Sura Ya Tisa
Ni Nani Atakayeutawala Ulimwengu?
1-3. Fafanua ndoto na maono ambayo Danieli aliona mwaka wa kwanza wa utawala wa Belshaza.
SASA unabii wa Danieli wenye kuvutia sana waturudisha nyuma hadi mwaka wa kwanza wa Mfalme Belshaza wa Babiloni. Danieli amekuwa uhamishoni Babiloni kwa muda mrefu, lakini uaminifu-maadili wake kwa Yehova haujayumbayumba kamwe. Sasa akiwa na umri wa miaka 70 na kitu, nabii huyo mwaminifu aona “ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake.” Nayo maono hayo yamwogofya wee!—Danieli 7:1, 15.
2 “Tazama,” Danieli asema kwa mshangao. “Hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa. Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali.” Wanyama wa ajabu kama nini! Wa kwanza ni simba mwenye mabawa, na wa pili ni kama dubu. Kisha chui mwenye mabawa manne na vichwa vinne atokea! Mnyama wa nne mwenye nguvu nyingi zisizo za kawaida ana meno ya chuma na pembe kumi. Pembe “ndogo” yatokea katikati ya pembe zake kumi ikiwa na “macho kama macho ya mwanadamu” na “kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu.”—Danieli 7:2-8.
3 Kisha maono ya Danieli yageukia mbingu. Mzee wa Siku aketi kwa utukufu akiwa Hakimu katika Mahakama ya kimbingu. ‘Maelfu elfu wanamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wamesimama mbele zake.’ Akiwahukumu wanyama hao vikali, awanyang’anya utawala na kumharibu mnyama wa nne. “Mmoja aliye mfano wa mwanadamu [“mwana wa binadamu,” NW]” apewa mamlaka atawale “watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote.”—Danieli 7:9-14.
4. (a) Danieli alimtegemea nani ili kupata maana ya kweli ya mambo hayo? (b) Kwa nini mambo ambayo Danieli aliona na kusikia usiku huo ni ya maana kwetu?
4 “Mimi,” Danieli asema, “roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha.” Kwa hiyo, amwuliza malaika “maana ya kweli ya hayo yote.” Kwa kweli malaika huyo amjulisha “tafsiri ya mambo hayo.” (Danieli 7:15-28) Kile ambacho Danieli aliona na kusikia usiku huo chatupendeza sana, kwa kuwa kilionyesha matukio ya ulimwengu ya wakati ujao yanayofikia nyakati zetu, wakati ambapo “mmoja aliye mfano wa mwanadamu [“mwana wa binadamu,” NW]” anapewa utawala juu ya “watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote.” Sisi pia twaweza kuelewa maana ya maono hayo ya kiunabii tukisaidiwa na Neno la Mungu na roho yake.a
WANYAMA WANNE WATOKA BAHARINI
5. Bahari iliyochafuliwa na upepo yafananisha nini?
5 “Wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini,” akasema Danieli. (Danieli 7:3) Ni nini kilichofananishwa na bahari iliyochafuliwa na upepo? Miaka mingi baadaye, mtume Yohana aliona hayawani-mwitu mwenye vichwa saba akitoka katika “bahari.” Bahari hiyo iliwakilisha “vikundi vya watu na umati na mataifa na lugha”—jamii kubwa ya wanadamu iliyotengana na Mungu. Basi, bahari ni ufananisho unaofaa wa umati wa watu waliojitenga na Mungu.—Ufunuo 13:1, 2; 17:15; Isaya 57:20.
6. Wale wanyama wanne wanafananisha nini?
6 Malaika wa Mungu akasema: “Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wanne watakaotokea duniani.” (Danieli 7:17) Malaika aliwatambulisha waziwazi wanyama wanne ambao Danieli aliwaona kuwa “wafalme wanne.” Kwa hiyo, wanyama hao wanafananisha serikali za ulimwengu. Lakini serikali zipi?
7. (a) Wafafanuzi fulani wa Biblia husema nini juu ya ono ambalo Danieli aliona katika ndoto juu ya wanyama wanne na ile ndoto ya sanamu kubwa aliyoota Mfalme Nebukadreza? (b) Kila moja ya sehemu nne za metali za sanamu hiyo zawakilisha nini?
7 Kwa kawaida, wafafanuzi wa Biblia huhusianisha ono la Danieli kwenye ndoto juu ya wanyama wanne na ile ndoto ya Nebukadreza ya sanamu kubwa. Kwa kielelezo, kichapo The Expositor’s Bible Commentary chataarifu hivi: “Sura ya 7 [ya Danieli] yalingana na sura ya 2.” Kichapo The Wycliffe Bible Commentary chasema: “Kwa ujumla yakubalika kwamba mfuatano wa tawala nne za wasio Wayahudi . . . [katika Danieli sura ya 7] unafanana na ule unaotajwa katika [Danieli] sura ya 2.” Zile serikali nne za ulimwengu zilizowakilishwa na zile metali nne za ndoto ya Nebukadreza zilikuwa Milki ya Babiloni (kichwa cha dhahabu), Umedi na Uajemi (kifua na mikono ya fedha), Ugiriki (tumbo na viuno vya shaba), na Milki ya Roma (miguu ya chuma).b (Danieli 2:32, 33) Acheni tuone jinsi falme hizo zinavyolingana na wale wanyama wanne wakubwa ambao Danieli aliona.
MKALI KAMA SIMBA, MWEPESI KAMA TAI
8. (a) Danieli alimfafanuaje mnyama wa kwanza? (b) Mnyama wa kwanza alifananisha milki gani, nayo ilitendaje kama simba?
8 Danieli aliona wanyama wa ajabu kama nini! Akimfafanua mmoja wao, alisema hivi: “Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake yakafutuka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu.” (Danieli 7:4) Mnyama huyo alifananisha utawala uleule uliowakilishwa na kichwa cha dhahabu cha ile sanamu kubwa, Serikali ya Ulimwengu ya Babiloni (607-539 K.W.K.). Kama ilivyo na “simba” mwindaji, Babiloni lilinyafua mataifa kwa ukali, kutia ndani watu wa Mungu. (Yeremia 4:5-7; 50:17) “Simba” huyo alisonga kasi katika ushindi wenye nguvu, kana kwamba alikuwa na mabawa ya tai.—Maombolezo 4:19; Habakuki 1:6-8.
9. Yule mnyama kama simba alibadilikaje, na mabadiliko hayo yalimwathirije?
9 Hatimaye, mabawa ya yule simba wa pekee “yakafutuka manyoya.” Mwishoni-mwishoni mwa utawala wa Mfalme Belshaza, Babiloni lilipoteza mwendo wake wa ushindi na ukuu wake kama simba juu ya mataifa. Halikwenda kasi kuliko binadamu akitembea kwa miguu miwili. Kwa kuwa lilipata “moyo wa kibinadamu,” likawa dhaifu. Babiloni halingeweza tena kutenda kama mfalme “kati ya wanyama wa msituni,” kwa kuwa halikuwa na “moyo wa simba.” (Linganisha 2 Samweli 17:10; Mika 5:8.) Mnyama mwingine mkubwa akamshinda.
MLAFI KAMA DUBU
10. “Dubu” alifananisha watawala gani?
10 “Tazama,” akasema Danieli, “mnyama mwingine, wa pili, kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake; wakamwambia mnyama huyo hivi, Inuka, ule nyama tele.” (Danieli 7:5) Mfalme aliyefananishwa na “dubu” huyo ndiye yuleyule aliyewakilishwa na kifua na mikono ya fedha ya ile sanamu kubwa—wale watawala mbalimbali wa Umedi na Uajemi (539-331 K.W.K.) kuanzia Dario Mmedi na Koreshi Mkuu hadi Dario wa Tatu.
