Sura Ya Kumi
Ni Nani Awezaye Kusimama Dhidi ya mkuu wa Wakuu?
1, 2. Kwa nini ono ambalo Danieli aliona mwaka wa tatu wa utawala wa Belshaza ni la maana kwetu?
MIAKA 57 imepita tangu hekalu la Yehova huko Yerusalemu liharibiwe. Belshaza na baba yake, Nabonido, wanatawala pamoja Milki ya Babiloni, serikali ya tatu ya ulimwengu ya unabii wa Biblia.a Danieli, nabii wa Mungu ni mhamishwa huko Babiloni. Na “mwaka wa tatu wa kumiliki kwake mfalme Belshaza,” Yehova amtumia Danieli ono linalofunua mambo fulani juu ya kurudishwa kwa ibada ya kweli.—Danieli 8:1.
2 Ono la kiunabii ambalo Danieli aliona lilimwathiri sana nalo latupendeza sana sisi tunaoishi “wakati wa mwisho.” Malaika Gabrieli amwambia Danieli hivi: “Nitakujulisha yatakayokuwa wakati wa mwisho wa ghadhabu; maana, ni ya wakati wa mwisho ulioamriwa.” (Danieli 8:16, 17, 19, 27) Basi, acheni tuchunguze tukiwa na hamu kubwa mambo ambayo Danieli aliona na maana yake kwetu leo.
KONDOO MUME MWENYE PEMBE MBILI
3, 4. Danieli aliona mnyama gani aliyekuwa amesimama mbele ya mto, na mnyama huyo anafananisha nini?
3 “Naliona katika maono,” Danieli aandika, “ilitukia, nilipoona, nalikuwako huko Shushani ngomeni, katika wilaya ya Elamu; nikaona katika maono, nami nalikuwa karibu na mto Ulai.” (Danieli 8:2) Haijulikani ikiwa kwa hakika Danieli alikuwa Shushani (Susa)—jiji kuu la Elamu, lililo umbali wa kilometa 350 mashariki mwa Babiloni—au alikuwa huko katika ono tu.
4 Danieli aendelea kusema hivi: “Nikainua macho yangu nikaona, na tazama, mbele ya mto alisimama kondoo mume, mwenye pembe mbili.” (Danieli 8:3a) Danieli apata kujua kondoo mume huyo ni nani. Malaika Gabrieli amwarifu hivi baadaye: “Yule kondoo mume uliyemwona, mwenye pembe mbili, hizo ndizo wafalme wa Umedi na Uajemi.” (Danieli 8:20) Wamedi walikuwa watu wa nyanda zenye milima mashariki mwa Ashuru, nao Waajemi awali waliishi maisha ya kuhamahama katika eneo lililo kaskazini mwa Ghuba ya Uajemi. Hata hivyo, Milki ya Umedi na Uajemi ilipositawi, wakazi wake walizidi kupenda anasa.
5. Ile pembe ‘iliyozuka mwisho’ ilipataje kuwa ndefu zaidi?
5 “Pembe zile mbili zilikuwa ndefu,” aripoti Danieli, “lakini moja ilikuwa ndefu kuliko ya pili, na ile iliyokuwa ndefu zaidi ilizuka mwisho.” (Danieli 8:3b) Ile pembe ndefu iliyozuka baadaye yafananisha Waajemi, ilhali ile pembe nyingine yawakilisha Wamedi. Mwanzoni, Wamedi walikuwa na mamlaka zaidi. Lakini mwaka wa 550 K.W.K., Koreshi mtawala wa Uajemi alimshinda kwa urahisi Mfalme Astyages wa Umedi. Koreshi aliunganisha desturi na sheria za mataifa hayo mawili, akaunganisha falme zao, na kupanua eneo lao kupitia ushindi. Tangu wakati huo, ikawa mamlaka ya serikali mbili.
KONDOO MUME AJITUKUZA NAFSI YAKE
6, 7. Ilikuwaje kwamba “hakuna mnyama ye yote awezaye kusimama mbele” ya yule kondoo mume?
