Je! Biblia Hujipinga Yenyewe?
MTUNGA vitabu Henry Van Dyke aliandika hivi wakati mmoja: “Ikiwa imetoka Mashariki na kuvikwa umbo na mfano wa Kimashariki, Biblia husema kuhusu mambo mengi mbalimbali ya ulimwengu nayo huingia nchi moja hadi nyingine na kupata kwamba inapendwa na watu kila mahali. Imejifunza jinsi ya kusema na moyo wa mwanadamu katika mamia ya lugha. Watoto huzisikiliza hadithi zayo kwa mshangao na furaha, na watu wenye hekima huzitafakari kuwa mifano kwa maisha. Waovu na wenye kiburi hutetemeka kwa ajili ya maonyo yayo, lakini kwa wale wenye uchungu na wenye kutubu ina sauti kama ya mama. . . . Mtu ambaye hazina hiyo ni yake mwenyewe si maskini wala hana upweke.”
Biblia kwa kweli ‘imejifunza jinsi ya kusema katika mamia ya lugha.’ Angalau kimoja cha vitabu vyayo 66 kimetafsiriwa katika ndimi zipatazo 1,970. Mamilioni huona Biblia kuwa zawadi kutoka kwa Mungu na huisoma kwa furaha na kwa manufaa yao. Hata hivyo, wengine husema kwamba inajipinga yenyewe na kwa hiyo haitegemeki. Uchunguzi wenye uangalifu hufunua nini?
Kama ionyeshwavyo na picha yetu ya jalada, Mungu alitumia wanaume waaminifu kuiandika Biblia. Kwa kweli, uchanganuzi wenye uangalifu wa Biblia hufunua kwamba iliandikwa na watu wapatao 40 kwa kipindi cha zaidi ya karne 16. Je! walikuwa waandishi wenye ustadi mwingi? La. Miongoni mwao mtu aweza kupata mchungaji, mvuvi, mkusanya kodi, tabibu, mfanyi hema, kuhani, nabii, na mfalme. Maandishi yao mara nyingi yalitaja watu na desturi ambazo hatufahamu katika karne ya 20. Kwa kweli, waandishi wa Biblia wenyewe hawakuelewa sikuzote umaana wa yale waliyoandika. (Danieli 12:8-10) Kwa hiyo hatupaswi kushangaa ikiwa tunakabili magumu fulani tunaposoma Biblia.
Je! magumu hayo yaweza kusuluhishwa? Je! Biblia hujipinga yenyewe? Ili tupate kujua, acheni tuchunguze baadhi ya mifano.
Haya kwa Kweli Ni Magumu?
▪ Kaini alipata wapi mke wake? (Mwanzo 4:17)
Mtu huenda akafikiri kwamba baada ya kuuawa kimakusudi kwa Abeli, ni ndugu yake mwenye hatia Kaini na wazazi wao, Adamu na Hawa tu, walioachwa duniani. Hata hivyo, Adamu na Hawa walikuwa na familia kubwa. Kulingana na Mwanzo 5:3, 4, Adamu alikuwa na mwana aliyeitwa Sethi. Usimulizi huo waongeza hivi: “Siku za Adamu baada ya kumzaa Sethi zilikuwa miaka mia nane, akazaa wana, waume na wake.” Kwa hiyo Kaini alimwoa dada yake au labda mmoja wa wapwa wake. Kwa kuwa ainabinadamu ilikuwa karibu sana na ukamilifu wa kibinadamu wakati huo, ndoa ya jinsi hiyo yaonekana haikuleta matatizo ya afya yawezayo kuhatarisha wazao wa muungano wa jinsi hiyo leo.
▪ Ni nani waliomwuza Yusufu Misri?
Mwanzo 37:27 husema kwamba ndugu zake Yusufu waliamua kumwuza kwa Waishmaeli fulani. Lakini mstari ufuatao hutaarifu hivi: “Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi [ndugu za Yusufu] wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.” Je! Yusufu aliuzwa kwa Waishmaeli au kwa Wamidiani? Huenda ikawa Wamidiani walikuwa pia wakiitwa Waishmaeli, waliokuwa na uhusiano wa kiukoo nao kupitia babu yao Abrahamu. Au huenda ikawa wafanya biashara Wamidiani walikuwa wakisafiri pamoja na msafara wa Waishmaeli. Kwa vyovyote vile, ndugu za Yusufu ndio walimwuza, na baadaye angeweza kuwaambia hivi: “Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri.”—Mwanzo 45:4.
