Sura Ya Nne
Jinsi Ulivyo Kiumbe cha Kipekee!
KABLA ya kuanza shughuli zako kila asubuhi, je, wewe hujiangalia kwenye kioo? Pindi hiyo, huenda usiwe na wakati wa kutafakari. Lakini, chukua wakati sasa ustaajabie mambo yanayohusika unapojitazama tu kifupi.
Macho yako hukuwezesha kujiona kwa rangi kamili, hata ingawa uwezo wa kuona rangi mbalimbali si muhimu kwa uhai. Mahali yalipo masikio yako hukuwezesha kusikia sauti kutoka sehemu zote; hivyo, waweza kutambua sauti hizo, kama vile sauti ya mtu umpendaye. Huenda tukaliona jambo hilo kivivi hivi tu, lakini kitabu cha wataalamu wa sauti chasema hivi: “Kwa kuchunguza mfumo wa kusikia wa binadamu kwa makini sana, ni rahisi kukata kauli ya kwamba utendaji wake na miundo yake yenye kutatanisha sana ilitokezwa na mtu fulani.”
Pua yako pia imebuniwa kwa njia ya kustaajabisha. Kupitia pua yako unaweza kupumua hewa, ambayo huendeleza uhai wako. Pia ina mamilioni ya vipokezi vya hisi, ambavyo hukuwezesha kutambua aina 10,000 za harufu. Unapofurahia mlo, hisi nyingine huhusika. Maelfu ya vionjio vilivyo katika ulimi hukupa ladha. Vitu vingine katika ulimi wako hukusaidia kuhisi ikiwa meno yako ni safi.
Ndiyo, una hisi tano za utambuzi—kuona, kusikia, kunusa, kuonja, na kugusa. Ni kweli kwamba wanyama fulani wanaona vizuri zaidi wakati wa usiku, wengine wana uwezo mkubwa zaidi wa kunusa, au wengine wana masikio makali zaidi, lakini jinsi ambavyo mwanadamu amesawazisha hisi hizo kwa hakika zamfanya awe bora kwa njia nyingi.
Lakini, ebu tuchunguze kwa nini tunaweza kunufaika na uwezo huo mbalimbali. Hisi hizo zote hutegemea kiungo kimoja chenye uzito wa kilogramu 1.4 kilichomo ndani ya kichwa chetu—ubongo wetu. Wanyama wana ubongo wenye kutenda. Lakini, ubongo wa binadamu unashinda wa wanyama kwa mbali sana, jambo ambalo kwa wazi linafanya tuwe viumbe vya kipekee. Kwa njia gani? Na kuwa kwetu viumbe vya kipekee kunahusianaje na kutaka kwetu kuwa na maisha yenye maana zaidi na yenye kudumu?
Ubongo Wako Wenye Kustaajabisha
Kwa miaka mingi ubongo wa mwanadamu umefananishwa na kompyuta, lakini mambo yaliyogunduliwa karibuni yanaonyesha kwamba ulinganifu wa ubongo na kompyuta haufai hata kidogo. “Mtu hata anawezaje kuanza kufahamu utendaji wa kiungo ambacho kina chembe za neva zipatazo bilioni 50 ambazo nazo zina miunganisho ipatayo bilioni milioni moja, na yenye utendaji wa ujumla wa labda bilioni milioni 10 kwa sekunde moja?” akauliza Dakt. Richard M. Restak. Yeye alijibuje? “Uwezo wa hata kompyuta za hali ya juu zaidi ambazo zinaiga utendaji wa ubongo . . . unashindwa na uwezo wa ubongo wa nzi kwa mara elfu kumi.” Basi, fikiria kadiri ambayo kompyuta inashindwa kufikia ubongo wa binadamu, ambao ni wa hali ya juu kabisa.
Ni kompyuta gani ambayo imetengenezwa na binadamu iwezayo kujirekebisha, ijiratibu yenyewe, au hata kujiboresha kadiri wakati upitavyo? Mfumo wa kompyuta unapohitaji kurekebishwa, ni lazima mtayarishaji wa programu aandike na kuingiza maagizo mapya katika mfumo huo. Ubongo wetu hufanya kazi hiyo peke yake, katika umri mchanga na vilevile katika umri wa uzee. Si kutia chumvi kusema kwamba kompyuta za hali ya juu zaidi ni bure sana kwa kulinganisha na ubongo. Wanasayansi wameuita ubongo “kitu tata zaidi kijulikanacho” na “kitu tata zaidi ulimwenguni.” Ebu fikiria baadhi ya ugunduzi ambao umefanya wengi wakate kauli ya kwamba ubongo wa binadamu umefanyizwa na Muumba mwenye kujali.
Utumie Ubongo Wako au Uupoteze
Uvumbuzi wenye mafaa kama vile magari na ndege hasa hudhibitiwa na injini na mifumo ya umeme isiyobadilika ambayo imetengenezwa na kuwekwa na wanadamu. Kwa kutofautisha, ubongo wetu ni angalau mfumo wa kibiolojia wenye kubadilikana sana. Huo unaweza kuendelea kubadilikana kulingana na jinsi unavyotumiwa vizuri—au vibaya. Inaonekana kwamba mambo makuu mawili huchangia jinsi ambavyo ubongo wetu husitawi katika maisha yetu yote—kile tunachoruhusu kiingie katika ubongo wetu kupitia hisi zetu na kile tunachochagua kufikiria.
