Michezo Katika Nyakati za Biblia
MAPEMA katika historia ya wanadamu watu walianza kutamani burudani. Inasemekana kuwa Yubali, aliyekuwa katika kizazi cha saba kutoka kwa Adamu, ndiye “mwanzilishi wa wote wanaotumia kinubi na zumari.” (Mwanzo 4:21) Baada ya muda, angalau baada ya Gharika, michezo ilibuniwa pia.
Katika maeneo mengi ya Misri, Palestina, na Mesopotamia, wataalamu wa vitu vya kale wamechimbua mbao mbalimbali za michezo, vidude vya mchezo wa chesi, na vitu vingine vya kuchezea, na baadhi ya vitu hivyo ni vya kabla ya wakati wa Abrahamu. Mchongo mmoja uliopatikana katika lango la hekalu huko Misri unaonyesha Mfalme Ramses wa Tatu akicheza pamoja na mmoja wa masuria wake mchezo kama wa dama. Katika michezo mingi, kidude chenye nyuso sita au vijiti vilitumiwa kuendesha mchezo.
Zaidi ya kuonyesha watu wakicheza dansi na kucheza vyombo vya muziki, michoro ya Misri huonyesha wasichana Wamisri wakirusha-rusha na kudaka mipira. Michezo mingine ya vijana, kama ile ya kuvutana kwa kamba, ilihitaji vikosi vya wachezaji. Pia gololi zilitumiwa sana.
Biblia haitaji moja kwa moja michezo iliyochezwa na Waebrania, lakini mambo fulani machache yanaonyesha kwamba kulikuwa na burudani mbalimbali kutia ndani muziki, kuimba, kucheza dansi, na kuzungumza. Andiko la Zekaria 8:5 linataja watoto wakicheza katika viwanja vya watu wote, nalo andiko la Ayubu 21:11, 12 linataja wavulana waliokuwa wakiimba na kucheza dansi. Katika siku za Yesu, watoto walicheza kwa kuigiza pindi zenye furaha na zenye huzuni. (Mathayo 11:16, 17) Kutokana na uchimbuzi uliofanywa Palestina, vitu vya kuchezea vya watoto vimegunduliwa, kama vile filimbi, vyungu vidogo, na vigari vya kukokotwa. Hata hivyo, inaonekana kwamba Wayahudi hawakuwa na michezo ya mashindano hadi wakati utamaduni wa Ugiriki ulipoenea.
Michezo ya Kipagani Yapelekwa Palestina
Wakati wa utawala wa Antioko Epifani katika karne ya pili K.W.K., Wayahudi waliofuata utamaduni wa Ugiriki walipeleka utamaduni huo na mashindano ya riadha Israeli. Kulingana na sura ya kwanza ya kitabu cha Kwanza cha Wamakabayo cha Apokrifa, kiwanja cha michezo kilijengwa Yerusalemu. Kitabu cha 2 Wamakabayo 4:12-15 kinaonyesha kwamba hata makuhani walipuuza majukumu yao ili kushiriki katika michezo hiyo. Hata hivyo, wengine walikataa katakata desturi hizo za kipagani.
Katika karne ya kwanza K.W.K., Herode Mkuu alijenga uwanja wa maonyesho huko Yerusalemu, na akajenga uwanja wa duara uwandani, pia alijenga uwanja wa maonyesho na uwanja wa duara huko Kaisaria, naye akaagiza kwamba sherehe za michezo zifanywe baada ya kila miaka mitano ili kumheshimu Kaisari. Zaidi ya kuanzisha mieleka, mashindano ya magari ya kukokotwa, na mashindano mengine, Herode Mkuu alianzisha pia michezo mingine kutokana na michezo ya Waroma, na akapanga mapambano kati ya wanyama-mwitu na vilevile mapambano kati ya wanyama hao na wanaume waliohukumiwa kifo. Kulingana na Yosefo, mambo yote hayo yaliwafanya Wayahudi waliochukizwa wapange njama ya kumuua Herode, lakini njama hiyo haikufanikiwa.
Mifano Iliyotokana na Michezo
Paulo na Petro walitumia vizuri mambo fulani ya michezo hiyo ili kufundisha kwa mifano. Tofauti na tuzo ambalo washindanaji walijitahidi kushinda katika michezo ya Ugiriki, taji ambalo Mkristo mtiwa-mafuta hujitahidi kupata, si la majani yanayoharibika, bali ni zawadi ya uhai usioweza kufa. (1 Petro 1:3, 4; 5:4) Mkristo huyo alipaswa kukimbia akiwa na nia ya kushinda tuzo hilo naye alipaswa kulikazia macho. Kutazama nyuma kungekuwa hatari. (1 Wakorintho 9:24; Wafilipi 3:13, 14) Mkristo huyo alipaswa kushindana kulingana na sheria za maadili ili asiondolewe kwenye mashindano. (2 Timotheo 2:5) Alipaswa ajizuie, ajitie nidhamu, na kufanya mazoezi. (1 Wakorintho 9:25; 1 Petro 5:10) Jitihada za Mkristo huyo zilipaswa kuelekezwa mahali panapofaa huku akifikiria ushindi, kama vile ngumi za mpiganaji aliyezoezwa vizuri zinavyokuwa na matokeo zinapolenga shabaha; ingawa pigano la Mkristo si dhidi ya mwanadamu mwenzake, bali dhidi ya vitu, kutia ndani vile vilivyo ndani yake, ambavyo vinaweza kumfanya asifaulu. (1 Wakorintho 9:26, 27; 1 Timotheo 6:12) Mkristo huyo alipaswa kuondoa kila uzito unaoweza kumzuia na vilevile dhambi inayotatanisha ya kukosa imani, sawa na vile washindanaji katika mbio walivyovua mavazi mazito. Mkimbiaji Mkristo alipaswa kujitayarisha kwa ajili ya mbio zinazohitaji uvumilivu, bali si kukimbia kasi kwa muda mfupi.—Waebrania 12:1, 2.
Kwenye Waebrania 12:1, Paulo anazungumza kuhusu ‘wingu kubwa la mashahidi [Kigiriki, mar·tyʹron] linalotuzunguka.’ Sura inayotangulia inaonyesha wazi kwamba Paulo hazungumzi kuhusu umati wa watazamaji. Paulo anairejelea sura hiyo kwa kusema, “Kwa hiyo, basi, . . . ” Hivyo, Paulo anawatia moyo Wakristo waendelee katika mbio kwa kuwaonyesha mifano bora ya wengine ambao walikuwa wakimbiaji wala si watazamaji, naye anawahimiza wamtazame kwa makini yule ambaye tayari alikuwa ameshinda na ambaye sasa ni Hakimu wao, yaani, Kristo Yesu.