Sura Ya Nne
Kuinuka na Kuanguka Kwa Sanamu Kubwa Sana
1. Kwa nini tupendezwe na hali iliyozuka miaka kumi baada ya Mfalme Nebukadreza kuwateka Danieli na wengine?
MIAKA kumi imepita tangu Mfalme Nebukadreza alipompeleka Danieli na “wakuu [wengine] wa nchi” ya Yuda utekwani Babiloni. (2 Wafalme 24:15) Kijana Danieli atumikia katika makao ya mfalme wakati ambapo hali yenye kuhatarisha uhai yazuka. Kwa nini hilo litupendeze? Kwa sababu njia ambayo Yehova Mungu aingilia jambo hilo yaokoa uhai wa Danieli na wa wengine na pia yatuonyesha mfuatano wa serikali za ulimwengu za unabii wa Biblia unaofikia nyakati zetu.
MTAWALA AKABILI TATIZO GUMU
2. Nebukadreza aliota ndoto yake ya kwanza ya kiunabii lini?
2 “Katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza,” nabii Danieli akaandika, “Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha.” (Danieli 2:1) Mwota-ndoto huyo alikuwa Nebukadreza, mfalme wa Milki ya Babiloni. Alipata kuwa mtawala wa ulimwengu mwaka wa 607 K.W.K. wakati ambapo Yehova Mungu alimruhusu aharibu Yerusalemu na hekalu lake. Mwaka wa pili wa utawala wa Nebukadreza akiwa mtawala wa ulimwengu (606/605 K.W.K.), Mungu alimwotesha ndoto yenye kuogofya.
3. Ni nani walioshindwa kufasiri ndoto ya mfalme, naye Nebukadreza aliamuaje?
3 Ndoto hiyo ilimtaabisha Nebukadreza sana hivi kwamba hakuweza kulala. Bila shaka, alikuwa na hamu sana ya kujua maana yake. Lakini mfalme huyo mwenye uweza alikuwa ameisahau ndoto hiyo! Kwa hiyo, akawaita waganga, wachawi, na wasihiri wa Babiloni na kudai wamsimulie ndoto na kuifasiri. Hawakuweza. Kushindwa kwao kulimghadhibisha sana Nebukadreza hivi kwamba akatoa amri ya “kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli.” Amri hiyo ingemfanya nabii Danieli aonane ana kwa ana na mfishaji aliyeteuliwa. Kwa nini? Kwa sababu yeye na waandamani wake watatu Waebrania—Hanania, Mishaeli, na Azaria—walikuwa miongoni mwa watu wenye hekima wa Babiloni.—Danieli 2:2-14.
DANIELI AOKOA JAHAZI
4. (a) Danieli alifahamuje ndoto ya Nebukadreza na maana yake? (b) Danieli alisema nini alipokuwa akimshukuru Yehova Mungu?
4 Baada ya kujua sababu ya amri kali ya Nebukadreza, “Danieli akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonyesha mfalme tafsiri ile.” Ombi hilo lilikubaliwa. Danieli alirudi nyumbani kwake, naye pamoja na rafikize watatu Waebrania wakasali, wakiomba “rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo.” Katika ono usiku huohuo, Yehova alimfunulia Danieli siri ya ndoto hiyo. Akishukuru, Danieli alisema hivi: “Na lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na uweza ni wake. Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa; yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake.” Danieli alimsifu Yehova kwa sababu ya ufahamu huo wenye kina.—Danieli 2:15-23.
5. (a) Alipokuwa mbele ya mfalme, Danieli alimpaje Yehova sifa? (b) Kwa nini ufafanuzi wa Danieli watupendeza leo?
5 Siku iliyofuata, Danieli alimwendea Arioko, amiri wa askari walinzi, aliyekuwa ameteuliwa awaharibu watu wenye hekima wa Babiloni. Alipojua kwamba Danieli angeweza kufasiri ndoto hiyo, Arioko akamkimbiza kwa mfalme. Bila kujisifu, Danieli alimwambia Nebukadreza hivi: “Yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho.” Danieli alikuwa tayari kufunua wakati ujao wa Milki ya Babiloni na pia mfululizo wa matukio ya ulimwengu tangu siku ya Nebukadreza hadi wakati wetu na kuendelea.—Danieli 2:24-30.
NDOTO—YAKUMBUKWA
6, 7. Ni ndoto gani ambayo Danieli alimkumbusha mfalme?
6 Nebukadreza alisikiliza kwa makini Danieli alipokuwa akieleza: “Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha. Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba; miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo. Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa [“mlima mkubwa,” NW], likaijaza dunia yote.”—Danieli 2:31-35.
