Walifanya mapenzi ya yehova
Mwanamke Mwenye Busara Aepusha Msiba
MWANAMKE mwenye akili aliyeolewa na mwanamume asiyefaa—hiyo ilikuwa ndiyo hali ya Abigaili na Nabali. Abigaili alikuwa “mwenye akili njema, mzuri wa uso.” Kwa tofauti, Nabali alikuwa “hana adabu, tena mwovu katika matendo yake.” (1 Samweli 25:3) Matukio yaliyofuata yaliyowahusu wenzi hao wa ndoa wasiofaana yaliacha majina yao bila kufutika katika historia ya Biblia. Acha tuone jinsi gani.
Fadhili Bila Shukrani
Ilikuwa karne ya 11 K.W.K. Daudi alikuwa ametiwa mafuta awe mfalme wa wakati ujao wa Israeli, lakini badala ya kutawala alikuwa akitoroka. Sauli, mfalme aliyekuwa akitawala, alikusudia kumwua. Tokeo ni kwamba, Daudi alilazimika kuishi akiwa mtoro. Yeye pamoja na wenzake wapatao 600 hatimaye walipata kimbilio katika nyika ya Parani, kusini ya Yuda na kuelekea nyika ya Sinai.—1 Samweli 23:13; 25:1.
Wakiwa huko, walikutana na wachungaji walioajiriwa na mtu fulani aliyeitwa Nabali. Mzao huyu wa Kalebu aliye tajiri alikuwa na kondoo 3,000 na mbuzi 1,000, naye alikuwa akikata manyoya ya kondoo zake katika Karmeli, jiji lililo kusini ya Hebroni na labda karibu kilometa 40 tu kutoka Parani.a Daudi na watu wake waliwasaidia wachungaji wa Nabali kulinda makundi yao dhidi ya wezi waliokuwa wakitembea-tembea nyikani.—1 Samweli 25:14-16.
Kwa wakati huohuo, ukataji wa manyoya ya kondoo ulikuwa umeanza katika Karmeli. Huu ulikuwa wakati wa sherehe, sawa na kipindi cha mavuno kwa mkulima. Pia ulikuwa wakati wa kuonyesha ukarimu sana, wakati wenye kondoo wangewapa zawadi wale ambao walikuwa wamewafanyia kazi. Hivyo Daudi hakuwa na kimbelembele wakati alipowatuma watu wake kumi katika mji wa Karmeli kumwomba Nabali chakula kikiwa malipo kutokana na utumishi ambao waliufanya kwa niaba ya mifugo yake.—1 Samweli 25:4-9.
Jibu la Nabali halikuwa lenye ukarimu hata kidogo. “Daudi ni nani?” akauliza kwa dharau. Kisha, akionyesha kwamba Daudi na watu wake walikuwa watumishi watoro tu, aliuliza: “Je! nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi?” Daudi aliposikia hayo, aliwaambia watu wake: “Haya! jifungeni kila mtu upanga wake”! Karibu wanaume 400 walijitayarisha kwa pigano.—1 Samweli 25:10-13.
Busara ya Abigaili
Maneno ya matusi ya Nabali yalimfikia mke wake, Abigaili. Pengine hii haikuwa mara ya kwanza kwake kuingilia kati na kuwa mpatanishi kwa ajili ya Nabali. Kwa vyovyote vile, Abigaili alitenda mara moja bila ya kumwambia Nabali, alikusanya maandalio—kutia ndani kondoo watano na chakula kingi—akaenda kukutana na Daudi katika nyika.—1 Samweli 25:18-20.
Abigaili alipomwona Daudi, mara moja alijinyenyekeza kwake. “Usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali,” akamsihi. “Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu.” Aliongezea: “Hili [kuhusu Nabali] halitakuwa kwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu.” Neno la Kiebrania hapa litafsiriwalo “kwazo” humaanisha usumbufu wa dhamiri. Hivyo Abigaili alimwonya Daudi dhidi ya kuchukua hatua ya haraka ambayo baadaye ingemfanya ajute.—1 Samweli 25:23-31.
Daudi alimsikiliza Abigaili. “Na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu,” akamwambia. “Ikiwa hungefanya haraka ili kukutana na mimi, kwa hakika Nabali asingebakiwa na yeyote akojoaye ukutani kufikia nuru ya asubuhi.”b—1 Samweli 25:32-34, linganisha NW.
Masomo Kwetu
Habari hii ya Biblia yaonyesha kwamba kwa hakika si kosa kwa mwanamke wa kimungu kuchukua hatua inayofaa ikiwa inahitajika. Abigaili alitenda dhidi ya mapendezi ya mume wake, Nabali, lakini Biblia haimlaumu kwa jambo hili. Kinyume cha hilo, inamsifu kuwa mwanamke mwenye busara na akili. Kwa kuchukua hatua ya kwanza katika tatizo hilo, Abigaili aliokoa uhai wa wengi.
Ingawa kwa ujumla mwanamke apaswa kuonyesha mtazamo wa ujitiisho wa kimungu, huenda kwa kufaa asikubaliane na mume wake kanuni adilifu zinapohatarishwa. Bila shaka, apaswa kujitahidi kudumisha “roho ya utulivu na ya upole” na hapaswi kutenda kwa kujitegemea kwa sababu tu ya chuki, kiburi, au uasi. (1 Petro 3:4) Lakini, mke wa kimungu hapaswi kuhisi kusongwa kufanya jambo lolote ambalo ajua si busara kabisa au ni lenye kuvunja kanuni za Biblia. Kwa kweli, habari ya Abigaili yatoa majadiliano imara dhidi ya wale wasisitizao kwamba Biblia yawaonyesha wanawake kuwa ni watumwa tu.
Habari hii pia yatufunza kuhusu kujidhibiti. Nyakati nyingine, Daudi alionyesha sifa hii kwa ukamili. Kwa kielelezo, alikataa kumwua Mfalme Sauli mwenye kisasi, ingawa alikuwa na fursa nzuri ya kumwua na kifo cha Sauli kingemletea Daudi amani. (1 Samweli 24:2-7) Kwa kutofautisha, Nabali alipomtukana kwa dharau, Daudi alikosa kuwa macho na aliapa kulipiza kisasi. Hili ni onyo la wazi kwa Wakristo, ambao hujitahidi ‘kutorudisha ovu kwa ovu kwa yeyote.’ Katika hali zote, wapaswa kufuata onyo la upole la Paulo: “Ikiwezekana, kwa kadiri itegemeavyo nyinyi, iweni wenye kufanya amani na watu wote. Wapendwa, msijilipizie kisasi wenyewe bali iachieni nafasi hasira ya kisasi.”—Waroma 12:17-19.
[Maelezo ya Chini]
a Nyika ya Parani yaeleweka kuwa yasambaa kuelekea kaskazini hadi Beer-sheba. Sehemu hii ya bara ilitia ndani eneo kubwa la malisho.
b Fungu la maneno “yeyote akojoaye ukutani” lilikuwa msemo wa Kiebrania umaanishao wanaume, waonekana ulikuwa msemo wa dharau.—Linganisha 1 Wafalme 14:10.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Abigaili amletea Daudi zawadi