11. Kuinuka upande mmoja kwa yule dubu wa mfano na kuwa na mifupa mitatu ya mbavu katika mdomo wake kulifananisha nini?
11 Yule dubu wa mfano “aliinuliwa upande mmoja,” huenda ili kuwa tayari kushambulia na kushinda mataifa na hivyo kudumu akiwa serikali ya ulimwengu. Au huenda kuinuka huko kulikusudiwa kuonyesha kwamba watawala wa Uajemi wangetawala kupita mfalme mmoja Mmedi, Dario. Ile mifupa mitatu ya mbavu katika meno ya dubu huyo ingeweza kufananisha pande tatu ambazo dubu huyo angeshinda. “Dubu” wa Umedi na Uajemi alienda kaskazini kuteka Babiloni mwaka wa 539 K.W.K. Kisha akaenda magharibi kupitia Asia Ndogo na kuingia Thrasi. Hatimaye, “dubu” huyo alienda kusini akashinde Misri. Kwa kuwa nambari tatu nyakati nyingine huonyesha mkazo, ile mifupa mitatu ya mbavu yaweza pia kukazia pupa ya ushindi, ya yule dubu wa mfano.
12. Kulitokea nini yule dubu wa mfano alipotii ile amri: “Inuka, ule nyama tele”?
12 “Dubu” huyo alishambulia mataifa kwa mujibu wa maneno haya: “Inuka, ule nyama tele.” Kwa kunyafua Babiloni kulingana na mapenzi ya Mungu, serikali ya Umedi na Uajemi ingeweza kutimiza utumishi wa maana kuelekea watu wa Yehova. Nayo ilifanya hivyo! (Ona “Mtawala Mvumilivu,” kwenye ukurasa wa 149.) Kupitia Koreshi Mkuu, Dario wa Kwanza (Dario Mkuu), na Artashasta wa Kwanza, serikali ya Umedi na Uajemi iliweka huru Wayahudi waliokuwa wametekwa na Babiloni na kuwasaidia kujenga upya hekalu la Yehova na kurekebisha kuta za Yerusalemu. Hatimaye, Umedi na Uajemi ikatawala wilaya 127, na mume wa Malkia Esta, Ahasuero (Shasta wa Kwanza), akamiliki “toka Bara Hindi mpaka Kushi.” (Esta 1:1) Hata hivyo, mnyama mwingine alikuwa akikaribia kuinuka.
MWEPESI KAMA CHUI MWENYE MABAWA!
13. (a) Mnyama wa tatu alifananisha nini? (b) Ni nini kiwezacho kusemwa juu ya mwendo wa mnyama wa tatu na milki yake?
13 Mnyama wa tatu alikuwa “kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka.” (Danieli 7:6) Kama lile tumbo na viuno vya shaba vya sanamu ya ndoto ya Nebukadreza, chui huyo mwenye mabawa manne na vichwa vinne alifananisha watawala wa Makedonia, au Ugiriki, kuanzia Aleksanda Mkuu. Akiwa na wepesi na mwendo wa chui, Aleksanda alipitia Asia Ndogo, kusini kuingia Misri, na kusonga mbele kufikia mpaka wa magharibi wa India. (Linganisha Habakuki 1:8.) Milki yake ilikuwa kubwa kuliko ile ya “dubu,” kwa kuwa ilitia ndani Makedonia, Ugiriki, na Milki ya Uajemi.—Ona “Mtawala Mchanga Aushinda Ulimwengu,” kwenye ukurasa wa 153.
14. “Chui” alipataje kuwa na vichwa vinne?
14 “Chui” huyo alipata vichwa vinne baada ya Aleksanda kufa mwaka wa 323 K.W.K. Wanne kati ya majenerali wake walitawala baada yake katika sehemu tofauti-tofauti za milki yake. Seleuko alitawala Mesopotamia na Siria. Ptolemy akatawala Misri na Palestina. Lisimako akatawala Asia Ndogo na Thrasi, naye Kasanda akatawala Makedonia na Ugiriki. (Ona “Ufalme Mkubwa Wagawanyika,” kwenye ukurasa wa 162.) Kisha tisho jingine likazuka.
MNYAMA MKALI AWA TOFAUTI
15. (a) Mfafanue mnyama wa nne. (b) Mnyama wa nne alifananisha nini, naye alivunja vipande vipande na kula kila kitu kilichokuwa mbele yake jinsi gani?
15 Danieli alimfafanua mnyama wa nne kuwa “mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi.” Aliendelea kusema hivi: “Naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.” (Danieli 7:7) Mnyama huyo mkali alianza akiwa serikali ya kisiasa na ya kijeshi ya Roma. Ikatwaa hatua kwa hatua yale maeneo manne ya Kiyunani ya Milki ya Ugiriki, na kufikia mwaka wa 30 K.W.K., Roma ilikuwa imeinuka na kuwa serikali ya ulimwengu iliyofuata katika unabii wa Biblia. Ikishinda kwa nguvu za kijeshi kila kitu kilichokuwa mbele yake, hatimaye Milki ya Roma ikaenea toka Visiwa vya Uingereza hadi sehemu kubwa ya Ulaya, kotekote kuzunguka Mediterania, na ng’ambo ya Babiloni hadi Ghuba ya Uajemi.
16. Malaika alisema nini juu ya mnyama wa nne?
16 Akitaka kujua maana kamili ya mnyama huyu “mwenye kutisha,” Danieli alimsikiliza kwa makini malaika alipokuwa akimfafanua: “Na habari za zile pembe [zake] kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali [“tofauti,” BHN] na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.” (Danieli 7:19, 20, 24) “Pembe kumi,” au “wafalme kumi” walikuwa nani?
17. Zile “pembe kumi” za mnyama wa nne zafananisha nini?
17 Roma ilipozidi kutajirika na kuharibika kwa sababu ya maisha ya ufisadi miongoni mwa jamii ya watawala wake, nguvu yake ya kijeshi ilipungua. Hatimaye, kupungua kwa nguvu za kijeshi za Roma kukaonekana waziwazi. Mwishowe milki hiyo yenye nguvu ikavunjika na kuwa falme nyingi. Kwa kuwa Biblia mara nyingi hutumia nambari kumi kudokeza ukamili, zile “pembe kumi” za mnyama wa nne zawakilisha falme zote zilizotokana na kuvunjika kwa Roma.—Linganisha Kumbukumbu la Torati 4:13; Luka 15:8; 19:13, 16, 17.
18. Roma iliendeleaje kutawala Ulaya kwa karne nyingi baada ya kuondolewa kwa maliki wake wa mwisho?
18 Hata hivyo, Serikali ya Ulimwengu ya Roma haikuisha wakati maliki wake wa mwisho katika Roma alipopinduliwa mwaka wa 476 W.K. Kwa karne nyingi, Roma ya papa iliendelea kutawala Ulaya kisiasa na hasa kidini. Ilifanya hivyo kupitia mfumo wa kikabaila, ambamo wakazi wengi wa Ulaya walikuwa chini ya bwana, kisha chini ya mfalme. Na wafalme wote walikuwa chini ya mamlaka ya papa. Kwa hiyo, Milki ya Roma Takatifu, Roma ya papa ikiwa kituo chake kikuu, ilitawala mambo ya dunia kwa kipindi chote hicho kirefu cha historia kilichoitwa Enzi za Giza.
19. Kulingana na mwanahistoria mmoja, Roma ilitofautianaje na milki zilizoitangulia?
19 Ni nani awezaye kupinga kwamba mnyama wa nne hakuwa ‘tofauti na zile falme za kwanza’? (Danieli 7:7, 19, 23) Kuhusu hilo, mwanahistoria H. G. Wells aliandika hivi: “Serikali hiyo mpya ya Roma . . . ilitofautiana kwa njia kadhaa na milki nyingine kuu ambazo zilikuwa zimeutawala ulimwengu mstaarabu awali. . . . [Hiyo] ilitia ndani karibu Wagiriki wote ulimwenguni, na haikuwa na watu wengi wa jamii ya Hamu na jamii ya Shemu kama milki zilizotangulia . . . Lilikuwa jambo jipya katika historia kufikia wakati huo . . . Milki ya Roma ilikuwa ukuzi, ukuzi mpya ambao haukupangiwa; Waroma walijikuta bila kujua katika mradi mkubwa wa kutawala.” Hata hivyo, yule mnyama wa nne angekua hata zaidi.
