Sura ya Kumi na Tatu
Wafalme Wawili Wapambana
1, 2. Kwa nini tupendezwe na unabii uliorekodiwa katika Danieli sura ya 11?
WAFALME wawili wapambana kufa na kupona ili kupata mamlaka kuu kupita zote. Miaka ipitapo, wapokezana mamlaka. Nyakati nyingine, mfalme mmoja atawala kwa ukuu ilhali yule mwingine awa asiyetenda, na kuna vipindi vya kutopambana. Lakini pigano jingine lazuka ghafula, na pambano laendelea. Baadhi ya wapambanaji hao ni Mfalme Niketa Seleuko wa Kwanza wa Siria, Mfalme Ptolemy Lagus wa Misri, Binti ya Mfalme wa Siria aliyekuwa pia Malkia wa Misri Kleopatra wa Kwanza, Wamaliki wa Roma Augusto na Tiberio, na Malkia Zenobia wa Palmyra. Pambano lielekeapo kwisha, Ujerumani ya Nazi, mataifa ya Kikomunisti, Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani, Ushirika wa Mataifa, na Umoja wa Mataifa pia zimehusika. Tamati ni kisa kisichotazamiwa na mashirika hayo yote ya kisiasa. Malaika wa Yehova alimjulisha Danieli unabii huo wenye kusisimua miaka 2,500 hivi iliyopita.—Danieli, sura ya 11.
2 Lazima Danieli awe alisisimuka kama nini alipomsikia malaika akimfunulia kinaganaga ushindani kati ya wafalme wawili wajao! Ushindani huo watupendeza sisi pia, kwa kuwa kushindania mamlaka kati ya wafalme hao wawili kwaendelea hata leo. Imani yetu na uhakika wetu kwamba sehemu ya mwisho ya unabii huo bila shaka itatimizwa zitatiwa nguvu tuonapo jinsi ambavyo historia imeonyesha vile sehemu ya kwanza ya unabii huo ilivyotimizwa. Kusikiliza unabii huu kutatusaidia kuona waziwazi mahali tulipo katika mkondo wa wakati. Pia kutatia nguvu azimio letu la kutokuwamo katika mapambano hayo tungojeapo kwa subira Mungu achukue hatua kwa niaba yetu. (Zaburi 146:3, 5) Basi, na tumsikilize kwa makini malaika wa Yehova akiongea na Danieli.
DHIDI YA UFALME WA UGIRIKI
3. Malaika alimwunga mkono nani “katika mwaka wa kwanza wa Dario, Mmedi”?
3 “Tena mimi,” akasema malaika, “katika mwaka wa kwanza wa Dario, Mmedi [539/538 K.W.K.], mimi nalisimama nimthibitishe na kumtia nguvu.” (Danieli 11:1) Dario hakuwa hai, lakini malaika alirejezea utawala wake kuwa mwanzo wa ujumbe wa kiunabii. Mfalme huyo ndiye aliyeamuru Danieli atolewe kutoka kwenye tundu la simba. Dario alikuwa ameagiza pia kwamba raia zake wamche Mungu wa Danieli. (Danieli 6:21-27) Hata hivyo, malaika huyo hakusimama ili kumwunga mkono Dario Mmedi, bali alimwunga mkono Mikaeli, mshirika wa malaika huyo—yule mkuu wa watu wa Danieli. (Linganisha Danieli 10:12-14.) Malaika wa Mungu alimwunga mkono Mikaeli alipokuwa akishindana na roho waovu wa Umedi na Uajemi.
4, 5. Wafalme wanne wa Uajemi waliotabiriwa walikuwa nani?
4 Malaika wa Mungu aliendelea kusema hivi: “Tazama, watasimama wafalme watatu katika Uajemi; naye mfalme wa nne atakuwa tajiri kuliko hao wote; naye atakapopata nguvu kwa utajiri wake, atawachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani [“Ugiriki,” NW].” (Danieli 11:2) Watawala hao wa Uajemi walikuwa kina nani?
5 Wafalme watatu wa kwanza walikuwa Koreshi Mkuu, Cambyses wa Pili, na Dario wa Kwanza. Kwa kuwa Bardiya (au pengine Gaumata, aliyejisingizia kuwa mfalme) alitawala kwa muda wa miezi saba peke yake, unabii huo haukutilia maanani utawala wake mfupi. Mwaka wa 490 K.W.K., mfalme wa tatu, Dario wa Kwanza, alijaribu kuvamia Ugiriki kwa mara ya pili. Hata hivyo, Waajemi walishindwa vibaya huko Marathon nao wakakimbilia Asia Ndogo. Ingawa Dario alipanga kwa uangalifu vita zaidi dhidi ya Ugiriki, hakuweza kupigana kabla ya kufa kwake miaka minne baadaye. Alimwachia mwana wake Shasta wa Kwanza, ambaye alitawala pia baada yake akiwa mfalme “wa nne.” Ndiye Mfalme Ahasuero aliyemwoa Esta.—Esta 1:1; 2:15-17.
6, 7. (a) Mfalme wa nne ‘aliwachocheaje wote juu ya ufalme wa Ugiriki’? (b) Vita ya Shasta dhidi ya Ugiriki ilikuwa na matokeo gani?
