Sura Ya Saba
Maneno Manne Yaliyoubadili Ulimwengu
1. Maneno manne yaliyoandikwa ukutani muda mrefu uliopita yalikuwa na matokeo makubwa kadiri gani?
MANENO manne sahili yaliandikwa kwenye ukuta uliopigwa plasta. Ingawa yalikuwa sahili, maneno hayo manne yalimwogofya sana mtawala mmoja mwenye nguvu. Yalitangaza kuondolewa kwa wafalme wawili, kifo cha mmoja wao, na mwisho wa serikali ya ulimwengu yenye nguvu. Maneno hayo yalitokeza kudhiliwa kwa jumuiya ya kidini iliyostahiwa sana. Isitoshe, yalikweza ibada safi ya Yehova na kuthibitisha tena enzi yake kuu wakati ambapo watu wengi hawakuheshimu ibada safi na enzi yake kuu. Naam, maneno hayo hata yalionyesha matukio ya ulimwengu leo! Maneno manne yangewezaje kufanya yote hayo? Acheni tuone.
2. (a) Ni nini kilichotokea Babiloni baada ya Nebukadreza kufa? (b) Ni nani aliyekuwa akitawala wakati huo?
2 Makumi ya miaka yalikuwa yamepita tangu mambo yaliyofafanuliwa katika sura ya 4 ya kitabu cha Danieli yalipotukia. Utawala wa Mfalme Nebukadreza mwenye kiburi uliochukua miaka 43 katika Babiloni ulikoma alipokufa mwaka wa 582 K.W.K. Washiriki kadhaa wa familia yake walitawala baada yake wakifuatana, lakini kifo cha mapema au kuuawa kulikomesha utawala wa mmoja baada ya mwingine. Hatimaye, mtu aitwaye Nabonido akakalia kiti hicho baada ya maasi. Kwa kuwa alikuwa mwana wa kuhani wa kike wa cheo cha juu wa Sin, mungu-mwezi, yaonekana Nabonido hakuwa na uhusiano wa damu na nyumba ya kifalme ya Babiloni. Wataalamu fulani hudokeza kwamba alimwoa binti ya Nebukadreza ili kuhalalisha utawala wake mwenyewe, akamfanya mwana wao Belshaza awe mtawala mwenzake, na kumwacha atawale Babiloni kwa vipindi virefu. Kwa hiyo, Belshaza angekuwa mjukuu wa Nebukadreza. Kutokana na mambo yaliyompata babu yake, je, alikuwa amejifunza kwamba Yehova ndiye Mungu Mkuu Zaidi, awezaye kumdhilisha mfalme yeyote? Hata kidogo!—Danieli 4:37.
KARAMU YAPITA KIASI
3. Karamu ya Belshaza ilikuwaje?
3 Sura ya 5 ya Danieli yaanza na simulizi juu ya karamu. “Belshaza, mfalme, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya elfu hao.” (Danieli 5:1) Kama uwezavyo kuwazia, lazima jumba hilo lilikuwa kubwa vya kutosha watu hao wote, pamoja na wake wa ziada wa mfalme na masuria wake. Msomi mmoja aandika hivi: “Sherehe za Wababiloni zilikuwa zenye fahari sana, ingawa kwa kawaida zilimalizika kwa ulevi. Divai, iliyoagizwa kutoka nchi za nje, na starehe za kila aina ziliandikwa mezani. Manukato yalinukia kotekote katika jumba hilo; waimbaji na wapigaji wa ala za muziki walitumbuiza wageni waliokusanyika.” Akiwa mahali ambapo watu wote wangeweza kumwona, Belshaza alikunywa divai yake—akanywa kupindukia.
4. (a) Kwa nini huenda likaonekana kuwa jambo la ajabu kwamba Wababiloni walikuwa na sherehe usiku wa Oktoba 5/6, 539 K.W.K.? (b) Ni nini hasa kilichowapa Wababiloni uhakika wajapovamiwa na majeshi?