6 Akiendelea kumfafanua yule kondoo mume, Danieli ataarifu hivi: “Nikamwona huyo kondoo mume akisukuma upande wa magharibi, na upande wa kaskazini, na upande wa kusini; wala hakuna mnyama ye yote awezaye kusimama mbele yake, wala hakuna mnyama ye yote awezaye kupokonya mkononi mwake; lakini alitenda kama alivyopenda mwenyewe, akajitukuza nafsi yake.”—Danieli 8:4.
7 Katika ono la Danieli lililotangulia, Babiloni lilikuwa limefananishwa na mnyama aliyetoka baharini aliyekuwa kama simba mwenye mabawa ya tai. (Danieli 7:4, 17) Mnyama huyo wa mfano hakuweza kusimama mbele ya “kondoo mume” wa ono hili jipya. Babiloni lilianguka mikononi mwa Koreshi Mkuu mwaka wa 539 K.W.K. Karibu miaka 50 baadaye, “hakuna mnyama ye yote,” au serikali za kisiasa, aliyeweza kusimama dhidi ya Milki ya Umedi na Uajemi—serikali ya nne ya ulimwengu ya unabii wa Biblia.
8, 9. (a) ‘Kondoo mume alisukumaje upande wa magharibi, na upande wa kaskazini, na upande wa kusini’? (b) Kitabu cha Esta husema nini juu ya mwandamizi wa Mfalme Dario wa Kwanza wa Uajemi?
8 Kwa kuwa ilitoka “mashariki,” Serikali ya Ulimwengu ya Umedi na Uajemi ilifanya ilivyopenda, “[i]kisukuma upande wa magharibi, na upande wa kaskazini, na upande wa kusini.” (Isaya 46:11) Mfalme Cambyses wa Pili, aliyetawala baada ya Koreshi Mkuu, akashinda Misri. Mfalme Dario wa Kwanza wa Uajemi ambaye alihamia upande wa magharibi ng’ambo ya Bosporus mwaka wa 513 K.W.K. na kuvamia eneo la Ulaya la Thrasi, ambalo jiji kuu lake lilikuwa Byzantium (paitwapo Istanbul sasa) ndiye aliyetawala baada yake. Mwaka wa 508 K.W.K., alimiliki Thrasi, na kushinda Makedonia mwaka wa 496 K.W.K. Kwa hiyo, kufikia wakati wa Dario, yule “kondoo mume” wa Umedi na Uajemi alikuwa ameteka maeneo pande tatu kuu: kaskazini katika Babiloni na Ashuru, magharibi katika Asia Ndogo, na kusini katika Misri.
9 Ikitolea ushuhuda ukuu wa Milki ya Umedi na Uajemi, Biblia husema juu ya mwandamizi wa Dario, Shasta wa Kwanza, kuwa “Ahasuero ali[ye]miliki toka Bara Hindi mpaka Kushi, juu ya majimbo mia na ishirini na saba.” (Esta 1:1) Lakini milki hiyo kuu ingeshindwa na nyingine, na kuhusu hilo, ono la Danieli laonyesha mambo yenye kuvuta fikira sana ambayo yapaswa kuimarisha imani yetu katika neno la Mungu la kiunabii.
BEBERU AMPIGA DAFRAO KONDOO MUME
10. Katika ono la Danieli, ni mnyama gani aliyempiga dafrao yule “kondoo mume”?
10 Wazia jinsi Danieli anavyoshangazwa na yale aonayo sasa. Simulizi lasema hivi: “Nami nilipokuwa nikifikiri, tazama, beberu akatoka upande wa magharibi, juu ya uso wa dunia nzima, bila kuigusa nchi; na beberu yule alikuwa na pembe mashuhuri kati ya macho yake. Naye akamwendea huyo kondoo mume mwenye pembe mbili, niliyemwona akisimama karibu na mto, akamshambulia kwa ghadhabu za nguvu zake. Nikamwona akimkaribia kondoo mume, akamwonea hasira kali, akampiga kondoo mume, akazivunja pembe zake mbili; na huyo kondoo mume alikuwa hana nguvu kusimama mbele yake; bali akamwangusha chini, akamkanyaga-kanyaga; wala hapakuwapo awezaye kumwokoa kondoo mume katika mkono wake.” (Danieli 8:5-7) Yote hayo yamaanisha nini?
