Matazamio ya Paradiso Ni Halali Kujapokuwako Kutotii kwa Kibinadamu
1. Baada ya wakati kupita, mwanamume na mwanamke wa kwanza waonwa wakiwa wapi na katika mazingira gani?
WAKATI umepita. Mwanamume na mwanamke wa kwanza hawana tena ule uchi usio na hatia. Wamevikwa nguo—mavazi marefu ya ngozi ya wanyama. Wapo pale pale nje ya mwingilio wa bustani kamilifu ya Edeni. Wameipa bustani visogo vyao. Wao waitazama tamasha iliyoko mbele yao. Waionayo tu ni nchi isiyolimwa. Ni wazi kabisa kwamba nchi hiyo haina baraka ya Mungu. Wao waweza kuona miiba na michongoma mbele yao. Je! hii siyo ardhi waliyopewa utume wa kuitiisha? Ndiyo, lakini sasa mwanamume na mwanamke wa kwanza hawapo hapo nje kwa kusudi la kuieneza bustani ya Edeni ifikie bara hilo lisilofanyiwa kazi.
2. Kwa nini mwanamume na mwanamke hawajaribu kuiingia tena bustani-Paradiso?
2 Waionapo hali hiyo iliyo tofauti sana, kwa nini hawarudi nyuma waiingie tena bustani ya Paradiso? Hilo ni dokezo rahisi, lakini tazama kilicho nyuma yao penye mwingilio wa bustani. Ni viumbe wasiokuwa wamepata kuwaona, hata ndani ya bustani yenyewe, makerubi, na ukali wenye kuwaka moto wa upanga unaoendelea kujigeuza-geuza. Mwanamume na mwanamke hawangeweza kamwe kuvipita vitu hivi wakiwa hai wakaiingie bustani!—Mwanzo 3:24.
3. Ni jambo gani lililokuwa limetukia likabadili hali za hao wenzi wa kwanza wawili kwa kadiri kubwa hivyo?
3 Ilikuwa imekuwaje? Hilo si fumbo lenye kutatanika sana hata liduwaze akili ya wanasayansi kwa maelfu ya miaka. Limeelezwa kwa urahisi. Mwanamume na mwanamke wa kwanza wangetimiziwa matazamio mazuri ajabu ambayo utume wa Mungu uliwawekea mbele yao siku ile waliyofunga ndoa, lakini kwa sharti la kwamba walipaswa kumtii Baba yao wa kimbingu hata katika jambo lililo dogo sana. Utii wao mkamilifu ungetahiniwa na katazo moja tu la chakula: Ni lazima wasile tunda la “mti wa ujuzi wa mema na mabaya.” (Mwanzo 2:16, 17) Kama wao wangefanya hivyo dhidi ya maagizo ya Mungu, wangekufa hakika. Hivyo ndivyo Adamu, akiwa mnabii wa Mungu, alivyomwambia mke wake, huyo kiumbe binadamu wa umri mchanga kuliko yeye. Lakini kwa kushangaza, yule na·chashʹ, yule nyoka, aliukanusha ukweli wa vile Mungu alivyokuwa amemwambia Adamu katika onyo Lake dhidi ya kula kutokana na “mti wa ujuzi wa mema na mabaya” uliokatazwa. Nyoka alimdanganya mwanamke kuamini kwamba kuvunja sheria ya Mungu na kula tunda lililokatazwa kungemfanya awe kama Mungu na kumfanya ajitegemee mwenyewe bila Mungu katika kuamua lililo jema na lililo baya. —Mwanzo 3:1-5.
Si Usimulizi wa Kihadithi Tu
4, 5. Mtume Paulo aonyeshaje kwamba usimulizi unaohusu vile nyoka alivyomdanganya mwanamke wa kwanza haukuwa hadithi tu?
4 Je! lasikika kuwa jambo lisiloaminika? Je! lasikika mno kama hadithi tu, hekaya ya kimapokeo isiyotegemea mambo ya uhakika na kwa hiyo isiyokubalika kwenye akili za watu wazima waliopata nuru ya elimu ya ki-siku-hizi? La, sivyo ilivyo kwa mwandikaji ambaye vitabu vyake vingali vyasomwa kwa wingi sana, mwandikaji anayestahiki kuaminiwa, mtume aliyechaguliwa kwa njia ya pekee, aliyejua usahihi wa mambo aliyoandika. Mtume huyu Paulo aliliandikia hivi kundi la Wakristo walio watu wazima katika jiji la Korintho lenye hekima ya kilimwengu: “Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.” —2 Wakorintho 11:3.
