Sura ya 37
Kuomboleza na Kushangilia Mwisho wa Babuloni
1. “Wafalme wa dunia” watatendaje kwa kuitikia uharibifu wa ghafula wa Babuloni Mkubwa?
MWISHO wa Babuloni ni habari njema kwa watu wa Yehova, lakini mataifa yanauonaje? Yohana anatuambia: “Na wafalme wa dunia ambao walifanya uasherati na yeye na wakaishi katika anasa yenye utovu wa aibu watatoa machozi na kujipigapiga wenyewe kwa kihoro juu yake, wanapotazama moshi kutoka kuchomwa kwake, huku wao wakisimama mbali kwa sababu ya hofu yao ya teso lake na kusema, ‘Ni vibaya mno, ni vibaya mno, wewe jiji kubwa, Babuloni wewe jiji imara, kwa sababu katika saa moja hukumu yako imewasili!’”—Ufunuo 18:9, 10, NW.
2. (a) Kwa kuwa pembe kumi za ufananisho za hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu zitamharibu Babuloni Mkubwa, ni kwa nini “wafalme wa dunia” wanahuzunikia mwisho wake? (b) Ni kwa nini hao wafalme wenye kihoro husimama mbali na jiji lililohukumiwa maangamizi?
2 Tendo-mwitikio la mataifa huenda likaonekana kuwa la kushangaza kwa sababu ya uhakika wa kwamba Babuloni aliharibiwa na zile pembe kumi za ufananisho za hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu. (Ufunuo 17:16) Lakini Babuloni atakapokuwa hayupo, kwa wazi “wafalme wa dunia” watang’amua jinsi alivyokuwa mwenye mafaa kwao katika kutuliza watu na kuwatiisha. Viongozi wa kidini wamejulisha wazi vita kuwa vitakatifu, wakatenda wakiwa mawakili wa kuandikisha askari-jeshi, na wakahubiri vijana waingie katika mapigano. Dini imeandaa kisetiri cha utakatifu ambacho nyuma yacho watawala wafisadi wameendesha mambo katika kukandamiza makabwela. (Linga Yeremia 5:30, 31; Mathayo 23:27, 28.) Hata hivyo, angalia kwamba wafalme hawa wenye kihoro sasa wanasimama mbali na hilo jiji lenye kuhukumiwa maangamizi. Wao hawakaribii vya kutosha ili kuliauni. Wao wanahuzunikia kuona linaenda lakini hawahuzuniki vya kutosha kujihatarisha kwa ajili yalo.
Wauza-Bidhaa Watoa Machozi na Kuomboleza
3. Ni nani wengine wanaojutia kupita kwa Babuloni Mkubwa, na Yohana hutoa sababu zipi juu ya hilo?
3 Wafalme wa dunia sio pekee wanaojutia kupita kwa Babuloni Mkubwa. “Pia, wauza-bidhaa wasafiri wa dunia wanatoa machozi na kuomboleza juu ya yeye, kwa sababu hakuna wa kununua tena bidhaa yao kamili, bidhaa kamili ya dhahabu na fedha na jiwe la thamani na lulu na kitani nzuri na zambarau na hariri na rangi-nyekundu-nyangavu; na kila kitu katika mbao zenye kutiwa manukato na kila aina ya kitu cha meno ya tembo na kila aina ya kitu kutokana na mbao iliyo ya thamani kubwa zaidi sana na cha shaba na cha chuma na cha marimari; pia mdalasini na vikolezo vya Kihindi na uvumba na mafuta yaliyotiwa harufu nzuri na ubani na divai na mafuta ya zeituni na unga safi sana na ngano na ng’ombe na kondoo, na farasi na makochi na watumwa na nafsi za kibinadamu. Ndiyo, na tunda zuri ambalo nafsi yako ilitamani limeondoka kutoka kwa wewe [Babuloni Mkubwa], na vitu vitamu-vitamu vyote na vitu vya umaridadi vimepotelea mbali kutoka kwa wewe, na watu hawatavipata tena kamwe.”—Ufunuo 18:11-14, NW.
