake: “Mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo ya kweli.” (Isaya 28:14, 15) Viongozi wa Yuda wajigamba wakisema kuwa miungano yao ya kisiasa inawalinda wasishindwe. Wanaona kwamba wamefanya “agano na mauti” ili isiwaguse. Lakini kimbilio lao la uwongo halitawalinda. Miungano yao ni uwongo, si ya kweli. Vivyo hivyo leo, uhusiano wa karibu wa Jumuiya ya Wakristo na viongozi wa ulimwengu hautailinda wakati ufikapo Yehova aihukumu. Kwa kweli, uhusiano huo ndio utakaosababisha maangamizi yake.—Ufunuo 17:16, 17.
13. Ni nani aliye “jiwe lililojaribiwa,” na Jumuiya ya Wakristo imemkataaje?
13 Basi, viongozi hao wa kidini wapaswa kuwa wakitazama wapi? Isaya sasa arekodi ahadi ya Yehova: “Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka. Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri.” (Isaya 28:16, 17) Muda mfupi baada ya Isaya kuyasema maneno hayo, Mfalme Hezekia mwaminifu atawazwa huko Sayuni, na ufalme wake waokolewa, si kupitia kwa washirika jirani, bali kupitia kwa Yehova kuingilia kati. Hata hivyo, Hezekia siye anayeyatimiza maneno hayo yaliyopuliziwa. Mtume Petro, akinukuu maneno ya Isaya, alionyesha kuwa Yesu Kristo, mzao wa baadaye sana wa Hezekia, ndiye “jiwe lililojaribiwa” na yeyote anayedhihirisha imani katika Yeye hapaswi kuogopa kamwe. (1 Petro 2:6) Yachukiza sana kwa sababu viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, wajapojiita Wakristo, wamefanya mambo ambayo Yesu alikataa kufanya! Wametafuta umashuhuri na mamlaka katika ulimwengu huu badala ya kumngojea Yehova alete Ufalme wake chini ya Yesu Kristo aliye Mfalme.—Mathayo 4:8-10.
14. “Agano na mauti” la Yuda litabatilishwa lini?
14 “Pigo lifurikalo” la majeshi ya Babiloni lipitapo nchini humo, Yehova atalifunua kimbilio la kisiasa la Yuda kuwa ni uwongo. “Agano lenu mliloagana na mauti litabatilika,” asema Yehova. “Pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo. Kila wakati litakapopita . . . kuifahamu habari ile kutakuwa kitisho tu.” (Isaya 28:18, 19) Naam, kuna fundisho kubwa tuwezalo kupata kutokana na mambo yanayowakumba watu wanaodai kumtumikia Yehova lakini badala yake wanaweka matumaini yao katika miungano na mataifa.
15. Isaya atoaje kielezi cha kutofaa kwa ulinzi wa Yuda?
15 Fikiria hali wanamojikuta sasa viongozi hao wa Yuda. “Kitanda kile ni kifupi asiweze mtu kujinyosha juu yake, na nguo ile ya kujifunika ni nyembamba asipate mtu kujizingisha.” (Isaya 28:20) Ni kana kwamba walala chini wapate pumziko, ila hilo ni bure tu. Miguu yao yabaki nje kwenye baridi, au waikunja miguu yao na nguo ya kujifunika ni nyembamba mno isiweze kuwafunika wapate joto. Hali ilikuwa isiyostarehesha jinsi hiyo katika siku ya Isaya. Na hali iko hivyo leo kwa mtu yeyote anayeweka tumaini lake katika kimbilio la uwongo la Jumuiya ya Wakristo. Yachukiza kama nini kwamba kwa sababu ya kujiingiza katika siasa, viongozi fulani wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wamehusika katika ukatili kama vile mauaji ya kikabila na mauaji ya jumla!
‘Tendo la Ajabu’ la Yehova
16. ‘Tendo la ajabu’ la Yehova ni nini, na kwa nini kazi hiyo ni ya ajabu?
