Sura ya 29
“Vitu vya Kuchukiwa na Mataifa Yote”
WAKATI wa jioni ya mwisho ambayo Yesu alitumia na mitume wake kabla ya kifo chake, yeye aliwakumbusha hivi: “Mtumwa si mkubwa zaidi kuliko bwana-mkubwa wake. Ikiwa wameninyanyasa mimi, watawanyanyasa nyinyi pia; ikiwa wameshika neno langu, watashika lenu pia. Lakini watafanya mambo yote haya dhidi yenu kwa ajili ya jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma.”—Yn. 15:20, 21, NW.
Yesu hakuwa akifikiria visa vya hapa na pale tu vya kutokuvumilia. Siku tatu tu mapema, alikuwa amesema hivi: “Nanyi mtakuwa vitu vya kuchukiwa na mataifa yote kwa sababu ya jina langu.”—Mt. 24:9, NW.
Na bado, Yesu aliwashauri wafuasi wake kwamba wanapokabiliwa na mnyanyaso, ni lazima wasiamue kutumia silaha halisi. (Mt. 26:48-52) Hawakupaswa kuwatukana wanyanyasi wao au kujaribu kuwalipiza kisasi. (Rum. 12:14; 1 Pet. 2:21-23) Je, labda haingekuwa kwamba hata wanyanyasi hao wangekuja kuwa waamini siku fulani? (Mdo. 2:36-42; 7:58–8:1; 9:1-22) Mungu angeachiwa alipize kisasi.—Rum. 12:17-19.
Inajulikana vema kwamba Wakristo wa mapema walinyanyaswa kikatili na serikali ya Roma. Lakini inastahili kuangaliwa kwamba wanyanyasi wakuu wa Yesu Kristo walikuwa viongozi wa kidini na kwamba Pontio Pilato, gavana Mroma, alimwua Yesu kwa sababu hao walidai hilo. (Luka 23:13-25) Baada ya kifo cha Yesu kwa mara nyingine tena ni viongozi wa kidini waliokuwa katika mstari wa mbele wakiwa wanyanyasi wa wafuasi wa Yesu. (Mdo. 4:1-22; 5:17-32; 9:1, 2) Je, hicho hakijakuwa ndicho kiolezo katika nyakati za hivi karibuni?
Makasisi Waomba Kuwe na Mjadala wa Hadhara
Mwenezo wa maandishi ya C. T. Russell ulipoongezeka upesi kufikia makumi ya mamilioni ya nakala katika lugha nyingi, makasisi Wakatoliki na Waprotestanti hawangeweza kupuuza kwa urahisi yale aliyokuwa akisema. Wakighadhibishwa na kule kufunuliwa kwa mafundisho yao kuwa yasiyo ya Kimaandiko, na wakifadhaishwa kwa kuwapoteza washiriki, makasisi wengi walitumia mimbari yao ili kushutumu maandishi ya Russell. Waliwaamuru makundi yao yasikubali fasihi zinazogawanywa na Wanafunzi wa Biblia. Idadi fulani yao walijaribu kuwachochea maofisa wa umma wakomeshe kazi hiyo. Katika sehemu nyingine katika Marekani—miongoni mwazo Tampa, Florida; Rock Island, Illinois; Winston-Salem, North Carolina; na Scranton, Pennsylvania—walisimamia kuchomwa hadharani kwa vitabu vilivyoandikwa na Russell.
Baadhi ya makasisi walihisi uhitaji wa kuangamiza uvutano wa Russell kwa kumfunua katika mjadala wa hadhara. Karibu na makao makuu ya utendaji wake, kikundi cha makasisi kilipendekeza Dakt. E. L. Eaton, pasta wa Kanisa la Methodisti ya Kiepiskopali ya North Avenue katika Allegheny, Pennsylvania, awe msemaji wacho. Katika 1903 yeye alidokeza kuwe na mjadala wa hadhara, na Ndugu Russell alikubali huo mwaliko.
Mambo sita ya kujadiliwa yalijulishwa kama ifuatavyo: Ndugu Russell alithibitisha, lakini Dakt. Eaton akakana, kwamba nafsi za wafu hazitambui lolote; kwamba “kuja kwa pili” kwa Kristo kunatangulia Mileani na kwamba kusudi la “kuja [kwake] kwa pili” na Mileani pia ni kubarikiwa kwa familia zote za dunia; pia kwamba ni watakatifu wa “kipindi cha Gospeli” tu wanaoshiriki katika ufufuo wa kwanza lakini kwamba halaiki kubwa watakuwa na fursa ya kuokoka kwa ufufuo unaofuata. Dakt. Eaton alithibitisha, lakini Ndugu Russell akakana, kwamba mtu yeyote hangejaribiwa baada ya kufa; kwamba wote wanaookolewa wataenda mbinguni; na kwamba waovu watundu watateswa milele. Mfululizo wa mijadala sita juu ya mambo hayo ulifanywa, kila mjadala mbele ya umati uliojaza Jumba la Carnegie katika Allegheny mwaka 1903.
Ni nini kilichochochea mwito huo wa kuwa na mjadala? Akitazama jambo hilo katika mwono wa kihistoria, Albert Vandenberg aliandika hivi baadaye: “Mijadala iliongozwa na mhubiri kutoka dhehebu tofauti la Protestanti akiwa msimamizi wakati wa kila kikao cha mazungumzo. Kwa kuongezea, wahubiri kutoka makanisa mbalimbali ya karibu waliketi kwenye jukwaa la msemaji pamoja na Mwadhama Eaton, inasemekana ili kumpa utegemezo wa kimaandiko na kumuunga mkono. . . . Jambo la kwamba muungano wa makasisi Waprotestanti usio rasmi ungeweza kufanyizwa lilionyesha kwamba waliogopa uwezo wa Russell wa kuwaongoa washiriki wa madhehebu yao.”—“Charles Taze Russell: Nabii wa Pittsburgh, 1879-1909,” iliyochapwa katika The Western Pennsylvania Historical Magazine, Januari 1986, uku. 14.
Mijadala kama hiyo kidogo ilikuwa michache. Haikuwa na matokeo yaliyotakwa na muungano wa makasisi. Baadhi ya watu wa kutaniko la Dakt. Eaton walivutiwa na yale waliyosikia wakati wa mfululizo wa mihadhara katika 1903, wakaacha kanisa lake na kuchagua kushirikiana na Wanafunzi wa Biblia. Hata kasisi mmoja aliyekuwako alikiri kwamba Russell alikuwa ‘ameelekeza bomba la maji kwenye helo na kuuzima moto huo.’ Hata hivyo, Ndugu Russell mwenyewe alihisi kwamba kusudi la ile kweli lingeweza kutimizwa vema zaidi kwa kutumia wakati na jitihada katika utendaji mwingineo badala ya mijadala.
Makasisi hawakuacha mashambulizi yao. Ndugu Russell alipozungumza katika Dublin, Ireland, na Otley, Yorkshire, Uingereza, waliweka wanaume miongoni mwa wasikilizaji ili wapaaze sauti wakipinga na kutoa mashtaka bandia dhidi ya Russell mwenyewe. Ndugu Russell alishughulikia hali hizo kwa ustadi, wakati wote akitegemea Biblia kuwa mamlaka kwa majibu yake.
Bila kujali dhehebu, makasisi Waprotestanti walishirikiana katika ule ulioitwa Muungano wa Kievanjeli. Wawakilishi wao katika nchi nyingi walikuwa wachochezi dhidi ya Russell na wale waliogawanya fasihi zake. Katika Texas (Marekani), kwa kielelezo, Wanafunzi wa Biblia walipata kwamba kila kasisi, hata katika miji na wilaya za mashambani zilizo ndogo zaidi, alikuwa na aina ileile ya mashtaka bandia dhidi ya Russell na upotovu uleule wa yale aliyofundisha.
Hata hivyo, nyakati nyingine mashambulizi dhidi ya Russell yalikuwa na matokeo ambayo makasisi hawakutarajia. Katika New Brunswick, Kanada, wakati mhubiri alipotumia mimbari yake ili kutoa hotuba yenye kuvunjia heshima Russell, miongoni mwa wasikilizaji kulikuwa na mtu aliyekuwa amesoma binafsi fasihi zilizoandikwa na Ndugu Russell. Aliudhika wakati mhubiri alipotumia uwongo wa kukusudia. Karibu na katikati ya hotuba, mtu huyo alisimama, akamshika mke wake kwa mkono, na kuwaita mabinti wake saba walioimba katika kwaya: “Njooni wasichana, tunaenda nyumbani.” Wote tisa walitoka nje, na mhubiri akatazama huku yule mtu aliyekuwa amejenga kanisa na alikuwa mwandalizi mkuu wa fedha za kutaniko alipoondoka. Upesi kutaniko likatokomea, na mhubiri huyo akaenda zake.
Kutumia Dhihaka na Uchongezi
Katika jitihada zao nyingi za kuangamiza uvutano wa C. T. Russell na washiriki wake, makasisi walipuuza dai kwamba yeye alikuwa mhudumu Mkristo. Kwa sababu hizohizo, viongozi wa kidini Wayahudi katika karne ya kwanza waliwatendea mitume Petro na Yohana kama “watu wasio na elimu na wa kawaida tu.”—Mdo. 4:13, NW.
Ndugu Russell hakuwa amehitimu kutoka mojawapo shule za kitheolojia za Jumuiya ya Wakristo. Lakini alisema hivi kwa ujasiri: “Tunawatolea [makasisi] mwito wa ushindani wathibitishe kwamba walikuwa wametawazwa Kimungu au kwamba wamepata kufikiri juu yalo. Wao hufikiri tu juu ya kutawazwa kimafarakano, au kuagizwa, kila mmoja kutoka kwa farakano au kikundi chake. . . . Kutawazwa au kuagizwa na Mungu kwa mtu yeyote ili ahubiri ni kwa kupewa Roho Takatifu. Mtu yeyote ambaye amepokea Roho Takatifu amepokea uwezo na mamlaka ya kufundisha na kuhubiri katika jina la Mungu. Mtu yeyote ambaye hajapokea Roho Takatifu hana mamlaka au idhini ya Kimungu ya kuhubiri kwake.”—Isa. 61:1, 2.
Ili kutilia shaka sifa yake, baadhi ya makasisi walihubiri na kuchapisha uwongo mbaya juu yake. Mojawapo waliyotumia mara nyingi—na bado hutumia—linahusu hali ya ndoa ya Ndugu Russell. Maoni ambayo wamejaribu kuonyesha ni kwamba Russell alikosa maadili. Mambo hakika ni yapi?
Katika 1879, Charles Taze Russell alioa Maria Frances Ackley. Walikuwa na uhusiano mzuri kwa miaka 13. Kisha, wengine walipombembeleza Maria na kwa vile yeye alikuwa na mwelekeo wa kiburi, uhusiano huo ulianza kudhoofika; lakini kusudi lao lilipojulikana, ni kama alipata usawaziko wake tena. Baada ya mtu aliyekuwa mshiriki kueneza mambo ya uwongo kuhusu Ndugu Russell, yeye hata alimwuliza ruhusa mume wake ili azuru makutaniko kadhaa ili akanushe mashtaka hayo, kwa kuwa ilikuwa imesemekana kuwa Ndugu Russell alimkandamiza. Hata hivyo, inaonekana kwamba upokezi mwema aliopata kwenye safari hiyo katika 1894 ulisababisha badiliko la hatua kwa hatua la jinsi alivyojiona. Alijaribu kupata uwezo zaidi katika kuelekeza yale ambayo yangewekwa katika Watch Tower.a Alipong’amua kwamba hakuna chochote alichoandika ambacho kingechapwa isipokuwa mume wake, aliye mhariri wa gazeti hilo, akubaliane na yaliyomo (kwa msingi wa upatano wayo na Maandiko), aliudhika sana. Russell alitia jitihada nyingi ili kumsaidia, lakini katika Novemba 1897 Maria alimwacha. Hata hivyo, alimwandalia mahali pa kuishi na utegemezo mwingineo. Miaka mingi baadaye, baada ya mashtaka ya mahakamani aliyokuwa amepeleka katika 1903, Maria alipata uamuzi katika 1908, si wa talaka kamili, bali wa haki ya kisheria ya kutoishi na Russell, huku Maria akipokea malipo kutoka kwake.
Baada ya kushindwa kumlazimisha mume wake akubaliane na matakwa yake, alitia jitihada nyingi baada ya yeye kumwacha ili kuharibu sifa ya jina lake. Katika 1903 alichapisha trakti iliyojaa, si kweli za Kimaandiko, bali masingizio mabaya juu ya Ndugu Russell. Alijaribu kuwatumia wahubiri wa madhehebu mbalimbali ili wazigawanye mahali ambapo Wanafunzi wa Biblia walikuwa wakifanya mikutano ya pekee. Wahubiri hao wanastahili kupewa sifa kwa sababu si wengi wakati huo waliotaka kutumiwa kwa njia hiyo. Hata hivyo, tangu wakati huo makasisi wengine wameonyesha roho tofauti.
Hapo awali, Maria Russell alikuwa ameshutumu, kwa mdomo na kwa maandishi, wale waliomshtaki Ndugu Russell na aina ya ukosefu wa adili ambao yeye mwenyewe alimshtaki nao. Wakitumia taarifa fulani zisizothibitishwa zilizofanywa wakati wa mashtaka ya mahakamani katika 1906 (taarifa ambazo zilifutwa katika rekodi kwa amri ya mahakama), baadhi ya wapinzani wa kidini wa Ndugu Russell wamechapisha mashtaka yaliyofanywa yaonekane kana kwamba alikuwa mtu asiye na maadili na hivyo hafai kuwa mhudumu wa Mungu. Hata hivyo, rekodi ya mahakama iko wazi kwamba mashtaka kama hayo si ya kweli. Wakili wake mwenyewe alimuuliza Bi. Russell kama aliamini mume wake alikuwa na hatia ya uzinzi. Yeye alijibu: “La.” Pia ni jambo linalostahili kuangaliwa kwamba wakati halmashauri ya wazee Wakristo iliposikiliza mashtaka ya Bi. Russell dhidi ya mume wake katika 1897, hakutaja yoyote ya mambo aliyosema baadaye mahakamani ili kusadikisha wasaidizi wa hakimu kwamba talaka yapaswa itolewe, ingawa matukio hayo yaliyosingiziwa yalitukia kabla ya mkutano huo.
Miaka tisa baada ya Bi. Russell kuwasilisha kesi hiyo mahakamani kwa mara ya kwanza, Hakimu James Macfarlane aliandika barua ya majibu kwa mtu aliyekuwa akitafuta nakala ya rekodi ya mahakama ili mmoja wa washiriki wake amfunue Russell. Hakimu alimwambia waziwazi kwamba kile alichotaka kingekuwa ni kupoteza wakati na pesa. Barua yake ilisema: “Msingi wa mashtaka yake na wa amri iliyotolewa baada ya uamuzi wa wasaidizi wa hakimu ulikuwa ‘ufidhuli’ na si uzinzi na kama ninavyoelewa, ushuhuda hauonyeshi kwamba Russell alikuwa akiishi ‘maisha ya uzinzi na mwenzi mwingine.’ Kwa kweli hakukuwa na mwenzi mwingine.”
Ungamo lililochelewa la Maria Russell mwenyewe lilikuja wakati wa maziko ya Ndugu Russell kwenye Jumba la Carnegie katika Pittsburgh mwaka 1916. Akiwa amevaa utaji, alitembea katika kijia kilicho kati ya viti hadi kwenye jeneza na kuweka hapo furushi la maua-lili ya bondeni. Kulikuwa na utepe uliofungishwa wenye maneno, “Kwa Mume Wangu Mpendwa.”
Ni wazi kwamba makasisi wametumia aina ileile ya mbinu zilizotumiwa na wenzao wa karne ya kwanza. Wakati ule, walijaribu kuharibu sifa ya Yesu kwa kushtaki kwamba alikuwa pamoja na watenda dhambi na kwamba yeye mwenyewe alikuwa mtenda dhambi na mkufuru. (Mt. 9:11; Yn. 9:16-24; 10:33-37) Mashtaka ya aina hiyo hayakubadili kweli kuhusu Yesu, lakini yalifunua wale walioamua kutumia uchongezi huo—na yanafunua wale wanaoamua kutumia mbinu hizohizo leo—kuwa baba yao wa kiroho ni Ibilisi, jina linalomaanisha “Mchongezi.”—Yn. 8:44.