6 Shasta wa Kwanza kwa kweli ‘aliwachochea wote juu ya ufalme wa Ugiriki,’ yaani, yale majimbo huru ya Ugiriki yote pamoja. “Akihimizwa na maofisa wa serikali yake wenye kutaka makuu,” chasema kitabu The Medes and Persians—Conquerors and Diplomats, “Shasta alishambulia toka nchi kavu na baharini.” Mwanahistoria Mgiriki Herodotus, wa karne ya tano K.W.K., aandika kwamba “hakuna mashambulizi mengine yaliyolingana na hili.” Rekodi yake yataarifu kwamba jeshi la majini “lilijumlika kuwa watu 517,610. Askari-jeshi walikuwa 1,700,000; wapanda-farasi walikuwa 80,000; na kuongezea Waarabu waliopanda ngamia, na Walibya waliopigana wakiwa kwenye magari ya vita, ninaokadiria walikuwa 20,000. Kwa hiyo, wanajeshi wote wa nchi kavu na wa majini walijumlika kuwa watu 2,317,610.”
7 Akipanga kupata ushindi kamili, Shasta wa Kwanza aliliongoza jeshi lake kubwa likapigane na Ugiriki mwaka wa 480 K.W.K. Waajemi waliharibu kabisa Athene waliposhinda mbinu ya Ugiriki ya kukawia huko Thermopylae. Hata hivyo, walipofika Salamis walishindwa vibaya. Ugiriki ilishinda tena huko Plataea, mwaka wa 479 K.W.K. Hakuna yeyote kati ya wale wafalme saba waliotawala Milki ya Uajemi baada ya Shasta katika miaka 143 iliyofuata aliyeshambulia Ugiriki. Lakini kukazuka mfalme mwenye nguvu huko Ugiriki.
UFALME MKUBWA WAGAWANYIKA NA KUWA FALME NNE
8. Ni ‘mfalme yupi hodari’ aliyesimama, naye alipataje ‘kutawala kwa mamlaka kubwa na kutenda apendavyo’?
8 “Mfalme hodari atasimama, atakayetawala kwa mamlaka kubwa, na kutenda apendavyo,” akasema malaika. (Danieli 11:3) Aleksanda mwenye umri wa miaka 20 ‘alisimama’ akiwa mfalme wa Makedonia mwaka wa 336 K.W.K. Akawa “mfalme hodari”—Aleksanda Mkuu. Akifuata mipango ya baba yake, Philip wa Pili, aliteka mikoa ya Uajemi huko Mashariki ya Kati. Walipovuka Mto Eufrati na Mto Tigris, watu wake 47,000 walivitawanya vikosi vya Dario wa Tatu vyenye watu 250,000 huko Gaugamela. Hatimaye, Dario akakimbia, akauawa, na hivyo utawala wa Uajemi ukakoma. Ugiriki ikawa serikali ya ulimwengu, na Aleksanda ‘akatawala kwa mamlaka kubwa na kutenda apendavyo.’
9, 10. Unabii wa kwamba ufalme wa Aleksanda hautakuwa wa uzao wake ulithibitikaje kuwa kweli?
9 Aleksanda angeutawala ulimwengu kwa kipindi kifupi tu, kwa kuwa malaika wa Mungu aliongezea kusema hivi: “Naye atakaposimama, ufalme wake utavunjika, na kugawanyika katika pepo nne za mbinguni; lakini hautakuwa wa uzao wake, wala hautakuwa kama mamlaka yake ambayo alitawala kwayo; kwa maana ufalme wake utang’olewa, hata kwa ajili ya wengine zaidi ya hao.” (Danieli 11:4) Umri wa Aleksanda haukuwa umetimia miaka 33 alipougua ghafula na kufa huko Babiloni mwaka wa 323 K.W.K.
10 Milki kubwa ya Aleksanda haikuendelea kutawalwa na “uzao wake.” Ndugu yake Arrhidaeus Philip wa Tatu alitawala kwa muda unaopungua miaka saba naye akauawa mwaka wa 317 K.W.K. kwa kuwa Olympias, mama ya Aleksanda, aliomba auawe. Mwana wa Aleksanda, Aleksanda wa Nne, alitawala hadi mwaka wa 311 K.W.K. wakati Kasanda, mmojawapo wa majenerali wa baba yake, alipomwua. Heracles, mwana haramu wa Aleksanda alijitahidi kutawala kwa kutumia jina la baba yake lakini akauawa mwaka wa 309 K.W.K. Ndivyo nasaba ya Aleksanda ilivyokoma, “mamlaka yake” ikaondoka katika familia yake.
11. Ufalme wa Aleksanda ‘uligawanyikaje katika pepo nne za mbinguni’?
11 Baada ya Aleksanda kufa, ufalme wake ‘uligawanyika katika pepo nne.’ Majenerali wake wengi walizozana walipokuwa wakinyakua maeneo. Jenerali Antigonus wa Kwanza aliyekuwa chongo alijaribu kutawala milki yote ya Aleksanda. Lakini akauawa katika pigano huko Ipsus, Frigia. Kufikia mwaka wa 301 K.W.K., wanne kati ya majenerali wa Aleksanda walikuwa mamlakani wakitawala eneo kubwa ambalo kamanda wao alikuwa ameshinda. Kasanda alitawala Makedonia na Ugiriki. Lisimako akatawala Asia Ndogo na Thrasi. Niketa Seleuko wa Kwanza akatawala Mesopotamia na Siria. Na Ptolemy Lagus akatawala Misri na Palestina. Kama vile neno la kiunabii lilivyokuwa limetabiri, milki kubwa ya Aleksanda iligawanyika na kuwa falme nne za Kigiriki.
