Gamalieli—Alimfundisha Sauli wa Tarso
UMATI ulitulia tuli. Muda mfupi tu mapema, ulikuwa karibu umuue mtume Paulo. Aliyeitwa pia Sauli wa Tarso, alikuwa ameokolewa na vikosi vya Roma na sasa aliwakabili watu kwenye ngazi karibu na hekalu katika Yerusalemu.
Akipunga mkono wake ili kuwe na unyamavu, Paulo alianza kuongea katika Kiebrania, akisema: “Enyi wanaume, ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni, nikijitetea mbele yenu sasa. . . . Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi.”—Matendo 22:1-3.
Maisha yake yakiwa hatarini, kwa nini Paulo alianza kujitetea kwake kwa kusema kwamba alikuwa amefundishwa na Gamalieli? Gamalieli alikuwa nani, na ni mambo gani yaliyohusishwa katika kufundishwa naye? Je, mazoezi hayo yalikuwa na uvutano juu ya Sauli hata baada ya yeye kuwa mtume Mkristo Paulo?
Gamalieli Alikuwa Nani?
Gamalieli alikuwa Farisayo aliyejulikana sana. Alikuwa mjukuu wa kiume wa Hillel yule Mkubwa, aliyekuwa ameanzisha kimojapo vile vikundi vikubwa viwili vya kitheolojia katika Dini ya Kiyahudi ya Kifarisayo.a Njia ya kufundisha ya Hillel ilionwa kuwa yenye uvumilivu zaidi kuliko ile ya mshindani wake, Shammai. Baada ya uharibifu wa hekalu la Yerusalemu katika 70 W.K., Bet Hillel (Nyumba ya Hillel) ilipendwa kuliko Bet Shammai (Nyumba ya Shammai). Nyumba ya Hillel ikawa wonyesho halali wa Dini ya Kiyahudi, kwa kuwa mafarakano mengine yote yalipotelea mbali pamoja na uharibifu wa hekalu. Maamuzi ya Bet Hillel mara nyingi ndiyo msingi wa sheria ya Kiyahudi katika Mishnah, ambayo ikawa msingi wa Talmud, na yaonekana uvutano wa Gamalieli ulikuwa jambo hasa lililofanya imani hiyo iongoze.
Gamalieli aliheshimiwa sana hivi kwamba alikuwa wa kwanza kuitwa raban, jina la cheo la juu kuliko la rabi. Kwa kweli, Gamalieli akawa mtu mwenye kustahiwa sana hivi kwamba Mishnah yasema hivi juu yake: “Raban Gamalieli mkubwa alipokufa utukufu wa Torah uliisha, na utakato na utakatifu [kihalisi “mtengano”] ukaisha.”—Sotah 9:15.
Alifundishwa na Gamalieli—Jinsi Gani?
Mtume Paulo alipouambia umati katika Yerusalemu kwamba alikuwa ‘amefundishwa miguuni pa Gamalieli,’ yeye alimaanisha nini? Ni nini kilichohusishwa katika kuwa mwanafunzi wa mwalimu kama Gamalieli?
Kuhusu mazoezi hayo, Profesa Dov Zlotnick wa Seminari ya Kitheolojia ya Kiyahudi ya Marekani aandika hivi: “Usahihi wa sheria ya mdomo, na basi kutegemeka kwayo, hutegemea karibu kabisa ule uhusiano kati ya bwana-mkubwa na mwanafunzi: ule uangalifu wa bwana-mkubwa afundishapo sheria na kule kuwa makini kwa mwanafunzi ajifunzapo. . . . Kwa hiyo wanafunzi walisihiwa sana waketi miguuni pa wasomi . . . ‘na kunywa maneno yao wakiwa na kiu.’”—Avot 1:4, Mishnah.
