“Fulizeni Kunitarajia”
“Basi ningojeni [“fulizeni kunitarajia,” “NW”], asema BWANA.”—SEFANIA 3:8.
1. Ni onyo gani lililotolewa na nabii Sefania, na hilo lina upendezi gani kwa watu wanaoishi leo?
“SIKU ya BWANA iliyo kuu i karibu.” Kilio hicho chenye onyo kilitolewa na nabii Sefania katikati ya karne ya saba K.W.K. (Sefania 1:14) Katika miaka 40 au 50 iliyofuata, huo unabii ulitimizwa wakati siku ya kutekeleza hukumu za Yehova ilipowadia Yerusalemu na pia mataifa yale yaliyokaidi enzi kuu ya Yehova kwa kuwatendea vibaya watu wake. Kwa nini jambo hili lipendeze watu wanaoishi mwishoni mwa karne ya 20? Tunaishi wakati ‘siku iliyo kuu’ ya mwisho ya Yehova inapokaribia upesi. Kama ilivyokuwa na wakati wa Sefania, “hasira kali” ya Yehova i karibu kutokea dhidi ya kifanani cha kisasa cha Yerusalemu—Jumuiya ya Wakristo—na dhidi ya mataifa yote yanayowatendea vibaya watu wa Yehova na kukaidi enzi yake kuu ya ulimwengu wote mzima.—Sefania 1:4; 2:4, 8, 12, 13; 3:8, NW; 2 Petro 3:12, 13.
Sefania—Shahidi Mwenye Moyo Mkuu
2, 3. (a) Twajua nini kuhusu Sefania, na ni nini kinachoonyesha kwamba alikuwa shahidi wa Yehova mwenye moyo mkuu? (b) Ni mambo gani yanayotusaidia kujua wakati na mahali ambapo Sefania alitoa unabii?
2 Ni mambo machache tu yanayojulikana kuhusu nabii Sefania, ambaye jina lake (Kiebrania, Tsephan·yahʹ) lamaanisha “Yehova Amesitiri (Amehazini).” Hata hivyo, tofauti na manabii wengine Sefania alitaja nasaba yake hadi kizazi cha nne, kufikia “Hezekia.” (Sefania 1:1; linganisha Isaya 1:1; Yeremia 1:1; Ezekieli 1:3.) Hili ni jambo lisilo la kawaida sana hivi kwamba wafafanuzi wengi husema kwamba babu ya babu yake alikuwa Mfalme Hezekia aliyekuwa mwaminifu. Ikiwa ni kweli, basi Sefania alikuwa wa uzao wa kifalme, na hilo lingeongezea uzito shutuma yake kwa wakuu wa Yuda na kuonyesha kwamba alikuwa shahidi mwenye moyo mkuu na nabii wa Yehova. Ujuzi wake mkubwa wa mandhari ya Yerusalemu na yale yaliyokuwa yakitendeka katika baraza la kifalme wadokeza kwamba huenda ikawa alitangaza hukumu za Yehova katika jiji kuu lenyewe.—Ona Sefania 1:8-11, New World Translation of the Holy Scriptures—With References, vielezi-chini.
3 Jambo kuu ni kwamba ingawa Sefania alitangaza hukumu za kimungu dhidi ya “wakuu” wa kijamii wa Yuda (watu wenye vyeo vikubwa, au wakuu wa makabila) na “wana wa mfalme,” yeye hakutaja kamwe mfalme mwenyewe katika uchambuzi wake.a (Sefania 1:8; 3:3) Hilo ladokeza kwamba Mfalme Yosia mchanga tayari alikuwa ameonyesha mwelekeo mzuri kwa ajili ya ibada safi, ingawa, kwa kutazama hali iliyoshutumiwa na Sefania, kwa wazi hakuwa ameanza kufanya marekebisho yake ya kidini. Hayo yote yadokeza kwamba Sefania alitoa unabii katika Yuda katika miaka ya mapema ya Yosia, aliyetawala kuanzia 659 hadi 629 K.W.K. Unabii uliotolewa kwa bidii na Sefania bila shaka ulimsaidia Yosia mchanga kutambua kwamba ibada ya sanamu, jeuri, na ufisadi ulienea katika Yuda wakati huo na kutia nguvu kampeni yake ya baadaye dhidi ya ibada ya sanamu.—2 Mambo ya Nyakati 34:1-3.