Ingawa urithi waweza kuchangia uwezo wa akili zetu, utafiti wa kisasa waonyesha kwamba ubongo wetu haudhibitiwi na chembe zetu za urithi mimba itungwapo. “Hakuna mtu aliyefikiria kwamba ubongo wetu ungeweza kubadilikana kama vile sayansi inavyojua sasa,” aandika mwandikaji wa vitabu Ronald Kotulak aliyeshinda tuzo la Pulitzer kwa sababu ya uandishi. Baada ya kuwahoji watafiti 300, yeye alikata kauli hivi: “Ubongo wetu si kitu ambacho hakibadilikani; huo umefanyizwa kwa miunganisho mingi ya chembe ambayo hubadilikana daima na kuathiriwa na mambo yanayoipata.”—Inside the Brain.
Na si mambo yanayotupata pekee yanayoathiri ubongo wetu. Ubongo pia huathiriwa na mawazo yetu. Wanasayansi wamepata kwamba ubongo wa watu ambao hudumisha utendaji wa kiakili una miunganisho mingi zaidi kati ya chembe za neva kuliko ubongo wa watu wazembe kiakili kwa asilimia 40. Wanasayansi wa ubongo wakata kauli hii: Ni lazima utumie ubongo au uupoteze. Lakini, namna gani juu ya walio wazee kwa umri? Inaonekana kwamba ubongo hupoteza chembe fulani mtu anapoendelea kuzeeka, na umri mkubwa sana waweza kumfanya mtu awe msahaulifu. Lakini huo ni upotezo kidogo sana kuliko ilivyodhaniwa hapo awali. Ripoti moja ya National Geographic juu ya ubongo wa binadamu ilisema: “Watu wenye umri wa uzee . . . hudumisha uwezo wa kufanyiza miunganisho mipya katika ubongo na kudumisha miunganisho ya zamani kupitia utendaji wa akili.”
Mambo yaliyogunduliwa karibuni kuhusu uwezo wa ubongo wetu wa kubadilikana wapatana na shauri linalopatikana katika Biblia. Kitabu hiki cha hekima kinawahimiza wasomaji wake ‘wageuzwe umbo kwa kufanya upya akili’ au ‘kufanywa kuwa mpya’ kupitia “ujuzi sahihi” unaoingizwa akilini. (Waroma 12:2; Wakolosai 3:10) Mashahidi wa Yehova wameona jambo hilo watu wanapojifunza Biblia na kutumia shauri lake. Maelfu ya watu—wa hali zote za maisha—wamefanya hivyo. Wao hudumisha utu wao, lakini sasa wamekuwa wenye furaha na wenye usawaziko zaidi, wakionyesha kile ambacho mwandikaji mmoja wa karne ya kwanza alikiita “utimamu wa akili.” (Matendo 26:24, 25) Maendeleo kama hayo hutokea kwa sababu ya kutumia utando wa bongo kubwa ulio katika sehemu ya mbele ya kichwa.
Sehemu ya Mbele ya Bongo Kubwa
Nyingi za chembe za neva zilizo katika utando wa bongo kubwa, hazijaunganika moja kwa moja na misuli na viungo vya utambuzi. Kwa mfano, ebu fikiria yale mabilioni ya chembe za neva ambazo zimefanyiza sehemu ya mbele ya bongo kubwa. (Ona mchoro, kwenye ukurasa wa 56.) Uchunguzi unaofanyiwa ubongo wathibitisha kwamba sehemu ya mbele ya bongo kubwa huwa yenye utendaji wakati unapofikiria neno au kukumbuka mambo. Sehemu ya mbele huchangia fungu muhimu la kukufanya uwe jinsi ulivyo.
“Utando wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa . . . huhusika sana katika kuchanganua kabisa mawazo, akili, kichocheo, na utu. Sehemu hiyo hushirikisha mambo yanayoonwa maishani ambayo ni muhimu katika kufikiria mambo, kufanya uamuzi, kuwa mwenye udumifu, kupangia mambo, kuwahangaikia wengine, na dhamiri. . . . Uchanganuzi wa habari katika sehemu hii ndio huwafanya wanadamu wawe tofauti na wanyama wengine.” (Human Anatomy and Physiology cha Marieb) Kwa kweli twaona uthibitisho wa tofauti hii kati ya wanadamu na wanyama kwa kutazama matimizo ya mwanadamu katika mambo kama hesabu, falsafa, na haki, mambo ambayo kwa msingi hutegemea utando wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa.
Kwa nini wanadamu wana utando mkubwa wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa, ambao ni wenye kubadilikana, na ambao huchangia sana kufikiri kwa hali ya juu, ilhali katika wanyama sehemu hiyo ni ndogo sana au hata haipo kabisa? Tofauti hiyo ni kubwa sana hivi kwamba wanabiolojia wanaosema kwamba sisi tumetokea kupitia mageuzi husema juu ya “ukuzi mkubwa sana wa ghafula wa ubongo wa binadamu.” Profesa wa Biolojia Richard F. Thompson, akisema juu ya ukubwa usio wa kawaida wa utando wa bongo kubwa wa binadamu, akiri hivi: “Kufikia sasa hatuelewi kabisa ni kwa nini jambo hili lilitukia.” Je, inawezekana sababu ni kwamba mwanadamu aliumbwa akiwa na ubongo wenye uwezo mkubwa usio na kifani?
Ubongo Hauna Kifani kwa Stadi za Kuwasiliana
Sehemu nyinginezo za ubongo pia huchangia kuwa kwetu viumbe vya kipekee. Nyuma ya utando wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa kuna ukanda unaovuka juu ya ubongo—ule utando unaoongoza miendo ya misuli. Huo una mabilioni ya chembe za neva ambazo zimeunganishwa kwa misuli yetu. Pia una sehemu mbalimbali zinazofanya tuwe tofauti kabisa na nyani au wanyama wengine. Utando mkuu wa kuongoza miendo ya misuli hutupatia “(1) uwezo bora sana wa kutumia mikono, vidole, na kidole gumba ili kutimiza mambo yanayohitaji ustadi sana, na (2) matumizi ya kinywa, midomo, ulimi, na misuli ya uso ili kuweza kuzungumza.”—Textbook of Medical Physiology cha Guyton.
