Matazamio Mazuri Ajabu ya Kibinadamu Katika Paradiso Yenye Ufurahishi
“Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi [dunia, NW].”—MWANZO 1.28.
1, 2. Yehova anafanya kazi kwa upendo akiwa na kusudi gani kuhusu wanadamu, naye alimpa Adamu migawo gani ya kazi?
“MUNGU ni upendo,” twaambiwa hivyo katika Biblia Takatifu. Yeye hupendezwa na aina ya binadamu kwa upendo na bila ubinafsi na hufanya kazi bila kukoma ili wao waweze kuona shangwe milele kuhusu maisha zenye kujaa afya na amani katika paradiso ya kidunia yenye ufurahishi. (1 Yohana 4:16; linganisha Zaburi 16:11.) Mwanadamu wa kwanza, Adamu mkamilifu, alikuwa na maisha yenye kujaa amani na kazi ya kupendeza na ya kuleta shangwe. Muumba wa mwanadamu alimgawia kulima bustani hiyo ya Edeni yenye ufurahifu mwingi. Sasa Muumba wa mwanadamu akampa furushi jingine la kazi ya pekee, mgawo wenye wito wa ushindani, kama unavyoonyesha usimulizi wa lililotukia:
2 “Sasa Yehova Mungu alikuwa akifanyiza kutoka chini kila hayawani-mwitu wa uwanda na kila kiumbe anayeruka wa mbingu, na yeye akaanza kuwaleta kwa mwanadamu aone angemwita nini kila mmoja; na lolote lile ambalo mwanadamu angemwita, kila nafsi aliye hai, hilo lilikuwa ndilo jina lake. Kwa hiyo mwanadamu alikuwa anaita majina ya wanyama wote wa kufugwa na ya viumbe wanaoruka wa mbingu na ya kila hayawani-mwitu wa uwanda.”—Mwanzo 2:19, 20, NW.
3. Kwa nini hakukuwa na hofu kwa upande wa Adamu na viumbe wanyama?
3 Mwanadamu huyo alimwita farasi sus, ng’ombe ndume akamwita shohr, kondoo akamwita seh, mbuzi akamwita ʽez ndege akamwita ʽohph, njiwa akamwita yoh·nahʹ, tausi akamwita tuk·kiʹ, simba akamwita ʼar·yehʹaau ʼariʹa dubu akamwita dov, sokwe akamwita qohph, mbwa akamwita keʹlev, nyoka akamwita na·chashʹ, na kadhalika.a Alipoenda kwenye mto uliotiririka kutoka bustani ya Edeni, aliwaona samaki. Aliwapa samaki jina da·gahʹ. Mwanadamu huyo asiye na silaha hakuhisi akiwahofu wanyama hawa, wa kufugwa na wa mwituni, wala hakuwahofu ndege, nao hawakuhisi wakimhofu yeye, ambaye kwa silika walimtambua kuwa ndiye mkubwa wao, wa aina ya maisha yaliyo ya juu zaidi. Wao walikuwa viumbe wa Mungu, waliopewa na Yeye zawadi ya uhai, na mwanadamu hakuwa na tamaa wala mwelekeo wa kutaka kuwaumiza wala kuwaondolea uhai wao.
4. Tungeweza kufikiri nini kuhusu Adamu alivyowapa majina wanyama na ndege wote, na ni lazima hili liwe lilikuwa tukio la aina gani?
4 Usimulizi hautuambii ni kwa muda gani hasa mwanadamu alikuwa akionyeshwa wanyama wa kufugwa na wa mwituni na viumbe wanaoruka wa mbingu. Yote hayo yalifanywa chini ya mwongozo na mpango wa kimungu. Yaelekea kwamba Adamu alichukua wakati wa kuchunguza kila mnyama tofauti, akiangalia-angalia tabia zake na umbo lake la kumpambanua na wengine; ndipo angechagua jina ambalo lingemfaa huyo sawasawa. Hii ingeweza kumaanisha kwamba muda mwingi vya kutosha ulipita. Lilikuwa tukio la kumpendeza sana Adamu kuzoeana hivyo na viumbe hai wa dunia hii walio wa aina nyingi, naye alihitaji kuwa na uwezo mkubwa wa kiakili na nguvu za uneni ndipo aweze kupambanua kila moja ya aina hizi za viumbe walio hai kwa kuipa jina lililofaa.
5-7. (a) Yaelekea ni maswali gani ambayo yangetokea? (b) Ni majibu ya aina gani yaliyotolewa katika usimulizi wa uumbaji kwenye Mwanzo 1:1-25?