5 Ingekuwa vigumu Paulo awe arejezea hadithi tu, ngano, na bado alitumie jambo hilo la kuwazia tu ili kukazia wazo lake kwa Wakorintho hao, waliojua habari nyingi kuhusu hadithi za dini pagani ya Kigiriki. Akinukuu kutokana na Maandiko ya Kiebrania yaliyovuviwa, aliyoyatangaza kuwa “neno la Mungu,” mtume Paulo alishikilia kwa uthabiti kwamba “nyoka alimtongoza Hawa kwa ujanja wake.” (1 Wathesalonike 2:13, W) Zaidi ya hilo, alipokuwa akiandikia mwangalizi Mkristo aliyeaminishwa wajibu wa kufundisha “kielelezo cha maneno yenye uzima,” mtume Paulo alisema: “Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”—2 Timotheo 1:13; 1 Timotheo 2:13, 14.
6. (a) Mkiuko wa sheria ambao Adamu alifanya dhidi ya Mungu ulitofautianaje na ule wa mwanamke? (b) Kwa nini sisi twaweza kuwa na uhakika kwamba mwanamke hakuwa akitunga hadithi tu kuhusu nyoka huyo?
6 Ni hakika, wala si hadithi, kwamba mwanamke alidanganywa na nyoka, sawa na vile ilivyo hakika kwamba magumu ambayo yamekuwako katika historia yamekuwa matokeo ya kutotii kwake kwa kula kutokana na tunda lililokatazwa. Baada ya kuingia hivyo katika mkiuko wa sheria dhidi ya Mungu, mwanamke alishawishi mume wake ashirikiane naye kula, lakini mume hakula kwa sababu yeye pia alidanganywa kabisa kabisa. (Mwanzo 3:6) Usimulizi wa jinsi walivyomtolea Mungu hesabu baadaye wasema hivi: “Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana [Yehova, NW] Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.” (Mwanzo 3:12, 13) Mwanamke hakuwa akitunga hadithi tu kuhusu na·chashʹ huyo, nyoka huyo, wala Yehova Mungu hakulichukua elezo lake kama kisingizio cha kutungwa tu, hadithi tu. Yeye alishughulika na nyoka huyo kama ambaye alikuwa amekuwa chombo cha kumdanganya mwanamke kukiuka sheria dhidi ya Yeye, Mungu na Muumba wake. Mungu angekuwa akijishushia heshima kwa kushughulika na nyoka wa kihadithi tu.
7. (a) Usimulizi wa Biblia waelezaje juu ya hukumu ambayo Mungu alimtolea nyoka? (b) Nyoka aliyemdanganya mwanamke wa kwanza angewezaje kutudanganya sisi pia? (Husisha maelezo ya chini.)
7 Ukieleza juu ya jinsi Mungu alivyomhukumu nyoka huyo katika bustani ya Edeni, usimulizi wasema hivi: “Bwana [Yehova, NW] Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” (Mwanzo 3:14, 15) Mahakama yoyote yenye uamuzi timamu hushughulikia mambo ya uhakika na kupekua-pekua ushahidi halisi, wala si hadithi za mapokeo tu. Yehova Mungu hakuwa akijifanya mpumbavu, mpuzi asiyetumia akili, kwa kuelekeza hukumu yake kwa nyoka wa kihadithi tu bali alikuwa akimtolea hukumu kiumbe wa kikweli mwenye kuwako, aliyekuwa na wajibu wa kutoa hesabu. Ingechekesha, lakini isikitishe sana ikiwa nyoka uyo huyo angetudanganya sisi tufikiri kwamba yeye hajapata kuwako kamwe, kwamba yeye ni hadithi tu, kwamba hakuwa na wajibu wa kutoa hesabu ya kosa lolote duniani.a
8. Mungu alimtolea mwanamke hukumu gani, na matokeo yakawa nini kwa binti zake na binti-wajukuu zake?
8 Kwa kuichukua taarifa ya mwanamke iliyohusu nyoka kuwa uhakika, maandishi yanayohusu mke wa mwanamume yule yasema hivi: “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” (Mwanzo 3:16) Jambo lolote kama hili halikuhusishwa katika baraka aliyoitoa Mungu wakati mwanamke alipokuwa akiolewa na Adamu, Mungu alipowaambia hivi: “Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi [dunia, NW].” (Mwanzo 1:28) Utume huo mbarikiwa uliopewa kwa hao wanadamu wakamilifu wawili ulionyesha kwamba mwanamke angeshika mimba kwa muda mrefu lakini asitaabishwe na mimba wala asiwe na maumivu makali mno ya uzazi wala mume wake asimkandamize kwa kumwonea. Hukumu hii iliyotamkwa juu ya mwanamke huyu mkiuka-sheria ingeathiri binti zake na binti-wajukuu zake kizazi hata kizazi.
