Sura 8
Sayansi: Je! Imethibitisha Biblia Kuwa Yenye Makosa?
Katika 1613 mwanasayansi Mwitalia Galileo alitangaza kitabu kinachoitwa “Letters on Sunspots.” Humo, alitokeza ushahidi wa kwamba dunia huenda ikilizunguka jua, badala ya jua kuizunguka dunia. Kwa kufanya hivyo alianzisha mfululizo wa matukio ambayo mwishowe yalimfikisha mbele ya Mahakama ya Katoliki ya Kuhukumu Wazushi kwa “shuku kali ya uzushi.” Hatimaye, alilazimishwa ‘atangue maneno yake.’ Ni kwa nini wazo hili kwamba dunia hufanya mwendo wa kulizunguka jua lilionwa kuwa uzushi? Kwa sababu washtaki wa Galileo walidai kwamba lilipinga yale inayosema Biblia.
1. (Tia ndani utangulizi.) (a) Ilitukia nini Galileo alipodokeza kwamba dunia ilifanya mwendo wa kulizunguka jua? (b) Ingawa Biblia si kitabu cha mafundisho ya sayansi, twapata nini tunapoilinganisha na sayansi ya ki-siku-hizi?
YASHIKILIWA sana leo kwamba Biblia si ya kisayansi, na wengine huelekeza kwa yaliyompata Galileo kuthibitisha hilo. Lakini je! ndivyo ilivyo? Tunapojibu swali hilo, lazima tukumbuke kwamba Biblia ni kitabu cha unabii, historia, sala, sheria, shauri, na maarifa juu ya Mungu. Haidai kuwa kitabu cha mafundisho ya kisayansi. Hata hivyo, Biblia inapogusia mambo ya kisayansi, inayosema ni sahihi kabisa.
Sayari Yetu Dunia
2. Biblia yasimuliaje kituo cha dunia katika anga?
2 Kwa kielelezo, fikiria, inayosema Biblia juu ya sayari yetu, dunia. Katika kitabu cha Ayubu, twasoma: “[Mungu] hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, na kuutundika ulimwengu pasipo kitu.” Linganisha hayo na taarifa ya Isaya, anaposema: “Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia.” (Isaya 40:22) Wazo linalotolewa la dunia mviringo ‘iliyotundikwa pasipo kitu’ “nafasi isiyo na kitu” hutukumbusha kwa nguvu juu ya picha zinazopigwa na wanaanga za duara la dunia linaloelea katika anga isiyo na kitu.
3, 4. Mrudio wa maji wa dunia ni nini, na Biblia yasema nini juu ya hilo?
3 Pia, fikiria mrudio wa kustaajabisha wa maji. Hivi ndivyo Compton’s Encyclopedia kinavyoeleza yanayotukia: “Maji . . . huvukiza kutoka uso wa bahari mpaka kwenye anga . . . Mikondo ya hewa yenye kuzidi kusonga katika anga la dunia huipeleka hewa hiyo yenye unyevu barani. Hewa hiyo inapokuwa baridi, mvuke huganda kufanyiza matone ya maji. Kwa kawaida hayo huonekana kuwa mawingu. Mara nyingi matone hayo huungana kufanyiza matone ya mvua. Anga likiwa baridi vya kutosha, chembe za theluji hufanyika badala ya matone ya mvua. Vyovyote vile, maji ambayo yamesafiri mamia au hata maelfu ya kilometa kutoka baharini huanguka kwenye uso wa dunia. Hapo hukusanyika katika vijito au kupenya ndani ya udongo na kuanza safari yayo ya kurudi baharini.”1
4 Utaratibu huo wa kutokeza, unaofanya maisha kwenye nchi kavu yawezekane, ulielezwa vizuri miaka karibu 3,000 iliyopita katika semi sahili, za moja kwa moja: “Vijito vyote huenda katika bahari, hata hivyo bahari haifuriki kamwe; vijito huenda tena mahali vilipotoka.”—Mhubiri 1:7, The New English Bible.
5. Maelezo ya mtunga zaburi juu ya historia ya milima ya dunia ni ya kisasa kwa kutokeza jinsi gani?
5 Labda lililo la kutokeza hata zaidi ni mwono-ndani wa Biblia katika historia ya milima. Hivi ndivyo kitabu kimoja cha mafundisho juu ya jiolojia kinavyosema: “Tangu nyakati za Kabla ya Cambria kufikia wakati huu, utaratibu wa kudumu wa kujenga na kuangamiza milima umeendelea. . . . Si kwamba tu milima imetokea katika sakafu za bahari zilizotoweka, bali pia mara nyingi imezama muda mrefu baada ya kuundwa kwayo, na kisha kuinuliwa tena.”2 Linganisha hilo na lugha ya kishairi ya mtunga zaburi: “Uliifunika [dunia] kwa vilindi kama kwa vazi. Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima. Yakapanda milima, yakatelemka mabondeni, mpaka mahali ulipoyatengenezea.”—Zaburi 104:6, 8.