5 Lakini viumbe hai hawa walikuwa wameumbwa kwa kufuata utaratibu gani? Je! wanyama wa bara waliumbwa au hawakuumbwa kabla ya ndege, na mwanadamu alikuja kuhusishwa ndani wakati gani na katika utaratibu gani kuhusiana na viumbe hai wote hawa wa aina ya chini? Mungu aliutayarishaje uso wa dunia kwa ajili ya viumbe hai wa namna nyingi hivyo, akaandaa hewa ambamo ndege wangeweza kuruka juu sana kama vile warukavyo, akaleta maji ya kunywa na mboga za kimajani ili ziwe chakula, akafanya kimulikaji kikubwa cha kuangazia mchana na kuwezesha mwanadamu aone, na akafanya kimulikaji kisichoangaza sana kama hicho kingine ili kipambe usiku kwa uzuri? Kwa nini hali ya hewa ilikuwa na uanana mzuri na ujotojoto mzuri hivi kwamba mwanadamu angeweza kwenda huko na huko na kufanya kazi na kulala akiwa amejifunua wazi na uchi?
6 Mwanadamu huyo hakuachiwa kukisia-kisia majibu akiwa peke yake. Akili yake yenye kuulizia-ulizia mambo ilistahili majibu ya kiakili kutoka chanzo chenye mamlaka alichokijua kwa usahihi. Yeye hakuachwa peke yake awe mwana wa Mungu asiyejua lolote, bali yaelekea kwamba aliheshimiwa sana kuwa mwenye akili ya kiwango cha juu kwa kupewa ile historia nzuri sana ya uumbaji kama ilivyosimuliwa kwenye Mwanzo 1:1-25.
7 Adamu angeshukuru sana kwa usimulizi huo wenye kusisimua juu ya uumbaji. Ulieleza mambo mengi. Kutokana na jinsi ilivyosemwa, yeye alielewa kwamba vilikuwako vipindi virefu vitatu ambavyo Mungu aliviita siku kulingana na njia Yake ya kupima wakati, kabla ya kile kipindi cha nne cha uumbaji ambamo Mungu alitokeza vimulikaji vikubwa viwili katika utandao wa mbingu ili viwe alama ya siku fupi zaidi ya mwanadamu iliyo ya saa 24. Siku hii fupi zaidi ya kibinadamu duniani ilianza wakati wa kushuka kwa kile kimulikaji kikubwa zaidi hadi kushuka kwacho tena. Adamu pia alipata kujua kwamba yeye angekuwa na miaka ya wakati, na bila shaka alianza mara iyo hiyo kuhesabu miaka ya maisha yake. Kimulikaji kilicho kikubwa zaidi katika utandao wa mbingu kingemwezesha kufanya hivyo. Lakini kwa habari ya zile siku ndefu zaidi za uumbaji wa Mungu, mwanadamu wa kwanza aling’amua kwamba wakati huo yeye alikuwa akiishi katika siku ya sita ya kazi ya uumbaji wa kidunia wa Mungu. Hakuna mwisho uliokuwa umekwisha tajwa wa siku hiyo ya sita ya kuumba wanyama wote hao wa bara halafu ya kuumba mwanadamu akiwa kando peke yake. Sasa yeye angeuelewa utaratibu uliofuatwa kuumba mboga hai za kimajani, viumbe hai wa baharini, ndege walio hai, na wanyama wa bara. Lakini akiwa peke yake katika bustani ya Edeni, Adamu hakuwa wonyesho kamili, ulio mtimilifu wa kusudi la Mungu lenye upendo la kufanya mwanadamu awe katika Paradiso yake ya kidunia.
Kuumba Mwanamke wa Kwanza wa Kibinadamu
8, 9. (a) Mwanadamu mkamilifu alichungua akaona nini kuhusu viumbe wanyama, lakini yeye alikata shauri gani kuhusu yeye mwenyewe? (b) Kwa nini ilifaa kwamba mwanadamu mkamilifu hakumwomba Mungu mwenzi? (c) Usimulizi wa Biblia waelezaje juu ya kuumbwa kwa mke wa kwanza wa kibinadamu?