4 Ni ajabu kwamba Wababiloni walikuwa na shamrashamra za sherehe usiku huo—Oktoba 5/6, 539 K.W.K. Taifa lao lilikuwa vitani, na mambo yalikuwa yakiwaendea mrama. Muda mfupi tu uliotangulia, Nabonido alikuwa ameshindwa na majeshi yenye kuvamia ya Umedi na Uajemi naye alikuwa amekimbilia Borsippa, upande wa kusini-magharibi mwa Babiloni. Na sasa majeshi ya Koreshi yalikuwa yamepiga kambi nje tu ya Babiloni. Hata hivyo, yaonekana Belshaza na wakuu wake hawakuwa na wasiwasi. Kwani, jiji lao lilikuwa Babiloni lisiloweza kushindwa! Kuta zake kubwa zilionekana ndefu sana zikiwa kwenye mahandaki yenye kina yaliyojazwa maji na Mto mkuu wa Eufrati unapopitia katikati ya jiji hilo. Hakuna adui aliyekuwa amevamia ghafula Babiloni kwa zaidi ya miaka elfu moja. Kwa hiyo, kuna haja gani ya kuwa na wasiwasi? Huenda Belshaza alifikiri kwamba kelele ya sherehe zao ingeonyesha adui zao waliokuwa nje uhakika wao na kuwavunja moyo.
5, 6. Akiwa amelewa Belshaza alifanya nini, na kwa nini hilo lilikuwa tukano zito kwa Yehova?
5 Punde si punde, Belshaza akaanza kulewa kwa sababu ya kule kunywa kupindukia. Kama vile Mithali 20:1 isemavyo, “mvinyo hudhihaki.” Katika kisa hicho, mvinyo ulimfanya mfalme atende upumbavu mbaya sana. Aliagiza vyombo vitakatifu vilivyokuwa katika hekalu la Yehova viletwe kwenye karamu. Vyombo hivyo, vilivyotekwa nyara Yerusalemu liliposhindwa na Nebukadreza, vilipasa kutumiwa katika ibada safi peke yake. Hata makuhani Wayahudi waliokuwa wameidhinishwa kuvitumia katika hekalu la Yerusalemu walikuwa wameonywa wadumishe usafi.—Danieli 5:2; linganisha Isaya 52:11.
6 Hata hivyo, Belshaza bado alikuwa akifikiria tendo jingine lililokuwa lenye ufidhuli hata zaidi. “Mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake . . . wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe.” (Danieli 5:3, 4) Kwa hiyo, Belshaza alinuia kukweza miungu yake isiyo ya kweli juu kuliko Yehova! Yaonekana Wababiloni wengi walikuwa na mtazamo huo. Waliwadharau mateka wao Wayahudi, wakidhihaki ibada yao na kutowapa matumaini yoyote ya kurudi nyumbani kwao walikokupenda. (Zaburi 137:1-3; Isaya 14:16, 17) Huenda mtawala huyo aliyelewa chakari alihisi kwamba kuwadhili wahamishwa hao na kumtukana Mungu wao kungewavutia wanawake wake na mawaziri wake, na kufanya aonekane kuwa mwenye nguvu.a Lakini hata ikiwa Belshaza alisisimuka kwa kuhisi kwamba alikuwa na nguvu, hilo halikudumu.
MAANDISHI YA MKONO UKUTANI
7, 8. Karamu ya Belshaza ilikatizwaje, na hilo lilimwathirije mfalme?
7 “Saa iyo hiyo,” lasema simulizi lililopuliziwa, “vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa [“plasta,” NW] ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika.” (Danieli 5:5) Ni jambo la ajabu kama nini! Mkono ulitokea tu, ukielea hewani karibu na sehemu yenye mwangaza mzuri ukutani. Wazia kimya kilichotokea katika karamu hiyo huku wageni walioalikwa wakizubaa na kuuangalia. Mkono huo ukaanza kuandika ujumbe wa kifumbo kwenye ukuta uliopigwa plasta.b Jambo hilo lilikuwa lenye kuashiria mabaya sana, na lisiloweza kusahaulika, hivi kwamba hata leo watu hutumia usemi “maandishi ya mkono ukutani” kuashiria hatari inayokaribia.
