Sura Ya Kumi Na Nane
Yehova Ahuisha Roho ya Wanyenyekevu
1. Yehova alitoa uhakikisho gani, na maneno yake yanatokeza maswali gani?
“YEYE aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua [“kuhuisha,” NW] roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.” (Isaya 57:15) Hivyo ndivyo alivyoandika nabii Isaya katika karne ya nane K.W.K. Ni nini kilichokuwa kikiendelea Yuda ambacho kilifanya ujumbe huo uwe wenye kutia moyo sana? Maneno haya yaliyopuliziwa yanawasaidiaje Wakristo leo? Mazungumzo ya Isaya sura ya 57 yatatusaidia kujibu maswali hayo.
“Ninyi Karibuni Hapa”
2. (a) Inaelekea kwamba maneno ya Isaya sura ya 57 yanatumika wakati gani? (b) Hali ya wenye haki ikoje siku za Isaya?
2 Sehemu hii ya unabii wa Isaya inaonekana kuwa inatumika katika siku za Isaya mwenyewe. Fikiria jinsi ambavyo uovu umekolea sasa: “Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya. Yeye huingia katika amani; wao hustarehe katika vitanda vyao, kila mtu aendaye katika unyofu wake.” (Isaya 57:1, 2) Mtu mwenye haki akianguka, hakuna anayejali. Akifa mapema mno, watu hawajali. Yeye hupata amani kwa kulala usingizi wa kifo; hiyo humwondolea mateso aliyoletewa na wasiomhofu Mungu, na ni njia ya kumwepusha na mabaya. Taifa teule la Mungu limezorota likawa na hali ya kusikitisha sana. Lakini, bila shaka wale wanaobaki wakiwa waaminifu wanatiwa moyo kweli kweli kwa kujua kwamba, licha ya kuona yanayoendelea,Yehova atawategemeza pia!
3. Yehova anatumia usemi wa namna gani anapoongea na kizazi kiovu cha Yuda, na kwa nini?
3 Yehova anakiita kizazi kiovu cha Yuda kimjie, akisema hivi: “Lakini ninyi karibuni hapa, enyi wana wa mwanamke mchawi [“mwaguzi,” “NW”], uzao wa mzinzi na kahaba.” (Isaya 57:3) Wamestahili kuitwa majina ya aibu, yaani wana wa mwanamke mwaguzi na wazao wa mzinzi na wa kahaba. Ibada ya uwongo ambayo wamegeukia inahusisha matendo ya kuchukiza sana ya ibada ya sanamu na uwasiliani-roho, na vilevile mazoea ya ngono zisizo za adili. Kwa hiyo, Yehova anawauliza hivi watenda-dhambi hao: “Mnafanya dhihaka [“mnakula raha,” “NW”] yenu juu ya nani? Mmepanua vinywa vyenu, na kutoa ndimi zenu? je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo; ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi; ninyi mnaoua watoto mabondeni, chini ya mianya ya majabali?”—Isaya 57:4, 5.
4. Waovu wa Yuda wana hatia ya jambo gani?
4 Waovu wa Yuda wanafanya ibada ya upagani yenye kuchukiza sana hadharani, ‘wakila raha.’ Wanawacheka-cheka manabii wa Mungu ambao wametumwa kuwarekebisha, wakiwatolea ndimi zao kwa madharau, bila aibu. Ingawa wao ni watoto wa Abrahamu, njia zao za uasi zinawafanya wawe wana wa uasi na uzao wa uwongo. (Isaya 1:4; 30:9; Yohana 8:39, 44) Wakiwa kule nje mashambani, miongoni mwa miti mikubwa, wanachochea vishindo vingi vya kidini katika ibada ya sanamu. Nayo ni ibada ya ukatili we! Kwani, hata wanachinja watoto wao wenyewe kama yale mataifa yaliyofukuzwa na Yehova nchini kwa sababu ya machukizo yao makubwa!—1 Wafalme 14:23; 2 Wafalme 16:3, 4; Isaya 1:29.
Kuyamwagia Mawe Toleo la Kinywaji
5, 6. (a) Wakaaji wa Yuda wamechagua kufanya nini badala ya kumwabudu Yehova? (b) Ibada ya sanamu ya Yuda inafanywaje waziwazi bila kujali, na imeenea kiasi gani?