11. (a) Malaika Gabrieli alimfafanuaje ‘beberu mwenye manyoya mengi’ na ‘pembe yake kubwa’? (b) Ni nani aliyefananishwa na pembe hiyo mashuhuri?
11 Danieli na hata sisi hatuhitaji kukisia-kisia juu ya maana ya ono hilo. “Yule beberu, mwenye manyoya mengi, ni mfalme wa Uyunani [“Ugiriki,” NW]; na ile pembe kubwa iliyo kati ya macho yake ni mfalme wa kwanza,” malaika Gabrieli amwarifu Danieli. (Danieli 8:21) Mwaka wa 336 K.W.K., mfalme wa mwisho wa Milki ya Uajemi, Dario wa Tatu (Codommanus), alitawazwa. Mwaka uo huo, Aleksanda akawa mfalme wa Makedonia. Historia yaonyesha kwamba Aleksanda Mkuu alikuwa yule ‘mfalme wa kwanza wa [Ugiriki].’ Akianzia “magharibi,” mwaka wa 334 K.W.K., Aleksanda alisonga haraka. Kana kwamba ‘hagusi nchi,’ alishinda maeneo kadhaa na kumpiga dafrao yule “kondoo mume.” Baada ya kuukomesha utawala wa Umedi na Uajemi uliodumu karibu karne mbili, Ugiriki ukawa serikali ya ulimwengu ya tano yenye umaana wa Kibiblia. Ulikuwa utimizo ulioje wa unabii wa Mungu!
12. Ile “pembe kubwa” ya beberu wa mfano ‘ilivunjwaje,’ nazo zile pembe nne zilizotokea mahali pake zilikuwa nini?
12 Lakini nguvu ya Aleksanda ilikuwa ya muda mfupi tu. Lile ono laendelea kufunua hivi: “Na yule beberu akajitukuza sana; na alipokuwa na nguvu, pembe ile kubwa ilivunjika na badala yake zikazuka pembe nne mashuhuri zilizoelekea pepo nne za mbinguni.” (Danieli 8:8) Gabrieli asema hivi akiufafanua unabii huo: “Katika habari ya pembe ile iliyovunjika, ambayo badala yake zilisimama pembe nne, falme nne zitasimama kutoka katika taifa lile, lakini si kwa nguvu kama zake.” (Danieli 8:22) Kama ilivyotabiriwa, kwenye upeo wa ushindi wake mbalimbali, Aleksanda ‘alivunjika,’ au akafa, akiwa na umri wa miaka 32 tu. Nayo milki yake kubwa hatimaye ikagawanywa miongoni mwa wanne kati ya majenerali wake.
PEMBE NDOGO YA KIFUMBO
13. Ni nini kilichotokea kwenye moja ya zile pembe nne, nacho kilitendaje?
13 Sehemu inayofuata ya ono hilo yaenea zaidi ya miaka 2,200, ikiwa na utimizo leo. Danieli aandika hivi: “Katika moja ya pembe hizo [zile pembe nne] ilitokea pembe ndogo, iliyokua sana, upande wa kusini, na upande wa magharibi, na upande wa nchi ya uzuri. Nayo ikakua, kiasi cha kulifikilia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga. Naam, ikajitukuza hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, ikamwondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini. Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.”—Danieli 8:9-12.
14. Malaika Gabrieli alisema nini juu ya utendaji mbalimbali wa ile pembe ndogo ya mfano, nayo ingepatwa na nini?
14 Kabla hatujaweza kuelewa maana ya maneno yaliyotoka kunukuliwa, lazima tumsikilize malaika wa Mungu. Baada ya kutaja juu ya kupata mamlaka kwa zile falme nne zilizotokana na milki ya Aleksanda, malaika Gabrieli asema hivi: “Wakati wa mwisho wa ufalme wao, wakosao watakapotimia, mfalme mwenye uso mkali, afahamuye mafumbo, atasimama. Na nguvu zake zitakuwa nyingi mno, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe; naye ataharibu kiasi cha kustaajabisha watu, na kufanikiwa, na kutenda apendavyo; naye atawaangamiza hao walio hodari na watu watakatifu. Na kwa mashauri yake atafanikisha hila mkononi mwake; naye atajitukuza nafsi yake moyoni mwake; naye atawaangamiza wengi katika hali yao ya salama; naye atasimama kushindana naye aliye Mkuu wa wakuu; lakini atavunjika, bila kazi ya mikono.”—Danieli 8:23-25.