Kutumia Harara ya Wakati wa Vita ili Kutimiza Malengo Yao
Huku kukiwa na harara ya utukuzo wa taifa uliokumba ulimwengu wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, silaha mpya ilipatikana ili itumiwe dhidi ya Wanafunzi wa Biblia. Uadui wa viongozi wa kidini wa Protestanti na Katoliki ya Roma ungeweza kuonyeshwa kwa kutumia kisitiri cha uzalendo. Walitumia msisimko wa wakati wa vita kwa faida yao ili kuwashtaki Wanafunzi wa Biblia kuwa wachochezi—shtaka lilelile ambalo lilielekezwa kwa Yesu Kristo na mtume Paulo na viongozi wa kidini wa Yerusalemu wa karne ya kwanza. (Luka 23:2, 4; Mdo. 24:1, 5) Bila shaka, ili makasisi wafanye shtaka hilo, wao wenyewe wangelazimika kuwa waungaji mkono walio watendaji wa vita, lakini hilo halikuonekana kuwa likiwasumbua wengi wao, hata ingawa lilimaanisha kutuma vijana wakawaue washiriki wa dini yao wenyewe katika nchi nyingine.
Ilikuwa katika Julai 1917, baada ya kifo cha Russell, kwamba Watch Tower Society ilitoa kitabu The Finished Mystery, ufafanuzi juu ya Ufunuo na Ezekieli pamoja na Wimbo Ulio Bora. Kitabu hicho kilifunua waziwazi unafiki wa makasisi wa Jumuiya ya Wakristo! Kiligawanywa sana kwa wakati mfupi. Mwishoni mwa Desemba 1917 na mapema katika 1918, Wanafunzi wa Biblia katika Marekani na Kanada pia walianza kugawanya nakala 10,000,000 za ujumbe wenye kuchoma katika trakti The Bible Students Monthly. Trakti hiyo ya kurasa nne yenye ukubwa wa kiasi ilikuwa na kichwa “Kuanguka kwa Babiloni,” na ilikuwa na kichwa kidogo “Sababu Kwa Nini Ni Lazima Jumuiya ya Wakristo Iteseke Sasa—Tokeo la Mwisho.” Ilitambulisha matengenezo ya kidini ya Katoliki na Protestanti yakiwa pamoja kuwa Babiloni ya kisasa, ambayo lazima ianguke hivi karibuni. Katika kuunga mkono yale yaliyosemwa, ilitokeza tena kutoka kitabu The Finished Mystery mafafanuzi juu ya unabii mbalimbali unaoonyesha hukumu ya kimungu dhidi ya “Babiloni wa Kifumbo.” Kwenye ukurasa wa nyuma kulikuwa na katuni iliyochorwa kuonyesha ukuta ukiporomoka. Mawe makubwa kutoka kwenye ukuta huo yalikuwa na vibandiko kama vile “Fundisho la Utatu (‘3 X 1 = 1’),” “Kutokufa kwa Nafsi,” “Nadharia ya Mateso ya Milele,” “Uprotestanti—mafundisho, makasisi, n.k.,” “Uroma—mapapa, makadinali, n.k., n.k.”—na mawe hayo yote yalikuwa yakianguka.
Makasisi walighadhibishwa na kufunuliwa huko, kama vile makasisi wa Kiyahudi walivyoghadhibika wakati Yesu alipofunua unafiki wao. (Mt. 23:1-39; 26:3, 4) Katika Kanada makasisi walitenda upesi. Katika Januari 1918, makasisi zaidi ya 600 wa Kanada walitia sahihi ombi lenye kusihi serikali izuie vichapo vya Shirika la Kimataifa la Wanafunzi wa Biblia. Kama ilivyoripotiwa katika Winnipeg Evening Tribune, baada ya Charles G. Paterson, pasta wa Kanisa la St. Stephen katika Winnipeg, kushutumu kutoka kwenye mimbari The Bible Students Monthly, iliyokuwa na makala “Kuanguka kwa Babiloni,” Mkuu wa Sheria Johnson aliwasiliana naye ili apate nakala. Punde baadaye, Februari 12, 1918, amri ya serikali ya Kanada ilifanya liwe kosa linalostahili adhabu ya kutozwa faini na kufungwa gerezani, mtu akipatikana ana ama kitabu The Finished Mystery ama trakti inayoonyeshwa juu.
Mwezi huohuo, mnamo Februari 24, Ndugu Rutherford, msimamizi mpya aliyechaguliwa wa Watch Tower Society, alihutubu katika Marekani kwenye Jumba la Temple jijini Los Angeles, California. Kichwa cha habari yake kilishtusha: “Ulimwengu Umekwisha—Mamilioni Wanaoishi Sasa Huenda Wasife Kamwe.” Katika kutoa ithibati kwamba ulimwengu kama ulivyojulikana kufikia wakati huo kwa kweli ulikuwa umekwisha katika 1914, alielekeza kwenye vita iliyokuwa ikiendelea, pamoja na njaa yenye kuandamana, na kuitambulisha kuwa sehemu ya ishara iliyotabiriwa na Yesu. (Mt. 24:3-8) Kisha alielekeza fikira kwa makasisi, akisema:
“Wakiwa jamii, kulingana na maandiko, makasisi ndio watu wenye kulaumika zaidi duniani kwa sababu ya vita kuu inayokumba wanadamu sasa. Kwa miaka 1,500 wamefundisha watu fundisho la kishetani la haki ya kimungu ya watawala kuweza kumiliki. Wamechanganya siasa na dini, kanisa na taifa; wamethibitika kuwa wasio waaminifu-washikamanifu kwa pendeleo lao walilopewa na Mungu la kupiga mbiu ya ujumbe wa ufalme wa Mesiya, na wamejitoa wenyewe ili kuwatia moyo watawala waamini kwamba mtawala humiliki kwa haki ya kimungu, na kwa hiyo lolote afanyalo linafaa.” Akionyesha tokeo la hilo, yeye alisema: “Wafalme wa Ulaya wenye tamaa ya kibinafsi walijihami tayari kwa vita, kwa sababu walitamani kunyakua maeneo ya watu wengineo; na makasisi waliwapongeza na kusema: ‘Fanyeni mtakalo, hamwezi kukosea; lolote mfanyalo lafaa.’” Lakini si makasisi wa Ulaya tu waliokuwa wakifanya hivyo, wahubiri katika Amerika walifanya ivyo hivyo.
Ripoti ndefu ya mhadhara huo ilichapwa siku iliyofuata katika gazeti Morning Tribune la Los Angeles. Makasisi walighadhibishwa sana hivi kwamba shirika la wahudumu lilifanya mkutano siku iyo hiyo na likamtuma msimamizi walo kwa mameneja wa gazeti hilo ili kuwajulisha juu ya kuudhika kwao kwingi. Kufuatia hilo, kulikuwa na kipindi cha kupekuliwapekuliwa kwa ofisi za Watch Tower Society na washiriki wa idara ya upelelezi ya serikali.
Wakati wa kipindi hicho cha harara ya utukuzo wa taifa, kongamano la makasisi lilifanywa jijini Philadelphia, katika Marekani, ambamo azimio lilipitishwa likiomba Sheria ya Ujasusi ipitiwe tena ili wakiukaji wanaoshtakiwa wajaribiwe katika mahakama ya kijeshi na kupewa adhabu ya kifo. John Lord O’Brian katibu wa pekee wa mkuu wa sheria kwa kazi ya vita, aliteuliwa kuwasilisha jambo hilo katika Bunge. Rais wa Marekani hakuruhusu mswada huo uwe sheria. Lakini Meja-Jenerali James Franklin Bell, wa jeshi la Marekani, akiwa ameghadhibika sana aliwaambia J. F. Rutherford na W. E. Van Amburgh yale yaliyokuwa yametukia kwenye kongamano hilo na kusudi la kutumia mswada huo dhidi ya maofisa wa Watch Tower Society.
Faili rasmi za serikali ya Marekani zinaonyesha kwamba angalau kuanzia Februari 21, 1918, na kuendelea, John Lord O’Brian, alihusika binafsi katika jitihada za kufanya mashtaka dhidi ya Wanafunzi wa Biblia. Rekodi ya Bunge ya Aprili 24 na Mei 4 ina hati kutoka kwa John Lord O’Brian ambayo alitoa hoja kwa nguvu kwamba ikiwa sheria iliruhusu kusemwa kwa “yale yaliyo ya kweli, kwa makusudi mema, na kwa njia zinazofaa,” kama ilivyosemwa katika ile iliyoitwa eti Sahihisho la Sheria ya Ujasusi ya Ufaransa na kama vile ilivyokuwa imekubaliwa na Bunge la Marekani, hangeweza kuwashtaki Wanafunzi wa Biblia kwa kufanikiwa.
Katika Worcester, Massachusetts, “Mwadhama” B. F. Wyland alitumia harara ya vita kwa faida yake kwa kudai kwamba Wanafunzi wa Biblia walikuwa wakiendeleza propaganda ya adui. Alichapa makala moja katika Daily Telegram ambayo alijulisha: “Mojawapo kazi za uzalendo zinazowakabili nyinyi mkiwa wananchi ni kulikandamiza Shirika la Kimataifa la Wanafunzi wa Biblia, lenye makao makuu katika Brooklyn. Chini ya kisitiri cha dini, wamekuwa wakiendeleza propaganda ya Ujerumani katika Worcester kwa kuuza kitabu chao, ‘The Finished Mystery.’” Aliwaambia wenye mamlaka waziwazi kwamba ilikuwa kazi yao kuwakamata Wanafunzi wa Biblia na kuwazuia wasifanye mikutano zaidi.
Kulikuwa na mnyanyaso wenye kuenea wa Wanafunzi wa Biblia katika masika na kiangazi cha 1918, katika Amerika Kaskazini na Ulaya pia. Miongoni mwa wachochezi mlikuwamo makasisi wa Baptisti, Methodisti, Episkopali, Luther, Katoliki ya Roma, na makanisa mengineyo. Fasihi za Biblia zilitwaliwa na maofisa bila hati ya upekuzi, na Wanafunzi wa Biblia wengi wakatiwa gerezani. Wengine walifukuzwa na wafanyaghasia, wakapigwa, wakachapwa mijeledi, wakamwagiwa lami na manyoya, au wakavunjwa mbavu au kukatwa vichwa. Wengine walilemazwa kabisa. Wanaume na wanawake Wakristo walitiwa gerezani bila kushtakiwa au bila kuhukumiwa. Visa hususa zaidi ya mia moja vya kutendwa kikatili viliripotiwa katika The Golden Age la Septemba 29, 1920.
Washtakiwa kwa Ujasusi
Kilele kilifikiwa Mei 7, 1918, wakati waranti za serikali zilipotolewa katika Marekani za kumkamata J. F. Rutherford, msimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society, na washiriki wake wa karibu.
Siku iliyotangulia, mashtaka mawili yalikuwa yamefanywa dhidi ya Ndugu Rutherford na washiriki wake, katika Brooklyn, New York. Kama matokeo yaliyotakwa hayakupatikana katika kesi moja, shtaka lile jingine lingefuatiliwa. Shtaka la kwanza, lililofanywa dhidi ya idadi kubwa zaidi ya watu, lilitia ndani mashtaka manne: Mawili yaliwashtaki kwa kufanya shauri ili kukiuka Sheria ya Ujasusi ya Juni 15, 1917; na mengine mawili yaliwashtaki kwa kujaribu kufanya mipango isiyo halali au kufanya hivyo hasa. Ilidaiwa kwamba walikuwa wanafanya shauri ili kuleta maasi na kukataa kazi ya uanajeshi katika Marekani na kwamba walikuwa wanafanya shauri kuzuia kusajiliwa na kuandikishwa kwa watu kwa ajili ya utumishi huo taifa lilipokuwa vitani, pia kwamba walikuwa wamejaribu kufanya au walikuwa hasa wamefanya mambo hayo yote mawili. Shtaka lilitaja kihususa kuchapwa na kugawanywa kwa kitabu The Finished Mystery. Shtaka la pili lilionyesha kwamba kule kupelekwa kwa hundi hadi Ulaya (ambayo ingetumiwa kwa kazi ya elimu ya Biblia katika Ujerumani) kuwa ni tisho kwa masilahi ya Marekani. Wakati washtakiwa walipopelekwa mahakamani, lile shtaka la kwanza, lenye mashtaka manne, ndilo lilifuatiwa.
Shtaka jingine la C. J. Woodworth na J. F. Rutherford chini ya Sheria ya Ujasusi lilikuwako katika Scranton, Pennsylvania. Lakini, kulingana na barua kutoka kwa John Lord O’Brian ya tarehe Mei 20, 1918, washiriki wa Idara ya Sheria walihofu kwamba Hakimu Witmer wa Wilaya ya Marekani, ambaye angeamua mashtaka, hangekubali utumizi wao wa Sheria ya Ujasusi ili kukandamiza utendaji wa watu ambao, kwa sababu ya masadikisho ya kidini yaliyo manyoofu, walisema mambo ambayo wengine wangeyaona kuwa propaganda ya kupinga vita. Kwa hiyo Idara ya Sheria iliikawiza kesi ya Scranton, ikingoja matokeo ya kesi ya Brooklyn. Serikali pia iliongoza mambo hivi kwamba Hakimu Harland B. Howe, kutoka Vermont, ambaye John Lord O’Brian alijua alikubaliana na maoni yake katika mambo kama hayo, angekuwa mwamuzi wa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Marekani kwa Wilaya ya Mashariki ya New York. Kesi ilianza Juni 5, washtaki wakiwa Isaac R. Oeland na Charles J. Buchner wa Katoliki ya Roma. Wakati kesi ilipokuwa ikiendelea, kama vile Ndugu Rutherford alivyoona, mapadri Wakatoliki walishauriana mara kwa mara na Buchner na Oeland.
Kadiri kesi ilivyoendelea, ilionyeshwa kwamba maofisa wa Sosaiti na watungaji wa kile kitabu hawakuwa na madhumuni ya kuingilia shughuli za vita za nchi. Ushahidi uliotolewa wakati wa mashtaka ulionyesha kwamba mipango kwa ajili ya kuandikwa kwa kitabu hicho—kwa kweli, uandishi wa sehemu kubwa ya kitabu hicho—ulikuwa umefanywa kabla ya Marekani kutangaza vita (Aprili 6, 1917) na kwamba maafikiano ya kwanza ya kukichapa yalikuwa yametiwa sahihi kabla ya Marekani kupitisha sheria (mnamo Juni 15) ambayo ilisemwa walikuwa wamekiuka.
Mashtaka yalikazia nyongeza kwenye kitabu hicho iliyofanywa wakati wa Aprili na Juni wa 1917, katika shughuli za kutayarisha nakala na kusoma zile zilizokamilishwa. Hiyo ilitia ndani nukuu kutoka kwa John Haynes Holmes, kasisi aliyekuwa amejulisha kwa nguvu kwamba vita ilikuwa kukiuka Ukristo. Kama ilivyoonyeshwa na mmojawapo mawakili watetezi, maelezo hayo ya kasisi, yaliyochapwa katika kitabu chenye kichwa A Statement to My People on the Eve of War, kilikuwa bado kikiuzwa katika Marekani wakati wa kesi hiyo. Wala kasisi huyo wala mchapaji wacho hawakushtakiwa. Lakini Wanafunzi wa Biblia waliorejezea hotuba yake ndio walioshtakiwa kwa mambo yaliyosemwa ndani yacho.
Kitabu The Finished Mystery hakikuwaambia watu wa ulimwengu kwamba hawakuwa na haki ya kushiriki vitani. Lakini, katika kueleza unabii, kilinukuu madondoo kutoka matoleo ya The Watch Tower la 1915 ili kuonyesha kutopatana kwa makasisi waliodai kuwa wahudumu wa Kristo lakini walikuwa wakitenda wakiwa wajumbe wa kuandikisha majeshi ya mataifa yaliyo vitani.
Ilipofahamika kwamba serikali ilipinga kitabu hicho, Ndugu Rutherford alikuwa amepeleka telegramu mara hiyo kwa mchapaji ili aache kukitokeza, na wakati uleule, mwakilishi wa Sosaiti alikuwa ametumwa kwenye idara ya upelelezi ya Jeshi la Marekani ili kujua sababu ya wao kukipinga. Ilipojulikana kwamba kwa sababu ya vita iliyokuwa ikiendelea, kurasa 247-253 za kitabu hicho zilionwa kuwa zisizofaa, Sosaiti ilielekeza kwamba kurasa hizo ziondolewe katika nakala zote za kitabu hicho kabla ya umma kupewa. Na wakati serikali ilipojulisha mawakili wa wilaya kwamba kugawanywa kwacho zaidi kungekuwa ni kukiuka Sheria ya Ujasusi (ingawa serikali ilikataa kutoa maoni kwa Sosaiti juu ya kitabu hicho kikiwa kimebadilishwa), Sosaiti ilielekeza kwamba kugawanywa kote kwa kitabu hicho kwa umma kukomeshwe.