Ebu fikiria kifupi jinsi utando huo wa kudhibiti miendo ya misuli unavyohusiana na uwezo wako wa kuzungumza. Zaidi ya nusu ya sehemu hiyo hudhibiti viungo vya mawasiliano pekee. Jambo hili lasaidia kuelewa sababu inayofanya wanadamu wawe na stadi zisizo na kifani za kuwasiliana. Ingawa mikono yetu inatimiza fungu kubwa katika kuwasiliana (katika maandishi, ishara za kawaida, au lugha ya ishara), mara nyingi mdomo huchangia sehemu kubwa sana. Usemi wa mwanadamu—tokea neno la kwanza la mtoto mchanga hadi sauti ya mtu aliye mzee kwa umri—ni ajabu sana isiyotilika shaka. Misuli ipatayo 100 iliyo katika ulimi, midomo, utaya, koo, na kifua hushirikiana ili kutokeza sauti mbalimbali. Ebu tazama tofauti hii: Chembe moja ya ubongo inaweza kuongoza nyuzi 2,000 zilizo katika msuli mmoja wa shavu la mguu la mwanariadha lakini chembe za ubongo zenye kuongoza zoloto zaweza kuongoza nyuzi 2 tu au 3 za msuli. Je, hilo halidokezi kwamba ubongo wetu umeandaliwa kwa njia ya kipekee kwa ajili ya mawasiliano?
Kila fungu la maneno mafupi ambayo wewe hutamka huhitaji mwendo fulani hususa wa misuli. Maana ya neno moja yaweza kubadilika kwa kutegemea kadiri ya mwendo na kuingiliana barabara kabisa kwa misuli mingine mingi. “Kwa kawaida,” aeleza mtaalamu wa usemi Dakt. William H. Perkins, “sisi hutamka karibu sauti 14 kwa sekunde moja. Hiyo inashinda kwa mara mbili uwezo wetu wa kudhibiti ulimi, midomo, utaya au sehemu yoyote ya usemi tunapozisogeza zikiwa tofauti-tofauti. Lakini ukitumia sehemu hizo zote pamoja ili zitokeze usemi, hizo hutenda kama vidole vya mstadi wa kuchapa taipu na jinsi ambavyo vidole vya wacheza-piano hucheza. Miendo yao hutokeza mchanganyiko uliopimwa barabara.”
Ile habari hasa inayohitajika ili kuuliza tu swali rahisi, “Hujambo leo?” imehifadhiwa katika eneo fulani la sehemu ya mbele ya bongo kubwa liitwalo eneo la Broca, ambalo wengine huliona kuwa kitovu cha usemi. Mshindi wa tuzo la Nobeli aliye mwanasayansi wa ubongo, Sir John Eccles aliandika: “Hakuna eneo lolote linalolingana . . . na eneo la usemi la Broca ambalo limetambuliwa katika nyani.” Hata kama sehemu nyinginezo zinazofanana na hizo zinapatikana katika wanyama, ukweli ni kwamba wanasayansi hawawezi kuwafundisha nyani watokeze usemi ila tu sauti chache tu rahisi. Lakini, wewe unaweza kutokeza lugha yenye mambo mengi sana. Ili kufanya hivyo, unapanga maneno yako kulingana na sarufi ya lugha yako. Eneo la Broca hukusaidia kufanya hivyo, katika usemi na katika maandishi.
Bila shaka, huwezi kudhihirisha muujiza huu wa usemi ila tu uwe unafahamu angalau lugha moja na kuelewa maana ya maneno yake. Hilo lahusisha sehemu nyingine ya pekee ya ubongo wako, ambayo huitwa eneo la Wernicke. Hapa, mabilioni ya chembe za neva hutambua maana na maneno yanayozungumzwa au kuandikwa. Eneo la Wernicke hukusaidia kuelewa maneno na kufahamu yale unayoyasikia au kusoma; likikusaidia kuweza kujifunza habari na kutenda ifaavyo.
Kuna mambo mengi hata zaidi yanayohusu usemi wenye ufasaha. Kwa mfano: Kusema “Hujambo” kwaweza kutokeza maana tofauti-tofauti. Sauti yako yaonyesha ikiwa umefurahi, umesisimuka, umechoshwa, una shughuli nyingi, umekasirika, una huzuni, au unaogopa, na pia inaweza kufunua kiwango cha kihisia-moyo cha hisia hizo. Eneo jingine la ubongo wako huandaa habari za hali yako ya kihisia-moyo katika usemi wako. Kwa hiyo sehemu mbalimbali za ubongo wako huhusika unapowasiliana.
Sokwe wengine wamefunzwa kutoa ishara chache, lakini ishara hizo ni za kuomba chakula au mambo mengine ya msingi pekee. Baada ya kufundisha sokwe mawasiliano rahisi ya ishara, Dakt. David Premack alikata kauli hivi: “Lugha ya wanadamu inafedhehesha sana nadharia ya mageuzi kwa sababu hiyo [lugha] ina uwezo sana kuliko inavyoweza kufafanuliwa.”
Huenda tukajiuliza: ‘Kwa nini wanadamu wana ustadi huu wa ajabu wa kuwasilisha mawazo na hisia, wa kuulizia na kuitikia?’ Kitabu The Encyclopedia of Language and Linguistics chasema kwamba “usemi wa [wanadamu] ni wa kipekee” nacho chakiri kwamba “utafutaji wa usemi wa awali katika mawasiliano ya wanyama hausaidii kuziba lile pengo kubwa lililopo kati ya lugha [ya wanadamu] na sauti za wanyama.” Profesa Ludwig Koehler alitaja kifupi tofauti iliyopo: “Usemi wa binadamu ni siri; ni zawadi ya Mungu, na muujiza.”
