Sura ya 27
Yehova Aghadhibikia Mataifa
1, 2. (a) Twaweza kuwa na uhakika gani kuhusiana na kisasi cha Yehova? (b) Mungu hutimiza nini kwa kulipa kisasi?
YEHOVA MUNGU ni mwenye subira, si kwa watumishi wake waaminifu peke yao tu bali pia kwa adui zake, ikiwa hilo lapatana na kusudi lake. (1 Petro 3:19, 20; 2 Petro 3:15) Huenda adui za Yehova wasitambue subira yake na huenda wakaiona kuwa udhaifu au kutotaka kutenda. Lakini, kama sura ya 34 ya Isaya inavyoonyesha, hatimaye sikuzote Yehova huwataka adui zake watoe hesabu. (Sefania 3:8) Kwa muda fulani, Mungu aliruhusu Edomu na mataifa mengine yawapinge watu wake bila kizuizi. Ijapokuwa hivyo, Yehova alikuwa na wakati wake mwenyewe wa kulipa kisasi. (Kumbukumbu la Torati 32:35) Vivyo hivyo, katika wakati wake uliowekwa, Yehova atalipa kisasi watu wote wa ulimwengu mwovu wa sasa wanaokaidi enzi kuu yake.
2 Mungu analipa kisasi hasa ili kuonyesha enzi kuu yake na kulitukuza jina lake. (Zaburi 83:13-18) Kisasi chake pia huwatetea watumishi wake kuwa wawakilishi wake wa kweli na kuwakomboa kutoka hali zisizofaa. Zaidi ya hayo, kisasi cha Yehova hupatana na haki sikuzote.—Zaburi 58:10, 11.
Sikilizeni, Enyi Mataifa
3. Yehova kupitia Isaya ayaalika mataifa yafanye nini?
3 Kabla ya kukaza fikira juu ya kisasi dhidi ya Edomu, Yehova amtumia Isaya kualika mataifa yote: “Karibuni, enyi mataifa, mpate kusikia; sikilizeni, enyi kabila za watu; dunia na isikie, nacho kiijazacho, ulimwengu na vitu vyote viutokavyo.” (Isaya 34:1) Nabii ameyashutumu tena na tena mataifa yasiyomhofu Mungu. Sasa akaribia kukamilisha shutuma za Mungu dhidi yao. Je, maonyo hayo yana umuhimu wowote leo?
4. (a) Mataifa yanaitwa yafanye nini, kama ilivyoandikwa katika Isaya 34:1? (b) Je, hukumu ya Yehova kwa mataifa huthibitisha kuwa yeye ni Mungu mkatili? (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 363.)
4 Ndiyo. Mwenye Enzi Kuu wa ulimwengu wote mzima ana ugomvi na vikundi vyote vya mfumo huu wa mambo usiomhofu Mungu. Hiyo ndiyo sababu “kabila za watu” na “dunia” zaitwa ili kusikiliza ujumbe wa Biblia ambao Yehova amefanya utangazwe ulimwenguni kote. Akitumia maneno yanayofanana na yale ya Zaburi 24:1, Isaya asema kuwa dunia yote itajaa ujumbe huo—unabii ambao umetimizwa siku zetu, Mashahidi wa Yehova wahubiripo “hadi sehemu ya mbali zaidi sana ya dunia.” (Matendo 1:8) Hata hivyo, mataifa hayajasikiliza. Hayajachukua kwa uzito onyo juu ya uharibifu wao unaokuja. Bila shaka hayo hayatamzuia Yehova asitimize neno lake.
5, 6. (a) Sababu gani Mungu ayatoza mataifa hesabu? (b) ‘Milima itayeyushwaje kwa damu yao’?
5 Unabii huo sasa waeleza matarajio mabaya kwa mataifa yasiyomhofu Mungu—kinyume kabisa cha matumaini mema ya watu wa Mungu yanayoelezwa baadaye. (Isaya 35:1-10) Nabii ataarifu: “BWANA ana ghadhabu juu ya mataifa yote, na hasira kali juu ya jeshi lao lote; amewaangamiza kabisa, amewatoa waende kuchinjwa. Watu wao waliouawa watatupwa nje, na uvundo wa maiti zao utapaa juu, na milima itayeyushwa kwa damu yao.”—Isaya 34:2, 3.
