Kusafiri Mbali Zaidi ya Mediterania Nyakati za Kale
Leo, haishangazi kuona mtu akisafiri kwa ndege kutoka bara moja mpaka lingine. Je, ungeshangaa kujua kwamba nyakati za Biblia, watu walifunga safari ndefu?
MIAKA elfu moja hivi kabla ya Kristo kuja duniani, Mfalme Sulemani alitengeneza kundi la meli ambazo zilisafiri baharini pamoja na meli za mfalme wa Tiro zikileta vitu vyenye thamani Israeli kutoka maeneo ya mbali. (1 Wafalme 9:26-28; 10:22) Katika karne ya tisa K.W.K., kwenye bandari ya Yopa huko Israeli, iliyo katika Mediterania, nabii Yona alipanda meli iliyokuwa ikielekea Tarshishi.a (Yona 1:3) Katika karne ya kwanza W.K., mtume Paulo alisafiri kutoka Kaisaria huko Israeli mpaka mji wa Puteoli, ambao sasa unaitwa Pozzuoli, kwenye Ghuba ya Naples, huko Italia.—Matendo 27:1; 28:13.
Wanahistoria wanajua kwamba kufikia siku za Paulo, kwa kawaida wafanyabiashara kutoka eneo la Mediterania walikuwa wakivuka Bahari Nyekundu mpaka India, na kufikia katikati ya karne ya pili, wengine wao walikuwa wakisafiri mpaka China.b Lakini, tunajua nini kuhusu safari za kale za kuvuka Mediterania kuelekea upande wa magharibi? Mabaharia wa kale walisafiri mbali kadiri gani kuelekea upande huo?
Safari za Kale za Wafoinike
Karne nyingi kabla ya siku za Paulo, watu waliokuwa wakisafiri baharini walikuwa wameanzisha maeneo ya kibiashara huko Magharibi. Inaaminiwa kwamba Wafoinike waliokuwa wakiishi katika nchi ambayo sasa inaitwa Lebanoni, walifika kwenye Bahari ya Atlantiki karibu mwaka wa 1200 K.W.K. Karibu mwaka wa 1100 K.W.K., mbele tu ya milango-bahari ya Gibraltar, walianzisha mji wa Gadir, ambao sasa ni jiji la bandarini la Cádiz, huko Hispania. Kati ya bidhaa ambazo zilipatikana huko ni madini ya fedha na bati yaliyochimbwa katika eneo hilo, na ambayo yalinunuliwa na wafanyabiashara wa bahari ya Atlantiki.
Mwanahistoria Mgiriki, Herodotus aliandika kwamba katika karne ya saba K.W.K., Farao Neko wa Misri alikusanya kwenye sehemu ya juu ya Bahari Nyekundu kundi la meli za Foinike, zilizoendeshwa na mabaharia Wafoinike. Alikusudia kuzunguka bara la Afrika kuanzia upande wa mashariki mpaka upande wa magharibi.
Kufikia wakati huo, tayari Wafoinike walikuwa wamefika kwenye pwani ya Afrika kwa karne nyingi. Hata hivyo, kwa sababu ya upepo mkali, mabaharia walioelekea kusini kwenye pwani ya bara hilo inayopakana na Bahari ya Atlantiki walijikaza sana ili wafike mbali. Herodotus anasema kwamba kwenye safari hiyo mpya ya uvumbuzi, Wafoinike walianzia Bahari Nyekundu na kufuata pwani ya mashariki ya Afrika wakielekea kusini katika Bahari ya Hindi. Baada ya miezi sita hivi walitia nanga na kuingia kwenye nchi kavu, wakapanda mbegu, wakakaa kwa muda wa kutosha kuvuna, kisha wakaendelea na safari. Herodotus alisema kwamba baada ya miaka mitatu, walilizunguka bara lote, wakaingia Mediterania, kisha wakarudi Misri.