8 Mfalme huyo mwenye kiburi aliyejaribu kujikweza mwenyewe na miungu yake juu kuliko Yehova alipatwa na nini? “Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.” (Danieli 5:6) Belshaza alikuwa amekusudia kuonekana kuwa mkuu na mwenye fahari mbele za raia zake. Badala yake, akahofu sana—uso wake ukambadilika, viungo vya viuno vyake vikatetema, akatetemeka sana mwili mzima hivi kwamba magoti yake yaligongana. Kwa hakika, maneno ya wimbo ambao Daudi alimwimbia Yehova yalikuwa kweli: “Macho yako ni juu ya wenye kiburi, uwadhili.”—2 Samweli 22:1, 28; linganisha Mithali 18:12.
9. (a) Kwa nini ogofyo la Belshaza halikuwa sawa na hofu ya kimungu? (b) Mfalme aliwaahidi nini watu wenye hekima wa Babiloni?
9 Yapaswa kueleweka kwamba hofu ya Belshaza haikuwa hofu ya kimungu, staha nyingi kwa Yehova, ambayo ni chanzo cha hekima yote. (Mithali 9:10) La, hiyo ilikuwa hofu ya mabaya, nayo haikumhekimisha hata kidogo mtawala huyo aliyekuwa akitetemeka.c Badala ya kuomba msamaha wa Mungu aliyekuwa ametoka tu kumtukana, aliwaita kwa sauti “wachawi, na Wakaldayo na wanajimu.” Hata alitangaza hivi: “Mtu awaye yote atakayesoma maandiko haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika ufalme.” (Danieli 5:7) Mtawala wa tatu katika ufalme angekuwa na uweza kwelikweli, akitanguliwa na wafalme wawili tu wenye kutawala, Nabonido na Belshaza mwenyewe. Cheo hicho kwa kawaida kingekuwa cha mwana mkubwa wa Belshaza. Na hiyo yaonyesha jinsi mfalme alivyotaka sana afafanuliwe ujumbe huo wa kimuujiza!
10. Watu wenye hekima walifanikiwa kiasi gani katika jitihada zao za kufasiri maandishi ya mkono ukutani?
10 Watu wenye hekima wakaingia katika jumba hilo kubwa. Walikuwa wengi kwa kuwa Babiloni lilikuwa jiji lililojaa dini zisizo za kweli na lenye mahekalu mengi. Bila shaka, kulikuwako watu wengi waliodai kuweza kubashiri mambo na kufumbua maandishi ya kifumbo. Lazima watu hao wenye hekima walisisimuka walipopata fursa hiyo. Sasa walikuwa na fursa ya kudhihirisha uwezo wao mbele ya waheshimiwa, mfalme apendezwe nao, na kupewa cheo kikubwa sana. Lakini walishindwa kama nini! “Hawakuweza kuyasoma yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake.”d—Danieli 5:8.
11. Huenda ni kwa nini watu wenye hekima wa Babiloni walishindwa kuyasoma maandishi hayo?
11 Hatuna uhakika ikiwa watu wenye hekima wa Babiloni walishindwa kufumbua maandishi hayo yenyewe, yaani herufi zenyewe. Ikiwa ndivyo ilivyokuwa, wafidhuli hao wangekuwa na fursa ya kutosha ya kubuni fasiri yoyote ile ya udanganyifu, labda hata wakimsifusifu mfalme isivyo kweli. Yawezekana pia kwamba herufi hizo zingeweza kusomeka vizuri. Hata hivyo, kwa kuwa lugha kama vile Kiaramu na Kiebrania ziliandikwa bila vokali kila neno lingaliweza kuwa na maana kadhaa. Ikiwa ndivyo ilivyokuwa, huenda watu hao wenye hekima walishindwa kuamua ni maneno gani yaliyokusudiwa. Hata ikiwa wangejua ni maneno gani, bado hawangeweza kufahamu maana ya maneno hayo ili waweze kuyafasiri. Vyovyote vile, kwa hakika: Watu wenye hekima wa Babiloni walishindwa vibaya!