▪ Ni Waisraeli wangapi waliokufa kwa ajili ya mahusiano yenye kukosa maadili pamoja na wanawake Wamoabi na kwa ajili ya kushiriki katika ibada ya Baali wa Peori?
Hesabu 25:9 hutaarifu hivi: “Waliokufa kwa hilo pigo [kutoka kwa Mungu kwa ajili ya mwenendo wao mwovu] walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao.” Hata hivyo, Mtume Paulo alisema hivi: “Wala tusifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.” (1 Wakorintho 10:8) Labda idadi ya wale wa-liouawa ilikuwa kati ya 23,000 na 24,000, hivi kwamba tarakimu yoyote kati ya hizo mbili ingefaa. Hata hivyo, kitabu cha Hesabu huonyesha mahususi kwamba “wakuu wote wa hao watu” waliohusika katika dhambi hiyo waliuawa na mahakimu. (Hesabu 25:4, 5) Huenda ikawa “wakuu” hao wenye hatia walikuwa 1,000, wakijumlika kuwa 24,000 wanapoongezwa kwa wale 23,000 waliotajwa na Paulo. Ingawa yaonekana 23,000 walikuwa wahanga wa moja kwa moja wa pigo hilo kutoka kwa Mungu, wote 24,000 walipatwa na pigo la Yehova kwa sababu wote walikufa chini ya amri yake ya hukumu kali.—Kumbukumbu la Torati 4:3.
▪ Kwa kuwa Agagi aliishi wakati wa mfalme Sauli, je, rejezeo la Balaamu la mapema zaidi kwa mfalme Mwamaleki mwenye jina hilo halikuwa hitilafu?
Katika yapata 1473 K.W.K., Balaamu alitabiri kwamba mfalme wa Israeli ‘angeadhimishwa kuliko Agagi.’ (Hesabu 24:7) Hakuna rejezeo jingine lililofanywa kwa Agagi mpaka utawala wa Mfalme Sauli (1117-1078 K.W.K.). (1 Samweli 15:8) Hata hivyo, hilo halikuwa hitilafu kwani huenda ikawa “Agagi” lilikuwa jina la cheo cha kifalme sawa na lile la Farao katika Misri. Yawezekana pia kwamba Agagi lilikuwa jina la kibinafsi lililotumiwa-tumiwa na watawala Waamaleki.
▪ Ni nani aliyemsababisha Daudi awahesabu Waisraeli?
Samweli ya pili 24:1 hutaarifu hivi: “Tena hasira ya BWANA [Yehova, New World Translation of the Holy Scriptures—With References] ikawaka juu ya Israeli, akamtia Daudi [au, “Daudi alipochochewa,” kielezi-chini] nia juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda.” Lakini si Yehova aliyemsukuma Mfalme Daudi atende dhambi, kwani 1 Mambo ya Nyakati 21:1 husema hivi: “Tena shetani [au, “mpingaji,” kielezi-chini, NW] akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli.” Mungu hakupendezwa na Waisraeli na kwa hiyo alimruhusu Shetani Ibilisi alete dhambi hiyo juu yao. Kwa sababu hiyo, 2 Samweli 24:1 husomwa kana kwamba Mungu mwenyewe ndiye alifanya jambo hilo. Kwa kupendeza, tafsiri ya Joseph B. Rotherham husomwa hivi: “Hasira ya Yahweh iliwaka dhidi ya Israeli, hivi kwamba akamsababisha Daudi asukumwe dhidi yao akisema, Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.”
▪ Mtu anaweza kupatanishaje zile tarakimu tofauti zilizotolewa za Waisraeli na Wayudea katika hesabu ya Daudi?