Herodotus alimalizia simulizi lake kwa kusema kwamba Wafoinike waliripoti mambo ambayo hangeweza kuamini, kutia ndani maelezo yao kwamba walipokuwa wakizunguka sehemu ya kusini ya Afrika, waliona jua likiwa upande wa kulia. Kwa kweli, ingekuwa vigumu kwa Mgiriki wa kale kuamini jambo hilo. Mtu ambaye ameishi maisha yake yote upande wa kaskazini wa ikweta amezoea kuona jua likiwa upande wa kusini. Hivyo, anapoelekea upande wa magharibi, jua linakuwa upande wake wa kushoto. Lakini kwenye Rasi ya Tumaini Jema, ambayo iko upande wa kusini wa ikweta, jua linakuwa upande wa kaskazini saa sita mchana, yaani, upande wa kulia wa mtu anayeelekea magharibi.
Kwa karne nyingi, wanahistoria wamejadiliana kuhusu simulizi la Herodotus. Huenda wengi wakaona kwamba mabaharia wa kale hawangeweza kuzunguka bara la Afrika. Ingawa hivyo, wasomi wanaamini kwamba Farao Neko hakupanga safari hiyo na kwamba safari kama hiyo haingewezekana ukifikiria ustadi na ujuzi uliokuwapo wakati huo. Mwanahistoria Lionel Casson anasema kwamba “safari kama hiyo ingewezekana kabisa. Hakuna jambo ambalo lingewazuia mabaharia Wafoinike kusafiri kwa kipindi na kwa njia ambayo Herodotus anasema walisafiri.” Usahihi wa simulizi la Herodotus hauwezi kuthibitishwa kikamili. Hata hivyo, simulizi hilo linatusaidia kuelewa jinsi mabaharia walivyojitahidi sana kusafiri mpaka kwenye maeneo ambayo hayakujulikana nyakati hizo.
Pytheas Asafiri Baharini Kuelekea Kaskazini
Nyakati za kale katika eneo la Mediterania, si Wafoinike tu waliosafiri mbali zaidi upande wa magharibi kuelekea Atlantiki. Moja kati ya koloni ambazo mabaharia Wagiriki walianzisha katika eneo la Mediterania ni Massalia, ambalo sasa ni jiji la Marseilles huko Ufaransa. Jiji hilo lilisitawi kwa sababu ya biashara ya baharini na ya nchi kavu. Huko Massalia, wafanyabiashara walichukua divai ya Mediterania, mafuta, vitu vya shaba na kuvipeleka kaskazini, nao walibeba chuma na kaharabu kutoka upande wa kaskazini. Bila shaka, wakaaji wa Massalia walitaka kujua mahali ambapo vitu hivyo vilitoka. Hivyo, karibu mwaka wa 320 K.W.K., Pytheas aliyekuwa akiishi Massalia alifunga safari ili ajionee maeneo hayo yaliyokuwa mbali upande wa kaskazini.
Baada ya kurudi, Pytheas aliandika simulizi kuhusu safari zake lenye kichwa On the Ocean (Kusafiri Baharini). Ingawa leo nakala za awali za Kigiriki za kitabu hicho hazipatikani, simulizi hilo lilinukuliwa na waandikaji 18 hivi wa kale. Sehemu zilizonukuliwa zinaonyesha kwamba Pytheas alieleza kwa makini kuhusu bahari, mawimbi, jiografia, na idadi ya watu katika maeneo aliyotembelea. Pia, alitumia urefu wa kivuli cha kijiti fulani cha kupimia ili ajue mwinamo wa jua saa sita mchana katika tarehe fulani hususa, na habari hiyo ilimsaidia kukadiria umbali ambao alikuwa amesafiri kuelekea kaskazini.
Pytheas alisafiri hasa kwa sababu za kisayansi. Hata hivyo, kusudi kuu la safari yake halikuwa tu kufanya uvumbuzi wa kisayansi. Wasomi wamedai kwamba kinyume na hilo, safari yake ilipangwa na kugharimiwa na wafanyabiashara huko Massalia, ambao walimtuma atafute njia ya baharini ya kuelekea kwenye pwani hizo za mbali ambako walijua kwamba wangepata madini ya kaharabu na bati. Hivyo basi, Pytheas alisafiri mpaka wapi?