4. Ni kwa nini “wauza-bidhaa wasafiri” hutoa machozi na kuombolezea mwisho wa Babuloni Mkubwa?
4 Ndiyo, Babuloni Mkubwa alikuwa rafiki ya karibu na mteja mwema wa wauza-bidhaa wenye ukwasi. Mathalani, kwa muda wa karne zilizopita nyumba za watawa-waume, nyumba za watawa wa kike na makanisa ya Jumuiya ya Wakristo zimejipatia kiasi kikubwa mno cha dhahabu, fedha, mawe ya thamani, mbao za thamani, na namna nyinginezo za ukwasi wa vitu vya kimwili. Na zaidi, baraka ya kidini imetolewa juu ya shamrashamra za ununuzi wa kianasa na karamu za ulafi, ulevi na uasherati zinazoandamana na mwadhimisho wa Krismasi wenye kuvunjia Kristo heshima na siku nyinginezo zinazoitwa eti takatifu. Wamisionari wa Jumuiya ya Wakristo wamepenya ndani ya mabara ya mbali, wakafungua masoko mapya kwa ajili ya “wauza-bidhaa wasafiri” wa ulimwengu huu. Katika Japani ya karne ya 17, Ukatoliki, uliokuja pamoja na wachuuzi hata ulijihusisha katika vita vyenye uhasama wa daima. Ikiripoti juu ya vita yenye kukata maneno chini ya kuta za ngome ya Osaka, The Encyclopædia Britannica hutaarifu hivi: “Vikosi vya Tokugawa vilijikuta vikipigana dhidi ya adui ambaye bendera zake zilikuwa zimepambwa kwa msalaba na mifano ya Mwokozi na ya [Mt.] James, mtakatifu mfadhili wa Hispania.” Chamkano yenye kushinda ilinyanyasa na karibu imalize Ukatoliki katika bara hilo. Ushiriki wa kanisa katika mambo ya ulimwengu leo vilevile hautaliletea baraka.
5. (a) Sauti kutoka katika mbingu inaelezaje zaidi kuomboleza kwa hao “wauza-bidhaa wasafiri”? (b) Ni kwa nini wauza-bidhaa ‘wanasimama mbali’ pia?
5 Sauti kutoka katika mbingu inasema zaidi hivi: “Wauza-bidhaa wasafiri wa vitu hivi, ambao wakawa na utajiri kutokana na yeye, watasimama mbali kwa sababu ya hofu yao ya teso lake na watatoa machozi na kuomboleza, kusema, ‘Ni vibaya mno, ni vibaya mno—jiji kubwa, lililovikwa kitani nzuri na zambarau na rangi-nyekundu-nyangavu, na kurembwa kitajiri kwa madoido ya dhahabu na jiwe la thamani na lulu, kwa sababu katika saa moja utajiri mwingi hivyo umeteketezwa!’” (Ufunuo 18:15-17a, NW) Kwa sababu ya kuharibiwa kwa Babuloni Mkubwa, “wauza-bidhaa” wanaombolezea hasara ya mshirika wa kibiashara huyo. Kwa kweli, “ni vibaya mno, ni vibaya mno” kwao. Hata hivyo, angalia kwamba sababu za kuomboleza kwao ni za ubinafsi kabisa na kwamba wao—kama vile wafalme—‘husimama mbali.’ Wao hawakaribii sana vya kutosha ili wasaidie Babuloni Mkubwa.
6. Sauti kutoka katika mbingu inaelezaje kuomboleza kwa makapteni wa meli na mabaharia, na ni kwa nini wao hutoa machozi?
6 Simulizi laendelea: “Na kila kapteni wa meli na kila mtu ambaye husafiri kwa meli kokote, mabaharia na wale wote ambao hupata riziki kwa bahari, walisimama mbali na kupiga kilio kikuu walipotazama moshi wa kuchomwa kwake na kusema, ‘Ni jiji gani lililo kama jiji kubwa?’ Na wao wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao na kupiga kilio kikuu, wakitoa machozi na kuomboleza, na wakasema, ‘Ni vibaya mno, ni vibaya mno—jiji kubwa, ambalo katika hilo wale wote wenye mashua kwenye bahari, wakawa na utajiri kwa sababu ya ughali walo, kwa kuwa katika saa moja limeteketezwa!’” (Ufunuo 18:17b-19, NW) Babuloni wa kale alikuwa jiji la kibiashara na alikuwa na kundi kubwa la meli. Hali moja na hiyo, Babuloni Mkubwa hufanya biashara nyingi sana kwa kutumia “maji mengi” ya watu wake. Hiyo huandaa kuajiriwa kwa raia wake wengi wa kidini. Uharibifu wa Babuloni Mkubwa utakuwa dharuba ya kiuchumi kama nini kwa watu hawa! Hakutakuwa kamwe na chimbuko jingine la riziki kama yeye.