“Katika Mwanzo”
6. Ni taarifa gani ya Biblia inayopatana na nadharia za kisayansi za wakati huu juu ya chanzo cha ulimwengu wote mzima?
6 Mstari wa kwanza kabisa wa Biblia husema: “Katika mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.” (Mwanzo 1:1, NW) Mambo yaliyochunguzwa yameongoza wanasayansi watokeze nadharia kwamba ulimwengu wote mzima uonekanao kweli kweli ulikuwa na mwanzo. Haukuwapo tangu kale na kale. Mtaalamu wa elimu-nyota Robert Jastrow, mwagnosti katika mambo ya kidini, aliandika: “Habari zatofautiana, lakini mambo ya msingi katika masimulizi ya kielimu-nyota na ya kibiblia ya Mwanzo ni yale yale: mfululizo wa matukio wenye kuongoza kwa binadamu ulianza ghafula na kwa mshtuko katika punde fulani kamili ya wakati, katika mmweko wa nuru na nishati.”3
7, 8. Ingawa hawakubali yaliyotimizwa na Mungu katika jambo hilo, wanasayansi wengi wanalazimika kukubali nini kwa habari ya chanzo cha ulimwengu wote mzima?
7 Ni kweli, wanasayansi wengi, wajapoamini kwamba ulimwengu wote mzima ulikuwa na mwanzo, hawakubali taarifa ya kwamba “Mungu aliumba.” Hata hivyo, baadhi sasa hukubali kwamba ni vigumu kupuuza uthibitisho wa aina fulani ya akili iliyotokeza kila kitu. Freeman Dyson, Profesa wa fizikia aeleza hivi: “Kwa kadiri ninavyozidi kuuchunguza ulimwengu wote mzima na kujifunza habari za muundo wao, ndivyo ninavyoona uthibitisho zaidi kwamba tulikusudiwa tutokee.”
8 Dyson aendelea kukubali hivi: “Nikiwa mwanasayansi, aliyezoezwa tabia za kufikiri na lugha ya karne ya ishirini badala ya ile ya kumi na nane, sidai kwamba muundo wa ulimwengu wote mzima wathibitisha kuwapo kwa Mungu. Nadai tu kwamba muundo wa ulimwengu wote mzima wapatana na lile dhana ya kwamba akili hutimiza fungu muhimu katika kutenda kwayo.”4 Bila shaka maelezo yake yaonyesha mtazamo wenye shaka wa wakati wetu. Lakini tukiachana na utiaji shaka huo, mtu anaona kuna upatano kati ya sayansi ya ki-siku-hizi na taarifa ya Biblia kwamba “katika mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.”—Mwanzo 1:1, NW.
Afya na Usafi
9. Sheria ya Biblia juu ya maradhi ya ngozi yenye kuambukia yaonyeshaje hekima yenye kutumika? (Ayubu 12:9, 16a)
9 Fikiria mazungumzo ya Biblia juu ya uwanja mwingine: afya na usafi. Endapo Mwisraeli alikuwa na waa la ngozi lililotiliwa shaka kuwa ukoma, alitengwa na wengine. “Sikuzote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.” (Mambo ya Walawi 13:46) Hata mavazi yaliyoambukiwa yalichomwa. (Mambo ya Walawi 13:52) Katika siku hizo, hiyo ilikuwa njia iliyofanikiwa ya kuzuia kuenea kwa ambukizo hilo.
10. Wengi katika baadhi ya mabara wangefaidikaje kwa kufuata shauri la Biblia juu ya elimusiha?
10 Sheria nyingine ya maana ilihusu uondoaji wa takamwili (mavi) ya mwanadamu, ambayo ilipasa izikwe nje ya kambi. (Kumbukumbu la Torati 23:12, 13) Bila shaka sheria hiyo iliokoa Waisraeli na maradhi mengi. Hata leo, matatizo makubwa ya afya husababishwa katika mabara fulani na uondoaji usiofaa wa takamwili ya mwanadamu. Kama watu katika mabara hayo wangefuata tu sheria iliyoandikwa katika Biblia maelfu ya miaka iliyopita, wangekuwa wenye afya zaidi.
11. Ni shauri gani la Biblia juu ya afya ya kiakili limepatikana kuwa lenye kutumika?
11 Kiwango cha juu cha Biblia cha elimusiha (elimu ihusuyo afya) kilihusu pia afya ya kiakili. Mithali moja ya Biblia ilisema: “Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; bali husuda ni ubovu wa mifupa.” (Mithali 14:30) Katika miaka ya karibuni, utafiti wa tiba umeonyesha kwamba kwa kweli afya yetu ya kimwili huathiriwa na mtazamo wetu wa kiakili. Kwa kielelezo, Daktari C. B. Thomas wa Johns Hopkins University alichunguza wahitimu zaidi ya elfu moja kwa kipindi cha miaka 16, akilinganisha tabia zao za kisaikolojia na kuambukiwa kwao na maradhi. Aliona jambo moja: Wahitimu walioambukiwa zaidi na maradhi walikuwa wale waliokuwa wenye kasirani zaidi na wenye wasiwasi zaidi chini ya mkazo.5
Biblia Husema Nini?