7 Lazima Nebukadreza awe alisisimuka kama nini kumsikia Danieli akifunua ndoto hiyo! Hebu ngoja kidogo! Watu wenye hekima wa Babiloni wangesalimika iwapo tu Danieli angeifasiri pia ndoto hiyo. Akisema juu yake mwenyewe na juu ya rafikize watatu Waebrania, Danieli alijulisha hivi: “Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme.”—Danieli 2:36.
UFALME WENYE KUSIFIKA SANA
8. (a) Danieli alifafanua kichwa cha dhahabu kuwa nani au nini? (b) Kichwa cha dhahabu kilitokea lini?
8 “Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu; na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu.” (Danieli 2:37, 38) Maneno hayo yalimhusu Nebukadreza baada ya Yehova kumtumia aharibu Yerusalemu, mwaka wa 607 K.W.K. Ndivyo ilivyo kwa kuwa wafalme waliotawazwa Yerusalemu walikuwa wazao wa Daudi, mfalme mtiwa-mafuta wa Yehova. Yerusalemu lilikuwa jiji kuu la Yuda, ufananisho wa ufalme wa Mungu uliowakilisha enzi kuu ya Yehova juu ya dunia. Jiji hilo lilipoharibiwa mwaka wa 607 K.W.K., ufananisho huo wa ufalme wa Mungu ulikoma. (1 Mambo ya Nyakati 29:23; 2 Mambo ya Nyakati 36:17-21) Serikali za ulimwengu zilizofuatana zilizowakilishwa na sehemu za metali za sanamu hiyo zingeweza kuutawala ulimwengu sasa bila kuingiliwa na ufananisho wa ufalme wa Mungu. Akiwa kichwa cha dhahabu, metali ya thamani sana iliyojulikana nyakati za kale, Nebukadreza alipata sifa ya kuupindua ufalme huo kwa kuharibu Yerusalemu.—Ona “Mfalme Mpiganaji Ajenga Milki,” kwenye ukurasa wa 63.
9. Kichwa cha dhahabu kiliwakilisha nini?
9 Nebukadreza, aliyetawala kwa miaka 43, aliongoza nasaba ya wafalme iliyotawala Milki ya Babiloni. Ilitia ndani mwana-mkwe wake Nabonido na mwana wake mkubwa, Evil-merodaki. Nasaba hiyo ya wafalme iliendelea kwa miaka mingine 43, hadi Belshaza, mwana wa Nabonido, alipokufa mwaka wa 539 K.W.K. (2 Wafalme 25:27; Danieli 5:30) Kwa hiyo, kichwa cha dhahabu katika sanamu ya ndoto hakikuwakilisha Nebukadreza tu bali watawala wote wa Babiloni.
10. (a) Ndoto ya Nebukadreza ilionyeshaje kwamba Serikali ya Ulimwengu ya Babiloni haingedumu? (b) Nabii Isaya alitabiri nini juu ya yule ambaye angeshinda Babiloni? (c) Umedi na Uajemi zilikuwaje ndogo kuliko Babiloni?
10 Danieli alimwambia Nebukadreza hivi: “Baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe.” (Danieli 2:39) Ufalme uliofananishwa na kifua na mikono ya fedha ya sanamu hiyo ungeandama nasaba ya wafalme ya Nebukadreza. Miaka 200 hivi mapema, Isaya alikuwa ametabiri ufalme huo, hata akataja jina la mfalme wake mshindi—Koreshi. (Isaya 13:1-17; 21:2-9; 44:24–45:7, 13) Utawala huo ulikuwa Milki ya Umedi na Uajemi. Hata ingawa Umedi na Uajemi zilitokeza ustaarabu mkubwa ambao haukuwa duni ukilinganishwa na ule wa Milki ya Babiloni, ufalme huo wa Umedi na Uajemi wawakilishwa na fedha, metali yenye thamani ndogo kuliko dhahabu. Ulikuwa mdogo kuliko Serikali ya Ulimwengu ya Babiloni kwa kuwa haukupata sifa ya kupindua Yuda, ufananisho wa ufalme wa Mungu wenye jiji lake kuu Yerusalemu.
11. Nasaba ya wafalme ya Nebukadreza ilikoma lini?
11 Miaka 60 hivi baada ya kufasiri ile ndoto, Danieli alishuhudia mwisho wa nasaba ya wafalme ya Nebukadreza. Danieli alikuwapo usiku wa Oktoba 5/6, 539 K.W.K., wakati ambapo jeshi la Umedi na Uajemi lilishinda Babiloni lililoonekana kuwa lisiloweza kushindwa, na kumwua Mfalme Belshaza. Belshaza alipokufa, kichwa cha dhahabu cha sanamu ya ndoto—Milki ya Babiloni—kikakoma.