5 Ebu ona jinsi ambavyo wakaaji wa Yuda wameingilia sana ibada ya sanamu: “Mnachagua mawe laini mabondeni, na kuyafanya kitovu cha maisha yenu. Mnayamiminia dhabihu ya kinywaji na kuyapelekea dhabihu ya nafaka! Je, mimi nitaridhishwa kwa vitu hivyo?” (Isaya 57:6, “BHN”) Wayahudi ni watu wa agano la Mungu, lakini badala ya kumwabudu yeye, wanaokota mawe chini ya mto na kuyafanya miungu. Daudi alitangaza kwamba Yehova ndiye fungu la maisha yake, lakini watenda-dhambi hawa wameamua kuabudu sanamu za mawe zisizo na uhai, na wanazimwagia matoleo ya vinywaji. (Zaburi 16:5; Habakuki 2:19) Yehova atawezaje kuridhika, na huku watu wanaoitwa kwa jina lake wanapotosha ibada jinsi hiyo?
6 Kila mahali—chini ya miti mikubwa, katika mabonde ya mito, juu ya vilima, katika majiji yao—Yuda anaabudu sanamu. Lakini Yehova anaona yote, na anamtumia Isaya kufichua upotovu wa nchi hiyo: “Umeweka kitanda chako juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; ukaenda huko ili kutoa dhabihu. Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako.” (Isaya 57:7-8a) Yuda anatandika kitanda chake chenye uchafu wa kiroho katika sehemu za juu, kisha anaitolea miungu ya kigeni dhabihu juu ya kitanda hicho.a Hata nyumba za watu binafsi zina sanamu nyuma ya milango na kwenye miimo ya milango.
7. Yuda anaingilia ibada ya kukosa adili akiwa na roho gani?
7 Huenda wengine wakashangaa wakijiuliza imekuwaje hata Yuda akahusika sana katika ibada chafu. Je, nguvu fulani yenye uwezo kumpita imemlazimisha kumwacha Yehova? La. Yeye anafanya hivyo kwa hiari, kwa hamu nyingi. Yehova anasema hivi: “Umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona [“ulikiangalia kiungo cha mwanamume,” “NW”].” (Isaya 57:8b) Yuda amefanya agano pamoja na miungu ya uwongo, na anaupenda uhusiano wake haramu pamoja na miungu hiyo. Hasa anayapenda mazoea ya ngono zisizo za adili, ambayo inaelekea kuwa yanahusu kutumia vitu vinavyofananisha kiungo cha uzazi cha mwanamume. Na hilo ni jambo la kawaida katika ibada ya miungu hiyo!
8. Ibada ya sanamu ilisitawi katika Yuda chini ya mfalme yupi hasa?
8 Maelezo hayo kuhusu ibada ya sanamu yenye ukatili na ukosefu mwingi sana wa adili yanalingana na yale tunayojua kuhusu wafalme kadhaa waovu wa Yuda. Kwa mfano, Manase alijenga sehemu za juu, akamsimamishia Baali madhabahu nyingi, na kuweka madhahabu za dini ya uwongo ndani ya nyua mbili za hekalu. Alifanya wanawe wapite katika moto, akazoea mizungu ya uchawi, akatumia uaguzi, na kuendeleza mazoea ya uwasiliani-roho. Mfalme Manase pia aliweka ndani ya hekalu la Yehova mfano wa kuchongwa wa mti mtakatifu aliokuwa ameutengeneza.b Alitongoza Yuda “wafanye mabaya, kuliko mataifa BWANA aliowaharibu mbele za wana wa Israeli.” (2 Wafalme 21:2-9) Wengine huamini kwamba Manase ndiye aliyeagiza Isaya auawe, ingawa jina la Manase halionekani katika Isaya 1:1.
‘Uliendelea Kuwatuma Wajumbe Wako’
9. Kwa nini Yuda anatuma wajumbe “mbali”?
9 Kosa la Yuda halikuwa kutumikia miungu ya uwongo tu. Akimtumia Isaya kama msemaji wake, Yehova anasema hivi: “Ulimwendea mfalme [“Meleki,” “NW”] na mafuta ya marhamu, ukaongeza manukato yako, ukawatuma wajumbe wako waende mbali, ukajidhili sana hata kuzimu [“Sheoli,” “NW”].” (Isaya 57:9) Ufalme wa Yuda usio na uaminifu unateremka kumwendea “Meleki,” neno ambalo kwa Kiebrania linamaanisha “aliye mfalme,” ambaye yaelekea kuwa ni mfalme wa mamlaka ya kigeni. Walimtolea mfalme huyo zawadi za bei kubwa, tena za kuvutia, zinazofananishwa na mafuta ya marhamu na manukato. Yuda anatuma wajumbe sehemu za mbali. Kwa nini? Ili kushawishi mataifa yasiyo ya Kiyahudi kufanya mapatano ya kisiasa naye. Akiisha kumpa Yehova kisogo, anawatumainia wafalme wa kigeni.