12. Kushindwa kwa watu wenye hekima kulithibitisha nini?
12 Kwa hiyo, ikathibitika kuwa watu wenye hekima walikuwa walaghai, na dini yao iliyostahiwa sana kuwa udanganyifu. Walivunja moyo kama nini! Belshaza alipoona kwamba aliwatumaini watu hao wa dini bure tu, akaogofywa hata zaidi, uso wake ukambadilika hata zaidi, na hata wakuu wake “wakaona fadhaa.”e—Danieli 5:9.
MTU MWENYE UFAHAMU WENYE KINA AITWA
13. (a) Kwa nini malkia alipendekeza Danieli aitwe? (b) Danieli alikuwa akiishi maisha ya aina gani?
13 Wakati huo wa uhitaji mkubwa, malkia mwenyewe—pengine malkia aliyekuwa mama ya mfalme—akaingia kwenye jumba la sherehe. Alikuwa amesikia zile rabsharabsha kwenye karamu, naye alijua mtu ambaye angeweza kufasiri maandishi ya mkono ukutani. Makumi ya miaka awali, Nebukadreza, babake, alikuwa amemweka Danieli asimamie watu wake wote wenye hekima. Malkia alimkumbuka kuwa mtu mwenye “nuru na ufahamu na hekima.” Kwa kuwa yaonekana Belshaza hakumjua Danieli, huenda nabii huyo alikuwa amepoteza cheo chake kikubwa katika serikali baada ya Nebukadreza kufa. Lakini umaarufu haukuwa wa maana kwa Danieli. Pengine wakati huo alikuwa na umri wa miaka 90 na kitu, bado akimtumikia Yehova kwa uaminifu. Licha ya kuwa uhamishoni Babiloni kwa miaka 80 hivi, bado aliitwa jina lake la Kiebrania. Hata malkia alimwita Danieli, hakutumia jina la Kibabiloni alilopewa. Kwa kweli, alimhimiza mfalme hivi: “Na aitwe Danieli, naye ataionyesha tafsiri.”—Danieli 1:7; 5:10-12.
14. Danieli alikuwa katika mashaka gani alipoona maandishi ya mkono ukutani?
14 Danieli aliitwa, akaja mbele za Belshaza. Lilikuwa jambo lenye kuaibisha kumwomba hisani Myahudi ambaye mfalme alikuwa ametoka tu kumtukana Mungu wake. Hata hivyo, Belshaza alijaribu kumsifusifu Danieli, na kumwahidi thawabu ileile—kuwa mtawala wa tatu katika ufalme—ikiwa angeweza kusoma na kufafanua yale maneno ya kifumbo. (Danieli 5:13-16) Danieli akainua macho yake na kuyaona maandishi ya mkono ukutani, nayo roho takatifu ikamwezesha kufahamu maana yake. Ulikuwa ujumbe wa maangamizi kutoka kwa Yehova Mungu! Danieli angetangazaje hukumu kali dhidi ya mfalme asiyefaa kitu machoni pake mwenyewe, na mbele ya wake zake na wakuu wake? Wazia hali ya mashaka aliyokuwamo Danieli! Je, alikuwa ameyumbishwa na maneno yenye kusifusifu ya mfalme na ahadi yake ya utajiri na umaarufu? Je, nabii huyo angepunguza uzito wa hukumu ya Yehova?
15, 16. Ni somo gani la maana katika historia ambalo Belshaza hakujifunza, na ni kwa kadiri gani watu hawajajifunza hilo leo?
15 Danieli alinena kwa ujasiri, akisema: “Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake.” (Danieli 5:17) Kisha, Danieli akakiri ukuu wa Nebukadreza, mfalme aliyekuwa na nguvu sana hivi kwamba angeweza kuua, kushambulia, kukweza, au kudhili yeyote aliyetaka. Hata hivyo, Danieli alimkumbusha Belshaza kwamba Yehova, “Aliye juu,” alikuwa amemkweza Nebukadreza. Yehova ndiye aliyekuwa amemdhili mfalme huyo mwenye uweza alipokuwa na kiburi. Naam, Nebukadreza alilazimishwa kujifunza kwamba “Aliye juu ndiye anayetawala katika ufalme wa wanadamu, na ya kuwa humweka juu yake yeye amtakaye, awaye yote.”—Danieli 5:18-21.