WATU WALIOHAMISHWA WAWEKWA HURU NA UFALME FULANI
12. Amri iliyotolewa na Koreshi mwaka wa 537 K.W.K. iliwanufaishaje Wayahudi waliokuwa uhamishoni?
12 Umedi na Uajemi ulichukua mahali pa Milki ya Babiloni na kuwa serikali kuu ya ulimwengu mwaka wa 539 K.W.K. Akiwa na umri wa miaka 62, Dario Mmedi akawa mtawala wa kwanza wa jiji lililoshindwa la Babiloni. (Danieli 5:30, 31) Kwa kipindi kifupi, yeye na Koreshi Mwajemi walitawala pamoja Milki ya Umedi na Uajemi. Dario alipokufa, Koreshi akawa mtawala pekee wa Milki ya Uajemi. Kwa Wayahudi katika Babiloni, kutawala kwa Koreshi kulimaanisha kuachiliwa kutoka utekwani. Mwaka wa 537 K.W.K., Koreshi alitoa amri iliyoruhusu Wayahudi waliohamishwa Babiloni warudi nyumbani na kujenga upya Yerusalemu na hekalu la Yehova. Hata hivyo, ufananisho wa ufalme wa Mungu, haukusimamishwa tena katika Yuda na Yerusalemu.—2 Mambo ya Nyakati 36:22, 23; Ezra 1:1–2:2a.
13. Kifua na mikono ya fedha ya sanamu ya ndoto ya Nebukadreza ziliwakilisha nini?
13 Kifua na mikono ya fedha ya sanamu ya ndoto zawakilisha wafalme wa Uajemi kuanzia Koreshi Mkuu. Nasaba hiyo ya wafalme ilidumu kwa zaidi ya miaka 200. Yadhaniwa kwamba Koreshi alikufa akiwa katika kampeni ya kijeshi mwaka wa 530 K.W.K. Kati ya wafalme wapatao 12 waliomwandama katika kiti cha ufalme cha Milki ya Uajemi, angalau 2 waliwatendea vizuri wateule wa Yehova. Mmoja alikuwa Dario wa Kwanza (Mwajemi), na yule mwingine alikuwa Artashasta wa Kwanza.
14, 15. Dario Mkuu na Artashasta wa Kwanza waliwasaidiaje Wayahudi?
14 Dario wa Kwanza alikuwa mfalme wa tatu wa Uajemi baada ya Koreshi Mkuu. Yawezekana kwamba wafalme wawili waliomtangulia walikuwa Cambyses wa Pili na ndugu yake Bardiya (au pengine Gaumata, Mamajusi aliyejisingizia kuwa mfalme). Kufikia wakati ambapo Dario wa Kwanza, aliyeitwa pia Dario Mkuu, alikalia kiti cha ufalme mwaka wa 521 K.W.K., kazi ya kujenga upya hekalu katika Yerusalemu ilikuwa imepigwa marufuku. Alipoipata hati iliyokuwa na amri ya Koreshi katika hifadhi za nyaraka huko Ecbatana, Dario aliondoa marufuku hiyo mwaka wa 520 K.W.K. na kufanya mengi zaidi. Pia alitoa fedha kwenye hazina ya kifalme kwa minajili ya ujenzi wa hekalu.—Ezra 6:1-12.
15 Mtawala Mwajemi wa pili aliyesaidia katika jitihada za kurudi kwa Wayahudi alikuwa Artashasta wa Kwanza, aliyemwandama baba yake Ahasuero (Shasta wa Kwanza) mwaka wa 475 K.W.K. Artashasta alipachikwa jina Longimanus kwa sababu mkono wake wa kulia ulikuwa mrefu kuliko wa kushoto. Mwaka wa 20 wa utawala wake, mwaka wa 455 K.W.K., alimwagiza Nehemia, mnyweshaji wake Myahudi, awe liwali wa Yuda na kujenga upya kuta za Yerusalemu. Tendo hilo liliashiria mwanzo wa ‘majuma sabini ya miaka’ yaliyotajwa katika sura ya 9 ya Danieli na kuweka tarehe ya kutokea na ya kifo cha Mesiya, au Kristo, Yesu wa Nazareti.—Danieli 9:24-27; Nehemia 1:1; 2:1-18.
16. Serikali ya Ulimwengu ya Umedi na Uajemi ilikoma lini, mfalme yupi akitawala?
16 Mfalme wa mwisho kati ya wale sita waliotawala baada ya Artashasta wa Kwanza wa Milki ya Uajemi alikuwa Dario wa Tatu. Utawala wake ulikoma ghafula mwaka wa 331 K.W.K. aliposhindwa vibaya na Aleksanda Mkuu huko Gaugamela, karibu na Ninewi la kale. Ushinde huo ulikomesha Serikali ya Ulimwengu ya Umedi na Uajemi iliyofananishwa na fedha katika sanamu ya ndoto ya Nebukadreza. Serikali ambayo ingefuata ilikuwa kuu katika njia fulani-fulani, na pia ndogo katika njia nyinginezo. Hilo ladhihirika tusikilizapo Danieli afasiripo zaidi ndoto ya Nebukadreza.