WAFALME WAWILI WENYE KUSHINDANA WATOKEA
12, 13. (a) Serikali nne za Kigiriki zilipataje kuwa serikali mbili? (b) Seleuko alianzisha nasaba gani ya watawala huko Siria?
12 Miaka michache baada ya kupata mamlaka, Kasanda akafa, na mwaka wa 285 K.W.K., Lisimako akamiliki sehemu ya Milki ya Ugiriki iliyokuwa Ulaya. Mwaka wa 281 K.W.K., Niketa Seleuko wa Kwanza alimshinda Lisimako vitani na kumiliki sehemu kubwa ya maeneo ya Asia. Gonatas Antigonus wa Pili, mjukuu wa mmoja wa majenerali wa Aleksanda, akaanza kutawala Makedonia mwaka wa 276 K.W.K. Hatimaye, Makedonia ikaanza kutegemea Roma na kisha kuwa mkoa wa Roma mwaka wa 146 K.W.K.
13 Falme mbili kati ya zile falme nne za Kigiriki ndizo zilizokuwa zimesalia zikiwa mashuhuri—ufalme mmoja ukitawalwa na Niketa Seleuko wa Kwanza na ufalme mwingine ukitawalwa na Ptolemy Lagus. Seleuko alianzisha nasaba ya watawala wa Seleuko huko Siria. Miongoni mwa majiji aliyoanzisha mlikuwemo Antiokia—jiji kuu jipya la Siria—na bandari ya Seleucia. Baadaye mtume Paulo alifundisha huko Antiokia, ambapo wafuasi wa Yesu waliitwa Wakristo kwa mara ya kwanza. (Matendo 11:25, 26; 13:1-4) Seleuko aliuawa mwaka wa 281 K.W.K., lakini watawala wa nasaba yake waliendelea kutawala hadi mwaka wa 64 K.W.K. wakati ambapo Jenerali Mroma Gnaeus Pompey aliifanya Siria kuwa mkoa wa Roma.
14. Wafalme wa nasaba ya Ptolemy walianza kutawala Misri lini?
14 Utawala wa Kigiriki uliodumu muda mrefu zaidi kati ya falme hizo nne ni ule wa Ptolemy Lagus, au Ptolemy wa Kwanza, aliyeanza kutawala mwaka wa 305 K.W.K. Nasaba ya wafalme ya Ptolemy aliyoanzisha iliendelea kutawala Misri hadi iliposhindwa na Roma mwaka wa 30 K.W.K.
15. Ni wafalme gani wawili wenye nguvu waliotokana na falme nne za Kigiriki, nao walianzisha ushindani gani?
15 Kwa hiyo, wafalme wawili wenye nguvu—Niketa Seleuko wa Kwanza aliyetawala Siria na Ptolemy wa Kwanza aliyetawala Misri—waliibuka wakiwa wafalme wawili wenye nguvu kutokana na zile falme nne za Kigiriki. Ushindani wa muda mrefu unaofafanuliwa katika Danieli sura ya 11 kati ya “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini,” ulianzishwa na wafalme hao wawili. Malaika wa Yehova hakutaja majina ya wafalme hao, kwa sababu wafalme hao na mataifa yao wangebadilika-badilika katika karne zilizofuata. Bila kutaja mambo yasiyo ya lazima, malaika huyo anataja tu watawala na matukio yanayohusiana na pambano hilo.
PAMBANO LAANZA
16. (a) Wale wafalme wawili walikuwa kaskazini na kusini mwa nani? (b) Ni wafalme gani waliokuwa “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini”?
16 Sikiliza! Akifafanua mwanzo wenye kutokeza wa pambano hilo, malaika wa Yehova asema hivi: “Mfalme wa kusini atakuwa hodari, na mmoja wa wakuu wake [wa Aleksanda]; naye [mfalme wa kaskazini] atakuwa hodari kuliko yeye, naye atakuwa na mamlaka; mamlaka yake itakuwa mamlaka kubwa.” (Danieli 11:5) Majina “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini” yarejezea wafalme walio kaskazini na kusini mwa watu wa Danieli, ambao wakati huo walikuwa wamewekwa huru kutokana na utekwa wa Babiloni na walikuwa wamerudi Yuda. “Mfalme wa kusini” wa kwanza alikuwa Ptolemy wa Kwanza wa Misri. Mmojawapo wa majenerali wa Aleksanda aliyemshinda Ptolemy wa Kwanza na kutawala akiwa na “mamlaka kubwa” alikuwa Mfalme wa Siria, Niketa Seleuko wa Kwanza. Akawa “mfalme wa kaskazini.”
17. Mwanzoni mwa pambano kati ya mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini, Yuda ilitawalwa na nani?
17 Mwanzoni mwa pambano, Yuda ilikuwa ikitawalwa na mfalme wa kusini. Kuanzia mwaka wa 320 K.W.K. hivi, Ptolemy wa Kwanza aliwachochea Wayahudi waende wakae Misri. Jumuiya ya Kiyahudi ikasitawi Aleksandria, ambapo Ptolemy wa Kwanza alianzisha maktaba maarufu. Mfalme wa kusini, Misri iliyokuwa ikitawalwa na nasaba ya Ptolemy, aliendelea kutawala Wayahudi huko Yuda hadi mwaka wa 198 K.W.K.