Kwa Nini Hukumu Kali Jinsi Hiyo?
Kujapokuwa na yote hayo, katika Juni 20, 1918, wasaidizi wa hakimu walifanya uamuzi na wakampata kila mshtakiwa kuwa na kosa kwa kila shtaka. Siku iliyofuata, sabab kati yao walihukumiwa vifungo vinne vya miaka 20 kila moja, vinavyotumika pamoja. Julai 10, yule wa nanec alihukumiwa vipindi vinne vyenye kutumika pamoja vya miaka 10. Hukumu hiyo ilikuwa kali jinsi gani? Katika barua kwa mkuu wa sheria katika Machi 12, 1919, rais wa Marekani Woodrow Wilson alikiri kwamba “vifungo hivyo kwa wazi vinapita kiasi.” Kwa kweli, yule mtu aliyefyatua risasi katika Sarajevo ambazo zilimwua maliki mwana-mfalme wa Milki ya Austria na Hungaria—jambo lililochochea matukio yaliyoingiza mataifa katika Vita ya Ulimwengu 1—hakuwa amepata hukumu kali jinsi hiyo. Hukumu yake ilikuwa miaka 20 gerezani—si vifungo vinne vya miaka 20, kama ilivyokuwa kwa Wanafunzi wa Biblia!
Ni nini kilichochea kuwekwa kwa vifungo hivyo vikali vya Wanafunzi wa Biblia? Hakimu Harland B. Howe alijulisha: “Kwa maoni ya Mahakama, propaganda ya kidini ambayo washtakiwa hawa wametetea kwa bidii na kuieneza kotekote katika taifa na miongoni mwa mataifa rafiki, ni hatari kubwa zaidi ya kikosi kimoja cha Jeshi la Ujerumani. . . . Mtu anayehubiri dini mara nyingi huwa na uvutano mwingi, na ikiwa ni mnyoofu, yeye ni mwenye matokeo hata zaidi. Hilo linazidisha badala ya kupunguza kosa walilofanya. Kwa hiyo, likiwa jambo lifaalo zaidi kufanyia watu kama hao, Mahakama imekata kauli kwamba hukumu lazima iwe kali.” Hata hivyo, inastahili kuangaliwa pia kwamba kabla ya kupitisha hukumu, Hakimu Howe alisema kwamba taarifa zilizotolewa na mawakili wa washtakiwa zilikuwa zimetia shuku na kutendea isivyofaa si maofisa wa sheria wa serikali tu bali pia “wahudumu wote wa kidini kotekote nchini.”
Baada ya uamuzi huo, rufani ilikatwa mara hiyo kwa mahakama ya mzunguko ya rufani ya Marekani. Lakini Hakimu Howe alikataa kuwaachilia kwa dhamana wakisubiri kusikizwa kwa rufani hiyo,d na katika Julai 4, kabla ya rufani ya tatu iliyokuwa ya mwisho ya kupata dhamana kusikizwa, ndugu saba wa kwanza walihamishwa upesi wakapelekwa kwenye gereza la kitaifa la Atlanta, Georgia. Baada ya hapo, ilidhihirishwa kwamba kulikuwa na makosa 130 ya kimahakama katika hukumu hiyo yenye kupendelea upande mmoja sana. Kazi ya miezi mingi ilifanywa ili kutayarisha karatasi zilizotakikana katika kusikizwa kwa rufani. Wakati uo huo, vita ilikwisha. Mnamo Februari 19, 1919, ndugu wanane walio gerezani walipeleka rufani ili wahurumiwe rasmi na rais wa Marekani, Woodrow Wilson. Barua nyinginezo zilizohimiza kuachiliwa kwa ndugu hao zilipelekwa na wananchi wengi kwa mkuu wa sheria mpya. Kisha, mnamo Machi 1, 1919, katika kujibu maulizo ya mkuu wa sheria, Hakimu Howe alipendekeza “kubadilishwa mara hiyo” kwa hukumu hiyo. Ingawa hilo lingepunguza hukumu, pia lingethibitisha kosa la washtakiwa. Kabla ya hilo kufanywa, mawakili wa akina ndugu walimpelekea wakili mkuu wa Marekani agizo la mahakama lililoleta kesi hiyo mbele ya mahakama ya rufani.
Miezi tisa baada ya Rutherford na washiriki wake kuhukumiwa—na vita ikiwa imekwisha—Machi 21, 1919, mahakama ya rufani iliagiza washtakiwa wote wanane wapate dhamana, na Machi 26, waliachiliwa katika Brooklyn kwa dhamana ya dola 10,000 kila mmoja. Katika Mei 14, 1919, mahakama ya mzunguko ya Marekani ya rufani katika New York ilikata kauli: “Washtakiwa katika kesi hii hawakupewa hukumu ya kiasi na isiyopendelea upande wowote ambayo walistahili kupewa, na kwa sababu hiyo hukumu hiyo imebatilishwa.” Kesi hiyo iliahirishwa ili ifanywe upya. Hata hivyo, Mei 5, 1920, baada ya washtakiwa kuja mahakamani, baada ya kupewa samansi, wakili wa serikali katika mahakama ya wazi katika Brooklyn, alitangaza mara tano kuondolewa kwa mashtaka.e Kwa nini? Kama ilivyofunuliwa na barua zilizohifadhiwa katika Jumba la Hati za Kitaifa la Marekani, Idara ya Sheria ilihofu kwamba ikiwa masuala hayo yangepelekwa mbele ya wasaidizi wa hakimu wasiopendelea upande wowote, huku harara ya vita ikiwa imekwisha, wangeshindwa kesi hiyo. Wakili wa Marekani aitwaye L. W. Ross alisema katika barua kwa mkuu wa sheria: “Ninafikiri ingekuwa afadhali, kwa uhusiano wetu na umma, ikiwa kwa hiari yetu wenyewe” tungesema kwamba kesi imefungwa.
Siku iyo hiyo, Mei 5, 1920, shtaka lile jingine lililokuwa limefanywa katika Mei 1918 dhidi ya J. F. Rutherford na wanne kati ya washirika wake lilifutiliwa mbali pia.
Ni Nani kwa Kweli Aliyeyachochea?
Je, yote hayo kwa kweli yalichochewa na makasisi? John Lord O’Brian alikana hilo. Lakini mambo ya hakika yalijulikana vema na wale walioishi wakati huo. Katika Machi 22, 1919, gazeti lililochapwa katika Girard, Kansas liitwalo Appeal to Reason, liliteta hivi: “Wafuasi wa Pasta Russell, Wakifuatiwa na Ukorofi wa Makasisi wa ‘Orthodoksi,’ Walihukumiwa na Kufungwa Bila Dhamana, Ingawa Walifanya Kila Jitihada Iliyowezekana ili Kushikamana na Masharti ya Sheria ya Ujasusi. . . . Tunajulisha kwamba, hata iwe au isiwe kwamba Sheria ya Ujasusi ilikuwa ya kikatiba kikweli au inayofaa kiadili, wafuasi hao wa Pasta Russell walihukumiwa isivyo haki chini ya masharti yayo. Uchunguzi wa akili iliyofunguka wa ithibati utamsadikisha yeyote upesi kwamba watu hao si kwamba tu hawakuwa na kusudi la kukiuka sheria, bali pia hawakuikiuka.”
Miaka mingi baadaye, katika kitabu Preachers Present Arms, Dakt. Ray Abrams alionelea hivi: “Ni jambo lenye kutokeza kwamba makasisi wengi walishiriki sehemu ya uchochezi katika kujaribu kuwaondolea mbali Warusselli [kama vile Wanafunzi wa Biblia walivyoitwa kwa dharau]. Mizozo ya kidini na chuki za muda mrefu, ambazo hazikushughulikiwa kwa vyovyote mahakamani katika wakati wa amani, sasa zilifika mahakamani chini ya uvutano wa harara ya wakati wa vita.” Yeye pia alisema: “Uchanganuzi wa kesi yote huongoza kwenye mkataa kwamba hapo awali makanisa na makasisi walichochea harakati ya kuwafutilia mbali Warusselli.”—Kur. 183-185.
Hata hivyo, mwisho wa vita haukuleta mwisho wa mnyanyaso wa Wanafunzi wa Biblia. Kipindi kipya cha mnyanyaso ndicho kilichoanza.
Mapadri Wawachochea Polisi
Vita ikiwa imekwisha, masuala mengine yalichochewa na makasisi ili kukomesha utendaji wa Wanafunzi wa Biblia, ikiwa ingewezekana. Katika Bavaria ya Katoliki na sehemu nyingine za Ujerumani, wengi walikamatwa katika miaka ya 1920 chini ya sheria za uchuuzi. Lakini wakati kesi hizo zilipokuja kwenye mahakama za rufani, mara nyingi mahakimu waliwaunga mkono Wanafunzi wa Biblia. Hatimaye, baada ya mahakama kugharikishwa kwa maelfu ya kesi kama hizo, Wizara ya Mambo ya Ndani ilitoa agizo katika 1930 kwa maofisa wote wa polisi ikiwaagiza waache kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Wanafunzi wa Biblia chini ya sheria za uchuuzi. Hivyo, kwa muda mfupi, msongo kutoka kwa chanzo hicho ulikoma, na Mashahidi wa Yehova wakaendelea na utendaji wao kwa kiwango kisicho cha kawaida katika shamba la Ujerumani.
Makasisi pia walikuwa na uvutano wenye nguvu katika Rumania wakati wa miaka hiyo. Walifanikiwa kufanya sheria zichapishwe zilizopiga marufuku fasihi na utendaji wa Mashahidi wa Yehova. Lakini mapadri waliogopa kwamba huenda watu bado wakasoma fasihi ambazo tayari walikuwa nazo na hivyo wangejifunza juu ya mafundisho yasiyo ya Kimaandiko na madai ya uwongo ya kanisa. Ili kuzuia hilo, mapadri hasa walienda pamoja na polisi nyumba hadi nyumba wakitafuta fasihi zozote ambazo zilikuwa zimegawanywa na Mashahidi wa Yehova. Hata wangeuliza watoto wadogo wasiotambua kitu kama wazazi wao walikuwa wamekubali fasihi hizo. Ikiwa yoyote ilipatikana, watu walitishwa kupigwa na kufungwa ikiwa wangekubali kupata zaidi. Katika baadhi ya vijiji padri alikuwa pia ndiye meya na hakimu, na mtu yeyote aliyekosa kufanya yale ambayo padri alisema, hakupata haki yoyote.
Rekodi ambayo baadhi ya maofisa Waamerika waliweka katika kufanya mapenzi ya makasisi wakati wa kipindi hicho si nzuri pia. Kufuatia ziara ya Askofu wa Katoliki O’Hara katika La Grange, Georgia, kwa kielelezo, meya na wakili wa jiji walikamata baadhi ya Mashahidi wa Yehova katika 1936. Wakati wa kufungwa kwao, walilazimishwa kulala kando ya rundo la mbolea wakilalia magodoro yaliyomwagiwa mkojo wa ng’ombe, wakapewa chakula chenye mabuu, na kulazimishwa kujenga barabara na wafungwa wengineo.
Katika Poland pia, makasisi Wakatoliki walitumia kila njia ambayo wangeweza kubuni ili kuzuia kazi ya Mashahidi wa Yehova. Waliwachochea watu wafanye jeuri, wakachoma fasihi za Mashahidi wa Yehova waziwazi, wakawashutumu kuwa Wakomunisti, na kuwapeleka mahakamani kwa mashtaka kwamba fasihi zao zilikuwa zenye “kukufuru.” Hata hivyo, si maofisa wote waliotaka kufuata matakwa yao. Kwa kielelezo, wakili mkuu wa mahakama ya rufani wa Posen (Poznan), alikataa kumshtaki mmoja wa Mashahidi wa Yehova ambaye makasisi walikuwa wamemshutumu kwa shtaka kwamba alikuwa amerejezea makasisi Wakatoliki kuwa “tengenezo la Shetani.” Wakili mkuu mwenyewe alitaja kwamba roho ya kukosa maadili ambayo imeenea kotekote katika Jumuiya ya Wakristo kutoka kwa mahakama ya kipapa ya Aleksanda 6 (1492-1503 W.K.) ilikuwa kwa kweli ni roho ya tengenezo la kishetani. Na wakati makasisi walipomshtaki mmoja wa Mashahidi wa Yehova kwa kukufuru Mungu kwa sababu ya kugawanya fasihi za Watch Tower, wakili mkuu wa mahakama ya rufani katika Thorn (Toruń) aliamuru aachiliwe, akisema: ‘Mashahidi wa Yehova wana msimamo uleule kama Wakristo wa kwanza. Wakisingiziwa na kunyanyaswa, wanategemeza maadili ya juu zaidi katika ulimwengu mpotovu unaoangamia.’
Jumba la kuhifadhia hati za serikali la Kanada lilifunua kwamba ilikuwa ni kupatana na barua kutoka kwa makao makuu ya Kadinali Mkatoliki Villeneuve, wa Quebec, kwa waziri wa sheria, Ernest Lapointe, kwamba Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku katika Kanada mwaka 1940. Baadaye maofisa wengine wa serikali waliomba maelezo kamili ya sababu ya hatua hiyo, lakini majibu ya Lapointe hayakuridhisha hata kidogo wengi wa washiriki wa Bunge la Kanada.
Katika upande ule mwingine wa dunia, kulikuwa hila hizohizo za makasisi. Jumba la kuhifadhia hati za serikali la Australia lina barua kutoka kwa askofu mkuu wa Katoliki ya Roma wa Sydney kwa Mkuu wa Sheria W. M. Hughes ikihimiza kwamba Mashahidi wa Yehova watangazwe kuwa wasio halali. Barua hiyo iliandikwa Agosti 20, 1940, miezi mitano tu kabla ya marufuku kuwekwa. Baada ya kupitia tena msingi wa marufuku hiyo, Bw. Justice Williams wa Mahakama Kuu ya Australia alisema baadaye kwamba ilikuwa na “tokeo la kufanya utetezi wa kanuni na mafundisho ya dini ya Kikristo kuwa usio halali na kila mkutano wa kanisa unaofanywa na waamini katika kuzaliwa kwa Kristo kuwa kusanyiko lisilo halali.” Juni 14, 1943, Mahakama iliamua kwamba marufuku haikupatana na sheria za Australia.
Katika Uswisi gazeti la Katoliki lilitaka wenye mamlaka watwae fasihi za Mashahidi ambazo kanisa liliona kuwa zenye kuudhi. Walitisha kwamba ikiwa hilo halingefanywa, wao wenyewe wangechukua hatua bila kutumia njia halali. Katika sehemu nyingi za ulimwengu, hivyo ndivyo walivyofanya hasa!
Viongozi wa Kidini Waamua Kutumia Jeuri
Makasisi Wakatoliki katika Ufaransa walihisi kwamba bado walikuwa na uvutano wenye nguvu juu ya watu, na waliazimia kutoruhusu jambo lolote liingilie umiliki huo. Wakati wa mwaka 1924-1925, Wanafunzi wa Biblia katika nchi nyingi walikuwa wakigawanya trakti Ecclesiastics Indicted (Makasisi Washtakiwa). Katika 1925, J. F. Rutherford alipaswa ahutubu katika Paris juu ya kichwa “Hila za Makasisi Zafunuliwa.” Kuhusu yale yaliyotukia kwenye mkutano huo, mmoja aliyekuwapo alisema: “Jumba lilikuwa limejaa. Ndugu Rutherford alitokea kwenye jukwaa, na kulikuwa na makofi ya uchangamfu. Alianza kusema, wakati ghafula mapadri na washiriki wa Aksio ya Katoliki kama 50, waliojihami kwa vijiti, walipoingia upesi ndani ya jumba wakiimba La Marseillaise [wimbo wa taifa wa Ufaransa]. Walitupa trakti kutoka juu ya ngazi. Padri mmoja alipanda jukwaani. Vijana wawili walimtupa chini. Mara tatu, Ndugu Rutherford aliondoka jukwaani na kurudi tena. Hatimaye, aliondoka kabisa. . . . Meza zilizoonyesha fasihi zetu zilipinduliwa na vitabu vyetu vikatupwa huku na huku. Kulikuwa na mvurugo kabisa!” Lakini visa kama hivyo vilitukia tena na tena.