UFALME—MKUBWA LAKINI HAFIFU
17-19. (a) Tumbo na viuno vya shaba viliwakilisha serikali gani ya ulimwengu, na utawala wake ulienea kiasi gani? (b) Aleksanda wa Tatu alikuwa nani? (c) Kigiriki kilipataje kuwa lugha ya kimataifa, nacho kilifaa kwa ajili ya nini?
17 Danieli alimwambia Nebukadreza kwamba tumbo na viuno vya sanamu hiyo kubwa vilikuwa “ufalme mwingine wa tatu wa shaba, [ambao ungeitawala] dunia yote.” (Danieli 2:32, 39) Ufalme huo wa tatu ungetawala baada ya Babilonia, na Umedi na Uajemi. Kama vile shaba ni duni kuliko fedha, hiyo serikali kuu mpya ya ulimwengu ingekuwa ndogo kuliko serikali ya Umedi na Uajemi kwa kuwa haingepata pendeleo kama lile la kuwaweka huru watu wa Yehova. Hata hivyo, ufalme huo ulio kama shaba ‘ungeitawala dunia yote,’ kuonyesha kwamba ungeenea zaidi kuliko Babilonia au Umedi na Uajemi. Mambo ya hakika ya historia yaonyesha nini juu ya serikali hiyo ya ulimwengu?
18 Punde baada ya kurithi utawala wa Makedonia mwaka wa 336 K.W.K. akiwa na umri wa miaka 20, Aleksanda wa Tatu mwenye kujitakia makuu alianza kampeni yake ya ushindi. Kwa sababu ya ushindi wake mbalimbali wa kijeshi, akaja kuitwa Aleksanda Mkuu. Akipata ushindi mmoja baada ya mwingine, alizidi kuingia katika eneo la Uajemi. Alipomshinda Dario wa Tatu katika pambano huko Gaugamela mwaka wa 331 K.W.K., Milki ya Uajemi ilianza kuporomoka na Aleksanda akasimamisha Ugiriki kuwa serikali kuu mpya ya ulimwengu.
19 Baada ya ushindi huko Gaugamela, Aleksanda akatwaa Babiloni, Susa, Persepolisi, na Ecbatana, yaliyokuwa majiji makuu ya Uajemi. Akiwa ametiisha sehemu iliyosalia ya Milki ya Uajemi, alieneza ushindi wake hadi India magharibi. Koloni za Kigiriki zilianzishwa katika nchi zilizoshindwa. Kwa hiyo, lugha na utamaduni wa Kigiriki ukaenea kotekote katika milki hiyo. Kwa hakika, milki ya Ugiriki ikawa kubwa kuliko milki zote zilizoitangulia. Kama vile ambavyo Danieli alikuwa ametabiri, ufalme wa shaba ‘ulitawala dunia yote.’ Tokeo lake moja ni kwamba Kigiriki (Kikoine) kikawa lugha ya kimataifa. Kwa kuwa kingeweza kueleza mambo kwa usahihi, kilifaa zaidi kutumiwa kuandika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo na katika kueneza habari njema ya Ufalme wa Mungu.
20. Milki ya Ugiriki ilipatwa na nini baada ya kifo cha Aleksanda Mkuu?
20 Aleksanda Mkuu aliishi miaka minane tu akiwa mtawala wa ulimwengu. Ingawa bado alikuwa mchanga, Aleksanda aliyekuwa na umri wa miaka 32 alishikwa na ugonjwa baada ya karamu na kufa muda mfupi baadaye, Juni 13, 323 K.W.K. Punde si punde, milki yake kubwa ikagawanyika kuwa maeneo manne, kila moja likitawalwa na mmoja wa majenerali wake. Hivyo, ufalme mmoja mkubwa ulitokeza falme nne ambazo hatimaye zilishindwa na Milki ya Roma. Serikali ya ulimwengu iliyokuwa kama shaba iliendelea hadi mwaka wa 30 K.W.K. wakati tu ambapo ufalme wa mwisho kati ya falme hizo nne—nasaba ya wafalme ya Ptolemy iliyokuwa ikitawala Misri—iliposhindwa hatimaye na Roma.
UFALME UVUNJAVUNJAO NA KUSETA
21. Danieli aliufafanuaje “ufalme wa nne”?
21 Danieli aliendelea kufafanua sanamu ya ndoto: “Ufalme wa nne [baada ya Babiloni, Umedi na Uajemi, na Ugiriki] utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta.” (Danieli 2:40) Katika nguvu na uweza wake wa kuvunjavunja, serikali hiyo ya ulimwengu ingekuwa kama chuma—yenye nguvu kuliko milki zilizowakilishwa na dhahabu, fedha, au shaba. Milki ya Roma ilikuwa na nguvu hiyo.