Brittany, Uingereza, na Maeneo ya Mbali Zaidi
Inaonekana kwamba Pytheas alisafiri baharini kuzunguka Iberia na akapanda juu kuelekea pwani ya Gaul mpaka Brittany, ambako alitia nanga. Tunajua jambo hilo kwa sababu rekodi yake moja ya mwinamo wa jua, ambayo huenda alipima akiwa kwenye nchi kavu, inalingana na eneo fulani la kaskazini mwa Brittany.c
Watu walioishi huko Brittany walikuwa na ujuzi wa kutengeneza meli na walikuwa mabaharia stadi waliofanya biashara na Uingereza. Eneo la Cornwall, lililo kwenye nchi iliyo kusini-magharibi ya Uingereza, lilikuwa na kiasi kikubwa cha madini ya bati, ambayo yanatumiwa kutengeneza shaba, na huko ndiko Pytheas alikoelekea. Ripoti yake ilitaja ukubwa wa nchi ya Uingereza na umbo lake linalokaribia kufanana na pembetatu, kuonyesha kwamba alizunguka kisiwa hicho.
Ingawa njia ambayo Pytheas alitumia haijulikani kikamili, huenda alisafiri katikati ya Uingereza na Ireland, na akakaa kwenye Kisiwa cha Man, ambacho kina latitudo ambayo inalingana na kipimo chake cha pili cha mwinamo wa jua. Huenda alipima kipimo chake cha tatu akiwa Lewis huko Outer Hebrides, karibu na pwani ya magharibi ya Scotland. Kutoka huko, huenda alielekea kaskazini kwenye Visiwa vya Orkney, kaskazini ya Scotland, kwa sababu simulizi lake lililonukuliwa na Plini Mkubwa, linaripoti kwamba kulikuwa na visiwa 40.
Pytheas aliandika kwamba baada ya kusafiri kwa siku sita kutoka Uingereza alifika kwenye eneo lililoitwa Thule. Waandikaji kadhaa wa kale wanataja maelezo ya Pytheas kuhusu Thule kuwa ni nchi iliyo na jua katikati ya usiku. Aliandika kwamba baada ya kusafiri kwa siku moja kutoka huko, alifika mahali ambapo bahari ilikuwa “imeganda.” Watu wengi wamebishana kuhusu mahali ambapo Pytheas alipaita Thule, wengine wanasema kwamba ni kwenye Visiwa vya Faeroe, wengine wanasema Norway, na wengine Iceland. Haijulikani Thule ilikuwa wapi, lakini waandishi wa kale waliamini kwamba ilikuwa “sehemu ya mbali zaidi ya kaskazini ya maeneo yaliyotajwa.”
Inawaziwa kwamba Pytheas alirudi Uingereza kwa njia ileile aliyofuata na hivyo akazunguka kisiwa hicho. Hatujui ikiwa aliendelea kuvumbua pwani ya kaskazini ya Ulaya kabla ya kurudi kwenye eneo la Mediterania. Kwa vyovyote vile, Plini Mkubwa anamtaja Pytheas kuwa mtu aliyejua sana maeneo yaliyokuwa na kaharabu. Maeneo ambayo zamani yalikuwa na kaharabu yalikuwa huko Jutland, sehemu ambayo sasa iko nchini Denmark, na pia kwenye ufuo wa kusini wa Bahari ya Baltiki. Bila shaka, huenda Pytheas alijua kuhusu maeneo hayo alipotembelea mojawapo ya bandari zilizo mashariki mwa Uingereza, ingawa hakuna habari zozote zinazoonyesha kwamba alisema kuwa alitembelea bandari hizo.
