Maoni ya Biblia
Je! Kila Siku ya Uumbaji Nyakati Zote Ilimaliza Kile Ilichoanza?
MARA kwa mara, Mashahidi wa Yehova hupokea maswali kuhusu utaratibu wa uumbaji kama ulivyoonyeshwa katika kitabu chao Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? Baadhi ya maswali hayo huelekeza kwenye tofauti iliyoko kati ya utaratibu kama ulivyo katika kitabu hicho na utaratibu wa matukio hayo kama unavyodaiwa na wanajiolojia.
Kwa mfano, inafahamika kwamba wanajiolojia huorodhesha ndege kuwa walitokea baada ya mamalia (wanyama wanaonyonyesha), hali kitabu Creation, ukurasa 37, huonyesha ndege kuwa walitokea kabla ya mamalia.
Kwa kupendeza, ingawa wanaakiolojia wengi huonelea kwamba ndege walikuja baada ya mamalia, wengine wanaamini kwamba mamalia walitokea baada ya ndege. Mfano mmoja wa jambo hilo la mwisho unapatikana katika kitabu Evolution, cha Colin Patterson, ukurasa 132. Hili laonyesha kwamba ithibati kutokana na visukuku si ya mkataa kabisa.
Lakini je, kila siku ya uumbaji ya Mwanzo sura 1 nyakati zote iliona kumalizwa kwa kile kilichoanzwa siku hiyo, au matukio ya uumbaji yaliendelea kupita siku ambayo yalianza? Kikitegemea Biblia, kitabu Creation chasema kwamba ndege warukao walianza kuumbwa kabla ya mamalia kutokea. Neno la Kiebrania lililotafsiriwa “viumbe virukavyo,” katika Mwanzo 1:20, NW ni ‛ohph na laweza kutia ndani wadudu wenye mabawa na watambaazi warukao, kama vile pterosaurs. Wadudu wa kwanza huenda walitangulia viumbe kama vile pterosaurs, na watambaazi hawa warukao wenye mabawa yenye utando huenda walitokea kabla ya ndege na mamalia.
Habari ya Biblia kuhusu uumbaji haionyeshi kwa maelezo mengi kazi zote za uumbaji wa Yehova Mungu. Hiyo huorodhesha tu kwa mfuatano baadhi ya matokeo makuu kuhusiana na utayarishaji wa dunia kwa ajili ya viumbe hai na huonyesha utaratibu wa kutokea kwa jamii kubwa za uhai wa mimea na wanyama. Kwa njia hiyo hiyo, habari ya Mwanzo haitenganishi wadudu wenye mabawa, watambaazi warukao, na ndege katika orodha tofauti bali huwaweka pamoja chini ya neno la Kiebrania la ujumla, linalotia yote ndani linalotafsiriwa “viumbe virukavyo.”
Katika Biblia vitenzi vya Kiebrania visivyo katika hali ya ukamili vinavyotumiwa katika Mwanzo sura 1 huonyesha kwamba uumbaji ulitia ndani utendaji mwendelevu wa Mungu. Na siku za uumbaji za Mwanzo sura ya 1 hazikuwa siku za saa 24, bali zilienea kupita maelfu mengi ya miaka.—Ona Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation?, kurasa 26-7.
Kwa mfano, Mwanzo 1:3 husema juu ya uumbaji wa nuru katika siku ya kwanza. Kulingana na tafsiri ya J. W. Watts, mstari huo husomwa hivi: “Baadaye Mungu akasema, ‘Na kuwe nuru’; na polepole nuru ikaja kuwako.” Tafsiri ya Benjamin Wills Newton hutoa wazo hilo hilo la mwendelezo wa jambo lililoanzwa: “Na Mungu akasema [wakati ujao], Nuru na ije kuwapo, na Nuru ikaja kuwapo [wakati ujao].” (vifungo ni vya Newton; italiki ni zetu katika tafsiri zote mbili.) Nuru iliyopenya hadi kwenye uso wa dunia ilizidi kuwa nyangavu, na mwendo huo uliendelea mbele kwenye wakati ujao.—Ona New World Translation of the Holy Scriptures—With References, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., Appendix 3C, kurasa 1572-3.
Siku ya kwanza haikukamilisha “uumbaji” wa nuru kuhusiana na dunia. Vyanzo vyayo, bila shaka, vilikuwako kabla ya siku hiyo ya kwanza lakini vilikuwa visivyoonekana kutoka usoni pa dunia. (Mwanzo 1:1) Katika siku ya kwanza nuru iliyotawanyika ilipenya hadi kwenye uso wa dunia, ikiwezeshwa na kupunguzwa kwa tabaka zenye kuzuia zilizoikumba dunia kama “nguo ya kuifungia.” (Ayubu 38:9) Mwangaza usoni pa dunia uliongezeka polepole kwa kupunguzwa kwa tabaka zilizozuia.
Katika siku ya pili ya uumbaji, Mungu alifanya kuwe na mtengano kati ya maji yaliyo usoni pa dunia na yale yaliyo juu yake, yakiacha eneo, au anga-hewa, kati ya maji yaliyoko juu na maji yaliyoko chini. Kama vile tafsiri ya Watt ya Mwanzo 1:6, 7, inavyosema: “Halafu Mungu akaendelea, akisema, ‘Na kuwe na eneo kati ya maji, pia na kuwe na mtengano kati ya maji.’ Basi, Mungu akayatenga maji yaliyokuwa chini ya eneo na yale yaliyokuwa juu ya eneo; na polepole ikaja kuwa hivyo.” (Italiki ni zetu.) Kama vile katika siku ya kwanza kulivyokuwa na mwangaza wa kwanza usoni pa dunia lakini siyo mwangaza ulio kamili, ndivyo kulivyokuwa na mwanzo wa eneo katika siku ya pili. Kukamilishwa kwayo hakukufikiwa mara hiyo hiyo.
