Uvuvi Katika Bahari ya Galilaya
WAVUVI katika Bahari ya Galilaya walikuwa na maisha ya aina gani katika karne ya kwanza? Jibu la swali hilo litatusaidia kuelewa masimulizi mengi ya Injili, kama yale yaliyozungumziwa katika makala iliyotangulia.
“Bahari” hiyo ni ziwa lenye maji baridi lenye urefu wa kilomita 21 na upana wa kilomita 12. Wavuvi wamevua kwa muda mrefu samaki wengi walio ndani ya ziwa hilo. Lango la Samaki la Yerusalemu lilikuwa soko la samaki hao. (Nehemia 3:3) Baadhi ya samaki waliouzwa hapo walikuwa wamevuliwa katika Bahari ya Galilaya.
Mtume Petro alitoka katika mji uliokuwa karibu na Bahari ya Galilaya unaoitwa Bethsaida, jina ambalo huenda linamaanisha “Nyumba ya Mvuvi.” Mji mwingine uliokuwa karibu na ziwa hilo ni Magadani, au Magdala, na Yesu aliwapeleka wanafunzi wake huko baada ya kutembea juu ya maji. (Mathayo 15:39) Kulingana na mwandishi mmoja, jina la Kigiriki la mji huo linaweza kutafsiriwa kuwa “Mji Ulio na Kiwanda cha Samaki.” Ulijulikana kwa viwanda vyake vikubwa vya samaki ambako samaki waliovuliwa walikaushwa na kutiwa chumvi au siki ili kutokeza mchuzi fulani uliohifadhiwa katika vyungu vinavyoitwa amphoras. Samaki hao walipakiwa na kusafirishwa katika sehemu zote za Israeli na huenda hata mbali zaidi.
Kwa sababu hiyo, kazi ya kuvua, kutayarisha, na kuuza samaki ilikuwa biashara kubwa huko Galilaya katika siku za Yesu. Huenda mtu akafikiri kwamba kazi hiyo iliwafanya watu wengi katika eneo hilo wapate faida nyingi za kiuchumi. Lakini huenda hali haikuwa hivyo. Uvuvi “haukuwa ‘biashara huru’ kama wasomaji wengi wa kisasa wa Agano Jipya wanavyoweza kufikiri,” anasema msomi mmoja. Ulikuwa sehemu ya “biashara zilizodhibitiwa na serikali na kuwanufaisha watu wachache tu mashuhuri.”
Herode Antipa alisimamia Galilaya akiwa mtawala wa wilaya hiyo, au mkuu wa eneo, aliyewekwa rasmi na Roma. Kwa hiyo, alidhibiti barabara, bandari, na mali za asili, kama vile migodi, misitu, ukulima, na uvuvi. Herode alikusanya kodi nyingi kutoka katika vitu hivyo vyote. Hatuna habari hususa kuhusu kodi ilivyokusanywa huko Galilaya katika karne ya kwanza. Hata hivyo, yaonekana kwamba njia ya Herode haikutofautiana sana na ile ya watawala wa Ugiriki au ile iliyotumiwa na Waroma katika mikoa yao mingine ya mashariki. Huenda watu mashuhuri ndio waliofaidika kutokana na shughuli za kiuchumi za eneo hilo na mali zake za asili. Watu wa kawaida ambao ndio waliofanya kazi nyingi hawakupata faida.
Kodi za Juu Sana
Katika siku za Yesu ardhi bora zaidi huko Galilaya ilimilikiwa na watawala na iligawanywa katika mashamba makubwa ambayo Herode Antipa aliwapa wakuu wake na marafiki wake wengine. Watu waliotawaliwa na Herode walipaswa kugharamia maisha yake ya anasa, miradi yake mikubwa ya ujenzi, uendeshaji wa serikali yake kubwa, na zawadi alizowapa marafiki na majiji mengine. Inasemekana kwamba watu wa kawaida walitozwa kodi na ushuru uliowalemea.