Akitoa ushahidi katika Ireland, Jack Corr, alighadhibikiwa na makasisi Wakatoliki mara kwa mara. Katika pindi moja, wafanyaghasia, wakichochewa na padri wa parishi, walimtoa kitandani usiku wa manane na kisha kuchoma fasihi zake zote katikati mwa mji. Mjini Roscrea katika Wilaya ya Tipperary, Victor Gurd na Jim Corby waliwasili mahali pao pa kulala na kupata kwamba wapinzani walikuwa wameiba fasihi zao, wakazimwagia petroli, na kuzichoma. Kuzunguka moto huo walikuwa polisi wa mahali hapo, makasisi, na watoto wa eneo hilo, wakiimba “Imani ya Baba Zetu.”
Kabla ya Mashahidi wa Yehova kukutana katika Madison Square Garden jijini New York mwaka 1939, matisho yalitolewa na wafuasi wa padri Mkatoliki Charles Coughlin kwamba kusanyiko hilo lingevunjwa. Polisi walijulishwa. Mnamo Juni 25, Ndugu Rutherford alisema kwa watu 18,000 au zaidi waliokuwa katika jumba hilo, kutia na wasikilizaji wengi wa kimataifa kwa njia ya redio, juu ya kichwa “Serikali na Amani.” Baada ya hotuba hiyo kuanza, Wakatoliki wa Roma na Wanazi 200 au zaidi, wakiongozwa na mapadri kadhaa Wakatoliki, walisongamana kwenye roshani. Baada ya kutolewa kwa ishara fulani, walianza kuvuma kwa sauti, wakipiga kelele kusema “Heil Hitler!” na “Viva Franco!” Walitumia kila aina ya lugha chafu na vitisho na kuwapiga wakaribishaji wengi waliochukua hatua kuzima mchafuko huo. Magenge hayo hayakufanikiwa kuvunja mkutano huo. Ndugu Rutherford aliendelea kusema kwa nguvu na bila kuogopa. Kwenye kilele cha mvurugo huo, alijulisha hivi: “Angalieni leo Wanazi na Wakatoliki ambao wangependa kuvunja mkutano huu, lakini kwa neema ya Mungu hawawezi kufanya hivyo.” Wasikilizaji waliunga mkono hilo kwa makofi mazito ya kurudiarudia. Mchafuko huo ulinaswa na vinasasauti katika pindi hiyo, na umesikiwa na watu katika sehemu nyingi za ulimwengu.
Hata hivyo, mahali ilipowezekana, kama katika siku za Baraza la Kuwahukumu Wazushi wa Kidini, makasisi wa Katoliki ya Roma walitumia Serikali ili kukandamiza wowote waliojaribu kutilia shaka mafundisho na mazoea ya kanisa.
Kutendwa Kikatili Katika Kambi za Mateso
Adolf Hitler alikuwa rafiki mkubwa wa makasisi. Wakati wa 1933, mwaka uleule ambao mwafaka kati ya Vatikani na Nazi ya Ujerumani ulitiwa sahihi, Hitler alianzisha kampeni ya kuwaangamiza Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani. Kufikia 1935 waliharimishwa katika taifa lote. Lakini ni nani aliyeanzisha hayo?
Padri mmoja Mkatoliki, akiandika katika Der Deutsche Weg (gazeti la Kijerumani lililochapwa katika Lodz, Poland), alisema katika toleo lalo la Mei 29, 1938 hivi: “Sasa kuna nchi moja duniani ambako wale waitwao eti . . . Wanafunzi wa Biblia [Mashahidi wa Yehova] wameharimishwa. Hiyo ni Ujerumani! . . . Wakati Adolf Hitler alipochukua mamlaka, na Episkopati (Baraza la Maaskofu) ya Wakatoliki wa Ujerumani ikarudia ombi lao, Hitler alisema: ‘Hawa waitwao eti Wanafunzi wa Biblia Wenye Bidii [Mashahidi wa Yehova] ni wazusha-fujo; . . . Mimi ninawaona kuwa watu bandia; Mimi sivumilii kwamba Wakatoliki Wajerumani watashushiwa heshima kwa njia hiyo na huyu Mwamerika Jaji Rutherford; Ninaharimisha [Mashahidi wa Yehova] katika Ujerumani.’”—Italiki ni zetu.
Je, ilikuwa tu ni Baraza la Maaskofu Wakatoliki wa Ujerumani waliotaka hatua hizo zichukuliwe? Kama ilivyoripotiwa katika Oschatzer Gemeinnützige, la Aprili 21, 1933, katika hotuba ya redio Aprili 20, mhudumu Mluther Otto alihutubu kuhusu “ushirikiano wa karibu zaidi” kwa upande wa Kanisa la Luther la Ujerumani la Jimbo la Saxony pamoja na viongozi wa kisiasa wa taifa, na kisha yeye akajulisha hivi: “Matokeo ya kwanza ya ushirikiano huo tayari yaweza kuonwa katika kupigwa marufuku leo kwa International Association of Earnest Bible Students [Mashahidi wa Yehova] na madhehebu yalo katika Saxony.”
Baadaye, Serikali ya Nazi ilianzisha mojawapo minyanyaso ya Wakristo iliyo ya unyama zaidi katika historia iliyorekodiwa. Maelfu ya Mashahidi wa Yehova—kutoka Ujerumani, Austria, Poland, Chekoslovakia, Uholanzi, Ufaransa, na nchi nyinginezo—walitupwa ndani ya kambi za mateso. Humo waliteswa kwa ukatili na unyama mwingi uwezao kuwaziwa. Ilikuwa kawaida kwao kutukanwa na kupigwa mateke, kisha kulazimishwa kuupinda mwili kuanzia kwenye magoti, kuruka, na kutambaa kwa saa nyingi, hadi walipozirai au kuanguka kwa sababu ya uchovu, huku askari-walinzi wakiangua kicheko. Wengine walilazimishwa kusimama wakiwa uchi au wakiwa wamevaa nguo chache sana katika ua wakati wa kipupwe. Wengi walichapwa viboko hadi wakazimia na migongo yao ikajaa damu. Wengine walitumiwa kama violezo katika majaribio ya kitiba. Wengine waliangikwa juu kwa viwiko vyao, huku mikono yao ikiwa imefungwa nyuma yao. Ingawa walikuwa hoi kwa sababu ya njaa na walikuwa na nguo haba katika hali ya hewa yenye baridi sana, walilazimishwa kufanya kazi nzito, wakifanya kazi kwa saa nyingi, mara nyingi wakitumia mikono yao wenyewe wakati koleo na vifaa vingine vilipohitajiwa. Wanaume na wanawake pia walitendwa vivyo hivyo. Umri wao ulianzia utineja hadi miaka ya sabini. Watesi wao walipiga kelele za kumkaidi Yehova.
Katika jitihada za kuvunja roho ya Mashahidi, kamanda wa kambi katika Sachsenhausen aliagiza August Dickmann, Shahidi mchanga, auawe mbele ya wafungwa wote, Mashahidi wa Yehova wakiwa mbele kabisa ambapo wangeathirika zaidi na matokeo ya jambo hilo. Baada ya hilo, wafungwa wale wengine waliambiwa waondoke, lakini Mashahidi wa Yehova walipaswa wabaki. Kwa mkazo mwingi kamanda aliwauliza, ‘Ni nani sasa aliye tayari kutia sahihi taarifa?’—taarifa ya kukana imani ya mtu na kuonyesha utayari wa kuwa mwanajeshi. Hakuna mmoja wa wale Mashahidi 400 au zaidi aliyeitikia. Kisha wawili wakajitokeza mbele! La, si ili kutia sahihi, lakini ili kuomba kwamba sahihi zao zilizotolewa karibu mwaka mmoja hivi uliokuwa umepita ziweze kufutwa.
Katika kambi ya Buchenwald, mkazo uo huo ulitumiwa. Ofisa wa Nazi Rödl aliwaambia Mashahidi: “Yeyote kati yenu akikataa kupigana dhidi ya Ufaransa au Uingereza, nyote lazima mtakufa!” Vikosi viwili vyenye silaha vya polisi wa SS vilikuwa vikingoja kwenye lango la kambi. Hakuna Shahidi hata mmoja aliyekubali. Kutendwa kikatili kukafuata, lakini tisho la yule ofisa halikutekelezwa. Ikaja kujulikana waziwazi kwamba, ingawa Mashahidi katika kambi wangefanya karibu kila aina ya kazi waliyopewa, hata ingawa waliadhibiwa kwa kunyimwa chakula na kazi nyingi, bado wangekataa kwa dhati kufanya lolote lenye kuunga mkono vita au lolote lililoelekezwa dhidi ya mfungwa mwingine.
Ni vigumu sana kueleza mambo mabaya waliyopatwa nayo. Mamia yao walikufa. Baada ya waokokaji kuachiliwa kutoka kwenye kambi mwishoni mwa vita, Shahidi mmoja kutoka Flanders aliandika: “Ni tamaa isiyoyumbayumba ya kutaka kuishi, tumaini na itibari katika Yeye, Yehova, ambaye ni mwenye nguvu zote, na kupenda Ile Theokrasi, kulikofanya iwezekane kuvumilia yote hayo na kupata ushindi.—Warumi 8:37.”
Wazazi walitenganishwa bila huruma na watoto wao. Wenzi waliooana walitenganishwa, na wengine hawakupata kuonana tena. Muda mfupi baada ya kuoa, Martin Poetzinger alikamatwa na kupelekwa kwenye kambi yenye sifa mbaya ya Dachau, kisha katika Mauthausen. Mke wake, Gertrud, alifungwa katika Ravensbrück. Hawakuonana kwa miaka tisa. Akikumbuka mambo aliyoona katika Mauthausen, aliandika hivi baadaye: “Gestapo walijaribu kila njia ili kutushawishi tuvunje imani yetu katika Yehova. Kunyimwa chakula, urafiki wa hila, ukatili, kusimama siku baada ya siku katika fremu, kuangikwa juu ya nguzo ya meta 3 kwa viwiko vilivyozungushwa nyuma, kuchapwa viboko—yote hayo na mengine ya aibu sana kuweza kutajwa yaliweza kujaribiwa.” Lakini alibaki akiwa mwaminifu-mshikamanifu kwa Yehova. Yeye pia alikuwa miongoni mwa waokokaji, na baadaye alitumikia akiwa mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova.
Wafungwa kwa Sababu ya Imani Yao
Mashahidi wa Yehova hawakuwa katika kambi za mateso kwa sababu walikuwa wahalifu. Maofisa walipotaka mtu wa kuwanyoa, walimwamini Shahidi akiwa na kijembe, kwa sababu walijua kwamba hakuna Shahidi ambaye angetumia kifaa hicho kuwa silaha ili kumdhuru mwanadamu mwingine. Maofisa wa SS kwenye kambi ya maangamizo ya Auschwitz walipohitaji mtu wa kuwasafishia nyumba zao au kutunza watoto wao, walichagua Mashahidi, kwa sababu walijua hao hawangejaribu kuwapatia sumu au kujaribu kutoroka. Wakati kambi ya Sachsenhausen ilipokuwa ikihamwa mwishoni mwa ile vita, walinzi waliweka miongoni mwa kikundi cha Mashahidi kigari ambacho ndani yacho walikuwa na nyara waliyoteka. Kwa nini? Kwa sababu walijua kwamba Mashahidi hawangeiba mali yao.
Mashahidi wa Yehova walifungwa kwa sababu ya imani yao. Mara kwa mara waliahidiwa kwamba wangefunguliwa kutoka kambi ikiwa tu wangetia sahihi taarifa ya kukana imani zao. Polisi wa SS walifanya kila jambo waliloweza ili kuwashawishi au kuwalazimisha Mashahidi kutia sahihi taarifa kama hiyo. Hasa hilo ndilo walilotaka.
Mashahidi wote isipokuwa wachache, walithibitika kuwa wenye uaminifu-maadili usiovunjika. Lakini wao walifanya mengi zaidi ya kuteseka kwa sababu ya uaminifu-mshikamanifu wao kwa Yehova na ujitoaji wao kwa jina la Kristo. Walifanya zaidi ya kuvumilia mateso ya kupata habari kwao ambayo walikumbwa nayo. Walidumisha mahusiano yenye nguvu ya umoja wa kiroho.
Roho yao haikuwa ile ya wokovu wa kibinafsi kwa vyovyote vile. Walionyeshana upendo wa kujidhabihu. Wakati mmoja wao alipokuwa hoi, wengine wangeshiriki naye chakula chao kidogo. Waliponyimwa utibabu wote, walitunzana kwa upendo.
Habari ya funzo la Biblia iliwafikia Mashahidi kujapokuwa na jitihada zote za wanyanyasi wao kuizuia—zikiwa zimefichwa katika vifurushi vya zawadi kutoka nje, kwa maelezo ya wafungwa wapya, hata kwa kufichwa katika mguu wa mbao wa mfungwa mpya, au kwa njia nyinginezo walipokuwa katika migawo ya kazi nje ya kambi. Nakala zilipitishwa kutoka kwa mmoja hadi mwingine; nyakati nyingine zilirudufishwa kisiri kwenye mashine mlemle ndani ya ofisi za maofisa wa kambi. Hata mikutano mingine ya Kikristo ilifanywa ndani ya kambi, ingawa hatari kubwa ilihusika.
Mashahidi waliendelea tu kuhubiri kwamba Ufalme wa Mungu ndio tumaini pekee la wanadamu—na walifanya hivyo katika kambi za mateso! Katika Buchenwald, kwa sababu ya utendaji uliopangwa, maelfu ya wafungwa walisikia habari njema. Katika kambi ya Neuengamme, karibu Hamburg, kampeni ya kutoa ushahidi kwa kadiri kubwa ilipangwa kwa uangalifu na kufanywa mapema katika 1943. Kadi za kutoa ushuhuda zilitayarishwa katika lugha kadhaa zilizosemwa kambini. Jitihada zilifanywa ili kufikia kila mfungwa wa vita. Mipango ilifanywa kwa ajili ya funzo la Biblia la kibinafsi la kawaida pamoja na waliopendezwa. Mashahidi walikuwa na bidii sana katika kuhubiri kwao hivi kwamba baadhi ya wafungwa wa kisiasa walilalamika hivi: “Mahali popote uendapo, yote unayosikia ni habari kuhusu Yehova!” Wakati maagizo yalipokuja kutoka Berlin ya kuwatawanya Mashahidi miongoni mwa wafungwa wengine ili kuwadhoofisha, jambo hilo hasa lilifanya iwezekane kwao kutoa ushahidi kwa watu zaidi.
Kuhusu Mashahidi wa kike waaminifu 500 au zaidi katika Ravensbrück, mpwa wa kike wa Jenerali wa Ufaransa Charles de Gaulle aliandika hivi kufuatia kuachiliwa kwake: “Mimi ninawastaajabia kikweli. Walikuwa watu wa kutoka mataifa tofauti: Wajerumani, Wapoland, Warusi na Wacheki, na wamevumilia mateso makubwa sana kwa sababu ya imani zao. . . . Wote walionyesha ujasiri mkubwa sana na mtazamo wao ulifanya hatimaye hata S.S wawaheshimu. Wangaliweza kuachiliwa huru mara hiyo ikiwa wangalikana imani yao. Lakini, kinyume cha hayo, hawakuacha ukinzani wao, hata wakafaulu kuleta vitabu na trakti kambini.”
Kama Yesu Kristo, walijithibitisha wenyewe kuwa washindi wa ulimwengu uliotaka kuwafanya washikamane na mfinyango wao wa kishetani. (Yn. 16:33) Christine King, katika kitabu New Religious Movements: A Perspective for Understanding Society, asema hivi kuwahusu: “Mashahidi wa Yehova walitoa mwito wa ushindani dhidi ya wazo la mamlaka kamili la jamii mpya, na mwito huo wa ushindani, kutia na udumifu wayo, kwa wazi uliwasumbua wabuni wa utaratibu mpya. . . . Njia zilizokuwa zimetumiwa kwa muda mrefu za mnyanyaso, mateso, kufungwa gerezani na kudhihakiwa hazikuwafanya Mashahidi wageuke wawe na msimamo wa Nazi na kwa kweli zilikuwa zikipata matokeo ya kinyume dhidi ya wapinzani wao. . . . Kati ya pande hizo mbili zenye kudai uaminifu-mshikamanifu, pambano lilikuwa kali sana, tena sana, kwa sababu Wanazi hao wenye nguvu zaidi kimwili hawakuwa na uhakika sana katika mambo mengi, hawakuwa na msingi imara sana katika usadikisho wao, hawakuwa na uhakika sana juu ya kudumu kwa Enzi ya miaka 1,000. Mashahidi hawakuwa na shaka juu ya msingi wao, kwa sababu imani yao ilikuwa imekuwa dhahiri tangu wakati wa Abeli. Ingawa Wanazi walilazimika kugandamiza upinzani na kuwasadikisha wategemezaji wao, mara nyingi wakitumia usemi na maneno ya mfano ya Ukristo wa kimafarakano, Mashahidi walikuwa na uhakika juu ya uaminifu-mshikamanifu wa washiriki wao ulio kamili, na usiotikisika, hata kufikia kifo.”—Kilichapwa katika 1982.