15. Malaika alimwambia Danieli afanye nini kuhusiana na ono hilo?
15 “Wewe yafunike maono hayo,” malaika amwambia Danieli, “maana ni ya wakati ujao baada ya siku nyingi.” (Danieli 8:26) Sehemu hiyo ya ono ingetimia “baada ya siku nyingi,” naye Danieli alipaswa ‘kuyafunika maono hayo.’ Yamkini maana yake ilikuwa fumbo kwa Danieli. Hata hivyo, kufikia leo, lazima zile “siku nyingi” ziwe zimepita. Kwa hiyo, twauliza: ‘Historia ya ulimwengu yafunua nini kuhusu utimizo wa ono hilo la kiunabii?’
ILE PEMBE NDOGO YAPATA NGUVU NYINGI
16. (a) Ile pembe ndogo ilitokana na pembe gani ya mfano? (b) Roma ilipataje kuwa serikali ya ulimwengu ya sita ya unabii wa Biblia, lakini kwa nini haikuwa ile pembe ndogo ya mfano?
16 Kulingana na historia, ile pembe ndogo ilitokana na mojawapo ya zile pembe nne za mfano—ile pembe iliyokuwa mbali zaidi upande wa magharibi. Hiyo ilikuwa ufalme wa Kigiriki wa Jenerali Kasanda aliyetawala Makedonia na Ugiriki. Baadaye, ufalme huo ulitwaliwa na Jenerali Lisimako, mfalme wa Thrasi na Asia Ndogo. Katika karne ya pili kabla ya Wakati wetu wa Kawaida, maeneo hayo ya magharibi ya utawala wa Kigiriki yalishindwa na Roma. Na kufikia mwaka wa 30 K.W.K., milki ya Roma ilitwaa falme zote za Kigiriki, na hivyo kuwa serikali ya ulimwengu ya sita ya unabii wa Biblia. Lakini Milki ya Roma haikuwa ile pembe ndogo ya ono la Danieli, kwa kuwa milki hiyo haikuendelea kuwapo hadi “wakati wa mwisho ulioamriwa.”—Danieli 8:19.
17. (a) Uingereza ilikuwa na uhusiano gani na Milki ya Roma? (b) Milki ya Uingereza yahusianaje na ufalme wa Makedonia na Ugiriki?
17 Kwa hiyo, basi, historia yamtambulisha yule “mfalme mwenye uso mkali” na mwenye ujeuri kuwa nani? Uingereza ilichipuka upande wa kaskazini-magharibi kutoka katika Milki ya Roma. Kufikia mwanzoni mwa karne ya tano W.K., kulikuwa na mikoa ya Roma mahali ilipo Uingereza ya sasa. Hatimaye, Milki ya Roma ikadidimia, lakini ustaarabu wa Ugiriki na Roma uliendelea kuwa na uvutano katika Uingereza na katika sehemu nyingine za Ulaya zilizokuwa chini ya milki ya Roma. “Milki ya Roma ilipoanguka, Kanisa lilichukua mahali pake,” akaandika mshindi wa Tuzo la Nobeli Octavio Paz, mshairi aliyekuwa pia mwandishi huko Mexico. Aliongezea kusema hivi: “Wakuu wa Kanisa, na pia wasomi wa baadaye, waliingiza falsafa za Kigiriki katika fundisho la Kikristo.” Na mwanafalsafa aliye pia mwana-hisabati wa karne ya 20, Bertrand Russell alionelea hivi: “Ustaarabu wa Magharibi, uliotokana na Ugiriki, wategemea desturi za kifalsafa na kisayansi zilizoanzia Mileto [jiji la Kigiriki katika Asia Ndogo] miaka elfu mbili na nusu iliyopita.” Kwa hiyo, tungeweza kusema kwamba utamaduni wa Milki ya Uingereza ulitokana na ufalme wa Makedonia na Ugiriki.