10. (a) Mfalme Ahazi anatafutaje njia ya kuungana na mfalme wa Ashuru? (b) Yuda ‘anajidhili sana hata Sheoli’ jinsi gani?
10 Mfano mmoja wa jambo hilo unapatikana siku za Mfalme Ahazi. Mfalme huyo asiye mwaminifu wa Yuda anaona ametishwa na muungano wa Israeli na Shamu, kwa hiyo anatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru, Tiglathi-pileseri wa Tatu, akisema hivi: “Mimi ni mtumishi, tena mwana wako; kwea, ukaniokoe mkononi mwa mfalme wa Shamu, na mkononi mwa mfalme wa Israeli, walioniinukia.” Ahazi anapeleka fedha na dhahabu ziwe rushwa kwa mfalme wa Ashuru, naye mfalme huyo anajibu kwa kushambulia Shamu vikali na kuiharibu. (2 Wafalme 16:7-9) Yuda anajiinamisha hadi kwenye “vilindi vya Sheoli” anapofanya shughuli zake na mataifa yasiyo ya Kiyahudi. (An American Translation) Kwa sababu ya shughuli hizo, atakufa, au akome kuwa taifa huru lenye mfalme.
11. Yuda anahisi usalama gani wa uwongo?
11 Yehova anaendelea kumwambia Yuda hivi: “Ulikuwa umechoka kwa ajili ya urefu wa njia yako; lakini hukusema, Hapana matumaini; ulipata kuhuishwa nguvu zako; kwa sababu hiyo hukuugua.” (Isaya 57:10) Naam, taifa hilo limechoka sana huku likifuata njia zake za uasi-imani, na linashindwa kuona kwamba jitihada zake hazina tumaini. Linajipumbaza kuamini kwamba linafanikiwa kwa nguvu zake lenyewe. Linajihisi kuwa lina nguvu na afya. Upumbavu we!
12. Ni hali zipi katika Jumuiya ya Wakristo zinazolingana na zile za Yuda?
12 Leo kuna tengenezo ambalo mwenendo wake ni kikumbusha cha mwenendo wa Yuda katika siku za Isaya. Jumuiya ya Wakristo hutumia jina la Yesu, lakini hufanya mapatano na mataifa na imeweka sanamu chungu nzima katika sehemu zake za ibada. Wafuasi wake hata huweka mifano ya ibada ya sanamu katika nyumba zao wenyewe. Jumuiya ya Wakristo imetoa vijana wawe dhabihu katika vita vya mataifa. Bila shaka jambo hili linamwudhi sana Mungu wa kweli, anayewaamuru Wakristo hivi: “Ikimbieni ibada ya sanamu”! (1 Wakorintho 10:14) Kwa kujihusisha katika siasa, Jumuiya ya Wakristo ‘imefanya uasherati na wafalme wa dunia.’ (Ufunuo 17:1, 2) Kwa kweli Jumuiya ya Wakristo ni mmoja wa wategemezaji wakuu wa Umoja wa Mataifa. Ni nini kinachomngoja kahaba huyu wa kidini? Ili tujue, tunapaswa kufahamu kile ambacho Yehova anaambia mfanani halisi wa kahaba huyo, yaani Yuda isiyo na uaminifu, ambayo inawakilishwa hasa na jiji lake kuu, Yerusalemu.
“Na Wakuponye Hao Uliowakusanya”
13. Yuda anaanza ‘kusema uwongo’ namna gani, na anatendaje kuhusu subira ya Yehova?
13 “Ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo?” Yehova anauliza. Swali safi! Hakika Yuda hamwonyeshi Yehova hofu ya kimungu inayofaa. Ama sivyo, hangekuwa taifa la waongo, waabudu wa miungu ya uwongo. Yehova anaendelea kusema hivi: “Hukunikumbuka mimi, wala kuweka hayo moyoni? je! mimi sikunyamaza tangu zamani, hata huniogopi?” (Isaya 57:11) Yehova amekaa kimya asiadhibu Yuda mara hiyo. Je, Yuda anashukuru? La. Badala yake, anauona uvumilivu wa Mungu kuwa ni kutokujali. Ameacha kabisa kumhofu Mungu.