22. Milki ya Roma ilikuwaje kama chuma?
22 Roma ilivunjavunja na kuseta Milki ya Ugiriki na kumaliza masalio ya serikali ya ulimwengu ya Umedi na Uajemi na ile ya Babiloni. Pasipo kustahi Ufalme wa Mungu uliotangazwa na Yesu Kristo, serikali hiyo ilimwua kwenye mti wa mateso mwaka wa 33 W.K. Ikijaribu kuseta Ukristo wa kweli, Roma iliwanyanyasa wanafunzi wa Yesu. Isitoshe, Waroma waliharibu Yerusalemu na hekalu lake mwaka wa 70 W.K.
23, 24. Zaidi ya Milki ya Roma, miguu ya sanamu yawakilisha nini?
23 Miguu ya chuma ya sanamu ya ndoto ya Nebukadreza haikuwakilisha Milki ya Roma peke yake bali pia tawala za kisiasa zilizotokana nao. Fikiria maneno haya yaliyorekodiwa kwenye Ufunuo 17:10: “Kuna wafalme saba: watano wameanguka, mmoja yuko, na mwingine bado hajawasili, lakini awasilipo lazima adumu kwa muda mfupi.” Mtume Yohana alipoandika maneno hayo, Waroma walikuwa wamempeleka uhamishoni, kwenye kisiwa cha Patmosi. Wafalme watano waliokuwa wameanguka, au serikali za ulimwengu, walikuwa Misri, Ashuru, Babiloni, Umedi na Uajemi, na Ugiriki. Mfalme wa sita—Milki ya Roma—angali alikuwa mamlakani. Lakini yeye pia angeanguka, na mfalme wa saba angeinuka kutoka katika mojawapo ya maeneo yaliyotekwa na Roma. Serikali hiyo ya ulimwengu ingekuwa gani?
24 Wakati mmoja, Uingereza ilikuwa sehemu ya kaskazini-magharibi ya Milki ya Roma. Lakini kufikia mwaka wa 1763, ilikuwa imekuwa Milki ya Uingereza—Uingereza iliyotawala bahari zote. Kufikia mwaka wa 1776 koloni zake 13 za Amerika zilikuwa zimejitangazia uhuru ili ziwe Marekani. Hata hivyo, miaka ya baadaye, Uingereza na Marekani zilikuja kushirikiana katika vita na katika amani. Kwa hiyo, muungano wa Uingereza na Marekani ukatokea ukiwa serikali ya saba ya ulimwengu, ya unabii wa Biblia. Sawa na Milki ya Roma, imethibitika kuwa yenye “nguvu mfano wa chuma,” yenye kutekeleza mamlaka kama ya chuma. Kwa hiyo, miguu ya chuma ya sanamu ya ndoto yatia ndani Milki ya Roma, na serikali ya ulimwengu yenye sehemu mbili ya Uingereza na Marekani.
MUUNGANO DHAIFU
25. Danieli alisema nini juu ya nyayo na vidole vya miguu ya sanamu hiyo?
25 Kisha Danieli akamwambia Nebukadreza hivi: “Kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope. Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika. Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo.”—Danieli 2:41-43.
26. Utawala unaowakilishwa na nyayo na vidole vya miguu wajidhihirisha lini?
26 Mfuatano wa serikali za ulimwengu uliowakilishwa na sehemu mbalimbali za sanamu katika ndoto ya Nebukadreza ulianzia kichwani hadi nyayo za miguu. Kupatana na akili, nyayo za miguu na vidole vya ‘chuma kilichochanganyika na udongo wa matope’ zingefananisha mwisho wa utawala wa kibinadamu ambao ungekuwako “wakati wa mwisho.”—Danieli 12:4.
27. (a) Ni hali gani inayowakilishwa na nyayo na vidole vya miguu vya chuma kilichochanganyika na udongo? (b) Vidole kumi vya miguu ya sanamu hiyo vyawakilisha nini?
27 Mwanzoni mwa karne ya 20, Milki ya Uingereza ilitawala zaidi ya robo moja ya dunia. Milki nyingine za Ulaya zilitawala mamilioni mengine ya watu. Lakini Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilitokeza vikundi vya mataifa badala ya milki mbalimbali. Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, mwelekeo huo uliongezeka. Utukuzo wa taifa ulipositawi zaidi, idadi ya mataifa ulimwenguni iliongezeka sana. Vile vidole kumi vya miguu ya sanamu vyawakilisha serikali zote zitawalazo wakati uleule, kwa kuwa katika Biblia nambari kumi nyakati nyingine huonyesha ukamili wa kidunia.—Linganisha Kutoka 34:28; Mathayo 25:1; Ufunuo 2:10.