18. Ile pembe ndogo iliyopata kuwa “mfalme mwenye uso mkali” katika “wakati wa mwisho” ni nini? Fafanua.
18 Kufikia mwaka wa 1763 Milki ya Uingereza ilikuwa imeshinda washindani wake wenye nguvu, Hispania na Ufaransa. Tangu wakati huo na kuendelea milki hiyo ilijidhihirisha kuwa mtawala wa bahari na pia serikali ya ulimwengu ya saba ya unabii wa Biblia. Hata baada ya zile koloni 13 za Amerika kujitenga na Uingereza mwaka wa 1776 na kuwa Marekani, Milki ya Uingereza ilipanuka na kufikia robo ya uso wa dunia na robo ya wakazi wa dunia. Serikali ya ulimwengu ya saba ilizidi kupata nguvu wakati ambapo Marekani ilishirikiana na Uingereza ili kufanyiza serikali ya ulimwengu ya Uingereza na Marekani. Kiuchumi na kijeshi, kwa kweli serikali hiyo ilikuwa imepata kuwa “mfalme mwenye uso mkali.” Kwa hiyo, ile pembe ndogo iliyokuwa kali kisiasa katika “wakati wa mwisho” ni Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani.
19. “Nchi ya uzuri” inayotajwa katika ono ni nini?
19 Danieli aliona kwamba ile pembe ndogo ‘ilikua sana’ kuelekea “upande wa nchi ya uzuri.” (Danieli 8:9) Lile Bara Lililoahidiwa, ambalo Yehova aliwapa wateule wake, lilikuwa zuri sana hivi kwamba liliitwa “utukufu wa nchi zote,” yaani, wa dunia yote. (Ezekieli 20:6, 15) Ni kweli kwamba Uingereza iliteka Yerusalemu Desemba 9, 1917, na katika mwaka wa 1920, Ushirika wa Mataifa uliipa Uingereza mamlaka juu ya Palestina, iendelee hadi Mei 14, 1948. Lakini ono hilo ni la kiunabii, na lenye ufanani mwingi. “Nchi ya uzuri” iliyotajwa katika ono yafananisha hali ya kidunia ya watu ambao Mungu awaona kuwa watakatifu wakati wa ile serikali ya saba ya ulimwengu, wala haifananishi Yerusalemu. Acheni tuone jinsi Serikali hii ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani inavyojaribu kuwatisha watakatifu.
“MAHALI PA PATAKATIFU PAKE” PAANGUSHWA CHINI
20. “Jeshi la mbinguni” na “nyota” ambazo ile pembe ndogo hujaribu kuangusha ni nani?
20 Ile pembe ndogo “ikakua, kiasi cha kulifikilia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota.” Kulingana na ufafanuzi wa malaika, “jeshi la mbinguni” na “nyota” ambazo ile pembe ndogo hujaribu kuangusha ni “watu watakatifu.” (Danieli 8:10, 24) “Watu [hao] watakatifu” ni Wakristo watiwa-mafuta kwa roho. Kwa sababu ya kuingizwa katika uhusiano pamoja na Mungu kupitia agano jipya, lililoanzishwa na damu ya Yesu Kristo iliyomwagwa, wametakaswa, wakasafishwa, na kutengwa kwa ajili ya utumishi wa Mungu peke yake. (Waebrania 10:10; 13:20) Baada ya kupata mgawo wa kuwa warithi pamoja na Mwana katika urithi wa kimbingu, Yehova huwaona kuwa watakatifu. (Waefeso 1:3, 11, 18-20) Basi, katika ono la Danieli, “jeshi la mbinguni” larejezea mabaki ya “watakatifu” 144,000 walio duniani, watakaotawala mbinguni pamoja na Mwana-Kondoo.—Ufunuo 14:1-5.