Kuna tofauti kubwa kama nini kati ya jinsi nyani atumiavyo ishara na uwezo mkubwa wa lugha ya watoto! Sir John Eccles alirejezea kile ambacho wengi wetu tumeona, uwezo “udhihirishwao na hata watoto wenye umri wa miaka 3 waulizapo maswali mengi wakitaka kuelewa mambo mengi wanayoyaona.” Yeye aliongezea: “Kwa kutofautisha, nyani hawaulizi maswali.” Ndiyo, ni wanadamu pekee waulizao maswali, kutia ndani maswali kuhusu maana ya maisha.
Kumbukumbu na Mengi Zaidi!
Utazamapo kioo, huenda ukafikiria jinsi ulivyofanana ulipokuwa mchanga, na hata kulinganisha hali hiyo na jinsi utakavyofanana miaka ijayo au jinsi ambavyo ungalifanana kwa kutumia vipodozi. Mawazo hayo yanaweza kutokea tu bila wewe kufahamu, lakini kuna kitu cha kipekee kinachotukia, kitu ambacho hakuna mnyama awezaye kuwa nacho.
Tofauti na wanyama, ambao hasa huishi na kutegemea mahitaji ya sasa, wanadamu wanaweza kutafakari yaliyopita na kupangia wakati ujao. Jambo linalokuwezesha kufanya hivyo ni uwezo mkubwa sana wa ubongo wako wa kukumbuka. Ni kweli kwamba wanyama wana kadiri fulani ya kumbukumbu, na hivyo wao waweza kukumbuka njia ya kurudi nyumbani au kukumbuka mahali pa kupata chakula. Kumbukumbu ya mwanadamu ni kubwa sana. Mwanasayansi mmoja alikadiria kwamba ubongo wetu unaweza kubeba habari ambazo “zinaweza kujaza mabuku yapatayo milioni ishirini, yaani yanayotoshana na vitabu vyote vilivyo katika maktaba kubwa zaidi za ulimwengu.” Wanasayansi fulani wa ubongo wakadiria kwamba katika maisha ya wastani, mtu hutumia sehemu 1 tu kati ya 10,000 (.0001) ya uwezo wa ubongo wake. Huenda ukajiuliza, ‘Kwa nini tuna ubongo wenye uwezo mkubwa hivyo ambao hatutumii hata sehemu kidogo sana yake katika muda wote wa maisha?’
Wala ubongo wetu si kama ghala kubwa tu ya habari, kama ilivyo kompyuta kubwa sana. Profesa wa biolojia Robert Ornstein na Richard F. Thompson waliandika: “Uwezo wa akili ya wanadamu wa kujifunza—kuhifadhi na kukumbuka habari—ndilo jambo lenye kutokeza sana katika vitu vyote vilivyo hai ulimwenguni. Kila kitu kitufanyacho kuwa wanadamu—lugha, mawazo, ujuzi, utamaduni—ni tokeo la uwezo huu mkubwa ajabu.”
Isitoshe, una akili yenye fahamu. Taarifa hiyo inaweza kuonekana kuwa rahisi sana, lakini inaonyesha jambo ambalo linakufanya uwe kiumbe cha kipekee. Akili imefafanuliwa kuwa “kitu kisichojulikana ambamo umo uwezo wa kufikiri, wa kufanya maamuzi, wa ufahamu na hali ya kujitambua kuwa wewe ni mwanadamu.” Kama vile vijito, na mito iingiavyo baharini, ndivyo kumbukumbu, mawazo, picha, sauti, na hisi ziingiavyo au kupitia akili zetu daima. Kuwa na fahamu, yasema kamusi moja, ni “hali ya mtu kutambua kile kinachopitia akilini mwake.”
Watafiti wa kisasa wamepiga hatua kubwa ya kuelewa muundo wa ubongo na baadhi ya utaratibu wa kemia na umeme ambao hutukia ndani yake. Wao pia waweza kufafanua miunganisho na utendaji wa kompyuta za hali ya juu. Lakini, kuna tofauti kubwa sana kati ya ubongo na kompyuta. Kwa kutumia ubongo wako wewe una fahamu na unajua ya kwamba uko hai, lakini kompyuta haijijui. Kwa nini kuna tofauti hiyo?
Kwa wazi, jinsi gani na kwa nini fahamu inatokana na utendaji katika ubongo wetu ni fumbo lisilojulikana. “Sioni vile sayansi yoyote inavyoweza kufafanua hilo,” mtaalamu mmoja wa ubongo akasema. Pia, Profesa James Trefil alionelea: “Kile ambacho hasa kinamaanishwa na binadamu kuwa na fahamu . . . ni swali pekee lililo kuu katika sayansi ambalo hatujui hata jinsi ya kuliuliza.” Sababu moja ni kwamba wanasayansi wanatumia ubongo kujaribu kuelewa ubongo. Na kujifunza tu utendaji wa ubongo huenda kusitoshe. Hali ya kuwa na fahamu ni “mojawapo ya mafumbo makubwa zaidi katika maisha,” asema Dakt. David Chalmers, “lakini kujua tu jinsi ubongo utendavyo hakuwezi kuwafanya [wanasayansi] wapate jawabu.”