16 Hali ya mwisho ya mambo itakuwa kinyume kabisa cha matumaini ya viongozi wa kidini wa Yuda. Yehova atawafanyia walevi wa kiroho wa Yuda jambo la ajabu. “BWANA ataondoka kama vile katika mlima Perasimu, ataghadhibika kama vile katika bonde la Gibeoni; apate kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu; na kulitimiza tendo lake, tendo lake la ajabu.” (Isaya 28:21) Katika siku za Mfalme Daudi, Yehova aliwapa watu wake ushindi mkubwa juu ya Wafilisti katika Mlima Perasimu na katika bonde la Gibeoni. (1 Mambo ya Nyakati 14:10-16) Katika siku za Yoshua, hata alifanya jua lisimame tuli juu ya Gibeoni ili ushindi wa Israeli juu ya Waamori ukamilike. (Yoshua 10:8-14) Hiyo ilikuwa ajabu! Sasa Yehova atapigana tena, lakini mara hii dhidi ya wale wanaodai kuwa watu wake. Je, kwaweza kuwapo ajabu nyingine kuliko hiyo? Haiwezekani, uzingatiapo uhakika wa kwamba Yerusalemu ndicho kituo cha ibada ya Yehova na jiji la mfalme wa Yehova aliyetiwa mafuta. Kufikia sasa, nyumba ya kifalme ya Daudi huko Yerusalemu haijawahi kupinduliwa kamwe. Ijapokuwa hivyo, pasipo shaka Yehova atatekeleza “tendo lake la ajabu.”—Linganisha Habakuki 1:5-7.
17. Kuonyesha dharau kutakuwa na matokeo gani kwa utimizo wa unabii wa Isaya?
17 Basi, Isaya atahadharisha: “Msiwe watu wenye kudharau, vifungo vyenu msije vikakazwa; maana nimesikia kwa Bwana, BWANA wa majeshi, habari ya hukumu itakayotimizwa, nayo imekusudiwa, itakayoipata dunia yote pia.” (Isaya 28:22) Ingawa viongozi hao waonyesha dharau, ujumbe wa Isaya ni wa kweli. Ameusikia kutoka kwa Yehova, ambaye viongozi hao wana uhusiano wa agano pamoja naye. Hali kadhalika leo, viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo huonyesha dharau wasikiapo ‘tendo la ajabu’ la Yehova. Wao hata hujigamba na kusema kwa hasira. Lakini ujumbe ambao Mashahidi wa Yehova hutangaza ni wa kweli. Umo katika Biblia, kitabu ambacho viongozi hao hudai kukiwakilisha.
18. Isaya atoaje kielezi cha usawaziko wa Yehova atoapo nidhamu?
18 Lakini Yehova atawarekebisha upya na kuwarudishia upendeleo wake watu wanyofu wasiofuata viongozi hao. (Soma Isaya 28:23-29.) Sawa na mkulima atumiaye mbinu za uangalifu ili kupura nafaka iliyo laini zaidi, kama vile kunde, vivyo hivyo Yehova huibadili nidhamu yake kulingana na mtu mmoja-mmoja na hali zake. Yeye hapiti kiasi au kuonea kamwe bali hutenda akiwa na kusudi la kuwarekebisha wakosaji. Naam, iwapo watu mmoja-mmoja wakubali sihi za Yehova, basi kuna tumaini. Vivyo hivyo leo, ingawa kwa jumla hatima ya Jumuiya ya Wakristo imetiwa muhuri, mtu yeyote anayejitiisha kwa Ufalme wa Yehova aweza kuepuka hukumu kali inayokuja.
Ole wa Yerusalemu!