16 Belshaza “[a]lijua hayo yote.” Hata hivyo, hakujifunza kutokana na historia. Hata alikuwa amezidi dhambi ya Nebukadreza ya kiburi chenye kosa, akatenda tendo la ufidhuli wa moja kwa moja dhidi ya Yehova. Danieli alifunua dhambi ya mfalme. Isitoshe, akiwa mbele ya wahudhuriaji wapagani, alimwambia Belshaza kwa ujasiri kwamba miungu wasio wa kweli walikuwa ‘hawaoni, wala kusikia, wala kujua neno lo lote.’ Nabii wa Mungu mwenye ujasiri aliongezea kusema kwamba tofauti na miungu hiyo isiyofaa kitu, Yehova ndiye Mungu “ambaye pumzi yako i mkononi mwake.” Hadi leo, watu hutengeneza miungu kutokana na vitu visivyo na uhai, wakiabudu fedha, kazi, sifa, hata anasa. Lakini hakuna kimojawapo cha vitu hivyo kiwezacho kutokeza uhai. Yehova peke yake ndiye chanzo cha uhai, ambaye twamtegemea kwa kila pumzi tunayovuta.—Danieli 5:22, 23; Matendo 17:24, 25.
KITENDAWILI CHATEGULIWA!
17, 18. Ni maneno gani manne yaliyoandikwa ukutani, nayo yalimaanisha nini kihalisi?
17 Nabii huyo mzee akafanya jambo lililowashinda watu wote wenye hekima wa Babiloni. Alisoma na kufasiri maandishi yaliyokuwa yameandikwa ukutani. Maneno hayo yalikuwa: “MENE, MENE, TEKELI, PARSINI.” (Danieli 5:24, 25, BHN) Yamaanisha nini?
18 Kihalisi, maneno hayo yamaanisha “mina, mina, shekeli, na nusu shekeli.” Kila neno lilikuwa kipimo cha uzito wa fedha, likiorodheshwa kuanzia chenye thamani zaidi hadi chenye thamani ya chini. Ajabu kama nini! Hata ikiwa watu wenye hekima wa Babiloni wangeweza kutambua herufi hizo, si ajabu kwamba hawakuweza kuzifasiri.
19. Neno “MENE” lilifasiriwa kuwa nini?
19 Akiongozwa na roho takatifu ya Mungu, Danieli alieleza hivi: “Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha.” (Danieli 5:26) Konsonanti za neno la kwanza zingeweza kufanyiza neno “mina” na pia namna ya neno la Kiaramu linalomaanisha “-hesabu,” au “hesabiwa,” ikitegemea vokali zinazotumiwa na msomaji. Danieli alijua vizuri kwamba uhamisho wa Wayahudi ulikuwa ukikaribia. Kati ya ile miaka 70 ya uhamisho iliyokuwa imetabiriwa, miaka 68 tayari ilikuwa imepita. (Yeremia 29:10) Mweka-Wakati Mkuu, Yehova, alikuwa amehesabu siku za utawala wa Babiloni ikiwa serikali ya ulimwengu, nao mwisho ulikuwa karibu kuliko vile ambavyo yeyote aliyekuwa katika karamu ya Belshaza alifikiri. Kwa hakika, wakati ulikuwa umeisha—si wakati wa Belshaza tu bali pia wa baba yake, Nabonido. Huenda ndiyo sababu neno “MENE” liliandikwa mara mbili—kutangaza mwisho wa tawala hizo mbili.