21. Ni nani wanaomiliki “patakatifu” ambapo serikali ya ulimwengu ya saba hujaribu kufanya ukiwa?
21 Leo mabaki ya 144,000 ni wawakilishi wa kidunia wa “Yerusalemu la kimbingu”—Ufalme wa Mungu ulio kama jiji—na mpango wake wa hekalu. (Waebrania 12:22, 28; 13:14) Vivyo hivyo, wapo “patakatifu” ambapo serikali ya ulimwengu ya saba hujaribu kukanyaga-kanyaga na kupafanya ukiwa. (Danieli 8:13) Akinena juu ya mahali hapo patakatifu kwamba ni “mahali pa patakatifu pake [Yehova],” Danieli asema hivi: “Ikamwondolea [Yehova] sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini. Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.” (Danieli 8:11, 12) Hilo lilitimizwaje?
22. Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, ile serikali ya ulimwengu ya saba ilifanya “makosa” gani yenye kuonekana wazi?
22 Mashahidi wa Yehova walipatwa na nini wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili? Walinyanyaswa vikali! Mnyanyaso ulianzia nchi za Nazi na za Ufashisti. Lakini punde si punde ‘kweli iliangushwa hata chini’ kotekote katika milki hiyo kubwa ya ‘pembe ndogo iliyokuwa imepata nguvu nyingi.’ “Jeshi” la wapiga-mbiu wa Ufalme na kazi yao ya kuhubiri “habari njema” lilipigwa marufuku katika karibu nchi zote za Jumuiya ya Madola ya Uingereza. (Marko 13:10) Mataifa hayo yalipopanga mbinu zao za kivita, yalikataa kuwapa Mashahidi wa Yehova uhuru wa wahudumu wa kutoshiriki utumishi wa kijeshi, wakionyesha kutostahi hata kidogo kuwekwa kwao kitheokrasi kuwa wahudumu wa Mungu. Watumishi waaminifu wa Yehova huko Marekani walitendewa jeuri na vikundi vya wafanya-ghasia na kuvunjiwa adhama kwa njia mbalimbali. Serikali ya ulimwengu ya saba, kwa hakika, ilijaribu kuondoa dhabihu ya sifa—“tunda la midomo”—ambayo watu wa Yehova walimtolea kwa ukawaida ikiwa “ya daima” katika ibada yao. (Waebrania 13:15) Kwa hiyo, serikali hiyo ya ulimwengu ilifanya “makosa” ya kuvamia milki halali ya Mungu Aliye Juu—“mahali pa patakatifu pake.”
23. (a) Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani ‘ilishindanaje na Mkuu wa wakuu’? (b) “Mkuu wa wakuu” ni nani?
23 Kwa kuwanyanyasa “watakatifu” wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, ile pembe ndogo ilijitukuza “hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo.” Au, kama vile malaika Gabrieli anavyotaarifu, ilisimama “kushindana naye aliye Mkuu wa wakuu.” (Danieli 8:11, 25) Jina la cheo “Mkuu wa wakuu” hutumika kwa Yehova Mungu peke yake. Neno la Kiebrania sar, linalotafsiriwa “mkuu,” lahusiana na neno linalomaanisha “tawala.” Zaidi ya kurejezea mwana wa mfalme au mtu mwenye wadhifa wa kifalme, neno hilo hutumika kurejezea kiongozi, au jumbe. Kitabu cha Danieli huwataja malaika wengine walio wakuu—kwa kielelezo, Mikaeli. Mungu ndiye Mkuu Zaidi wa wakuu hao. (Danieli 10:13, 21; linganisha Zaburi 83:18.) Je, twaweza kumwazia mtu awaye yote akishindana na Yehova—Mkuu wa wakuu?
“PATAKATIFU” PATAKASWA
24. Danieli 8:14 hutuhakikishia nini?
24 Hakuna awezaye kushindana na Mkuu wa wakuu—hata mfalme mwenye “uso mkali” kama vile Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani! Mfalme huyo hapati mafanikio katika kujaribu kwake kufanya ukiwa patakatifu pa Mungu. Baada ya kipindi cha “jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu,” asema malaika mjumbe, ‘patakatifu patatakaswa,’ au “patashinda.”—Danieli 8:13, 14; The New English Bible.