Kushangilia Juu ya Utowesho Wake
7, 8. Sauti kutoka katika mbingu inafikiaje upeo wa ujumbe wayo kuhusu Babuloni Mkubwa, na ni nani watakaoitikia maneno hayo?
7 Babuloni wa kale alipopinduliwa na Wamedi na Waajemi, Yeremia alisema kiunabii hivi: “Na juu ya Babuloni mbingu na dunia na wale wote walio ndani yazo kwa hakika watapiga kilio kikuu kwa kushangilia.” (Yeremia 51:48, NW) Wakati Babuloni Mkubwa aharibiwapo, sauti kutoka katika mbingu inafikisha ujumbe wayo kwenye upeo kwa kusema juu ya Babuloni Mkubwa hivi: “Uwe na nderemo juu yake, O mbingu, pia nyinyi watakatifu na nyinyi mitume na nyinyi manabii, kwa sababu kwa hukumu Mungu ametoza adhabu kutoka kwake kwa ajili ya nyinyi!” (Ufunuo 18:20, NW) Yehova na malaika watapendezwa sana kuona utowesho wa adui wa kale wa Mungu, kama vile watakavyopendezwa mitume na wale manabii Wakristo wa mapema, ambao kwa sasa wamefufuliwa na wamechukua cheo chao katika ule mpango wa wazee 24.—Linga Zaburi 97:8-12.
8 Kweli kweli, “watakatifu” wote,—wawe wamefufuliwa kwenda kwenye mbingu au wangali wanaendelea kuishi duniani—watapiga kilio kikuu kwa shangwe, kama vile utakavyofanya umati mkubwa wa kondoo wengine unaoshirikiana nao. Baada ya wakati kupita, watu wote waaminifu wa zamani watafufuliwa ndani ya mfumo mpya wa mambo, na wao vilevile watajiunga katika kushangilia. Watu wa Mungu hawakujaribu kujilipiza kisasi wenyewe juu ya wanyanyasaji wao wa dini bandia. Wao wamekumbuka maneno ya Yehova: “Kisasi ni changu mimi; mimi nitalipa, asema Yehova.” (Warumi 12:19; Kumbukumbu 32:35, 41-43, NW) Basi, Yehova amelipa sasa. Damu yote iliyomwagwa na Babuloni Mkubwa itakuwa imekwisha lipizwa kisasi.
Kuvurumisha Jiwe Kubwa la Kusagia
9, 10. (a) Sasa malaika kabambe anafanya na kusema nini? (b) Ni tendo gani kama hilo linalofanywa na huyo malaika wa Ufunuo 18:21 lilitukia katika siku ya Yeremia, na hilo lilitoa dhamana gani? (c) Tendo linalochukuliwa na malaika kabambe aliyeonwa na Yohana linatoa dhamana gani?
9 Jambo ambalo Yohana anafuata kuona linathibitisha kwamba hukumu ya Yehova juu ya Babuloni Mkubwa ni ya kukata maneno: “Na malaika kabambe akainua juu jiwe kama jiwe kubwa la kusagia na kulivurumisha ndani ya bahari, kusema: ‘Hivyo kwa mtupo wa kasi sana Babuloni jiji kubwa atavurumishwa chini, na yeye hatapatikana kamwe tena.’” (Ufunuo 18:21, NW) Katika wakati wa Yeremia, tendo kama hilo likiwa na maana kubwa ya kiunabii lilifanywa. Yeremia alivuviwa aandike katika kitabu “mabaa yote ambayo yangekuja juu ya Babuloni.” Yeye alimpa Seraya kitabu na kumwambia asafiri hadi Babuloni. Huko, akifuata maagizo ya Yeremia, Seraya alisoma julisho-wazi dhidi ya jiji hilo: “O Yehova, wewe mwenyewe umesema dhidi ya mahali hapa, ili kupakatilia mbali pasipate kuwa na mkazi ndani yapo, ama binadamu ama hata mnyama wa nyumbani, bali kwamba pawe mahali patupu tu penye ukiwa hadi wakati usio dhahiri.” Kisha Seraya akafungilia jiwe kwenye kitabu na kukitupa ndani ya mto Eufrati, akisema: “Hivi ndivyo Babuloni litazama chini na halitainuka kamwe kwa sababu ya baa ambalo mimi ninaleta juu yake.”—Yeremia 51:59-64, NW.