Mwanzo 1:9, 11, husema hivi kuhusu siku ya tatu kulingana na tafsiri ya Watts: “Halafu Mungu akaendelea, akisema, ‘Na maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanywe pamoja katika mahali pamoja, na nchi kavu itokee’; na polepole ikaja kuwa hivyo. Halafu Mungu akaendelea, akisema, ‘Na dunia itoe majani, mche utoao mbegu, miti ya matunda ambayo mbegu zake zimo ndani yake izaayo matunda kwa jinsi yake juu ya dunia’; na polepole ikaja kuwa hivyo.” (Italiki ni zetu.) Utumizi wa neno “polepole” huonyesha utendaji mwendelevu wa uumbaji, tofauti na tukio moja katika wakati mmoja tu katika mkondo wa wakati.
Siku ya nne kulikuwa na mabadiliko makubwa: “Halafu Mungu akaendelea, akisema, ‘Na kuwe mianga katika aneo la mbingu kutenganisha kati ya mchana na usiku, nayo itakuwa dalili na majira na siku na miaka. Pia itakuwa ya kuangazia katika eneo la mbingu ili kutoa nuru juu ya dunia’; na polepole ikaja kuwa hivyo. Hivyo Mungu akaumba mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku, vivyo hivyo na nyota.”—Mwanzo 1:14-16, Watts, italiki ni zetu.
Sasa, kwa mara ya kwanza, mwangaza wa jua ulioelekezwa mahali pamoja ulifikia usoni pa dunia. Vyanzo vya mwanga—jua na mwezi na nyota—vingeweza kuonwa kutoka usoni pa dunia. Katika habari ya siku ya kwanza ya uumbaji, neno la Kiebrania linalomaanisha mwangaza ni ʹohr, mwangaza katika maana ya kijumla; lakini katika siku ya nne, ni ma·ʹohŕ, linalomaanisha chanzo cha mwangaza huo.
Siku ya tano ilikuwa na uumbaji wa aina za uhai uishio majini, kwa wazi ikitia ndani watambaazi wakubwa wa majini. Habari ya Mwanzo inasomwa hivi: “Na Mungu akaendelea kusema: ‘Yaache maji yasongamane na kundi la nafsi hai na viache viumbe virukavyo viruke juu ya dunia juu ya uso wa eneo la mbingu.’ Na Mungu akaendelea kuumba wanyama wakubwa mno ajabu wa baharini na kila nafsi hai inayojimudu, ambayo maji yalisongamana nayo kulingana na aina zao, na kila kiumbe chenye mabawa kirukacho kulingana na aina yake. Na Mungu akapata kuona kwamba ilikuwa vyema.” (Mwanzo 1:20, 21, NW) Hivyo, basi, hiki pia kilikuwa kipindi ambacho viumbe warukao walianza kutokezwa. Uumbaji wa “kila kiumbe chenye mabawa kirukacho kulingana na aina yake” uliendelea baada ya kuanzishwa kwa kipindi hicho cha uumbaji katika siku ya tano.
Inaonekana kwamba Mwanzo 2:19 inaelekeza kwenye uumbaji mwendelevu unaotia ndani viumbe warukao, kwa sababu hiyo husema: “Yahweh Mungu akaendelea kufanyiza kutoka ardhini wanyama wote wa kondeni na ndege wote [“kila kiumbe kirukacho,” NW] wa mbinguni na kuwaleta kwa yule mtu kuona atawaitaje.”—Watts, italiki ni zetu.a
Hivyo habari ya Biblia katika Mwanzo sura 1 huonyesha kwamba jamii kubwa za uhai wa mimea na wanyama zilianza kuumbwa na Mungu baada ya dunia kutayarishwa hadi kwenye kiwango ambacho kingefaa aina fulani ya viumbe wa uhai. Kuletwa kwa jamii hizi kubwa zikiwa na aina nyingi mbalimbali za uhai, kama vile “viumbe virukavyo,” kulikuwa utendaji mwendelevu, wa Mungu. Utendaji huu wa kimungu wenye kuendelea huenda ikawa uliendelea kupita mwisho wa siku ile ya uumbaji ulioanzia.
Rekodi ya kijiolojia si kamili na hufasiriwa kulingana na maelekeo ya kinadharia ya wale wanaojitahidi kuifumbua. Kama vile ilivyoonyeshwa katika kitabu Creation, Biblia ina upatano sahihi inapozungumzia mambo ya kisayansi, kutia ndani utaratibu wa uumbaji.
[Maelezo ya Chini]
a Ona “All Scripture Is Inspired of God and Beneficial,” chapa ya 1990, iliyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., ukurasa 287.
[Blabu katika ukurasa wa 29]
Utendaji mwendelevu wa uumbaji huonyeshwa na utumizi wa neno “polepole”
[Blabu katika ukurasa wa 30]
Uumbaji wa aina mbalimbali za uhai ulikuwa utendaji mwendelevu wa Mungu
[Picha katika ukurasa wa 31]
Mwangaza ulitokea duniani kwa mara ya kwanza katika siku ya Siku kwanza, lakini ukaongezeka katika siku zilizofuata
Siku ya 1
Siku ya 2
Siku ya 3
Siku ya 4
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 28]
The Bettmann Archive