18, 19. Kadiri wakati ulivyopita, wafalme hao wawili wenye kushindana ‘walifanyaje mapatano’?
18 Kuhusu wafalme hao wawili, malaika alitabiri hivi: “Baada ya miaka kadha wa kadha watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile.” (Danieli 11:6) Hilo lilitimizwaje?
19 Unabii haukumtaja mwana wa Niketa Seleuko wa Kwanza, Antiochus wa Kwanza, ambaye pia alitawala baada yake, kwa sababu hakupigana vita vya kukata maneno dhidi ya mfalme wa kusini. Lakini Antiochus wa Pili, aliyetawala baada yake, alipigana kwa muda mrefu dhidi ya Ptolemy wa Pili, mwana wa Ptolemy wa Kwanza. Antiochus wa Pili na Ptolemy wa Pili walikuwa mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini. Antiochus wa Pili alimwoa Laodice, wakapata mwana aitwaye Seleuko wa Pili, ilhali Ptolemy wa Pili alikuwa na binti aitwaye Berenice. Mwaka wa 250 K.W.K., wafalme hao wawili ‘walifanya mapatano.’ Ili kulipa gharama ya mapatano hayo, Antiochus wa Pili alimtaliki mke wake Laodice na kumwoa Berenice, “binti ya mfalme wa kusini.” Berenice alimzalia mwana aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme cha Siria badala ya wana wa Laodice.
20. (a) “Mkono” wa Berenice ulishindwaje kusimama? (b) Berenice, “hao waliomleta,” na “yeye aliyemtia nguvu” walishindwaje? (c) Ni nani aliyetawala Siria baada ya Antiochus wa Pili kupoteza “mkono wake,” au mamlaka yake?
20 “Mkono” wa Berenice, au nguvu zilizomtegemeza zilitokana na baba yake, Ptolemy wa Pili. Ptolemy wa Pili alipokufa mwaka wa 246 K.W.K., Berenice ‘hakuwa na nguvu za mkono wake’ kwa mume wake. Antiochus wa Pili alimkataa, akamwoa tena Laodice, na kumteua mwana wao kuwa mtawala atakayemfuata. Kama vile Laodice alivyopanga, Berenice na mwana wake wakauawa. Yaonekana kwamba wahudumu waliomleta Berenice toka Misri hadi Siria—“hao waliomleta”—waliuawa pia. Laodice hata alimtilia sumu Antiochus wa Pili, na kwa sababu hiyo “mkono wake,” au mamlaka yake, pia ‘haikusimama.’ Kwa hiyo, baba ya Berenice—“yeye aliyemzaa”—na mume wake wa Siria—ambaye alikuwa amemfanya kuwa mwenye “nguvu” kwa muda—wakafa. Basi Seleuko wa Pili, mwana wa Laodice, akawa mfalme wa Siria. Mambo yote hayo yangemfanya mfalme wa nasaba ya Ptolemy aliyefuata atendeje?
MFALME ALIPIZA KISASI KUUAWA KWA DADA YAKE
21. (a) Ni nani aliyekuwa “chipukizi la mizizi” ya Berenice, naye ‘alisimamaje’? (b) Ptolemy wa Tatu ‘aliingiaje katika ngome ya mfalme wa kaskazini’ na kumshinda?
21 “Katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda,” akasema malaika. (Danieli 11:7) Ndugu ya Berenice ndiye aliyekuwa “chipukizi” la wazazi au “mizizi” ya Berenice. Baba yake alipokufa, ndugu ya Berenice ‘alisimama’ akiwa mfalme wa kusini, Farao wa Misri Ptolemy wa Tatu. Mara moja akaanza kupanga jinsi ya kulipiza kisasi kuuawa kwa dada yake. Kwa kushambulia Mfalme wa Siria Seleuko wa Pili, ambaye Laodice alimtumia kuua Berenice na mwana wake, aliingia katika “ngome ya mfalme wa kaskazini.” Ptolemy wa Tatu aliteka sehemu ya Antiokia yenye ngome na kumwua Laodice. Akielekea mashariki kupitia milki ya mfalme wa kaskazini, alipora Babilonia na kupiga mwendo hadi India.
22. Ptolemy wa Tatu alirudi na nini Misri, na kwa nini ‘alijizuia miaka kadha wa kadha asimwendee mfalme wa kaskazini’?
22 Kisha ikawaje? Malaika wa Mungu atuambia hivi: “Na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadha wa kadha asimwendee mfalme wa kaskazini.” (Danieli 11:8) Zaidi ya miaka 200 mapema, Mfalme wa Uajemi Cambyses wa Pili alikuwa ameshinda Misri na kuichukua miungu ya Misri, “sanamu zao.” Ptolemy wa Tatu alipora Susa, lililokuwa jiji kuu la Uajemi, akachukua miungu hiyo na kuichukua ‘mateka’ hadi Misri. Pia aliteka nyara ‘vyombo vingi vizuri vya fedha na dhahabu’ na kurudi navyo nyumbani. Kwa kuwa alilazimika kurudi nyumbani akakomeshe uasi uliozuka huko, Ptolemy wa Tatu ‘alijizuia asimwendee mfalme wa kaskazini,’ na kutomdhuru zaidi.