PEMBE NDOGO YAPATA UTAWALA
20. Malaika alisema nini juu ya kumea kwa pembe ndogo kwenye kichwa cha mnyama wa nne?
20 “Nikaziangalia sana pembe zake,” akasema Danieli, “na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang’olewa kabisa.” (Danieli 7:8) Kuhusu ukuzi huo, malaika alimwambia Danieli hivi: “Mwingine ataondoka baada ya hao [wale wafalme kumi]; naye atakuwa mbali [“tofauti,” BHN] na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.” (Danieli 7:24) Mfalme huyo ni nani, aliinuka lini, naye alishusha wafalme gani watatu?
21. Uingereza ilipataje kuwa ile pembe ndogo ya mfano ya mnyama wa nne?
21 Fikiria mambo yafuatayo. Mwaka wa 55 K.W.K., Jenerali Mroma Juliasi Kaisari alivamia Uingereza lakini akashindwa kuidhibiti daima. Mwaka wa 43 W.K., Maliki Klaudio alianza ushindi wa kudumu zaidi dhidi ya Uingereza kusini. Kisha, mwaka wa 122 W.K., Maliki Hadriani akaanza kujenga ukuta kutoka Mto Tyne hadi Ghuba ya Solway, akiweka mpaka wa kaskazini wa Milki ya Roma. Mapema katika karne ya tano, majeshi ya Roma yaliondoka kisiwa hicho. “Katika karne ya kumi na sita,” akaeleza mwanahistoria mmoja, “Uingereza haikuwa serikali yenye nguvu sana. Haikuwa na utajiri mwingi kama Uholanzi. Ilikuwa na watu wachache kuliko Ufaransa. Majeshi yake (kutia ndani jeshi la wanamaji) hayakuwa na nguvu kama majeshi ya Hispania.” Yaonekana kwamba Uingereza ulikuwa ufalme mdogo wakati huo, uliokuwa pembe ndogo ya mfano ya mnyama wa nne. Lakini hali hiyo ingebadilika.
22. (a) Ile pembe “ndogo” ilishinda pembe zipi nyingine tatu za yule mnyama wa nne? (b) Kisha Uingereza ikawa nini?
22 Mwaka wa 1588, Philip wa Pili wa Hispania alituma Manowari za Hispania zikashambulie Uingereza. Kundi hilo la meli 130, zilizobeba watu zaidi ya 24,000, lilisafiri kupitia Mlango-Bahari wa Uingereza, nalo lilishindwa na jeshi la wanamaji la Uingereza na kuhasiriwa na pepo zilizovuma dhidi yao na dhoruba kali za Atlantiki. Tukio hilo “lilionyesha kwamba sasa Uingereza ndiyo iliyokuwa na jeshi kuu la wanamaji na wala si Hispania,” akasema mwanahistoria mmoja. Katika karne ya 17, Waholanzi walikuwa na meli nyingi zaidi ulimwenguni za kufanyia biashara. Hata hivyo, kwa sababu ya koloni zenye kuongezeka ng’ambo, Uingereza iliushinda ufalme huo pia. Katika karne ya 18, Waingereza na Wafaransa walipigana huko Amerika Kaskazini na India, hilo likiongoza kwenye Mkataba wa Paris mwaka wa 1763. Mwandishi William B. Willcox alisema kwamba mkataba huo “ulitambua wadhifa mpya wa Uingereza ikiwa serikali kuu ya Ulaya katika ulimwengu nje ya Ulaya.” Ukuu wa Uingereza ulithibitishwa ilipomshinda vibaya Napoléon wa Ufaransa mwaka wa 1815 W.K. Kwa hiyo, wale “wafalme watatu” ambao Uingereza ‘ilishusha’ ni Hispania, Uholanzi, na Ufaransa. (Danieli 7:24) Kwa hiyo, Uingereza ikawa serikali kubwa zaidi ulimwenguni ya kikoloni na ya kibiashara. Naam, ile pembe “ndogo” ikakua na kuwa serikali ya ulimwengu!
23. Ile pembe ndogo ya mfano ‘ilikulaje dunia yote’?
23 Malaika alimwambia Danieli kwamba mnyama wa nne, au ufalme wa nne, ‘ungekula dunia yote.’ (Danieli 7:23) Ndivyo ilivyokuwa kuhusu mkoa wa Roma ambao wakati mmoja uliitwa Uingereza. Hatimaye ukawa Milki ya Uingereza na ‘kula dunia yote.’ Wakati mmoja, milki hiyo ilimiliki robo moja ya nchi kavu ya dunia na robo moja ya wakazi wa dunia.
24. Mwanahistoria mmoja alisema Milki ya Uingereza ilikuwaje tofauti?
24 Kama vile Milki ya Roma ilivyokuwa tofauti na serikali za ulimwengu zilizotangulia, mfalme aliyefananishwa na ile pembe “ndogo” pia angekuwa “mbali [“tofauti,” BHN] na hao wa kwanza.” (Danieli 7:24) Kuhusu Milki ya Uingereza, mwanahistoria H. G. Wells alitaarifu hivi: “Hakujawa na [serikali] yoyote ya aina hiyo. Jambo la kwanza na kuu katika mfumo wote huo lilikuwa ‘jamhuri yenye mfalme’ ya Muungano wa Falme za Uingereza . . . Hakuna ofisi yoyote wala akili yoyote iliyopata kamwe kufahamu Milki yote ya Uingereza. Ilikuwa muungano wa ukuzi na mamlaka zaidi tofauti kabisa na yoyote iliyopata kuitwa milki hapo awali.”
25. (a) Katika matukio ya karibuni zaidi, ile pembe ndogo ya mfano ni nini? (b) Ile pembe “ndogo” ina “macho kama macho ya mwanadamu,” na ‘kinywa kinachonena maneno makuu’ katika maana gani?
25 Ile pembe “ndogo” ilihusisha mengi zaidi ya Milki ya Uingereza. Mwaka wa 1783, Uingereza ilizipa uhuru koloni zake 13 za Amerika. Hatimaye, Marekani ikawa mshirika wa Uingereza, na kuibuka ikiwa taifa lenye nguvu zaidi duniani baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili. Bado ingali na uhusiano wenye nguvu na Uingereza. Serikali ya Uingereza na Marekani iliyotokezwa ndiyo ‘pembe yenye macho.’ Kwa kweli, serikali hiyo ya ulimwengu inaona sana, na ina akili! ‘Hunena mambo makuu,’ ikiamua sera zitakazofuatwa na sehemu kubwa ya ulimwengu na kuwa msemaji wake, au “nabii asiye wa kweli.”—Danieli 7:8, 11, 20; Ufunuo 16:13; 19:20.
ILE PEMBE NDOGO YAMPINGA MUNGU NA WATAKATIFU WAKE
26. Malaika alitabiri nini juu ya maneno na matendo ya ile pembe ya mfano kumwelekea Yehova na watumishi wake?
26 Danieli aliendelea kufafanua ono lake, akisema: “Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda.” (Danieli 7:21) Kuhusu “pembe” hiyo, au mfalme huyo, malaika wa Mungu alitabiri hivi: “Atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.” (Danieli 7:25) Sehemu hiyo ya unabii huu ilitimia jinsi gani na lini?
27. (a) “Watakatifu” wanaonyanyaswa na ile pembe “ndogo” ni nani? (b) Ile pembe ya mfano iliazimiaje “kubadili majira na sheria”?
27 “Watakatifu” walionyanyaswa na ile pembe “ndogo”—Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani—ni wafuasi watiwa-mafuta kwa roho wa Yesu walio duniani. (Waroma 1:7; 1 Petro 2:9) Kwa miaka kadhaa kabla ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, mabaki ya watiwa-mafuta hao walionya waziwazi kwamba mwaka wa 1914 ungekuwa mwisho wa “nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa.” (Luka 21:24) Vita vilipozuka mwaka huo, ilikuwa dhahiri kwamba ile pembe “ndogo” ilikuwa imepuuza onyo hilo, kwa kuwa iliwasumbua daima watiwa-mafuta “watakatifu.” Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani hata ilipinga jitihada zao za kuendeleza matakwa (au, “sheria”) ya Yehova ya kwamba mashahidi wake wahubiri habari njema ya Ufalme ulimwenguni pote. (Mathayo 24:14) Kwa hiyo, ile pembe “ndogo” ilijaribu “kubadili majira na sheria.”
