-
Ulimwengu Usio na MagonjwaAmkeni!—2004 | Mei 22
-
-
Alisema kwamba mojawapo ya mambo hayo ni kuzuka kwa ‘tauni mahali pamoja baada ya pengine.’ (Luka 21:10, 11; Mathayo 24:3, 7) Neno la Kigiriki linalotafsiriwa “tauni” linamaanisha “ugonjwa wowote hatari wa kuambukiza.” Bila shaka, katika karne ya 20 kulikuwa na magonjwa mengi sana ya kuambukiza, licha ya maendeleo mengi katika sayansi ya tiba.—Ona sanduku “Vifo Kutokana na Tauni Mbalimbali Tangu 1914.”
Unabii wa kitabu cha Ufunuo, unaolingana na maneno ya Yesu katika Injili, unaonyesha wapanda-farasi kadhaa wanaoandamana na Yesu Kristo anapoanza kutawala mbinguni. Mpanda-farasi wa nne ameketi juu ya “farasi wa rangi ya kijivu,” naye anatokeza “pigo lenye kufisha.” (Ufunuo 6:2, 4, 5, 8) Idadi ya watu ambao wamekufa kutokana na magonjwa hatari ya kuambukiza tangu mwaka wa 1914 inathibitisha kwamba mpanda-farasi huyo amekuwa akimwendesha farasi wake. Kuenea kwa “pigo lenye kufisha” ulimwenguni pote ni uthibitisho mwingine wa kwamba Ufalme wa Mungu uko karibu.b—Marko 13:29.
-
-
Ulimwengu Usio na MagonjwaAmkeni!—2004 | Mei 22
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 12]
Vifo Kutokana na Tauni Mbalimbali Tangu 1914
Takwimu zinazofuata ni makadirio tu. Hata hivyo, zinaonyesha kiwango ambacho tauni mbalimbali zimewahangaisha wanadamu tangu 1914.
◼ Ndui (kati ya milioni 300 na milioni 500) Hakuna matibabu yoyote yanayofaa yaliyovumbuliwa. Hatimaye mradi mkubwa wa kimataifa wa kuwachanja watu ulifanikiwa kuondolea mbali ugonjwa huo kufikia mwaka wa 1980.
◼ Kifua-kikuu (kati ya milioni 100 na milioni 150) Leo, ugonjwa huo huua watu wapatao milioni mbili kila mwaka, na mtu 1 kati ya watu 3 ulimwenguni ana viini vya ugonjwa huo.
◼ Malaria (kati ya milioni 80 na milioni 120) Miaka 50 ya kwanza ya karne ya 20, idadi ya watu waliokuwa wakifa kutokana na malaria ilikuwa milioni mbili hivi kila mwaka. Leo, idadi kubwa ya watu wanaokufa kutokana na ugonjwa huo inapatikana barani Afrika, kusini mwa Sahara, ambapo bado malaria huua zaidi ya watu milioni moja kila mwaka.
◼ Homa ya Hispania (kati ya milioni 20 na milioni 30) Wanahistoria fulani husema kwamba watu wengi zaidi walikufa kutokana na ugonjwa huo kuliko inavyokadiriwa. Ugonjwa huo hatari ulienea ulimwenguni mwaka wa 1918 na 1919, baada tu ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. “Hata ile tauni ya majipu haikuua watu wengi hivyo mara moja,” chasema kitabu Man and Microbes.
◼ Homa ya Chawa (milioni 20 hivi) Mara nyingi ugonjwa huo ulikuwa ukizuka wakati wa vita, navyo Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilitokeza tauni ya chawa iliyokumba nchi za Ulaya Mashariki.
◼ UKIMWI (zaidi ya milioni 20) Tauni hii ya siku zetu sasa inaua watu milioni tatu kila mwaka. Makadirio ya sasa ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na UKIMWI yanaonyesha kwamba “kusipokuwa na jitihada za kutosha za kuuzuia na kuutibu, watu milioni 68 watakufa . . . kati ya mwaka wa 2000 na 2020.”
-