Msafiri mwingine anayejulikana kutoka Mediterania ambaye aliandika kuhusu safari zake za Uingereza ni Julius Caesar, ambaye alifika upande wa kusini wa kisiwa hicho mwaka wa 55 K.W.K. Kufikia mwaka wa 6 W.K., wasafiri wengine kutoka Roma walikuwa wamefika kaskazini mwa Jutland.
Kuvumbua Maeneo Mapya
Wafoinike na Wagiriki waliendelea kuvumbua maeneo mengine ambayo hayakujulikana huko Mediterania, wakaingia Atlantiki, na mwishowe wakafika sehemu za mbali zaidi kusini mwa Afrika, na kaskazini huko Aktiki. Wakati huo, watu wengi walikuwa wavumbuzi, wafanyabiashara, walisafiri mpaka kwenye maeneo mapya, walisafiri mbali sana, na hivyo kueneza ujuzi na mawazo mapya.
Rekodi zilizopo sasa za uvumbuzi uliofanywa kale zinaonyesha safari chache sana ambazo mabaharia wajasiri walifunga kwa mafanikio. Ni mabaharia wangapi wa kale ambao walirudi mahali walipoanzia safari lakini hawakuandika kuhusu maeneo waliyofika? Na ni wangapi waliosafiri kutoka nchi zao kwenda kwenye fuo za mbali na hawakurudi kamwe? Maswali hayo hayawezi kujibiwa. Lakini tunaweza kujifunza jambo fulani kuhusu kuenea kwa Ukristo hapo kale.—Ona sanduku lililo hapo juu.
[Maelezo ya Chini]
a Mara nyingi jina hili linahusianishwa na eneo lililo kusini mwa Hispania ambalo waandikaji Wagiriki na Waroma waliliita Tartessus.
b Ili upate habari zaidi kuhusu safari za kuelekea upande wa mashariki, ona habari yenye kichwa “Wamishonari Wangesafiri Hadi Wapi Upande wa Mashariki?” katika gazeti Mnara wa Mlinzi la Januari 1, 2009 (1/1/2009).
c Kwa vipimo vya kisasa, ni kwenye latitudo ya 48° 42’ N.
[Sanduku katika ukurasa wa 29]
Habari Njema “Ilihubiriwa Katika Uumbaji Wote”
Karibu mwaka wa 60-61 W.K., mtume Paulo aliandika kwamba habari njema ilikuwa ‘imehubiriwa katika uumbaji wote ulio chini ya mbingu.’ (Wakolosai 1:23) Je, alimaanisha kwamba tayari Wakristo walikuwa wamehubiri huko India, Mashariki ya Mbali, Afrika, Hispania, Gaul, Uingereza, Baltiki, na eneo ambalo Pytheas aliliita Thule? Inaonekana kwamba hilo halingewezekana, lakini hatuwezi kuwa na hakika.
Hata hivyo, hakuna shaka kwamba habari njema ilikuwa imeenea sana. Kwa mfano, Wayahudi na watu waliogeuzwa imani ambao walikubali kuwa Wakristo siku ya Pentekoste 33 W.K., walipeleka imani yao mpya katika maeneo ya Parthia, Elamu, Umedi, Mesopotamia, Arabia, Asia Ndogo, sehemu za Libya kuelekea Kirene, na Roma, yaani, ulimwengu ambao wasomaji wa Paulo waliujua.—Matendo 2:5-11.
[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 26, 27]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Herodotus aliripoti kwamba mabaharia waliokuwa wakisafiri kwenye ncha ya kusini ya Afrika waliona jua likiwa upande wa kulia
[Ramani]
AFRIKA
BAHARI YA MEDITERANIA
BAHARI YA HINDI
BAHARI YA ATLANTIKI
[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 28, 29]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Safari ndefu ya baharia Mgiriki Pytheas
[Ramani]
Marseilles
RASI YA IBERIA
IRELAND
ICELAND
NORWAY
Bahari ya Kaskazini
UINGEREZA
BRITTANY
RASI YA IBERIA
PWANI YA KASKAZINI YA AFRIKA
BAHARI YA MEDITERANIA
Marseilles