28. “Wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati” zina urefu gani?
28 Malaika wa Yehova alirejezea kipindi cha wakati cha kiunabii kuwa “wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.” Kipindi hicho kilikuwa na urefu gani? Wafafanuzi wa Biblia hukubaliana kwa ujumla kwamba usemi huo hurejezea nyakati tatu na nusu—jumla ya wakati mmoja, nyakati mbili, na nusu wakati. Kwa kuwa zile “nyakati saba” za kichaa cha Nebukadreza zilijumlika kuwa miaka saba, zile nyakati tatu na nusu ni miaka mitatu na nusu.c (Danieli 4:16, 25) Tafsiri ya An American Translation husema: “Watatiwa mikononi mwake kwa mwaka mmoja, miaka miwili, na nusu mwaka.” Tafsiri ya Biblia Habari Njema husema: “Kwa muda wa miaka mitatu na nusu.” Kipindi hichohicho chatajwa kwenye andiko la Ufunuo 11:2-7, linalotaarifu kwamba mashahidi wa Mungu wangehubiri wakiwa wamevaa nguo za gunia kwa miezi 42, au siku 1,260, kisha wauawe. Kipindi hicho kilianza na kuisha lini?
29. Ile miaka mitatu na nusu ya kiunabii ilianza lini na jinsi gani?
29 Kwa Wakristo watiwa-mafuta, wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ulikuwa wakati wa kujaribiwa. Kufikia mwisho wa mwaka wa 1914, walikuwa wakitarajia mnyanyaso. Kwa hakika, andiko la mwaka lenyewe lililochaguliwa kwa ajili ya mwaka wa 1915 lilikuwa swali la Yesu alilowauliza wanafunzi wake, “Je, mwaweza kukinywa kikombe ambacho mimi niko karibu kunywa?” Lilitegemea Mathayo 20:22. Kuanzia Desemba mwaka wa 1914, mashahidi hao wachache walihubiri “wakiwa wamevaa nguo ya gunia.”
30. Wakristo watiwa-mafuta walisumbuliwaje na Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza?
30 Vita vilipopamba moto, Wakristo watiwa-mafuta walikabili upinzani wenye kuongezeka. Baadhi yao walifungwa gerezani. Watu mmoja-mmoja, kama vile Frank Platt aliyekuwa Uingereza na Robert Clegg huko Kanada, waliteswa na wenye mamlaka wakatili. Februari 12, 1918, Kanada iliyokuwa Milki ya Uingereza ilipiga marufuku buku la saba la Studies in the Scriptures, liitwalo The Finished Mystery, lililokuwa limechapishwa karibuni, pamoja na trakti ziitwazo The Bible Students Monthly. Mwezi uliofuata, Ofisi ya Mkuu wa Sheria ya Marekani ilitangaza kugawanywa kwa buku hilo la saba kuwa kinyume cha sheria. Ikawaje? Nyumba zilisakwa, fasihi zikatwaliwa, na waabudu wa Yehova wakakamatwa!
31. “Wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati” ziliisha lini na jinsi gani?
31 Kusumbuliwa kwa watiwa-mafuta wa Mungu kulifikia upeo Juni 21, 1918, wakati ambapo msimamizi, J. F. Rutherford, na washiriki mashuhuri wa Watch Tower Bible and Tract Society walihukumiwa vifungo vya muda mrefu gerezani kwa sababu ya mashtaka yasiyo ya kweli. Ikiazimu “kubadili majira na sheria,” ile pembe “ndogo” ilikuwa imefanikiwa kuharibu utaratibu wa kazi ya kuhubiri. (Ufunuo 11:7) Kwa hiyo, kile kipindi kilichotabiriwa cha “wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati” kilimalizika Juni 1918.
32. Kwa nini ungeweza kusema kwamba “watakatifu” hawakufutiliwa mbali na ile pembe “ndogo”?
32 Lakini “watakatifu” hawakuharibiwa na ule usumbufu wa ile pembe “ndogo.” Kama ilivyotabiriwa katika kitabu cha Ufunuo, baada ya kipindi kifupi cha kutotenda, Wakristo watiwa-mafuta walipata uhai na kuwa watendaji tena. (Ufunuo 11:11-13) Machi 26, 1919, msimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society na washiriki wake waliachiliwa kutoka gerezani, na baadaye wakaondolewa mashtaka yote yasiyo ya kweli waliyokuwa wameshtakiwa. Punde baadaye, mabaki watiwa-mafuta wakaanza kufanya mipango mipya kwa ajili ya utendaji zaidi. Hata hivyo, ile pembe “ndogo” ingepatwa na nini?
MZEE WA SIKU AHUKUMU
33. (a) Mzee wa Siku ni nani? (b) Ni ‘vitabu gani vilivyofunuliwa’ katika Mahakama ya kimbingu?
33 Baada ya kuwatambulisha wale wanyama wanne, Danieli aacha kumwangalia mnyama wa nne na kuona kikao mbinguni. Aona Mzee wa Siku ameketi katika kiti chake chenye utukufu akiwa Hakimu. Mzee wa Siku si mwingine ila Yehova Mungu. (Zaburi 90:2) Mahakama ya kimbingu iketipo, Danieli aona ‘vitabu vikifunuliwa.’ (Danieli 7:9, 10) Kwa kuwa Yehova ni wa tangu milele, anajua historia yote ya binadamu kana kwamba imeandikwa katika kitabu. Amewaangalia wanyama wote hao wanne naye aweza kuwahukumu kulingana na mambo ajuayo yeye mwenyewe.
34, 35. Ile pembe “ndogo” na serikali nyingine za mnyama zitapatwa na nini?
34 Danieli aendelea kusema hivi: “Nikatazama wakati huo; kwa sababu ya sauti ya yale maneno makubwa iliyoyasema ile pembe; nalitazama hata mnyama yule akauawa, mwili wake ukaharibiwa, akatolewa ateketezwe kwa moto. Na kwa habari za wale wanyama wengine, walinyang’anywa mamlaka yao; walakini maisha yao yalidumishwa kwa wakati na majira.” (Danieli 7:11, 12) Malaika amwambia Danieli hivi: “Hukumu itawekwa, nao watamwondolea mamlaka yake, kuyapoteza na kuyaangamiza, hata milele.”—Danieli 7:26.
35 Kwa amri ya Hakimu Mkuu, Yehova Mungu, pembe iliyomkufuru Mungu na kuwasumbua “watakatifu” wake itapatwa na jambo lilelile lililoipata Milki ya Roma, ambayo iliwanyanyasa Wakristo wa mapema. Utawala wake hautaendelea. Hata wale “wafalme” wadogo walio kama pembe waliotokana na Milki ya Roma hawataendelea. Hata hivyo, vipi juu ya tawala zilizotokana na serikali za awali zilizofananishwa na mnyama? Kama ilivyotabiriwa, maisha yao yalidumishwa “kwa wakati na majira.” Maeneo yao yameendelea kuwa na watu hadi leo. Kwa mfano, Iraki iko kwenye eneo la Babiloni ya Kale. Uajemi (Iran) na Ugiriki zingaliko. Mabaki ya serikali hizo za ulimwengu ni sehemu ya Umoja wa Mataifa. Falme hizo pia zitaangamia serikali ya ulimwengu ya mwisho itakapoangamizwa. Serikali zote za kibinadamu zitafutiliwa mbali kwenye “vita ya siku kubwa ya Mungu Mweza-Yote.” (Ufunuo 16:14, 16) Lakini, ni nani basi atakayeutawala ulimwengu?
UTAWALA WENYE KUDUMU U KARIBU!
36, 37. (a) ‘Mmoja aliye mfano wa mwana wa binadamu’ ni nani, naye alitokea kwenye Mahakama ya kimbingu lini na kwa kusudi gani? (b) Ni nini kilichosimamishwa mwaka wa 1914 W.K.?