20. Neno “TEKELI” lilifafanuliwa kuwa nini, nalo lilimhusuje Belshaza?
20 Nalo neno “TEKELI,” liliandikwa mara moja tu, tena kwa umoja. Hilo laweza kuonyesha kwamba lilielekezwa hasa kwa Belshaza. Na kufanya hivyo kungefaa, kwa kuwa yeye mwenyewe alikuwa ameonyesha ukosefu mkubwa wa staha kwa Yehova. Neno lenyewe lamaanisha “shekeli,” lakini konsonanti zaweza kufanyiza neno “-pimwa.” Kwa hiyo, Danieli alimwambia Belshaza hivi: “TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka.” (Danieli 5:27) Kwa maoni ya Yehova, mataifa yote si kitu kama vile mavumbi membamba katika mizani. (Isaya 40:15) Hawana nguvu za kuzuia makusudi yake. Basi, mfalme mmoja mwenye kiburi ni nini mbele zake? Belshaza alijaribu kujikweza mwenyewe juu kuliko Mwenye Enzi kuu ya ulimwengu wote. Mtu huyo duni tu alikuwa amethubutu kumtukana Yehova na kudhihaki ibada safi lakini ‘akaonekana kuwa amepunguka.’ Naam, Belshaza alistahili kikamili hukumu iliyokuwa ikikaribia haraka!
21. Neno “PARSINI” lilikuwa na maana gani tatu, nalo neno hilo lilionyesha nini juu ya wakati ujao wa Babiloni likiwa serikali ya ulimwengu?
21 Neno la mwisho ukutani lilikuwa “PARSINI.” Huenda Danieli alilisoma katika hali ya umoja, “PERESI,” kwa sababu alikuwa akiongea na mfalme mmoja ilhali yule mwingine hakuwepo. Neno hilo lilitamatisha kitendawili kikuu cha Yehova kwa kutumia neno lenye maana tatu. Kihalisi, “parsini” lamaanisha “nusu shekeli.” Lakini herufi hizo zaweza kuwa na maana nyingine mbili—“migawanyiko” na “Waajemi.” Kwa hiyo, Danieli akatabiri: “PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.”—Danieli 5:28.
22. Belshaza alitendaje kitendawili kilipoteguliwa, na huenda alikuwa na matumaini gani?
22 Hivyo, kitendawili kikateguliwa. Babiloni lenye nguvu lilikaribia kuangushwa na majeshi ya Umedi na Uajemi. Ingawa alihuzunishwa na tangazo hilo la maangamizi, Belshaza alitimiza ahadi yake. Aliwaagiza watumishi wake wamvike Danieli mavazi ya rangi ya zambarau, wamvishe mkufu wa dhahabu shingoni mwake, na kumtangaza kuwa mtawala wa tatu katika ufalme. (Danieli 5:29) Danieli hakukataa kutendewa hivyo, akitambua kwamba walionyesha heshima iliyomstahili Yehova. Bila shaka, huenda Belshaza alitumaini kupunguza hukumu ya Yehova kwa kumheshimu nabii Wake. Ikiwa ndivyo, alikuwa amechelewa sana.
KUANGUKA KWA BABILONI
23. Ni unabii gani wa kale uliokuwa ukitimizwa huku karamu ya Belshaza ikiendelea?
23 Hata Belshaza na wafanyakazi wa makao yake walipokuwa wakinywa hali wakiitakia heri miungu yao na kumdhihaki Yehova, mambo makubwa yalikuwa yakiendelea gizani nje ya makao ya kifalme. Unabii uliokuwa umetolewa kupitia nabii Isaya karibu karne mbili awali, ulikuwa ukitimia. Yehova alikuwa ametabiri hivi kuhusu Babiloni: “Majonzi yote anayoyasababisha nimeyakomesha.” Naam, dhuluma zote za jiji hilo ovu dhidi ya watu wateule wa Mungu zingeisha. Vipi? Unabii uo huo ulisema hivi: “Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi.” Elamu lilipata kuwa sehemu ya Uajemi baada ya siku za nabii Isaya. Wakati wa karamu ya Belshaza, ambayo ilikuwa imetabiriwa pia katika unabii uo huo wa Isaya, Uajemi na Umedi yalikuwa yameunganisha majeshi yao ili ‘kupanda’ na ‘kuhusuru’ Babiloni.—Isaya 21:1, 2, 5, 6, linganisha NW.