12. Ni kwa nini Kanisa Katoliki lilisisitiza kwamba nadharia ya Galileo juu ya dunia ilikuwa ni uzushi?
12 Ikiwa Biblia ni sahihi hivyo katika nyanja za kisayansi, ni kwa nini Kanisa Katoliki likasema fundisho la Galileo la kwamba dunia ilienda ikilizunguka jua halikuwa la kimaandiko? Kwa sababu ya namna ambavyo wenye mamlaka walifasiri mistari fulani ya Biblia.6 Je! walikuwa sahihi? Acheni tusome vifungu viwili walivyonukuu tuone.
13, 14. Kanisa Katoliki lilitumia vibaya mistari gani ya Biblia? Fafanua.
13 Kifungu kimoja chasema: “Jua huchomoza, jua hutua; kisha huharakisha kwenda mahali palo na hapo huchomoza.” (Mhubiri 1:5, The Jerusalem Bible) Kulingana na hoja ya Kanisa hilo, semi kama vile “jua huchomoza” na “jua hutua” humaanisha kwamba jua, wala si dunia, husonga. Lakini hata leo sisi husema kwamba jua huchomoza na kutua, na wengi wetu twajua kwamba dunia ndiyo husonga, si jua. Tunapotumia semi kama hizo, twafanya kueleza tu mwendo uonekanao wa jua kama ionekanavyo kwa mtazamaji wa kibinadamu. Mwandikaji wa Biblia alikuwa akifanya vivyo hivyo.
14 Kile kifungu kingine husema: “Wewe uliiimarisha dunia juu ya misingi yayo, isitikisike milele na milele.” (Zaburi 104:5, The Jerusalem Bible) Hilo lilifasiriwa kuwa lilimaanisha kwamba baada ya kuumbwa kwayo dunia haingeweza kusonga. Lakini, kwa kweli mstari huo hukazia udumifu wa dunia, wala si hali yayo ya kutosonga. Dunia haitapata kamwe ‘kutikiswa’ isiwepo, au kuangamizwa, kama inavyothibitishwa na mistari mingine ya Biblia. (Zaburi 37:29; Mhubiri 1:4) Andiko hili, pia, halihusu mwendo husianifu wa dunia na jua. Katika wakati wa Galileo, Kanisa, wala si Biblia, ndilo lililozuia mazungumzo huru ya kisayansi.
Mageuzi na Uumbaji
15. Nadharia ya mageuzi ni nini, nayo yapingaje Biblia?
15 Hata hivyo, kuna eneo ambalo wengi wangesema kwamba sayansi ya ki-siku-hizi na Biblia zapingana kabisa. Wanasayansi walio wengi huamini nadharia ya mageuzi, inayofundisha kwamba vitu vyote vilivyo hai viligeuka-geuka kutoka namna ya uhai iliyo sahili iliyokuja kuwapo mamilioni ya miaka iliyopita. Kwa upande mwingine, Biblia hufundisha kwamba kila kikundi kikubwa cha vitu vilivyo hai kiliumbwa kwa njia ya pekee na huzaa “kwa jinsi yake” tu. Husema binadamu aliumbwa “kwa mavumbi ya ardhi.” (Mwanzo 1:21; 2:7) Je! hilo ni kosa katika Biblia linaloonyeshwa wazi kabisa kisayansi? Kabla ya kuamua, acheni tutazame kwa uangalifu zaidi yale ambayo sayansi yajua, kinyume cha yale ambayo yatokeza kuwa nadharia.
16-18. (a) Ni uchunguzi gani mmoja aliofanya Charles Darwin ambao ulimwongoza aamini mageuzi? (b) Twaweza kutoaje hoja kwamba alichochunguza Darwin katika Visiwa Galápagos hakipingi inayosema Biblia?
16 Nadharia ya mageuzi ilifanywa na Charles Darwin kuwa maarufu wakati wa karne iliyopita. Alipokuwa kwenye Visiwa Galápagos katika Pasifiki, Darwin alivutiwa sana na namna tofauti za ndege-chiriku kwenye visiwa tofauti, ambao, yeye alikata kauli, lazima wawe walitokana na namna moja tu ya wazazi wa kale. Kwa sehemu, kwa sababu ya uchunguzi huo, alikuza nadharia ya kwamba vitu vyote vilivyo hai vimetoka kwa umbo moja sahili la awali. Yeye alisisitiza kwamba nguvu yenye kuongoza kwenye mageuzi ya viumbe vya juu kutoka kwa vile vya chini, ilikuwa ni uteuzi wa asili, kuokoka kwa vyenye nguvu zaidi. Akadai kupitia mageuzi, wanyama wa bara walisitawi kutoka kwa samaki, nyuni kutoka kwa jamii ya watambaachi, na kadhalika.