8 Mwanadamu huyo wa kwanza, akiwa na akili yake kamilifu na nguvu za kuchungua mambo, aliona kwamba katika makao ya ndege na wanyama, walikuwamo wa kiume na wa kike na kwamba walizaana kwa aina zao. Lakini kwa habari ya mwanadamu mwenyewe, mambo hayakuwa hivyo wakati huo. Ikiwa maoni ya mchunguo huu yalimwelekeza awe na wazo la kuona shangwe akiwa na mwandamani fulani, yeye hakupata mwenzi anayefaa miongoni mwa yeyote wa wanyama wale, wala hata miongoni mwa masokwe. Adamu angekata shauri kwamba hakukuwa na mwenzi wa kumfaa yeye kwa sababu kama angalikuwako, je! kwani Mungu asingalimletea yeye mwenzi huyo? Mwanadamu alikuwa ameumbwa peke yake kando na aina zote hizo za wanyama, na alikusudiwa awe tofauti! Yeye hakuwa na mwelekeo wa kujiamulia mambo mwenyewe na kukosa busara na kumwomba Mungu Muumba wake ampe mwenzi. Ilifaa mwanadamu huyo mkamilifu aache yote hayo mikononi mwa Mungu, kwa maana muda mfupi baadaye alikuta kwamba Mungu alikuwa amekata mashauri Yake mwenyewe kuhusu hali hiyo. Kuhusu hilo na lile ambalo sasa lilitukia, usimulizi watuambia hivi:
9 “Lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye [kuwa kikamilishio chake, NW]. Bwana [Yehova, NW] Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana [Yehova, NW] Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.”—Mwanzo 2:20-25.
10. Mwanamume mkamilifu aliitikiaje alipopewa mwanamke mkamilifu, na huenda maneno yake yakawa yalionyesha nini?
10 Mwanamume huyo alionyesha katika maneno yake kwamba alitosheka kikamili alipoletewa mwanamke mkamilifu awe msaidiaji na kikamilisho: “Sasa [hatimaye, NW] huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu.” Kulingana na maneno haya aliyoyasema alipomwona mwishowe mke wake aliyekuwa ametoka kuumbwa sasa hivi, ingeweza kuwa kwamba yeye alikuwa amengojea kwa muda fulani ndipo akampokea mfanani wake wa kibinadamu. Akieleza juu ya huyo kikamilisho chake, Adamu alimwita mke wake “Mwanamke” (ʼish·shahʹ au, kwa uhalisi, “mwanadamu wa kike”), “kwa sababu kutoka kwa mwanamume alitwaliwa huyu.” (Mwanzo 2:23, New World Translation Reference Bible, maelezo ya chini) Adamu hakuhisi akiwa na ujamaa wowote wa kimnofu pamoja na viumbe wanaoruka na wanyama wa bara ambao Mungu alikuwa ametangulia kumwonyesha ili awape majina. Mnofu wake ulikuwa tofauti na wao. Lakini mwanamke huyu alikuwa wa aina ya mnofu wake kweli kweli. Mfupa wa ubavu uliotolewa kwenye upande wa mwili wake ulifanyiza-fanyiza damu ya namna ile ile iliyokuwa katika mwili wake mwenyewe. (Ona Mathayo 19:4-6.) Sasa alikuwa na mtu ambaye yeye angeweza kumtendea akiwa kama mnabii wa Mungu na ambaye angeweza kushiriki naye ule usimulizi wa uumbaji.
11-13. (a) Adamu alipopokea mke, ni maswali gani yangeweza kutokea? (b) Kusudi la Mungu lilikuwa nini kwa wanadamu wa kwanza wawili? (c) Ni nini kingekuwa chakula kwa jamaa kamilifu ya kibinadamu?
11 Ingawa hivyo, kusudi la Muumba wa mwanadamu lilikuwa nini kwa kumpa mke? Je! lilikuwa kumwandalia msaidiaji na kikamilisho tu, mwandamani wa aina yake mwenyewe ili asiwe mpweke? Maandishi yaeleza kusudi la Mungu kwa kutusimulia baraka ya Mungu iliyotangazwa juu ya ndoa yao:
12 “Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.
13 “Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo.”—Mwanzo 1:26-30.
Matazamio Mbele ya Wanadamu Wawili wa Kwanza
14. Kwa baraka ya Mungu, ni wakati ujao gani uliokuwa mbele ya mwanamume na mwanamke wakamilifu, na kwa kufaa wao wangeweza kuwazia nini?