6 Fikira zakazwa kwenye hatia ya damu ya mataifa. Leo mataifa ya Jumuiya ya Wakristo yana hatia kubwa ya damu kushinda mengine yote. Yamejaza damu ya binadamu duniani kupitia vita viwili vya ulimwengu na vita vingine vidogo-vidogo vingi. Ni nani anayestahili kudai haki kwa sababu ya hatia hiyo yote ya damu? Si mwingine ila Muumba, Mpaji-Uhai mkuu. (Zaburi 36:9) Sheria ya Yehova imeweka kiwango: “Utatoza uhai kwa uhai.” (Kutoka 21:23-25; Mwanzo 9:4-6) Kupatana na sheria hiyo, yeye atasababisha damu ya mataifa imwagike—hadi wafe. Hewa itajaa uvundo wa maiti zao ambazo hazikuzikwa—kifo cha aibu kwelikweli! (Yeremia 25:33) Itakuwa kana kwamba milima inayeyuka kwa sababu ya wingi wa damu inayodaiwa. (Sefania 1:17) Majeshi yao yatakapoharibiwa kabisa, mataifa ya kilimwengu yataona kuanguka kwa serikali zao, ambazo nyakati nyingine hufananishwa na milima katika unabii wa Biblia.—Danieli 2:35, 44, 45; Ufunuo 17:9.
7. “Mbingu” ni nini, na ‘jeshi la mbinguni’ ni nini?
7 Isaya aendelea kusema, akitumia mifano iliyo wazi: “Jeshi lote la mbinguni litafumuliwa, na mbingu zitakunjwa kama karatasi [“hati-kunjo,” “NW”], na jeshi lao lote litanyauka kama vile jani la mzabibu linyaukavyo na kupukutika, na kama jani la mtini linyaukavyo na kupukutika.” (Isaya 34:4) Usemi “jeshi lote la mbinguni” haumaanishi nyota na sayari halisi. Mistari ya 5 na 6 yasema kuhusu upanga wa machinjo ulioshiba damu katika ‘mbingu’ hizo. Kwa hiyo, lazima huo ni mfano wa kitu fulani katika eneo la binadamu. (1 Wakorintho 15:50) Kwa sababu ya ukuu wake zikiwa mamlaka zilizo kubwa, serikali za wanadamu zafananishwa na mbingu zinazotawala juu ya jamii ya kibinadamu duniani. (Waroma 13:1-4) Kwa hiyo, ‘jeshi la mbinguni’ lawakilisha majeshi ya mwungano ya serikali hizo za wanadamu.
8. Mbingu za mfano zathibitikaje kuwa “kama hati-kunjo,” na ‘majeshi’ yao yapatwa na nini?
8 “Jeshi” hilo “litafumuliwa,” litaoza, kama kitu kinachoharibika upesi. (Zaburi 102:26; Isaya 51:6) Mbingu halisi zilizo juu yetu huonekana kuwa zimepindika machoni petu, kama kitabu cha kale cha hati-kunjo, ambamo kwa kawaida maandishi yalikuwa upande wa ndani. Msomaji amalizapo kusoma maandishi yaliyo upande wa ndani, yeye huikunja na kuihifadhi hati-kunjo hiyo. Vivyo hivyo, “mbingu zitakunjwa kama hati-kunjo,” ikimaanisha kwamba serikali za binadamu lazima zikome. Lazima zikomeshwe kwenye Har–Magedoni zifikapo ukurasa wa mwisho wa historia yake. ‘Majeshi’ yao yenye fahari yataanguka kama vile majani yaliyonyauka yaangukavyo kutoka kwenye mzabibu au vile “jani la mtini linyaukavyo” na kuanguka kutoka kwenye mtini. Wakati wao utakuwa umekwisha.—Linganisha Ufunuo 6:12-14.
