Kutokeza Taswira kwa Kutumia Maneno
WASHAIRI ni kama wasanii na watunzi wa nyimbo. Mioyo yao huwasukuma kuandika hata zaidi ya akili zao. Hivyo, mashairi yaliyotungwa vizuri yaweza kukuchochea. Pia, yanaweza kukufanya ufikiri, ucheke, au ulie. Kitabu The Need for Words chasema: “Ushairi ni mpangilio mzuri tu wa maneno yaliyokusudiwa kuchochea sana kwa ghafula. Hilo pia laeleza ni kwa nini mashairi bora . . . hayasauliki kamwe.”
Mtu anayechukua mambo kijuujuu tu hawezi kuandika mashairi yanayopendeza. Kwa muda mrefu, mashairi yanayopendeza yamekuwa yale yanayohusu mambo ya maana zaidi maishani—mahusiano, upendo, maoni ya kidini, vitu vya asili, na kusudi la maisha. Basi, haishangazi kwamba ushairi ni mojawapo ya sanaa za kale zaidi. Alipokuwa akilinganisha ushairi na nathari (maandishi ya kawaida), mshairi mmoja maarufu alisema kwamba iwapo njia hizo mbili zingetumiwa kueleza jambo lilelile kwa usanifu, “shairi litasomwa mara mia moja ilhali nathari itasomwa mara moja tu.”
Hata hivyo, labda umeona kwamba kuna ushairi wa aina mbalimbali. Kuna mashairi yenye vina na yale yasiyo na vina. Nyakati nyingine, mashairi huelekea kufanana na nathari. Basi, ushairi ni nini hasa?
Ushairi Ni Nini?
Kamusi inayoitwa The Macquarie Dictionary huufafanua ushairi kuwa “usanii wa kutunga utungo wenye ridhimu nzuri, ulioandikwa au unaosimuliwa, kwa madhumuni ya kusisimua kwa kutumia mawazo yanayopendeza, yaliyobuniwa vizuri au yaliyotukuka.” Pia, huufafanua kuwa “maandishi yaliyo na ridhimu iliyo taratibu.” Angalia mambo makuu mawili ya ushairi—ridhimu (mfuatano mzuri wa sauti) na ridhimu iliyo taratibu. Twaona ridhimu katika mazingira yetu. Twaona ridhimu wakati maji yanapojaa na kupwa baharini, katika majira mbalimbali, na hata moyo wetu unapopiga. Katika ushairi, ridhimu ni ule mtiririko wa sauti inayotokezwa na lugha. Twahisi jambo likijirudia-rudia tunaposoma. Ridhimu iliyo taratibu ni ridhimu iliyopangwa katika njia maalumu na hutofautiana katika mashairi mbalimbali. Mbinu nyingine ya ushairi ni utumizi wa vina. Kwa kawaida, vina hutiwa katika sehemu ya mwisho ya mstari. Hapana shaka kuwa vina vyaweza kupangwa katika njia mbalimbali. Nyakati nyingine, vina vinavyomalizia mstari ndivyo vinavyoanza mstari unaofuata, au hata vinaweza kutumiwa katikati ya mstari.
Utungo wa Kijapani usio na vina unaoitwa haiku, unajulikana sana kwa sababu hueleza mambo kifupi sana na kwa njia inayopendeza. Mawazo yote huandikwa katika mistari mitatu yenye silabi 17—silabi 5 katika mstari wa kwanza na wa tatu, na silabi 7 katika mstari wa pili.a Kwa kuwa haiku ni wenye kupendeza na ni rahisi kuelewa, utungo huo huwawezesha watu wengi kutia ndani watoto wanaoanza shule, kupata mwanzo wa ushairi unaofurahisha.
Kwa kawaida, ushairi hutumia maneno machache kueleza mawazo mengi. Kichapo The World Book Encyclopedia chasema kwamba maneno ya mashairi “huwa na maana ya ndani. Hayo hufanya ufikiri . . . Lugha ya ushairi huwa na maana nyingi, na maana ya neno moja yaweza kufunua maana ya shairi, na kukuwezesha kuelewa shairi lote waziwazi.” Bila shaka, huenda ukahitaji kusoma mashairi mengine tena na tena ili ‘yaingie’ akilini na upate maana.
Ili kuwasilisha hisia na mawazo yao, washairi huteua maneno kama vile muuza-vito anavyoteua vito vyake. Mfalme Solomoni wa Israeli, aliyetunga mithali na nyimbo, ‘alitafakari, akatafuta-tafuta’ ili apate “maneno yapendezayo” na “maneno ya kweli.”—Mhubiri 12:9, 10; 1 Wafalme 4:32.
Solomoni na Daudi baba yake, waliandika kwa mtindo wa Kiebrania cha siku zao. Mashairi ya Kiebrania, yaliyoimbwa pamoja na mfuatano wa muziki, hayakuwa na vina. Badala yake, mashairi hayo yalikuwa na mfuatano maalumu wa fikira, au mawazo. Mbinu hiyo ya uandishi huitwa ulinganifu. Mistari ilikuwa na maneno yenye maana sawa, au ililinganisha mawazo tofauti. (Zaburi 37:6, 9) Kwa kawaida, mstari wa pili ulifafanua wazo lililokuwa kwenye mstari wa kwanza kwa kuongeza jambo la ziada. Angalia jinsi hilo linavyoonyeshwa kwenye Zaburi 119:1:
Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya BWANA.