17 Kwa kweli, kile ambacho Darwin alichunguza katika visiwa hivyo hakikuwa kisichopatana na Biblia, ambayo huruhusu kuwapo kwa namna-namna ndani ya aina moja kubwa iliyo hai. Kwa kielelezo, jamii zote za ainabinadamu zilitokana na wanadamu wawili wa kwanza tu. (Mwanzo 2:7, 22-24) Kwa hiyo si jambo geni kwamba namna zote hizo za ndege-chiriku zingetokana na namna moja ya wazazi wa kale. Lakini waliendelea kuwa ndege-chiriku. Hawakugeuka kuwa mwewe au tai.
18 Wala namna mbalimbali za ndege-chiriku wala kingine chochote alichoona Darwin hakikuthibitisha kwamba vitu vyote vilivyo hai, iwe ni papa au shakwe, tembo au nyungunyungu, vilikuwa na mzazi mmoja wa kale. Hata hivyo, wanasayansi wengi husisitiza kwamba mageuzi si nadharia tena bali ni uhakika. Wengine, wajapotambua matatizo ya nadharia hiyo, husema kwamba wanaiamini vyovyote vile. Ni jambo la umaarufu kufanya hivyo. Hata hivyo, sisi twahitaji kujua kama mageuzi yamethibitishwa kwa kadiri ambayo lazima Biblia iwe imekosea.
Je! Yamethibitishwa?
19. Vizibiti huunga mkono mageuzi au Biblia?
19 Nadharia ya mageuzi yaweza kutiwaje kwenye mtihani? Njia iliyo wazi kabisa ni kuchunguza vizibiti ili kuona kama badiliko la hatua kwa hatua kutoka aina moja mpaka nyingine lilitukia kweli kweli. Je! lilitukia? La, sawa na ambavyo idadi fulani ya wanasayansi inakubali kwa kufuatia haki. Mmoja, Francis Hitching, aandika: “Unapotazama uone viunzi kati ya vikundi vikubwa vya wanyama, havipo kamwe.”7 Ukosefu huo wa uthibitisho katika kumbukumbu ya vizibiti uko wazi sana hivi kwamba wanamageuzi wametokeza nadharia zilizo badala ya ile ya Darwin ya badiliko la hatua kwa hatua. Lakini, ukweli ni kwamba kutokea kwa ghafula kwa aina za wanyama katika vizibiti kwaunga mkono uumbaji wa kipekee zaidi sana kushinda mageuzi.
20. Ni kwa nini jinsi ambayo chembe-chembe zilizo hai huzaana hairuhusu mageuzi kutukia?
20 Zaidi ya hayo, Hitching aonyesha kwamba viumbe vilivyo hai vimeamriwa vizae vingine vinavyofanana navyo kabisa badala ya kugeuka kuwa kitu kingine. Asema: “Chembe-chembe zilizo hai hujinakili kwa ufanano unaokaribiana kabisa. Kiwango cha kosa ni kidogo sana hivi kwamba hakuna mashine yoyote iliyoundwa na binadamu iwezayo kukikaribia. Pia kuna mipaka ya kindani iliyofanyizwa. Mimea hufikia ukubwa fulani na kukataa kukua zaidi. Nzi wa matunda hukataa kuwa kitu kingine ila tu nzi wa matunda katika hali zozote zilizobuniwa.”8 Mageuzi ya kutokeza hitilafu yaliyochochewa na wanasayansi katika nzi wa matunda kwa makumi ya miaka yameshindwa kuwalazimisha wageuke kuwa kitu kingine.
Chanzo cha Uhai
21. Ni mkataa gani uliothibitishwa na Louis Pasteur unaotokeza tatizo kubwa kwa wanamageuzi?
21 Swali jingine lenye kusumbua ambalo wanamageuzi wameshindwa kujibu ni: Chanzo cha uhai kilikuwa nini? Aina ya uhai ya kwanza iliyo sahili—ambayo sisi sote twapaswa kuwa tulitokana nalo—ilikujaje kuwapo? Karne nyingi zilizopita, hilo halingalionekana kuwa tatizo. Wakati huo watu walio wengi walifikiri kwamba nzi wangeweza kusitawi kutokana na nyama yenye kuoza na kwamba rundo la matambara lingeweza lenyewe kutokeza panya. Lakini, miaka zaidi ya mia moja iliyopita, mwanakemia Mfaransa Louis Pasteur alionyesha waziwazi kwamba uhai waweza kutoka tu kwa uhai uliotangulia kuwapo.
22, 23. Kulingana na wanamageuzi, uhai ulianzaje, lakini mambo ya hakika yaonyesha nini?