Sababu za Hasira Kali ya Yehova
4. Ni katika maneno gani Yehova alitaja hasira yake dhidi ya Yuda na Yerusalemu?
4 Yehova alikuwa na sababu nzuri za kuhisi hasira dhidi ya viongozi na wakazi wa Yuda na jiji lalo kuu la Yerusalemu. Kupitia nabii wake Sefania, yeye alisema: “Nitaunyosha mkono wangu juu ya Yuda, na juu ya watu wote wakaao Yerusalemu; nami nitayakatilia mbali mabaki ya Baali, yasionekane mahali hapa, na hilo jina la Wakemari pamoja na makuhani; na wale walisujudiao jeshi la mbinguni juu ya dari za nyumba; na hao waabuduo, waapao kwa BWANA na kuapa pia kwa Malkamu.”—Sefania 1:4, 5.
5, 6. (a) Kulikuwa na hali gani ya kidini katika Yuda wakati wa Sefania? (b) Viongozi wa kijamii wa Yuda na wale waliotumikia chini yao walikuwa na hali gani?
5 Yuda lilichafuliwa na matendo yenye kupotoka ya ibada ya kiuzazi ya Baali, unajimu wa kishetani, na ibada ya mungu wa kipagani Malkamu. Ikiwa Malkamu ndiye Moleki, kama vile wengine wanavyodokeza, basi ibada bandia ya Yuda ilitia ndani tendo lenye kuchukiza mno la kuwadhabihu watoto. Mazoea hayo ya kidini yalimchukiza sana Yehova. (1 Wafalme 11:5, 7; 14:23, 24; 2 Wafalme 17:16, 17) Walimfanya akasirike hata zaidi kwa kuwa hawa waabudu sanamu bado waliapa kwa jina la Yehova. Hangevumilia tena ukosefu huo wa usafi wa kidini naye angewakatilia mbali wote makuhani wapagani na makuhani waasi-imani.
6 Isitoshe, viongozi wa kijamii wa Yuda walikuwa wafisadi. Wakuu walo walikuwa kama “simba wangurumao,” na waamuzi wao walilinganishwa na “mbwa-mwitu” wenye pupa. (Sefania 3:3) Wale waliotumikia chini yao walishutumiwa ‘kujaza nyumba ya bwana wao udhalimu na udanganyifu.’ (Sefania 1:9) Ufuatiaji wa vitu vya kimwili ulienea. Wengi walikuwa wakitumia fursa hiyo kurundika mali.—Sefania 1:13.
Shaka Kuhusu Siku ya Yehova
7. Sefania alitoa unabii muda gani kabla ya “siku ya BWANA iliyo kuu,” na Wayahudi wengi walikuwa na hali gani ya kiroho?
7 Kama tulivyokwisha kuona, hali mbaya sana ya kidini iliyoenea katika siku ya Sefania yaonyesha kwamba alifanya kazi yake akiwa shahidi na nabii kabla ya Mfalme Yosia kuanza kampeni yake dhidi ya ibada ya sanamu, karibu 648 K.W.K. (2 Mambo ya Nyakati 34:4, 5) Basi, yaelekea kwamba Sefania alitoa unabii angalau miaka 40 kabla ya “siku ya BWANA iliyo kuu” kuja juu ya ufalme wa Yuda. Katika kipindi hicho, Wayahudi wengi walikuwa na shaka ‘wakarudi nyuma’ wakiacha kumtumikia Yehova na kuwa wasiojali. Sefania asema juu ya wale “wasiomtafuta BWANA, wala kumwulizia.” (Sefania 1:6) Kwa wazi, watu mmoja-mmoja katika Yuda walikuwa na ubaridi, wasijihusishe na Mungu.
8, 9. (a) Kwa nini Yehova angekagua “watu walioganda juu ya sira zao”? (b) Ni katika njia zipi Yehova angewapa uangalifu wakazi wa Yuda na viongozi wao wa kijamii na kidini?
8 Yehova alijulisha kusudi lake la kukagua wale wanaodai kuwa watu wake. Miongoni mwa wale waliodai kuwa waabudu wake, angewatafuta wale waliokuwa na shaka katika mioyo yao juu ya uwezo wake au kusudi lake la kuingilia mambo ya wanadamu. Yeye alisema hivi: “Kisha itakuwa wakati ule, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; nami nitawaadhibu watu walioganda juu ya sira zao; wasemao katika mioyo yao, BWANA hatatenda mema, wala hatatenda mabaya.” (Sefania 1:12) Usemi “watu walioganda juu ya sira zao” (kwa kurejezea kutengeneza divai) warejezea wale ambao wametulia, kama sira chini ya pipa la divai, wasiotaka kusumbuliwa na tangazo lolote kwamba karibuni Mungu ataingilia mambo ya wanadamu.