14, 15. Yehova anasema nini juu ya matendo ya Yuda na ‘hao aliowakusanya’?
14 Hata hivyo, kipindi cha ustahimilivu wa Mungu kitafikia mwisho. Akiutazamia wakati huo, Yehova anatangaza hivi: “Mimi nitatangaza haki yako [“uadilifu wako,” “NW”] na matendo yako hayatakufaa. Utakapolia, na wakuponye hao uliowakusanya; lakini upepo utawachukua; uvuvio tu utawachukulia mbali.” (Isaya 57:12, 13a) Yehova atafichua kwamba uadilifu wa Yuda ni bandia. Matendo yake ya unafiki hayatakuwa na faida. ‘Hao aliowakusanya,’ maana yake sanamu zake nyingi, hawatamponya. Maafa yatakapotokea ghafula, miungu anayoitumaini itapeperushwa mbali kwa pumzi moja tu.
15 Maneno ya Yehova yanatimizwa mwaka wa 607 K.W.K. wakati Mfalme Nebukadreza wa Babiloni anapoharibu Yerusalemu, anachoma hekalu kwa moto na kuteka idadi kubwa ya watu. “Hivyo Yuda wakachukuliwa utumwani kutoka nchi yao.”—2 Wafalme 25:1-21.
16. Ni nini kinachoingoja Jumuiya ya Wakristo na sehemu nyinginezo za “Babiloni Mkubwa”?
16 Vivyo hivyo, sanamu chungu nzima za Jumuiya ya Wakristo hazitamkomboa katika siku ya hasira ya Yehova. (Isaya 2:19-22; 2 Wathesalonike 1:6-10) Jumuiya ya Wakristo itaangamizwa kabisa pamoja na sehemu nyingine zote za “Babiloni Mkubwa,” ile milki ya ulimwengu ya dini za uwongo. Hayawani wa mfano mwenye rangi nyekundu nyangavu na pembe zake kumi ‘watamfanya Babiloni Mkubwa awe ukiwa na uchi, na watakula kabisa sehemu zake zenye nyama na watamchoma kabisa kwa moto.’ (Ufunuo 17:3, 16, 17) Sisi tunafurahi kama nini kwamba tumetii amri hii: “Tokeni kwake, watu wangu, ikiwa hamtaki kushiriki pamoja naye dhambi zake, na ikiwa hamtaki kupokea sehemu ya tauni zake”! (Ufunuo 18:4, 5) Tusirudi kwake wala kwenye njia zake kamwe.
‘Atakayekimbilia Usalama Kwangu Ataimiliki Nchi’
17. ‘Mwenye kukimbilia usalama kwa Yehova’ anapewa ahadi gani, na inatimizwa lini?
17 Namna gani maneno yanayofuata ya unabii wa Isaya? “Watakaokimbilia usalama kwangu, wataimiliki nchi, mlima wangu mtakatifu utakuwa mali yao.” (Isaya 57:13b, “BHN”) Yehova anaongea na nani sasa? Anaeleza mambo yatakayotokea baada ya yale maafa makubwa yanayokuja, na anatabiri kwamba watu wake watakombolewa kutoka Babiloni kisha ibada safi irudishwe katika mlima wake mtakatifu, Yerusalemu. (Isaya 66:20; Danieli 9:16) Hiki ni kitia-moyo kweli kweli kwa Wayahudi wowote wanaobaki wakiwa waaminifu! Zaidi ya hilo, Yehova anasema hivi: “Naye atasema, Tutieni, tutieni, itengenezeni njia, kiondoeni kila kikwazacho katika njia ya watu wangu.” (Isaya 57:14) Wakati ufikapo wa Mungu kuwakomboa watu wake, njia itakuwa tayari, huku vipingamizi vyote vikiwa vimeondolewa.—2 Mambo ya Nyakati 36:22, 23.
18. Kutukuka kwa Yehova kunaelezwaje, hata hivyo anaonyesha hangaiko gani lenye upendo?
18 Hapo sasa ndipo nabii Isaya anapoyasimulia maneno yaliyonukuliwa pale mwanzoni: “Yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua [“kuhuisha,” “NW”] roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu [“wanaopondwa,” “NW”].” (Isaya 57:15) Kiti cha ufalme cha Yehova kiko katika mbingu za juu kabisa. Hakuna cheo kingine chochote kilicho juu wala kilichotukuka kuliko hicho. Inafariji kama nini kujua kwamba akiwa huko juu yeye huona kila kitu—si dhambi za waovu tu, bali hata matendo ya haki ya wale wanaojaribu kumtumikia! (Zaburi 102:19; 103:6) Tena, yeye anasikia sauti za kuugua za wale wanaoonewa, na anahuisha mioyo ya waliopondwa. Bila shaka maneno haya yaliigusa mioyo ya Wayahudi waliotubu nyakati za kale. Na hakika yanaigusa mioyo yetu sisi leo.