Mwishoni mwa vita, Mashahidi zaidi ya elfu moja waliookoka walitoka kwenye kambi hizo, imani yao ikiwa imara na upendo wao kwa mmoja na mwenzake ukiwa wenye nguvu. Majeshi ya Warusi yalipokaribia, walinzi walihama Sachsenhausen upesi. Waliwakusanya wafungwa kulingana na taifa. Lakini Mashahidi wa Yehova walibaki pamoja wakiwa kikundi kimoja—230 kutoka kambi hiyo. Huku Warusi wakiwafuatia kwa karibu, walinzi wakaanza kuona wasiwasi. Hakukuwa chakula, na wafungwa walikuwa hoi; na bado, yeyote aliyebaki nyuma au akaanguka kwa sababu ya uchovu alipigwa risasi. Maelfu ya wale waliopigwa risasi kwa njia hiyo walitapanyika huku na huku katika njia waliyopitia. Lakini Mashahidi walisaidiana hivi kwamba hata wale walio hoi zaidi hawakubaki barabarani! Hata ingawa baadhi yao walikuwa na umri wa miaka kati ya 65 na 72. Wafungwa wengine walijaribu kuiba chakula njiani, na wengi walipigwa risasi wakijaribu kufanya hivyo. Kinyume cha hayo, Mashahidi wa Yehova walitumia fursa kuwaambia watu kwenye njia ya uhamiaji kuhusu makusudi yenye upendo ya Yehova, na baadhi yao, kwa sababu ya shukrani kwa ujumbe wenye kufariji, waliwaandalia chakula wao wenyewe na cha ndugu zao wa Kikristo.
Makasisi Waendelea Kupigana
Kufuatia Vita ya Ulimwengu 2, makasisi katika sehemu ya mashariki mwa Chekoslovakia waliendelea kuchochea mnyanyaso wa Mashahidi wa Yehova. Wakati wa kipindi cha kukaliwa na Wanazi, walikuwa wameshtaki kwamba Mashahidi walikuwa Wakomunisti; sasa walidai kwamba Mashahidi walipinga serikali ya Ukomunisti. Nyakati nyingine, wakati Mashahidi wa Yehova walipozuru nyumba za watu, mapadri walihimiza walimu wawaache mamia ya watoto waondoke shuleni ili wakawarushie Mashahidi mawe.
Vivyo hivyo, mapadri Wakatoliki katika Santa Ana, El Salvador, walifanya uchochezi dhidi ya Mashahidi katika 1947. Wakati ndugu walipokuwa na Funzo la Mnara wa Mlinzi la kila juma, wavulana walirusha mawe kupitia kwa mlango uliokuwa wazi. Kisha ukaja mwandamano ulioongozwa na mapadri. Wengine walibeba mianga; wengine walibeba mifano. “Bikira na aishi milele!” wakapaaza sauti. “Yehova na afe!” Kwa muda wa saa mbili hivi, jengo hilo lilipigwa kwa mawe.
Katika miaka ya katikati ya 1940, Mashahidi wa Yehova katika Quebec, Kanada, walitendwa vibaya sana pia, mikononi mwa magenge ya Wakatoliki na maofisa vilevile. Wajumbe kutoka jumba kuu la askofu walienda kila siku kwenye idara ya polisi ili kudai kwamba polisi wawaondolee mbali Mashahidi. Mara nyingi, kabla ya mtu kukamatwa, polisi walionwa wakitokea mlango wa nyuma wa kanisa. Katika 1949, wamishonari wa Mashahidi wa Yehova walifukuzwa kutoka Joliette, Quebec, na magenge ya Wakatoliki.
Lakini si watu wote katika Quebec waliokubaliana na yale yaliyokuwa yakifanywa. Leo, kuna Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova lililo zuri katika mojawapo barabara kuu katika Joliette. Ile iliyokuwa seminari ya huko ilifungwa, ikanunuliwa na serikali, na kugeuzwa kuwa chuo cha jumuiya. Na katika Montreal, Mashahidi wa Yehova wamefanya mikusanyiko mikubwa ya kimataifa, kukiwa na hudhurio kubwa kama 80,008 katika 1978.
Hata hivyo, Kanisa Katoliki limetumia kila njia iwezekanayo ili kudumisha udhibiti imara wa watu. Kwa kuwakaza maofisa wa serikali, walihakikisha kwamba wamishonari Mashahidi waliamriwa waondoke Italia mwaka 1949 na kwamba, ilipowezekana, ruhusa zilizopatikana na Mashahidi kwa ajili ya makusanyiko huko zilifutwa wakati wa miaka ya 1950. Kujapokuwa hayo, idadi ya Mashahidi wa Yehova iliendelea kukua, na kufikia 1992 kulikuwa na Mashahidi waeneza-evanjeli zaidi ya 190,000 katika Italia.
Kama vile katika wakati wa Baraza la Kuwahukumu Wazushi wa Kidini, makasisi katika Hispania walishutumu kisha wakaachia Serikali iwashtaki Mashahidi. Kwa kielelezo, katika Barcelona, ambako askofu mkuu alianzisha kampeni dhidi ya Mashahidi katika 1954, makasisi walitumia mimbari zao pamoja na shule na redio ili kuwashauri watu kwamba wakati Mashahidi watakapowazuru, wanapaswa kuwaalika ndani—kisha kuwaita polisi upesi.
Mapadri walihofu kwamba labda Wahispania wangejifunza yale yaliyokuwa katika Biblia na hata wawaonyeshe wengine yale waliyokuwa wameona. Wakati Manuel Mula Giménez alipofungwa katika Granada katika 1960 kwa ajili ya “uhalifu” wa kuwafunza wengine Biblia, mhubiri wa gereza (padri Mkatoliki) aliondoa ile iliyokuwa Biblia pekee katika maktaba ya gereza. Na wakati mfungwa mwingine alipomwazima Manuel nakala ya Gospeli, hiyo ilitwaliwa. Lakini Biblia sasa imefikia watu wa kawaida katika Hispania, wamekuwa na fursa ya kujionea wenyewe yale inayosema, na kufikia 1992, kulikuwa na zaidi ya watu 90,000 waliokuwa wameanza kuabudu Yehova wakiwa Mashahidi wake.
Katika Jamhuri ya Dominika, makasisi walishirikiana na Dikteta Trujillo, wakimtumia ili kutimiza malengo yao kwa jinsi ileile aliyowatumia kutimiza makusudi yake. Katika 1950, baada ya makala za magazeti zilizoandikwa na mapadri kuwashutumu Mashahidi wa Yehova, mwangalizi wa tawi la Watch Tower Society aliitwa na Katibu wa Mambo ya Ndani na Polisi. Alipokuwa akingoja nje ya ofisi, mwangalizi wa tawi aliona mapadri wawili Wayesuiti wakiingia na kisha kuondoka. Mara tu baada ya hiyo, aliitwa ndani katika ofisi ya yule Katibu, na huyo Katibu akasoma kwa wasiwasi sheria iliyopiga marufuku utendaji wa Mashahidi wa Yehova. Baada ya marufuku kuondolewa kifupi katika 1956, makasisi walitumia redio na magazeti pia katika uchongezi mpya dhidi ya Mashahidi. Makutaniko mazimamazima yalikamatwa na kuagizwa kutia sahihi taarifa ya kukana imani yao na kuahidi kurudi kwenye Kanisa la Katoliki ya Roma. Mashahidi walipokataa, walipigwa, wakapigwa kwa mateke, wakapigwa kwa viboko, na nyuso zao zikapondwa kwa matako ya bunduki. Lakini walisimama imara, na idadi zao zikaongezeka.
Katika Sucre, Bolivia, kulikuwa na jeuri zaidi. Katika wakati wa kusanyiko la Mashahidi wa Yehova katika 1955, genge la wavulana kutoka Shule ya Katoliki ya Sacred Heart walizunguka mahali pa kusanyiko, wakapiga kelele, na kutupa mawe. Kutoka jengo la kanisa lililo upande ule mwingine wa barabara, kipaza sauti chenye nguvu kilihimiza Wakatoliki wote walinde kanisa lao na “Bikira” dhidi ya “washupavu Waprotestanti.” Askofu mkuu na mapadri walijaribu binafsi kuvunja mkutano huo lakini waliamriwa na polisi waondoke katika jumba hilo.
Mwaka uliotangulia, wakati Mashahidi wa Yehova walipokuwa na kusanyiko jijini Riobamba, Ekuado, programu yao ilikuwa na hotuba ya watu wote yenye kichwa “Upendo, Unatumika Katika Ulimwengu Wenye Ubinafsi?” Lakini padri Myesuiti alikuwa amechochea Wakatoliki, akiwahimiza wazuie mkutano huo usifanyike. Hivyo, hotuba hiyo ilipoanza, genge lingeweza kusikika likipiga kelele: “Kanisa Katoliki na liishi milele!” na, “Waprotestanti chini!” Kwa shukrani polisi waliwazuia, panga zao zikiwa zimechomolewa. Lakini genge hilo lilitupa mawe katika sehemu ya mkutano na, baadaye, kwenye jengo ambamo wamishonari waliishi.
Makasisi wa Katoliki ya Roma wamekuwa katika mstari wa mbele wa mnyanyaso, lakini si hao tu. Makasisi wa Orthodoksi ya Ugiriki wamekuwa wakali vivyo hivyo na wametumia mbinu zilezile katika eneo lao ndogo zaidi wanaloongoza. Kwa kuongezea, makasisi wengi Waprotestanti wameonyesha roho iyo hiyo mahali walipohisi kwamba wangeweza kuionyesha. Kwa kielelezo, katika Indonesia wameongoza magenge yaliyovunja mafunzo ya Biblia katika nyumba za faragha na ambayo yalipiga kikatili wale Mashahidi wa Yehova waliokuwapo. Katika baadhi ya nchi za Afrika, wamejaribu kuwavuta maofisa wawafukuze Mashahidi wa Yehova kutoka nchi hizo au kuwanyima uhuru wa kuzungumza juu ya Neno la Mungu kwa wengine. Ingawa huenda makasisi Wakatoliki na Waprotestanti wakatofautiana katika mambo mengine, wao wanakubaliana katika kuwapinga Mashahidi wa Yehova. Pindi nyingine hata wameungana pamoja ili kujaribu kuvuta maofisa wa serikali wakomeshe utendaji wa Mashahidi. Mahali ambako dini zisizo za Kikristo ndizo zimemiliki maisha, mara nyingi wao pia wametumia serikali ili kuzuia watu wao wasipate kujua mafundisho yanayoweza kuwafanya waulize maswali juu ya dini za uzawa wao.
Nyakati nyingine, vikundi hivyo visivyo vya Kikristo vimeungana na wale wanaodai kuwa Wakristo katika kupanga kudumisha hali ya kidini iliyoko. Katika Dekin, nchini Dahomey (sasa Benin), mganga mmoja mkuu na padri Mkatoliki walishauriana pamoja kuwafanya maofisa wakandamize utendaji wa Mashahidi wa Yehova mapema katika miaka ya 1950. Katika jitihada zao walitunga mashtaka bandia yaliyokusudiwa kuzusha aina zote za hisiamoyo za uhasama. Walishtaki kwamba Mashahidi walikuwa wakiwahimiza watu waasi dhidi ya serikali, hawakuwa wakilipa kodi, walisababisha waganga wasilete mvua, na walisababisha kule kukosa kufanikiwa kwa maombi ya padri. Viongozi hao wote wa kidini walihofu kwamba labda watu wao wangejifunza mambo ambayo yangewaweka huru na imani za kishirikina na maisha ya utii bila kupata sababu.
Hata hivyo, hatua kwa hatua, uvutano wa makasisi umefifia katika sehemu nyingi. Sasa makasisi hawapati kwamba wakati wote polisi wanawaunga mkono wanapowasumbua Mashahidi. Wakati padri wa Orthodoksi ya Ugiriki alipojaribu kuvunja kusanyiko la Mashahidi wa Yehova kwa kutumia jeuri ya genge katika Larissa, Ugiriki, mwaka 1986, wakili wa wilaya pamoja na kikosi kikubwa cha polisi aliingilia kwa niaba ya Mashahidi hao. Na nyakati nyingine magazeti yamekuwa wazi sana katika kushutumu matendo ya kukosa uvumilio wa kidini.
Hata hivyo, katika sehemu nyingi za ulimwengu, masuala mengine yameleta mawimbi ya mnyanyaso. Mojawapo masuala hayo limehusisha mtazamo wa Mashahidi wa Yehova kuelekea mifano ya kitaifa.
Kwa Sababu Wanaabudu Yehova Pekee
Katika nyakati za kisasa ilikuwa kwanza katika Ujerumani wa Nazi kwamba Mashahidi wa Yehova walikabiliwa kwa njia ya kutokeza na masuala yaliyohusu sherehe za kitaifa. Hitler alijaribu kupanga kijeshi taifa la Ujerumani kwa kufanya salamu ya Kinazi “Heil Hitler!” iwe ya lazima. Kama ilivyoripotiwa na mwandikaji safu za magazeti Msweden na mtangazaji wa BBC Björn Hallström, wakati Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani walipokamatwa wakati wa enzi ya Wanazi, mashtaka yaliyofanywa dhidi yao mara nyingi yalitia ndani “kukataa kusalimu bendera na kutoa salamu ya Nazi.” Upesi mataifa mengine yakaanza kudai kwamba kila mtu asalimu bendera yayo. Mashahidi wa Yehova walikataa—si kwa sababu ya kutokuwa waaminifu lakini kwa sababu ya dhamiri ya Kikristo. Wanaheshimu bendera lakini huona kule kusalimu bendera kuwa ni kitendo cha ibada.f
Baada ya Mashahidi kama 1,200 kufungwa katika Ujerumani mapema katika enzi ya Nazi kwa kukataa kutoa salamu ya Nazi na kukataa kuvunja kutokuwamo kwao kwa Kikristo, maelfu walitendwa vibaya kimwili katika Marekani kwa sababu walikataa kusalimu bendera ya Amerika. Wakati wa juma la Novemba 4, 1935, idadi fulani ya watoto wa shule katika Canonsburg, Pennsylvania, walipelekwa kwenye chumba cha kuchemshia maji na kuchapwa viboko kwa kukataa kusalimu bendera. Grace Estep, aliyekuwa mwalimu, aliachishwa wadhifa wake katika shule hiyo kwa sababu iyo hiyo. Mnamo Novemba 6, William na Lillian Gobitas walikataa kusalimu bendera na wakafukuzwa shuleni katika Minersville, Pennsylvania. Baba yao alipeleka mashtaka mahakamani ili watoto wake waruhusiwe kwenda shuleni. Mahakama ya wilaya ya jimbo na mahakama ya mzunguko ya rufani pia ziliamua kesi kwa kuwapendelea Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, katika 1940, huku taifa likikaribia kuingia vitani, Mahakama Kuu ya Marekani, katika Minersville School District v. Gobitis, iliunga mkono sharti la kusalimu bendera kwa shule zote za umma, kwa uamuzi wa 8 kwa 1. Hiyo iliongoza kwenye jeuri ya taifa lote dhidi ya Mashahidi wa Yehova.
Kulikuwa na mashambulizi mengi sana ya jeuri dhidi ya Mashahidi wa Yehova hivi kwamba Bi. Eleanor Roosevelt (mke wa Rais F. D. Roosevelt) alisihi umma uache jeuri hiyo. Mnamo Juni 16, 1940, msaidizi wa wakili mkuu wa Marekani, Francis Biddle, katika matangazo ya redio ya kutoka pwani moja hadi ile nyingine, alirejezea kihususa maovu waliyotendwa Mashahidi na akasema kwamba hayo hayangevumiliwa. Lakini hilo halikukomesha maovu hayo.