22 Kwa hiyo wanamageuzi hufafanuaje chanzo cha uhai? Kulingana na nadharia yenye kupendwa na wengi, muungano wa nasibu wa kemikali na nishati ulitokeza kizazi cha uhai chenye kujifanyiza chenyewe tu mamilioni ya miaka iliyopita. Vipi juu ya kanuni ile aliyothibitisha Pasteur? The World Book Encyclopedia chaeleza: “Pasteur alionyesha kwamba uhai hauwezi kujifanyiza wenyewe tu chini ya hali za kemikali na fizikia zilizopo duniani leo. Hata hivyo, mabilioni ya miaka iliyopita, hali za kemikali na fizikia duniani zilikuwa tofauti sana”!9
23 Hata hivyo, chini ya hali tofauti sana kuna pengo kubwa kati ya mata ambayo haiko hai na kitu sahili zaidi kilicho hai. Michael Denton, katika kitabu chake Evolution: A Theory in Crisis, asema: “Kati ya chembe-chembe iliyo hai na mfumo usio wa kibayolojia wenye utaratibu wa juu zaidi, kama vile fuwele au chembe ya theluji, kuna shimo kubwa sana na pana kwa kadiri iwezekanayo kuwaziwa.”10 Wazo la kwamba kitu kisicho na uhai kingeweza kuja kuishi kwa nasibu fulani ya kihobelahobela ni dogo mno hivi kwamba ni lisilowezekana. Maelezo ya Biblia, kwamba ‘uhai ulitoka kwa uhai’ ikimaanisha kwamba uhai uliumbwa na Mungu, yanapatana kabisa na mambo ya hakika.
Kwa Nini Si Uumbaji
24. Nadharia hiyo ijapokuwa na matatizo, ni kwa nini wanasayansi walio wengi wangali wanashikilia nadharia ya mageuzi?
24 Ijapokuwa matatizo yanayoambatana na nadharia ya mageuzi, imani katika uumbaji huonwa leo kuwa isiyo ya kisayansi, hata kuwa ya kiajabu-ajabu. Ni kwa nini? Ni kwa nini hata mtaalamu kama Francis Hitching, ambaye kwa kufuatia haki anaonyesha udhaifu wa mageuzi, anakataa wazo la uumbaji?11 Michael Denton aeleza kwamba mageuzi, yajapokuwa na kasoro, yataendelea kufunzwa kwa sababu nadharia zinazohusiana na uumbaji “kwa wazi hutolea dua wafanyizaji wenye nguvu zinazozidi zile za kawaida.”12 Ndiyo kusema, uhakika wa kwamba uumbaji watia ndani Muumba waufanya uwe usiokubalika. Hakika, huko ndiko kusababu kulikoenea tulikokabili katika kisa cha miujiza: Miujiza haiwezekani kwa sababu ni ya kimwujiza!
25. Kisayansi, ni udhaifu gani wa mageuzi, unaoonyesha kwamba mageuzi si jambo linalostahili kuchukua mahali pa uumbaji katika kueleza chanzo cha uhai?
25 Isitoshe, nadharia ya mageuzi yenyewe inatatizika sana kwa maoni ya kisayansi. Michael Denton aendelea kusema: “Hiyo ikiwa kwa msingi ni nadharia ya kuwazia yaliyotukia kihistoria, haiwezekani kuhakikisha [nadharia ya Darwin] kwa kufanya jaribio au kuchunguza moja kwa moja kama ilivyo kawaida ya sayansi. . . . Zaidi ya hayo, nadharia ya mageuzi hushughulika na mfululizo wa matukio yasiyo ya kawaida, chanzo cha uhai, chanzo cha akili na kadhalika. Matukio yasiyo ya kawaida hayawezi kurudiwa na hayawezi kufanyiwa uchunguzi wowote wa kuyajaribu.”13 Ukweli ni kwamba nadharia ya mageuzi, ijapopendwa na wengi, imejaa mapengo na matatizo. Haitoi sababu nzuri ya kukataa simulizi la Biblia la chanzo cha uhai. Sura ya kwanza ya Mwanzo yatoa simulizi lenye sababu nzuri kabisa juu ya jinsi ‘matukio hayo yasiyo ya kawaida yasiyoweza kurudiwa’ yalivyokuja kutukia wakati wa “siku” za uumbaji ambazo zilihusisha mamileani ya wakati.a
Vipi Juu ya Furiko?
26, 27. (a) Biblia yasema nini juu ya Furiko? (b) Kwa sehemu, lazima maji ya furiko hilo yawe yalitoka wapi?
26 Wengi huelekeza kwenye jambo jingine linalodhaniwa kuwa ni kupingana kati ya Biblia na sayansi ya ki-siku-hizi. Katika kitabu cha Mwanzo, twasoma kwamba maelfu ya miaka iliyopita uovu wa binadamu ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba Mungu akaazimia kuwaharibu. Hata hivyo, aliagiza yule binadamu mwadilifu Nuhu ajenge chombo kikubwa cha mbao, safina. Kisha Mungu akaleta furiko juu ya ainabinadamu. Ni Nuhu na familia yake tu waliookoka, pamoja na viwakilishi vya namna-namna za wanyama. Furiko hilo lilikuwa kubwa sana hivi kwamba “milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa.”—Mwanzo 7:19.
27 Maji hayo yote yaliyofunika dunia yote yalitoka wapi? Biblia yenyewe yajibu. Mapema katika utendaji wa uumbaji, eneo la angahewa lilipoanza kuumbika, kulikuja kuwa “maji yaliyo chini ya anga” na “maji yaliyo juu ya anga.” (Mwanzo 1:7; 2 Petro 3:5) Furiko lilipokuja, Biblia yasema: “Madirisha ya mbinguni yakafunguka.” (Mwanzo 7:11) Bila shaka, “maji yaliyo juu ya anga” yalianguka na kutoa mengi ya maji yaliyofunikiza.