28, 29. (a) Kulingana na Danieli, udongo uliwakilisha nini? (b) Ni nini kiwezacho kusemwa juu ya mchanganyiko wa chuma na udongo?
28 Kwa kuwa sasa tuko katika “wakati wa mwisho,” tumefikia nyayo za miguu ya sanamu. Baadhi ya serikali zilizowakilishwa na nyayo na vidole vya miguu ya sanamu hiyo, vya chuma kilichochanganyika na udongo, ni kama chuma—za kimabavu au kidikteta. Nyingine ni kama udongo. Vipi? Danieli alihusianisha udongo na “mbegu [“uzao,” NW] za wanadamu.” (Danieli 2:43) Licha ya kwamba udongo, ambao wazao wa binadamu wamefanyizwa kutokana nao, waweza kuvunjika kwa urahisi, tawala za kawaida zilizo kama chuma zimelazimika kuwasikiliza watu wa kawaida zaidi na zaidi, wanaotaka kuwa na usemi katika serikali inayowatawala. (Ayubu 10:9) Lakini utawala wa kimabavu hauwezi kamwe kushikamana na watu wa kawaida—kama vile tu chuma hakiwezi kuungana na udongo. Sanamu hiyo itakapofikia mwisho wake, ulimwengu utakuwa umegawanyika kisiasa kwelikweli!
29 Je, mgawanyiko wa nyayo na vidole vya miguu utasababisha sanamu nzima iporomoke? Ni nini kitakachoipata sanamu hiyo?
UPEO WENYE KUTOKEZA!
30. Fafanua upeo wa ndoto ya Nebukadreza.
30 Fikiria upeo wa ndoto hiyo. Danieli alimwambia mfalme hivi: “Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa [“mlima mkubwa,” NW], likaijaza dunia yote.”—Danieli 2:34, 35.
31, 32. Ni nini kilichotabiriwa juu ya sehemu ya mwisho ya ndoto ya Nebukadreza?
31 Unabii huo waendelea kufafanua hivi: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. Na kama vile ulivyoona ya kuwa jiwe lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunja-vunja kile chuma, na ile shaba, na ule udongo, na ile fedha, na ile dhahabu; basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti.”—Danieli 2:44, 45.
32 Akitambua kuwa amekumbushwa na kufafanuliwa ndoto yake, Nebukadreza alikiri kwamba Mungu wa Danieli peke yake ndiye “Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri.” Vilevile mfalme alimpa Danieli na waandamani wake watatu Waebrania vyeo vya madaraka makubwa. (Danieli 2:46-49) Ingawa hivyo, ‘tafsiri thabiti’ ya Danieli yamaanisha nini leo?
‘MLIMA WAIJAZA DUNIA’
33. “Jiwe” lilichongwa kutoka “mlima” gani, na jambo hilo lilitukia lini na jinsi gani?
33 “Nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa” zilipokoma Oktoba mwaka wa 1914, “Mungu wa mbinguni” aliusimamisha Ufalme wa kimbingu kwa kumtawaza Mwana wake mtiwa-mafuta, Yesu Kristo, awe “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.”a (Luka 21:24; Ufunuo 12:1-5; 19:16) Kwa hiyo, “jiwe” la Ufalme wa Kimesiya lilichongwa kutoka katika “mlima” wa enzi kuu ya ulimwengu ya Yehova kwa nguvu za Mungu, wala halikuchongwa kwa mikono ya kibinadamu. Serikali hiyo ya kimbingu imo mikononi mwa Yesu Kristo, ambaye Mungu amemvika kutoweza kufa. (Waroma 6:9; 1 Timotheo 6:15, 16) Kwa hiyo, “ufalme [huo] wa Bwana [Mungu] wetu na wa Kristo wake”—unaowakilisha enzi kuu ya ulimwengu ya Yehova—hautaachiwa mtu mwingine. Utadumu milele.—Ufunuo 11:15.
34. Ufalme wa Mungu ulizaliwaje “siku za wafalme hao”?
34 Ufalme huo ulizaliwa “siku za wafalme hao.” (Danieli 2:44) Hao hawakuwa tu wafalme waliowakilishwa na vile vidole kumi vya miguu bali pia waliowakilishwa na chuma, shaba, fedha, na dhahabu. Ingawa milki ya Babiloni, Uajemi, Ugiriki, na Roma zilikuwa zimepitilia mbali zikiwa serikali za ulimwengu, masalio yake yangali yalikuwako mwaka wa 1914. Wakati huo Milki ya Uturuki ilitawala eneo la Babiloni, na serikali za kitaifa zilikuwako Uajemi (Iran) na Ugiriki na Roma, Italia.
35. “Jiwe” litaipiga sanamu lini, nayo sanamu hiyo itaharibiwa kwa kiasi gani?