Kwenye 2 Samweli 24:9 tarakimu ya Waisraeli ni 800,000, na ya Wayudea ni 500,000, hali 1 Mambo ya Nyakati 21:5 huhesabu wanaume wa vita wa Israeli kuwa 1,100,000 na wa Yuda kuwa 470,000. Wanajeshi 288,000 waliorodheshwa kwa kawaida katika utumishi wa kifalme, wakigawanywa katika vikundi 12 kila kimoja kikiwa na wanajeshi 24,000, kila kikundi kikitumikia mwezi mmoja kwa mwaka. Kulikuwako wengine 12,000 waliotumikia wakuu 12 wa makabila, wakijumlika kuwa 300,000. Yaonekana kwamba wale 1,100,000 wa 1 Mambo ya Nyakati 21:5 wanatia ndani wale 300,000 waliokwisha orodheshwa, hali 2 Samweli 24:9 haiwatii ndani. (Hesabu 1:16; Kumbukumbu la Torati 1:15; 1 Mambo ya Nyakati 27:1-22) Kwa habari ya Yuda, 2 Samweli 24:9 yaonekana lilitia ndani watu 30,000 katika jeshi la kuchunguza lililokuwa karibu na mahali pa majeshi ya Wafilisti lakini ambao hawakutiwa ndani ya tarakimu ya 1 Mambo ya Nyakati 21:5. (2 Samweli 6:1) Tukikumbuka kwamba 2 Samweli na 1 Mambo ya Nyakati yaliandikwa na wanaume wawili wenye maoni na makusudi tofauti, twaweza kwa urahisi kupatanisha tarakimu hizo.
▪ Ni nani aliyekuwa babake Shealtieli?
Maandiko fulani huonyesha kwamba Yekonia (Mfalme Yehoyakini) ndiye alikuwa baba wa kimnofu wa Shealtieli. (1 Mambo ya Nyakati 3:16-18; Mathayo 1:12) Lakini mwandishi wa Gospeli Luka alimwita Shealtieli mwana “wa Neri.” (Luka 3:27) Neri yaonekana alimpa Shealtieli binti yake kuwa mke. Kwa kuwa Waebrania kwa kawaida walirejezea mwana mkwe kuwa mwana, hasa katika orodha za vizazi, Luka angeweza kwa kufaa kumwita Shealtieli mwana wa Neri. Vivyo hivyo, Luka alimrejezea Yusufu kuwa mwana wa Heli, ambaye kwa kweli alikuwa baba ya Mariamu, mke wa Yusufu.—Luka 3:23.
Kupatanisha Maandiko Yanayohusu Yesu
▪ Yesu Kristo aliondosha kutoka wanaume wangapi, wale roho waovu walioingia lile kundi kubwa la nguruwe?
Mwandishi wa Gospeli Mathayo ataja wanaume wawili, lakini Marko na Luka wanamtaja mmoja tu. (Mathayo 8:28; Marko 5:2; Luka 8:27) Yaonekana, Marko na Luka huelekeza fikira kwa mwanamume mmoja tu aliyepagawa na roho waovu kwa sababu Yesu alisema naye na kisa chake kilitokeza zaidi. Yawezekana, mwanamume huyo alikuwa mwenye jeuri zaidi au alikuwa ameteseka chini ya udhibiti wa roho waovu kwa muda mrefu zaidi. Baadaye, labda ni mwanamume huyo peke yake aliyetaka kuandamana na Yesu. (Marko 5:18-20) Katika kisa kilichofanana na hicho, Mathayo alisema juu ya watu wawili vipofu walioponywa na Yesu, hali Marko na Luka hutaja mmoja tu. (Mathayo 20:29-34; Marko 10:46; Luka 18:35) Hayo hayakupingana, kwani kulikuwako angalau mtu mmoja wa jinsi hiyo.
▪ Yesu alivaa vazi la rangi gani siku ya kifo chake?
Kulingana na Marko (15:17) na Yohana (19:2), askari-jeshi walimvika Yesu vazi la zambarau. Lakini Mathayo (27:28) aliliita “vazi jekundu,” akikazia wekundu walo. Kwa kuwa zambarau ni rangi yoyote yenye mchanganyiko wa rangi nyekundu na buluu pia, Marko na Yohana wanaafikiana kwamba vazi hilo lilikuwa na rangi nyekundu. Mrudisho wa nuru na mandhari-nyuma ingeweza kutokeza rangi tofauti-tofauti za vazi hilo, na waandishi wa Gospeli walitaja ile rangi waliyoona zaidi au iliyoonwa zaidi na wale waliowapa habari hiyo. Tofauti hiyo ndogo yaonyesha hali ya utu tofauti ya kila mwandishi na inathibitisha kwamba hakukuwa kupingana kokote.
▪ Ni nani aliyebeba mti wa mateso wa Yesu?