28. Watumishi wa kale wa Mungu, kutia ndani Yesu, walionaje Furiko hilo?
28 Vitabu vya ki-siku-hizi vya mafundisho vyaelekea kukanusha furiko la ulimwengu wote mzima. Kwa hiyo lazima tuulize: Je! Furiko hilo ni ngano tu, au je! lilitukia kikweli? Kabla ya kujibu hilo, twapaswa kuangalia kwamba waabudu wa baadaye wa Yehova walikubali Furiko kuwa historia ya kweli; hawakuliona kuwa ngano. Isaya, Yesu, Paulo, na Petro walikuwa kati ya wale waliolirejezea kuwa kitu kilichotukia kikweli. (Isaya 54:9; Mathayo 24:37-39; Waebrania 11:7; 1 Petro 3:20, 21; 2 Petro 2:5; 3:5-7) Lakini kuna maswali ambayo lazima yajibiwe juu ya Gharika ya ulimwengu wote mzima.
Maji ya Furiko
29, 30. Ni mambo gani ya hakika juu ya ugavi-maji wa dunia huonyesha kwamba Furiko hilo lasadikisha?
29 Kwanza, je! wazo la dunia yote kufurikwa ni la kutilika shaka? Sivyo. Kwa kweli, kwa kadiri fulani dunia ingali imefurikwa. Asilimia 70 yayo imefunikwa na maji na ni asilimia 30 pekee iliyo nchi kavu. Na zaidi, asilimia 75 ya maji yote yasiyo na chumvi ya dunia yamegandamana katika barafuto (mitiririko mikubwa ya barafu) na katika ncha za dunia zenye barafu. Kama barafu hii yote ingeyeyuka, usawa wa bahari ungeinuka zaidi sana. Majiji kama New York na Tokyo yangetoweka.
30 Na zaidi, The New Encyclopædia Britannica chasema: “Kina cha wastani cha bahari zote kimekadiriwa kuwa meta 3,790, tarakimu iliyo juu sana zaidi ya ile ya mwinuko wa wastani wa nchi kavu juu ya usawa wa bahari, ambao ni meta 840. Kina cha wastani kikizidishwa na eneo lacho la uso, mjao wa Bahari ya Ulimwengu ni mara 11 ya mjao wa nchi kavu iliyo juu ya usawa wa bahari.”14 Kwa hiyo, kama kila kitu kingelainishwa—kama milima ingefanywa kuwa tambarare na mabonde ya bahari ya kina kirefu kujazwa—bahari ingefunika dunia yote kufikia kina cha maelfu ya meta.
31. (a) Ili Furiko hilo liwe lilitukia, lazima hali ya dunia ya kabla ya Furiko iwe ilikuwaje? (b) Ni nini kinachoonyesha yawezekana kwamba milima ilikuwa chini zaidi na kwamba mabonde ya bahari yalikuwa ya kina kifupi zaidi kabla ya Furiko hilo?
31 Ili iwe Furiko lilitukia, mabonde ya kabla ya Furiko lazima yawe yalikuwa ya kina kifupi zaidi, na milima kuwa ya chini zaidi ya ilivyo sasa. Je! hilo lawezekana? Kitabu kimoja cha mafundisho chasema: “Ingawa milima ya ulimwengu yainuka urefu mkubwa sana sasa, wakati mmoja, mamilioni ya miaka iliyopita, bahari na nyanda zilinyooka zikiwa tambarare hali moja. . . . Kusonga kwa mabamba ya miamba ya kontinenti husababisha nchi kavu kuinuka kufikia urefu ambao ni wanyama na mimea yenye uvumilivu zaidi yaweza kuishi na, kwa upande ule mwingine, hutumbukia na kukaa katika uzuri uliofichwa kina kirefu chini ya sakafu ya bahari.”15 Kwa kuwa milima na mabonde ya bahari huinuka na kushuka, ni wazi kwamba wakati mmoja milima haikuwa mirefu kama ilivyo sasa na mabonde ya bahari kuu hayakuwa ya kina kirefu hivi.
32. Lazima kuwe kulitukia nini kwa maji ya Furiko? Fafanua.
32 Kulitukia nini kwa maji ya furiko baada ya Furiko hilo? Lazima yawe yaliingia katika mabonde ya bahari. Jinsi gani? Wanasayansi huamini kwamba kontinenti hukalia mabamba ya miamba mikubwa. Kusonga kwa mabamba ya miamba hiyo kwaweza kusababisha mabadiliko katika usawa wa uso wa dunia. Katika sehemu fulani leo, kuna mashimo makubwa sana ya chini ya maji yenye kina cha zaidi ya kilometa kumi kwenye mipaka ya mabamba ya miamba hiyo.16 Yawezekana sana kwamba—labda kwa kusababishwa na Furiko hilo lenyewe—mabamba ya miamba hiyo yalisonga, sakafu ya bahari ikazama, na mitaro hiyo mikubwa ikafunguka, hivyo kuruhusu maji yabubujike kutoka nchi kavu.b
Alama za Furiko?