9 Yehova angeelekeza fikira kwa wakazi wa Yuda na Yerusalemu na kwa makuhani wao waliokuwa wamechanganya ibada yake na upagani. Ikiwa walihisi salama, kana kwamba walifichwa na giza la usiku ndani ya kuta za Yerusalemu, yeye angewafichua kwa taa nyangavu ambazo zingepenya giza la kiroho ambamo walikuwa wamekimbilia. Angewaondoa kwenye ubaridi wao wa kidini, kwanza kwa jumbe zenye nguvu sana za hukumu, kisha kwa kutekeleza hukumu hizo.
“Siku ya BWANA Iliyo Kuu I Karibu”
10. Sefania alifafanuaje “siku ya BWANA iliyo kuu”?
10 Yehova alimpulizia Sefania kupiga mbiu: ‘Siku ya BWANA iliyo kuu i karibu; i karibu, nayo inafanya haraka sana; naam, sauti ya siku ya BWANA ni chungu.’ (Sefania 1:14) Kwa kweli siku zenye uchungu mno zilikuwa mbele ya kila mtu—makuhani, wakuu, na watu—aliyekataa kutii onyo na kurudia ibada safi. Ukifafanua siku hiyo ya kutekeleza hukumu, unabii huo waendelea kusema: “Siku ile ni siku ya ghadhabu, siku ya fadhaa na dhiki, siku ya uharibifu na ukiwa, siku ya giza na utusitusi, siku ya mawingu na giza kuu, siku ya tarumbeta na ya kamsa, juu ya miji yenye maboma, juu ya buruji zilizo ndefu sana.”—Sefania 1:15, 16.
11, 12. (a) Ni ujumbe gani wenye hukumu uliotangazwa dhidi ya Yerusalemu? (b) Je, ufanisi wa kimwili ungeokoa Wayahudi?
11 Katika miongo michache mifupi, majeshi ya Babiloni yangevamia Yuda. Yerusalemu halingeponyoka. Maeneo yalo ya makazi na ya biashara yangeharibiwa kabisa. “Katika siku ile, asema BWANA kutakuwako sauti ya kilio kutoka lango la samaki, na mlio mkuu katika mtaa wa pili, na mshindo mkuu kutoka milimani. Haya! lieni, ninyi mkaao katika Makteshi [eneo fulani la Yerusalemu], maana wafanya biashara wote wameangamia; hao wote waliokuwa na mizigo ya fedha wamekatiliwa mbali.”—Sefania 1:10, 11.
12 Wakikataa kuamini kwamba siku ya Yehova ilikuwa karibu, Wayahudi wengi walijihusisha sana na biashara zenye faida nyingi. Lakini kupitia Sefania, nabii wake mwaminifu, Yehova alitabiri kwamba utajiri wao “utakuwa mateka, na nyumba zao zitakuwa ukiwa.” Wao hawangekunywa divai waliyotengeneza, wala “fedha yao wala dhahabu yao havi[nge]weza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya BWANA.”—Sefania 1:13, 18.
Mataifa Mengine Yahukumiwa
13. Sefania alitangaza ujumbe gani wenye hukumu dhidi ya Moabu, Amoni, na Ashuru?
13 Kupitia nabii wake Sefania, Yehova alionyesha hasira yake pia dhidi ya mataifa yaliyokuwa yamewatendea watu wake vibaya. Alitangaza hivi: “Mimi nimeyasikia matukano ya Moabu, na dhihaka za wana wa Amoni, ambazo kwa hizo wamewatukana watu wangu, na kujitukuza juu ya mpaka wao. Basi kama niishivyo, asema BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, Hakika Moabu atakuwa kama Sodoma, na wana wa Amoni kama Gomora, yaani, milki ya upupu, na mashimo ya chumvi, ukiwa wa daima. . . . Naye atanyosha mkono wake juu ya upande wa kaskazini, na kuiangamiza Ashuru; naye ataufanya Ninawi kuwa ukiwa, kuwa mahali pakavu kama jangwa.”—Sefania 2:8, 9, 13.