Yohana (19:17) alisema hivi: “[Yesu] akatoka, hali akijichukulia msalaba [mti wa mateso, NW] wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.” Lakini Mathayo (27:32), Marko (15:21), na Luka (23:26) husema kwamba ‘walipokuwa wakitoka, walimshurutisha Simoni Mkirene auchukue mti wa mateso wake.’ Yesu aliubeba mti wa mateso wake, kama vile Yohana alivyotaarifu. Hata hivyo, katika usimulizi wake uliofupishwa, Yohana hakuongeza jambo la kwamba baadaye Simoni alishurutishwa auchukue mti wa mateso. Kwa hiyo, masimulizi ya Gospeli yanapatana kwa habari hiyo.
▪ Yuda Iskariote alikufaje?
Mathayo 27:5 hutaarifu kwamba Yuda alijinyonga mwenyewe, hali Matendo 1:18 husema kwamba “akaanguka kwa kasi akapasuka, matumbo yake yote yakatoka.” Hali Mathayo huonekana akishughulikia njia ya jaribu hilo la kujiua, Matendo hueleza matokeo. Yaonekana Yuda alifunga kamba kwenye tawi la mti, akaweka tanzi shingoni pake, akajaribu kujinyonga mwenyewe kwa kuruka kutoka kwenye genge. Yaonekana kwamba ama kamba ama tawi la mti lilivunjika hivi kwamba akaanguka chini na kupasuka kwenye miamba iliyokuwa chini. Sura ya nchi izungukayo Yerusalemu hufanya mkataa huo ufae.
Wewe Utayaonaje Mambo?
Tukikabili mambo yanayoonekana kuwa hitilafu katika Biblia, ni vema kutambua kwamba watu mara nyingi husema mambo yanayoonekana yakipingana lakini ambayo huelezwa au hueleweka kwa urahisi. Kwa mfano, mfanya biashara huenda akamwandikia mtu barua kwa kumpa karani wake imla ya barua hiyo. Akiulizwa, angesema kwamba yeye ndiye alipeleka barua hiyo. Lakini kwa kuwa karani wake ndiye aliyeipiga chapa na kuipeleka barua hiyo kwa njia ya posta, yeye angeweza kusema kwamba yeye ndiye aliyeipeleka. Vivyo hivyo, Mathayo (8:5) aliposema kwamba akida mmoja alikuja kumwomba Yesu hisani, hali Luka (7:2, 3) akasema kwamba mwanamume huyo aliwatuma wawakilishi, hawakupingana.
Mifano iliyotangulia huonyesha kwamba magumu ya Biblia yaweza kusuluhishwa. Kwa hiyo, kuna sababu nzuri kuwa na mtazamo chanya kuelekea Maandiko. Mtazamo huo ulipendekezwa kwa maneno haya yaliyo katika Biblia moja ya familia iliyotangazwa kwa chapa katika mwaka wa 1876:
“Mtazamo ufaao wa kushughulika na magumu hayo ni, kuyaondolea mbali sana iwezekanavyo, na kushikamana na kujitiisha kwa ukweli, hata iwapo kila wingu haliwezi kuondolewa mbali. Twapaswa kuuiga mfano wa mitume, ambao, wakati baadhi ya wanafunzi walipoudhika na yale waliyoita ‘neno gumu,’ hivi kwamba wakamwacha Kristo, walinyamazisha kila upinzani kwa maneno haya: ‘Bwana, twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uhai wa milele, nasi tuna uhakika wa kwamba Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.’ . . . Tunapoona kweli ionekanayo kupinga kweli nyingine, acheni tujaribu kuzipatanisha, na kuzionyesha kwa wote kuwa zapatana.”—Yohana 6:60-69.
Je! wewe utachukua msimamo huo? Baada ya kuchunguza mifano michache tu inayoonyesha upatani wa Maandiko, inatazamiwa kwamba unaafikiana na mtunga zaburi aliyemwambia Mungu hivi: “Jumla ya neno lako ni kweli.” (Zaburi 119:160) Mashahidi wa Yehova wana maoni hayo juu ya Biblia nzima nao watatoa kwa furaha sababu za imani yao katika Biblia. Kwa nini usizungumzie kitabu hiki kisicho na kifani pamoja nao? Ujumbe wacho wenye kuchangamsha moyo waweza kwa kweli kukujaza na tumaini na furaha ya kweli.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Je! wewe umewauliza Mashahidi wa Yehova ni kwa nini wao wana imani katika Biblia?