19. Hasira ya Yehova hukoma wakati gani?
19 Maneno ya Yehova yanayofuata ni yenye faraja pia: “Sitashindana na watu siku zote, wala sitakuwa na hasira siku zote; maana roho ingezimia mbele zangu, na hizo nafsi nilizozifanya.” (Isaya 57:16) Kama ghadhabu ya Yehova ingekuwa ya daima dawamu, hakuna kiumbe chochote cha Mungu ambacho kingeweza kubaki hai. Lakini ni jambo la kufurahisha kwamba hasira ya Mungu ni ya muda tu. Ghadhabu hiyo hukoma baada ya kutimiza kusudi lake. Ufahamu huo wa kina kirefu uliopuliziwa hutusaidia kuelewa sana kwamba Yehova anaupenda uumbaji wake.
20. (a) Yehova hushughulikaje na mkosaji asiyetubu? (b) Yehova humfariji jinsi gani mtu mwenye majuto?
20 Yehova anapoendelea kuongea, tunapata ufahamu wa kina kirefu zaidi. Kwanza anasema hivi: “Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake naliona hasira, nikampiga; nalificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe.” (Isaya 57:17) Hakuna shaka kwamba makosa yaliyofanywa kwa sababu ya pupa ndiyo yanayochochea ghadhabu ya Mungu. Maadamu mtu anabaki akiwa mkaidi moyoni, Yehova naye anabaki na hasira yake. Lakini namna gani mkaidi huyo akikubali nidhamu? Hapo ndipo Yehova huonyesha jinsi upendo na huruma zake humsukuma kutenda: “Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia.” (Isaya 57:18) Baada ya Yehova kutoa nidhamu, yeye humponya mtu mwenye majuto na kumfariji huyo na wale pia wanaoomboleza pamoja naye. Ndiyo sababu Wayahudi waliweza kurudi nyumbani mwaka wa 537 K.W.K. Ni kweli kwamba Yuda haikuweza tena kamwe kuwa ufalme wenye kujitawala chini ya mfalme wa ukoo wa Daudi. Hata hivyo, hekalu katika Yerusalemu lilijengwa upya, na ibada ya kweli ikarudishwa.
21. (a) Yehova alihuishaje roho ya Wakristo watiwa-mafuta mwaka wa 1919? (b) Sisi mmoja-mmoja tunapaswa kusitawisha sifa gani?
21 Yehova, “yeye aliye juu, aliyetukuka,” aliihangaikia pia hali njema ya mabaki watiwa-mafuta mwaka wa 1919. Kwa sababu ya roho yao ya majuto na unyenyekevu, huyo Mungu mkuu, Yehova, aliwafadhili kwa kuyaona mateso yao na kuwakomboa kutoka katika utekwa wa Kibabiloni. Aliondoa vikwazo vyote, akawapeleka mahali penye uhuru ili waweze kumtolea ibada safi. Hivyo maneno ya Yehova kupitia Isaya yakatimia wakati huo. Isitoshe, maneno hayo yana kanuni za milele zinazohusu kila mmoja wetu. Yehova hukubali ibada ya wale tu walio na akili ya unyenyekevu. Na mmoja wa watumishi wa Mungu akitenda dhambi, anapaswa kufanya haraka kukiri kosa lake, kukubali karipio, na kurekebisha njia zake. Sisi tusisahau kamwe kwamba Yehova huwaponya na kuwafariji wanyenyekevu, bali “huwapinga wenye kiburi.”—Yakobo 4:6.
‘Amani Kwao Walio Mbali na Walio Karibu’
22. Yehova anatabiri wakati gani ujao kwa (a) wenye kutubu? (b) waovu?
22 Akitofautisha wakati ujao wa wale wanaotubu na wakati ujao wa wale wanaoendelea tu kufuata njia zao za uovu, Yehova anatangaza hivi: “Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; . . . nami nitamponya. Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka. Hapana amani kwa wabaya.”—Isaya 57:19-21.