Ona jinsi mstari wa pili unavyoeleza maana ya kuwa kamili, yaani kwenda katika sheria ya Yehova. Kwa kuwa Kiebrania cha Biblia hutumia ulinganifu au mfuatano wa mawazo, badala ya kutumia vina, ni rahisi kukitafsiri.b
Njia ya Kuwasilisha Hisia za Namna Zote
Kama vile nyimbo, ushairi ni njia bora sana ya kuwasilisha hisia mbalimbali. Ona jinsi mchanganyiko wa shangwe kubwa na hisia ya subira iliyothawabishwa unavyoonyeshwa kwa maneno ya Adamu, Yehova alipomleta Hawa kwake kwenye bustani ya Edeni:
Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu,
Na nyama katika nyama yangu,
Basi ataitwa mwanamke,
Kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.
Jambo la pekee hasa katika fungu hilo, ni jinsi linavyoeleza mambo mengi na kuwasilisha hisia nyingi kwa mistari michache tu. Hiyo ni mbinu fupi na yenye matokeo inayoonekana waziwazi zaidi katika lugha ya awali. Vivyo hivyo, vitabu vya mashairi kama vile Ayubu, Zaburi, Mithali, na Maombolezo huwasilisha hisia mbalimbali, zaidi ya kufundisha kweli muhimu za Biblia. Kwa kweli, katika Kiebrania cha asili, zaburi ya kwanza kabisa huanza kwa neno “furaha” au “aliyebarikiwa.” Ungefafanuaje hisia za mwandishi wa maneno yafuatayo ya Zaburi 63:1? Ona jinsi alivyotumia mifano, mbinu inayoonekana sana katika mashairi ya Kiebrania.
E Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu,
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.
Vilevile, kitabu cha Maombolezo chawasilisha hisia nyingine. Katika kitabu hicho, Yeremia aombolezea msiba uliolikumba Yerusalemu kupitia kwa Wababiloni katika mwaka wa 607 K.W.K. Yeye afunua hisia zake zote katika nyimbo tano za maombolezo zinazoonyesha wazi huzuni ya nabii huyo, na ufahamu wake kuwa haki ya Mungu ilitekelezwa.
Mashairi Husaidia Kukumbuka Mambo
Muundo wa mashairi hufanya yawe rahisi kukumbukwa. Mashairi ya kale zaidi ya Kigiriki yanayopatikana leo, yanayoitwa Iliad na Odyssey, yalikaririwa kwenye sherehe za Wagiriki. Hilo lilikuwa jambo la ajabu sana kwa kuwa mashairi hayo yalikuwa marefu! Ni wazi kwamba zaburi za Biblia zilikaririwa pia. Angalia jinsi mifano, uwazi, na kusababu kusikoweza kupingwa kunavyowasilishwa kupitia ridhimu ya mistari ifuatayo ya Zaburi 115:4-8, inayoonyesha upumbavu wa ibada ya sanamu:
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu.
Zina vinywa lakini hazisemi,
Zina macho lakini hazioni,
Zina masikio lakini hazisikii,
Zina pua lakini hazisikii harufu,
Mikono lakini hazishiki,
Miguu lakini haziendi,
Wala hazitoi sauti kwa koo zake.
Wazifanyao watafanana nazo,
Kila mmoja anayezitumainia.
Hapana shaka watu wengi wanaweza kukumbuka kwa urahisi fungu kama hilo lililo wazi na lenye ujumbe mzito.
Je, Ungependa Kutunga Mashairi?
Mashairi ni sehemu ya maisha yetu, yawe ni mashairi ya watoto au yale yanayotumiwa katika matangazo ya biashara. Hivyo, watu wengi wanajua angalau mambo ya msingi kuhusu mashairi. Lakini ikiwa ungependa kutunga mashairi, ingekuwa vizuri kwanza usome mashairi ya aina mbalimbali. Licha ya kukuza msamiati wako, jambo hilo litakusaidia kufahamu kanuni mbalimbali za utungaji. Bila shaka, wapaswa kuwa mteuzi ili usisome mambo yasiyofaa au yanayopotosha. (Wafilipi 4:8, 9) Kwa kawaida, njia bora ya kujifunza kutunga mashairi ni kuketi chini ukiwa na kalamu na karatasi, kisha uandike.
Baada ya muda, huenda utaweza kutunga mashairi ili kufurahisha familia na marafiki. Unapomtumia mtu fulani kadi ya shukrani au ya kumtakia afya njema, mbona usiwasilishe mawazo yako kwa kutunga shairi? Si lazima shairi lako liwe refu au lenye madoido. Andika mistari michache tu inayofunua mambo yaliyo moyoni mwako. Kufanya hivyo kutakufurahisha na kutakuridhisha. Licha ya hayo, atakayesoma shairi lako atafurahi sana kwa kuona jinsi ulivyojitahidi kufikiri sana ili kutunga mawazo kutoka moyoni.
Huhitaji kuwa bingwa wa maneno ili ufurahie kuandika mashairi, kama vile huhitaji kuwa mpishi stadi ili ufurahie kutayarisha mlo. Kwa kuchanganya tamaa, ubunifu, jitihada na kutokukata tamaa pamoja na kipawa chako cha kutunga mashairi, huenda utashangaa kuona jinsi utakavyotokeza tungo tamu.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa mazungumzo kuhusu haiku, tafadhali ona gazeti la Amkeni! la Januari 8, 1989 la Kiingereza.
b Gazeti la Amkeni! hutafsiriwa katika lugha 83. Hivyo, tumechagua kutumia mashairi ya Biblia kama mifano badala ya mashairi yasiyo kwenye Biblia.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Sehemu kubwa ya Maandiko ya Kiebrania ina mashairi