24. Ni mambo gani kuhusu kuanguka kwa Babiloni ambayo unabii wa Isaya ulikuwa umetabiri?
24 Kwa hakika, jina lenyewe la kiongozi wa majeshi hayo lilikuwa limetabiriwa, kama vile mbinu zake kuu za kivita zilivyokuwa zimetabiriwa. Miaka 200 mapema, Isaya alikuwa ametabiri kwamba Yehova angemtia mafuta mtu aitwaye Koreshi dhidi ya Babiloni. Wakati wa mashambulizi yake makali, vizuizi vyote vingeondolewa mbele yake. Maji ya Babiloni ‘yangekauka,’ na milango yake mikubwa ingeachwa wazi. (Isaya 44:27–45:3) Ikawa hivyo. Majeshi ya Koreshi yaligeuza mkondo wa Mto Eufrati, yakipunguza kina cha maji hivi kwamba yangeweza kupita kwenye sakafu ya mto. Milango ya ukuta wa Babiloni ilikuwa imeachwa wazi na walinzi wazembe. Kama vile wanahistoria hukubali, jiji hilo lilivamiwa wakazi wake wakiwa na sherehe yenye kelele za ulevi. Babiloni lilishindwa kwa urahisi sana. (Yeremia 51:30) Hata hivyo, kulikuwa na angalau kifo kimoja chenye kutokeza. Danieli aliripoti hivi: “Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa. Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili.”—Danieli 5:30, 31.
KUJIFUNZA KUTOKANA NA MAANDISHI YA MKONO UKUTANI
25. (a) Kwa nini Babiloni la kale lafananisha kwa kufaa mfumo wa dunia nzima wa dini isiyo ya kweli? (b) Watumishi wa Mungu wa leo walikuwaje mateka katika Babiloni?
25 Simulizi lililopuliziwa katika Danieli sura ya 5 lina maana sana kwetu. Likiwa kitovu cha mazoea ya dini isiyo ya kweli, Babiloni la kale ni mfano unaofaa wa milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli. Uwongo huo wa ulimwengu wote unaofananishwa na kahaba mwenye kiu ya damu kwenye Ufunuo, waitwa “Babiloni Mkubwa.” (Ufunuo 17:5) Bila kutii maonyo yote dhidi ya mafundisho na mazoea yake yenye kumvunjia Mungu heshima, amewanyanyasa wale wanaohubiri kweli ya Neno la Mungu. Kama vile wakazi wa Yerusalemu na Yuda za kale, mabaki waaminifu wa Wakristo watiwa-mafuta walihamishwa na kupelekwa katika “Babiloni Mkubwa” wakati ambapo mnyanyaso uliochochewa na makasisi ulikaribia sana kufunga kazi ya kuhubiri Ufalme mwaka wa 1918.
26. (a) “Babiloni Mkubwa” aliangukaje mwaka wa 1919? (b) Ni onyo gani ambalo sisi wenyewe twapaswa kutii na kuwajulisha wengine?
26 Hata hivyo, “Babiloni Mkubwa” alianguka ghafula! Ah, lilikuwa anguko la kimya—kama vile Babiloni la kale lilivyoanguka kimyakimya, mwaka wa 539 K.W.K. Hata hivyo, anguko hilo lilikuwa lenye kuharibu. Lilitukia mwaka wa 1919 W.K. wakati ambapo watu wa Yehova waliachiliwa kutoka katika utekwa wa Kibabiloni na kubarikiwa kwa kupata kibali cha Mungu. Hilo lilikomesha nguvu za “Babiloni Mkubwa” dhidi ya watu wa Mungu na kuashiria mwanzo wa kufunuliwa kwake hadharani kuwa mlaghai asiyetegemeka. Anguko hilo haliwezi kubadilika, nao uharibifu wake wa mwisho wakaribia. Kwa hiyo, watumishi wa Yehova wamekuwa wakitoa onyo hili: “Tokeni kwake, watu wangu, ikiwa hamtaki kushiriki pamoja naye dhambi zake.” (Ufunuo 18:4) Je, umetii onyo hilo? Je, wawaonya wengine?f
27, 28. (a) Sikuzote Danieli alikumbuka kweli gani muhimu? (b) Tuna uthibitisho gani leo wa kwamba karibuni Yehova atachukua hatua dhidi ya ulimwengu mwovu wa leo?