Sheria ya Mungu Yatukuzwa na Hukumu Dhidi ya Adamu
9, 10. (a) Mungu alikuwa amempa Adamu onyo gani la moja kwa moja, na matokeo yangekuwa nini kama Mungu angeshikilia adhabu hiyo? (b) Mungu alitoa hukumu gani dhidi ya Adamu?
9 Ingawa hivyo, mwanamke huyo angeshirikiana hali gani zilizobadilika pamoja na mwanamume ambaye yeye alikuwa amemshawishi ajiunge naye katika mkiuko wa sheria? Mungu alisema hivi akimwambia moja kwa moja mwanamume huyo: “Walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” (Mwanzo 2:17) Je! Mungu, aliye Hakimu, angeshikilia hukumu hiyo mkataa kwa sababu Adamu alikula kipande cha tunda tu? Ebu fikiria ni mambo gani yangemaanishwa na utekelezi wa adhabu hiyo! Hiyo yenyewe ingeharibu tazamio lile lenye kuchangamsha nafsi ambalo Adamu na Hawa walikuwa wamefurahia siku waliyofunga ndoa, tazamio la kuijaza dunia nzima kwa wazao wao, huku jamii kamilifu ya kibinadamu ikikaa milele kwa njia yenye amani katika dunia-paradiso kwa ujana wa milele, katika mahusiano yenye kujaa amani pamoja na Mungu na Baba yao wa kimbingu! Kwa uhakika, haingetazamiwa kwamba Mungu angelishinda kusudi lake mwenyewe lililo zuri sana kwa aina ya binadamu na kwa makao ya kidunia ya mwanadamu kwa kufuatilia sana kufikiliza adhabu ya kifo juu ya wanadamu wa kwanza walio wazazi wa aina ya binadamu wote! Lakini sikiliza uamuzi ulioamrishwa kimungu kama ulivyoandikwa wazi katika usimulizi wa Biblia:
10 “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.”—Mwanzo 3:17-19.
11. Ni mambo gani ya uhakika kuhusu utii yatoa kielezi cha ustahili wa hukumu ya Mungu dhidi ya Adamu?
11 Hukumu hiyo ilimaanisha kutekelezwa kwa adhabu ya kifo juu ya mwanadamu bila kujali jambo hilo lingekuwa na matokeo gani kwa kusudi la Mungu kwamba dunia-paradiso ijazwe wanaume na wanawake wakamilifu wenye kukaa pamoja kwa ujazo wa amani wakiilima na kuitunza milele bustani-Paradiso duniani pote. Mwanamume alikuwa amesikiliza sauti ya mke wake badala ya sauti ya Mungu iliyomwambia asile kutokana na “mti wa ujuzi wa mema na mabaya” uliokatazwa. Na ikiwa yeye mwenyewe hakutii sauti ya Mungu na Muumba wake, je! angefundisha watoto wake kwa upatani mzuri ili wafanye hivyo? Je! kielelezo chake mwenyewe kingeweza kuwa zungumzo katika kuwafundisha wamtii Yehova Mungu?—Linganisha 1 Samweli 15:22.
12, 13. (a) Dhambi ya Adamu ingeathirije watoto wake? (b) Kwa nini Adamu hakustahili kamwe kuishi milele katika Paradiso wala hata duniani?
12 Je! watoto wa Adamu wangeweza kuishika sheria ya Mungu kikamilifu, kama vile yeye mwenyewe alivyokuwa ameweza kufanya wakati mmoja akiwa katika ukamilifu wake wa kibinadamu? Kwa utendaji wa sheria za urithi, je! yeye hangewapitishia watoto wake udhaifu wake na elekeo la kutotii sauti ya Mungu na kusikiliza sauti fulani nyingine? Historia ya kikweli yatoa majibu kwa maswali haya.—Warumi 5:12.