35 Karibuni Ufalme wa Mungu wa kimbingu utaipiga sanamu ya mfano kwenye nyayo za miguu yake. Tokeo litakuwa kwamba falme zote zinazofananishwa na sanamu hiyo ya metali zitavunjwa vipande-vipande, na kukomeshwa. Kwa kweli, kwenye “vita ya siku kubwa ya Mungu Mweza-Yote,” “jiwe” hilo litaipiga sanamu hiyo kwa kishindo kikubwa hivi kwamba itapondwa iwe ungaunga nao upepo wa dhoruba ya Mungu utaupeperusha kama vile makapi ya viwanja vya kupepetea. (Ufunuo 16:14, 16) Kisha, kama lile jiwe lililokua likawa kubwa kama mlima na kuijaza dunia, Ufalme wa Mungu utakuwa mlima wa kiserikali utakaoitawala “dunia yote.”—Danieli 2:35.
36. Kwa nini Ufalme wa Kimesiya waweza kusemwa kuwa serikali thabiti?
36 Ingawa Ufalme wa Kimesiya ni wa kimbingu, utamiliki dunia yetu ili kubariki wakaaji wote watiifu wa dunia. Serikali hiyo thabiti “ha[i]taangamizwa milele” wala “watu wengine hawataachiwa enzi yake.” Tofauti na falme za watawala wa kibinadamu ambao hufa, “[i]tasimama milele na milele.” (Danieli 2:44) Na uwe na pendeleo la kuwa mmoja wa raia zake milele.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Sura ya 6 ya kitabu hiki.
UMEFAHAMU NINI?
• Ni serikali gani za ulimwengu zinazowakilishwa na sehemu za ile sanamu kubwa sana ya ndoto ya Nebukadreza?
• Ni hali gani ya ulimwengu inayowakilishwa na nyayo na vidole kumi vya miguu ya chuma kilichochanganyika na udongo?
• “Jiwe” lilichongwa kutoka “mlima” gani, na lini?
• “Jiwe” litaipiga sanamu lini?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 63-67]
MFALME MPIGANAJI AJENGA MILKI
MWANA-MFALME atakayerithi ufalme wa Babiloni na jeshi lake aseta majeshi ya Misri ya Farao Neko huko Karkemishi, Siria. Wamisri walioshindwa watorokea kusini kuelekea Misri, nao Wababiloni wawafuata. Lakini ujumbe fulani kutoka Babiloni wamlazimisha mwana-mfalme mshindi aache kuwafuata. Habari hiyo yasema kwamba Nabopolasa, baba yake, amekufa. Akiwapa majenerali wake jukumu la kuleta mateka na nyara, Nebukadreza arudi nyumbani haraka na kutwaa kiti cha ufalme kilichoachwa na babake.
Hivyo, Nebukadreza akakalia kiti cha ufalme wa Babiloni mwaka wa 624 K.W.K. na kuwa mtawala wa pili wa Milki Mpya ya Babiloni. Katika utawala wake wa miaka 43, alitwaa maeneo yaliyokuwa ya Serikali ya Ulimwengu ya Ashuru na kupanua utawala wake, akitwaa Siria iliyokuwa kaskazini na Palestina iliyokuwa magharibi hadi mpaka wa Misri.—Ona ramani.
Mwaka wa nne wa kutawala kwake (620 K.W.K.), Nebukadreza aliufanya ufalme wa Yuda kuwa chini yake. (2 Wafalme 24:1) Miaka mitatu baadaye, uasi wa Yuda ulifanya Yerusalemu lizingirwe na Babiloni. Nebukadreza alimchukua Yehoyakimu, Danieli, na wengine na kuwapeleka Babiloni wakiwa mateka. Mfalme huyo alichukua pia baadhi ya vyombo vya hekalu la Yehova. Alimfanya Sedekia, mjomba wa Yehoyakimu, awe mfalme kibaraka wa Yuda.—2 Wafalme 24:2-17; Danieli 1:6, 7.
Wakati fulani baadaye, Sedekia pia aliasi, akajiunga na Misri. Nebukadreza alizingira Yerusalemu tena, na mwaka wa 607 K.W.K., alibomoa kuta zake, akalichoma hekalu, na kuliharibu jiji hilo. Aliwaua wana wote wa Sedekia kisha akampofusha Sedekia na kumfunga, ili amtwae akiwa mfungwa hadi Babiloni. Nebukadreza aliteka watu wengi na kusafirisha vyombo vya hekalu vilivyosalia hadi Babiloni. “Hivyo Yuda wakachukuliwa utumwani kutoka nchi yao.”—2 Wafalme 24:18–25:21.