14 Lilikuwa jambo zuri kama nini kwa mwanadamu huyo mkamilifu na mke wake mkamilifu kuisikia sauti ya Mungu ikiongea nao, ikiwaambia la kufanya na kuwabariki! Kwa baraka ya Mungu, maisha hayangekuwa ya ubatili mtupu, bali wao wangewezeshwa kufanya waliloambiwa. Wakati ujao ulikuwa mzuri kama nini mbele yao! Wenzi hao wawili waliofunga ndoa yenye furaha waliposimama humo katika makao yao, bustani ya Edeni, yaelekea kwamba waliyatafakari mambo ambayo yangetokea walipokuwa wakitimiza penzi la Mungu kwao. Jicho la akili yao lilipotazama mbele ndani ya wakati ujao wa mbali, walichoona hakikuwa ile “bustani upande wa mashariki wa Edeni,” tu, bali waliona dunia nzima ikiwa imejawa na wanaume na wanawake wenye nyuso zenye kung’aa furaha. (Mwanzo 2:8) Moyo wa mwanamume na mwanamke hao ungeruka kwa kuwaza kwamba wote hawa walikuwa watoto wao, wazao wao. Wote walikuwa wakamilifu, wasio na dosari katika umbo na muundo wa kimwili, wakiwa na ujana wa daima uliojaa utele wa afya nzuri na shangwe ya kuishi, wote wakionyeshana upendo mkamilifu mmoja na mwenzake, wote kwa muungamano wakimwabudu Muumba wao mkubwa, Baba yao wa kimbingu, wakifanya hivi pamoja na baba na mama wa kwanza wa kibinadamu. Lo, ni lazima moyo wa mwanamume na mwanamke wa kwanza uwe ulifurikwa na furaha iliyoje kwa kuwaza wakiwa na jamaa ya jinsi hiyo!
15, 16. (a) Kwa nini kungekuwako chakula kingi kwa ajili ya jamaa ya kibinadamu? (b) Kwa kadiri ambayo jamaa hiyo yenye furaha ingeongezeka hesabu, kungekuwako kazi gani kwa ajili yao nje ya bustani ya Edeni?
15 Kungekuwako chakula kingi kwa kila mshiriki wa jamaa hii ya kibinadamu iliyojaza dunia nzima. Hapo mwanzo kulikuwako chakula kingi, kule katika bustani ya Edeni. Mungu alikuwa amewaandalia riziki na kuwapa mboga zote za majani yenye kuzaa mbegu ili yawe chakula chenye kujaa afya, chenye kuendeleza uhai, pamoja na ile miti yenye kuzaa matunda.—Linganisha Zaburi 104:24.
16 Kwa kadiri ambayo jamaa yao yenye furaha ingeongezeka hesabu, wao wangeipanua bustani ifikie mabara ya ng’ambo za mipaka ya Edeni, kwa maana maneno ya Mungu yaonyesha kwamba nje ya bustani ya Edeni, dunia ilikuwa katika hali ya kutotayarishwa. Angalau, haikutunzwa wala haikuletwa kwenye kiwango kile kile cha ulimwaji wa hali ya juu uliokuwa katika bustani ya Edeni. Ndiyo sababu Muumba wao aliwaambia ‘watiishe’ ardhi kwa kadiri ambayo waliijaza.—Mwanzo 1:28.
17. Kwa nini kungekuwako chakula kingi kwa ajili ya wakaaji wenye kuongezeka, na hatimaye ni kitu gani kingekuwapo kila mahali kwa kadiri ambayo bustani ingepanuliwa?
17 Kwa kadiri ambayo bustani hiyo ingepanuliwa na walimaji na watunzaji wakamilifu, ardhi iliyotiishwa ingewazalia utele wakaaji wayo wenye kuongezeka. Mwishowe, bustani hiyo yenye kuzidi kupanuka ingefunika dunia yote, na paradiso ya duniani pote ingekuwapo kila mahali, isitawi sana ikiwa makao ya milele ya aina ya binadamu. Ingekuwa kidoa chenye sura nzuri cha kuonwa kutoka mbinguni, na Muumba wa kimbingu angeweza kuitangaza kuwa njema sana.—Linganisha Ayubu 38:7.