13 Je! mwanamume wa jinsi hiyo ambaye, kwa ajili ya kiumbe cha kibinadamu tu, aligeuka akaacha kumtii Mungu kikamilifu kwa kumwonyesha Mungu upendo mkamilifu, angestahili hata kidogo kuishi milele katika Paradiso au hata duniani? Je! hata ingekuwa salama kumwacha aishi duniani milele? Je! kuruhusiwa aishi milele duniani akiwa katika mkiuko wake wa sheria kungeitukuza sheria ya Mungu na kuonyesha haki Yake kamili, au kungefundisha kutostahi sheria ya Mungu na kudokeza kwamba neno la Mungu lilikuwa lisilotegemeka?
Kaondoshwa Katika Bustani ya Edeni
14. Maandishi ya Biblia yaelezaje juu ya vile Mungu alivyochukua hatua dhidi ya Adamu na mke wake?
14 Maandishi ya Biblia yatuambia jinsi Mungu alivyoamua mambo haya: “Bwana [Yehova, NW] Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Bwana [Yehova, NW] Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; [—, NW] kwa hiyo Bwana [Yehova, NW] Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.”—Mwanzo 3:21-24.
15. (a) Mungu alionyeshaje ufikirio kwa hisia ya aibu ambayo Adamu na mke wake walihisi kwa kuwa uchi? (b) Mwanamume na mwanamke wa kwanza waliondoshwaje katika bustani ya Edeni? (c) Ni hali gani zenye badiliko zilizokabili Adamu na mke wake nje ya bustani ya Edeni?
15 Hakimu wa kimungu alionyesha ufikirio kwa hisia ya aibu ambayo sasa watenda dhambi Adamu na mke wake walihisi kwa kuwa uchi. Kwa njia fulani isiyotaarifiwa, yeye aliwaandalia mavazi marefu ya ngozi ili yawe badala ya vifunika-kiuno vya majani ya mtini yaliyoshonwa pamoja, ambavyo wao walikuwa wamejifanyia. (Mwanzo 3:7) Mavazi hayo ya ngozi yangekaa muda mrefu zaidi na kuwapa himaya nyingi zaidi dhidi ya miiba na michongoma na viumizaji vingine nje ya bustani ya Edeni. Kwa sababu ya kuwa na dhamiri mbaya baada ya kutenda dhambi, wao walijaribu kujificha miongoni mwa miti ya bustani ya Edeni ili wasionwe na Mungu. (Mwanzo 3:8) Sasa, baada ya kuhukumiwa, walipata namna fulani ya mbano wa kimungu kwa kuondoshwa na Mungu katika bustani hiyo. Waliondoshwa kuelekea mashariki, na upesi wakajikuta nje ya bustani, wakiwa wamepigwa marufuku humo milele. Hawangekuwa tena wakifanya kazi kupanua bustani hiyo na kueneza hali zayo za Paradiso kwenye miisho ya dunia. Tangu sasa, wangekula mkate wenye kufanywa kutokana na mboga za kimajani za uwandani, lakini hazingewaruzuku milele katika uhai wa kibinadamu. Walikatiliwa mbali kutoka kwenye “mti wa uzima.” Baada ya muda fulani—lakini wa urefu gani?—ilikuwa lazima wafe!
Kusudi la Yehova la Awali Halishindiki
16. Mungu hakuwa amekusudia kufanya nini, na kwa nini?
16 Je! sasa Mungu aliamua kuiharibu dunia, pamoja na mwezi na jua na nyota, katika mteketezo mkubwa wa ulimwengu wote mzima kwa sababu viumbe wawili hawa wa mavumbi walikuwa wametenda dhambi dhidi yake? Kama angefanya jambo la jinsi hiyo, je! hii haingemaanisha kwamba alikuwa ameshindwa katika kusudi lake tukufu, eti kwa sababu ya jambo lililokuwa limeanzishwa na na·chashʹ fulani? Je! nyoka wa kikawaida tu angeweza kuvunja-vunja kusudi lote la Mungu? Mungu alikuwa amewaonyesha wazi Adamu na Hawa kusudi lake katika siku waliyofunga ndoa wakati alipowabariki na kuwaambia penzi lake lilikuwa nini kwao: kuijaza dunia nzima jamii kamilifu ya kibinadamu, dunia yote ikiwa imetiishwa kufikia ukamilifu wa bustani ya Edeni, na aina ya binadamu wote ikiwa inawatiisha kiamani viumbe hai wote wa hali ya chini duniani na katika maji yaliyomo. Lo, kulikuwako tazamio jangavu sana kwamba kusudi la Mungu lingetimizwa, akiwa amelifanyia matayarisho ya siku sita za kazi ya uumbaji kwa muda wa maelfu ya miaka! Je! sasa kusudi hili lenye kustahiki sifa lingeachwa tu bila kutimizwa eti kwa sababu tu ya nyoka fulani na kupotoka kwa hao wenzi wa kwanza wawili wa kibinadamu? Sivyo!—Linganisha Isaya 46:9-11.