MFALME WA SIRIA ALIPIZA KISASI
23. Kwa nini mfalme wa kaskazini ‘alirudi mpaka nchi yake mwenyewe’ baada ya kuingia katika ufalme wa mfalme wa kusini?
23 Mfalme wa kaskazini alitendaje? Danieli aliambiwa hivi: “Ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe.” (Danieli 11:9) Mfalme wa kaskazini—Mfalme Seleuko wa Pili wa Siria—naye pia alishambulia. Aliingia ndani ya “ufalme” au milki ya mfalme wa kusini wa Misri lakini akashindwa. Jeshi lake likiwa limesalia watu wachache tu, Seleuko wa Pili ‘alirudi mpaka nchi yake mwenyewe,’ na kurudi Antiokia, jiji kuu la Siria wapata mwaka wa 242 K.W.K. Alipokufa, mwana wake Seleuko wa Tatu akatawala baada yake.
24. (a) Ni nini kilichompata Seleuko wa Tatu? (b) Mfalme Antiochus wa Tatu wa Siria ‘alifurika na kupita katikati’ ya milki ya mfalme wa kusini jinsi gani?
24 Ni nini kilichotabiriwa kuhusu uzao wa Mfalme Seleuko wa Pili wa Siria? Malaika alimwambia Danieli hivi: “Na wanawe watafanya vita, na kukusanya mkutano wa majeshi makuu; watakaokuja na kufurika na kupita katikati; nao watarudi na kufanya vita mpaka penye ngome yake.” (Danieli 11:10) Na kabla ya miaka mitatu kutimia, utawala wa Seleuko wa Tatu ukakoma alipouawa. Ndugu yake, Antiochus wa Tatu, akatawala Siria baada yake. Mwana huyo wa Seleuko wa Pili alikusanya majeshi mengi ili akamshambulie mfalme wa kusini, ambaye wakati huo alikuwa Ptolemy wa Nne. Mfalme huyo mpya wa kaskazini wa Siria alipigana dhidi ya Misri na kukomboa bandari ya Seleucia, mkoa wa Coele-Siria, jiji la Tiro na jiji la Ptolemaïs, na miji ya karibu. Aliyashinda vibaya majeshi ya Mfalme Ptolemy wa Nne na kutwaa majiji mengi ya Yuda. Masika ya mwaka wa 217 K.W.K., Antiochus wa Tatu aliliacha Ptolemaïs na kwenda kaskazini, “mpaka penye ngome yake” huko Siria. Lakini punde si punde badiliko kubwa lingetokea.
MAMBO YAGEUKA
25. Ptolemy wa Nne na Antiochus wa Tatu walipigana wapi, na ni nini ‘lililowekwa mikononi’ mwa mfalme wa kusini wa Misri?
25 Sawa na Danieli, twasikiza kwa hamu malaika wa Yehova atabiripo hivi: “Mfalme wa kusini ataingiliwa na ghadhabu, naye atatoka na kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini; naye atapanga jeshi kubwa; na jeshi hilo litawekwa mikononi mwake.” (Danieli 11:11) Akiwa na wanajeshi 75,000, mfalme wa kusini, Ptolemy wa Nne, alielekea kaskazini dhidi ya adui. Mfalme wa Siria wa kaskazini, Antiochus wa Tatu, alikuwa ‘amepanga jeshi kubwa’ la watu 68,000 limkabili. Lakini “jeshi” hilo ‘liliwekwa mikononi’ mwa mfalme wa kusini katika pigano huko Raphia, jiji lililo pwani, karibu na mpaka wa Misri.
26. (a) Ni “jeshi” gani lililochukuliwa na mfalme wa kusini katika pigano huko Raphia, na mkataba wa amani uliofanywa huko ulitia ndani nini? (b) Ni katika njia gani Ptolemy wa Nne ‘hakutumia wadhifa wake wenye nguvu’? (c) Mfalme wa kusini aliyefuata alikuwa nani?
26 Unabii huo waendelea kusema hivi: “Atakapokwisha kuchukua lile jeshi, moyo wake utatukuzwa; naye atawaangusha makumi elfu; lakini hataongezewa nguvu [“hatatumia wadhifa wake wenye nguvu,” NW].” (Danieli 11:12) Ptolemy wa Nne, mfalme wa kusini, ‘alichukua’ askari 10,000 wa miguu na askari-wapanda-farasi 300 wa Siria akawaua na kutwaa wafungwa 4,000. Kisha wafalme hao wakafanya mkataba ambamo Antiochus wa Tatu aliachiwa Seleucia, bandari yake ya Siria lakini akapoteza Foinike na Coele-Siria. Kwa sababu ya ushindi huo, moyo wa mfalme wa kusini wa Misri ‘ulitukuzwa,’ hasa dhidi ya Yehova. Ptolemy wa Nne aliendelea kutawala Yuda. Lakini, ‘hakutumia wadhifa wake wenye nguvu’ baada ya ushindi wake dhidi ya mfalme wa kaskazini wa Siria. Badala yake, Ptolemy wa Nne alianza maisha ya ufasiki, na mwana wake mwenye umri wa miaka mitano, Ptolemy wa Tano, akawa mfalme wa kusini aliyefuata miaka kadhaa kabla ya kifo cha Antiochus wa Tatu.