23. Tunda la midomo ni nini, na Yehova ‘anaumbaje’ tunda hilo?
23 Tunda la midomo ni ile dhabihu ya sifa ambayo hutolewa kuelekea Mungu—tangazo la peupe kuhusu jina lake. (Waebrania 13:15) Yehova ‘anaumbaje’ tangazo hilo la peupe? Ili kutoa toleo la dhabihu ya sifa, ni lazima kwanza mtu ajifunze juu ya Mungu kisha amwamini. Imani, ambayo ni tunda la roho ya Mungu, humchochea mtu huyo awaambie wengine mambo ambayo amesikia. Yaani, yeye hufanya tangazo la peupe. (Waroma 10:13-15; Wagalatia 5:22) Vilevile, na ikumbukwe kwamba Yehova ndiye hasa anayewapa watumishi wake utume wa kutangaza sifa yake. Tena Yehova ndiye anayewakomboa watu wake, na kufanya iwezekane kwao kutoa dhabihu hizo za sifa. (1 Petro 2:9) Kwa hiyo ni sawa kusema kwamba Yehova ndiye anayeumba tunda hilo la midomo.
24. (a) Ni nani wanaopata kujua amani ya Mungu, na matokeo ni nini? (b) Ni nani ambao hawapati kujua amani, na wanapatwa na matokeo gani?
24 Lo, Wayahudi wanatoa tunda la midomo lenye kusisimua kama nini wakati wanapoirudia nchi yao wakimwimbia Yehova sifa! Bila shaka wana shangwe ya kuijua amani ya Mungu, hata kama wako “mbali”—mwendo mrefu kutoka Yuda, wakiwa wangali wanangojea kurudi—au wakiwa “karibu,” yaani wakiwa tayari katika nchi yao. Lakini mambo ni tofauti kabisa kwa waovu! Waovu wowote wasioitikia nidhamu za Yehova, hata wawe akina nani, na hata wawe wapi, hawana amani hata kidogo. Wanachacha kama bahari iliyochafuka, wakiendelea kuzaa, si lile tunda la midomo, bali “tope na takataka” za baharini, uchafu wa kila aina.
25. Watu wengi wa mbali na wa karibu huja kujua amani jinsi gani?
25 Leo, pia, waabudu wa Yehova kila mahali wanatangaza habari njema za Ufalme wa Mungu. Wakristo wa mbali na karibu, katika nchi zaidi ya 230, wanatoa tunda la midomo yao, wakivumisha sifa za yule Mungu mmoja tu wa kweli. Sifa wanazoimba zinasikiwa “tokea mwisho wa dunia.” (Isaya 42:10-12) Wale wanaozisikia semi zao na kuziitikia wanaikubali kweli ya Neno la Mungu, Biblia. Watu wa jinsi hiyo huja kujua amani, inayopatikana kwa kumtumikia “Mungu apaye amani.”—Waroma 16:20.
26. (a) Ni nini kinachowangojea waovu? (b) Watu wapole wanapewa ahadi gani bora, nasi tunapaswa kupiga moyo konde kufanya nini?
26 Ni kweli kwamba waovu hawasikizi ujumbe wa Ufalme. Ingawa hivyo, hivi karibuni hawataruhusiwa kuivuruga amani ya wenye haki. “Bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo,” ndivyo Yehova anavyoahidi. Wale wanaomkimbilia Yehova watairithi nchi kwa njia nzuri ajabu. “Wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.” (Zaburi 37:10, 11, 29) Wakati huo dunia yetu itakuwa mahali pazuri wee! Sisi sote na tupige moyo konde tusipoteze kamwe amani ya Mungu, ili tuweze kuimba sifa ya Mungu milele hata milele.
[Maelezo ya Chini]
a Inaelekea kwamba neno “kitanda” linamaanisha madhabahu ama mahali pa ibada ya kipagani. Mahali hapo panaitwa kitanda ili neno hilo liwe kikumbusha cha kwamba ibada hiyo ni ukahaba wa kiroho.
b Huenda ikawa kwamba miti mitakatifu iliwakilisha kiungo cha uke, na huenda ikawa nguzo takatifu zilifananisha kiungo cha uzazi cha mwanamume. Vitu hivyo viwili vilitumiwa na wakaaji wa Yuda wasio waaminifu.—2 Wafalme 18:4; 23:14.
[Picha katika ukurasa wa 263]
Yuda anafuata ibada isiyo na maadili chini ya kila mti wenye majani mabichi
[Picha katika ukurasa wa 267]
Yuda anajenga madhabahu kotekote nchini
[Picha katika ukurasa wa 275]
“Nayaumba matunda ya midomo”