27 Kwa hiyo, yale maandishi ya mkono yako ukutani leo—lakini si kwa ajili ya “Babiloni Mkubwa” peke yake. Kumbuka kweli ya maana sana inayokaziwa katika kitabu cha Danieli: Yehova ndiye Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu Wote. Yeye, yeye peke yake, ndiye mwenye haki ya kumweka mtawala juu ya wanadamu. (Danieli 4:17, 25; 5:21) Lolote linalozuia makusudi ya Yehova litaondolewa. Wakati wa Yehova kuchukua hatua utafika hakika. (Habakuki 2:3) Kwa habari ya Danieli, wakati huo ulifika hatimaye alipokuwa akikaribia miaka 100. Kisha akamwona Yehova akiondoa serikali ya ulimwengu—serikali iliyowaonea watu wa Mungu tangu Danieli alipokuwa mvulana.
28 Kuna uthibitisho usioweza kupingwa wa kwamba Yehova Mungu alitawaza Mtawala wa wanadamu katika kiti cha kimbingu. Uhakika wa kwamba ulimwengu umempuuza Mfalme huyo na kupinga utawala wake wathibitisha kabisa kwamba hivi karibuni Yehova atafutilia mbali wapinzani wote wa utawala wa Ufalme. (Zaburi 2:1-11; 2 Petro 3:3-7) Je, unatenda kulingana na uharaka wa nyakati zetu na kuwa na uhakika katika Ufalme wa Mungu? Ikiwa ndivyo, kwa kweli umejifunza kutokana na maandishi ya mkono ukutani!
[Maelezo ya Chini]
a Katika maandishi ya kale, Mfalme Koreshi alisema hivi juu ya Belshaza: “Mtu mnyonge amewekwa kuwa [mtawala] wa nchi yake.”
b Hata jambo hilo dogo katika simulizi la Danieli limethibitika kuwa sahihi. Waakiolojia wamegundua kwamba kuta za makao ya kifalme katika Babiloni la kale zilijengwa kwa matofali na kupigwa plasta.
c Huenda ushirikina wa Kibabiloni ulifanya muujiza huo uwe wenye kuogofya hata zaidi. Kitabu Babylonian Life and History chataarifu hivi: “Zaidi ya ile miungu ambayo Wababiloni waliabudu, twaona kwamba waliamini sana roho hivi kwamba vichapo vyao vingi vya kidini ni vya sala na tabano dhidi [ya roho].”
d Jarida Biblical Archaeology Review lataarifu hivi: “Wataalamu Wababiloni waliandika maelfu ya ishara zenye kuashiria mabaya . . . Belshaza alipotaka kujua maana ya maandishi yaliyokuwa ukutani, yawezekana kwamba wenye hekima wa Babiloni walichunguza vitabu vya ishara hizo. Lakini havikuwasaidia.”
e Watungaji wa kamusi wataarifu kwamba neno lililotumiwa hapa “-ona fadhaa” lamaanisha msukosuko mkubwa, kana kwamba watu waliokuwa wamekusanyika walivurugika.
f Ona ukurasa wa 205-271 katika kitabu Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
UMEFAHAMU NINI?
• Karamu ya Belshaza ilikatizwaje usiku wa Oktoba 5/6, 539 K.W.K.?
• Maandishi ya mkono ukutani yalimaanisha nini?
• Ni unabii gani juu ya kuanguka kwa Babiloni uliokuwa ukitimizwa huku karamu ya Belshaza ikiendelea?
• Simulizi la maandishi ya mkono ukutani lina maana gani kwetu leo?
[Picha katika ukurasa wa 98]
[Picha katika ukurasa wa 103]