MPORAJI AREJEA
27. Mfalme wa kaskazini alirudije “mwisho wa zamani zile” ili kukomboa eneo lililotekwa na Misri?
27 Kwa sababu ya uporaji wake wote, Antiochus wa Tatu akaja kuitwa Antiochus Mkuu. Malaika alisema hivi juu yake: “Mfalme wa kaskazini atarudi, naye atapanga jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; naye hakika atakuja mwisho wa zamani zile, yaani baada ya miaka kadha wa kadha, pamoja na jeshi kubwa na mali nyingi.” (Danieli 11:13) “Zamani zile” zilikuwa miaka 16 au zaidi baada ya Wamisri kuwashinda Wasiria huko Raphia. Mfalme Ptolemy wa Tano aliyekuwa mchanga alipotawazwa kuwa mfalme wa kusini, Antiochus wa Tatu alipanga “jeshi kubwa kuliko lile la kwanza” ili kukomboa maeneo yaliyokuwa yametwaliwa na mfalme wa kusini wa Misri. Ili kutekeleza lengo lake, alijiunga na Mfalme Philip wa Tano wa Makedonia.
28. Mfalme mchanga wa kusini alikuwa na matatizo gani?
28 Mfalme wa kusini alikuwa na matatizo pia ndani ya ufalme wake. “Zamani zile watu wengi watasimama ili kumpinga mfalme wa kusini,” malaika akasema. (Danieli 11:14a) Watu wengi “wa[li]simama ili kumpinga mfalme wa kusini.” Zaidi ya kukabili majeshi ya Antiochus wa Tatu na mwenzake Mmakedonia, mfalme huyo mchanga wa kusini alikuwa na matatizo nyumbani Misri. Kwa sababu mlezi wake Agathocles, aliyetawala akitumia jina lake, alikuwa akiwatenda vibaya Wamisri, wengi wao waliasi. Malaika aliongezea kusema hivi: “Wenye jeuri [“wana wa wapokonyaji,” NW] miongoni mwa watu wako watajiinua ili kuyathibitisha maono; lakini wataanguka.” (Danieli 11:14b) Hata baadhi ya watu wa Danieli walipata kuwa “wana wa wapokonyaji,” au wanamapinduzi. Lakini ‘ono’ lolote waliloona wanaume hao Wayahudi juu ya mwisho wa utawala wa wasio Wayahudi halikuwa la kweli, nao wangeshindwa, au ‘kuanguka.’
29, 30. (a)“Silaha za kusini” zilishindwaje kukabiliana na shambulio kutoka kaskazini? (b) Mfalme wa kaskazini alipataje ‘kusimama katika nchi ya uzuri’?
29 Malaika wa Yehova alitabiri hivi zaidi: “Mfalme wa kaskazini atakuja, na kufanya kilima [“atauzingira,” BHN], na kuupiga mji wenye maboma; na silaha za kusini hazitaweza kumpinga, wala watu wake wateule, wala hapatakuwa na nguvu za kumpinga. Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, walahapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake.”—Danieli 11:15, 16.
30 Majeshi ya Ptolemy wa Tano, au “silaha za kusini,” yalishindwa na shambulio kutoka kaskazini. Huko Paneas (Kaisaria Filipi), Antiochus wa Tatu alimfukuza Jenerali Scopas wa Misri pamoja na watu 10,000 aliochagua, au ‘wateule wake,’ hadi Sidoni, “mji wenye maboma.” Huko Antiochus wa Tatu ‘aliuzingira,’ na kuiteka bandari hiyo ya Foinike mwaka wa 198 K.W.K. Alitenda “kadiri apendavyo” kwa sababu majeshi ya mfalme wa kusini wa Misri hayakuweza kusimama mbele yake. Kisha Antiochus wa Tatu akapiga mwendo kuelekea Yerusalemu, jiji kuu la “nchi ya uzuri,” Yuda. Mwaka wa 198 K.W.K., Yerusalemu na Yuda ziliacha kutawalwa na mfalme wa kusini wa Misri na kuanza kutawalwa na mfalme wa kaskazini wa Siria. Naye Antiochus wa Tatu, mfalme wa kaskazini, akaanza ‘kusimama katika nchi ya uzuri.’ Mlikuwemo ‘uharibifu mikononi mwake’ kwa Wayahudi wote na Wamisri wote waliompinga. Mfalme huyo wa kaskazini angefanya apendavyo kwa muda mrefu kadiri gani?
ROMA YAMZUIA MPORAJI
31, 32. Kwa nini mfalme wa kaskazini hatimaye “a[li]fanya mapatano” ya amani na mfalme wa kusini?
31 Malaika wa Yehova ajibu hivi: “Naye [mfalme wa kaskazini] atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti wa watu ili amharibu; lakini hilo halitasimama wala kumfaa [“naye hataendelea kuwa wake,” NW].”—Danieli 11:17.
32 Mfalme wa kaskazini, Antiochus wa Tatu, ‘alikaza uso wake’ ili atawale Misri “pamoja na nguvu zote za ufalme wake.” Lakini hatimaye “alifanya mapatano” ya amani na Ptolemy wa Tano, mfalme wa kusini. Madai ya Roma yalikuwa yamemfanya Antiochus wa Tatu abadili mipango yake. Alipoungana na Mfalme Philip wa Tano wa Makedonia dhidi ya mfalme wa Misri mwenye umri mchanga ili watwae eneo lake, walezi wa Ptolemy wa Tano waliomba Roma iwalinde. Roma ilitwaa fursa hiyo ili kuongeza uvutano wake, ikaonyesha nguvu zake.