Nebukadreza alishinda Tiro pia kwa kulizingira—mazingiwa yaliyodumu kwa miaka 13. Wakati wa mazingiwa hayo, vichwa vya askari-jeshi wake “[v]ilitiwa upaa” kwa sababu ya kusuguliwa na kofia za chuma, na mabega yao ‘yaliambuliwa ngozi’ kwa sababu ya kubeba vifaa vya kujengea kuta za mazingiwa. (Ezekieli 29:18) Hatimaye, Tiro likasalimu amri mikononi mwa majeshi ya Babiloni.
Ni dhahiri kwamba mfalme wa Babiloni alikuwa askari-jeshi mwerevu sana. Vitabu fulani vya marejezo, hasa vya Babiloni, vyamfafanua pia kuwa mfalme asiye na upendeleo. Ingawa Maandiko hayasemi kihususa kwamba Nebukadreza hakuwa na upendeleo, nabii Yeremia alisema kwamba hata ingawa Sedekia alikuwa ameasi, angetendewa kwa haki ‘kama angetoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli.’ (Yeremia 38:17, 18) Na baada ya kuharibiwa kwa Yerusalemu, Nebukadreza alimtendea Yeremia kwa heshima. Kuhusu Yeremia, mfalme aliamuru hivi: “Mtwae, umtunze sana, wala usimtende neno baya lo lote; lakini umtendee kama atakavyokuambia.”—Yeremia 39:11, 12; 40:1-4.
Akiwa msimamizi, Nebukadreza alitambua upesi sifa na uwezo wa Danieli na waandamani wake watatu—Shadraka, Meshaki, na Abednego—ambao majina yao ya Kiebrania yalikuwa Hanania, Mishaeli, na Azaria. Kwa hiyo, mfalme aliwatumia katika vyeo vikubwa katika ufalme wake.—Danieli 1:6, 7, 19-21; 2:49.
Nebukadreza alimcha hasa Marduki, mungu mkuu wa Babiloni. Mfalme alimsifia Marduki ushindi wake wote. Katika Babiloni, alijenga na kurembesha mahekalu ya Marduki na miungu mingine kadhaa ya Babiloni. Huenda ikawa sanamu ya dhahabu iliyosimamishwa kwenye uwanda wa Dura ilikuwa imewekwa wakfu kwa Marduki. Na yaonekana Nebukadreza alitegemea sana uaguzi akipanga mambo yake ya kijeshi.
Pia Nebukadreza alionea fahari kujenga upya Babiloni, lililokuwa jiji kuu zaidi lenye kuta la wakati huo. Kwa kumalizia ujenzi wa zile kuta mbili kubwa za jiji hilo ambazo baba yake alikuwa ameanza kujenga, Nebukadreza alifanya jiji hilo lionekane lisiloweza kushindwa. Mfalme alirekebisha makao ya zamani ya kifalme yaliyokuwa katikati ya jiji na kujenga makao ya kifalme ya wakati wa kiangazi kilometa mbili hivi upande wa kaskazini. Ili kumridhisha mke wake Mmedi, aliyetamani vilima na misitu ya nyumbani kwao, yaripotiwa kwamba Nebukadreza alijenga zile bustani zenye kuning’inia—ambazo zasemwa kuwa mojawapo ya maajabu saba ya ulimwengu wa kale.
“Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?” akajisifu mfalme siku moja alipokuwa akitembea huku na huku katika makao ya kifalme ya Babiloni. “Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme,” akarukwa na akili. Kwa kuwa hakustahili kutawala kwa miaka saba, alikula majani, kama vile Danieli alivyokuwa ametabiri. Mwishoni mwa kipindi hicho, Nebukadreza alirudishiwa ufalme wake, akatawala mpaka alipokufa mwaka wa 582 K.W.K.—Danieli 4:30-36.
UMEFAHAMU NINI?
Ni nini kiwezacho kusemwa juu ya Nebukadreza akiwa
• askari-jeshi mwerevu?
• msimamizi?
• mwabudu-Marduki?
• mjenzi?
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MILKI YA BABILONI
BAHARI NYEKUNDU
Yerusalemu
Mto Eufrati
Mto Tigris
Ninewi
Susa
Babiloni
Uru
[Picha]
Babiloni, jiji kubwa zaidi lenye kuta la wakati huo
[Picha]
Joka lilifananisha Marduki
[Picha]
Bustani zenye kuning’inia za Babiloni zilizo maarufu
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 56]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
SERIKALI ZA ULIMWENGU ZA UNABII WA DANIELI
Ile sanamu kubwa sana (Danieli 2:31-45)
BABILONI kuanzia 607 K.W.K.
UMEDI NA UAJEMI kuanzia 539 K.W.K.
UGIRIKI kuanzia 331 K.W.K.
ROMA kuanzia 30 K.W.K.
UINGEGEREZA NA MAREKANI kuanzia 1763 W.K.
ULIMWENGU ULIOGAWANYIKA KISIASA wakati wa mwisho
[Picha katika ukurasa wa 47]
[Picha katika ukurasa wa 58]