Siku ya Kulipa Kisasi
9. (a) Taifa la Edomu lilitoka wapi, na kulitokea uhusiano gani baina ya Israeli na Edomu? (b) Yehova atoa agizo gani kuhusu Edomu?
9 Sasa unabii wachagua taifa fulani ambalo lipo siku ya Isaya—Edomu. Waedomi ni wazao wa Esau (Edomu), aliyemwuzia Yakobo, ndugu yake pacha, haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mkate na chakula cha dengu. (Mwanzo 25:24-34) Esau alimchukia sana Yakobo ndugu yake kwa sababu alichukua haki ya kuwa mzaliwa wa kwanza. Baadaye mataifa ya Edomu na Israeli yakawa adui, hata ingawa yalikuwa uzao wa ndugu pacha. Kutokana na uhasama huo dhidi ya watu wa Mungu, Edomu imejiletea hasira ya kisasi ya Yehova, ambaye sasa asema: “Upanga wangu umekunywa na kushiba mbinguni; tazama, utashukia Edomu, na juu ya watu wa laana yangu, ili kuwahukumu. Upanga wa BWANA umeshiba damu, umenona kwa unono, kwa damu ya wana-kondoo na mbuzi, kwa mafuta ya figo za kondoo waume; maana BWANA ana dhabihu huko Bozra, machinjo makubwa katika nchi ya Edomu.”—Isaya 34:5, 6.
10. (a) Yehova amwangusha nani atumiapo upanga wake “mbinguni”? (b) Edomu yaonyesha mtazamo gani Yuda ishambuliwapo na Babiloni?
10 Edomu iko katika nchi iliyoinuka, yenye milima mingi. (Yeremia 49:16; Obadia 8, 9, 19, 21) Ijapokuwa hivyo, hata ngome hizo za asili hazitafaa kitu Yehova atumiapo upanga wake wa hukumu huko “mbinguni,” akishusha watawala wa Edomu kutoka katika mahali pao palipoinuka. Edomu ina nguvu nyingi za kijeshi, na majeshi yake yashika doria katika safu ndefu za milima ili kuilinda nchi. Lakini Edomu yenye nguvu haitoi msaada wowote Yuda ishambuliwapo na majeshi ya Babiloni. Badala yake, Edomu yajawa na shangwe ionapo kuanguka kwa ufalme wa Yuda nayo yawahimiza washindi wake. (Zaburi 137:7) Edomu hata yawaandama Wayahudi wanaokimbia kuokoa uhai wao na kuwakabidhi mikononi mwa Wababiloni. (Obadia 11-14) Waedomi wapanga kutwaa nchi ya Waisraeli iliyoachwa, nao wanena kwa majivuno dhidi ya Yehova.—Ezekieli 35:10-15.
11. Yehova atawalipaje Waedomi kwa sababu ya tabia yao yenye udanganyifu?
11 Je, Yehova aachilia tabia hiyo ya Waedomi inayokosa udugu? La. Badala yake, atabiri hivi kuhusu Edomu: “Nyati watatelemka pamoja nao, na mahasai pamoja na mafahali, na nchi yao italewa kwa damu, na mavumbi yake yatanoneshwa kwa shahamu.” (Isaya 34:7) Yehova awafananisha wakuu na wadogo katika taifa hilo na nyati na mahasai, wana-kondoo na mabeberu. Nchi ya taifa hilo lenye hatia ya damu italewa damu ya watu wenyewe kupitia kwa “upanga” wa Yehova wenye kufisha.
12. (a) Yehova atumia nani kuleta adhabu dhidi ya Edomu? (b) Nabii Obadia atabiri nini kuhusu Edomu?