36 “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama,” akasema Danieli kwa mshangao. “Mmoja aliye mfano wa mwanadamu [“mwana wa binadamu,” NW] akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye.” (Danieli 7:13) Alipokuwa duniani, Yesu Kristo alijiita “Mwana wa binadamu,” akionyesha uhusiano wake na wanadamu. (Mathayo 16:13; 25:31) Yesu aliiambia Sanhedrini, au mahakama kuu ya Kiyahudi hivi: “Mtaona Mwana wa binadamu ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” (Mathayo 26:64) Kwa hiyo, katika ono la Danieli, yule ajaye, asiyeonekana kwa macho ya kibinadamu, na kumwendea Yehova Mungu alikuwa Yesu Kristo aliyefufuliwa na kutukuzwa. Hilo lilitukia lini?
37 Mungu amefanya agano na Yesu Kristo kwa ajili ya Ufalme, kama vile tu alivyokuwa amefanya agano na Mfalme Daudi. (2 Samweli 7:11-16; Luka 22:28-30) “Nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa” zilipoisha mwaka wa 1914 W.K., Yesu Kristo, akiwa mrithi wa ufalme wa Daudi, alikuwa na haki ya kupokea utawala wa Ufalme. Rekodi ya kiunabii ya Danieli yasema hivi: “Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.” (Danieli 7:14) Kwa hiyo, Ufalme wa Kimesiya ulisimamishwa mbinguni mwaka wa 1914. Hata hivyo, wengine pia wanapewa utawala huo.
38, 39. Ni nani watakaopokea utawala udumuo milele juu ya dunia?
38 “Watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme,” akasema malaika. (Danieli 7:18, 22, 27) Yesu Kristo ndiye mtakatifu mkuu. (Matendo 3:14; 4:27, 30) Wale “watakatifu” wengine ambao watatawala naye ni wale Wakristo waaminifu watiwa-mafuta kwa roho 144,000, ambao ni warithi wa Ufalme pamoja na Kristo. (Waroma 1:7; 8:17; 2 Wathesalonike 1:5; 1 Petro 2:9) Wanafufuliwa wakiwa roho zisizoweza kufa ili watawale pamoja na Kristo katika Mlima Zayoni wa kimbingu. (Ufunuo 2:10; 14:1; 20:6) Kwa hiyo, Kristo Yesu na Wakristo watiwa-mafuta waliofufuliwa watautawala ulimwengu wa wanadamu.
39 Kuhusu utawala wa Mwana wa binadamu na wale “watakatifu” wengine waliofufuliwa, malaika wa Mungu alisema hivi: “Ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.” (Danieli 7:27) Wanadamu watiifu watabarikiwa kama nini chini ya Ufalme huo!
40. Twaweza kunufaikaje kwa kusikiliza ndoto na maono ya Danieli?
40 Danieli hakujua utimizo wote wa ajabu wa maono yake kutoka kwa Mungu. Alisema hivi: “Huu ndio mwisho wa jambo lile. Nami, Danieli, fikira zangu zilinifadhaisha, na uso wangu ulinibadilika; lakini naliliweka jambo hilo moyoni mwangu.” (Danieli 7:28) Hata hivyo, sisi twaishi wakati ambao twaweza kuelewa utimizo wa mambo aliyoona Danieli. Kusikiliza unabii huu kutaimarisha imani yetu na kutia nguvu usadikisho wetu kwamba Mfalme wa Kimesiya wa Yehova atautawala ulimwengu.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Sura ya 4 ya kitabu hiki.
b Ili kuwa wazi na kuepuka kurudia-rudia maneno, tutaambatanisha mistari yenye kufafanua maono, iliyo kwenye Danieli 7:15-28 kwa kuchunguza mstari kwa mstari maono yaliyorekodiwa kwenye Danieli 7:1-14.
c Ona Sura ya 6 ya kitabu hiki.
UMEFAHAMU NINI?
• Kila mmoja wa wale ‘wanyama wakubwa wanne wanaotoka baharini’ anafananisha nini?
• Ile pembe “ndogo” ni nini?
• “Watakatifu” walisumbuliwaje na pembe ndogo ya mfano wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza?
• Ni nini kitakachoipata pembe ndogo ya mfano na zile serikali nyingine za mnyama?
• Umenufaikaje kwa kusikiliza ndoto na maono ya Danieli juu ya “wanyama wakubwa wanne”?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 149-152]
MTAWALA MVUMILIVU
MWANDIKAJI Mgiriki wa karne ya tano K.W.K. alimkumbuka kuwa mtawala mzuri. Katika Biblia anaitwa “masihi” wa Mungu na “ndege mkali” atokaye “mashariki.” (Isaya 45:1; 46:11) Mtawala asemwaye hivyo ni Koreshi Mkuu, wa Uajemi.
Koreshi alianza kupata fahari mwaka wa 560/559 K.W.K. hivi, alipomwandama baba yake Cambyses wa Kwanza katika kiti cha ufalme cha Anshan, jiji au wilaya katika Uajemi ya kale. Wakati huo, Anshan ilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Astyages wa Umedi. Akiasi dhidi ya utawala wa Umedi, Koreshi alipata ushindi wa haraka kwa kuwa jeshi la Astyages lilijiunga naye. Kisha Wamedi wakawa washikamanifu kwa Koreshi. Tangu wakati huo, Wamedi na Waajemi waliungana pamoja vitani chini ya uongozi wake. Ndivyo utawala wa Umedi na Uajemi ulivyotokea, utawala ambao ulipanuka kutoka Bahari ya Aegea hadi Mto Indus.—Ona ramani.
Akiwa na jeshi la muungano la Wamedi na Waajemi, Koreshi alipiga hatua ili kudhibiti sehemu yenye matata—sehemu ya magharibi ya Umedi ambapo Mfalme Croesus wa Lidia alikuwa akipanua milki yake kuingia katika eneo la Umedi. Akisonga mbele kuelekea mpaka wa mashariki wa Milki ya Lidia katika Asia Ndogo, Koreshi alimshinda Croesus, akateka Sardisi, jiji lake kuu. Kisha Koreshi akashinda majiji ya Kigiriki na kuweka Asia Ndogo yote chini ya Milki ya Umedi na Uajemi. Kwa hiyo, akawa mpinzani mkubwa wa Babiloni na mfalme wake Nabonido.
Kisha Koreshi akajitayarisha kukabiliana na Babiloni lenye nguvu. Tangu hapo na kuendelea, akaanza kutimiza unabii wa Biblia. Kupitia nabii Isaya, karibu karne mbili mapema, Yehova alikuwa amemtaja Koreshi kuwa mtawala ambaye angeshinda Babiloni na kuwaweka Wayahudi huru kutoka kifungoni. Maandiko humwita Koreshi “masihi” wa Yehova kwa kuwa alichaguliwa mapema.—Isaya 44:26-28.
Koreshi alipoliendea Babiloni mwaka wa 539 K.W.K., alikuwa na jukumu gumu. Likiwa limezungukwa na kuta kubwa na handaki pana lenye kina kirefu lililofanyizwa na mto Eufrati, jiji hilo lilionekana kuwa lisiloweza kushindwa. Mahali ambapo Eufrati ulipitia Babiloni, ukuta mkubwa kama mlima, wenye malango ya shaba ulienda sambamba na kingo za mto. Koreshi angewezaje kushinda Babiloni?
Zaidi ya karne moja mapema, Yehova alikuwa ametabiri ‘ukosefu wa mvua juu ya maji yake’ akasema kwamba “yatakaushwa.” (Yeremia 50:38) Kama unabii huo ulivyosema, Koreshi aligeuza mkondo wa maji ya Mto Eufrati kilometa chache kaskazini mwa Babiloni. Kisha jeshi lake lilipitia matopeni likiteremka kwenye sakafu ya mto, likapanda kilima kilichoelekea ukutani, na kuingia jiji hilo kwa urahisi kwa kuwa malango yake ya shaba yalikuwa yameachwa wazi. Kama “ndege mkali” arukiaye windo lake haraka, mtawala huyo “kutoka mashariki” aliteka Babiloni kwa usiku mmoja!
