“Mimi Nakata Rufani kwa Kaisari!”
KIKUNDI cha wafanya-ghasia chamkamata mtu fulani asiyeweza kujitetea na kuanza kumpiga. Wafanya-ghasia hao wafikiri kwamba mtu huyo anastahili kuuawa. Wakati tu inapoonekana kwamba mtu huyo atauawa na wafanya-ghasia hao wenye jeuri, askari watokea na wajitahidi sana kumwokoa mtu huyo. Mtu huyo ni mtume Paulo. Wafanya-ghasia hao wanaomshambulia ni Wayahudi ambao wanapinga vikali mahubiri ya Paulo na kumshtumu kwamba anatia hekalu unajisi. Watu wanaomwokoa ni Waroma, wakiongozwa na kamanda wao, Klaudio Lisiasi. Katika vurugu hiyo, Paulo anakamatwa kwa kushukiwa kuwa mtenda-maovu.
Sura saba za mwisho za kitabu cha Matendo zaonyesha kesi iliyoanza baada ya kukamatwa huko. Kuelewa malezi ya Paulo, mashtaka aliyofanyiwa, jinsi alivyojitetea, na jinsi Waroma walivyotoa adhabu kutatusaidia kuelewa sura hizo zaidi.
Azuiwa na Klaudio Lisiasi
Baadhi ya majukumu ya Klaudio Lisiasi yalitia ndani kudumisha amani jijini Yerusalemu. Mkubwa wa Lisiasi, gavana Mroma wa Yudea, aliishi Kaisaria. Hatua aliyochukua Lisiasi kuhusiana na Paulo yaonyesha kwamba alitaka kumlinda Paulo na pia kumweka kizuizini mtu aliyekuwa anavuruga amani. Kwa sababu ya itikio la Wayahudi, Lisiasi alimpeleka mfungwa wake kwenye kambi ya askari katika Mnara wa Antonia.—Matendo 21:27–22:24.
Ilimbidi Lisiasi achunguze kile Paulo alichokuwa amefanya. Hakujua chochote wakati wa mchafuko. Kwa hiyo pasipo kupoteza wakati, aliagiza kwamba Paulo ‘achunguzwe kwa kupigwa mijeledi, ili apate kujua kabisa ni kwa sababu gani walikuwa wakipaaza sauti dhidi ya Paulo.’ (Matendo 22:24) Hiyo ilikuwa njia ya kawaida ya kupata habari kutoka kwa wahalifu, watumwa, na watu wengine wa hali ya chini. Huenda mjeledi (flagrum) ulifaa kutimiza kusudi hilo, lakini ulikuwa kitu cha kuogofya. Baadhi ya mijeledi hiyo ilikuwa na vipande vya chuma vilivyoning’inia kwenye minyororo. Mingine ilikuwa na mikanda ya ngozi iliyosokotwa kwa mifupa yenye ncha kali na vipande vya chuma. Ilisababisha vidonda vibaya sana kwa kurarua-rarua ngozi.
Wakati huo, Paulo alieleza kwamba alikuwa raia wa Roma. Raia wa Roma ambaye hajahukumiwa hangeweza kupigwa mijeledi, kwa hiyo mara tu alipothibitisha haki zake, matokeo yakawa mazuri. Afisa Mroma angeweza kupoteza kazi yake kwa kumtendea vibaya au kumwadhibu raia wa Roma. Twaweza kuelewa ni kwa nini tokea wakati huo na kuendelea, Paulo alitendewa tofauti na wafungwa wengine, hata akaruhusiwa kupokea wageni.—Matendo 22:25-29; 23:16, 17.
Kwa kuwa Lisiasi hakujua mashtaka yangekuwaje, alimpeleka Paulo mbele ya Sanhedrini ili apate kuelezwa jambo lililosababisha makelele. Lakini Paulo alisababisha ubishi aliposema kwamba alikuwa anahukumiwa kwa sababu ya suala la ufufuo. Kulitokea ugomvi mkubwa sana hivi kwamba Lisiasi aliogopa kuwa Paulo angeraruliwa vipande-vipande, na kwa mara nyingine Lisiasi alilazimika kumwokoa Paulo mikononi mwa Wayahudi wenye hasira.—Matendo 22:30–23:10.