12 Mungu akusudia kuiadhibu Edomu kwa sababu ya matendo yenye nia mbaya dhidi ya tengenezo Lake la duniani, liitwalo Sayuni. Unabii wasema: “Ni siku ya kisasi cha BWANA, mwaka wa malipo, ili kushindania Sayuni.” (Isaya 34:8) Muda mfupi baada ya uharibifu wa Yerusalemu mwaka wa 607 K.W.K., Yehova aanza kuonyesha kisasi chake chenye haki juu ya Waedomi kupitia Nebukadreza, mfalme wa Babiloni. (Yeremia 25:15-17, 21) Majeshi ya Babiloni yavamiapo Edomu, hakuna kiwezacho kuwaokoa Waedomi! Ni “mwaka wa malipo” dhidi ya nchi hiyo yenye milima mingi. Yehova atabiri kupitia nabii Obadia: “Kwa sababu ya udhalimu aliotendwa ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele. . . . Kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.”—Obadia 10, 15; Ezekieli 25:12-14.
Wakati Ujao Usio na Matumaini kwa Jumuiya ya Wakristo
13. Ni nani aliye kama Edomu leo, na kwa nini?
13 Leo, kuna tengenezo ambalo mambo yake ni kama ya Edomu. Ni tengenezo gani hilo? Ni nani leo wamekuwa kwenye mstari wa mbele kutukana na kunyanyasa watumishi wa Yehova? Je, si Jumuiya ya Wakristo, kupitia jamii yake ya makasisi? Ndiyo! Jumuiya ya Wakristo imejiinua kufikia mahali pa juu kama mlima katika mambo ya ulimwengu huu. Hiyo ina cheo cha juu katika mfumo wa mambo wa wanadamu, na dini zake ni sehemu kubwa ya Babiloni Mkubwa. Lakini Yehova ameamuru kuwepo “mwaka wa malipo” dhidi ya Edomu hii ya leo kwa sababu ya tabia yake mbaya ya jeuri kuelekea watu Wake, Mashahidi Wake.
14, 15. (a) Nchi ya Edomu na pia Jumuiya ya Wakristo zitapatwa na nini? (b) Mitajo kuhusu lami iwakayo na moshi unaopaa milele yamaanisha nini, nayo haimaanishi nini?
14 Basi, tuchunguzapo sehemu hii iliyobaki ya unabii wa Isaya, twakumbuka Edomu ya kale na Jumuiya ya Wakristo vilevile: “Vijito vyake vitageuzwa kuwa lami, na mavumbi yake yatageuzwa kuwa kiberiti, na ardhi yake itakuwa lami iwakayo. Haitazimwa mchana wala usiku, moshi wake utapaa milele.” (Isaya 34:9, 10a) Nchi ya Edomu yawa ukiwa kabisa hivi kwamba mavumbi ni kama kiberiti na mabonde yamejaa lami, wala si maji. Kisha vifaa hivyo vinavyoweza kuwaka rahisi vyawashwa moto!—Linganisha Ufunuo 17:16.
15 Wengine wana maoni ya kwamba moto, lami, na kiberiti zinazotajwa ni uthibitisho wa kuwapo kwa helo ya moto. Lakini Edomu haitupwi ndani ya moto unaowaziwa kuwa helo ili ichomeke milele. Badala yake, hiyo yaharibiwa, ikitoweka kutoka ulimwenguni kana kwamba imechomwa kabisa kwa moto na kiberiti. Kama unabii uendeleavyo kuonyesha, tokeo la mwisho si mateso ya milele, bali “ukiwa . . . utupu . . . si kitu.” (Isaya 34:11, 12) Moshi ‘unaopaa milele’ waonyesha jambo hilo vizuri. Nyumba inapochomeka, moshi huendelea kutoka katika majivu kwa muda fulani baada ya miale kuzima, na kuwathibitishia watazamaji kwamba moto umekuwapo. Kwa kuwa Wakristo leo wanajifunza kutokana na uharibifu wa Edomu, moshi wa kuchomeka kwa Edomu bado unapaa kwa njia fulani.
16, 17. Edomu itakuwaje, nayo itaendelea katika hali hiyo kwa muda gani?
