Kupanda Juu kwa Mbawa Kama Tai
MTU huhisije baada ya kuvumilia kwa miaka mitano katika kambi za mateso za Nazi? Kuvunjika moyo? Kuwa na uchungu mwingi? Kutaka kulipiza kisasi?
Ingawa huenda likaonekana kuwa jambo la ajabu, mtu mmoja kama huyo aliandika: “Maisha yangu yalitajirishwa zaidi kuliko vile ningaliweza kutumainia wakati wowote.” Ni kwa nini alihisi hivyo? Yeye alieleza: “Nilipata kimbilio chini ya mbawa za Aliye Juu Zaidi Sana, nikajionea utimizo wa maneno ya nabii Isaya, aliposema: ‘Wao wamgojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; . . . watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.’”—Isaya 40:31.
Mwanamume huyo Mkristo, ambaye mwili wake uliteswa kwa njia yenye kuhofisha zaidi iwezayo kuwazika, alikuwa na mwelekeo wa akilini ulioruka kwa wepesi kitamathali, mwelekeo ambao unyama wa Nazi usingeweza kuushinda. Kama Daudi alipata kimbilio katika uvuli wa “mbawa” za Mungu. (Zaburi 57:1) Mkristo huyo alitumia tashbiha iliyotumiwa na nabii Isaya, akilinganisha nguvu zake za kiroho na zile za tai angani azidiye kuruka juu kwa wepesi.
Je, wewe hupata kuhisi ukiwa umelemezwa na matatizo? Hakuna shaka kwamba wewe pia ungependa kupata kimbilio chini ya mbawa za Aliye Juu Zaidi Sana, ili ‘kupanda juu kwa mbawa kama tai.’ Ili kuelewa jinsi hilo liwezekanavyo, yasaidia kujua jambo fulani juu ya tai, ambaye mara nyingi hutumiwa kitamathali katika Maandiko.
Chini ya Bendera ya Tai
Kati ya ndege wote ambao watu wa kale walichunguza, huenda ikawa tai ndiye aliyestaajabisha zaidi kwa sababu ya nguvu zake na kuruka kwake kwa fahari. Majeshi mengi ya kale, kutia ndani yale ya Babiloni, Uajemi, na Roma, yalipiga mwendo chini ya bendera ya tai. Mojapo majeshi hayo lilikuwa lile la Koreshi Mkubwa. Biblia ilitoa unabii kwamba mfalme huyo wa Uajemi angekuwa kama ndege mwindaji akija kutoka mashariki kunyafua Milki ya Babiloni. (Isaya 45:1; 46:11) Miaka mia mbili baada ya unabii huo kuandikwa, vikosi vya Koreshi, vilivyokuwa na tai kwenye bendera zao za vita, viliruka chini kwa ghafula juu ya jiji la Babiloni kama tai arukavyo chini kwa ghafula juu ya windo lake.
Majuzi zaidi, tai amechaguliwa kuwa ufananisho wa wanavita kama Charlemagne na Napoleon na nchi kama Marekani na Ujerumani. Waisraeli waliamuriwa wasisujudie mifano ya tai au kiumbe kinginecho. (Kutoka 20:4, 5) Hata hivyo, waandikaji wa Biblia walirejezea kwa njia isiyo ya moja kwa moja sifa za tai ili kutolea kielezi ujumbe wao. Kwa njia hiyo tai, ndege atajwaye mara nyingi zaidi katika Maandiko kuliko ndege wengine, hutumiwa kufananisha mambo kama hekima, ulinzi wa kimungu, na wepesi.
Jicho la Tai
Sikuzote mwono mkali wa tai umetumika kitamathali. Ingawa tai mkubwa wa kizio cha kaskazini mara nyingi huwa na uzito unaopungua kilo tano, kwa kweli jicho lake ni kubwa kuliko la mwanadamu, na mwono wake ni mkali hata zaidi. Yehova mwenyewe, akimfafanulia Ayubu uwezo wa tai wa kutafuta chakula chake, alisema: ‘Macho yake hukiangalia toka mbali.’ (Ayubu 39:27, 29) Katika kitabu chake All the Birds of the Bible, Alice Parmelee aripoti kwamba “wakati mmoja tai aliona samaki mfu akielea ziwani umbali wa kilometa tano akaruka kimshazari hadi mahali penyewe. Huyo tai aliweza kuona kitu kidogo kikiwa umbali mkubwa zaidi ya awezavyo kuona mwanadamu, na pia akakazia macho samaki huyo daima muda wote wa mruko wake wa kilometa tano.”
Kwa sababu ya mwono wake mkali, tai ni ufananisho ufaao wa hekima, mojapo sifa kuu za Yehova. (Linganisha Ezekieli 1:10; Ufunuo 4:7.) Kwa nini iwe hivyo? Hekima huhusisha kutangulia kuona matokeo ya utendaji wowote tuwezao kufanya. (Mithali 22:3) Tai, akiwa na uwezo wa kuona mbali sana, aweza kuona hatari ikiwa mbali na kutahadhari, kama tu yule mtu mwenye busara katika kielezi cha Yesu, aliyeona uwezekano wa dhoruba akajenga nyumba yake juu ya mwamba. (Mathayo 7:24, 25) Kwa kupendeza, katika Kihispania, kumfafanua mtu kuwa kama tai humaanisha kwamba yeye ana ufahamu wenye kina au busara.