Kwa Wayahudi waliokuwa Babiloni, ushindi wa Koreshi ulimaanisha kuachiliwa kutoka utekwa kulikongojewa sana na mwisho wa ule ukiwa wa miaka 70 wa nchi ya kwao. Lazima wawe walisisimuka kama nini Koreshi alipotoa tangazo lenye kuwaidhinisha warudi Yerusalemu na kujenga upya hekalu! Koreshi aliwarudishia pia vyombo vitakatifu ambavyo Nebukadreza alikuwa amepeleka Babiloni, akawapa idhini ya kuagiza mbao kutoka Lebanoni, na kuidhinisha fedha kutoka kwa nyumba ya mfalme zilipie gharama za ujenzi.—Ezra 1:1-11; 6:3-5.
Kwa ujumla Koreshi alikuwa mvumilivu aliposhughulika na watu aliowashinda. Huenda ikawa sababu moja ya kuwa hivyo ilikuwa dini yake. Yamkini, Koreshi alishikamana na mafundisho ya nabii Mwajemi Zoroaster na kumwabudu Ahura Mazda—mungu adhaniwaye kuwa ndiye aliyeumba vitu vyote vizuri. Katika kitabu chake The Zoroastrian Tradition, Farhang Mehr aandika hivi: “Zoroaster alisema kwamba Mungu ni ukamilifu wa kiadili. Aliwaambia watu kwamba Ahura Mazda halipizi kisasi bali ni mwenye haki na, kwa hiyo, hapasi kuogopwa bali kupendwa.” Huenda ikawa itikadi katika mungu mwenye maadili na mwenye haki iliathiri maadili ya Koreshi na kumchochea awe mvumilivu na mwenye haki.
Hata hivyo, mfalme hakuvumilia sana halihewa ya Babiloni. Hakutaka kuvumilia yale majira yenye joto jingi. Kwa hiyo, ingawa Babiloni liliendelea kuwa jiji la kifalme la milki hiyo, na vilevile kituo cha kidini na kitamaduni, mara nyingi lilitumika kama jiji kuu wakati wa majira ya baridi kali tu. Kwa hakika, baada ya kushinda Babiloni, Koreshi alirudi kwenye jiji lake kuu la wakati wa kiangazi, Ecbatana, lililokuwa meta 1,900 juu ya usawa wa bahari, chini ya Mlima Alwand. Huko, alipenda yale majira ya baridi kali yaliyosawazishwa na majira ya joto yenye kumpendeza. Koreshi alijenga pia jumba tukufu la kifalme katika jiji kuu la awali, Pasargadae, (karibu na Persepolisi), yapata kilometa 650 kusini-mashariki mwa Ecbatana. Makao hayo yalikuwa kimbilio lake.
Kwa hiyo, Koreshi akumbukwa kuwa mshindi mwenye ujasiri na mtawala mvumilivu. Utawala wake wa miaka 30 ulimalizika alipokufa mwaka wa 530 K.W.K. alipokuwa katika kampeni ya kijeshi. Mwana wake Cambyses wa Pili akamfuata kwenye utawala huo wa Uajemi.
UMEFAHAMU NINI?
• Koreshi Mwajemi alithibitikaje kuwa “masihi” wa Yehova?
• Koreshi aliwafanyia watu wa Yehova utumishi gani wa maana?
• Koreshi aliwatendeaje watu aliowashinda?
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MILKI YA UMEDI NA UAJEMI
MAKEDONIA
Memphis
MISRI
ETHIOPIA
Yerusalemu
Babiloni
Ecbatana
Susa
Persepolisi
INDIA
[Picha]
Kaburi la Koreshi, huko Pasargadae
[Picha]
Sanamu ya Koreshi iliyo Pasargadae
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 153-161]
MTAWALA MCHANGA AUSHINDA ULIMWENGU
MIAKA 2,300 hivi iliyopita, jenerali wa kijeshi mwenye nywele za manjano, mwenye umri wa miaka 20 na kitu alisimama ukingoni mwa Bahari ya Mediterania. Alikaza macho yake kwenye jiji lililokuwa kisiwa umbali wa karibu kilometa moja. Akiwa amekatazwa kuingia, jenerali huyo mwenye hasira aliazimu kulishinda jiji hilo. Alipanga kushambuliaje? Alipanga kujenga barabara iliyoinuka juu kwenye maji hadi kisiwani na kuyapanga majeshi yake yakapige vita dhidi ya jiji hilo. Ujenzi wa barabara hiyo tayari ulikuwa umeanza.
Lakini ujumbe kutoka kwa mfalme mkuu wa Milki ya Uajemi ulimkatiza jenerali huyo kijana. Akitaka sana kufanya amani, mtawala wa Uajemi aliahidi jambo lisilo la kawaida: Talanta 10,000 za dhahabu (zaidi ya dola bilioni mbili za Marekani kwa thamani ya kisasa), aoe mmoja wa binti za mfalme, na sehemu yote ya magharibi ya Milki ya Uajemi. Mfalme aliahidi yote hayo ili kuipata familia yake, ambayo jenerali huyo alikuwa ameiteka.
Kamanda aliyepaswa kuamua kukubali au kukataa toleo hilo alikuwa Aleksanda wa Tatu wa Makedonia. Je, akubali toleo hilo? “Ilikuwa pindi muhimu kwa ulimwengu wa kale,” asema mwanahistoria Ulrich Wilcken. “Matokeo ya uamuzi wake, kwa kweli, yameenea katika Enzi za Kati hadi siku zetu wenyewe, Mashariki na vilevile Magharibi.” Kabla ya kufikiria jibu la Aleksanda, acheni tuone ni matukio gani yaliyotangulia pindi hiyo muhimu.
MALEZI YA ALEKSANDA
Aleksanda alizaliwa Pella, Makedonia, mwaka wa 356 K.W.K. Baba yake alikuwa Mfalme Philip wa Pili, na mama yake alikuwa Olympias. Aleksanda alifundishwa na mama yake kwamba wafalme wa Makedonia walitokana na Hercules, mwana wa mungu wa Wagiriki, Zeus. Kulingana na Olympias, Achilles—yule mhusika mkuu wa shairi la Homer liitwalo Iliad—alikuwa babu wa zamani wa Aleksanda. Baada ya kufundishwa hivyo na wazazi wake kwa ajili ya ushindi na utukufu wa kifalme, Aleksanda mchanga hakupendezwa sana na mambo mengine. Alipoulizwa ikiwa angekimbia mbio fulani kwenye Michezo ya Olimpiki, Aleksanda alidokeza kwamba angekimbia iwapo tu angekimbia na wafalme. Alikuwa na tamaa ya kufanya mambo makuu kuliko baba yake na kupata utukufu kupitia mambo aliyotimiza.
Akiwa na umri wa miaka 13, Aleksanda alifundishwa na Aristotle, mwanafalsafa Mgiriki, ambaye alimsaidia kukuza upendezi katika falsafa, tiba, na sayansi. Watu wana maoni tofauti juu ya kiwango ambacho mafundisho ya Aristotle ya falsafa yaliathiri njia ya kufikiri ya Aleksanda. “Yaelekea kuwa sahihi kusema kwamba kuna mambo mengi ambayo watu hao wawili hawakukubaliana,” akaonelea Bertrand Russell, mwanafalsafa wa karne ya 20. “Maoni ya kisiasa ya Aristotle yalitegemea serikali za jiji za Ugiriki zilizokuwa zikielekea kutoweka.” Ile dhana ya serikali ndogo ya jiji haingemvumtia mwana-mfalme mwenye kutaka makuu aliyetaka kujenga milki kubwa yenye utawala mmoja. Lazima Aleksanda alitilia shaka sera ya Aristotle ya kuwatumikisha wasio Wagiriki kwa kuwa alitarajia milki yenye ushirikiano mzuri kati ya washindi na washinde.
Hata hivyo, hakuna shaka kwamba Aristotle alikuza kupendezwa kwa Aleksanda katika kusoma na kujifunza. Aleksanda aliendelea kuwa msomaji mwenye bidii katika maisha yake yote, akipendezwa hasa na maandishi ya Homer. Yadaiwa kwamba alikariri mistari yote 15,693 ya shairi liitwalo Iliad.