Katika kitabu chake A History of the Jewish People in the Time of Jesus Christ, Emil Schürer hutuelimisha juu ya njia za walimu wa kirabi wa karne ya kwanza. Yeye aandika hivi: “Mara nyingi wale Marabi maarufu zaidi walikusanya idadi kubwa za vijana waliotamani maagizo ili wawafahamishe kikamili ile ‘sheria ya mdomo’ yenye sehemu nyingi na yenye habari nyingi. . . . Hayo maagizo yalitia ndani mazoezi ya kumbukumbu yenye kuendelea daima. . . . Mwalimu aliwatolea wanafunzi wake maswali kadhaa ya kisheria ili yaamuliwe nao kisha akawaacha wayajibu au aliyajibu mwenyewe. Wanafunzi waliruhusiwa pia kumtolea mwalimu maswali.”
Kwa maoni ya marabi, wanafunzi walihangaikia mengi zaidi kuliko kupokea tu maksi za kupita. Wale waliokuwa wakijifunza chini ya walimu hao walionywa hivi: “Yeyote asahauye jambo lolote kati ya yale ambayo amejifunza—Andiko huonyesha kwamba astahili kufa.” (Avot 3:8) Sifa iliyo kubwa kupita zote ilipewa mwanafunzi aliyekuwa sawa na “kisima kilichokandikwa, ambacho hakipotezi tone la maji.” (Avot 2:8) Hiyo ndiyo aina ya mazoezi ambayo Paulo, ambaye kwa wakati huo alijulikana kwa jina lake la Kiebrania, Sauli wa Tarso, alipokea kutoka kwa Gamalieli.
Kusudi la Mafundisho ya Gamalieli
Kwa kufuata mafundisho ya Kifarisayo, Gamalieli aliendeleza itikadi katika sheria ya mdomo. Kwa njia hiyo alikazia mapokeo ya marabi zaidi kuliko Andiko lililopuliziwa. (Mathayo 15:3-9) Mishnah humnukuu Gamalieli kuwa akisema hivi: “Jipatie mwalimu [rabi] na hutakuwa na shaka, kwa kuwa hupaswi kutoa sehemu ya kumi ya ziada kwa sababu ya kukisia-kisia.” (Avot 1:16) Hilo lilimaanisha kwamba wakati ambapo Maandiko ya Kiebrania hayakusema waziwazi la kufanya, mtu hakupaswa kutumia kufikiri kwake mwenyewe au kufuata dhamiri yake ili kufanya uamuzi fulani. Badala ya hivyo, alipaswa kutafuta rabi astahiliye ambaye angemwamulia. Kulingana na Gamalieli, mtu angeepuka kutenda dhambi kwa njia hiyo tu.—Linganisha Warumi 14:1-12.
Hata hivyo, Gamalieli alijulikana kwa ujumla kuwa na mtazamo wenye uvumilivu zaidi, usiofuata sana mapokeo katika maamuzi yake halali ya kidini. Kwa kielelezo, aliwaonyesha wanawake ufikirio alipoamua kwamba yeye “angeruhusu mke aolewe tena kwa ushuhuda wa shahidi mmoja [wa kifo cha mumeye].” (Yevamot 16:7, Mishnah) Kwa kuongezea, ili kumlinda mwanamke aliyetalikiwa, Gamalieli alianzisha vizuizi kadhaa vya kutoa barua ya talaka.
Mtazamo huo usiofuata sana mapokeo huonekana pia katika mahusiano ya Gamalieli pamoja na wafuasi wa mapema wa Yesu Kristo. Kitabu cha Matendo husimulia kwamba viongozi wengine Wayahudi walipojaribu kuwaua mitume wa Yesu waliokuwa wamewakamata kwa sababu ya kuhubiri, “mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. . . . Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; . . . msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.” Shauri la Gamalieli lilisikiwa, nao mitume wakaachiliwa.—Matendo 5:34-40.
Mazoezi Aliyopata Paulo Yalimaanisha Nini Kwake?
