Walifanya Mapenzi ya Yehova-
Tendo la Kusamehe Latokeza Wokovu
WANA kumi wa Yakobo waliokuwa mbele ya waziri mkuu wa Misri walijua siri yenye kutia hofu. Miaka kadhaa mapema walikuwa wamemwuza Yosefu, ndugu yao wa kambo, akawe mtumwa, wakinuia kumwambia baba yao kwamba alikuwa ameuawa na mnyama mkali.—Mwanzo 37:18-35.
Sasa, miaka 20 hivi baadaye, njaa kali ilikuwa imewalazimisha wanaume hao kumi waende Misri kununua nafaka. Lakini mambo hayakuwa rahisi hivyo. Waziri mkuu, aliyekuwa pia msimamizi wa chakula, alidai ya kwamba walikuwa wapelelezi. Akamfunga mmoja wao na kuwaamuru wale wengine warudi kwao wakamlete ndugu yao mchanga zaidi, Benyamini. Walipomleta, waziri mkuu huyo akapanga njama Benyamini akamatwe.—Mwanzo 42:1–44:12.
Yuda, mmoja wa wana wa Yakobo, akateta. ‘Tukirudi nyumbani bila Benyamini,’ akasema, ‘baba yetu atakufa.’ Kisha jambo fulani likatendeka ambalo wala Yuda wala wenzake waliosafiri pamoja naye hawakutarajia. Baada ya kuamuru wote watoke nje isipokuwa wana wa Yakobo, waziri mkuu huyo akalia kwa sauti kubwa. Ndipo, baada ya kutulia, akawajulisha hivi: “Mimi ndimi Yusufu [“Yosefu,” NW].”—Mwanzo 44:18–45:3.
Rehema na Ukombozi
“Baba yangu angali hai bado?” Yosefu akawauliza ndugu zake wa kambo. Hawakumjibu. Kwa kweli, ndugu za Yosefu wa kambo hawakujua la kusema. Je, wafurahi, au waogope? Kwa vyovyote, miaka 20 iliyopita, walikuwa wamemwuza mtu huyu utumwani. Yosefu alikuwa na uwezo wa kuwafunga, kuwafukuza warudi nyumbani bila chakula, au hata kuwaua! Kwa sababu nzuri, ndugu za Yosefu wa kambo “hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake.”—Mwanzo 45:3.
Upesi Yosefu akawatuliza wanaume hawa. “Karibuni kwangu,” akawaambia. Wakamsikiza. Kisha akasema: “Mimi ni Yusufu [“Yosefu,” NW], ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha za watu.”—Mwanzo 45:4, 5.
Yosefu hakuwarehemu bila sababu. Tayari alikuwa amethibitisha kwamba walikuwa na toba. Kwa mfano, Yosefu alipodai ya kwamba ndugu zake wa kambo walikuwa wapelelezi, aliwasikia wakisemezana kwa siri: “Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, . . . kwa hiyo shida hii imetupata.” (Mwanzo 42:21) Isitoshe, Yuda alikuwa amejitolea kuwa mtumwa badala ya Benyamini ili mwanamume huyo mchanga arudishwe kwa baba yake.—Mwanzo 44:33, 34.
Hivyo basi, Yosefu alikuwa na haki ya kuwarehemu. Naam, alitambua kwamba kufanya hivyo kungeokoa familia yao yote. Kwa hiyo, Yosefu akawaambia ndugu zake wa kambo warudi kwa baba yao, Yakobo, na kumwambia hivi: “Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu [“Yosefu,” NW], Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie. Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, utakuwa karibu nami, wewe, na wanao, na wana wa wanao, na wanyama wako, ng’ombe zako, na yote uliyo nayo. Nami nitakulisha huko.”—Mwanzo 45:9-11.
Yosefu Mkubwa Zaidi
Yesu Kristo aweza kuitwa Yosefu Mkubwa Zaidi, kwa maana hawa wanaume wawili wanafanana kwa mambo mengi yenye kutokeza. Kama Yosefu, Yesu alitendwa vibaya na ndugu zake, wazao wa Abrahamu kama yeye. (Linganisha Matendo 2:14, 29, 37.) Hata hivyo, mambo ya hawa wanaume wawili yalibadilika kiajabu. Baada ya muda, utumwa wa Yosefu ulibadilishwa, akafanywa waziri mkuu, cheo cha pili kutoka kwa Farao. Vivyo hivyo, Yehova alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, akamkweza kwa kumpa cheo kilicho bora zaidi “kwenye mkono wa kuume wa Mungu.”—Matendo 2:33; Wafilipi 2:9-11.
Akiwa waziri mkuu, Yosefu angeweza kuwagawia chakula wote waliokuja Misri kununua nafaka. Siku zetu, Yosefu Mkubwa Zaidi ana jamii ya mtumwa mwaminifu na mwenye busara duniani ambaye kupitia yeye anagawa chakula cha kiroho “kwa wakati ufaao.” (Mathayo 24:45-47; Luka 12:42-44) Kwa kweli, wale wanaomjia Yesu “hawatakuwa na njaa tena kamwe . . . kwa sababu Mwana-Kondoo, ambaye yuko katikati ya kiti cha ufalme, atawachunga, na kuwaongoza kwenye mabubujiko ya maji ya uhai.”—Ufunuo 7:16, 17.
Somo Kwetu
Yosefu aandaa mfano wenye kutokeza wa rehema. Kufuatia haki bila kusababu kungemlazimisha kuwaadhibu wale waliomwuza utumwani. Kwa upande mwingine, hisia za moyoni zingemfanya asitilie maanani makosa yao. Yosefu hakufanya lolote la hayo. Badala yake, alitahini toba ya ndugu zake wa kambo. Kisha, alipoona kwamba sikitiko lao lilikuwa la kweli, akawasamehe.
Twaweza kumwiga Yosefu. Iwapo mtu ambaye ametukosea aonyesha badiliko la kweli, twapaswa kumsamehe. Bila shaka, hatupaswi kamwe kuruhusu hisia za kijuujuu tu zitufanye tupuuze makosa mazito. Kwa upande mwingine, hatupaswi kuruhusu uchungu wa moyo utuzuie kuona vitendo vya toba ya kweli. Kwa hiyo acheni “[tuendelee] kuchukuliana mtu na mwenzake na kusameheana kwa hiari mtu na mwenzake.” (Wakolosai 3:13) Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tukimwiga Mungu wetu, Yehova, ambaye yuko “tayari kusamehe.”—Zaburi 86:5; Mika 7:18, 19.