33. (a) Ni masharti gani ya amani yaliyowekwa kati ya Antiochus wa Tatu na Ptolemy wa Tano? (b) Kusudi la ndoa kati ya Kleopatra wa Kwanza na Ptolemy wa Tano lilikuwa nini, na kwa nini mpango huo haukufua dafu?
33 Akishurutishwa na Roma, Antiochus wa Tatu alimwekea masharti ya amani mfalme wa kusini. Badala ya kusalimisha maeneo aliyokuwa ameteka, kama vile Roma ilivyotaka, Antiochus wa Tatu alipanga kuyahamisha kwa jina tu kwa kumwoza binti yake Kleopatra wa Kwanza—“binti wa watu”—kwa Ptolemy wa Tano. Mikoa iliyotia ndani Yuda, “nchi ya uzuri,” ingetolewa ikiwa mahari. Hata hivyo, wakati wa ndoa mwaka wa 193 K.W.K. mfalme wa Siria hakuachilia mikoa hiyo imwendee Ptolemy wa Tano. Hiyo ilikuwa ndoa ya kisiasa, iliyofanywa ili kutiisha Misri chini ya Siria. Lakini, mpango huo haukufua dafu kwa sababu Kleopatra wa Kwanza ‘hakuendelea kuwa wake,’ kwa kuwa baadaye aliamua kumwunga mkono mume wake. Vita vilipozuka kati ya Antiochus wa Tatu na Waroma, Misri ilijiunga na Roma.
34, 35. (a) Mfalme wa kaskazini aliuelekeza uso wake kwenye ‘nchi zipi za pwani’? (b) Roma ilikomeshaje “aibu” kutoka kwa mfalme wa kaskazini? (c) Antiochus wa Tatu alikufaje, na mfalme wa kaskazini aliyefuata alikuwa nani?
34 Malaika alisema hivi akirejezea kushindwa huko kwa mfalme wa kaskazini: “Baada ya hayo [Antiochus wa Tatu] atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi [“nchi nyingi za pwani na kuzishinda,” BHN]; lakini mkuu mmoja [Roma] ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye [Roma]; naam, aibu yake [kutoka kwa Antiochus wa Tatu] hiyo [Roma] atamrudishia mwenyewe. Ndipo [Antiochus wa Tatu] atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.”—Danieli 11:18, 19.
35 ‘Nchi hizo za pwani’ ni Makedonia, Ugiriki, na Asia Ndogo. Vita vilizuka Ugiriki mwaka wa 192 K.W.K., na Antiochus wa Tatu akashawishiwa aende Ugiriki. Hatimaye Roma ikatangaza vita dhidi yake kwa kuwa ilikasirishwa na jitihada za mfalme wa Siria za kuteka maeneo zaidi huko. Huko Thermopylae alishindwa na Waroma. Mwaka mmoja hivi baada ya kushindwa katika vita ya Magnesia mwaka wa 190 K.W.K., alilazimika kuacha kila kitu huko Ugiriki, Asia Ndogo, na maeneo yaliyo magharibi mwa Milima Taurus. Roma ilimtoza faini kubwa na kusitawisha utawala wake juu ya mfalme wa kaskazini wa Siria. Akiwa amefukuzwa kutoka Ugiriki na Asia Ndogo na baada ya kupoteza karibu meli zake zote, Antiochus wa Tatu ‘aliuelekeza uso wake mwenyewe kwenye ngome za nchi yake mwenyewe,’ Siria. Waroma walikuwa ‘wamemrudishia aibu yake mwenyewe.’ Antiochus wa Tatu alikufa akijaribu kupora hekalu huko Elymaïs, Uajemi, mwaka wa 187 K.W.K. Kwa hiyo, ‘akaanguka’ katika kifo naye mwana wake Seleuko wa Nne, akatawala baada yake akiwa mfalme wa kaskazini aliyefuata.
PAMBANO LAENDELEA
36. (a) Mfalme wa kusini alijaribu kuendelezaje pambano, lakini akapatwa na nini? (b) Seleuko wa Nne aliangukaje, na ni nani aliyetawala baada yake?
36 Akiwa mfalme wa kusini, Ptolemy wa Tano alijaribu kuipata mikoa ambayo alipaswa kupewa ikiwa mahari ya Kleopatra, lakini alitiliwa sumu. Ptolemy wa Sita akatawala baada yake. Vipi juu ya Seleuko wa Nne? Kwa kuwa alihitaji fedha za kulipa faini kubwa aliyodaiwa na Roma, alimtuma mweka-hazina Heliodorus akatwae mali ambazo yasemekana zilikuwa zimewekwa katika hekalu la Yerusalemu. Heliodorus akamuua Seleuko wa Nne kwa kuwa alikitamani kiti cha ufalme. Hata hivyo, Mfalme Eumenes wa Pergamamu na ndugu yake Attalus wakamtawaza Antiochus wa Nne, ndugu ya mfalme aliyeuawa.
37. (a) Antiochus wa Nne alijaribuje kujionyesha kuwa mwenye nguvu kuliko Yehova Mungu? (b) Makufuru ya Antiochus wa Nne dhidi ya hekalu la Yerusalemu yalisababisha nini?