Hata hivyo, kila mmoja wetu ana fahamu. Kwa mfano, kumbukumbu zetu dhahiri juu ya mambo yaliyopita si mambo ya kuhifadhiwa tu, kama habari za kompyuta. Tunaweza kutafakari juu ya mambo yaliyopita, tujifunze kutokana na mambo hayo, kisha tuyatumie kuboresha wakati wetu ujao. Tuna uwezo wa kufikiria hali kadhaa za wakati ujao na kuchanganua jinsi kila mojawapo ya hali hizo iwezavyo kutuathiri. Tuna uwezo wa kuchanganua, kufanyiza, kuthamini, na kupenda. Tunaweza kufurahia mazungumzo yenye kufurahisha kuhusu wakati uliopita, wakati huu, na wakati ujao. Tuna maadili ya tabia na tunaweza kuyatumia kufanya maamuzi ambayo huenda yakaleta manufaa ya haraka au hapana. Tunavutiwa na umaridadi wa michoro na maadili. Akilini mwetu tunaweza kuwazia na kurekebisha mawazo yetu na kufikiria jinsi watu wengine watakavyotenda tukiyafanya.
Mambo kama hayo hutokeza fahamu ambayo hutenganisha wanadamu na viumbe vingine duniani. Mbwa, paka, au ndege hutazama kioo na kutenda kana kwamba ameona mwingine wa jinsi yake. Lakini utazamapo kioo, wewe una fahamu ya kwamba ni wewe ndiye una ule uwezo mbalimbali ambao umetajwa. Unaweza kuwazia mambo yenye kutatanisha, kama vile: ‘Kwa nini kasa wengine huishi kwa miaka 150 na miti mingine kuishi kwa zaidi ya miaka 1,000, lakini linakuwa jambo la kipekee kwa mwanadamu kufikia umri wa miaka 100?’ Dakt. Richard Restak asema: “Ubongo wa mwanadamu, na ni ubongo wa mwanadamu pekee, ndio una uwezo wa kufikiri na kuchunguza uwezo wake, na hivyo kufikia kadiri fulani ya upekee. Kwa kweli, uwezo wetu wa kufikiria tena mipango yetu na kujirekebisha katika ulimwengu ndio unaotutofautisha na viumbe vingine vyote ulimwenguni.”
Hali ya mwanadamu kuwa na fahamu hushangaza watu fulani. Ingawa kitabu Life Ascending kinapendelea kufafanua hali ya mwanadamu kuwa na fahamu kwa njia ya biolojia, hicho chakiri hivi: “Tuulizapo jinsi ambavyo mfumo mmoja [mageuzi] ambao unafanana na mchezo wa nasibu, wenye adhabu kali sana kwa wanaoshindwa, ungetokeza sifa kama kupenda urembo na kweli, huruma-nyororo, uhuru, na, zaidi ya yote, uwezo mkubwa sana wa mtazamo wa binadamu, tunaduwaa. Kadiri tufikirivyo juu ya uwezo wetu wa kuwa wa kiroho, ndivyo tuzidivyo kushangaa.” Huo ni ukweli mtupu. Basi, twaweza kukata kauli juu ya upekee wa mwanadamu kwa kupitia uthibitisho mchache wa fahamu ambao unathibitisha sababu ambayo imefanya wengi wasadiki kwamba ni lazima kuwe na Mbuni mwenye akili, Muumba, ambaye anatujali.
Sanaa na Umaridadi
“Kwa nini watu hupenda sanaa sana?” akauliza Profesa Michael Leyton katika kitabu Symmetry, Causality, Mind. Kama alivyotaja, huenda wengine wakasema kwamba utendaji wa akili kama vile hesabu hunufaisha wanadamu kwa njia ya wazi, lakini sanaa inanufaishaje? Leyton alitoa mfano wa jambo analokazia kwa kusema kwamba watu husafiri mbali sana ili kuhudhuria maonyesho ya sanaa na ya muziki. Ni hisi gani ya ndani ambayo imehusika? Vivyo hivyo, watu duniani pote huweka picha au michoro ya rangi yenye kuvutia kwenye kuta za nyumba zao au ofisi zao. Au fikiria muziki. Watu wengi hupenda kusikiliza muziki wa aina fulani nyumbani na katika magari yao. Kwa nini? Kamwe si kwa sababu pindi moja muziki ulichangia kusalimika kwa viumbe bora. Asema Leyton: “Sanaa labda ni mojawapo ya mambo ya wanadamu ambayo hayawezi kuelezeka.”
Na bado, sisi sote twajua kwamba kufurahia sanaa na umaridadi ni sehemu ya kile kinachotufanya tuhisi sisi ni “binadamu.” Mnyama aweza kuketi kwenye kilima na kutazama anga lenye rangi, lakini je, kweli yeye anavutiwa na umaridadi huo? Twatazama kijito cha mlimani kikimetameta kwenye jua, twatazama viumbe tofauti-tofauti vyenye kuvutia katika msitu wa mvua katika tropiki, twatazama ufuo wenye minazi, au kustaajabia nyota zilizotapakaa kotekote katika anga jeusi kama mahameli. Mara nyingi sisi hustaajabu sana, sivyo? Umaridadi wa aina hiyo hufanya mioyo yetu ichangamke, na kutufurahisha. Kwa nini?
Kwa nini sisi hutamani sana kiasili mambo ambayo, kwa uhalisi, hayachangii uhai wetu? Mapendezi hayo ya umaridadi yanatoka wapi? Ikiwa twampuuza Mfanyi ambaye aliingiza mapendezi hayo wakati wa kuumba mwanadamu, maswali hayo yanakosa majibu yenye kuridhisha. Ndivyo ilivyo pia kuhusu wema wa maadili.
Maadili
Wengi hutambua kwamba uzuri mkubwa zaidi ni matendo mema. Kwa mfano, kushikamana na kanuni unaponyanyaswa, kuondoa mateseko ya wengine bila ubinafsi, na kusamehe mtu anayetuumiza ni matendo ambayo yanavutia maadili ya watu wenye kufikiri kila mahali. Aina hii ya uzuri inatajwa na mithali moja ya kale ya Biblia: “Busara ya mtu huiahirisha hasira yake; nayo ni fahari yake kusamehe makosa.” Au kama vile mithali nyingine isemavyo: “Mahitaji ya mutu ni wema wake.”—Mithali 19:11, 22, linganisha Zaire Swahili Bible.