14. Kuna uthibitisho gani kwamba mataifa ya kigeni ‘yalijitukuza’ juu ya Waisraeli na Mungu wao, Yehova?
14 Moabu na Amoni walikuwa maadui wa Israeli wa tangu zamani. (Linganisha Waamuzi 3:12-14.) Jiwe la Moabu, lililo katika Louvre Museum katika Paris, lina maandiko yenye taarifa ya kujisifu iliyotolewa na Mfalme Mesha wa Moabu. Yeye asimulia kwa majivuno jinsi alivyotwaa majiji kadhaa ya Israeli kwa msaada wa mungu wake Kemoshi. (2 Wafalme 1:1) Yeremia, aliyeishi wakati wa Sefania, alisema juu ya Waamoni kuwa wanakalia eneo la Israeli la Gadi katika jina la mungu wao Malkamu. (Yeremia 49:1) Kuhusu Ashuru, Mfalme Shalmanesa 5 alizingira na kuteka Samaria karibu karne moja kabla ya siku ya Sefania. (2 Wafalme 17:1-6) Baadaye kidogo, Mfalme Senakeribu alishambulia Yuda, akateka majiji mengi yenye ngome, na hata kutisha Yerusalemu. (Isaya 36:1, 2) Msemaji wa mfalme wa Ashuru alijitukuza juu ya Yehova alipokuwa akidai Yerusalemu lisalimu amri.—Isaya 36:4-20.
15. Yehova angeaibishaje miungu ya mataifa yaliyojitukuza juu ya watu wake?
15 Zaburi 83 hutaja mataifa kadhaa, kutia ndani Moabu, Amoni, na Ashuru, waliojitukuza juu ya Israeli, na kusema hivi kwa kujigamba: “Njoni, tuwakatilie mbali wasiwe taifa, na jina la Israeli halitakumbukwa tena.” (Zaburi 83:4) Nabii Sefania alitangaza kwa moyo mkuu kwamba mataifa hayo yote yenye kiburi na miungu yayo yangeaibishwa na Yehova wa majeshi. “Mambo hayo yatawapata kwa sababu ya kiburi chao, kwa kuwa wamewatukana watu wa BWANA wa majeshi, na kujitukuza juu yao. BWANA atakuwa mwenye kuwatisha sana; kwa maana atawafisha kwa njaa miungu yote ya dunia; na watu watamsujudia yeye, kila mtu toka mahali pake; naam, nchi zote za mataifa.”—Sefania 2:10, 11.
“Fulizeni Kunitarajia”
16. (a) Ni kwa akina nani kuja kwa siku ya Yehova kulikuwa chanzo cha shangwe, na kwa nini? (b) Ni amri gani yenye kuamsha iliyotolewa kwa mabaki waaminifu?
16 Huku ulegevu wa kiroho, shaka, ibada ya sanamu, ufisadi, na ufuatiaji wa vitu vya kimwili ukienea miongoni mwa viongozi na wakazi wengi wa Yuda na Yerusalemu, yaonekana kwamba baadhi ya Wayahudi waaminifu walisikiliza unabii mbalimbali wenye onyo aliotoa Sefania. Wao walisikitishwa na matendo ya kuchukiza ya wakuu, waamuzi, na makuhani wa Yuda. Matangazo ya Sefania yalikuwa chanzo cha faraja kwa hawa waaminifu-washikamanifu. Badala ya kuwa kisababishi cha huzuni, kuja kwa siku ya Yehova kulikuwa chanzo cha shangwe kwao, kwa sababu kungekomesha matendo hayo yenye kuchukiza. Hawa mabaki waaminifu walitii amri ya Yehova ya kuwaamsha: “Basi ningojeni [“fulizeni kunitarajia,” NW] asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu.”—Sefania 3:8.
17. Ni lini na ni jinsi gani jumbe zenye hukumu za Sefania zenye hukumu zilianza kutimizwa dhidi ya mataifa?
17 Wale waliotii onyo hilo hawakushangaa. Wengi waliishi wakaona utimizo wa unabii wa Sefania. Katika 632 K.W.K., Ninawi lilitekwa na kuharibiwa na muungano wa Wababiloni, Wamedi, na vikundi kutoka kaskazini, labda Waskaithia. Mwanahistoria Will Durant asimulia: “Jeshi la Wababiloni chini ya Nabopolasari liliungana na jeshi la Wamedi chini ya Siaksaresi na vikundi vya Waskaithia kutoka Kaukasi, na kwa urahisi na wepesi wenye kushangaza waliteka ngome za kaskazini. . . . Kwa pigo moja Ashuru ilipotea katika historia.” Hivyo ndivyo alivyotabiri Sefania.—Sefania 2:13-15.