10 Kutupwa kwa kitabu ndani ya mto kikiwa kimefungiliwa jiwe kulikuwa dhamana kwamba Babuloni lingetumbukia ndani ya hali ya kutokomea kabisa, lisipate kupona kamwe. Kuona kwa mtume Yohana malaika kabambe akifanya tendo linalofanana na hilo hali kadhalika ni dhamana yenye nguvu kwamba kusudi la Yehova kuelekea Babuloni Mkubwa litatimizwa. Hali ya kuangamia kabisa ya Babuloni wa kale leo hushuhudia kwa nguvu sana kitakachoangukia dini bandia katika wakati ujao ulio karibu.
11, 12. (a) Sasa malaika kabambe anahutubiaje Babuloni Mkubwa? (b) Yeremia alitoaje unabii kuhusu Yerusalemu lililoasi imani, na huo uliashiria nini kwa ajili ya siku yetu?
11 Sasa malaika kabambe anahutubia Babuloni Mkubwa, kusema hivi: “Na sauti ya waimbaji ambao hujifuatanisha kwa kinubi na ya wanamuziki na ya wanafilimbi na ya wanatarumbeta haitasikiwa tena kamwe ndani ya wewe, na hakuna fundi wa kazi ya uchumi yoyote ambaye atapatikana tena wakati wowote ndani ya wewe, na hakuna sauti ya jiwe la kusagia itakayosikika tena wakati wowote ndani yako, na hakuna nuru ya taa ambayo itaangaza tena wakati wowote ndani ya wewe, na hakuna sauti ya bwana-arusi na ya bibi-arusi ambayo itasikiwa tena wakati wowote ndani ya wewe; kwa sababu wauza-bidhaa wasafiri wako walikuwa ndio watu wenye vyeo vya juu wa dunia, kwa maana kwa zoea lako la uwasiliano na roho mataifa yote yaliongozwa vibaya.”—Ufunuo 18:22, 23, NW.
12 Kwa semi zinazolinganika, Yeremia alitoa unabii kuhusu Yerusalemu asi-imani: “Mimi nitaharibu kutoka wao mvumo wa mchachawo na mvumo wa kushangilia, na sauti ya bwana-arusi na sauti ya bibi-arusi, na mvumo wa kinu cha mkono na nuru ya taa. Na bara hili lote lazima liwe mahali palipoteketezwa na kitu cha kutia kimako.” (Yeremia 25:10, 11, NW) Ikiwa ndiyo sehemu kuu ya Babuloni Mkubwa, Jumuiya ya Wakristo itakuwa magofu yasiyo na uhai, kama vile imeonyeshwa wazi sana na ukiwa wa Yerusalemu baada ya 607 K.W.K. Jumuiya ya Wakristo ambayo wakati mmoja ilishangilia kwa moyo mkunjufu na ikashughulika kwa kelele ya kila siku itajikuta yenyewe ikiwa imeshindwa na kutupiliwa mbali.
13. Ni badiliko gani la ghafula linalomfikilia Babuloni Mkubwa, na tokeo ni nini kwa “wauza-bidhaa wasafiri” wake?
13 Kweli kweli, kama vile malaika huyo anavyomwambia Yohana, Babuloni Mkubwa wote atageuka kutoka milki ya ulimwengu yenye nguvu, na kuwa bara-ukiwa kavu mithili ya mahame. “Wauza-bidhaa” wake, kutia na mamilionea wa vyeo vya juu, wametumia dini yake kwa kujinufaisha kibinafsi au kama kisetiri cha mabaya, na hao viongozi wa kidini wameliona kuwa jambo lenye kufaidi kushiriki pamoja nao katika umashuhuri huo. Lakini wauza-bidhaa hao hawatakuwa tena na Babuloni Mkubwa akiwa mshirika wao katika kufanya mabaya. Yeye hatayapofusha macho tena mataifa ya dunia kwa mazoea ya mafumbo yake ya kidini.
Hatia ya Damu Yenye Kutisha
14. Ni nini anayotoa malaika kabambe kuwa ndiyo sababu ya ukali wa hukumu ya Yehova, na Yesu alisema nini hali moja na hivyo wakati alipokuwa duniani?