Katika kila hali inayoweza kuwaziwa—barabarani, mahali pa kazi, Mashahidi walipozuru nyumba katika huduma yao—bendera ziliwekwa mbele yao, kwa dai kwamba wazisalimu—au sivyo wangekiona! Mwishoni mwa 1940, Kitabu-Mwaka cha Mashahidi wa Yehova kiliripoti: “Viongozi wa kidini na Jeshi la Amerika, kupitia magenge kama hayo yanayotenda bila kujali sheria, walileta uharibifu mkubwa wa jeuri. Mashahidi wa Yehova wametendwa vibaya, wakapigwa, wakatekwa nyara, wakafukuzwa katika miji, wilaya na majimbo, wakamwagiwa lami na manyoya, wakalazimishwa kunywa mafuta ya mbarika, wakafungwa pamoja na kukimbizwa barabarani kama hayawani wapumbavu, wakahasiwa na kulemazwa, wakaudhiwa na kutukanwa na umati wa kiibilisi, wakafungwa kwa mamia bila mashtaka na kufungwa bila njia ya kuwasiliana na wengine na kunyimwa pendeleo la kuwasiliana na watu wa ukoo, marafiki au mawakili. Mamia yao wengine wamefungwa gerezani na kuwekwa katika kile kiitwacho eti ‘kifungo cha ulinzi’; wengine wamepigwa risasi usiku; wengine wakatishwa kunyongwa na kupigwa hadi wakazimia. Namna mbalimbali ya jeuri ya magenge imetukia. Wengi wameraruliwa nguo zao, Biblia zao na fasihi nyinginezo zikatwaliwa na kuchomwa hadharani; magari yao, nyumba za trela, makao yao na sehemu za kusanyiko zikaharibiwa na kuchomwa . . . Katika visa vingi ambavyo kesi zimefanywa katika jumuiya zinazoongozwa na magenge, mawakili pamoja na mashahidi wamezingirwa na umati na kupigwa wanapoenda mahakamani. Katika karibu kila kisa ambako kumekuwa na jeuri ya magenge maofisa wa umma hawakufanya lolote na walikataa kutoa ulinzi, na katika visa kadhaa polisi wameshiriki katika magenge hayo na nyakati nyingine hata kuongoza magenge hasa.” Kuanzia 1940 hadi 1944, magenge zaidi ya 2,500 yenye jeuri yaliwadhulumu Mashahidi wa Yehova katika Marekani.
Kwa sababu watoto wengi wa Mashahidi wa Yehova walifukuzwa shuleni, kwa muda fulani wakati wa miaka ya mwishoni mwa 1930 na mapema miaka ya 1940 ilihitajika kwamba wao waendeshe shule zao wenyewe katika Marekani na Kanada ili kuandaa elimu kwa watoto wao. Hizo ziliitwa Shule za Ufalme.
Nchi nyinginezo pia zimewanyanyasa Mashahidi kikatili kwa sababu ya kukataa kusalimu au kubusu mifano ya kitaifa. Katika 1959 nchini Kosta Rika, watoto wa Mashahidi wa Yehova ambao hawangeshiriki katika ile ambayo sheria hueleza kuwa ‘ibada ya Mifano ya Kitaifa’ walizuiwa kwenda shule. Katika 1984, watoto Mashahidi walitendwa vivyo hivyo katika Paraguay. Katika 1959, Mahakama Kuu ya Filipino iliamua kwamba, kujapokuwa vipingamizi vya kidini, watoto wa Mashahidi wa Yehova wangelazimishwa kusalimu bendera. Hata hivyo, katika pindi nyingi, wasimamizi wa shule huko walishirikiana na Mashahidi hivi kwamba watoto wao wangeweza kuhudhuria shule bila kutenda kinyume cha dhamiri zao. Katika Liberia, Afrika Magharibi, maofisa waliwashtaki Mashahidi mwaka 1963 kwa kutokuwa waaminifu kwa Serikali; walivunja kwa nguvu kusanyiko la Mashahidi katika Gbarnga na kudai kwamba kila mtu aliyekuwapo—Waliberia na wageni—waape ushikamanifu kwa bendera ya taifa. Katika 1976 ripoti yenye kichwa “Mashahidi wa Yehova Katika Kuba” ilisema kwamba katika miaka miwili iliyokuwa imepita, wazazi elfu moja, wanaume kwa wanawake, walikuwa wamepelekwa gerezani kwa sababu watoto wao hawangesalimu bendera.
Si kila mtu amekubaliana na hatua hizo za uonevu dhidi ya watu ambao, kwa sababu ya dhamiri, hujizuia kwa staha kushiriki katika sherehe za uzalendo. The Open Forum, kilichochapishwa na Tawi la California Kusini la Shirika la Haki za Umma la Marekani, kilisema hivi katika 1941: “Wakati umefika wa sisi kutumia akili kuhusu jambo hili la kusalimu bendera. Mashahidi wa Yehova si Waamerika wasio waaminifu. . . . Wao si wavunja sheria kwa ujumla, bali huishi maisha yanayofaa, na yenye utaratibu, wakishiriki sehemu yao katika mambo yanayowafaa wote.” Katika 1976 mwandikaji safu za magazeti katika Argentina, katika Herald ya Buenos Aires, alionelea waziwazi kwamba “itikadi [za Mashahidi] ni zenye kuudhi kwa wale tu wanaofikiria kuwa uzalendo ni jambo hasa la kupeperusha bendera na kuimba wimbo wa taifa, na si jambo la moyoni.” Yeye aliongeza: “Hitler na Stalin waliwaona [Mashahidi] kuwa wasiovumilika, na kuwatenda vibaya sana. Madikteta wengine wengi wakitamani kuwafanya waridhiane wamejaribu kuwakandamiza. Na wameshindwa.”
Inajulikana vema kwamba baadhi ya vikundi vya kidini vimeunga mkono jeuri ya kutumia silaha dhidi ya serikali walizokataa. Lakini hakuna mahali popote duniani ambapo Mashahidi wa Yehova wameshiriki katika mapinduzi ya kisiasa. Si kwa sababu ya kutokuwa washikamanifu—kwa sababu ya kuunga mkono serikali nyingine ya kibinadamu—kwamba wanakataa kusalimu mfano wa kitaifa. Wanachukua msimamo uleule katika kila nchi ambako wanapatikana. Mtazamo wao si wa kutokuwa na staha. Hawapigi mbinja au kelele ili kuvunja sherehe za uzalendo; hawatemei mate bendera, hawaikanyagii chini, au kuichoma. Si wapinga-serikali. Msimamo wao unategemea yale ambayo Yesu Kristo mwenyewe alisema, kama ilivyorekodiwa kwenye Mathayo 4:10 (NW): “Ni Yehova Mungu wako ambaye lazima uabudu, na ni kwake peke yake lazima utoe utumishi mtakatifu.”
Msimamo unaochukuliwa na Mashahidi wa Yehova ni kama ule uliochukuliwa na Wakristo wa mapema katika siku za Milki ya Roma. Kuhusu Wakristo hao wa mapema, kitabu Essentials of Bible History kinasema: “Tendo la kuabudu maliki lilitia ndani kunyunyiza punje chache za uvumba au matone machache ya divai juu ya madhabahu iliyosimama mbele ya mfano wa maliki. Labda kwa sababu ya muda mrefu ambao umepita tangu wakati huo hatuoni tofauti ya tendo hilo katika . . . kuinua mkono ili kusalimu bendera au mtawala fulani mashuhuri wa serikali, kuwa wonyesho wa staha, heshima, na uzalendo. Yawezekana kwamba watu wengi katika karne ya kwanza waliliona kwa njia iyo hiyo lakini sivyo walivyoliona Wakristo. Wao waliliona jambo hilo lote kuwa ni ibada ya kidini, kumkiri maliki kuwa mungu na hivyo wakose kuwa waaminifu-washikamanifu kwa Mungu na Kristo, nao walikataa kufanya hivyo.”—Elmer W. K. Mould, 1951, uku. 563.
Wachukiwa kwa Sababu “Wao Si Sehemu ya Ulimwengu”
Kwa sababu Yesu alisema kwamba wanafunzi wake hawangekuwa “sehemu ya ulimwengu,” Mashahidi wa Yehova hawashiriki katika mambo yao ya kisiasa. (Yn. 17:16; 6:15, NW) Katika hilo pia, wao ni kama Wakristo wa mapema, ambao kuwahusu wanahistoria husema:
“Ukristo wa mapema haukueleweka sana na haukupendelewa sana na wale waliotawala ulimwengu wa kipagani. . . . Wakristo walikataa kushiriki katika kazi fulani za raia wa Roma. . . . Hawangekuwa na cheo cha kisiasa.” (On the Road to Civilization—A World History, A. K. Heckel na J. G. Sigman, 1937, kur. 237-238) “Walikataa kushiriki sehemu yoyote ya utendaji katika usimamizi wa raia au kulinda milki hiyo kijeshi. . . . Haingewezekana kwamba Wakristo wangefanya kazi ya askari-jeshi, ya hakimu, au ya kuwa wakuu, na bado wawe hawakukana wajibu fulani mtakatifu zaidi.”—History of Christianity, Edward Gibbon, 1891, kur. 162-163.
Msimamo huo haupendelewi na ulimwengu, hasa katika nchi ambako watawala wanataka kwamba kila mtu ashiriki katika utendaji fulani mbalimbali ili kudhihirisha utegemezo wao wa mfumo huo wa kisiasa. Matokeo ni kama vile Yesu alivyosema: “Kama mngekuwa sehemu ya ulimwengu, ulimwengu ungependa sana kilicho chao wenyewe. Sasa kwa sababu nyinyi si sehemu ya ulimwengu, bali nimewachagua nyinyi kutoka ulimwenguni, kwa ajili ya hili ulimwengu huwachukia nyinyi.”—Yn. 15:19, NW.
Katika nchi nyinginezo, kupiga kura katika uchaguzi wa kisiasa huonwa kuwa jambo la lazima. Adhabu ya kukosa kupiga kura ni kutozwa faini, kufungwa, au mabaya zaidi. Lakini Mashahidi wa Yehova huunga mkono Ufalme wa Mungu wa Kimesiya, ambao, kama vile Yesu alivyosema, “si sehemu ya ulimwengu.” Kwa hiyo, hawashiriki katika mambo ya kisiasa ya mataifa ya ulimwengu huu. (Yn. 18:36, NW) Uamuzi ni wa mtu binafsi; hawamlazimishi mtu awe na maoni yao. Mahali ambako uvumilio wa kidini unakosekana, maofisa wa serikali wametumia kule kutoshiriki kwa Mashahidi kuwa kisingizio cha mnyanyaso wa ukatili. Kwa kielelezo, wakati wa enzi ya Wanazi, jambo hili lilifanywa katika nchi zilizodhibitiwa nao. Limefanywa pia katika Kuba. Hata hivyo, maofisa katika nchi nyingi wamekuwa na uvumilio zaidi.
Na bado, katika sehemu nyinginezo wale walio mamlakani wamedai kwamba kila mtu aonyeshe kwamba anaunga mkono chama cha kisiasa kinachotawala kwa kupaaza sauti shime fulani. Kwa sababu hawangeweza kufanya hivyo kwa kudhamiria, maelfu ya Mashahidi wa Yehova katika sehemu za mashariki mwa Afrika wamepigwa, hali yao ya maisha ikabadilishwa, na wakafukuzwa kutoka makao yao wakati wa miaka ya 1970 na 1980. Lakini Mashahidi wa Yehova katika nchi zote, ingawa ni wenye bidii na wenye kufuata sheria, ni Wakristo wasiokuwemo kuhusiana na masuala ya kisiasa.
Katika Malawi, kuna chama kimoja tu cha kisiasa, na mtu huonyesha kwamba ni mwanachama akiwa na kadi ya chama. Ingawa Mashahidi ni kielelezo kizuri katika kulipa kodi zao, wao hawanunui kadi za chama cha kisiasa, kwa kupatana na itikadi zao za kidini. Kufanya hivyo kungekuwa ni kukana imani yao katika Ufalme wa Mungu. Kwa sababu hiyo, mwishoni mwa mwaka 1967, kwa kuchochewa na maofisa wa serikali, magenge ya vijana kotekote Malawi yalianzisha mashambulizi makali sana dhidi ya Mashahidi wa Yehova ambayo hayakuwa yamepata kutukia namna yayo katika ukatili wa kunyarafisha na wa unyama. Wanawake Wakristo wenye kujitoa kama zaidi ya elfu moja walinajisiwa. Baadhi yao walivuliwa nguo mbele ya magenge makubwa, wakachapwa kwa vijiti na makonde, na kisha wakatendwa vibaya kingono na mtu mmoja baada ya mwingine. Misumari ilipigiliwa chini ya miguu ya wanaume na tindi za baiskeli zikapitishiwa ndani ya miguu yao, na kisha wakaamriwa wakimbie. Kotekote nchini makao yao, fanicha, nguo, na ugavi wa chakula viliharibiwa.
Kwa mara nyingine, katika 1972, kulitokea ukatili kama huo kufuatia mkusanyiko wa kila mwaka wa Chama cha Congress cha Malawi. Kwenye mkusanyiko huo iliamuliwa rasmi kuwanyima ajira Mashahidi wa Yehova na kuwafukuza kutoka nyumbani mwao. Hata maombi ya waajiri ili kuendelea kuwa na wafanyakazi hao wanaotumainiwa hayakufanikiwa. Nyumba, mimea, na wanyama wa kufugwa walitwaliwa au kuharibiwa. Mashahidi walizuiwa kuteka maji kutoka kisima cha kijiji. Idadi kubwa yao walipigwa, wakanajisiwa, wakalemazwa, au kuuawa kimakusudi. Wakati huohuo, walichekwa na kudhihakiwa kwa ajili ya imani yao. Zaidi ya 34,000 yao hatimaye walikimbia nchi hiyo ili kuepuka kuuawa.
Lakini mambo yalikuwa hayajakwisha. Kwanza kutoka nchi moja kisha katika nyingine, walilazimishwa kurudi kwao kuingia mikononi mwa watesi wao, ambako walitendwa ukatili zaidi. Na bado, kujapokuwa hayo yote, hawakuridhiana, na hawakuacha imani yao katika Yehova Mungu. Walithibitika kuwa kama wale watumishi waaminifu wa Mungu ambao kuwahusu Biblia husema: “Wengine walipokea jaribu lao kwa dhihaka na mapigo kwa mijeledi, kwa kweli, zaidi ya hilo, kwa vifungo na magereza. Walipigwa kwa mawe, walijaribiwa, walikatwa vipande-vipande kwa msumeno, walikufa kwa kuchinjwa kwa upanga, walienda wakizunguka huku na huku katika ngozi za kondoo, katika ngozi za mbuzi, huku wakiwa katika uhitaji, katika dhiki, chini ya kutendwa vibaya; na ulimwengu haukuwafaa.”—Ebr. 11:36-38, NW.
Wanyanyaswa Katika Mataifa Yote
Je, ni mataifa machache tu ya ulimwengu kwa kadiri fulani ambayo yameonyesha unafiki wao wa uhuru kwa mnyanyaso huo wa kidini? La sivyo! Yesu Kristo alionya wafuasi wake: “Nanyi mtakuwa vitu vya kuchukiwa na mataifa yote kwa sababu ya jina langu.”—Mt. 24:9, NW.
Wakati wa siku za mwisho za huu mfumo wa mambo, tangu 1914, chuki hiyo imeongezeka sana hasa. Kanada na Marekani ziliongoza ushambulizi huo kwa kupiga marufuku fasihi za Biblia wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, na upesi India na Nyasaland (sasa ni Malawi) zikajiunga nazo. Wakati wa miaka ya 1920, Wanafunzi wa Biblia katika Ugiriki, Hungaria, Italia, Rumania, na Hispania waliwekewa vizuizi visivyo na sababu nzuri. Katika sehemu nyinginezo, ugawanyaji wa fasihi za Biblia ulikatazwa; nyakati nyingine, hata mikutano ya faragha ilikatazwa. Nchi zaidi zilijiunga katika mashambulizi hayo wakati wa miaka ya 1930, wakati marufuku (mengine juu ya Mashahidi wa Yehova, mengine juu ya fasihi) yalipowekwa katika Albania, Austria, Bulgaria, Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, wilaya fulani za Uswisi, ile iliyokuwa wakati huo Yugoslavia, na Gold Coast (sasa ni Ghana), maeneo ya Ufaransa barani Afrika, Trinidad, na Fiji.