Pia, Herode alidhibiti kabisa maziwa yote. Kwa hiyo, uvuvi ulisimamiwa na serikali ya Herode au na watu binafsi waliopewa maeneo hayo kama zawadi. Katika maeneo yaliyodhibitiwa na serikali yake, madalali wa kukusanya kodi au wakuu wa wakusanya kodi, ambao walikuwa matajiri walionunua haki za kukusanya kodi kwenye mnada, na hivyo wangekuwa na mamlaka ya kuweka mkataba na wavuvi ili waweze kununua haki ya kuvua. Baadhi ya wafafanuzi wa Biblia wanasema kwamba kwa kuwa ofisi ya kodi ya Mathayo ilikuwa huko Kapernaumu, kituo muhimu cha uvuvi katika Bahari ya Galilaya, huenda aliwafanyia kazi hao wakuu wa kukusanya kodi akiwa “muuzaji wa haki za uvuvi.”a
Uthibitisho wa karne ya kwanza na ya pili K.W.K., unaonyesha kwamba huko Palestina kodi ililipwa “kwa kubadilishana vitu” badala ya pesa taslimu. Hivyo wafanyabiashara fulani wavuvi walilipa asilimia 25 hadi 40 hivi ya samaki wao waliovua ili wapate haki ya kuvua. Hati za kale zinaonyesha kwamba angalau maeneo fulani ya uvuvi yaliyokuwa chini ya serikali ya Roma, yalidhibitiwa na wakaguzi wa Serikali. Huko Pisidia kulikuwa na askari wa uvuvi waliohakikisha kwamba hakuna mtu aliyevua bila ruhusa na kwamba wavuvi waliwauzia tu madalali walioidhinishwa ambao pia walikuwa chini ya Serikali na walitozwa kodi.
Mchanganuzi mmoja anasema kwamba utaratibu huo na kodi hizo zote zilihakikisha kwamba “mfalme au wamiliki wa maeneo hayo walipata faida kubwa sana huku wavuvi wakipata faida ndogo sana.” Wale waliojihusisha katika biashara nyingine walipata faida ndogo sana kwa sababu ya kutozwa kodi nyingi vilevile. Watu hawakufurahia hata kidogo kulipa kodi. Hata hivyo, uhasama kuwaelekea wakusanya kodi tunaosoma katika masimulizi ya Injili ulitokana na udanganyifu na pupa ya watu waliojitajirisha kwa kuwatoza watu wa kawaida kodi kubwa.—Luka 3:13; 19:2, 8.
Wavuvi Wanaotajwa Katika Injili
Vitabu vya Injili vinaonyesha wazi kwamba Simoni Petro alishirikiana na wengine katika biashara ya uvuvi. Watu hao alioshirikiana nao ndio waliokuja kumsaidia kuvuta wavu uliojaa samaki kimuujiza. (Luka 5:3-7) Wasomi fulani wanasema kwamba “wavuvi wangeweza kuunda ‘vyama vya ushirika’ . . . ili wakodi maeneo na wapate mikataba ya kuvua.” Huenda wana wa Zebedayo, Petro, Andrea, na washirika wao walifanya hivyo ili kupata idhini ya kuendesha biashara yao ya uvuvi.
Maandiko hayatuambii waziwazi ikiwa wavuvi hao wa Galilaya walimiliki mashua na vifaa walivyotumia katika kazi yao. Watu fulani wanaamini kwamba walifanya hivyo. Kwa kweli inasemwa kwamba Yesu alipanda mashua “iliyokuwa ya Simoni.” (Luka 5:3) Hata hivyo, kitabu kimoja kilichozungumzia habari hiyo kinasema, “kuna uwezekano mkubwa mashua hizo zilikuwa za madalali na zilitumiwa na vyama vya wavuvi.” Iwe hiyo ilikuwa kweli au la, Maandiko yanawataja Yakobo na Yohana wakirekebisha nyavu zao. Huenda wavuvi walihitaji kuuza samaki wao na ilipohitajika waliajiri vibarua.
Kwa hiyo, mengi zaidi yalihusika katika kazi ya wavuvi wa karne ya kwanza kuliko mtu anavyoweza kufikiri. Biashara yao ilikuwa sehemu ya mfumo tata wa kiuchumi. Kukumbuka jambo hilo kunamwezesha mtu kuelewa vizuri zaidi masimulizi ya Injili na kuelewa maneno ya Yesu kuhusu uvuvi na wavuvi. Zaidi ya hilo, habari hii inatusaidia kuelewa imani ya Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana. Maisha yao yalitegemea uvuvi. Hata wawe walikuwa na hali gani ya kiuchumi wakati Yesu alipowaita, mara moja waliacha biashara yao ambayo waliitegemea sana kupata riziki, ili wawe “wavuvi wa watu.”—Mathayo 4:19.
[Maelezo ya chini]
a Ni wazi kwamba mtume Petro alihama kutoka Bethsaida hadi Kapernaumu ambako alifanya biashara ya uvuvi pamoja na ndugu yake, Andrea, na wana wa Zebedayo. Pia, Yesu aliishi huko Kapernaumu kwa muda fulani.—Mathayo 4:13-16.
[Ramani katika ukurasa wa 25]
ˈOna mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwaˈ
Ziwa Hula
Bethsaida
Kapernaumu
Magadani
Bahari ya Galilaya
Yerusalemu
Bahari ya Chumvi
[Hisani]
Todd Bolen/Bible Places.com
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
Todd Bolen/Bible Places.com