Lisiasi hakutaka kuhusika katika mauaji ya raia Mroma. Alipojua kwamba kuna njama ya kumwua Paulo, aliagiza mfungwa wake apelekwe Kaisaria haraka. Sheria ilidai kwamba wafungwa wanapopelekwa kwa mahakimu wenye cheo cha juu, ripoti zilizohusu kesi zao zipelekwe pia. Ripoti hizo zilitia ndani uchunguzi wa mwanzoni, sababu ya hatua zilizochukuliwa, na maoni ya mpelelezi kuhusu kesi hiyo. Lisiasi aliripoti kwamba Paulo alikuwa ‘ameshtakiwa juu ya maswali ya Sheria ya Wayahudi, lakini si kwa jambo lolote la kustahili kifo au vifungo,’ naye aliwaamuru watu waliomshtaki Paulo wapeleke malalamishi yao kwa ofisa Mroma, Feliksi.— Matendo 23:29, 30.
Gavana Feliksi Ashindwa Kutoa Hukumu
Utekelezaji wa sheria za jimbo ulitegemea mamlaka ya Feliksi. Iwapo angetaka angeweza kufuata desturi za huko au sheria ya mashtaka ya uhalifu iliyotumiwa kuwashtaki watu mashuhuri katika jamii na maofisa wa serikali. Mashtaka hayo ya jinai yaliitwa ordo, au orodha. Pia angeweza kutumia extra ordinem au sheria ya jimbo ambayo ingeweza kutumiwa kuamua kesi yoyote ya uhalifu. Gavana wa jimbo alitazamiwa ‘kufikiria si mambo yaliyofanyika huko Roma, bali kile kilichopaswa kufanywa kwa ujumla.’ Kwa hiyo, yeye ndiye aliyepaswa kufanya uamuzi.
Mambo yote yanayohusu sheria ya Waroma hayajulikani, lakini kesi ya Paulo huonwa kuwa ‘simulizi linaloonyesha jinsi sheria ya jimbo ilivyotumiwa.’ Gavana alisikiliza mashtaka kutoka kwa watu mmojammoja akisaidiwa na washauri. Mshtakiwa aliitwa akutane uso kwa uso na mshtaki wake, na angeweza kujitetea, lakini mlalamishi ndiye aliyekuwa na daraka la kuthibitisha mashtaka. Hakimu alitoa adhabu aliyoona kuwa inafaa. Angeweza kuamua mara moja au kuahirisha uamuzi hadi wakati usiojulikana, wakati huo mshtakiwa angezuiliwa. Msomi Henry Cadbury asema, “Basi haishangazi kwamba afisa Mroma aliyekuwa na mamlaka hiyo isiyo na msingi maalum angeweza kukubali ‘kushawishiwa isivyofaa’ na kuhongwa—ili aachilie mtu, amhukumu, au aahirishe hukumu.”
Kuhani wa Cheo cha Juu Anania, wanaume wazee Wayahudi, na Tertulo walimshtaki Paulo rasmi mbele ya Feliksi kuwa ‘msumbufu na mwenye kufanya uchochezi wa uasi miongoni mwa Wayahudi.’ Walidai kwamba alikuwa kiongozi mkuu wa “farakano la Wanazareti” na kwamba alijaribu kulichafua hekalu.—Matendo 24:1-6.
Watu waliomshambulia Paulo hapo awali walidhani kwamba Paulo alimwingiza Trofimo mtu asiye Myahudi, kwenye ua uliotengwa kwa ajili ya Wayahudi peke yao.a (Matendo 21:28, 29) Kwa kweli, Trofimo alijipeleka mwenyewe kwenye ua bila ruhusa. Lakini iwapo Wayahudi waliona kosa la Paulo kuwa ni kumsaidia mtu aingie kwenye ua bila ruhusa, basi kosa hilo lingefanya mtu ahukumiwe kifo. Na yaonekana Roma ilikubali hukumu ya kifo kwa kosa hilo. Kwa hiyo, iwapo Paulo angekamatwa na polisi Wayahudi wa hekalu badala ya kukamatwa na Lisiasi, Sanhedrini ingemshtaki na kumhukumu bila tatizo lolote.
Wayahudi walisababu kwamba Paulo hakufundisha Dini ya Wayahudi, au dini inayokubalika kisheria (religio licita). Badala yake, mambo aliyofundisha yalipaswa kuonwa kuwa haramu, au hata ya uchochezi.
Pia walidai kwamba Paulo alikuwa ‘akifanya uchochezi wa uasi miongoni mwa Wayahudi wote katika dunia yote inayokaliwa.’ (Matendo 24:5) Muda mfupi kabla ya hapo, Maliki Klaudio aliwashutumu Wayahudi wa Alexandria kwa “kuchochea usumbufu ulimwenguni pote.” Visa hivyo vinafanana sana. ‘Myahudi angeshtakiwa kwa kosa hilo wakati wa utawala wa Klaudio au miaka ya mapema ya utawala wa Nero,’ asema mwanahistoria A. N. Sherwin-White. “Wayahudi walikuwa wakijaribu kumchochea gavana aone mahubiri ya Paulo kuwa sawa na kuvuruga amani na utengamano miongoni mwa Wayahudi wote katika Milki yake. Walijua kwamba magavana hawakutaka kuhukumu mtu kwa sababu za kidini pekee na hivyo wakajaribu kufanya mashtaka hayo yaonekane kuwa ya kisiasa.”