Kuelimishwa na Aristotle kulikoma ghafula mwaka wa 340 K.W.K. wakati ambapo mwana-mfalme huyo mwenye umri wa miaka 16 alirudi Pella akatawale Makedonia kwa kuwa baba yake hakuwako. Upesi, mrithi huyo wa kiti cha ufalme akaonyesha uhodari wake kivita. Alilikomesha haraka Maedi, kabila la Thrasi lililoasi, akateka jiji lao kuu mara moja, na kupaita mahali hapo Alexandroúpolis, kutokana na jina lake mwenyewe, jambo lililomfurahisha sana Philip.
KUENDELEA NA USHINDI
Aleksanda alirithi kiti cha ufalme cha Makedonia mwaka wa 336 K.W.K., akiwa na umri wa miaka 20 Philip alipouawa. Akiingia Asia kupitia Hellespont (paitwapo Dardanelles leo) mapema Mei mwaka wa 334 K.W.K., Aleksanda alianzisha kampeni ya ushindi akiwa na jeshi dogo lakini hodari la askari-jeshi 30,000 wa miguu na askari wapanda-farasi 5,000. Wahandisi, mabwana-pima, wasanifuujenzi, wanasayansi, na wanahistoria waliandamana na jeshi lake.
Kwenye Mto Granicus upande wa kaskazini magharibi mwa Asia Ndogo (leo inaitwa Uturuki), Aleksanda alishinda vita yake ya kwanza dhidi ya Uajemi. Katika kipindi cha majira ya baridi kali cha wakati huo alishinda sehemu ya magharibi ya Asia Ndogo. Katika masika ya mwaka wa 333 K.W.K. vita vingine vya kukata maneno dhidi ya Uajemi vilipiganwa Issus, upande wa kusini-mashariki mwa Asia Ndogo. Akiwa na jeshi la watu wapatao nusu milioni, Mfalme mkuu wa Uajemi, Dario wa Tatu, akaja kupigana na Aleksanda. Akiwa na uhakika kupita kiasi, Dario akaja pia na mama yake, mke wake, na washiriki wengine wa familia yake ili washuhudie kile ambacho kilipaswa kuwa ushindi mkubwa ajabu. Lakini Waajemi hawakuwa tayari kukabili shambulio la Wamakedonia la ghafula na lenye nguvu. Majeshi ya Aleksanda yalilishinda kabisa jeshi la Uajemi, na Dario akakimbia, akaiacha familia yake mikononi mwa Aleksanda.
Badala ya kuwafuata Waajemi waliokuwa wakikimbia, Aleksanda alielekea kusini kandokando ya Pwani ya Mediterania, akishinda vituo vilivyotumiwa na meli zenye nguvu za Uajemi. Lakini Tiro, kisiwa kilichokuwa jiji, kilikinza uvamizi. Akiwa ameazimia kulishinda, Aleksanda alianza mazingiwa yaliyodumu miezi saba. Wakati wa mazingiwa hayo ndipo Dario alipotoa ahadi iliyotajwa awali. Mambo yaliyoahidiwa yalikuwa yenye kuvutia sana hivi kwamba Parmenio, mshauri ambaye Aleksanda alimtumaini, aripotiwa kuwa alisema: ‘Ningalikuwa Aleksanda, ningalikubali.’ Lakini jenerali huyo mchanga akajibu hivi: ‘Hata mimi ningefanya hivyo, ikiwa ningekuwa Parmenio.’ Akikataa kufanya mapatano, Aleksanda aliendelea na mazingiwa na kuharibu Tiro mwezi wa Julai mwaka wa 332 K.W.K.
Akiliacha Yerusalemu, lililosalimu amri mbele zake, Aleksanda alisonga mbele kuelekea kusini, na kushinda Gaza. Wakiwa wamechoshwa na utawala wa Uajemi, Misri ilimkaribisha kama mwokozi. Huko Memphis, aliwapendeza makuhani wa Misri kwa kumtolea dhabihu mungu Apis mwenye sura ya fahali. Alianzisha pia jiji la Aleksandria, ambalo baadaye lilishindana na Athene likiwa kituo cha kujifunza nalo bado laitwa hivyo.
Kisha, Aleksanda akageuka kuelekea kaskazini-mashariki, akipitia Palestina na kuelekea Mto Tigris. Mwaka wa 331 K.W.K., alipigana vita kubwa ya tatu dhidi ya Uajemi, huko Gaugamela, karibu na magofu ya Ninewi. Huko, askari-jeshi 47,000 wa Aleksanda walilishinda nguvu jeshi la Uajemi lililopangwa upya la angalau askari-jeshi 250,000! Dario alikimbia na baadaye akauawa na watu wake mwenyewe.
Akiwa amesisimuka kwa sababu ya ushindi, Aleksanda aligeuka na kuelekea kusini na kulitwaa Babiloni, jiji kuu la Uajemi la wakati wa majira ya baridi kali. Pia alimiliki majiji makuu huko Susa na Persepolisi, akanyakua hazina kubwa ya Uajemi na kuyachoma makao makuu ya mfalme Shasta. Hatimaye, jiji kuu la Ecbatana likaanguka mikononi mwake. Mshindi huyo wa haraka akatiisha sehemu iliyosalia ya milki ya Uajemi, akienda mbali upande wa mashariki hadi Mto Indus, ulio katika Pakistan ya leo.
Alipovuka Indus, mpakani mwa mkoa wa Uajemi uitwao Taxila, Aleksanda alikutana na mpinzani mgumu sana, Porus, mtawala wa India. Aleksanda alipigana vita yake kubwa ya nne na ya mwisho dhidi yake mwezi wa Juni mwaka wa 326 K.W.K. Jeshi la Porus lilitia ndani askari-jeshi 35,000 na tembo 200, ambao waliwaogofya farasi wa Wamakedonia. Vita hivyo vilikuwa vikali na watu wengi walikufa, lakini majeshi ya Aleksanda yakashinda. Porus alisalimu amri na kujiunga nao.
Zaidi ya miaka minane ilikuwa imepita tangu jeshi la Makedonia livuke na kuingia Asia, nao askari-jeshi walikuwa wachovu na walitamani kurudi nyumbani. Wakiwa wamechoshwa na vile vita vikali dhidi ya Porus, walitaka kurudi nyumbani. Ingawa alisitasita mwanzoni, Aleksanda alikubali waliyotaka. Kwa kweli, Ugiriki ilikuwa imekuwa serikali ya ulimwengu. Koloni za Ugiriki zikiwa zimeanzishwa katika nchi zilizoshindwa, lugha na utamaduni wa Kigiriki zikaenea kotekote katika milki hiyo.
KIONGOZI WA JESHI HILO
Utu wa Aleksanda uliliunganisha jeshi la Makedonia kwa miaka yote hiyo. Baada ya vita, Aleksanda alikuwa na desturi ya kuwatembelea waliojeruhiwa, kuchunguza majeraha yao, kuwasifu askari-jeshi kwa sababu ya matendo yao ya kishujaa, na kuwapa zawadi za fedha kwa sababu ya mambo waliyotimiza. Aleksanda alipanga wale waliokufa vitani wazikwe kwa fahari. Wazazi na watoto wa watu waliokufa hawakutakiwa kulipa kodi wala kufanya aina fulani za utumishi. Ili kugeuza fikira baada ya vita, Aleksanda alipanga michezo na mashindano. Pindi moja, hata aliwapa wanaume waliokuwa wameoa karibuni likizo, ikiwawezesha kuwa na wake zao wakati wa majira ya baridi kali, huko Makedonia. Matendo hayo yalifanya watu wake wampende na kuvutiwa naye.
Kuhusu Aleksanda kumwoa Roxana, Binti-Mfalme wa Bactria, mwandika-wasifu Mgiriki Plutarch aandika hivi: “Kwa kweli, walipendana, na kwa wakati uleule ilionekana kama jambo hilo lilifaa kusudi lake. Kwa kuwa watu aliowashinda waliridhika kumwona akimchagua mke miongoni mwao, na kuwafanya wampende sana, kwa kuona kwamba hata katika upendo pekee ambao ulimshinda yeye, mtu asiyeonyesha hisia sana, alijidhibiti hadi alipoweza kumwoa kihalali kwa njia yenye kuheshimika.”