Katika sehemu nyingi za ulimwengu, wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku, kutia na huduma yao ya hadharani, na fasihi zao za Biblia. Mambo yalikuwa hivyo si katika Ujerumani tu, Italia, na Japani—ambazo zilikuwa chini ya utawala wa dikteta—bali pia katika nchi nyingi zilizokaliwa nazo moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kabla ya au wakati wa vita hiyo. Zilizotiwa ndani ya hizo ni Albania, Austria, Chekoslovakia, Indies Mashariki ya Uholanzi (sasa ni Indonesia), Korea, Norway, Ubelgiji, na Uholanzi. Wakati wa miaka hiyo ya vita, Argentina, Brazili, Finland, Hungaria, na Ufaransa zilitoa amri rasmi dhidi ya Mashahidi wa Yehova au utendaji wao.
Uingereza haikuharimisha moja kwa moja utendaji wa Mashahidi wa Yehova wakati wa vita, lakini ilifukuza mwangalizi wa tawi mzaliwa wa Amerika wa Watch Tower Society na ikajaribu kukatiza utendaji wa Mashahidi kwa kuweka kizuizi cha wakati wa vita juu ya safirisho la fasihi zao za Biblia. Kotekote katika Milki ya Uingereza na Jumuiya ya Madola ya Uingereza, marufuku kamili juu ya Mashahidi wa Yehova au vizuizi vya fasihi zao viliwekwa. Afrika Kusini, Australia, Bahamas, Basutoland (sasa ni Lesotho), Bechuanaland (sasa ni Botswana), Burma (sasa ni Myanmar), Ceylon (sasa ni Sri Lanka), Dominika, Fiji, Gold Coast (sasa ni Ghana), Guiana ya Uingereza (sasa ni Guyana), India, Jamaika, Kanada, New Zealand, Nigeria, Nyasaland (sasa ni Malawi), Rhodesia Kaskazini (sasa ni Zambia), Rhodesia Kusini (sasa ni Zimbabwe), Saiprasi, Singapore, Swaziland, na Visiwa vya Leeward (B.W.I.) zote zilichukua hatua hizo ili kuonyesha uhasama dhidi ya watumishi wa Yehova.
Baada ya vita kwisha, mnyanyaso ulipungua kutoka kwa vikundi fulani vya watu lakini ukaongezeka kutoka kwa vingine. Wakati wa miaka 45 iliyofuata, kwa kuongezea uhakika wa kwamba Mashahidi wa Yehova walikataliwa kutambuliwa kisheria katika nchi nyingi, marufuku kamili iliwekwa juu yao au utendaji wao katika nchi 23 barani Afrika, 9 barani Asia, 8 barani Ulaya, 3 barani Amerika ya Latin, na 4 katika mataifa fulani ya visiwa. Kufikia 1992, Mashahidi wa Yehova walikuwa wangali chini ya vizuizi katika nchi 24.
Hiyo haimaanishi kwamba maofisa wote wa serikali hupinga kibinafsi kazi ya Mashahidi wa Yehova. Maofisa wengi hupendelea uhuru wa kidini na hutambua kwamba Mashahidi ni tunu kwa jumuiya. Watu hao hawakubaliani na wale wanaochochea kuchukuliwa kwa hatua rasmi dhidi ya Mashahidi. Kwa kielelezo, kabla ya Ivory Coast (sasa ni Côte d’Ivoire) kuwa taifa huru, wakati padri Mkatoliki na mhudumu Mmethodisti walipojaribu kuwakaza maofisa wawafukuze Mashahidi wa Yehova nje ya nchi, walipata kwamba walikuwa wakisema na maofisa ambao hawakutaka kuwa vibaraka vya makasisi. Katika 1990, wakati ofisa mmoja alipojaribu kubadilisha sheria katika Namibia, ili kuwaonea wakimbizi waliojulikana kuwa Mashahidi wa Yehova, Bunge halikukubali. Na katika nchi nyingi ambako wakati mmoja Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku, sasa wanafurahia utambulisho wa kisheria.
Na bado, katika njia mbalimbali, katika kila sehemu ya dunia, Mashahidi wa Yehova hunyanyaswa. (2 Tim. 3:12) Katika maeneo mengine, mnyanyaso huo huenda ukaletwa na wenye nyumba wenye kutukana, watu wa ukoo wenye kupinga, au wafanyakazi wenzi au wanadarasa wenzi wasioonyesha hofu yoyote kwa Mungu. Hata hivyo, bila kujali wanyanyasi ni akina nani au jinsi wanavyojaribu kutetea yale wanayofanya, Mashahidi wa Yehova wanajua kile hasa kinachochochea mnyanyaso wa Wakristo wa kweli.
Lile Suala
Vichapo vya Watch Tower vimetaja kwa muda mrefu kwamba katika usemi wa ufananisho kitabu cha kwanza cha Biblia kilitabiri juu ya uadui, au chuki, ya Shetani Ibilisi na wale walio chini ya udhibiti wake kuelekea tengenezo la kimbingu la Yehova na wawakilishi walo wa kidunia. (Mwa. 3:15; Yn. 8:38, 44; Ufu. 12:9, 17) Hasa tangu 1925, The Watch Tower limeonyesha kwa Maandiko kwamba kuna matengenezo mawili tu makuu—la Yehova na la Shetani. Na, kama vile 1 Yohana 5:19 (NW), inavyosema, “ulimwengu mzima”—yaani, wanadamu wote walio nje ya tengenezo la Yehova—“unakaa katika nguvu ya mwovu.” Hiyo ndiyo sababu ifanyayo Wakristo wote wa kweli wanyanyaswe.—Yn. 15:20.
Lakini mbona Mungu huruhusu hayo? Je, jambo lolote jema linatimizwa? Yesu Kristo alieleza kwamba kabla yeye akiwa Mfalme wa kimbingu hajaangamiza Shetani na tengenezo lake ovu, watu wangepewa fursa ya kusikia juu ya Ufalme wa Mungu na kuchukua msimamo wao upande wa Ufalme. Wapiga-Mbiu wa Ufalme huo wanaponyanyaswa, swali hili hukaziwa hata zaidi: Je, wale wanaosikia kuuhusu watafanya mema kwa “ndugu” za Kristo na washiriki wao na hivyo kumpenda Kristo mwenyewe? Au watajiunga na wale wanaorundika mabaya juu ya wawakilishi hao wa Ufalme wa Mungu—au labda wataendelea kunyamaza wengine wanapofanya hivyo? (Mt. 25:31-46; 10:40; 24:14) Wengine nchini Malawi waliona wazi ni nani waliokuwa wakimtumikia Mungu wa kweli na hivyo wakajiunga na Mashahidi walionyanyaswa. Wafungwa wengi pamoja na walinzi katika kambi za mateso za Ujerumani walifanya vivyo hivyo.
Hata ingawa mashtaka ya uwongo hufanywa dhidi yao na wao hutendwa vibaya kimwili, hata kusutwa kwa ajili ya imani yao kwa Mungu, Mashahidi wa Yehova hawahisi kuwa wameachwa na Mungu. Wanajua kwamba Yesu Kristo alipata mambo ayo hayo. (Mt. 27:43) Wanajua pia kwamba kwa uaminifu-mshikamanifu wake kwa Yehova, Yesu alimthibitisha Ibilisi kuwa mwongo na akaleta utukuzo juu ya jina la Baba yake. Ni tamaa ya kila Shahidi wa Yehova kufanya vivyo hivyo.—Mt. 6:9.
Suala si ikiwa wao wanaweza au hawawezi kuokoka mateso na kuepuka kifo. Yesu Kristo alitabiri kwamba baadhi ya wafuasi wake wangeuawa. (Mt. 24:9) Yeye mwenyewe aliuawa. Lakini hakuridhiana kamwe na Mshindani mkuu wa Mungu, Shetani Ibilisi, “mtawala wa ulimwengu.” Yesu aliushinda ulimwengu. (Yn. 14:30; 16:33, NW) Basi, suala ni ikiwa waabudu wa Mungu wa kweli watabaki waaminifu kwake kujapokuwa magumu yoyote ambayo huenda wakapata. Mashahidi wa kisasa wa Yehova wametoa ithibati tele kwamba wana akili ileile kama ya mtume Paulo, aliyeandika: “Kwa maana tukiishi, twaishi kwa Yehova, na tukifa, twafa kwa Yehova pia. Kwa hiyo tukiishi na tukifa pia, sisi ni wa Yehova.”—Rum. 14:8, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Wanafunzi wa Biblia hawakuelewa waziwazi wakati huo yale ambayo Mashahidi wanajua sasa kutoka Biblia kuhusu wanaume kuwa walimu katika kutaniko. (1 Kor. 14:33, 34; 1 Tim. 2:11, 12) Kama tokeo, Maria Russell alikuwa amekuwa mhariri mshiriki wa Watch Tower na mchangaji wa kawaida wa safu zalo.
b Joseph F. Rutherford, msimamizi wa Watch Tower Society; William E. Van Amburgh, katibu-mweka-hazina wa Sosaiti; Robert J. Martin, meneja wa ofisi; Frederick H. Robison, mshiriki wa halmashauri ya uhariri wa The Watch Tower; A. Hugh Macmillan, mkurugenzi wa Sosaiti; George H. Fisher na Clayton J. Woodworth, watungaji wa The Finished Mystery.
c Giovanni DeCecca, aliyefanya kazi katika Idara ya Italia katika ofisi ya Watch Tower Society.
d Hakimu wa Mzunguko Martin T. Manton, wa Katoliki ya Roma aliye mshupavu, alikataa rufani ya pili ya kupewa dhamana Julai 1, 1918. Wakati mahakama ya kitaifa ya rufani ilipobatilisha hukumu ya washtakiwa, Manton pekee ndiye ambaye hakupendelea hilo. Inastahili kuangaliwa kwamba Desemba 4, 1939, mahakama ya rufani iliyofanyizwa kipekee ilitetea kuhukumiwa kwa Manton kwa ajili ya utumizi mbaya wa uwezo wa mahakama, kutokuwa mnyoofu, na kutumia hila.
e Jambo la kwamba wanaume hao walifungwa isivyo haki, na hawakuwa wenye hatia, linaonyeshwa na uhakika wa kwamba J. F. Rutherford aliendelea kuwa mshiriki wa mawakili wa Mahakama Kuu ya Marekani tangu kusajiliwa kwake katika Mei 1909 hadi kifo chake katika 1942. Katika kesi 14 zilizokatwa rufani katika Mahakama Kuu kuanzia 1939 hadi 1942, J. F. Rutherford alikuwa mmoja wa mawakili. Katika kesi zilizoitwa Schneider v. State of New Jersey (katika 1939) na Minersville School District v. Gobitis (katika 1940), yeye mwenyewe alitoa hoja za maneno mbele ya Mahakama Kuu. Pia, wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, A. H. Macmillan, mmojawapo wanaume waliofungwa isivyo haki mwaka 1918-1919, alikubaliwa na mkurugenzi wa Idara ya Magereza ya kitaifa kuwa akifanya ziara za kawaida kwenye magereza ya kitaifa ya Marekani ili kutunza faida za kiroho za vijana waliokuwa huko kwa sababu ya kuwa wamechukua msimamo wa kutokuwamo kwa Kikristo.
f The Encyclopedia Americana, Buku 11, 1942, kurasa 316, husema: “Kama vile msalaba, bendera ni takatifu. . . . Sheria na miongozo inayohusiana na mtazamo wa kibinadamu kuelekea bendera za kitaifa hutumia maneno mazito, yenye kueleza mambo, kama vile, ‘Utumishi kwa Bendera,’ . . . ‘Uchaji kwa Bendera,’ ‘Ujitoaji kwa Bendera.’” Katika Brazili, Diário da Justiça, Februari 16, 1956, ukurasa 1904, liliripoti kwamba kwenye sherehe ya kitaifa, ofisa wa jeshi alisema: “Bendera zimekuwa uungu wa dini ya kizalendo . . . Bendera inaheshimiwa sana na kuabudiwa.”
[Blabu katika ukurasa wa 642]
Wanyanyasi wakuu wa Yesu Kristo walikuwa viongozi wa kidini
[Blabu katika ukurasa wa 645]
“Kutawazwa au kuagizwa na Mungu kwa mtu yeyote ili ahubiri ni kwa kupewa Roho Takatifu”
[Blabu katika ukurasa wa 647]
Kitabu “The Finished Mystery” kilifunua waziwazi unafiki wa makasisi wa Jumuiya ya Wakristo!
[Blabu katika ukurasa wa 650]
Wanaume na wanawake Wakristo walipigwa na magenge, wakatiwa gerezani, na kuzuiwa humo bila kushtakiwa au bila kuhukumiwa
[Blabu katika ukurasa wa 652]
“Vifungo hivyo kwa wazi vinapita kiasi”—rais wa Marekani Woodrow Wilson
[Blabu katika ukurasa wa 656]
Mtu yeyote aliyekosa kufanya yale ambayo padri alisema, hakupata haki yoyote
[Blabu katika ukurasa wa 666]
Mapadri walihimiza walimu wawaache watoto waondoke shuleni ili wakawarushie Mashahidi mawe
[Blabu katika ukurasa wa 668]
Makasisi waliungana pamoja ili kupinga Mashahidi
[Blabu katika ukurasa wa 671]
Magenge yaliwatenda vibaya Mashahidi wa Yehova katika Marekani
[Blabu katika ukurasa wa 676]
Katika kila sehemu ya dunia, Mashahidi wa Yehova hunyanyaswa
[Sanduku katika ukurasa wa 655]
Makasisi Waonyesha Hisia Zao
Maitikio ya magazeti ya kidini baada ya kuhukumiwa kwa J. F. Rutherford na washiriki wake mwaka 1918 yanastahili kuangaliwa:
◆ “The Christian Register”: “Kile ambacho Serikali hapa inashambulia moja kwa moja kwa njia ya kufisha ni ile dhana kwamba mawazo ya kidini, hata yawe ya kichaa na yenye kudhuru jinsi gani, yanaweza kuenezwa bila hofu ya kuadhibiwa. Dhana hiyo ni uwongo wa kale, na kufikia sasa hatujakuwa waangalifu sana kulihusu. . . . Hukumu hiyo inaonekana kuwa ndiyo mwisho wa Urusselli.”
◆ “The Western Recorder,” kichapo cha Baptisti, kilisema: “Haishangazi kwamba kiongozi wa kidhehebu hicho chenye ukaidi amefungiwa katika mojawapo ya vituo vya watu wakaidi. . . . Tatizo lenye kutatanisha kwelikweli kuhusiana na jambo hilo ni ikiwa washtakiwa wangepaswa wapelekwe kwenye makao ya wenye kichaa au kwenye gereza.”
◆ “The Fortnightly Review” lilielekeza fikira kwenye maelezo katika gazeti la New York “Evening Post,” ambalo lilisema: “Tunatumaini kwamba walimu wa dini kila mahali wataona maoni ya hakimu huyu kwamba kufunza dini yoyote isipokuwa ile ambayo inapatana kabisa na sheria zilizowekwa ni hatia kubwa ambayo inafanywa kuwa kubwa zaidi, ikiwa wewe ukiwa mhudumu wa gospeli, ungali mnyoofu.”
◆ “The Continent” kwa kuwashushia heshima liliwaonyesha washtakiwa kuwa “wafuasi wa ‘Pasta’ Russell aliyekufa” na likapotoa imani zao kwa kusema kwamba waliunga mkono “kwamba watu wote wanapaswa wasipelekwe kupigana na kaiser wa Ujerumani isipokuwa wale wenye dhambi.” Lilidai kwamba kulingana na wakili mkuu katika Washington, “muda fulani uliopita serikali ya Italia ililalamikia Marekani kwamba Rutherford na washiriki wake . . . walikuwa wameeneza kiasi fulani cha propaganda ya kupinga vita katika majeshi ya Italia.”
◆ Juma moja baadaye, “The Christian Century” lilichapa sehemu kubwa ya habari iliyo juu neno kwa neno, ikionyesha kwamba walikubaliana nayo kabisa.
◆ Gazeti la Katoliki “Truth” liliripoti kifupi ile hukumu waliyopewa na kisha likaeleza hisi za wahariri walo, likisema: “Fasihi za shirika hilo zimejaa mashambulizi makali sana juu ya Kanisa Katoliki na upadri walo.” Ili kujaribu kuweka kibandiko cha “uasi” juu ya yeyote ambaye huenda akapinga hadharani maoni ya Kanisa Katoliki, liliongezea hivi: “Inazidi kuwa wazi kwamba roho ya kutovumilia inafungamanishwa kwa ukaribu na ile ya uasi.”