16 Unabii wa Isaya waendelea, ukitabiri kuwa mahali pa watu wa Edomu patachukuliwa na wanyama wa mwituni, ikiashiria ukiwa unaokuja: “Tangu kizazi hata kizazi itakuwa ukiwa; hapana mtu atakayepita kati yake milele na milele. Kaati na nungu wataimiliki, bundi na kunguru watakaa huko, naye atanyosha juu yake kamba ya ukiwa na timazi ya utupu. Watawaitia wakuu wake ufalme, lakini hawatakuwapo; wakuu wake wote wamekuwa si kitu. Miiba itamea majumbani mwake, upupu na mbigili ndani ya maboma yake; nayo itakuwa kao la mbweha, na ua la mbuni. Na hayawani wa nyikani watakutana na mbwa-mwitu, na beberu anamwita mwenziwe; naam, babewatoto anakaa huko na kujipatia raha. Huko pili atafanya kioto chake na kuzaa na kuotamia.”—Isaya 34:10b-15.a
17 Naam, Edomu itakuwa nchi tupu. Itakuwa nchi yenye ukiwa yenye wanyama wa mwituni, ndege, na nyoka pekee ndani yake. Hali hiyo yenye ukiwa nchini itaendelea, kama mstari wa 10 usemavyo, “milele na milele.” Haitarudishwa tena.—Obadia 18.
Utimizo Hakika wa Neno la Yehova
18, 19. “Kitabu cha Yehova” ni nini, na mna nini katika “kitabu” hicho kwa ajili ya Jumuiya ya Wakristo?
18 Huo ni wakati ujao usio na tumaini kama nini kwa Jumuiya ya Wakristo, ambayo ndiyo Edomu ya leo! Hiyo imejithibitisha kuwa adui mkali wa Yehova Mungu, nayo huwanyanyasa vikali Mashahidi wake. Na hakuna shaka yoyote kwamba Yehova atatimiza neno lake. Wakati wowote mtu alinganishapo unabii huo na utimizo wake, hayo mawili yatalingana—kama vile viumbe wanaokaa katika Edomu iliyoachwa ukiwa wafananavyo na ‘wenzao.’ Isaya azungumza na wanafunzi wa unabii wa Biblia wa wakati ujao, akisema: “Tafuteni katika kitabu cha BWANA [“Yehova,” “NW”] mkasome; hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapana mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru, na roho yake imewakusanya. Naye amewapigia kura, na mkono wake umewagawanyia kwa kamba; wataimiliki hata milele, watakaa ndani yake kizazi hata kizazi.”—Isaya 34:16, 17.
19 Uharibifu unaokaribia wa Jumuiya ya Wakristo umetabiriwa katika “kitabu cha Yehova.” “Kitabu [hicho] cha Yehova” chaonyesha jinsi Yehova atakavyowatoza hesabu adui zake wasiotulizika na ambao ni waoneaji wasiotubu wa watu wake. Mambo yaliyoandikwa juu ya Edomu ya kale yalitimia, na hilo huimarisha uhakika wetu kwamba unabii unaohusu Jumuiya ya Wakristo ambayo ni mfano wa leo wa Edomu, utatimia vivyo hivyo. “Kamba,” yaani, kanuni ya Yehova ya kutenda, yatoa uhakikishio kwamba tengenezo hilo linalokufa kiroho litakuwa nchi yenye ukiwa.
20. Sawa na Edomu ya kale, ni nini kitakachoipata Jumuiya ya Wakristo?
20 Jumuiya ya Wakristo yafanya yote iwezayo kuwatuliza rafiki zake wa kisiasa, lakini hapana mafanikio! Kwa mujibu wa Ufunuo sura ya 17 na ya 18, Mungu Mweza Yote, Yehova, atatia mioyoni mwao fikira ya kutenda dhidi ya tengenezo zima la Babiloni Mkubwa, kutia ndani Jumuiya ya Wakristo. Hatua hiyo itaondoa duniani kote Ukristo wote bandia. Hali ya Jumuiya ya Wakristo itakuwa kama hali isiyo na tumaini inayoelezwa katika Isaya sura ya 34. Hiyo hata haitakuwapo wakati wa “vita ya siku kubwa ya Mungu Mweza-Yote” yenye kuamua mambo yote! (Ufunuo 16:14) Sawa na Edomu ya kale, Jumuiya ya Wakristo itafagiliwa mbali kabisa kutoka usoni pa dunia, “milele na milele.”