Paulo alijitetea kwa kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine. ‘Sijasababisha usumbufu wowote. Ni kweli kwamba mimi ni mshiriki wa “farakano” kama wanavyoliita, lakini kuwa mshiriki wa farakano huonyesha kwamba mtu anafuata sheria za Wayahudi. Wayahudi fulani wa Asia ndio waliochochea ghasia hizo. Ikiwa wana malalamiko, wanapaswa kuja hapa na kuyataja.’ Kwa kweli Paulo alionyesha kwamba mashtaka hayo hayakuwa ya kisiasa bali ni mzozo tu wa kidini miongoni mwa Wayahudi, ambao Roma haingeweza kufanya chochote kuuhusu. Huku akiwa mwenye hadhari asiwaudhi Wayahudi wasiopenda kutawaliwa, Feliksi aliahirisha uamuzi huo wa mahakama na hivyo hakuna hatua yoyote ambayo ingeweza kuchukuliwa. Paulo hakukabidhiwa kwa Wayahudi waliodai kuwa na uwezo wa kuhukumu, wala hakuhukumiwa kwa Sheria ya Roma, wala hakuachiliwa. Feliksi hangelazimishwa kutoa hukumu, na mbali na kutaka kuwapendeza Wayahudi, alikuwa na sababu nyingine ya kuchelewesha mambo—alifikiri kwamba Paulo angemhonga.—Matendo 24:10-19, 26.b
Mambo Yabadilika Chini ya Porkio Festo
Huko Yerusalemu, Wayahudi walianzisha upya mashtaka yao miaka miwili baadaye wakati gavana mpya Porkio Festo alipowasili, wakiomba kwamba Paulo apelekwe katika jimbo lao. Lakini Festo alikataa katakata akisema: “Si utaratibu wa Kiroma kukabidhi mtu yeyote ili kujipendekeza kabla ya huyo mtu aliyeshtakiwa kukutana uso kwa uso na washtaki wake na kupata nafasi ya kujitetea kuhusu lalamiko.” Mwanahistoria Harry W. Tajra asema: “Festo alitambua kwamba watu walikuwa wakipanga njama za kumwua raia wa Roma.” Kwa hiyo Wayahudi waliambiwa wapeleke kesi yao Kaisaria.—Matendo 25:1-6, 16.
Huko Kaisaria Wayahudi walisisitiza kwamba Paulo ‘hakupaswa kuishi tena kamwe,’ hata hivyo hawakutoa uthibitisho wowote, naye Festo akaona kwamba Paulo hakuwa na hatia ya kufanya auawe. Festo alimweleza ofisa fulani kwamba, “Walikuwa tu na mabishano fulani pamoja naye kuhusu ibada yao wenyewe ya mungu na kuhusu mtu fulani Yesu aliyekuwa mfu lakini ambaye Paulo alifuliza kusisitiza kwamba alikuwa hai.”—Matendo 25:7, 18, 19, 24, 25.
Bila shaka, Paulo hakuwa na hatia ya shtaka lolote la kisiasa, lakini kuhusiana na mzozo wa kidini, yaelekea Wayahudi walidai kwamba mahakama yao pekee ndiyo iliyofaa kuamua kesi hiyo. Je, Paulo angeenda Yerusalemu ili akahukumiwe huko kuhusu mambo hayo? Festo alimwuliza Paulo kama atafanya hivyo, lakini kwa kweli hakupaswa kumpendekezea jambo hilo. Kurudishwa Yerusalemu ambako walalamishi ndio wangekuwa mahakimu kungemaanisha kwamba Paulo angekabidhiwa kwa Wayahudi. “Mimi nimesimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ambako napaswa kuhukumiwa,” akasema Paulo. “Sijawatendea Wayahudi kosa. . . Hakuna mtu awezaye kunikabidhi kwao ili kujipendekeza. Mimi nakata rufani kwa Kaisari!”—Matendo 25:10, 11, 20.
Raia wa Roma aliposema maneno kama hayo, hakuna mamlaka yoyote ya kisheria ya jimbo ambayo ingeweza kumshtaki. Haki yake ya kukata rufani (provocatio) ilikuwa “halisi, ilieleweka na ilifanikiwa.” Kwa hiyo baada ya kuzungumza na washauri wake kwa kindani kuhusu suala hilo, Festo alisema: “Kwa Kaisari umekata rufani; kwa Kaisari hakika wewe utaenda.”—Matendo 25:12.