25. Kile kipindi cha kiunabii cha siku 2,300 kina urefu gani, nacho lazima kihusianishwe na tukio gani?
25 Zile siku 2,300 ni kipindi cha kiunabii. Kwa hiyo, mwaka wa kiunabii wa siku 360 wahusika. (Ufunuo 11:2, 3; 12:6, 14) Basi, hizo siku 2,300 zingejumlika kuwa miaka 6, miezi 4, na siku 20. Hicho kilikuwa kipindi gani? Miaka ya 1930 na kitu, watu wa Mungu walianza kunyanyaswa zaidi katika nchi mbalimbali. Na katika Vita ya Ulimwengu ya Pili, Mashahidi wa Yehova walinyanyaswa vikali katika nchi za serikali ya ulimwengu ya Uingereza na Marekani. Kwa nini? Kwa sababu ya kusisitiza kwao ‘kumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.’ (Matendo 5:29) Kwa hiyo, lazima zile siku 2,300 ziwe zahusiana na vita hiyo.b Lakini ni nini kiwezacho kusemwa juu ya mwanzo na mwisho wa kipindi hicho cha kiunabii?
26. (a) Kuhesabiwa kwa zile siku 2,300 kwapaswa kuanza angalau lini? (b) Kile kipindi cha siku 2,300 kilimalizika lini?
26 Ili ‘patakatifu patakaswe’ au parudishwe katika hali yake ipapasayo, zile siku 2,300 lazima ziwe zilianza wakati ambapo mahali hapo palikuwa ‘patakatifu’ kwa maoni ya Mungu. Mapema zaidi, hilo lilikuwa Juni 1, 1938, wakati ambapo The Watchtower lilichapisha sehemu ya 1 ya makala “Tengenezo.” Sehemu ya 2 ilichapishwa Juni 15, 1938. Kuhesabu siku 2,300 (miaka 6, miezi 4, na siku 20 kwenye kalenda ya Kiebrania) kuanzia Juni 1 au 15, 1938, hutufikisha Oktoba 8 au 22, 1944. Siku ya kwanza ya kusanyiko la pekee lililofanywa Pittsburgh, Pennsylvania, Marekani, Septemba 30 na Oktoba 1, 1944, msimamizi wa Watch Tower Society, alitoa hotuba yenye kichwa “Mpango wa Kitheokrasi Leo.” Kwenye mkutano wa washirika wa kila mwaka uliofanywa Oktoba 2, katiba ya Sosaiti ilisahihishwa ili ipatane na mpango wa kitheokrasi kwa kadiri ambavyo sheria ingeruhusu. Matakwa ya Biblia yaliyorekebishwa yalipochapishwa, upesi tengenezo la kitheokrasi lilianza kutenda kikamili katika makutaniko ya Mashahidi wa Yehova.
27. Kulikuwa na uthibitisho gani wa kwamba “sadaka ya kuteketezwa daima” ilizuiliwa katika miaka iliyojaa minyanyaso wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili?
27 Ingawa zile siku 2,300 zilimalizika wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, iliyoanza mwaka wa 1939, kutolewa kwa “sadaka ya kuteketezwa ya daima” kwenye patakatifu pa Mungu kulizuiwa sana kwa sababu ya mnyanyaso. Mwaka wa 1938, Watch Tower Society ilikuwa na ofisi za tawi 39 zilizokuwa zikisimamia kazi ya Mashahidi ulimwenguni pote, lakini kufikia mwaka wa 1943 zilikuwa 21 tu. Pia, idadi ya wapiga-mbiu wa Ufalme wakati huo haikuongezeka sana.
28, 29. (a) Vita ya Ulimwengu ya Pili ilipokaribia kwisha, ni jambo gani lililotukia katika tengenezo la Yehova? (b) Ni nini kiwezacho kusemwa juu ya jitihada za adui za kufanya ukiwa na kuharibu “patakatifu”?