14 Kwa kumalizia, malaika kabambe amwambia Yohana sababu ya Yehova kumhukumu Babuloni Mkubwa kwa ukali hivyo. “Ndiyo,” asema malaika, “katika yeye ilipatikana damu ya manabii na ya watakatifu na ya wale wote ambao wamechinjwa juu ya dunia.” (Ufunuo 18:24, NW) Alipokuwa duniani, Yesu aliambia viongozi wa kidini kwamba wao walistahili kutozwa hesabu kwa ajili ya “damu yote yenye uadilifu iliyomwagwa juu ya dunia, kutoka damu ya Abeli mwadilifu” na kuendelea. Kulingana na hilo, kizazi hicho kombokombo kiliharibiwa katika 70 W.K. (Mathayo 23:35-38, NW) Leo, kizazi kingine cha wanadini kinabeba hatia ya damu kwa ajili ya kunyanyasa watumishi wa Mungu.
15. Kanisa Katoliki katika Ujeremani ya Nazi lilikuwaje na hatia ya damu katika visa viwili?
15 Katika kitabu chake The Catholic Church and Nazi Germany, Guenter Lewy anaandika: “Wakati Mashahidi wa Yehova walipokandamizwa katika Bavaria Aprili 13 [1933] Kanisa hata lilikubali mgawo liliopewa na Wizara ya Elimu na Dini wa kuripoti juu ya washiriki wa farakano hilo walioendelea kuzoea dini hiyo iliyokatazwa.” Hivyo Kanisa Katoliki linashiriki daraka la kupelekwa kwa maelfu ya Mashahidi kwenye kambi za mateso; mikono yalo imetiwa madoa ya damu ya uhai wa mamia ya Mashahidi ambao walinyongwa. Wakati Mashahidi vijana, kama Wilhelm Kusserow, walipoonyesha kwamba wangekufa kijasiri kwa kupigwa risasi na kikosi cha wapiga risasi, Hitla aliamua kwamba kikosi cha wapiga risasi hakikuwafaa wakataaji kidhamira; kwa hiyo Wolfgang ndugu ya Wilhelm, akiwa na umri wa miaka 20, alikufa kwa njia ya gilotini. Wakati ule ule, Kanisa Katoliki lilikuwa likiwatia moyo vijana Wakatoliki Wajeremani wafe katika jeshi la bara-baba lao. Hatia ya damu ya hilo kanisa yaonekana wazi!
16, 17. (a) Ni hatia gani ya damu ambayo ni lazima Babuloni Mkubwa ashtakiwe, na Vatikani ilikuwaje na hatia ya damu kuhusu Wayahudi waliouawa katika michinjo-chinjo ya Kinazi? (b) Ni katika njia gani moja ambayo kwayo dini bandia ina lawama kwa ajili ya kuuawa kwa mamilioni ya watu katika mamia ya vita katika nyakati zetu?
16 Hata hivyo, unabii unasema kwamba lazima Babuloni Mkubwa ashtakiwe kwa damu ya “wale wote ambao wamechinjwa juu ya dunia.” Hakika hilo limekuwa kweli katika nyakati za ki-siku-hizi. Mathalani, kwa kuwa hila ya Katoliki ndiyo iliyomsaidia Hitla apate mamlaka katika Ujeremani, Vatikani inashiriki hatia ya damu iliyo mbaya sana juu ya Wayahudi milioni sita waliokufa katika michinjo-chinjo ya Kinazi. Na zaidi, katika nyakati zetu, watu zaidi ya milioni mia moja wameuawa katika mamia ya vita. Je! dini bandia ina lawama kwa habari hii? Ndiyo, kwa njia mbili.
17 Njia moja ni kwamba vita vingi vinahusiana na tofauti za kidini. Mathalani, jeuri katika India kati ya Waislamu na Wahindu katika 1946-48 ilichochewa na dini. Mamia ya maelfu ya maisha yalipotea. Pambano kati ya Iraki na Irani katika miaka ya 1980 lilihusiana na tofauti za kimafarakano, kukiwa na mamia ya maelfu waliouawa. Jeuri kati ya Wakatoliki na Waprotestanti katika Ailandi ya Kaskazini imetwaa maelfu ya maisha. Akichunguza uwanja huu, mleta habari za magazetini C. L. Sulzberger alisema hivi katika 1976: “Ni ukweli wenye kuhuzunisha kwamba pengine nusu au zaidi ya vita vinavyopiganwa sasa kotekote katika ulimwengu ama kwa wazi ni mapambano ya kidini ama yanahusu mabishano ya kidini.” Kweli kweli, imekuwa hivyo muda wote wa historia yenye msukosuko ya Babuloni Mkubwa.