Sote twajua kwamba watu fulani, na hata vikundi, hupuuza au kukataa maadili, lakini watu wengi hawayakatai. Hayo maadili ambayo yanapatikana katika karibu kila eneo na katika pindi zote yalitoka wapi? Ikiwa hakuna Chanzo cha maadili, basi hakuna Muumba, na basi, je, mema na mabaya yalitokezwa tu na watu, jamii ya wanadamu? Ebu fikiria mfano mmoja: Watu wengi na vikundi vya watu huuona uuaji wa kimakusudi kuwa mbaya. Lakini mtu aweza kuuliza, ‘Ni mbaya kwa kulinganisha na nini?’ Kwa wazi kuna maadili fulani ambayo yapo katika jamii ya wanadamu kwa ujumla na ambayo yameingizwa katika sheria za nchi nyingi. Maadili hayo yalitoka wapi? Je, hayakutokana na Muumba mwenye maadili na ambaye aliwapa wanadamu dhamiri, au ufahamu wa maadili?—Linganisha Waroma 2:14, 15.
Unaweza Kutafakari Juu ya Wakati Ujao na Kuupangia
Jambo jingine la fahamu ya binadamu ni uwezo wetu wa kufikiria wakati ujao. Alipoulizwa ikiwa wanadamu wana tabia ambazo zinawatofautisha na wanyama, Profesa Richard Dawkins alikiri kwamba mwanadamu ana sifa za kipekee sana. Baada ya kutaja “uwezo wa kupanga mambo kimbele kwa kuweza kuona mbele na kufikiri na kuwaza,” Dawkins aliongezea: “Manufaa ya punde tu sikuzote imekuwa jambo la pekee linalohusika katika mageuzi; manufaa ya baadaye hayajapata kutajwa. Haijapata kuwezekana kamwe kwa kitu kugeuka japo kuna madhara yanayotokana na maendeleo ya punde tu ya kitu hicho. Kwa mara ya kwanza kabisa, inawezekana kwa angalau watu fulani kusema, ‘Usifikiri kwamba unaweza kupata faida ya haraka kwa kukata msitu huu; vipi manufaa ya baadaye?’ Sasa nafikiri hilo kwa kweli ni jambo jipya la kipekee.”
Watafiti wengine wanathibitisha kwamba uwezo wa wanadamu kupanga mambo kimbele kwa kufikiria hauna kifani. Mtaalamu wa utendaji wa ubongo William H. Calvin asema: “Mbali na matayarisho ya kujikinga na baridi kali yanayotokezwa na homoni za mwili na vilevile mambo ya kujamiiana, kwa kushangaza wanyama hawaonyeshi uthibitisho wa kuweza kupanga mambo hata kwa dakika chache zijazo.” Wanyama wanaweza kuhifadhi chakula kabla ya msimu wa baridi kali, lakini wao hawafikirii na kupanga mambo. Kwa kutofautisha, wanadamu hufikiria wakati ujao, hata wa mbali sana. Wanasayansi wengine hufikiria kile ambacho kinaweza kutukia kwa ulimwengu mabilioni ya miaka ijayo. Je, ulipata kujiuliza kwa nini mwanadamu—akiwa tofauti sana na wanyama—ana uwezo wa kufikiri kuhusu wakati ujao na kuupangia?
Biblia yasema hivi juu ya wanadamu: “[Muumba] ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao.” Biblia ya Revised Standard Version imeitafsiri: “Ameweka umilele katika akili ya mwanadamu.” (Mhubiri 3:11) Sisi hutumia uwezo huu wa kipekee kila siku, hata katika tendo la kawaida kama vile kujiangalia kwenye kioo na kufikiria jinsi tutakavyofanana miaka 10 au 20 ijayo. Na tunathibitisha yale ambayo andiko la Mhubiri 3:11 lasema hata tunapofikiria kwa muda mfupi mambo kama umilele wa wakati na wa anga. Jambo la kwamba tuna uwezo huu linapatana na maelezo ya kwamba Muumba ameweka “umilele katika akili ya mwanadamu.”
Binadamu Huvutiwa kwa Muumba
Hata hivyo, watu wengi hawaridhiki kabisa na kufurahia umaridadi, kuwafanyia wengine mema, na kufikiria wakati ujao. “Kwa kushangaza,” asema Profesa C. Stephen Evans, “hata katika pindi ambazo tunahisi tunapendwa, mara nyingi sisi huhisi kwamba kuna kitu kinachokosekana. Twajikuta tukitaka zaidi lakini bila kujua ni nini hicho tunachokosa.” Kwa kweli, wanadamu wenye fahamu—mbali na wanyama ambao wanashiriki nao sayari hii—huona uhitaji mwingine.
“Dini imekolea sana binadamu na watu huona uhitaji wa kidini katika kila kiwango cha kiuchumi na kielimu.” Jambo hilo lilitajwa kifupi na utafiti wa Profesa Alister Hardy uliotolewa katika kitabu The Spiritual Nature of Man. Hilo lathibitisha uchunguzi mwingine mwingi ambao umefanywa—kwamba mwanadamu anafahamu kwamba Mungu yupo. Ingawa watu mmoja-mmoja huenda wakawa hawaamini kuwako kwa Mungu, si mataifa mazima-mazima yanayoona hivyo. Kitabu Is God the Only Reality? chasema hivi: “Kutafuta maana [ya maisha] katika dini . . . ndilo jambo la kawaida zaidi katika kila utamaduni na katika kila kizazi tangu kutokea kwa wanadamu.”