◆ Dakt. Ray Abrams, katika kitabu chake “Preachers Present Arms,” alionelea hivi: “Wakati habari za hukumu ya vifungo hivyo vya miaka ishirini zilipofikia wahariri wa magazeti ya kidini, karibu kila kimoja cha vichapo hivyo, kikubwa na kidogo, kilishangilia tukio hilo. Mimi nimeshindwa kupata maneno yoyote ya masikitiko katika yoyote ya majarida ya kidini yanayokubaliwa.”
[Sanduku katika ukurasa wa 660]
“Wanyanyaswa kwa Sababu za Kidini”
“Kulikuwa na kikundi cha watu katika Kambi ya Mateso ya Mauthausen walionyanyaswa kwa sababu za kidini tu: washiriki wa farakano liitwalo ‘Wanafunzi wa Biblia Wenye Bidii,’ au ‘Mashahidi wa Yehova’ . . . Kukataa kwao kula kiapo cha uaminifu-mshikamanifu kwa Hitler na kukataa kwao kutoa aina yoyote ya utumishi wa kijeshi—likiwa tokeo la itikadi yao kuhusu siasa—ndiyo iliyokuwa sababu ya kunyanyaswa kwao.”—“Die Geschichte des Konzentrationslagers Mauthausen” (Historia ya Kambi ya Mateso ya Mauthausen), iliyotungwa na Hans Maršálek, Vienna, Austria, 1974.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 661]
Tafsiri ya Taarifa Ambayo Polisi wa SS Walijaribu Kuwalazimisha Mashahidi Watie Sahihi
Kambi ya mateso .......................................
Idara 2
TAARIFA
Mimi, ...................................................
niliyezaliwa tarehe ..................................................
katika .......................................................
ninatoa taarifa ifuatayo:
1. Mimi nimekuja kujua kwamba International Bible Students Association inapiga mbiu ya mafundisho yasiyo kweli na hiyo hufuatilia makusudi ya uhasama dhidi ya Serikali chini ya kisitiri cha dini.
2. Mimi kwa sababu hiyo niliacha tengenezo hilo kabisa na nikajiweka huru kabisa na mafundisho ya farakano hilo.
3. Mimi ninatoa uhakikisho hapa kwamba sitakuwa na sehemu yoyote kamwe katika utendaji wa International Bible Students Association. Watu wowote wanaonijia na mafundisho ya Wanafunzi wa Biblia, au ambao kwa njia yoyote ile wanafunua uhusiano wao nao, nitawashutumu mara hiyo. Fasihi zote kutoka kwa Wanafunzi wa Biblia ambazo zitaletwa nyumbani kwangu nitazipeleka mara hiyo kwa kituo cha polisi kilichoko karibu.
4. Mimi nitaheshimu sheria za Serikali kuanzia sasa, hasa kukiwa vita, mimi nitachukua silaha mkononi, na kulinda nchi yangu, na kuungana kwa kila njia na jumuiya ya watu.
5. Mimi nimejulishwa kwamba nitachukuliwa tena mara hiyo ndani ya kifungo cha ulinzi ikiwa nitatenda tofauti na taarifa niliyotoa leo.
.................................., Tarehe ................ ...........................................................
Sahihi
[Sanduku katika ukurasa wa 662]
Barua Kutoka kwa Baadhi ya Wale Waliohukumiwa Kifo
Kutoka kwa Franz Reiter (aliyekabili kifo kwa kukatwa kichwa) kwa mama yake, Januari 6, 1940, kutoka kwa gereza la Berlin-Plötzensee:
“Ninasadiki kwa nguvu katika imani yangu kwamba ninatenda vile inavyofaa. Nikiwa hapa, bado ningeweza kubadili nia yangu, lakini kwa Mungu hiyo ingekuwa ni kutokuwa mwaminifu-mshikamanifu. Sisi sote hapa twataka kuwa waaminifu kwa Mungu, kwa heshima yake. . . . Kwa yale niliyojua, ikiwa ningalikula kiapo [cha kijeshi], ningalitenda dhambi inayostahili kifo. Huo ungekuwa uovu kwangu. Nisingepata ufufuo. Lakini nashikamana na yale aliyosema Kristo: ‘Yeyote atakayeokoa uhai wake ataupoteza; lakini yeyote atakayepoteza uhai wake kwa ajili yangu, huyo ataupokea.’ Na sasa, Mama yangu mpendwa na ndugu na dada zangu wote, leo niliambiwa hukumu yangu, na msiogopeshwe, ni kifo, nami nitauawa kesho asubuhi. Nina nguvu yangu kutoka kwa Mungu, sawa na ilivyokuwa sikuzote kwa Wakristo wote wa kweli huko nyuma. Mitume wanaandika, ‘Yeyote aliyezaliwa kutoka kwa Mungu hawezi kufanya dhambi.’ Ndivyo ilivyo kwangu mimi. Hilo nilikuthibitishia, na ungeweza kulitambua. Mpendwa wangu, usihuzunike. Ingekuwa vizuri kwa nyinyi nyote kuyajua Maandiko Matakatifu vizuri hata zaidi. Ikiwa mtasimama imara hadi kifo, tutaonana tena kwenye ufufuo. . . .
“Wako Franz
“Hadi tutakapoonana tena.”
Kutoka kwa Berthold Szabo, aliyeuawa kwa kupigwa risasi, katika Körmend, Hungaria, mnamo Machi 2, 1945:
“Dada yangu mpendwa, Marika!
“Muda huu wa saa moja unusu ambao nimebaki nao, nitajaribu kukuandikia ili uweze kuwajulisha wazazi wetu kuhusu hali yangu, ninapokabili kifo mara hii.
“Ninawatakia wao amani ya akili ileile ambayo ninayo katika pindi hii ya mwisho katika ulimwengu uliojaa misiba. Sasa ni saa nne, na nitauawa saa tano unusu; lakini mimi ni mtulivu sana. Uhai wangu wa baadaye ninauweka mikononi mwa Yehova na Mwana wake Mpendwa, Yesu Kristo, Mfalme, ambaye hatasahau kamwe wale wanaowapenda kikweli. Ninajua pia kwamba karibuni kutakuwa na ufufuo wa wale waliokufa au, ndiyo kusema waliolala, katika Kristo. Ningependa pia kutaja hasa kwamba ninawatakia nyote baraka za Yehova zenye utajiri zaidi kwa ajili ya upendo mlionionyesha. Tafadhali mbusu baba na mama kwa ajili yangu, na Annus pia. Hawapaswi kunisikitikia; tutaonana tena karibuni. Mkono wangu ni mtulivu sasa, na nitaenda kupumzika hadi Yehova atakaponiita tena. Hata sasa nitatimiza nadhiri niliyofanya kwa ajili yake.
“Sasa wakati wangu umekwisha. Mungu na awe nanyi na mimi pia.
“Kwa upendo mwingi, . . .
“Berthi”
[Sanduku katika ukurasa wa 663]
Watambuliwa Kuwa Wajasiri na Wenye Masadikisho
◆ “Wajapokabiliwa na matatizo makubwa ajabu, Mashahidi katika kambi walikutana na kusali pamoja, wakatokeza fasihi na kugeuza watu wafuate imani yao. Wakitegemezwa na ushirika wao, na wakiwa tofauti na wafungwa wengine wengi, wakifahamu vema sababu za kuwapo kwa sehemu kama hizo na sababu za wao kuteseka hivyo, Mashahidi walithibitika kuwa kikundi kidogo cha wafungwa wanaokumbukwa, waliopewa alama ya pembe-tatu ya zambarau na kutambuliwa kwa ujasiri na masadikisho yao.” Ndivyo alivyoandika Dakt. Christine King, katika “The Nazi State and the New Religions: Five Case Studies in Non-Conformity.”
◆ “Values and Violence in Auschwitz,” cha Anna Pawełczyńska, chasema: “Kikundi hicho cha wafungwa kilikuwa kani imara ya kimafundisho na kilishinda vita dhidi ya Unazi. Kikundi cha Wajerumani cha farakano hilo kilikuwa kimekuwa kisiwa duni cha upinzani usiotikisika miongoni mwa taifa lililotiwa hofu, na katika roho iyo hiyo ya kutoghadhibika walifanya kazi kambini katika Auschwitz. Waliheshimiwa na wafungwa wenzao . . . wafanyakazi wa magereza, na hata maofisa wa SS. Kila mtu alijua kwamba hakuna ‘Bibelforscher’ [Shahidi wa Yehova] ambaye angefuata amri iliyo kinyume cha imani zake za kidini.”
◆ Rudolf Hoess, katika masimulizi yake ya maisha yaliyochapwa katika kitabu “Commandant of Auschwitz,” alisema juu ya kuuawa kwa Mashahidi wa Yehova fulani kwa kukataa kuvunja kutokuwamo kwao kwa Kikristo. Yeye alisema: “Hivyo ndivyo ninavyowazia kwamba lazima wafia-imani Wakristo wa kwanza wawe walionekana huku wakingoja katika sarakasi ili hayawani mwitu waje kuwararuararua. Nyuso zao zikiwa zimebadilika kabisa, macho yao yakiwa yameinuliwa mbinguni, na mikono yao ikiwa imefumbwa na kuinuliwa katika sala, wakakabili kifo. Wote waliowaona wakifa waliguswa moyo sana, na hata kikosi cha wauaji chenyewe kiliguswa moyo.” (Kitabu hicho kilitangzwa katika Poland chini ya kichwa “Autobiografia Rudolfa Hössa-komendanta obozu oświęcimskiego.”)
[Sanduku katika ukurasa wa 673]
“Wao Si Wapinga-Nchi”
“Wao si wapinga-nchi; wao ni wapenda-Yehova tu.” “Huwa hawachomi kadi za usajili wa jeshini, hawaasi . . . au kushiriki katika aina yoyote ya uhaini.” “Mashahidi hudumu katika ufuatiaji-haki na uaminifu-maadili. Mambo yoyote ambayo mtu anaweza kufikiri kuhusu Mashahidi—na watu wengi hufikiri mengi yasiyofaa kuwahusu—wao huishi maisha yaliyo kielelezo chema.”—“Telegram,” Toronto, Kanada, Julai 1970.
[Sanduku katika ukurasa wa 674]
Ni Nani Aliye Msimamizi?
Mashahidi wa Yehova wanajua kwamba daraka lao la kuhubiri halitegemei kuendelea kutenda kwa Watch Tower Society au shirika jingine lolote la kisheria. “Acha Watch Tower Society ikatazwe na ofisi zayo za Tawi katika nchi mbalimbali zifungwe kwa nguvu na serikali! Hilo halibatilishi au kuondoa agizo la kimungu juu ya wanaume na wanawake waliojitakasa ili kufanya mapenzi ya Mungu na ambao juu yao Yeye ameweka roho yake. ‘Hubiri!’ limeandikwa waziwazi katika Neno lake. Agizo hilo linachukua mahali pa kwanza kupita lile la binadamu yeyote.” (“Mnara wa Mlinzi,” Desemba 15, 1949, Kiingereza) Wakitambua kwamba maagizo yao hutoka kwa Yehova Mungu na Yesu Kristo, wao hudumu katika kupiga mbiu ya ujumbe wa Ufalme kujapokuwa upinzani wanaokabili.
[Sanduku katika ukurasa wa 677]
Kama Wakristo wa Mapema
◆ “Mashahidi wa Yehova wana dini wanayochukua kwa uzito zaidi sana ya jinsi watu wengi wanavyoichukua. Kanuni zao hutukumbusha juu ya Wakristo wa mapema ambao hawakupendwa na wengi na ambao walinyanyaswa kwa ukatili sana na Waroma.”—“Akron Beacon Journal,” Akron, Ohio, Septemba 4, 1951.
◆ “Wao [Wakristo wa mapema] walikuwa na maisha matulivu, maadilifu, kwa kweli yaliyo kielelezo. . . . Katika kila jambo isipokuwa lile jambo moja la kufukiza uvumba walikuwa wananchi walio kielelezo chema.” “Ingawa kutoa dhabihu kwa Roho iliyomwongoza maliki kulibaki kuwa jaribu la uzalendo, je, wenye mamlaka wa serikali wangeweza kupuuza upinzani wenye kukaidi wa Wakristo hao wasio wazalendo? Tatizo ambalo Wakristo hao walijipata kwalo halikutofautiana sana na tatizo ambalo, wakati wa miaka ya vita, farakano hilo lenye ukaidi linalojulikana kuwa Mashahidi wa Yehova lilijipata kwalo katika Marekani kuhusu kusalimu bendera ya taifa.”—“20 Centuries of Christianity,” cha Paul Hutchinson na Winfred Garrison, 1959, uku. 31.
◆ “Labda jambo moja ambalo linatokeza sana kuhusu Mashahidi ni kule kusisitiza juu ya ushikamanifu unaotangulizwa kwanza kwa Mungu, kabla ya taifa jingine lolote ulimwenguni.”—“These Also Believe,” cha Dakt. C. S. Braden, 1949, uku. 380.
[Picha katika ukurasa wa 644]
“The Pittsburgh Gazette” lilitangaza kwa kadiri kubwa mijadala iliyotokana na mwito wa ushindani wa Dakt. Eaton kwa C. T. Russell
[Picha katika ukurasa wa 646]
Uwongo mkubwa kuhusu hali ya ndoa ya Charles na Maria Russell ulienezwa sana na wapinzani
[Picha katika ukurasa wa 648]
Makasisi walighadhibika wakati nakala 10,000,000 za trakti hii zilipogawanywa zikifunua mafundisho na mazoea yao kwa maoni ya Neno la Mungu
[Picha katika ukurasa wa 649]
Magazeti yalichochea moto wa mnyanyaso wa Wanafunzi wa Biblia katika 1918
[Picha katika ukurasa wa 651]
Wakati wa kuhukumiwa hapa kwa washiriki wa wafanyakazi wa makao makuu ya Sosaiti, fikira nyingi zilielekezwa kwenye kitabu “The Finished Mystery”
Mahakama kuu na posta, Brooklyn, N.Y.
[Picha katika ukurasa wa 653]
Wahukumiwa kwa kifungo kikubwa zaidi ya kile cha muuaji aliyepiga risasi na kuanzisha Vita ya Ulimwengu 1. Kutoka kushoto kwenda kulia: W. E. Van Amburgh, J. F. Rutherford, A. H. Macmillan, R. J. Martin, F. H. Robison, C. J. Woodworth, G. H. Fisher, G. DeCecca
[Picha katika ukurasa wa 657]
Wakati kusanyiko hili la Mashahidi lilipofanywa katika New York mwaka 1939, wanagenge kama 200 wakiongozwa na mapadri Wakatoliki walijaribu kulivunja
[Picha katika ukurasa wa 659]
Wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, maelfu ya Mashahidi wa Yehova walitupwa katika kambi hizi za mateso
Nishani ya fuvu ya walinzi wa SS (kushoto)
[Picha katika ukurasa wa 664]
Sehemu ya kitabu cha funzo la Biblia kilichopunguzwa ukubwa kwa kupigwa picha, kilichowekwa katika gamba (kibumba) la kiberiti, na kuingizwa kwa siri katika kambi ya mateso kwa ajili ya Mashahidi
[Picha katika ukurasa wa 665]
Baadhi ya Mashahidi ambao imani yao ilistahimili jaribu kali la kambi za mateso za Nazi
Mauthausen
Wewelsburg
[Picha katika ukurasa wa 667]
Jeuri ya magenge karibu na Montreal, Quebec, mwaka 1945. Jeuri kama hiyo iliyochochewa na makasisi dhidi ya Mashahidi ilikuwa ya kawaida wakati wa miaka ya 1940 na 1950
[Picha katika ukurasa wa 669]
Maelfu ya Mashahidi wa Yehova (kutia na John Booth, anayeonyeshwa hapa) walikamatwa walipogawanya fasihi za Biblia
[Picha katika ukurasa wa 670]
Kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu dhidi ya Mashahidi katika 1940, jeuri ya magenge ilienea kotekote Marekani, mikutano ilivunjwa, Mashahidi wakapigwa, na mali ikaharibiwa
[Picha katika ukurasa wa 672]
Katika sehemu nyingi kulikuwa na uhitaji wa kuanzisha Shule za Ufalme kwa sababu watoto Mashahidi walikuwa wamefukuzwa kutoka shule za umma