33, 34. (a) Tayari wanasayansi wana uthibitisho gani ambao waweza kuwa ni uthibitisho wa Furiko hilo? (b) Je! ni jambo la kufikiri kuzuri kusema kwamba yawezekana wanasayansi wanafasiri kimakosa uthibitisho huo?
33 Tukikubali kwamba furiko kubwa lingeweza kuwa lilitukia, ni kwa nini wanasayansi hawajaona alama yoyote yalo? Labda wameona, lakini wanafasiri uthibitisho huo kwa njia nyingine. Kwa kielelezo, sayansi inayokubaliwa na wengi hufundisha kwamba uso wa dunia umeundwa katika sehemu nyingi na barafuto zenye nguvu wakati wa mfululizo wa enzi za barafu. Lakini uthibitisho ulio wazi wa utendaji wa barafuto nyakati nyingine waweza kuwa ni tokeo la tendo la maji. Basi, yaelekea sana, baadhi ya uthibitisho wa Furiko unafasiriwa kimakosa kuwa ni uthibitisho wa enzi ya barafu.
34 Makosa kama hayo yamefanywa. Kuhusu wakati ambao wanasayansi walipokuwa wakisitawisha nadharia ya enzi za barafu, twasoma: “Walikuwa wakipata enzi za barafu kwenye kila hatua ya historia ya jiolojia, kwa kufuatia falsafa ya ufanano. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni uchunguzi mpya wa uangalifu juu ya uthibitisho huo, umekanusha nyingi za enzi hizi za barafu; maumbo ambayo wakati mmoja yalitambulishwa kuwa kokoto iliyorundikwa na barafuto imefasiriwa tena kuwa matuta yaliyotandikwa na mtiririko wa tope, maporomoko ya ardhi iliyofunikwa na maji na mikondo yenye tope: maporomoko ya maji yenye tope yanayopeleka changarawe, mchanga na kokoto kwenye sakafu ya bahari yenye kina kirefu.”18
35, 36. Ni uthibitisho gani katika vizibiti na katika jiolojia unaoweza kuwa wahusiana na Furiko hilo? Fafanua.
35 Uthibitisho mwingine wa Furiko waonekana upo katika vizibiti. Wakati mmoja, kulingana na kizibiti hiki, simba-milia wakubwa wenye meno mawili yaliyochomoza waliotea-otea mawindo yao katika Ulaya, farasi wakubwa zaidi ya wowote walio hai sasa walizunguka-zunguka Amerika Kaskazini, na tembo-majitu walitafuta-tafuta chakula katika Siberia. Kisha, ulimwenguni pote, namna-namna za wanyama wanyonyeshao (mamalia) zikatoweka. Wakati uo huo, kulikuwako badiliko la ghafula la hali ya tabia ya nchi. Makumi ya maelfu ya tembo-majitu yaliuawa na kugandishwa upesi katika Siberia.c Alfred Wallace, mrika wa Charles Darwin ajulikanaye sana, alionelea kwamba uharibifu huo mkubwa lazima uwe ulisababishwa na tukio fulani la ulimwengu lisilo la kawaida.19 Wengi wametoa hoja kwamba tukio hilo lilikuwa ni Furiko.
36 Makala moja ya mhariri katika gazeti Biblical Archaeologist ilionelea hivi: “Ni jambo la maana kukumbuka kwamba hadithi ya furiko kubwa ni mojawapo mapokeo yaliyoenea sana katika utamaduni wa kibinadamu . . . Hata hivyo kisababishi cha mapokeo ya kale zaidi yanayopatikana katika vyanzo vya Mashariki ya Karibu, yawezekana sana kuwako na furiko halisi la viwango vikubwa la wakati wa tarehe mojawapo vipindi vya mvua nyingi . . . maelfu ya miaka mingi iliyopita.”20 Vipindi hivyo vya mvua nyingi vilikuwa nyakati ambapo uso wa dunia ulikuwa umelowa zaidi ya ulivyo sasa. Maji yasiyo na chumvi ya maziwa kuzunguka ulimwengu yalikuwa makubwa zaidi. Nadharia moja hutolewa kwamba uowevu huo ulisababishwa na mvua kubwa zilizoshirikishwa na mwisho wa enzi za barafu. Lakini wengine wamedokeza kwamba katika pindi moja uowevu mkubwa wa uso wa dunia ulikuwa ni tokeo la Furiko.
Ainabinadamu Haikusahau
37, 38. Mwanasayansi mmoja aonyeshaje kwamba, kulingana na uthibitisho, yaelekea kuwa Furiko hilo lilitukia, nasi twajuaje lilitukia?