Je, hilo linaloonekana kuwa kama fahamu ya kutambua Mungu ambayo mtu amezaliwa nayo hutoka wapi? Ikiwa binadamu alikuwa tu mkusanyo wa kiaksidenti wa asidi za kiini cha chembe na molekuli za protini, ni kwa nini molekuli hizi zingesitawisha upendo kwa sanaa na umaridadi, ziwe za kidini, na kutafakari juu ya umilele?
Sir John Eccles alikata kauli ya kwamba maelezo ya mageuzi kuhusu kuwako kwa mwanadamu “yanashindwa kueleza jambo muhimu sana. Hayaelezi ni kwa nini kila mmoja wetu ana ufahamu wa kipekee wa kwamba yu hai.” Kadiri tujifunzavyo kuhusu utendaji wa ubongo wetu na akili zetu, ndivyo iwavyo rahisi kuona ni kwa nini mamilioni ya watu wamekata kauli ya kwamba hali ya mwanadamu ya kufahamu kuwako kwake ni uthibitisho wa kuwako kwa Muumba ambaye anatujali.
Katika sura ifuatayo, tutaona ni kwa nini watu wa namna zote wamepata kwamba huu mkataa wenye kupatana na akili unaweka msingi wa kupata majibu yenye kuridhisha ya maswali haya muhimu, Kwa nini tuko hai, na twaelekea wapi?
[Sanduku katika ukurasa wa 51]
Bingwa wa Mchezo wa Chesi Dhidi ya Kompyuta
Wakati kompyuta ya hali ya juu iitwayo Deep Blue iliposhinda bingwa wa ulimwengu wa mchezo wa chesi, swali lilizushwa, “Je, hatulazimiki kukiri kwamba hiyo Deep Blue lazima iwe na akili?”
Profesa David Gelernter wa Chuo Kikuu cha Yale alijibu: “La. Deep Blue ni mashine tu. Haina akili kama vile chungu cha maua kisivyo na akili. . . . Jambo kuu ni hili: wanadamu ni bingwa wa kutengeneza mashine.”
Profesa Gelernter alitaja tofauti hii kubwa: “Ubongo ni mashine ambayo ina uwezo wa kukufanya ‘ujitambue.’ Ubongo unaweza kufanyiza picha akilini, na kompyuta haziwezi.”
Yeye alimalizia: “Pengo lililopo kati ya wanadamu na [kompyuta] ni la daima nalo haliwezi kuzibwa kamwe. Mashine zitaendelea kufanya maisha yawe rahisi, bora, yenye kupendeza na yenye kutatanisha zaidi. Na hatimaye, wanadamu wataendelea kushughulikia mambo yaleyale ambayo wao wamekuwa wakiyashughulikia: kujihusu, kuhusu mmoja na mwenzake na, wengi wao, kuhusu Mungu. Katika mambo haya, mashine hazijapata kutokeza tofauti. Nazo hazitaweza kamwe.”
[Sanduku katika ukurasa wa 53]
Kompyuta Bora Zaidi Yatoshana na Konokono
“Kompyuta za leo hata hazifikii mwanadamu mwenye umri wa miaka 4 kwa uwezo wa kuona, kuzungumza, kusonga, au kutumia akili. Bila shaka sababu moja ni utendaji wa hali ya juu wa ubongo. Imekadiriwa kwamba uwezo wa kuchanganua habari wa hata kompyuta yenye nguvu zaidi unatoshana na uwezo wa mfumo wa neva wa konokono—sehemu kidogo sana ya uwezo wa ubongo wetu.”—Steven Pinker, mkurugenzi wa Kituo cha Sayansi ya Ufahamu na Ubongo katika Taasisi ya Tekinolojia ya Massachusetts.
[Sanduku katika ukurasa wa 54]
“Karibu ubongo wote wa binadamu umefanyizwa na utando [wa bongo kubwa]. Kwa mfano, ubongo wa sokwe una utando pia, lakini ni mdogo sana kwa kulinganishwa. Huo utando hutuwezesha kufikiri, kukumbuka, na kuwazia mambo. Kwa msingi, sisi ni binadamu kwa sababu ya utando wetu.”—Edoardo Boncinelli, mkurugenzi wa utafiti wa biolojia ya molekuli, Milan, Italia.
[Sanduku katika ukurasa wa 55]
Uchunguzi wa Fizikia ya Nishati Nyingi Kuhusu Ubongo
Profesa Paul Davies alitafakari juu ya uwezo wa ubongo wa kushughulika na hesabu. “Hesabu si kitu ambacho unapata mahali popote. Inatokezwa na akili ya mwanadamu. Lakini tukiuliza ni sehemu gani ambapo hesabu hutumika zaidi, ni maeneo kama fizikia ya nishati nyingi na fizikia ya anga, maeneo ya sayansi ya msingi ambayo hayahusiani kabisa na mambo ya kawaida.” Hilo laonyesha nini? “Linadokeza kwamba fahamu na uwezo wetu wa kufanya hesabu si aksidenti tu, si kitu kidogo tu, si tokeo tu lisilo la maana la mageuzi.”—Are We Alone?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 56, 57]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Utando wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa
Sehemu ya mbele ya bongo kubwa
Eneo la Broca
Eneo la Wernicke
Utando wa kuongoza miendo ya misuli
●Utando wa Bongo Kubwa ndio utando wa nje wa bongo unaohusika sana na akili. Utando wa bongo kubwa wa binadamu ukilainishwa unaweza kufunika kurasa nne; wa sokwe unaweza kufunika ukurasa mmoja tu; na wa panya unaweza kufunika stampu ya barua.—Scientific American.