Aleksanda aliheshimu pia ndoa za wengine. Ingawa mke wa Mfalme Dario alikuwa mateka wake, alihakikisha kwamba alitendewa kwa njia ya heshima. Hali kadhalika, alipopata kujua kwamba askari-jeshi wawili wa Makedonia walikuwa wamewatenda vibaya wake za wageni fulani, aliagiza wauawe ikiwa wangepatikana na hatia.
Sawa na mama yake, Olympias, Aleksanda alikuwa mtu wa dini kwelikweli. Alitoa dhabihu kabla na baada ya vita naye aliwasiliana na wanajimu wake ili kujua maana ya ishara fulani za mambo ya wakati ujao. Pia aliwasiliana na mwaguzi wa Ammon, huko Libya. Na akiwa Babiloni alitekeleza maagizo ya Wakaldayo kuhusu kutoa dhabihu, hasa kwa mungu wa Babiloni, Bel (Marduki).
Ingawa Aleksanda alikuwa na kiasi katika mazoea yake ya kula, hatimaye alianza kunywa kupindukia. Kwa kadiri alivyokunywa, ndivyo alivyoongea sana na kujisifia mafanikio yake. Mojawapo ya matendo maovu zaidi aliyofanya Aleksanda lilikuwa kumwua rafiki yake Clitus, akiwa na hasira za ulevi. Lakini Aleksanda alijilaumu sana hivi kwamba alilala siku tatu kitandani, bila kula wala kunywa. Hatimaye, rafiki zake walifaulu kumshawishi ale.
Kadiri wakati ulivyopita, tamaa ya Aleksanda ya kupata utukufu ilimfanya atokeze vitabia vingine visivyopendeza. Alianza kusadiki kwa urahisi mashtaka yasiyo ya kweli na kuanza kutoa adhabu kali sana. Kwa mfano, baada ya kufanywa aamini kwamba Philotas alihusika katika jaribio la kumwua, Aleksanda aliagiza yeye na baba yake, Parmenio, ambaye alikuwa mshauri aliyemtumaini wakati mmoja, wauawe.
KUSHINDWA KWA ALEKSANDA
Punde baada ya kurudi Babiloni, Aleksanda akaugua malaria, naye hakupona. Juni 13, 323 K.W.K., baada ya kuishi miaka 32 na miezi 8 tu, Aleksanda akasalimu amri mikononi mwa adui mwenye kutisha zaidi, kifo.
Ni kama vile tu watu fulani wenye hekima wa India walivyosema: “Ee Mfalme Aleksanda, kila mtu humiliki kiasi kidogo tu cha dunia kama mahali hapa tunaposimama; na kwa kuwa u mwanadamu kama wanadamu wengine, isipokuwa tu kwamba una utendaji mwingi na bidii, wazurura kotekote katika dunia hii mbali na nyumbani kwako, ukisumbuka, na kuwasumbua wengine. Lakini punde si punde utakufa, nawe utamiliki kiasi cha dunia kinachotosha maziko yako.”
UMEFAHAMU NINI?
• Aleksanda Mkuu alikuwa na malezi ya aina gani?
• Punde baada ya kurithi kiti cha ufalme cha Makedonia, Aleksanda alianzisha kampeni gani?
• Fafanua baadhi ya ushindi mbalimbali wa Aleksanda.
• Aleksanda alikuwa mtu wa aina gani?
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
USHINDI MBALIMBALI WA ALEKSANDA
MAKEDONIA
MISRI
Babiloni
Mto Indus
[Picha]
Aleksanda
[Picha]
Aristotle na mwanafunzi wake Aleksanda
[Picha]
[Picha]
Medali isemwayo kwamba ina picha ya Aleksanda Mkuu
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 162, 163]
UFALME MKUBWA WAGAWANYIKA
KUHUSU ufalme wa Aleksanda Mkuu, Biblia ilitabiri ungevunjika na kugawanyika “lakini hautakuwa wa uzao wake.” (Danieli 11:3, 4) Kwa hiyo, miaka 14 baada ya Aleksanda kufa ghafula mwaka wa 323 K.W.K., mwana wake mwenyewe, Aleksanda wa Nne, na mwana haramu wake Heracles waliuawa.
Kufikia mwaka wa 301 K.W.K., wanne kati ya majenerali wa Aleksanda walijiimarisha katika mamlaka juu ya milki kubwa ambayo kamanda wao alikuwa ameijenga. Jenerali Kasanda alitawala Makedonia na Ugiriki. Jenerali Lisimako akapokea Asia Ndogo na Thrasi. Seleuko Niketa wa Kwanza akapokea Mesopotamia na Siria. Naye Ptolemy Lagus, au Ptolemy wa Kwanza, akatawala Misri na Palestina. Kwa hiyo, ufalme mmoja mkubwa wa Aleksanda ukatokeza falme nne za Kigiriki.
Kati ya zile falme nne za Kigiriki, ufalme wa Kasanda ndio uliodumu muda mfupi zaidi. Miaka michache baada ya Kasanda kupata mamlaka, wazao wake wa kiume wakafa, na mwaka wa 285 K.W.K., Lisimako akatwaa sehemu ya Ulaya ya Milki ya Ugiriki. Miaka minne baadaye, Lisimako akashindwa vitani dhidi ya Seleuko Niketa wa Kwanza, ikifanya Seleuko atawale sehemu kubwa ya eneo la Asia. Seleuko akawa mtawala wa kwanza katika wafalme wa nasaba yake huko Siria. Alianzisha Antiokia katika Siria na kulifanya kuwa jiji lake kuu jipya. Seleuko aliuawa mwaka wa 281 K.W.K., lakini utawala wake aliouanzisha uliendelea kuwa na mamlaka hadi mwaka wa 64 K.W.K. wakati ambapo Jenerali Mroma Pompey alifanya Siria kuwa mkoa wa Roma.
Kati ya ile migawanyiko minne ya milki ya Aleksanda, ufalme wa Ptolemy ndio uliodumu muda mrefu zaidi. Ptolemy wa Kwanza alianza kuitwa mfalme mwaka wa 305 K.W.K. naye akawa mfalme wa kwanza wa Makedonia, au Farao wa kwanza wa Misri. Akilifanya Aleksandria kuwa jiji lake kuu, alianzisha programu ya kusitawisha jiji hilo mara moja. Mojawapo ya majengo yake makuu zaidi lilikuwa ile Maktaba maarufu ya Aleksandria. Ili kuusimamia mradi huo mkubwa, Ptolemy alimleta Demetrius Phalereus, msomi Mwathene kutoka Ugiriki. Yaripotiwa kwamba kufikia karne ya kwanza W.K., maktaba hiyo ilikuwa na hatikunjo milioni moja. Nasaba ya Ptolemy iliendelea kutawala Misri hadi ilipoanguka mikononi mwa Roma mwaka wa 30 K.W.K. Kisha Roma ikawa serikali kuu ya ulimwengu badala ya Ugiriki.
UMEFAHAMU NINI?
• Milki kubwa ya Aleksanda iligawanyikaje?
• Nasaba ya wafalme wa Seleuko iliendelea kutawala Siria hadi lini?
• Nasaba ya Ptolemy huko Misri ilikoma kutawala lini?
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KUVUNJIKA KWA MILKI YA ALEKSANDA
Kasanda
Lisimako
Ptolemy wa Kwanza
Seleuko wa Kwanza
[Picha]
Ptolemy wa I
Seleuko wa I
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 139]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
SERIKALI ZA ULIMWENGU ZA UNABII WA DANIELI
Ile sanamu kubwa (Danieli 2:31-45)
Wanyama wanne kutoka baharini (Danieli 7:3-8, 17, 25)
BABILONIA tangu 607 K.W.K.
UMEDI NA UAJEMI tangu 539 K.W.K.
UGIRIKI tangu 331 K.W.K.
ROMA tangu 30 K.W.K.
SERIKALI YA ULIMWENGU YA UINGEREZA NA MAREKANI tangu 1763 W.K.
ULIMWENGU ULIOGAWANYIKA KISIASA wakati wa mwisho
[Picha katika ukurasa wa 128]
[Picha katika ukurasa wa 147]