37 Profesa wa jiolojia John McCampbell aliandika hivi wakati mmoja: “Tofauti za msingi kati ya msiba [lile Furiko] na ufanano wa kimageuzi hazihusu data ya hakika ya jiolojia bali mafasirio ya data hizo. Ufasiri unaopendelewa utategemea kwa kadiri kubwa malezi na dhana za kimbele za mwanafunzi mmoja mmoja.”21
38 Kwamba Furiko lilipata kutukia yaonyeshwa na uhakika wa kwamba ainabinadamu haikulisahau. Ulimwenguni pote, katika sehemu zilizo mbali mbali kama vile Alaska na Visiwa vya Bahari ya Kusini, kuna hadithi za kale juu yalo. Wazaliwa wa Amerika wa staarabu za kabla ya Columbus, na pia Waaborijini wa Australia, wote wana hadithi juu ya Furiko hilo. Ingawa baadhi ya masimulizi hayo hutofautiana katika vijambo vidogo, uhakika wa msingi kwamba dunia ilifurikwa na ni wanadamu wachache tu waliookolewa katika chombo kilichotengenezwa na binadamu huonekana karibu katika namna zote. Sababu pekee ya ukubali huo ulioenea sana ni kwamba Furiko hilo lilikuwa tukio la kihistoria.d
39. Ni uthibitisho gani wa ziada ambao tumeona wa uhakika wa kwamba Biblia ni Neno la Mungu, si la binadamu?
39 Hivyo, katika mambo ya msingi Biblia yapatana na sayansi ya ki-siku-hizi. Kunapokuwa mgongano kati ya hizo mbili, uthibitisho wa wanasayansi watilika shaka. Zinapokubaliana, mara nyingi Biblia inakuwa sahihi sana hivi kwamba twapaswa kuamini ilipata habari zayo kutoka kwa akili inayozidi uwezo wa mwanadamu. Kweli kweli, kukubaliana kwa Biblia na sayansi iliyothibitishwa kwatoa ushuhuda zaidi kwamba hiyo ni Neno la Mungu, si la binadamu.
[Maelezo ya Chini]
a Mazungumzo marefu zaidi juu ya habari ya mageuzi na uumbaji yapatikana katika kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? kilichotangazwa katika 1985 na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
b Kitabu Planet Earth—Glacier chavuta fikira kwenye njia ambayo maji yakiwa katika umbo la miamba ya barafu inavyobonyeza uso wa dunia. Kwa kielelezo, chasema: “Kama barafu ya Greenland ingetoweka, kisiwa hicho kingeinuka futi 2,000 (meta 600) hivi hatimaye.” Kwa sababu hiyo, tokeo la furiko la tufe lote la ghafula kwenye sehemu za ganda la dunia lingalikuwa lenye msiba.17
c Kadirio moja lasema milioni tano.
d Kwa habari zaidi juu ya Furiko hilo, ona Insight on the Scriptures, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., Buku 1, kurasa 327, 328, 609-612.
[Sanduku katika ukurasa wa 105]
“Kutoka Mavumbi”
“The World Book Encyclopedia” charipoti: “Elementi zote za kemikali zinazofanyiza vitu vilivyo hai zimo pia katika mata isiyo na uhai..” Yaani, kemikali za msingi zinazofanyiza viumbe vilivyo hai, kutia ndani binadamu, zapatikana pia katika dunia yenyewe. Hilo lapatana na taarifa ya Biblia: “BWANA [Yehova, “NW”] akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi.”—Mwanzo 2:7.
[Sanduku katika ukurasa wa 107]
‘Kwa Mfano wa Mungu’
Baadhi huelekeza kwenye mifanano ya kimwili kati ya binadamu na baadhi ya wanyama ili kuthibitisha uhusiano wao. Ingawa hivyo, lazima wakubali kwamba uwezo wa kiakili wa binadamu ni wa juu zaidi sana ya ule wa mnyama yeyote. Ni kwa nini binadamu ana uwezo wa kufanya mipango na kupanga kitengenezo ulimwengu unaomzunguka, uwezo wa upendo, akili ya juu, dhamiri, na wazo la wakati uliopita, wakati uliopo, na wakati ujao? Mageuzi hayawezi kujibu hilo. Lakini Biblia hujibu, isemapo: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba.” (Mwanzo 1:27) Kwa habari ya uwezo na uwezekano wa kiakili na kiadili wa binadamu, yeye ni mwakisho wa Baba yake wa kimbingu.
[Picha katika ukurasa wa 99]
Usimulizi wa Biblia wa dunia ikining’inia angani wakubaliana sana na ambayo wanaanga wameripoti kuwa wameona
[Picha katika ukurasa wa 102]
Biblia haijihusishi katika kusema kama dunia huzunguka jua au jua huzunguka dunia
[Picha katika ukurasa wa 112, 113]
Kama dunia ingefanywa kuwa tambarare, isiwe na milima au na vilindi vikubwa, vingefunikwa kabisa na tabaka la kina kirefu cha maji
[Picha katika ukurasa wa 114]
Tembo-majitu walipatikana ambao waligandishwa upesi baada ya kifo chao
[Picha katika ukurasa wa 115]
Louis Pasteur alithibitisha kwamba uhai waweza kutoka tu kwa uhai uliopo tayari
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 109]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Biblia yatoa usimulizi sahihi wa mrudio maji wa dunia