[Sanduku katika ukurasa wa 58]
Kila Kabila Lina Lugha Yake
Katika historia yote, makabila yalipokutana, kila kabila lilikuwa na lugha fulani. Kitabu The Language Instinct chaeleza: “Hakuna kabila lililo bubu ambalo limepata kugunduliwa, na hakuna rekodi yoyote ya kwamba eneo fulani lilikuwa ‘chanzo’ cha lugha ambayo ilienea kwa makabila ambayo awali hayakuwa na lugha. . . . Kuwako kwa lugha iliyo tata duniani kote ni ugunduzi ambao unastaajabisha wataalamu wa lugha, na ndiyo sababu ya kwanza ya kufikiria kwamba lugha ni . . . tokeo la silika ya kipekee ya wanadamu.”
[Sanduku katika ukurasa wa 59]
Lugha na Akili
Kwa nini akili ya binadamu inashinda sana akili ya wanyama, kama vile nyani? Jambo kubwa ni uwezo wetu wa kuunganisha sauti kufanyiza maneno na kutumia maneno kufanyiza sentensi. Mtaalamu wa utendaji wa ubongo Dakt. William H. Calvin aeleza:
“Sokwe wasiofugwa hutoa karibu dazani tatu za sauti tofauti-tofauti ili kuwasilisha karibu dazani tatu za maana tofauti-tofauti. Wao waweza kurudia sauti ili kukazia maana, lakini wao hawaunganishi sauti tatu tofauti-tofauti ili kufanyiza neno jipya katika msamiati wao.
“Sisi wanadamu pia hutumia karibu dazani tatu za sauti, ambazo huitwa fonimi. Lakini ni miunganisho ya hizo ndiyo hutokeza maana: sisi huunganisha sauti zisizo na maana ili kuunda maneno yenye maana.” Dakt. Calvin alitaja kwamba “hakuna mtu ambaye ameeleza sababu ya kuwako kwa” tofauti kubwa sana kati ya “sauti moja/maana moja” ya wanyama na uwezo mkubwa wa ajabu wa mwanadamu wa kuunda maneno.
[Sanduku katika ukurasa wa 60]
Unaweza Kufanya Mengi Kuliko Kuchora Tu Vitu Visivyo na Maana
“Je, ni mwanadamu tu ambaye ana uwezo wa kuwasiliana kwa lugha? Kwa wazi ni lazima jibu litegemee kile kinachomaanishwa na ‘lugha’—kwa kuwa wanyama huwasiliana kwa njia nyingi tofauti-tofauti kama vile ishara, harufu, miito, milio na nyimbo, na hata kucheza dansi kama vile nyuki. Lakini inaonekana kwamba mbali na mwanadamu, wanyama hawana lugha yenye kufuata sarufi. Na jambo muhimu zaidi ni kwamba wanyama hawachori picha za kuwakilisha mambo wanayotaka kuwasilisha. Hawawezi kufanya chochote zaidi ya kuchora tu vitu visivyo na maana.”—Profesa R. S. na D. H. Fouts.
[Sanduku katika ukurasa wa 61]
“Tukifikiria akili ya binadamu, sisi pia hupata utaratibu wenye mambo mengi ajabu,” asema Profesa A. Noam Chomsky. “Lugha ni mfano mmoja, lakini kuna mifano mingineyo. Ebu fikiria uwezo wa ubongo wa kushughulika na mambo yanayohitaji akili kama hesabu [ambayo inaonekana] ni mwanadamu pekee aliye na uwezo wa kuifanya.”
[Sanduku katika ukurasa wa 62]
“Wana Uwezo” wa Kuuliza
Kuhusu wakati ujao wa ulimwengu wetu, mtaalamu wa fizikia Lawrence Krauss aliandika: “Tuna uwezo wa kuuliza maswali kuhusu mambo ambayo huenda hayatuhusu moja kwa moja kwa sababu twaweza kuyauliza. Watoto wetu, au watoto wao, siku moja watayajibu. Sisi tumepewa uwezo wa kuwazia mambo.”
[Sanduku katika ukurasa wa 69]
Ikiwa ulimwengu pamoja na uhai wetu ulio ndani yake ulitokea kwa aksidenti tu, maisha zetu haziwezi kuwa na maana yenye kudumu. Lakini ikiwa uhai katika ulimwengu uliumbwa, basi ni lazima kuwe na majibu yenye kuridhisha.
[Sanduku katika ukurasa wa 72]
Je, Uwezo wa Mwanadamu wa Kisayansi Watokana na Kuepa Wanyama Wakali?
John Polkinghorne, wa Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza, alisema:
“Mtaalamu wa fizikia ya nadharia Paul Dirac aligundua kitu kiitwacho kanuni ya tabia ya vitu ambayo ni muhimu sana ili tuelewe ulimwengu wetu wa asili. Siwezi kuamini kwamba uwezo wa Dirac wa kugundua nadharia hiyo, au uwezo wa Einstein wa kuvumbua nadharia ya ujumla ya uwiano, eti umetokana na hali ya wazazi wa kale kutafuta mbinu za kuwaepa wanyama wakali ili kusalimika. Kuna jambo kubwa zaidi, ambalo halifahamiki zaidi . . .
“Tutazamapo utaratibu mzuri na umaridadi uonekanao wazi wa ulimwengu, ambao umefunuliwa na sayansi halisi, twaona ulimwengu ambao umejaa alama za kubuniwa na mtu mwenye akili. Kwa mtu wa kidini, ni akili ya Muumba ambayo inaonekana kwa njia hiyo.”—Commonweal.
[Picha katika ukurasa wa 63]
Ni wanadamu tu huuliza maswali. Mengine ni maswali kuhusu maana ya maisha
[Picha katika ukurasa wa 64]
Tofauti na wanyama, wanadamu wana fahamu kujihusu na kuhusu wakati ujao
[Picha katika ukurasa wa 70]
Ni binadamu pekee ambaye huthamini umaridadi, hufikiri juu ya wakati ujao, na kuvutiwa kwa Muumba