18. Kwa nini bustani ya Edeni ya duniani pote haingekuwa na machafuko, na ni uamanifu gani ambao ungekuwapo kila mahali?
18 Yote ingejaa amani na kukosa machafuko kama ile bustani ya Edeni walimojikuta mwanamume na mwanamke waliokuwa wametoka sasa hivi kufunga ndoa. Hakungekuwa na uhitaji wa kuhofu hatari wala madhara kutoka kwa wanyama wale wote na viumbe wanaoruka ambao mwanadamu wa kwanza, Adamu, alikuwa amewakagua na kuwapa majina. Wakiwa kama baba na mama yao wa kwanza wa kibinadamu, wakaaji hao wakamilifu wa Paradiso ya duniani pote wangewatiisha samaki wa baharini, viumbe wanaoruka wa mbingu, na kila kitu hai chenye kwenda huko na huko duniani, hata hayawani-mwitu wa uwandani. Wakiwa na hisia ya kisilika ya kujitiisha kwa mwanadamu, aliyeumbwa “kwa mfano wa Mungu,” viumbe hai hawa wa hali ya chini kuliko yeye wangekuwa na amani pamoja naye. Katika kuwatiisha viumbe hai hawa wa hali ya chini, mabwana-wakubwa wao walio wanadamu wakamilifu wenye huruma nyororo wangeendeleza hali ya amani miongoni mwa viumbe wanyama. Uvutano wenye amani wa mabwana-wakubwa hawa walio wanadamu wacha-Mungu ungeenea kwa kuweka himaya juu ya viumbe hai hawa wa hali ya chini wenye uradhi. Juu ya yote, aina ya binadamu wakamilifu ingekuwa na amani pamoja na Mungu, ambaye baraka yake haingeondolewa kamwe kwao.—Linganisha Isaya 11:9.
Mungu Apumzika Kutoka Kazi Zake za Uumbaji
19. (a) Ni lazima mwanamume na mwanamke wa kwanza wawe waling’amua nini kuhusu kusudi la Mungu? (b) Mungu alionyesha nini kuhusu wakati?
19 Kwa kadiri ambayo wanadamu wa kwanza wawili wangeifikiria tamasha kamili ya kidunia kulingana na kusudi la Mungu, wangeng’amua jambo fulani. Walihitaji wakati ili watimize utume huu mzuri sana uliotoka kwa Mungu. Wakati wa kiasi gani? Muumba na Baba yao wa kimbingu ndiye aliyejua. Yeye aliwaonyesha kwamba ule mfululizo mkubwa wa siku za uumbaji ulikuwa sasa umefikia kikomo kingine na kwamba wao walikuwa kwenye ile “jioni,” hatua ya kuanzia siku mpya kulingana na njia ya Mungu mwenyewe ya kuzitia alama siku za uumbaji. Ingekuwa siku iliyobarikiwa na kutakaswa kwa kusudi la Mungu mwenyewe lenye kutakata na lenye uadilifu. Yule mwanadamu mkamilifu, mnabii wa Mungu, alitia jambo hilo maanani. Usimulizi uliovuviwa watuambia hivi:
20. Usimulizi wa Biblia wasema nini kuhusu “siku ya saba”?
20 “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe [alipumzika, NW], akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi [dunia, NW] zilipoumbwa. Siku ile Bwana [Yehova, W] Mungu alipoziumba mbingu na nchi [dunia, NW].” —Mwanzo 1:31–2:4.
21. (a) Je! Biblia yasema kwamba Mungu aliifikisha siku yake ya pumziko kwenye mwisho na kwamba ilikuwa njema sana? Eleza. (b) Ni maswali gani ambayo yatokea?
21 Usimulizi hausemi kwamba Mungu aliifikisha siku ya pumziko kwenye mwisho wayo, na kuona kwamba ilikuwa njema sana na kwamba ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya saba. Ili ilingane na siku sita za uumbaji zilizotangulia, siku ya saba ingali yapasa itangazwe kuwa njema sana, kwa maana haijafikia mwisho bado. Je! Yehova Mungu aweza kuitangaza siku hiyo kuwa njema sana kufikia hapo? Je! imekuwa siku yake ya pumziko lenye kujaa amani kufikia hapo? Namna gani lile tazamio lenye kusisimua sana moyo ambalo mwanamume na mwanamke wa kwanza waliwazia kuliona siku ile waliyofunga ndoa katika Paradiso? Acheni tuone kwa kadiri ambayo tamasha yaendelea kufunguka katika makala ifuatayo.
[Maelezo ya Chini]
a Haya ni majina yapatikanayo katika andishi-awali la Kiebrania la Mwanzo na vitabu vingine vilivyovuviwa vya Maandiko ya Kiebrania.
Wewe Ungejibuje?
◻ Mungu alimpa Adamu furushi gani la kazi kuongezea kuitunza bustani, na hiyo ilihusisha mambo gani?
◻ Usimulizi wa uumbaji kwenye Mwanzo 1:1-25 ulifunua nini?
◻ Mke wa kwanza wa kibinadamu aliumbwaje, na Adamu aliitikiaje katika siku waliyofunga ndoa?
◻ Ni matazamio gani yaliyokuwa mbele ya wanadamu wa kwanza wawili?
◻ Mungu alionyeshaje kwamba ule mfululizo mkubwa wa siku za uumbaji ulikuwa umefikia kikomo kingine?