19. Yerusalemu litakuwaje “meko ya madhabahu,” na jambo hilo latukia lini, na jinsi gani?
19 Ingawa hivyo, Yehova sasa asema juu ya nini? “Ole wa Arieli, Arieli, mji ambao Daudi alifanya kituo chake ndani yake; ongezeni mwaka baada ya mwaka; sikukuu na zirudi wakati wake, ndipo nitamwudhi Arieli; kutakuwapo maombolezo na kilio; naye atakuwa kwangu kama Arieli.” (Isaya 29:1, 2) Huenda neno “Arieli” lamaanisha “Meko ya Madhabahu ya Mungu,” na yaonekana hapa neno hilo larejezea Yerusalemu. Huko ndiko liliko hekalu na madhabahu yake ya dhabibu. Wayahudi wana desturi ya kufanyia misherehekeo na kutolea dhabihu hapo, lakini Yehova haifurahii ibada yao. (Hosea 6:6) Badala yake, atoa agizo kwamba jiji lenyewe litakuwa “meko ya madhabahu” kwa maana tofauti. Kama vile madhabahu, jiji hilo litafurika damu na kuchomwa moto. Yehova hata aeleza jinsi hilo litakavyotendeka: “Nami nitapiga kimo juu yako pande zote, nitakuhusuru kwa ngome, nami nitajenga maboma yakuzunguke. Nawe utashushwa, nawe utanena toka chini ya nchi, na maneno yako yatakuwa chini toka mavumbini.” (Isaya 29:3, 4) Hayo yatimizwa juu ya Yuda na Yerusalemu mwaka wa 607 K.W.K., majeshi ya Babiloni yazingiapo na kuliharibu jiji na kulichoma hekalu. Yerusalemu lashushwa chini kabisa kwenye ardhi ambako lilijengwa.
20. Mwisho kamili wa adui za Mungu utakuwa nini?
20 Kabla ya wakati huo wenye maafa, mara kwa mara Yuda yapata mfalme anayetii Sheria ya Yehova. Kisha nini? Yehova awapigania watu wake. Hata adui wakiifunika nchi, wapata kuwa kama “mavumbi membamba” na “makapi.” Kwa wakati wake ufaao, Yehova awatawanya “kwa ngurumo, na tetemeko la nchi, na sauti kuu, na chamchela, na tufani, na mwali wa moto uteketezao.”—Isaya 29:5, 6.
21. Fafanua kielezi kwenye Isaya 29:7, 8.
21 Huenda majeshi ya adui yakatazamia kwa hamu kupora Yerusalemu na kujishibisha kwa nyara za vita. Lakini ole wao, watashtuka! Kama vile mtu mwenye njaa aotapo kwamba anakula lakini aamkapo, kumbe, ana njaa kama kawaida, vivyo hivyo adui za Yuda hawatafurahia mlo wanaotazamia kwa hamu. (Soma Isaya 29:7, 8.) Fikiria mambo yanayolikumba jeshi la Ashuru chini ya uongozi wa Senakeribu litishapo Yerusalemu katika siku ya Mfalme Hezekia mwaminifu. (Isaya, sura ya 36 na 37) Katika usiku mmoja, pasipo kuinuliwa hata mkono mmoja wa kibinadamu, jeshi la Ashuru larudishwa nyuma—wapiganaji wake wapatao 185,000 wamekufa! Matumaini ya ushindi yatazimwa tena wakati jeshi la Gogu wa Magogu lijitayarishapo kushambulia watu wa Yehova hivi karibuni.—Ezekieli 38:10-12; 39:6, 7.
22. Ulevi wa kiroho wa Yuda waiathirije?
22 Wakati Isaya atoapo sehemu hiyo ya unabii wake, viongozi wa Yuda hawana imani kama ya Hezekia. Wamelewa chakari kiroho kupitia miungano yao na mataifa yasiyomwogopa Mungu. “Ngojeni mstaajabu; fanyeni anasa zenu na kuwa vipofu; wamelewa wala si kwa mvinyo; wamewaya-waya wala si kwa sababu ya kileo.” (Isaya 29:9) Huku wakiwa wamelewa kiroho, viongozi hawa hawana uwezo wa kutambua maana ya maono aliyopewa nabii wa kweli wa Yehova. Isaya ataarifu: “BWANA amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu, yaani, waonaji. Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya chuo kilichotiwa muhuri, ambacho watu humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri; kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi.”—Isaya 29:10-12.