18. (a) Hukumu ya kimungu ilitekelezwaje juu ya Yerusalemu, na kwa nini? (b) Unabii wa Sefania kuhusu Moabu na Amoni ulitimizwaje?
18 Wayahudi wengi waliofuliza kumtarajia Yehova pia waliishi wakaona hukumu zake zikitekelezwa juu ya Yuda na Yerusalemu. Kuhusu Yerusalemu, Sefania alikuwa ametabiri: “Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini BWANA; hakumkaribia Mungu wake.” (Sefania 3:1, 2) Kwa sababu ya kukosa uaminifu, Yerusalemu lilizingirwa mara mbili na Wababiloni na hatimaye kutekwa na kuharibiwa katika 607 K.W.K. (2 Mambo ya Nyakati 36:5, 6, 11-21) Kwa habari ya Moabu na Amoni, kulingana na Yosefo, mwanahistoria Myahudi, katika mwaka wa tano baada ya Yerusalemu kuanguka, Wababiloni walipiga vita nao na kuwashinda. Wao nao walipotelea mbali, kama ilivyotabiriwa.
19, 20. (a) Yehova alithawabishaje wale waliofuliza kumtarajia? (b) Kwa nini matukio haya yanatuhusu, na ni mambo yapi yatakayozungumzwa katika makala ifuatayo?
19 Utimizo wa jambo hili na mambo mengine madogo-madogo ya unabii wa Sefania uliimarisha imani ya Wayahudi na wasio-Wayahudi waliofuliza kumtarajia Yehova. Miongoni mwa wale waliookoka uharibifu uliopata Yuda na Yerusalemu walikuwa Yeremia, Ebed-Meleki Mwethiopia, na nyumba ya Yehonadabu, Mrekabu. (Yeremia 35:18, 19; 39:11, 12, 16-18) Wayahudi waaminifu waliokuwa katika uhamisho na wazao wao, walioendelea kumngoja Yehova, walikuja kuwa sehemu ya mabaki wenye furaha waliokombolewa kutoka Babiloni katika 537 K.W.K. na kurudi Yuda kuanzisha tena ibada safi.—Ezra 2:1; Sefania 3:14, 15, 20.
20 Mambo haya yote yana maana gani kwetu? Katika njia nyingi hali iliyokuwa katika siku ya Sefania yalingana na mambo yenye kuchukiza yanayotendeka katika Jumuiya ya Wakristo. Isitoshe, mitazamo mbalimbali ya Wayahudi katika nyakati hizo yafanana na mitazamo iwezayo kuonwa leo, nyakati nyingine hata miongoni mwa watu wa Yehova. Haya ni mambo yatakayozungumzwa katika makala ifuatayo.
[Maelezo ya Chini]
a Yaonekana kwamba maneno “wana wa mfalme” yarejezea wakuu wote wa kifalme, kwa kuwa wana wa Yosia mwenyewe walikuwa wachanga sana wakati huo.
Kwa Njia ya Pitio
◻ Kulikuwa na hali gani ya kidini katika Yuda katika siku ya Sefania?
◻ Ni hali zipi zilizoenea miongoni mwa viongozi wa kijamii, na watu wengi walikuwa na mtazamo gani?
◻ Mataifa yalijitukuzaje juu ya watu wa Yehova?
◻ Sefania alitoa onyo gani kwa Yuda na mataifa mengine?
◻ Wale waliofuliza kumtarajia Yehova walithawabishwaje?
[Picha katika ukurasa wa 9]
Jiwe la Moabu lathibitisha kwamba Mfalme Mesha wa Moabu alisema maneno yenye suto dhidi ya Israeli la kale
[Hisani]
Jiwe la Moabu: Musée du Louvre, Paris
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kwa kuunga mkono unabii wa Sefania, bamba hili la Tarihi ya Babiloni larekodi uharibifu wa Ninawi uliofanywa na majeshi yaliyoungana
[Hisani]
Bamba la tarihi: Kwa hisani ya British Museum