37 Mfalme mpya wa kaskazini, Antiochus wa Nne, alijaribu kujionyesha kuwa mwenye nguvu kuliko Mungu kwa kujaribu kufutilia mbali mpango wa Yehova wa ibada. Alimkaidi Yehova na kuweka wakfu hekalu la Yerusalemu kwa Zeo, au Jupita. Desemba mwaka wa 167 K.W.K., hekalu la kipagani lilijengwa juu ya madhabahu kubwa katika ua wa hekalu ambapo matoleo ya kuteketezwa yalikuwa yakitolewa kwa Yehova kila siku. Siku kumi baadaye, dhabihu ilitolewa kwa Zeo kwenye madhabahu ya kipagani. Wayahudi wakiongozwa na Wamakabayo waliasi kwa sababu ya makufuru hayo. Antiochus wa Nne alipigana nao kwa miaka mitatu. Mwaka wa 164 K.W.K., kwenye ukumbusho wa kila mwaka wa makufuru hayo, Yudasi Makabayo aliliweka wakfu tena hekalu kwa Yehova nao msherehekeo wa wakfu uitwao Hanuka, ukaanzishwa.—Yohana 10:22.
38. Utawala wa Wamakabayo ulikomaje?
38 Huenda Wamakabayo walifanya mkataba na Roma mwaka wa 161 K.W.K. na kuanzisha ufalme mwaka wa 104 K.W.K. Lakini waliendelea kuzozana na mfalme wa kaskazini wa Siria. Hatimaye, Roma ikaitwa iingilie kati. Jenerali Mroma Gnaeus Pompey akateka Yerusalemu mwaka wa 63 K.W.K. baada ya mazingiwa yaliyodumu miezi mitatu. Mwaka wa 39 K.W.K., Seneti ya Roma ikamweka rasmi Herode—Mwedomu—awe mfalme wa Yudea. Baada ya kuukomesha utawala wa Wamakabayo, aliteka Yerusalemu mwaka wa 37 K.W.K.
39. Umenufaikaje kwa kuchunguza Danieli 11:1-19?
39 Yasisimua kama nini kuona sehemu ya kwanza ya unabii juu ya wafalme wawili wanaopambana ikitimia kikamili! Kwa kweli, yasisimua kama nini kuchunguza historia ya miaka ipatayo 500 baada ya Danieli kupokea ujumbe wa kiunabii na pia kuwatambua watawala waliokuwa mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini! Hata hivyo, pambano kati ya wafalme hao wawili liendeleapo wakati wa Yesu Kristo na hata leo, wafalme hao wawili wabadilika-badilika kisiasa. Kwa kuhusianisha mambo ya kihistoria na mambo yenye kupendeza yanayofunuliwa katika unabii huo, tutaweza kuwatambua wafalme hao wawili wenye kushindana.
UMEFAHAMU NINI?
• Ni nasaba zipi mbili za wafalme wenye nguvu zilizotokana na falme za Kigiriki, nao wafalme hao walianza pambano gani?
• Kama ilivyotabiriwa kwenye Danieli 11:6, wafalme hao wawili walifanyaje “mapatano”?
• Pambano liliendeleaje kati ya
Seleuko wa Pili na Ptolemy wa Tatu (Danieli 11:7-9)?
Antiochus wa Tatu na Ptolemy wa Nne (Danieli 11:10-12)?
Antiochus wa Tatu na Ptolemy wa Tano (Danieli 11:13-16)?
• Kleopatra wa Kwanza aliolewa na Ptolemy wa Tano kwa kusudi gani, na kwa nini mpango huo haukufua dafu (Danieli 11:17-19)?
• Kusikiliza Danieli 11:1-19 kumekunufaishaje?
[Chati/Picha katika ukurasa wa 228]
WAFALME KATIKA DANIELI 11:5-19
Mfalme wa Mfalme wa
Kaskazini Kusini
Danieli 11:5 Niketa Seleuko wa I Ptolemy wa Kwanza
Danieli 11:6 Antiochus wa Pili Ptolemy wa Pili
(mke Laodice) (binti Berenice)
Danieli 11:7-9 Seleuko wa Pili Ptolemy wa Tatu
Danieli 11:10-12 Antiochus wa Tatu Ptolemy wa Nne
Danieli 11:13-19 Antiochus wa Tatu Ptolemy wa Tano
(binti, Kleopatra I) Mwaandamizi:
Waandamizi: Ptolemy wa Sita
Seleuko wa Nne na
Antiochus wa Nne
[Picha]
Sarafu yenye picha ya Ptolemy wa Pili na mke wake
[Picha]
Niketa Seleuko wa Kwanza
[Picha]
Antiochus wa Tatu
[Picha]
Ptolemy wa Sita
[Picha]
Ptolemy wa Tatu na waandamizi wake walijenga hekalu hili la Horus huko Idfu, Misri ya Juu
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 216, 217]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MAKEDONIA
UGIRIKI
ASIA NDOGO
ISRAELI
LIBYA
MISRI
ETHIOPIA
SIRIA
Babiloni
ARABIA
[Picha]
Ptolemy wa Pili
[Picha]
Antiochus Mkuu
[Picha]
Bamba la jiwe lenye maagizo rasmi yaliyotolewa na Antiochus Mkuu
[Picha]
Sarafu yenye picha ya Ptolemy wa Tano
[Picha]
Lango la Ptolemy wa Tatu, huko Karnak, Misri
[Picha katika ukurasa wa 210]
[Picha katika ukurasa wa 215]
Seleuko Niketa
[Picha katika ukurasa wa 218]
Ptolemy wa kwanza