23. Kwa nini Yehova ataihukumu Yuda, naye atafanyaje hivyo?
23 Viongozi wa kidini wa Yuda wadai wana busara ya kiroho, lakini wamemwacha Yehova. Badala yake wanafundisha mawazo yao wenyewe yaliyopotoka juu ya jema na baya, wakitetea matendo yao yasiyo ya imani na yenye upotovu wa maadili na uongozi wao unaowanyima watu upendeleo wa Mungu. Kwa kutumia “kazi ya ajabu”—‘tendo lake la ajabu’—Yehova atawahukumu kwa sababu ya unafiki wao. Yeye asema: “Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa; kwa sababu hiyo mimi nitafanya tena kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na mwujiza; na akili za watu wao wenye akili zitapotea, na ufahamu wa wenye busara wao utafichwa.” (Isaya 29:13, 14) Hekima na uelewevu wa kujigamba wa Yuda vitatoweka Yehova atakapoongoza mambo ili Serikali ya Ulimwengu ya Babiloni iufagilie mbali mfumo wake wote wa kidini ulioasi. Jambo hilohilo lilitendeka katika karne ya kwanza baada ya viongozi wa Wayahudi, waliojidai kuwa na hekima, kupotosha taifa hilo. Jambo kama hilo litatendeka leo kwa Jumuiya ya Wakristo.—Mathayo 15:8, 9; Waroma 11:8.
24. Wayudea waonyeshaje kwamba hawamwogopi Mungu?
24 Kwa sasa, hata hivyo, viongozi wenye majigambo wa Yuda waamini kuwa ni wajanja sana hivi kwamba wataepuka adhabu ya kupotoa ibada safi. Je, watafaulu? Isaya afunua ficho lao, akiwafichua kuwa watu wasiomwogopa Mungu kikweli na hivyo basi hawana hekima ya kweli: “Ole wao wanaojitahidi kumficha BWANA mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? nani atujuaye? Ninyi mnapindua mambo; Je! mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?” (Isaya 29:15, 16; linganisha Zaburi 111:10.) Haidhuru wanadhani wamejificha kadiri gani, wao wasimama ‘uchi na wakiwa wamefunuliwa wazi’ machoni pa Mungu.—Waebrania 4:13.
“Viziwi Watasikia”
25. “Viziwi” watasikiaje?
25 Ijapokuwa hivyo, kuna wokovu kwa watu mmoja-mmoja wanaodhihirisha imani. (Soma Isaya 29:17-24; linganisha Luka 7:22.) “Viziwi watasikia maneno ya hicho chuo,” ujumbe ulio katika Neno la Mungu. Naam, huo si uponyaji wa uziwi wa kimwili. Ni uponyaji wa kiroho. Mara nyingine tena Isaya aelekeza mbele kwenye kuanzishwa kwa Ufalme wa Kimesiya na kurudishwa kwa ibada safi duniani kupitia utawala wa Mesiya. Jambo hilo limetukia siku zetu, na mamilioni ya watu wenye mioyo minyofu wanakubali kusahihishwa na Yehova nao wanajifunza kumsifu. Utimizo huo wasisimua kama nini! Hatimaye, siku itafika ambapo kila mtu, kila mwenye kupumua, atamsifu Yehova na kulitukuza jina lake takatifu.—Zaburi 150:6.
26. “Viziwi” leo husikia vikumbusha gani vya kiroho?