18. Ni ipi njia ya pili ambayo kwayo dini za ulimwengu zina hatia ya damu?
18 Ni ipi ile njia nyingine? Kwa maoni ya Yehova, dini za ulimwengu zina hatia ya damu kwa sababu hizo hazikufundisha kwa kusadikisha wafuasi wazo ukweli wa matakwa ya Yehova kwa ajili ya watumishi wake. Hizo hazikufundisha watu kwa kusadikisha kwamba waabudu wa kweli lazima wamwige Yesu Kristo na kuonyesha wengine upendo bila kujali asili yao ya kitaifa. (Mika 4:3, 5; Yohana 13:34, 35; Matendo 10:34, 35; 1 Yohana 3:10-12) Kwa sababu dini ambazo zinajumlika kuwa Babuloni Mkubwa hazikufundisha vitu hivi, wafuasi wazo wamevutwa kuingizwa ndani ya kizingo cha vita vya kimataifa. Lo! jinsi hilo lilivyokuwa wazi katika vile vita viwili vya ulimwengu vya nusu ya kwanza ya karne ya 20, ambavyo vyote viwili vilianza katika Jumuiya ya Wakristo na vikatokeza kuchinjana kwa wanadini! Ikiwa wote wanaodai kuwa Wakristo wangalishikamana na kanuni za Biblia, vita hivyo havingaliweza kutukia kamwe.
19. Ni hatia ya damu gani yenye kutisha sana anayobeba Babuloni Mkubwa?
19 Yehova anaweka lawama la umwagaji-damu huu wote kwenye nyayo za Babuloni Mkubwa. Ikiwa viongozi wa kidini, hasa wale walio katika Jumuiya ya Wakristo, wangalifundisha watu wao ukweli wa Biblia, umwagaji-damu mkubwa sana hivyo haungalitukia. Kwa kweli, basi, kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, Babuloni Mkubwa—yule kahaba mkubwa na milki ya ulimwengu ya dini bandia—lazima amjibu Yehova si kwa ajili ya “damu ya manabii na ya watakatifu” tu ambao yeye amenyanyasa na akaua bali pia kwa ajili “ya wale wote ambao wamechinjwa juu ya dunia.” Kweli kweli Babuloni Mkubwa anabeba hatia ya damu yenye kutisha sana. Na apotelee mbali wakati uharibifu wake unapotukia!
[Sanduku katika ukurasa wa 270]
Gharama ya Kuridhiana
Guenter Lewy anaandika katika kitabu chake The Catholic Church and Nazi Germany: “Kama Ukatoliki wa Ujeremani tangu mwanzo ungalishikamana na mwongozo wa kupinga kwa dhati utawala wa Nazi, historia ya ulimwengu ingaliweza kuchukua mwendo tofauti. Hata kama mng’ang’ano huu ungalikosa mwishowe kabisa kumshinda Hitla na kuzuia uhalifu wake mwingi, kwa oni hili ungaliinua sana hadhi ya kiadili ya Kanisa hilo. Gharama ya kibinadamu kwa ukinzani huu ingalikuwa kubwa bila kukanika, lakini dhabihu hizo zingalikuwa zimetolewa kwa ajili ya kusudi kubwa zaidi ya yote. Hitla akiwa haungwi mkono nyumbani, yamkini hangalithubutu kwenda vitani na kihalisi mamilioni ya maisha yangaliokolewa. . . . Wakati Wajeremani wapinga Unazi walipoteswa mpaka kifo katika kambi za mateso za Hitla, wakati weledi wa Polandi walipochinjwa, wakati mamia ya maelfu ya Warusi walipokufa kama tokeo la kutendwa kama Untermenschen [nusu-binadamu] wa Kislavi, na wakati binadamu 6,000,000 walipouawa kimakusudi kwa kuwa ‘si Waarya,’ maofisa wa Kanisa Katoliki katika Ujeremani walitegemeza utawala uliokuwa ukifanya uhalifu huu. Papa katika Roma, kichwa cha kiroho na mwalimu wa kiadili mkuu zaidi ya wote wa Kanisa Katoliki la Roma, alikaa kimya.”—Kurasa 320, 341.
[Picha katika ukurasa wa 268]
“Ni vibaya mno, ni vibaya mno,” wasema watawala
[Picha katika ukurasa wa 268]
“Ni vibaya mno, ni vibaya mno,” wasema wauza-bidhaa