28 Kama vile tumeona tayari, miezi ya mwisho-mwisho ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, Mashahidi wa Yehova walithibitisha tena azimio lao la kutukuza utawala wa Mungu kwa kumtumikia wakiwa tengenezo la kitheokrasi. Mpango wa kazi yao na muundo wa usimamizi ulianzishwa mwaka wa 1944 ukiwa na lengo hilo. Kwa hakika, gazeti la The Watchtower la Oktoba 15, 1944, lilikuwa na makala yenye kichwa “Waliopangwa kwa Ajili ya Kazi ya Mwisho.” Gazeti hilo pamoja na makala nyingine juu ya utumishi za kipindi hichohicho zilionyesha kwamba zile siku 2,300 zilikuwa zimeisha na kwamba “patakatifu” palikuwa ‘pametakaswa’ tena.
29 Adui alishindwa kabisa katika kujaribu kwake kufanya ukiwa na kuharibu “patakatifu.” Kwa kweli, “watakatifu” waliokuwa duniani bado, pamoja na waandamani wao wa “umati mkubwa,” walikuwa wameshinda. (Ufunuo 7:9) Napo patakatifu, pakiwa katika hali yake ya kitheokrasi ipapasayo, sasa paendelea kumtolea Yehova utumishi mtakatifu.
30. Ni nini kitakachompata “mfalme mwenye uso mkali” hivi karibuni?
30 Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani bado inatawala. “Lakini [i]tavunjika, bila kazi ya mikono,” akasema malaika Gabrieli. (Danieli 8:25) Karibuni sana, serikali hii ya ulimwengu ya saba ya unabii wa Biblia—“mfalme mwenye uso mkali”—itavunjwa kwenye Har–Magedoni, bila kazi ya mikono, bali kwa nguvu zinazozidi zile za kibinadamu. (Danieli 2:44; Ufunuo 16:14, 16) Yasisimua kama nini kujua kwamba enzi kuu ya Yehova Mungu, Mkuu wa wakuu, itatetewa wakati huo!
[Maelezo ya Chini]
a Serikali saba za ulimwengu zenye umuhimu wa Kibiblia ni Misri, Ashuru, Babiloni, Umedi na Uajemi, Ugiriki, Roma, na serikali ya ulimwengu ya muungano ya Uingereza na Marekani. Zote hizo zastahili kukaziwa fikira kwa kuwa zimeshughulika na watu wa Yehova.
b Danieli 7:25 pia hutaja juu ya kipindi cha wakati ambacho ‘watakatifu wa Aliye juu watadhoofishwa.’ Kama ilivyoelezwa kwenye sura inayotangulia, hilo lilihusiana na vita ya kwanza ya ulimwengu.
[UMEFAHAMU NINI?
• Ni nini kinachofananishwa na
“kondoo mume” mwenye “pembe mbili”?
“beberu mwenye manyoya mengi” na “pembe kubwa”?
pembe nne zilizotokea mahali ilipokuwa ile “pembe mashuhuri”?
pembe ndogo iliyotokana na mojawapo ya zile pembe nne?
• Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani ilijaribuje kufanya “patakatifu” ukiwa, na je, ilifanikiwa?
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 166]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Milki ya Umedi na Uajemi
MAKEDONIA
MISRI
Memphis
ETHIOPIA
Yerusalemu
Babiloni
Ecbatana
Susa
Persepolisi
INDIA
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 169]
Milki ya Ugiriki
MAKEDONIA
MISRI
Babiloni
Mto Indus
[Ramani katika ukurasa wa 172]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Milki ya Roma
UINGEREZA
ITALIA
Roma
Yerusalemu
MISRI
[Picha katika ukurasa wa 164]
[Picha katika ukurasa wa 174]
Watu maarufu katika Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani:
1. George Washington, rais wa kwanza wa Marekani (1789-1797)
2. Malkia Victoria wa Uingereza (1837-1901)
3. Woodrow Wilson, rais wa Marekani (1913-1921)
4. David Lloyd George, waziri mkuu wa Uingereza (1916-1922)
5. Winston Churchill, waziri mkuu wa Uingereza (1940-1945, 1951-1955)
6. Franklin D. Roosevelt, rais wa Marekani (1933-1945)