[Maelezo ya Chini]
a Kufikia wakati wa Malaki, unabii huo ulikuwa umetimizwa. (Malaki 1:3) Malaki asema kuwa Waedomi walitarajia kuimiliki tena nchi yao iliyoachwa ukiwa. (Malaki 1:4) Hata hivyo, hayo hayakuwa mapenzi ya Yehova, na baadaye watu wengine, Wanabatea, waliimiliki nchi iliyokuwa ya Edomu awali.
[Sanduku katika ukurasa wa 363]
Je, Ni Mungu Mwenye Hasira?
Maneno kama yale yaliyo kwenye Isaya 34:2-7 yamefanya watu wengi wafikiri kwamba Yehova, kama afafanuliwavyo katika Maandiko ya Kiebrania, ni Mungu mkatili, mwenye hasira ya kisasi. Je, ndivyo ilivyo?
La. Ingawa nyakati nyingine Mungu huonyesha hasira yake, hasira hiyo ni ya haki sikuzote. Sikuzote hasira hiyo hutegemea kanuni, wala si hisia zisizodhibitiwa. Isitoshe, sikuzote hiyo huongozwa na haki ya Muumba ya kupokea ujitoaji usiohusisha wengine na uthabiti wake katika kutegemeza kweli. Hasira ya Mungu huongozwa na upendo wake kwa uadilifu na upendo wake kwa wale wanaotenda uadilifu. Yehova huona masuala yote yanayohusika katika jambo naye anajua kikamili hali yoyote ile. (Waebrania 4:13) Yeye huuchunguza moyo; hutambua ni kwa kiasi gani mtu hakuwa na ujuzi, alipuuza, au alitenda dhambi ya kukusudia; naye hutenda bila upendeleo.—Kumbukumbu la Torati 10:17, 18; 1 Samweli 16:7; Matendo 10:34, 35.
Hata hivyo, Yehova Mungu “si mwepesi wa hasira, [naye] ni mwingi wa rehema.” (Kutoka 34:6) Wale wanaomhofu na kujitahidi kutenda uadilifu hupata rehema, kwa maana Mweza Yote hutambua kutokamilika kwa mwanadamu kulikorithiwa na kwa sababu hiyo humrehemu. Leo, dhabihu ya Yesu humwezesha Mungu kufanya hivyo. (Zaburi 103:13, 14) Wakati unaofaa ufikapo, hasira ya Yehova huondolewa juu ya wale wanaokiri dhambi zao, kutubu, na kumtumikia kikweli. (Isaya 12:1) Yehova hasa si Mungu mwenye hasira bali Mungu mwenye furaha, si mkali bali mwenye urafiki, mwenye amani, na mtulivu kwa wale wanaomwendea inavyofaa. (1 Timotheo 1:11) Sifa hizo ni kinyume kabisa cha ukatili usio na rehema unaohusianishwa na miungu ya wapagani isiyo ya kweli na kuonyeshwa katika mifano ya miungu hiyo.
[Ramani katika ukurasa wa 362]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Bahari Kuu
Dameski
Sidoni
Tiro
ISRAELI
Dani
Bahari ya Galilaya
Mto Yordani
Megido
Ramoth-gileadi
Samaria
UFILISTI
YUDA
Yerusalemu
Libna
Lakishi
Beer-sheba
Kadesh-barnea
Bahari ya Chumvi
AMONI
Raba
MOABU
Kir-haresethi
EDOMU
Bozra
Temani
[Picha katika ukurasa wa 358]
Jumuiya ya Wakristo imejaza damu duniani
[Picha katika ukurasa wa 360]
“Mbingu zitakunjwa kama hati-kunjo”