Festo alifurahi kumwondoa Paulo mikononi mwake. Kama alivyokiri kwa Herode Agripa wa Pili siku kadhaa baadaye, alitatanishwa na kesi hiyo. Festo alipaswa kumwandikia maliki taarifa ya kesi hiyo, lakini Festo hakuelewa mashtaka hayo kwa kuwa yalihusu sheria tata ya Wayahudi. Hata hivyo, Agripa alikuwa stadi katika sheria, kwa hiyo alipoonyesha upendezi, aliombwa mara moja asaidie kuandika barua hiyo. Aliposhindwa kuelewa hoja ambazo Paulo alitoa baadaye akiwa mbele ya Agripa, Festo alipaza sauti na kusema: “Unashikwa na kichaa, Paulo! Kusoma kwingi kunakusukuma kuingia katika kichaa!” Lakini Agripa alielewa kabisa hoja hizo. “Kwa muda mfupi ungenishawishi niwe Mkristo,” akasema. Bila kujali walizionaje hoja za Paulo, Festo na Agripa walikubali kwamba Paulo hakuwa na hatia na kwamba angeweza kuachiliwa kama hangekuwa amekata rufani kwa Kaisari.—Matendo 25:13-27; 26:24-32.
Mwisho wa Mashtaka
Alipowasili Roma, Paulo aliwaita Wayahudi mashuhuri ili awahubirie na pia ajue walichofahamu kumhusu. Kwa kufanya hivyo huenda angejua nia ya washtaki wake. Lilikuwa jambo la kawaida kwa watu wenye mamlaka huko Yerusalemu kuwaomba Wayahudi Waroma wawasaidie kuamua kesi, lakini Paulo alipata habari kwamba hawakuwa wamepewa maagizo yoyote kumhusu. Alipokuwa akisubiri kuhukumiwa, Paulo alipewa ruhusa ya kukodisha nyumba na kuhubiri kwa uhuru. Kupatana na maoni ya Waroma, huenda fadhili hizo zilionyesha kwamba Paulo hakuwa na hatia.—Matendo 28:17-31.
Paulo alikaa rumande kwa miaka miwili zaidi. Kwa nini? Biblia haitoi habari zaidi. Kwa kawaida mkata rufani angeweza kuzuiliwa hadi washtaki wake wawakilishe mashtaka yao, lakini Wayahudi wa Yerusalemu hawakuja kwa kuwa walitambua kwamba kesi yao dhidi ya Paulo ilikuwa na kasoro. Labda njia ambayo ingekuwa bora kabisa ya kumnyamazisha Paulo kwa muda mrefu iwezekanavyo ilikuwa kususia kwenda. Vyovyote iwavyo, yaonekana Paulo alipelekwa mbele ya Nero, akatangazwa kuwa hana hatia, na hatimaye akaachiliwa ili aendelee na kazi yake ya mishonari—miaka mitano hivi baada ya kukamatwa.—Matendo 27:24.
Kwa muda mrefu wapinzani wa ile kweli ‘wametunga madhara kwa njia ya sheria’ ili kupinga kazi ya kuhubiri ya Kikristo. Hatupaswi kushangazwa na jambo hilo. Yesu alisema: “Ikiwa wameninyanyasa mimi, watawanyanyasa nyinyi pia.” (Zaburi 94:20; Yohana 15:20) Hata hivyo, Yesu pia anatuhakikishia uhuru wa kuhubiri habari njema ulimwenguni pote. (Mathayo 24:14) Kwa hiyo, kama vile mtume Paulo alivyopinga mnyanyaso na upinzani, Mashahidi wa Yehova leo ‘hutetea na kuthibitisha kisheria habari njema.’—Wafilipi 1:7.
[Maelezo ya Chini]
a Ukuta wa mawe uliojengwa vizuri, wenye urefu upatao sentimeta 24 ulitenganisha ua wa ndani na ua wa wasio Wayahudi. Maonyo yaliandikwa kwenye ukuta huo, baadhi yake kwa Kigiriki na mengine kwa Kilatini: “Mgeni yeyote haruhusiwi kuvuka ukuta au kuingia ndani ya ua unaozunguka patakatifu. Yeyote atakayekamatwa akifanya hivyo atauawa.”
b Bila shaka jambo hilo lilikuwa kinyume cha sheria. Kichapo kimoja chasema hivi: “Chini ya sheria inayohusu kutoza pesa kwa nguvu, Lex Repetundarum, mtu yeyote aliyekuwa na mamlaka au usimamizi fulani hakuruhusiwa kuomba au kukubali hongo ili kumfunga au kumfungua mtu, kumhukumu au kutomhukumu au kumwachilia mfungwa.”