Ukipata fursa wakati wowote ya kumwona tai kwa ukaribu, chunguza jinsi atumiavyo macho yake. Yeye hakutupii jicho tu; badala ya hivyo, aonekana kwamba anachunguza kila sehemu ya sura yako. Vivyo hivyo, mtu mwenye hekima huchanganua jambo kwa uangalifu kabla ya kufanya uamuzi badala ya kutumainia silika yake au hisia zake. (Mithali 28:26) Hali mwono mkali wa tai humfanya awe ufananisho wa kufaa wa sifa ya kimungu ya hekima, kuruka kwake kwa utukufu pia hutumiwa kitamathali na waandikaji wa Biblia.
“Mwendo wa Tai Katika Hewa”
“Mwendo wa tai katika hewa” hustaajabisha kwa sababu ya mwendo wake na pia jinsi aonekanavyo kuruka kwa urahisi sana, bila kufuata njia yoyote iliyowekwa na bila kuacha alama zozote. (Mithali 30:19) Wepesi wa tai hurejezewa kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwenye Maombolezo 4:19, ambapo wanajeshi wa Babiloni wanafafanuliwa hivi: “Waliotufuatia ni wepesi kuliko tai za mbinguni; hao walitufuatia milimani.” Tai anayezunguka-zunguka juu hewani aonapo windo lake, yeye huinamisha mbawa zake na kuteremka chini, wakati ambapo, kulingana na ripoti fulani, aweza kufikia mwendo wa kilometa 130 kwa saa. Haishangazi kwamba Maandiko humtumia tai akiwa kisawe cha kasi, hasa kuhusiana na nguvu za kijeshi.—2 Samweli 1:23; Yeremia 4:13; 49:22.
Kwa upande mwingine, Isaya hurejezea kule kuruka kwa urahisi kwa tai. “Wao wamgojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu wala hawatazimia.” (Isaya 40:31) Ni nini iliyo siri ya mruko wenye kuelea wa tai? Kupanda juu huhitaji nguvu kidogo kwa kuwa tai hutumia hewa yenye joto, au safu za hewa zenye joto zinazoinuka. Hewa zenye joto hazionekani kwa macho, lakini tai ni stadi wa kuzipata. Mara tu hewa zenye joto zipatikanapo, tai hutanda mbawa zake na mkia wake na kuzunguka palipo na safu ya hewa yenye joto, ambayo humpandisha tai juu zaidi na zaidi. Kimo cha kutosha kifikiwapo, yeye husonga kwa urahisi hadi safu inayofuata ya hewa yenye joto, ambapo utaratibu huo hurudiwa. Kwa njia hiyo tai aweza kukaa juu hewani kwa saa nyingi akitumia kiasi kidogo sana cha nishati.
Katika Israeli, hasa katika Bonde la Ufa ambalo huenea toka Ezion-geber kwenye fuo za Bahari Nyekundu hadi Dani ulio kaskazini, kuona tai ni jambo la kawaida. Idadi yao huwa kubwa hasa wakati wa masika na vuli wahamapo. Katika miaka fulani tai karibu 100,000 wamehesabiwa. Jua la asubuhi lipashapo hewa joto, mamia ya ndege walao mizoga yaweza kuonekana yakiruka juu ya majabali yanayopakana na Bonde la Ufa.
Kuruka kwa tai kwa urahisi ni kielezi kizuri cha jinsi nguvu za Yehova ziwezavyo kutuinua kiroho na kihisia-moyo ili tuweze kuendelea na kazi yetu. Sawa na vile tai hawezi kuruka juu sana kwa wepesi kufikia vimo hivyo kwa kutumia nguvu zake mwenyewe, sisi hatuwezi kukabiliana na hali tukitegemea uwezo wetu wenyewe mbalimbali. “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu,” akaeleza mtume Paulo. (Wafilipi 4:13) Kama tai ambaye huendelea kutafuta hewa zenye joto zisizoonekana, ‘twafuliza kuomba’ kupitia sala zetu zenye bidii ili kupata kani ya utendaji isiyoonekana ya Yehova.—Luka 11:9, 13, NW.
Mara nyingi tai wanaohama hupata hewa zenye joto kwa kuchunguza ndege wengine wawindaji. Mtaalamu wa mambo ya asili D. R. Mackintosh aliripoti kwamba pindi moja tai na tai-mzoga 250 walionekana wakizunguka-zunguka kuelekea juu katika hewa ileile yenye joto. Leo Wakristo vilevile waweza kujifunza kutegemea nguvu za Yehova kwa kuiga vielelezo vya uaminifu vya watumishi wengine wa kimungu.—Linganisha 1 Wakorintho 11:1.