17. Mungu alikuwa ameazimia kufanya nini kuhusu siku ya saba, na kwa hiyo mwisho wa siku hii utakuwaje?
17 Ilikuwa ingali ni siku ya pumziko, siku ya saba, ya Yehova Mungu. Yeye alikuwa ameazimia kubariki siku hiyo na akawa ameifanya takatifu. Hangeacha chochote kiifanye iwe siku iliyolaaniwa, naye angekinza njama ya mtu yeyote kuweka laana yoyote juu ya siku hiyo yake ya pumziko na kuigeuza iwe baraka, akifanya mwisho wa siku hiyo ukawe wenye baraka. Ingeiacha dunia nzima ikiwa mahali patakatifu, huku penzi la Mungu likifanywa hapa chini duniani kama lifanywavyo mbinguni, tena lifanywe na jamii ya wanadamu wakamilifu.—Linganisha Mathayo 6:10.
18, 19. (a) Kwa nini wazao wanaoteseka wa wanadamu wa kwanza wawili waweza kuchangamka? (b) Safu zaidi za Mnara wa Mlinzi zitazungumza juu ya nini?
18 Mungu hakuhisi mvurugiko wowote wa kusudi lake. Yeye hakuachilia mbali kusudi lake. Aliazimia kujitetea kuwa ndiye Mmoja aliye wa kutegemeka kikamili ambaye hufanya mambo yote mawili, kuyakusudia na kuyatekeleza kikamili mambo ayakusudiayo, akijistahilisha sifa yote impasayo. (Isaya 45:18) Wazao wasiokamilika, wenye kuteseka wa wanadamu wa kwanza wawili wenye dhambi waweza kuchangamka na kutazama mbele wakaone Mungu akitekeleza kusudi lake la awali kwa uaminifu, huku wao wakipata manufaa ya milele. Tayari, mileani kadhaa za siku yake ya pumziko zimepita, na ni lazima ile sehemu ya mwisho ya siku hiyo itakayopata baraka yake ya pekee iwe inakaribia. “Jioni” ya siku yake ya pumziko inapita, na kama ilivyokuwa katika siku zote sita za uumbaji ambazo zilitangulia, ni lazima “asubuhi” ije. “Asubuhi” hii ifikiapo ukamilifu na kuufanya utimio mtukufu wa makusudi ya Mungu yasiyobadilika yawe yenye kuonekana kikamili kwa watazamaji wote, hapo itawezekana kuandika kumbukumbu hii: ‘Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya saba.’ Lo, ni tazamio la kustaajabisha kweli kweli!
19 Kufikiria hayo yote kunasisimusha hisia kweli kweli! Na katika safu zaidi za Mnara wa Mlinzi, mengi zaidi yatasemwa kuhusu matazamio ya Paradiso yaliyo ya kuwafurahisha sana wanadamu watiifu, wapendao sheria ya Mungu.
[Maelezo ya Chini]
a Kwenye Ufunuo 12:9, Shetani Ibilisi atambulishwa kuwa “nyoka wa zamani”; na kwenye Yohana 8:44, Yesu Kristo ananena juu yake kuwa ndiye ‘baba ya uongo.’
Wewe Ungesema Nini?
◻ Kwa nini wenzi wa kwanza wawili wa kibinadamu walipoteza makao yao ya Paradiso?
◻ Kwa nini sisi twajua kwamba haikuwa hadithi tu kwamba Hawa alidanganywa kwa njia ya nyoka?
◻ Mungu alitangaza hukumu gani juu ya mwanamke?
◻ Mungu alitangaza hukumu gani juu ya Adamu, na kwa nini kufanya hivyo kuliitukuza sheria ya Mungu?
◻ Kwa nini Mungu hakuhisi mvurugiko wowote kuhusu kusudi lake kwamba dunia ijazwe wanadamu wakamilifu katika Paradiso?