26 “Viziwi” hao wanaosikia Neno la Mungu leo hujifunza nini? Wanajifunza kuwa Wakristo wote, hasa wale ambao kutaniko linawaiga wakiwa vielelezo, lazima wajitahidi sana ‘wasikose kwa kileo.’ (Isaya 28:7) Na zaidi, tusichoke kamwe kuvisikia vikumbusha vya Mungu, vinavyotusaidia kuwa na mtazamo wa kiroho kwa mambo yote. Ingawa kwa kufaa Wakristo hujitiisha kwa mamlaka za kiserikali na kuzitegemea ziwaandalie huduma fulani, wokovu huja kutoka kwa Yehova Mungu, wala sio kwa ulimwengu. Pia, hatupaswi kusahau kamwe kwamba, kama vile ilivyokuwa hukumu dhidi ya Yerusalemu lenye kuasi, hukumu ya Mungu dhidi ya kizazi hiki haiepukiki. Kwa msaada wa Yehova, twaweza kuendelea kutangaza onyo lake licha ya upinzani, kama Isaya alivyofanya.—Isaya 28:14, 22; Mathayo 24:34; Waroma 13:1-4.
27. Wakristo waweza kujifunza nini kutokana na unabii wa Isaya?
27 Wazee na wazazi waweza kujifunza kutokana na jinsi Yehova atoavyo nidhamu, sikuzote wakitafuta kuwarejesha wakosaji kwenye upendeleo wa Mungu, wala sio kuwaadhibu tu. (Isaya 28:26-29; linganisha Yeremia 30:11.) Nasi sote, pamoja na vijana, twakumbushwa umuhimu wa kumtumikia Yehova kutoka moyoni, pasipo kujifanya Wakristo ili kuwapendeza wanadamu. (Isaya 29:13) Ni lazima tuonyeshe kwamba, tofauti na wakazi wa Yuda wasio na imani, sisi tuna hofu ifaayo na staha yenye kina kwa Yehova. (Isaya 29:16) Isitoshe, twahitaji kuonyesha kuwa tuna nia ya kusahihishwa na kufunzwa na Yehova.—Isaya 29:24.
28. Watumishi wa Yehova huyaonaje matendo yake ya kuokoa?
28 Basi ni muhimu kama nini kuwa na imani na kumtumaini Yehova na njia yake ya kufanya mambo! (Linganisha Zaburi 146:3.) Kwa maoni ya watu wengi, ujumbe wenye onyo tunaohubiri utaonekana kuwa wa kitoto. Wazo la kutazamia kuharibiwa kwa tengenezo la Jumuiya ya Wakristo, linalodai kumtumikia Mungu, ni la ajabu. Lakini Yehova atatekeleza ‘tendo lake la ajabu.’ Hapana shaka yoyote kuhusu hilo. Kwa hiyo, kwa muda wote wa siku za mwisho za mfumo huu wa mambo, watumishi wa Mungu huutumaini kikamili Ufalme wake na Mfalme aliyewekwa rasmi, Yesu Kristo. Wanajua kwamba matendo ya Yehova ya kuokoa—yatakayofanywa pamoja na ‘kazi yake ya ajabu’—yataleta baraka za milele kwa wanadamu wote watiifu.
[Maelezo ya Chini]
a Katika Kiebrania cha awali, Isaya 28:10 ni shairi linalorudiwa-rudiwa, kama vile shairi la kusimulia watoto hadithi. Basi, viongozi wa kidini waliuona ujumbe wa Isaya kuwa wenye kurudiwa-rudiwa na wa kitoto.
[Picha katika ukurasa wa 289]
Jumuiya ya Wakristo imetegemea miungano na watawala wa kibinadamu badala ya kumtegemea Mungu
[Picha katika ukurasa wa 290]
Yehova atekeleza “tendo lake la ajabu” anaporuhusu Babiloni iharibu Yerusalemu
[Picha katika ukurasa wa 298]
Wale waliokuwa viziwi kiroho hapo awali waweza ‘kulisikia’ Neno la Mungu