Paulo alikuwa amezoezwa na kufundishwa na mmojapo walimu wa kirabi walio wakubwa zaidi wa karne ya kwanza W.K. Hakuna shaka kwamba rejezo la huyo mtume kwa Gamalieli lilifanya ule umati katika Yerusalemu uelekezee hotuba yake uangalifu wa pekee. Lakini aliwaambia kuhusu Mwalimu aliye bora zaidi kuliko Gamalieli—Yesu, yule Mesiya. Paulo aliuhutubia umati huo sasa akiwa mwanafunzi wa Yesu, wala si wa Gamalieli.—Matendo 22:4-21.
Je, kuzoezwa na Gamalieli kulikuwa na uvutano juu ya mafundisho ya Paulo akiwa Mkristo? Huenda, yale maagizo yenye mkazo katika Maandiko na sheria ya Kiyahudi yalithibitika kuwa yenye mafaa kwa Paulo akiwa mwalimu Mkristo. Hata hivyo, barua za Paulo zilizopuliziwa kimungu zipatikanazo katika Biblia huonyesha kwa wazi kwamba alikataa mafundisho ya msingi ya itikadi ya Kifarisayo ya Gamalieli. Paulo aliwaelekeza Wayahudi wenzake na wengine wote, si kwa marabi wa Dini ya Kiyahudi au kwa mapokeo yaliyofanyizwa na mwanadamu, bali kwa Yesu Kristo.—Warumi 10:1-4.
Ikiwa Paulo angaliendelea kuwa mwanafunzi wa Gamalieli, angalikuwa na cheo kikubwa. Wengine katika kikundi cha Gamalieli walisaidia katika kuamua wakati ujao wa Dini ya Kiyahudi. Kwa mfano, Simeoni, mwana wa Gamalieli, labda mwanafunzi pamoja na Paulo, alikuwa na fungu kubwa katika kuasi kwa Wayahudi dhidi ya Roma. Baada ya uharibifu wa hekalu, Gamalieli 2, mjukuu wa kiume wa Gamalieli, alirudisha mamlaka ya Sanhedrini, akiihamisha hadi Yavneh. Judah Ha-Nasi, mjukuu wa kiume wa Gamalieli 2, alikuwa mkusanyaji wa Mishnah, ambayo imekuwa jiwe la msingi la imani ya Kiyahudi kufikia siku yetu.
Akiwa mwanafunzi wa Gamalieli, Sauli wa Tarso huenda angalikuwa maarufu sana katika Dini ya Kiyahudi. Hata hivyo, kuhusu kazi-maisha hiyo, Paulo aliandika hivi: “Mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo.”—Wafilipi 3:7, 8.
Kwa kukataa kazi-maisha yake akiwa Farisayo na kuwa mfuasi wa Yesu Kristo, Paulo alikuwa akitumia kihalisi shauri la aliyekuwa mwalimu wake hapo awali la kujilinda dhidi ya ‘kuonekana kuwa wenye kupigana na Mungu.’ Kwa kuacha kunyanyasa kwake wanafunzi wa Yesu, Paulo aliacha kupigana na Mungu. Badala ya hivyo, kwa kuwa mfuasi wa Kristo, akawa mmoja wa “wafanya kazi pamoja na Mungu.”—1 Wakorintho 3:9.
Ujumbe wa Ukristo wa kweli waendelea kupigwa mbiu na Mashahidi wa Yehova wenye bidii katika siku yetu. Sawa na Paulo, wengi wao wamefanya mabadiliko makubwa maishani mwao. Baadhi yao hata wameacha kazi-maisha zenye matarajio mazuri ili washiriki hata zaidi katika utendaji wa kuhubiri Ufalme, ambao kwa kweli ni kazi ambayo “imetoka kwa Mungu.” (Matendo 5:39) Jinsi walivyo na furaha kwamba wamefuata kielelezo cha Paulo badala ya kile cha aliyekuwa mwalimu wake hapo awali, Gamalieli.
[Maelezo ya Chini]
a Vyanzo fulani husema kwamba Gamalieli alikuwa mwana wa Hillel. Talmud haisemi wazi kuhusu jambo hili.
[Picha katika ukurasa wa 28]
Akiwa mtume Paulo, Sauli wa Tarso alipiga mbiu ya habari njema kwa watu wa mataifa