Katika Uvuli wa Mbawa za Tai
Kimojapo vipindi vya hatari zaidi vya maisha ya tai ni wakati ajifunzapo kuruka. Tai kadhaa hufa wajaribupo kufanya hivyo. Taifa changa la Israeli pia lilikuwa hatarini lilipoondoka Misri. Kwa hiyo maneno ya Yehova kwa Waisraeli yalifaa sana: “Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai nikawaleta ninyi kwangu mimi.” (Kutoka 19:4) Kuna ripoti za tai wanaobeba ndege mchanga mgongoni mwao kwa muda mfupi ili mchanga asianguke kwa kishindo ajaribupo kuruka mara za kwanza-kwanza. G. R. Driver, akitoa maelezo katika Palestine Exploration Quarterly juu ya ripoti kama hizo, alisema: “Hicho kielezi [cha Kibiblia] si wazo la kuwaziwa tu bali kina msingi katika jambo la hakika.”
Tai ni wazazi wazuri katika njia nyinginezo vilevile. Wanamwandalia kinda milo kwa ukawaida na pia ndege aliye mama hukata-kata kwa uangalifu nyama ambayo tai wa kiume huleta kiotani ili tai mchanga aweze kuimeza. Kwa kuwa viota vyao kwa kawaida hujengwa juu ya jabali au katika miti mirefu, ndege wachanga hukabili halihewa mbalimbali. (Ayubu 39:27, 28) Jua kali, lipatikanalo sana katika mabara ya Biblia, lingeweza kusababisha kifo cha ndege mchanga kama isingalikuwa kwa sababu ya utunzi wa wazazi wake. Tai mzima hutanda mbawa zake, nyakati nyingine kwa saa kadhaa kwa wakati mmoja, ili kuwekea kivuli kinda lake jororo.
Hivyo yafaa sana kwamba mbawa za tai hutumiwa katika Maandiko kuwa ufananisho wa ulinzi wa kimungu. Kumbukumbu la Torati 32:9-12 hufafanua jinsi Yehova alivyowalinda Waisraeli wakati wa safari yao ya jangwani: “Maana, sehemu ya BWANA ni watu wake, Yakobo ni kura ya urithi wake. Alimkuta katika nchi ya ukame, na katika jangwa tupu litishalo; alimzunguka, akamtunza; akamhifadhi kama mboni ya jicho; mfano wa tai ataharikishaye kioto chake; na kupapatika juu ya makinda yake, alikunjua mbawa zake, akawatwaa, akawachukua juu ya mbawa zake; BWANA peke yake alimwongoza.” Yehova atatupa ulinzi huohuo wenye upendo tukimtumainia.
Njia ya Kukimbia
Nyakati nyingine tukabiliwapo na matatizo, huenda tukajikuta tukitamani kuruka mbali kutoka kwa magumu yetu yote. Hizo ndizo zilizokuwa hisia barabara za Daudi. (Linganisha Zaburi 55:6, 7.) Lakini ingawa Yehova ameahidi kutusaidia tukabilipo majaribu na kuteseka katika mfumo huu, yeye hatoi njia ya kukimbia kabisa. Sisi tuna uhakikishio huu wa Biblia: “Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.”—1 Wakorintho 10:13, Habari Njema Kwa Watu Wote.
“Njia ya kutoka humo” au “njia ya kukimbia” (Zaire Swahili Bible) hutia ndani kujifunza kumtumainia Yehova. Hilo ndilo alilogundua Max Liebster, ambaye maelezo yake yalinukuliwa mwanzoni mwa makala hii. Wakati wa ile miaka aliyokuwa katika kambi za mateso, alikuja kumjua na kumtegemea Yehova. Kama alivyogundua Max, Yehova hututia nguvu kupitia Neno lake, roho yake, na tengenezo lake. Hata katika hizo kambi, Mashahidi walitafuta waamini wenzao na kuwatolea msaada wa kiroho, wakishiriki mawazo ya Kimaandiko na fasihi zozote za Biblia zilizopatikana. Na kama waokokaji waaminifu wametoa ushuhuda tena na tena, kwa kweli Yehova aliwategemeza. “Niliendelea kumwomba Yehova asaidie,” Max aeleza, “nayo roho yake ilinihifadhi.”
Katika majaribu yoyote tukabiliyo, twaweza vivyo hivyo kuitegemea roho takatifu ya Mungu, maadamu tu twaendelea kuomba kuipata. (Mathayo 7:7-11) Tukiwa tumetiwa nguvu na “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida,” badala ya kushindwa na matatizo yetu, tutaruka kwa wepesi. Tutaendelea kutembea katika njia ya Yehova, nasi hatutachoka. Tutapanda juu kwa mbawa kama tai.—2 Wakorintho 4:7, NW; Isaya 40:31.
[Blabu katika ukurasa wa 10]
Yeye hakutupii jicho tu
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Foto: Cortesía de GREFA
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]
Foto: Cortesía de Zoo de Madrid